Maombi kwa ajili ya kanisa la Tanzania 1 June, 2012

Kuanzia tarehe 1 June 2012 tunaanza maombi maalumu kwa ajili ya toba, amani, upendo na ustawi na kukua kwa kanisa Tanzania. Tunamkaribisha yeyote atakayeweza kushiriki nasi popote pale ulipo, atakayeweza kufunga atafunga, ni maombi ya mwezi mzima!

Mistari ya kusimamia
2 Wafalme 5: 16-17
2 Nyakati 7: 14-18
Nehemia 1: 4-6
Nehemia 2: 4 na Nehemia 2: 7-8
Nehemia 4: 7-8 na 1Timotheo 2: 1-6

Mjipe moyo ndugu zetu wa Zanzibar, aliye ndani yetu ni mkuu kuliko wote!

Mungu Ibariki na kuilinda Tanzania!

–Rose Lusinde

Usiku wa Sifa – April


Bukuku, Mkesha wa SG September

Steven Mwikwabe wa album ya KUISHI KWANGU, na wimbo wa RAFIKI WA KWELI atakuwepo

Shalom wana SG na wote, nawasalimu katika jina la Yesu! Napenda kuchukua fursa hii kuwataka wote kufika bila kukosa ili kumsifu Mungu, kumwabudu na kupeleka haja zetu mbele zake tarehe 13/4/2012. Njoo tumuombe Mungu ili atuonekanie katika maisha yetu, huduma zetu, afya zetu, kazi zetu na yote yanayotuhusu. Anza kupanga kuanzia sasa kutokukosa mkesha huu. Mkesha utaanza saa 4:00 usiku mpaka 11:30 alfajiri.

Ni pale Jesus Celebration Centre, Shekilango karibu na uwanja wa Kinesi.  Walete wagonjwa na wenye matatizo wataombewa kwa Jina la Yesu. Pia kama nawe umeandika maombi yako hapa kwenye blog yataombewa ukiweza pia unaweza kufika, Tafadhali upatapo ujumbe huu mwambie na mwingine!

Ni kila Ijumaa ya pili ya mwezi.

Simu: 0767022096/0715 422096

Email: strictlygospel@yahoo.co.uk

Kumradhi!

Bwana Yesu asifiwe Watembeleaji SG na Familia ya SG! Kuna wengi wanaotuma mail, simu kuhusu mjadala huu na ule kuwahusu watumishi wa Mungu Nabii TB Joshua na Mtume na Nabii Josephat Mwingira. Tunaomba ieleweke kwamba nia na lengo letu sio KUBOMOA ila ni kufundishana, kuonyana ili KUJENGA mwili wa Kristo.

Hivyo basi kutokana na maoni mbali mbali, tunajifunza kutoka kwa watumishi wanaotuma maoni yao hapa na kuna ambao wengine tunafahamu huduma zao wanazozifanya na kuwaona wakifundisha sehemu mbalimbali pamoja na magazetini Mfano: CK Lwembe ambaye wamemlalamikia sana.

Hii inatufanya kufahamiana, uwezo wetu katika kumjua Mungu pamoja na kupokea changamoto na naamini kuna ambao Roho Mtakatifu anasema nao kupitia maoni ya mada mbali mbali zinazojadiliwa hapa…kuna ambao Mungu anawatumia hapa vyema, kazi yenu si bure, kuna mbegu inapandwa kwa mtu.

Msimamo wa Strictly Gospel ni Neno la Mungu. Nasi tutajitahidi kukaa hapo. Kama Mtu atakuja kwa nia ya kuharibu. Hatutaruhusu maoni yake. Yapo maoni tunayoyazuia, yanaoonekana hewani ni kwa kujifunza, Mtu asipotaka kujifunza. Tafadhali unaweza kujadili kwenye blogs nyingine zisizo na mipaka ya Neno la Mungu.

Tunaomba radhi kwa makwazo yoyote mliyoyapata.

Mungu awabariki na karibuni tena!

Usiku wa Sifa – Strictly Gospel

Shalom wana SG na wote, nawasalimu katika jina la Yesu! Napenda kuchukua fursa hii kuwataka wote kufika bila kukosa ili kumsifu Mungu, kumwabudu na kupeleka haja zetu mbele zake tarehe 9/3/2012. It is dangerous to remain in a comfort zone whilst things are not okay… Njoo tumuombe Mungu ili atuonekanie katika maisha yetu, huduma zetu, afya zetu, kazi zetu na yote yanayotuhusu. Anza kupanga kuanzia sasa kutokukosa mkesha huu. Mkesha utaanza saa 4:00 usiku mpaka 11:30 alfajiri.

Ni pale Jesus Celebration Centre, Shekilango karibu na uwanja wa Kinesi. Inawezekana umehudhuria mikesha mingi, lakini nakuhakikishia huu ni mkesha wa tofauti kabisa, utakaobadilisha hatima ya maisha yako kuwa njema. Wanaohudhuria mikesha hii watakubaliana nami kuwa huwa tunashangaa asubuhi imefikaje? Hio ni kwa ajili ya uzuri wa program na muda wa kutosha wa kujimimina mioyo yetu kwa Bwana. Tafadhali upatapo ujumbe huu mwambie na mwingine!

Ni kila Ijumaa ya pili ya mwezi.

Wito wa kumtumikia Mungu!

Strictly Gospel tunaamini kila aliyeokoka ni mtumishi wa Mungu, haijalishi uko ofisini, chuoni, nyumbani nakadhalika. Tunaamini utakuwa na kitu Mungu ameweka ndani yako kwa ajili ya Utukufu wake, pengine unakosa nafasi kuhudumu kanisani ama umekuwa na majukumu mengi ya kazi za nyumbani, ofisini na chuoni.

Tunapenda kuwaalika wote kutoka kila sehemu, wenye mzigo na kazi ya Mungu, wenye huduma mbalimbali za kiroho tumtumikie Mungu pamoja kwa nafasi tutakazopata.

Na kama hujampokea Yesu kuwa Bwana Na Mwokozi wa Maisha yako, unakaribishwa kwenye familia.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Strictly Gospel:

Email: strictlygospel@yahoo.co.uk

Simu: +255 714 915 424

Mungu awabariki!

