Tukiwa Kwenye Giza Nene, Kuna Mwanga Utatokea!

Kuna ushuhuda wa mama mmoja ambaye alikuwa na maumivu mengi moyoni mwake.

Ni mjane aliyelea watoto wake saba, ilikuwa ni family kubwa yenye furaha na kila sikukuu ya Krismas walikutana na kufurahia pamoja.

Lakini furaha yake ikaanza kutoweka baada ya mtoto wake wa mwisho kufariki ghafla. Alikuwa ni kijana mwenye miaka 27 pekee, huyu mama alilia sana alitamani angekufa pia, alijitesa kwa kulaumu kwanini imetokea kwa kijana wake.

Alimuomba Mungu ampe nguvu na baada ya muda mrefu kupita akakubaliana na hali kwamba kijana wake hayupo tena.

Baada ya miaka miwili kupita, kijana wake mkubwa na mkewe, wakauawa na majambazi. Imani ya mama huyu iliyumba zaidi, alimuuliza Mungu, mbona mimi? Mbona familia yangu unaiacha ipoteze sana?mchana alijiweka busy ili asahau ikifika usiku amejaa uchungu na majonzi, alianza kudhoofika mwili na kutaka kujimaliza.

Alikuwa ni mama aliyelea watoto kwa taabu, akapoteza watoto wake wawili na mkwe wake. Hivyo akajua hakuna kitakachoweza kumpa furaha tena!

Kazi yake hakuifurahia tena, marafiki zake na hata watoto wake waliobaki. Uchungu ulimuathiri kimwili na kiroho pia. Akipata nafasi ya kualikwa na marafiki zake, atatafuta sababu ya kutojumuika pamoja nao. Alijiona mpweke hana matumaini.

Alijiuliza kama atasherehekea sikukuu ya Krismas tena. Siku moja alikuwa chumbani kwake akilia “Mungu wangu Mungu wangu, Mbona umeniacha? Alijifunika uso wake kwa mikono yake, akijijibu mwenyewe “haya maswali Yesu alimuuliza Mungu alipokuwa ameteswa, amekataliwa na yuko peke yake anakufa msalabani”

Ghafla akasikia moyoni aende kanisani, ilipita miaka mingi hajaenda, (alizira) kwenda huko. Alipofika kanisani akapiga magoti na kuomba  Mungu ampe amani, ampe Neema yake aweze kuangalia vile alivyonavyo badala ya kuangalia alivyopoteza. Akashukuru kwa unyonge na kusema “Nashukuru kwa kunipa zawadi ya watoto, hata kama ilikuwa niwe nao kwa muda mfupi”

Alipokuwa akisema hivyo, ghafla akasikia sauti moyoni mwake “Siyo kwa muda mfupi vijana wako ni zawadi yangu ya milele, kwako”

Ghafla akapata jibu, kwamba maisha tunayoishi ni zawadi kutoka kwa Mungu, pia hata kama tutakufa, tutaishi milele. Akapata amani, uchungu wake ukaondoka, akafurahia kazi yake na marafiki zake. Aliweza kusherehekea sikukuu za Krismas zilizobakia na kuelezea Upendo wa Mungu kwetu, haulinganishwi na upendo wa familia zetu tulizo nazo, haulinganishwi na kitu chochote. Upendo unatoka kwa Mungu, hata tukiwa kwenye giza nene, Kuna Mwanga utatokea.

Yawezekana ndugu nawe uko na jambo linasumbua moyo wako, umepoteza sana, kazi, ndoa, watoto, nyumba nk nk. Hakuna anayeweza kuondoa uchungu wako isipokuwa Bwana Yesu Pekee, Hakuna pengine utakapopata amani, isipokuwa kwa Yesu pekee ambaye ndiye mfalme wa Amani, Upendo wa vitu vyote unapita, lakini Upendo wa Mungu, Unadumu Milele!

—twitter @MARYDAMIA

Lugha yako ya maombi ni ipi?

Maombi ya muhitaji yananoga. Wakati wa shida hata wasiofuatilia Mungu watamkumkubuka na kuita jina lake. Kuna lugha nyingi kwenye maombi, mfano wengine wanaimba, wengine husikiliza muziki wa kuabudu, wengine hunena kwa lugha, wengine wanaenda sehemu iliyotulia nje kwenye fukwe za bahari, vijito, milima ili tu waweze kuongea na Mungu hiyo yote ni jinsi ya kuingia, jinsi ya kutaka kusikika na Mungu ni Lugha ya maombi.

Kuna mambo ambayo hatuwezi kwa nguvu zetu, hatuwezi kufanya lolote, Mtunzi wa zaburi aliandika “Mchana BWANA ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami, Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu” Zaburi 42:8

Siku ya Mateso yangu nitakuita, kwa maana utaniitikia” Zaburi 86:7

Unapokuwa huna tumaini, umechoka sana ndio wakati wa kupaza sauti yako kwa Mungu na kumuita akusaidie. Imani yako itakuwa na kuendelea na Mungu atatengeneza nafasi kwako ya kukutana na nguvu zake zitakazokutana na tatizo lako kwa jinsi ambavyo hukutegemea.

Kama watoto wa Mungu wetu aliye hai, inabidi maombi yawe ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, Maombi ni mahusiano yako na Mungu, Maombi ni yanakupa nguvu ya kuingia na kupita mahali ambapo ni pagumu kwa akili za mwanadamu. Maombi ni daraja, Maombi yana faida kwetu.

Una jambo gani linalokushinda? Ni gumu kiasi gani? Hakuna jambo gumu la kumshinda Mungu.


Kama Chembe ya Haradali – I

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali  mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu” Mathayo 17:20

Kama mbegu ya haradali unavyoipanda, unaweka mbolea na kumwagilizia,  inakuwa mmea mkubwa wenye afya. Ndivyo hivyo nasi tunavyompokea Bwana Yesu, Unapanda Neno la Mungu ndani yako, unazidi kukuwa zaidi na zaidi, unapata mafunuo na mwenye kukuwa kiroho. Neno litazungumza ndani yako, Neno litakuwa chakula chako, na nguvu ya Neno itatembea ndani yako na kuhusika katika kila sehemu ya maisha yako.

Unaanza kidogo tu, kama chembe ya haradali.

Mara nyingi tunaangalia mambo mengi ya kiroho kwa nje, Ashukuriwe Mungu wetu huangalia ndani kabisa ya mioyo yetu. Sio mpaka uwe mkuubwa kwa nje, una huduma kuubwa au unahamasa kwa watu wengi ndio umekuwa mkubwa kwenye ulimwengu wa roho, Mungu anaangalia tofauti na wanadamu. Kama mtoto anavyotungwa, anazaliwa, anatambaa na baadae kukimbia!! Haanzi kukimbia mara tu anapotoka tumboni mwa mama yake! Kama chembe ya Haradali!

Nadhani wengi tunajua kuhusu Mbegu kwenye maisha yetu, tunaipanda kwanza, mti haukuwi pasipo mbegu yake kupandwa (kwenye udongo) Nasi tumeitwa kukuwa (kwenye roho) kama mfano wa mti. Msongamano unaweza kusababisha mti usikuwe, jua kali, upepo na mvua kali, lakini uwezo wa Mungu uko ndani yetu!

Imani, Kama chembe ya Haradali!

Tukimtafuta Mungu, Tutamuona!

Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji“ Zaburi 63:1

Katika safari ya kupanda mlima, tunapanda mlima unaoonekana ni mrefu sana, lakini tunaufuata. Mpaka wakati tunaumaliza na kushinda, tunajipoza kwa maji na kujipongeza kwamba ulikua mlima mkali na katikati ya mlima hapakua na sehemu kuna kijito cha maji au mahali unapoweza kupoza kiu yako, wakati mwingi ulikua ukipanda mlima masaa mengi ukiwaza jinsi gani utafurahi ukipata maji ya kunywa japo kidogo.

Huu ni mlima wa kawaida, ni sawa kabisa na wakati tunapopata jaribu. Linakua gumu na refu sana wakati mwingine unadhani huwezi kutoka, wakati mwingine unapata jaribu moja kabla halijaisha hutokeza jaribu jingine, na katika majaribu hayo hauna jinsi ambavyo unaweza kupata nafuu, hakuna jinsi unaweza kuburudika na kusahau. Mpaka jaribu likishaisha na ukiangalia ulipotoka unaweza kuona palivyokua pagumu.

Daudi alipoandika “Nafsi yangu inakuonea kiu..katika nchi kame na uchovu, isiyokua na maji” ni wakati adui zake walikua wakimuandama na Mfalme Daudi, akadhani Mungu amemuacha, akajiona yuko peke yake na hana msaada. Je umewahi kuwa mahali hapo? Una uchungu na unadhani Mungu yuko mbali nawe? kama ilivyo kwa kiu ya   kawaida, mwili wako kuna jinsi unakuambia unahitaji maji hivyo hivyo katika roho uko na kiu ambayo hakuna mwingine atakayeiondoa isipokuwa ni Mungu peke yake.