Mwambie Mungu, Asante

1 Wathesalonike 5:18Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu

Ikiwa zimebaki siku chache kuumaliza mwaka huu wa 2011. Je unalo jambo gani la kumshukuru Mungu? Je umewaza kwamba katika yote umepitia mazuri au mabaya, Bado mkono wa Mungu umekua pamoja nawe?

Kwa baadhi yetu umekua ni mwaka wa mafanikio, umejenga nyumba, umeponywa, kuongezewa mshahara, umepata mwenzi, biashara, umepata mtoto, umeinuliwa kihuduma nk.. hauna budi kumwambia Mungu asante, si kwa nguvu zako wala akili zako ila ni Mungu amekuona na kukukumbuka.

Kwa waliopita katika wakati mgumu ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba katika yote umepitia bado unaishi ingekua mbaya sana kama Mungu asingekusaidia, wengine wamekoswakoswa kuachishwa kazi, ajali, wameshindwa kulipa ada, kodi ya nyumba, kufukuzwa shule, magonjwa, kuondokewa na mpendwa wako… nk

Bado tunaishi,  bado tuko mikononi mwa Mungu kama anavyosema kwenye Neno lake katika Kumbukumbu 31:6 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu, kwa maana BWANA, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha“. Na hata sasa hajakuacha, ukiangalia miezi kadhaa iliyopita haumini kama umepita kwenye moto ule. Huyo ni Mungu anayeenda pamoja nasi, hatuna budi kumwambia, Asante.

Kwa wale ambao bado wanapita kwenye wakati ngumu, bado mwaka haujaisha, kuna Neema ya Mungu kukuvusha katika hilo unapitia sio kwa nguvu zako, bali ni kwa nguvu za Mungu, mshukuru Mungu na uendelee kumwamini yeye anaweza kukusaidia. Kama amewasaidia wote hao nawe pia  subiri utauona mkono wake.

Mungu wetu anatenda mambo makuu mpaka hatuna maneno mengi ya kusema yeye pekee anastahili sifa na shukrani hizi kwa matendo anayotutendea. Hakuna Mungu kama Mungu wa Ibrahim, Isaka na Israel.

Zaburi 107:8-16, Zaburi 106:1-2

Tuwe na Moyo wa Kujitolea

Bwana Yesu asifiwe sana!

Watu wengi hupiga simu, wengine huandika ujumbe mfupi wa maneno na wengine ujumbe wa barua pepe wakitaka kujiunga na Strictly Gospel kwa sababu za kiuchumi. Wapo ambao huuliza wakijiunga watapata mshahara wa shilingi ngapi. Wapo ambao husema kuwa hali yao ya kifedha ni mbaya sana hivyo wanaona wakijiunga na Strictly Gospel wataboresha kipato chao cha pesa. Hata kuna watu wa karibu ambao hutuuliza kuwa kwa kuendesha blog hii na Strictly Gospel kwa ujumla tunapata nini mifukoni?

Hivi karibuni kuna mtu mmoja ambaye alitaka maelekezo ya namna kujiunga na Freemasons kwa kuwa ameona habari zao katika blog hii. Na sababu kubwa aliyosema inamlazimu ajiunge na Freemasons ni kuwa anataka kuwa tajiri! Baada ya kumhakikishia kuwa sisi si washirika wa Freemasons bali ni wahubiri wa Injili alibadili mwelekeo na kusema basi ajiunge nasi Strictly Gospel kwa sababu hali yake kifedha si nzuri na anaamini akijiunga nasi maisha yake yatakuwa mazuri!

Jumla ya hayo yote ni kielelezo kuwa tunahitaji moyo wa kujitolea ili badala ya mtu kuhitaji au kufanya jambo fulani kwa ajili yake tu tuwe tayari kufanya jambo fulani hata kama faida yake ni kwa mtu mwingine.

Katika kitabu kile cha Mathayo 7:12, Bwana Yesu alisema hivi: “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati yote na manabii”

Ni kweli watu wote tuna mahitaji ya kiuchumi na kila mtu anapambana ili aweze kukabiliana na uhitaji huo. Japo kuna wale ambao walishatoka katika hali ya uhitaji lakini haina maana wamekaa tu na hawajishughulishi tena. Na hata matajiri zaidi nao wako bize wakitafuta kuongeza zaidi utajiri uliopo.

Jambo moja la kufahamu ni kuwa, pamoja na uhitaji uliopo lakini njia mojawapo ya kibiblia ya kupata ni kutoa. Waweza kuwa na uhitaji fulani na ukatamani upate ufumbuzi wa uhitaji huo, kumbe ili upate unatakiwa utoe. Waweza kuwa na uhitaji wa pesa lakini ili uzipate kumbe si lazima uombe au upewe pesa. Waweza toa muda wako kwa ajili ya kushughulikia jambo la mtu mwingine na katika kufanya hivyo ukafungua mlango wa wewe kupata. Si lazima iwe ni kutoka kwa mtu huyo ambaye umetoa muda wako kwa ajili yake. Inaweza kuwa ni kutoka kwa mtu mwingine kabisa ambaye Mungu atakuwa amemgusa kwa ajili yako. Mungu yupo na anatenda hata sasa!

Waafrika na hasa Watanzania tuna kiwango kidogo sana cha moyo wa kujitolea.  Tumenaswa katika mtego wa ubinafsi. Kuanzia maisha ya kawaida ya kimwili hadi katika Huduma za kiroho:.

Ukiingia maofisini hali ni mbaya sana. Kila mwenye nafasi ya “kutengeneza” pesa hutaka kufanya hivyo kwa ajili yake tu. Watu hutafuta marupu rupu kwa njia hata zisizo halali; mfano anaweza kujiongezea masaa ya OT (Over-time). Anaweza kulazimisha safari za kikazi ili tu apate traveling allowance, hata kama safari hizo hazima maslahi kwa umma. Walio katika sehemu za manunuzi nao hali ni mbaya. Risiti nyingi za uongo huandikwa na zingine zinaongezwa kiasi cha pesa ili kinachozidi kiingie katika mfuko binafsi. Mikataba mingi huingiwa kwa hila na asilimia kumi, (teni pesenti) ikipotosha lengo la mikataba hiyo pasipo kujali hasara yake kwa umma. Wako mabosi ambao huendelea kuchukua mishahara ya watu ambao walishakufa. Loh!

Ukienda kwa wafanya biashara hali ni mbaya sana. Mizani na vipimo vya uzito vimekazwa au kulegezwa ili visipime kihalali (hili nalo ni chukizo kwa Bwana Mithali 20:23). Vipimo vya ujazo vimepunguzwa kwa kukatwa au kuwekwa vitu vingine ndani ili vipime kidogo. Vipimo vya urefu vimefutwa alama zisionekane vizuri ili kipimo kiwe kifupi kuliko inavyotakiwa. Kuanzia mfanya biashara mkubwa hadi mdogo kabisa, kila mmoja hutafuta namna yoyote ya hila ili apate faida isiyo halali kwa kuharibu vipimo!

Kwa ujumla hali ya ubinafsi ni mbaya. Inatafuna nchi kuanzia Ikulu hadi mitaani, kwenye ngazi ya mwanzo kabisa. Maana hata muuza mafuta, anayeuza kwenye vibaba vya shilingi 50-50 za kitanzania naye hujitahidi afanye litakalowezekana ili apime mafuta kidogo kuliko alivyomwambia mteja wake.  Hata muuza nyanya, anayeuza nyanya za mafungu, hujitajidi apate njia ya “kumzunguka” mteja kwa kupanga nyanya kubwa juu katika chombo halafu chini anaweka zile ndogo na pengine mbovu!

Mambo ni mengi mno na tukisema tuyaandike yote hapa inaweza ikawa ni usumbufu kuyasoma maana itabidi yasomwe kwa siku nyingi. Lakini hayo machache hapo juu yanaonyesha kuwa hali ya ubinafsi iko juu sana. Na hiyo ndiyo sababu watanzani wengi ni wezi au wana wasi wasi wa kuibiwa. Hakuna kuaminiana kwa kuwa si rahisi mwizi kumwamini mtu mwingine kwa kuwa anajua kuwa naye ataiba tu kama ambavyo yeye huiba. Tunaishi maisha ya kuogopana, maisha yaliyofarakana. Maisha yaliyomeguka!

Katika mambo ya kiroho, yaani makanisani na katika Huduma mbali mbali za kiroho hali nako si nzuri. Watumishi mbali mbali huingia katika migogoro kwa sababu za maslahi ya binafsi. Ni mara nyingi inapofanyika mikutano ya Injili ambayo bajeti yake ni pesa nyingi na ambazo hutolewa na wafadhili au wahubiri wageni, wachungaji hubaki katika mtafaruku wakigombea kile kilichobakia maana kila mmoja hutaka apate zaidi kuliko mwenzake. Matangazo katika television, redio pamoja na magazeti hufupishwa muda au nafasi kuliko makubaliano na kinachobakia huingia katika mifuko binafsi. Vifaa vya matangazo kwa njia ya vipaza sauti pamoja na magari kwa kazi hiyo huandikiwa kiasi tofauti cha pesa kuliko makubaliano na kinachobakia huingia mfukoni. Na wakati mwingine hali huwa ni mbaya sana kiasi cha wachungaji kupigana ngumi kwa kuwa muafaka wa namna ya kugawana ‘nyara’ unashindikana! Sasa hii ni kujitakia laana, tena ni kuivuta kwa kamba!

Vikundi vingi vya muziki wa injili huanzishwa lakini mara tu husambaratika. Ukiuliza sababu utaambiwa kuna pesa fulani ilipatikana lakini viongozi wakaitumia kibinafsi. Kwaya nyingi nzuri zimekwama kabisa kwa sababu tu ya kugombania mapato. Zipo ambazo baada ya kupata mafanikio viongozi walichota pesa na kuacha uongozi na uanakwaya kabisa. Mifano hai tunayo!

Katika mambo ya kiroho pia mambo ni mengi sana ambayo kuyaandika yote itakuwa ni kukosekana kwa kiasi. Lakini kwa ujumla hali ni mbaya mno, mno!. Na yote hii ni kwa sababu ya ubinafsi. Kila mtu hutaka kujinufaisha yeye tu kabla ya mwingine au huyo mwingine asipate kabisa.

Lakini katika Biblia tunafundishwa kuwatanguliza wengine. Na pia kila mtu kutokuangalia mambo yake tu bali ya wengine. Kila mtu anahimizwa kumhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Wafilipi 2:3-5.

Maana ya maneno hayo ni kuwa wewe unapomtanguliza mtu mwingine na yeye akakutanguliza itafika mahali wote mtakuwa mbele. Hakuna atakayekuwa amebaki nyuma. Utakapoanza kuangalia mambo ya wengine: wanapata shida gani uwasaidie, wanahitaji nini ili ufanyike sababu ya wao kufanikiwa au japo kufurahi na kisha mtu mwingine akafanya hivyo kwa ajili yako utakuta jamii nzima tumekuwa kila mtu ni mtaji kwa mwingine. Wewe utafanyika mtaji kwa mwingine na yeye atafanyika mtaji kwako na hatimaye wote tutajikuta tumefanikiwa! Hiyo  ndiyo Biblia na Ukristo kwa ujumla!

Tuhahitaji kubadilika. Jamii nzima inahitaji kubadilika. Tukibadilika nchi itapata amani ya kweli. Watu watajisikia salama maana anajua kuna mtu anahangaika kwa ajili yake kama yeye anavyohangaika kwa ajili ya wengine. Uadui utaondoka. Kila mtu atapenda awe chanzo cha furaha kwa mwingine kama ambavyo yeye amefurahishwa na mwingine. Tutatamani kumuona ndugu yako, mwajiri/mwajiriwa wako,dereva au mfanyakazi wako wa nyumbani,  jirani yako nk akitabasamu kwa kuwa amekuona! Na kinyume chake naye atajitahidi akufanye utabasamu. Maisha yatapata nuru mpya na maana mpya!

Katika Huduma ya kazi ya Bwana Mungu, kazi itasonga mbele kwa kuwa Mungu ataruhusu Baraka kwa kuwa tumeandaa mazingira ya Yeye kufanya hivyo. Watu wengi wataokoka kwa uwepo uwepo wa Haki ya Mungu itakuwa kati kati yetu. Tutabarikiwa na Bwana kwa kuwa tunawapa na wengine. Siyo rahisi kwa mchoyo kubarikiwa. Siyo rahisi kwa mbinafsi kubarikiwa. Kinachoonekana kwa wabinafsi na wachoyo ni Mafanikio tu na siyo Baraka maana mafanikio yanaweza patikana hata kwa kuiba na kuua!