Ndiyo, ni yeye tu awezaye kuiondoa kiu yako, kama (UTAKAPOMTAFUTA) Kwa moyo wako wote (UTAMUONA) Yeremia 29:13

Jinsi gani tumjue Mungu, ni kutengeneza mahusiano na yeye, kukaa karibu yake. Kuna jinsi ambavyo tunaenenda tukidhani tunamjua Mungu, lakini tunaishi tofauti na jinsi tunavyomjua!! tunatamani wengine watuombee bila kujiombea wenyewe, kupewa mistari na kusomewa biblia pasipo kutafuta na kujisomea mwenyewe, Kila mtu anahitaji kujaribu..kutafuta Mungu..kumuona kama ndiye YEYE anayejisema NDIYE. Kama atajibu maombi yako,  kama atakuwa nawe unapomuhitaji, kama atakupa hekima, nguvu na uhakika wa maisha yako. Basi YEYE NDIYE! Na kila wakati atafanya hivyo kwa ajili yako.

Yesu anakuja kukufufua!


SIKILIZA: Lazaro alikuwa anapendwa na Bwana Yesu…lakini ujumbe ulipotumwa kwa Bwana Yesu kuhusu ugonjwa wake, Yesu hakuacha shughuli zake alizokuwa anafanya kwenda kwa Lazaro. Nataka kuongea na mtu mmoja ambaye amekuwa akimuita Bwana Yesu na akidhani Yesu hamsikii, umejaribu maombi mengi, mara nyingi, umeshirikisha watumishi wengi wakati mwingine kwa kufunga, hayo yote ili Yesu akusikie na atende jambo kwako… Bwana Yesu anakuja kukutoa mahali ulipo, subiri!

Kwa nguvu zote ulizojaribu kupata msaada kwa Bwana Yesu umeona umbali umekuwa mkubwa na unazidi kuwa mkubwa siku hadi siku unaona kama hausogei na Bwana Yesu yuko mbali….Lakini ilikuwa ni baada ya Lazaro kufariki ndiyo Yesu akaenda kwake. Ni wakati utakapofika mwisho wa kifo cha tatizo lako ndiyo Yesu atakutokezea. Kifo kinapotokea hapo hakuna tena huruma, hakuna sababu ni kifo na ni mwisho baada hayo unapelekwa kuzikwa…Tatizo unalopitia sio kifo, halitakuua, ni sababu ya ushuhuda utakaowaleta wengi kwa Kristo. Ni kwa sababu Bwana Yesu ili akainuliwe kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yako. Yesu akawaambia wanafunzi wake “Rafiki yetu Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha”  Yohana 11:11-15.

Unapita kwenye tatizo? liambie “Hautakaa sana, Yesu anakuja kufufua, utaishi tena”

Yuko njiani…hiyo ndoa itaishi tena, ile furaha itarudi tena, pesa zitajibu tena kwako…ile karama iliyokufa itafufuka tena. Familia yako itarudi tena pamoja…Ile kiu ya kumtumikia Mungu itarudi tena…miguu yako itatembea tena…afya yako itarejea tena kwa Jina la Yesu Kristo. Anakuja!!

Ili mkristo asirudie dhambi ile ile!

Wakristo wengi tumekua na tatizo la kurudia dhambi ileile ambayo tumetubu. Wengi tumeomba na kufunga mara nyingi, lakini hakuna mabadiliko. Japokua maombi na kufunga yanamfanya mkristo kuwa na nguvu za kuutiisha mwili, lakini hayatoshi pekee kukufanya uishi kwa kuepuka vishawishi vya kufanya dhambi. Na tukumbuke shetani alimjaribu Bwana Yesu baada ya kuwa amefunga kwa siku arobaini mchana na usiku. Lakini Silaha gani Bwana Yesu alitumia kumshinda shetani? Ilikua ni Neno la Mungu. Zaburi 119:11 inasema “Moyoni mwako nimeliweka Neno lako nisije nikakutenda dhambi

Warumi. 12:2 imeandikwa “wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu

Siri ya kuacha kufanya dhambi ni kufanywa upya ufahamu, nia yako. Kufanywa upya kunatokana na kulisoma Neno la Mungu. Ulishawahi kugundua? Jinsi unavyolisoma na kulisikia Neno ni ngumu kufanya dhambi. Lakini unapoacha kulisoma ile dhambi ya zamani iliyokufa inajirudia? Ndio maana Bwana Yesu anasisitiza kushika Neno yake, Neno la Mungu lijae ndani yetu. Unaweza kufunga na kuomba sana, lakini kama ufahamu wako haujakaa sawasawa kwenye Neno, shetani anaweza kukushawishi kwa wepesi sana, kurudia dhambi ile ile uliyotubu kabla!!