Tukiwa na moyo wa kujitolea tutatamani kila mtu awe sababu ya kuwezesha jambo fulani lifanikiwe. Mfano badala ya  mtu kupiga simu hapa na kuuliza akijiunga atapata mshahara kiasi gani atapiga simu na kuuliza afanye nini ili achangie kufanikisha Huduma hii. Kila mtu akifanyika sababu ya jambo au mtu mwingine kufanikiwa, kinyume chake ni kuwa yeye atajikuta amefanikiwa kupitia mtu mwingine aliyejitahidi ili amfanikishe!

Tunahitaji kuwa na moyo wa kujitolea. Kila mtu akiwa na moyo wa kujitolea ufisadi hautakuwepo; wizi hautakuwepo. Tutaishi pamoja. Tutagawana sawa kwa sawa kilicho cha umma. Maisha ya kila siku mitaani yatabadilika. Watu hawataogopa kuwatuma watoto wao madukani kwa kuwa hata mtoto atapimiwa sawa sawa na mtu mkubwa. Wakaguzi wa mahesabu hawatakuwa na kazi kubwa maana mahesabu yote maofisini yako sahihi, hakuna kilichoghushiwa. Maendeleo katika nchi yatashamiri. Hata wale wasiojiweza, ambao wana matatizo katika maumbile yao watakuwa na matumaini mapya kwa kuwa pesa inayotolewa na wahisani kwa ajili ya kuwasaidia itawafikia kwa kadri ya makubaliano.

Faida za Moyo wa kujitolea ni nyingi. Hata wewe msomaji unaweza kuendelea kuziorodhesha na ukishafanya hivyo Omba Mungu akuwezeshe uwe na moyo wa huo ili Uwe sababu ya furaha au mafanikio kwa mtu mwingine; kwa kazi ya Mungu na kwa jamii nzima.

Na wewe unayeiba ofisini kwako, au una kipimo batili katika biashara yako au pengine unatumia mali ghafi zilizokwisha muda wake (expired) katika kutengeza mfano chakula hotelini/mgawahawani kwako; Pengine unauza madawa ya binadamu yalipo-expire maana yali-expire kwenye makabati dukani kwako, [na unaona ukitupa itakuwa hasara] geuka! Badilika leo. Baada ya kusoma ujumbe huu gundua kuwa kwa kufanya hivyo unakuwa sababu ya huzuni kwa wengi na Mungu anakuona kuwa wewe ni mkosaji na atakuhumu. Geuka. Rudi katika haki! Mwamini na kumfuata Yesu. Yeye ndiye kielelezo cha Moyo Wa Kujitolea. Alijjitolea kwa ajili kwa ajili ya uzima wa milele. Nasi twaweza kujitolea kwa ajili ya furaha na mafanikio ya mwingine.

Mungu akubariki unapochukua hatua ya kufanyia kazi ujumbe huu! Na endelea kutembelea blog hii pia mfahamishe na mtu mwingine ambaye hajaifahamu.

 

 

MAUAJI YA ALBINO NI TISHIO KWA TAIFA!

Mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kwegyir akitokwa machozi baada ya kumuona kijana Robert Tangawizi wakati alipomtembelea hospitalini Geita, mkoani Mwanza.

Tatizo la kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino, nchini Tanzania limekuwa ni tatizo linalofanya watu hao, albino, waishi kwa mashaka wakati wote.

Sababu za mauaji pamoja na mateso kwa albino, ikiwemo kukatwa viungo vya mwilini, ni kuwa suala hili linahusishwa na utafutaji wa mali/utajiri kwa kupitia njia za kishirikina. Katika tukio la hivi karibuni kijana mmoja kwa jina Robert Tangawizi (14) ambaye ni mlemavu wa ngozi alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na kisha kunyofolewa vidole vitatu.

Je, sisi kama kanisa, Wa-Kristo tunalichukuliaje suala hili na hatua gani tunatakiwa kuzichukua ili kukabiliana nalo?

-Picha na David Azaria

Viwango Ndani Ya Wokovu

 Kuna aina mbili za viwango vinavyotofautisha watu ndani ya wokovu:

 1) Kiwango cha kwanza ni kile ambacho kila mtu aliyeokoka ingefaa au anahitajika kufikia, japo wengi bado hawajafika.

Mtu ukiwa katika kiwango hiki utakubali kuwajibika 100% kwa makosa yako unapokosea. Wengi bado hawajafikia. Wengi hutafuta sababu au huwasingizia wengine. Mfano Adamu alipomlaumu Eva. Wengi wanakiri dhambi au makosa ya wenzao bila kujijua (kupitia kulaumu au kusingizia) badala ya kutubu zao.

2) Kiwango cha pili ni wachache sana wanaokifikia kwa kuamua kutafuta kufanana na Yesu. Wameamua kufa kabisa ili Yesu awe hai ndani yao, ni kigumu na wengi hawakiwezi.

Katika kiwango hiki mtu unakuwa tayari kukubali kuwajibika kwa makosa, au dhambi za mtu/watu mwingine/wengine hata kama wewe hauna kosa kabisa. Kiwango hiki kina gharama sana. Ni kiwango ambacho Yesu mwenyewe alikidhihirisha kwa kubeba, dhambi, makosa yangu, yako na ya yule. Hakuwa na makosa. Lakini alikubali kuchukua makosa yetu.

Je! Wewe uko katika kiwango kipi? Je! Uko tayari kukubali makosa yako na kuomba msamaha kwa ajili ya hayo. Je! Uko tayari kukubali kuambiwa una makosa hata wakati ambao hujakosea kabisa na ukawa tayari kuomba msamaha kwa kosa ambalo hukulitenda?

Kama watu tunaomfuata Yesu, yatupasa kufikia kiwango cha juu kabisa katika maisha ya wokovu. Kiwango cha kufanana na Yesu mwenyewe!

Mkutano wa Injili wa Strictly Gospel, Mtwara

Siku ya kwanza ya Mkutano Mwinjilisti Moses Mayila akiwasha moto

Kaka Herman Mapunda akikagua eneo la mkutano

Kaka Iqualiptus Malle wakipakia vyombo kupeleka eneo la Mkutano

Spika zikipangwa

Kaka Malle na Moses wakiweka mambo sawa

Dada Rebekah Lucas akiwasili eneo la Mkutano

Wakisogea karibu

Wakisubiria mkutano kuanza, kushoto ni Herman Mapunda na Frederick Marandu

Frederick Marandu akifungua mkutano, siku ya pili

Wakati wa kumsifu Mungu

Muimbaji Jackob akiimba

Ilikua ni furaha kwa wakazi wa Mtwara

Mwinjilisti Moses Mayila akiwasha moto siku ya pili

Injili ikipenya hadi ndani kwenye mioyo

Wenyeji wa Mtwara wakiukaribia mkutano

Kaka Iqualiptus Malle akifunga mkutano, siku ya pili

Kwa neema Strictly Gospel tulifanya mkutano wa Injili, viwanja vya Bima, Mtwara katikati ya mji. Tunamshukuru Mungu kwa kufanikisha mkutano huu, tunajipanga kwa ajili ya mikutano mingine. Pia wakazi wa Dar es salaam tunawakaribisha kwenye mkesha mkubwa wa sifa na kuabudu pamoja na maombi utakaofanyika tarehe 15 July 2011 kuanzia saa tatu Usiku, kwenye kumbi wa Bustani ya Betheli, Kimara karibu kabisa na kanisa la KKKT – Kimara, unashuka kituo cha Korogwe. Mungu awabariki

Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi 0714915424, 0752730813

Strictly Gospel yaandaa Mkesha wa Maombi na Mkutano wa Injili!

Tunawakaribisha wana SG mlio Dar es salaam na wote watakaopenda kujumuika nasi kwenye mkesha wa maombi utakaofanyika ijumaa wiki hii ya tarehe 10 June 2011 kwenye eneo la Bustani ya Betheli- Kimara karibu kabisa na Kimara KKKT.

Pia tutakua na Mkutano wa Injili tarehe 17 June 2011 mkoa wa MTWARA. Tafadhali watu walio Mtwara wajulishe wengine pia walete wagonjwa na wenye shida mbalimbali wataombewa kwa Jina la Yesu. (Mtaona matangazo yetu)

Tutumie mahitaji ya maombi, watakaohudhuria kwenye mkesha na mkutano wa injili wasiliana nasi kwa email strictlygospel@yahoo.co.uk.

Mbarikiwe!

TANZANIA, Wake Up!

Dear All,

JEREMIAH  23:23-32 (KJV)

23 Am I a God at hand, saith the Lord, and not a God afar off? 24 Can any hide himself in secret places that I shall not see him? saith the Lord. Do not I fill heaven and earth? saith the Lord. 25 I have heard what the prophets said, that prophesy lies in my name, saying, I have dreamed, I have dreamed. 26 How long shall this be in the heart of the prophets that prophesy lies? yea, they are prophets of the deceit of their own heart; 27 Which think to cause my people to forget my name by their dreams which they tell every man to his neighbour, as their fathers have forgotten my name for Baal. 28 The prophet that hath a dream, let him tell a dream; and he that hath my word, let him speak my word faithfully. What is the chaff to the wheat? saith the Lord. 29 Is not my word like as a fire? saith the Lord; and like a hammer that breaketh the rock in pieces? 30 Therefore, behold, I am against the prophets, saith the Lord, that steal my words every one from his neighbour. 31 Behold, I am against the prophets, saith the Lord, that use their tongues, and say, He saith. 32 Behold, I am against them that prophesy false dreams, saith the Lord, and do tell them, and cause my people to err by their lies, and by their lightness; yet I sent them not, nor commanded them: therefore they shall not profit this people at all, saith the Lord.

JEREHEMIA 23:23-32 (KJV)

Mwisho wa dunia hii unakaribia!

Tumesikia habari hizi mara nyingi karibu kila kizazi kwamba Bwana Yesu anakaribia kurudi na wainjilisti wengi walihubiri miaka mingi imepita kusisitiza watu watubu maana ufalme wa Mungu umekaribia!

Hili wazo na haya maneno ya kurudi kwa Bwana Yesu ni ya kweli?

Kama wakristo tunaoenda mbinguni, tunahitaji kuzungumza kwa kina kuhusu suala la kurudi kwa Bwana Yesu, tukumbuke mambo yanayotokea sasa ni kwa kasi pengine haijatokea kutokea katika vizazi vya nyuma kuna tetesi za kivita na ugaidi, uchumi wa dunia kutikiswa, matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali na manabii wa uongo wanaokuja kwa wingi katika kanisa.

Na bado tutasikia habari nyingi, ndoto na nabii mbalimbali  kuhusu kurudi kwa Bwana Yesu, nyingine zilitolewa hazikutimia na nyingine bado zinatolewa na kusambazwa dunia nzima.

Bila shaka hakuna anayeijua siku wala saa ya Kurudi kwa Bwana Yesu, lakini kitu tunachoweza kuona ni dalili za wakati.

Dalili hizi ni zipi?  Tunaziona na kusikia kwenye vyombo vya habari.

Matetemeko ya ardhi ni moja ya dalili nyingi, zaidi ya watu  10,000 wamekufa kwenye tetemeko na tsunami iliyotokea tarehe 11 March Japan.

Wiki chache zimepita tetemeko la ardhi lilitokea New Zealand, na mwaka mmoja sasa umepita tulisikia kuhusu tetemeko la ardhi la Haiti ambalo linakadiriwa kupoteza maisha ya watu 316,000.

Haya matukio na zaidi yanaweza kutokea wakati wowote sehemu yoyote, yu mkini ikatokea Tanzania, Je mioyo yetu iko tayari? na Bwana Yesu Akija leo Tuko Tayari kwenda naye?

Kama tukielewa yaliyoandikwa kwenye Biblia, huu ni wakati wa kuwa karibu sana na Mungu.

Hatujui mwisho wa dunia hii ni lini lakini mwisho wa dunia yako u karibu mno. Mungu ametupa wakati, tuutumie kwa hekima. Bwana Yesu anaweza kurudi leo!

Mungu atubariki sote!

Ujumbe wa Weekend – 1Wakorintho 2:9

Mungu ana mipango mizuri juu ya maisha yetu, anasema anajua mawazo anayotuwazia sisi kwamba ni mawazo ya amani yenye kutupa sisi matumaini.