Mmoja anaweza kuuliza, Utawezaje kuishi bila kufanya dhambi na nitawezaje kulisoma Neno la Mungu mara kwa mara? Katika Yoshua 1:8 Imeandikwa, “kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia na kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndimo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

Hivyo basi kulitafakari na kulifanyia kazi Neno la Mungu tutafanikisha njia zetu, tutaweza kufanywa upya nia zetu. Barikiweni Mno!!!

MD

Imani yako ikimgusa Mungu, hautabaki jinsi ulivyokua!

“Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyonavyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema. Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia. Je wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amuone aliyetenda hilo. Na Yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena”. Marko 5:25-34

Bwana Yesu apewe sifa, wengi tunafahamu na kuvutiwa na historia ya mama aliyetokwa na damu miaka kumi na mbili, Leo nataka tujifunze kuhusu kumgusa Mungu, naye atuguse!

Mungu ana mipango mizuri kwetu leo na baadaye. Mungu anataka tuishi “wakati wa sasa hivi”, Hatuwezi kuishi wakati wa jana, Mungu anataka uishi maisha yako leo, kesho ina mambo yake. Lakini leo! Imani yako ikoje kwa Mungu? Je, unaweza kumgusa? Wakati Petro akitoka nje ya boti (Mathayo 14:22-31) Yesu alipomwambia “Njoo” Petro alipoona upepo, akaogopa, akaanza kuzama, Alikua na mashaka akapoteza mguso wa nguvu ya Mungu, (kutembea juu ya maji).  Tukirudi Marko 5, Huyu mwanamke aliishi wakati wa sasa ili amguse Mungu. Aliteseka miaka 12 iliyopita kwa tatizo la kutokwa damu.

Wakati ule alihangaika akitafuta matibabu sehemu mbalimbali, pengine alienda kwa waganga wa kienyeji lakini haikuwezekana kupona, aligharamia pesa nyingi na vitu pengine na ndugu walimchangia gharama mbalimbali, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Siku moja huyu mama, akasikia habari za Bwana Yesu, akapita katikati ya kusanyiko la mkutano, akawaza kumkaribia Bwana Yesu, akapiga hatua, Akamgusa. Hata leo tunaweza kupiga hatua, tunaweza kumgusa Yesu kwa imani. Yule mama alipomgusa Yesu, ndio ulikua uponyaji wake. Bwana Yesu alimgusa.

Imani ni ufunguo wa kumgusa Mungu, Umekuwa na tatizo gani limekusumbua miaka mingi? hakuna mwanadamu au chochote kitakachokusaidia isipokua Mungu tu. Lipo tumaini la ugonjwa wako, tatizo nk. Mungu peke yake ndiye anaweza kuyatatua.  Imani inahama, inagusa, inafungua…na Imani yako ndogo uliyonayo inaweza kumgusa Mungu, Hatujui yule mama alikua dhehebu gani.  Lakini aliamini akimgusa Yesu maisha yake yatabadilika

Imani ya yule mama haikuwa kubwa ya kutisha sana, alikua kama mimi na wewe tu…akachukua hatua, akaamini, akagusa. Imani yake aliiweka sawasawa, akaifanyia kazi kwa kuamini. Waebrania 10:35 “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu”

Imani yako ikimgusa Mungu, hautabaki jinsi ulivyokua!

 

Unaweza Kubadili Historia ya Maisha Yako!

Watu walioweka historia katika maisha yao walikua wa kawaida kama mimi na wewe. Kitu kilichowatofautisha na wengine ni kuona tofauti, kuwaza tofauti na kufanya tofauti, tofauti na wengine walivyoona kuwaza na kufanya.

Waebrania 11:8-10 “Kwa IMANI alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchiisiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile, Maana alikua akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”

Ibrahimu alitoka akaenda mahali ambapo hakupajua, pengine ilikua ngumu kwa jamii yake kukubaliana na wazo lake kwamba atoke aende mahali ambapo ALIPAONA ni urithi wake, yawezekana jamii yake haikuona kile Ibrahimu alichokiona, yeye aliona anaenda mahali pa urithi wake, uzao wake mkubwa na Taifa teule. Alijaa IMANI iliyompelekea kuanza kuondoka na kufanyia kazi kile alichokiona sawasawa na Neno la Bwana lilivyosema juu yake.

Haijalishi unafananaje, unajionaje, unaweza kubadili historia yako, haijalishi unatoka familia duni kiasi gani, unaweza kuchomoza na kuweka historia, haijalishi historia ya maisha yako ni mbaya namna gani, Neno la Mungu linasema umeondolewa aibu yako, unainuliwa juu kutoka mavumbini hadi jaani. Weka historia katika ukoo wako, familia yako, mahali unapofanya kazi na kila mahali unapokanyaga. Uwe na IMANI thabiti, uone tofauti na wengine wanavyoona. Kuona kabla ya mambo hayajatokea!! Matendo 20:22-24

Huwezi kuweka historia kama wewe mwenyewe unajidharau, wewe ni sura ya Mungu, wewe umeumbwa kuwa wa tofauti kuliko wengine!! fanyia kazi kile unachokiona, Kabla hujaondoka duniani, ACHILIA MAMBO!!!

Maombi ni Silaha – Waefeso 4:27

Bwana Yesu apewe sifa, Mungu anatafuta mtu anayemjua vyema, anayemtafuta Mungu kwa BIDII aliye tayari kurejesha mawasiliano yake kwa Mungu waweze kuwasiliana tena,  waweze kuzungumza. Mtu ambaye yuko tayari kusikizisha sauti yake na kumsikia Mungu akisema naye.

Maombi kwetu ni Silaha, silaha ya kuangusha na kuwasambaratisha adui zetu, tunaishi kwenye mikanganyiko mingi ya maisha, magonjwa, hofu imetanda, ndoa zinasuasua, kushindwa kufanya maamuzi sahihi nk nk

Haya mambo hayatawezekana kuyashinda tusipotengeneza mawasiliano yetu na Mungu wetu kwanza, kurejesha urafiki, kusemezana naye, kumuita aje karibu, kukaa miguuni pake na kumshirikisha yanayotusibu naye ashuke kutuokoa.  Kila tutakapoenda kwa Bwana Yesu hatatupita, atakuwa karibu nasi kutusikiliza na atujibu mahitaji yetu sawasawa na NENO lake, sawasawa na AHADI yake kwetu, sawasawa na MAPENZI yake kwetu.

Wapenzi, kumtegemea Mungu kuna faida, zaidi sana kuishi ukimsikia akisema nawe juu ya maisha yako, akikuongoza njia yako. Roho Mtakatifu atayafanya maombi yako kudhihirika kwa wazi sawa sawa na ulivyotamka “……Kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu” Efeso 3:20. Ikiwa maombi yako yamejaa NENO la Mungu, ikiwa SIFA na SHUKRANI zimejaa NENO la Mungu. Basi utayajua mapenzi ya Mungu kwako (KUSUDI).

“Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu  iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu” Warumi 12:1-2

Basi rafiki yangu, adui yetu hatujui sisi kwa vile tumeokoka, ama tuna upako mwingi wa kuhamisha milima, ama tuna waume na wake wazuri, ama tuna pesa nyingi anatujua sisi vile tunavyotambua mapenzi ya Mungu kwetu (KUSUDI) sasa nia yake ni kuua, kuharibu na kuchinja kile kilicho ndani yako ili mapenzi ya Mungu yasitimie. Vile sasa tunajua anachokitaka kwetu na tuzivae silaha zetu za vita tayari kwa kumpinga Yakobo 4:7-8, Tuamke!

Tumepewa amri ya kukanyaga nge na nyoka na nguvu zote za yule adui, Luka 10:19 na ”kupigana kwetu si juu ya damu na nyama bali juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi wa pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” Waefeso 6:1.

Barikika!!

Kilicho ndani yako ni kikubwa, kuliko maisha unayoishi!

Bwana Yesu apewe sifa, Mungu alivyoweka ndani yako ni vikubwa kuliko maisha unayoishi, Mungu ametuumba kwa mfano wake, amepuliza pumzi yake kwetu ili tuishi na kutembea kama watu wanaotoka kwenye ufalme wake.