Wakati mwingine anatushangaza anafanya zaidi ya tunavyowaza na kuhitaji. Ni Mungu anayefanya zaidi ya tunavyomuomba!

Ila sasa, hawezi kuilazimisha hiyo mipango au mawazo yake yaje kwetu kwa haraka pasipo sisi kufanya lolote! Inabidi kumtafuta kujua anasema nini juu ya mipango/mahitaji yetu (tuliyonayo tayari)

Kaa katika line ya Mungu kwa utii, sikiliza Roho wa Mungu anasema nini na kukuonya nini. Kama ilivyotokea kwa Abrahamu, tutauona uaminifu wa Mungu hata kama tunapita katika magumu yasiyotuelekeza katika mipango yetu. Mungu atasimama na kuturudisha katika mpango wake halisi na atafanya zaidi ya tuliyopanga!

“Mungu hana tatizo juu ya mipangilio yako, tatizo hatujampa hiyo mipango…anataka kusikia unataka kufanya nini ili yeye akuweke kwenye mpango wake halisi wenye utukufu zaidi”

Andika mipango yako…mwambie Mungu juu ya mipango yako. Dumu katika IMANI!

Mkesha wa Mabinti tarehe 28 Januari.

Bwana Yesu asifiwe, Ijumaa ya tarehe 28. Kutakua na mkesha wa kuombea mabinti, utafanyika Mbezi Goigi. Kuanzia saa tatu usiku. Wale wanaopenda kuhudhuria tafadhali wasiliana nasi kwa maelekezo zaidi, simu 0752730813 au tuma email strictlygospel@yahoo.co.uk

Tutaombea masuala mbalimbali yanayohusu mabinti, kama unauhitaji ama jambo unaloona linafaa kuombea siku hiyo, tafadhali tujulishe tuweke ratiba sawa! Mungu awabariki sana Mabinti wazuri.

 

2011: Mwaka Mpya na Mtu Mpya

Ndugu mpendwa, mwaka 2010 umekwisha na sasa tuko katika mwaka mwingine, mwaka mpya, 2011. Mwaka 2010 ulikuwa wa furaha, vilio, mafanikio, misiba, huzuni na kila aina ya matukio kwa watu tofauti tofauti. Matukio yote hayo, pamoja na wingi wake, yamegawanyika katika makundi mawili tu: Yenye kuleta furaha na yale yenye kuleta huzuni.  Na kila mmoja wetu alipitia katika hali fulani ambayo ni ya huzuni na/au ambayo ni ya furaha.

Unaweza kuwa mmoja wa wale waliopita katika matukio yenye kuleta huzuni. Yawezekana ulifukuzwa kazi, Ulifiwa na mpendwa wako [ndugu, mzazi, rafiki, mtoto, nk], au yawezekana ulikuwa una mchumba na ulikuwa umeweka moyo wako katika uhusiano huo kwa muda mrefu lakini ghafla akakuacha. Pengine ulikuwa katika masomo lakini baada ya mitihani matokeo hayakwenda kama ulivyotarajia. Yawezekana ulikuwa na biashara yako lakini ikafilisika. Wako wale ambao walitarajia kufikia malengo fulani kama vile kukamilisha nyumba na kuhamia lakini wakakwama, au kutafuta kazi lakini haikupatikana. Pengine ulisingiziwa jambo kwa uongo na watu wakakuchukia pasipo sababu yoyote!  Au ulipita katika majaribu mengi kwenye wokovu wako kiasi cha kukufanya uanze kupoteza tumaini. Kutokana na mambo kama hayo, moyo wako ulishuka nawe ukawa na huzuni!

Lakini wakati tunaanza mwaka huu mpya, wa 2011, Hebu tuanze na Neno hili la Mungu katika Isaya 43:18-19 lisemalo;

“Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.”

Kwa hali yoyote uliyopitia, hata iwe ni ya kuhuzunisha kiasi gani, lichukuwe Neno  hili la Mungu kama la kwako: Usikumbuke mambo hayo, wala usiyatafakari. Kutafakari matatizo yaliyopita huwa kizuizi moyoni cha kufanya mtu asipokee mawazo na matumaini mapya. Usikumbuke uchungu wa yale ambayo ulishatangaza msamaha kwayo. Usianze kutafakari jinsi ulivyokosa kazi!… Usiwaze tena jinsi ulivyipigwa vita kanisani kwa sababu ya kulisimamia Neno la Mungu. Kwa ujumla: Usitafakari lolote la zamani ambalo lilishusha  moyo wako!

Unapoingia katika mwaka huu 2011, hebu futa yote ya zamani.  Delete!  Anza kujiona wewe ni mtu mpya unayestahili mambo mapya. Mambo ya zamani yanafaa watu wa zamani. Jione wewe ni mtu mpya. Bwana yuko tayari kutenda jambo jipya kwa mtu mpya! Achilia kila kilichoumiza moyo wako na sasa umwangalie Mungu ambaye ameahidi kutenda jambo jipya;  Kwako!

Simama kwenye nafasi yako. Ishi maisha matakatifu. Tembea na Yesu maishani mwako. Neema ya Mungu inatosha kufuta kila uchungu uliokuwa umeingia moyoni kwako kutokana na mambo kwenda kwa namna ambayo ilikuhuzunisha. Ukishafuta kila kitu, andaa moyo kwa ajili ya kupokea jambo jipya. Mwamini Mungu kwa mapambazuko ya tumaini jipya  lenye kuleta furaha na amani maishani mwako.

Soma neno la Mungu. Kataa kuishi maisha ambayo yanaipungukia Neema ya Mungu. Kataa kutenda mambo yenye kumchukiza Mungu. Chukia dhambi. Kaa karibu na Mungu kwa kusoma Neno, kwa maombi na kwa kufanya kazi ya Mungu.

Kaa mahali ambapo Bwana Mungu anapotaka kutenda jambo jipya atakukuta uko kwenye nafasi sahihi! Ukishakaa kwenye nafasi sahihi Jiandae kupokea jambo jipya kutoka kwa BWANA Mungu katika mwaka huu wa 2011.

SG.

Maombi ya Uchaguzi Mkuu Tanzania: Amani Itawale

Shalom wapendwa,

Ninamshukuru Mungu kwa kumaliza kupiga kura salama na kwa amani. Tuna siku 3 hadi jumatano matokeo rasmi yatangazwe,  kama mnavyoona vyama 3 vinachuana hasa nafasi za juu.

Tumsihi Mungu kwa ajili ya Uongozi mpya na Taifa letu Tanzania:

1.Watu na vyama vipokee matokeo kwa amani, tuvunje roho zozote za mauti na umwagaji damu (1 Timothy 2: 1-2)

2.Tuwaweke wakfu chama na viongozi walioshinda watawale kwa amani na kuwajibika kwa ahadi zao, tumwombe Mungu amfunge kila aliyetoa ahadi aitimize.

3.Tuombee ustawi na amani ktk kipindi tutachoongozwa   na hii serikali mpya,  tumwombe Mungu atupe serikali mpya yenye hofu ya Mungu na kujali maslahi ya taifa la Tanzania, tumwombe Mungu ustawi wa taifa letu kiuchumi na kiroho pia ktk uongozi huu.  2Nyakati 7: 14-18 ni andiko zuri kwa kutafakari kwa viongozi tunaomuomba Mungu awaweke wakfu watuongoze miaka 5 ijayo.

Tumwombe Mungu wapendwa.

Rosemary L, Mary D na Herman M.
kny WANAMAOMBI SG

Kuelekea Uchaguzi 31 Oktoba, Jumapili!

Shalom wapendwa wa SG,
Tukiwa katika wiki ya mwisho kuelekea uchaguzi Jumapili, nikukumbushe kuwa hata kama hukuwa pamoja nasi kimaombi katika wiki Nne zilizopita, Mungu akuwezeshe kuungana nasi katika maombi ya wiki hii. Ni wiki ya muhimu sana usionyeshe kushoka, ungana nasi kuombea yafuatayo katika wiki ya
5. Kuombea uchaguzi huru,wa haki na amani.
  • Tuombee mbinu zozote za giza zinazokwenda kinyume na wagombea wateule zishindwe ktk Jina la Yesu, pamoja na wizi wa kura, majina kufutwa, wizi wa vitabu.
  • Tuombee watu wapige kura kwa haki na amani,
  • Tuombee amani baada ya matokeo ya uchaguzi na kukubalika mbele za Mungu hao viongozi waliochaguliwa
  • Tuombe wale wenye hofu ya Mungu waendelee kumtii na sio kugeuka baada ya kupata uongozi
  • Tuombe kila ahadi walizotoa viongozi wetu wafungwe kuzitimiza ktk Jina la Yesu
  • Tuombe amani na ustawi kwa taifa letu ktk kipindi hiki cha utawala wa hawa waliochaguliwa
Maandiko ya kusimama nayo au Mistari ya kukumbuka katika maombi haya ni:
- 2Nyakati 7:14, 1Samweli 2:9-10, 1 Timothy 2: 1-2 na Ebrania 12:14

Mungu akutie nguvu kusimama katika zamu yako mahali palipobomoka.
Herman Mapunda
KNY: Wanamaombi wa SG

Kuelekea uchaguzi mkuu (IV)- Mambo ya kuombea wiki hii

Shalom wapendwa ktk Bwana,

Tupo tena wiki nyingine kuelekea uchaguzi mkuu. Katika wiki hii ya nne Neno la kusimamia maombi haya kwa ujumla ni 2Nyakati 7:14. Sisi kama watu wa Mungu tukisimama na kuomba kwa ajili ya Nchi yetu Mungu ataiponya.

Mambo ya kuombea wiki hii ni:

1. Kuombea Ulinzi na amani.

Katika kuombea ulinzi na amani tuombe kwa kuzingatia vipengere vifuatavyo-

-Tuombe Mungu aweke ulinzi  kwa wagombea kwa ngazi ya Urais, Ubunge na  Udiwani

- Kuomba Ulinzi wakati wa kupiga kura kuwe na amani

- Kuomba Ulinzi wakati wa kutangaza matokeo

- Kuomba Ulinzi katika Mipaka ya Nchi yetu Zaburi 127:1

3.Tuombe Uchaguzi uwe huru na wa Haki

4.Mungu atupe viongozi wale aliowakusudia kuanzia Rais,Wabunge na  Madiwani

5.Mungu asimamie Uundwaji wa Serikali Mpya. [kwa viongozi watakaokuwa wamechaguliwa].

6.Matokeo yakubaliwe na watu wote – Rumi 13:1

7.Tuombe Mungu ahadi walizotoa na wazitimize kweli

Mungu awabariki wote na tunawatakia maombi mema.

NB:  Siku za maombi ni Jumatatu hadi Jumamosi. Jumapili kila mtu anaabudu na kushukuru. Maombi mengine ya kuwaombea wahitaji yanaendelea kama kawaida

Sauna na Rosemary
kny WANAMAOMBI SG

Kuelekea Uchaguzi Mkuu – Kuombea Macho ya Rohoni (III)

Bwana asifiwe wapendwa! Natumaini mmeianza wiki na nguvu mpya ya kumtumikia Mungu na kupambana na yule mwovu, wiki yetu hii ya tatu kuelekea uchaguzi tunaomba Mungu akatupe macho ya rohoni ili tuweze kuchagua kwa hekima ya kiMungu wagombea wetu kama  anavyosema katika Efeso 5: 15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima

Hivyo tumwombe Mungu atufunulie hiyo hekima katika uchaguzi huu, isitokee nguvu nyingine yoyote ikatuchanganya katika maamuzi yetu Efeso 1: 17-18 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo”

Mungu wetu anaweza yote na kama alivyomwezesha Yesu Kristo pale msalabani basi atuwezesha hili sisi pia.

 Efeso 1:19-23 “Na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”

NB:  Wiki ya maombi ni Jumatatu hadi Jumamosi, Jumapili kila mtu anaabudu na kushukuru. Maombi mengine ya kuwaombea wahitaji yanaendelea kama kawaida

Mungu awabariki wote
Rose Lusinde
kny WANAMAOMBI SG

Ratiba Ya Maombi Kuelekea Uchaguzi Mkuu Tanzania, (Ulinzi wa Mungu) II

Shalom wapendwa ktk Kristo, Tuko wiki ya pili kuelekea Uchaguzi Mkuu, kumekuwa na vitisho, kuhusisha nabii za kichawi na maaskofu kutoa unabii kuwa wanaona kutakuwa na umwagaji damu wakati na baada ya uchaguzi (Kati ya wiki 3-9 Oktoba 2010)
Wiki hii twende mbele za Mungu kwa ujasiri kama makuhani tukiombea ulinzi na amani ktk uchaguzi huu kama neno linavyosema ktk Ebrania 10:22-23.
Wiki ya 2 (4-9 Octoba 2010). Kuombea ulinzi wa Mungu kwa wagombea wote na kampeni zenye amani.
  • Tutawafunika kwa damu ya Yesu wagombea wote na kampeni nzima kwa ujumla
  • tutakwenda kufuta vitisho na maneno yoyote yanayokwenda kinyume na amani ya nchi kwa kutumia damu ya Yesu.
  • tutavunja maagano yote yaliyowekwa na wakuu wa nchi na nguvu za giza, makafara, matambiko ili kuharibu uchaguzi huru na wa haki. Waefeso 2:12-17, Kutoka 12:21-24
Rose Lusinde
kny WANAMAOMBI SG.

Kundi La Strictly Gospel Lajipanga!

Pichani Mchungaji Abel Orgenes Akiombea Viongozi Wa Kundi

Kundi La Strictly Gospel limejipanga kuanza kufanya kazi ya Mungu kwa vitendo. Akiongea kwenye mkutano wa wana SG uliofanyika tarehe 18/9/2010, kiongozi wa kikundi Bi. Mary Damian alisema: “Tunahitaji tuwafikie wengine, tunahitaji kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii yetu, Tuwaambie watu Waache Kufanya Maovu Wamgeukie Mungu. Tuwafikie wafungwa, wagonjwa wa hospitalini, yatima na kuwahubiri masikini habari njema za Bwana Yesu pia kuwategemeza wachungaji wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu”

Bi Mary Aliendelea Kusema “Tunahitaji watu wenye huduma na wito wa kumtumikia Mungu, japokuwa watu wako busy na majukumu mbalimbali inawezekana kuutoa muda wao hata kwa siku moja na kufanya kazi ya Mungu hali ambayo tasaidia kusimama imara na kuwa karibu  na Mungu”

Dada Rose Lusinde Kwenye Maombezi

Mkutano Huo Ulifanyika Jijini Dar es salaam Na Kuhudhuriwa na wajumbe wa kikundi cha Strictly Gospel na kupanga mikakati ya kuanza kazi mara moja Oktoba mwaka huu.  Akiongea kwenye mkutano huo, mgeni mualikwa Mchungaji Abel Orgenes Alisema “Huu ni wakati mzuri wa kumtumikia Mungu, watu wanapata fursa kupitia kundi hili pasipo kujali madhehebu yao”

Kundi la Strictly Gospel Group linataraji kuanza huduma hizo kuanzia October mwaka huu na kuanzia January 2011 Watakuwa wakifanya semina na matamasha mbalimbali ya Injili. kwa maelezo jinsi ya kujiunga na kundi hili wasiliana nasi kwa simu. +255 715 730 813, +255 752 730 813.

Waweza pia kututumia email kupitia: strictlygospel@yahoo.co.uk

Onyo!

Ole wenu nyie watumishi wa Mungu, Mungu amewapaka mafuta mumtumikie, ameweka Neno lake ndani yenu, lakini nyie msimamapo mnachanganya na maneno yenu, mnapenda sifa na kujisifu, mnatafuta kujulikana na kuonekana kwa watu kwamba hakuna zaidi kwa sababu ya ishara mnazoonesha, mmetafuta nguvu za giza kwa waganga wa kienyeji na wanajimu. Wahubiri  wa namna hiyo Ole wenu, Waimbaji na Wachungaji mnaotumia nguvu za giza Ole wenu! Tubuni la sivyo Mungu atawaondoa kwa aibu! Ezekiel 13:3; Ezekiel 13:20-23, Ezekiel 18:30, Ezekiel 34:1-2, Luka 6:26; Isaya 33:1; Jeremia 23:1-4.

Kwa heri 2009!

Mwaka 2009 unapita na hautarudi tena. Tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuupita katika hali zote tulizopitia, ziwe nzuri au mbaya. Bado Mungu yu pamoja nasi anatupigania!

Katika historia ya Muziki wa Injili Tanzania, mwaka huu tulipata pigo la kuondokewa na kipenzi chetu FANUEL SEDEKIA, imewasikitisha watu wengi lakini Jina la Bwana Libarikiwe ni fundisho kwetu tuliobaki kwamba tuwe tayari wakati wote, maana hatujui siku wala saa. Tunasubiri siku yetu ifike,kama jina lako limeandikwa kwenye kitabu cha uzima, tutaonana kwa BABA!

OIC na Mahakama ya Kadhi imetikisa sana, Hakika tumemuona Mungu akijibu maombi ya watu wake, makundi mbalimbali yalijitoa kuombea suala hili,  Ashukuriwe Mungu, sisi ni zaidi wa washindi! na tukio hili la OIC na Mahakama ya kadhi lisirudi tena kwa jina la YESU!

Tunaelea mwaka 2010 hali yawezekana isiwe shwari kama hatutasimama na kuliombea Taifa, Kanisa likisimama katika Umoja  pasipo ubinafsi na udini. Taifa litasimama. Tunao uchaguzi ambapo mambo mengi yanaendelea, kuna wanaotumia nguvu za giza ili wapate uongozi mbalimbali na kuna wanaomtumaini Mungu.

Tuanzisheni makundi mbalimbali, tujikusanye pamoja na kuombea Taifa, kujiombea sisi kwa sisi ili Mungu afungue Milango ambayo wanaoitumaini miungu wameifunga! tukimaanisha tena bila kuchoka tutakujivunia kuwa wana wa Mungu kwa jinsi Mungu atakavyounyoosha mkono wake kwetu kutusaidia!

Tusisikie tena mauaji ya Albino na kutawaliwa na watu ambao ni washirikina, kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, Taasisi mbalimbali binafsi, serikalini, wafanyabiashara, mashuleni n.k. Mungu asimame kama Mungu, wanaotumia miungu wakaaibike na kuokoka kwa jina la Yesu!

Heri ya Mwaka Mpya! Mawazo Mapya, Nguvu Mpya ya kumtumainia Bwana na mafanikio mema katika jina la BWANA wetu YESU KRISTO!