Unaishi maisha ya taabu, magonjwa, huzuni, kulia sana, kukataliwa na kukosa matumaini. Mungu hajaviweka hivyo vitu ndani yako adui amevipanda JUU yako ili usione na kutafakari  yaliyo NDANI yako, ameweka pazia kuubwa usione mbele, amefunga ufahamu wako, usitambue na kuuona mpango mzuri, Mungu aliokupangia kabla haujazaliwa, kabla ya misingi ya ulimwengu haijawekwa. Fumbua macho yako uone kilicho NDANI yako!

Umejaa uzima, umejaa ujuzi na maarifa, umejaa mafanikio, wewe umeumbwa tofauti kwa jinsi ya ajabu na kushangaza Zaburi 139:14. Umeumbwa ili ufanikiwe kila jambo, Shetani ni simba anayeunguruma na kukutisha kwa yale unayopitia, anakufanya usione kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Usijione kama panzi, usijione haufai,Wewe ni wa thamani mno! Basi mshangilie Mungu kwa ajili ya vitu ameweka ndani yako, kwa ajili ya uzima, karama na vipaji vilivyo ndani yako, changamka sasa! Ukachipuke kwa jina la Yesu.

Yeye ni Baba Yetu!

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikua wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Mstari wa 3. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata humweka mabegani pake akifurahi” Luka 15:1-3

Bwana Yesu asifiwe wapenzi, hapo zamani kulikua na watoto wawili, Mmoja alikua mtoza ushuru na mwingine farisayo. Mtoza ushuru alitambua kwamba Mungu yupo na pia Mfarisayo alitambua Mungu yupo. Mtoza ushuru alijua japokua Mungu yupo ila yeye ni mwenye dhambi hivyo atamsamehe akiacha dhambi zake. Lakini Farisayo yeye alijiona yu mwenye haki kuliko mtoza ushuru maana aliamini ni mfuata sheria.

Kama baba anavyowaangalia watoto wake wawili ndani ya familia, wote wanajua wanapendwa na baba  yao na kutambiana, kwamba mi baba ananipenda sana maana ni mchapakazi kuliko wewe, na mwenzake anajibu nami baba ananipenda sana japokua  ni mvivu.

Katika kuyatafakari haya ninayoandika, nikautafakari upendo wa Baba kwa watoto wake, Mungu anawaonaje hao watu wawili? Anawaona kwa upendo usiokua na kifani, japokua tunawaudhi wazazi wetu wa kimwili, lakini wanatuona tuko familia moja kwenye zizi moja, japokua hatusikilizi sauti ya baba yetu anapotuonya, lakini anatuhesabu ni watoto wake, japokua tunalalamika tunapenda kujitegemea, tunatoka nje ya familia lakini bado sisi ni watoto wa baba. Kwa hiyo nimejifunza kuwa ndani ya familia haitokani na bidii yako ya kufanya kazi sana na kufuata sheria za ndani ya familia! Ila kikubwa ni BABA wa familia anakuona u wa thamani kiasi gani kwake. Mwanaye anayempenda sana  japokua ni mzinzi, mlevi, mwizi, jambazi, kahaba, bado anamuona ni mtoto wake kutoka familia moja. Yohana 3:16. Haleluya!!

Mathayo 7:11 “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, si zaidi sana atawapa mema wale wamwombao?”

Mungu aliyeziumba mbingu na nchi, Yeye ndiye Baba Yetu, Japokua tumemhuzunisha sana Zaburi 14:1, japokua tumefiwa na wazazi wetu wa kimwili yeye ni Baba wa ukweli, Tumekataliwa na kukosa ndugu na marafiki wa karibu Yeye ni Baba, Tumetukanwa na kudharauliwa Bado yupo Baba Yetu anayetuangalia kwa macho ya upendo mkubwa, amechora majina ya watoto wake kwenye kitanga cha mkono wake Isaya 49:16. Yeye ni Baba.

Kwa vile tunaye Baba Yetu, Mungu wa wote wenye mwili hakuna jambo linalomshinda tunapomwendea na kuzungumza naye, basi tumwendee yeye kama watoto wanaopendwa sana na Baba yao, tutubu tulipotoka nje ya familia, turejee kwake nyumbani, atukumbatie na kutubembeleza kwenye bega lake, tukae kwenye meza moja na yeye, tule na kunywa tukiwa ndani ya nyumba ya Baba. Yeye ni Baba Yetu!

Atakunyunyizia Maji Jangwani!!

Isaya 43:20 “……kwasababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu

Bwana Yesu Asifiwe, Mungu yupo…YAHWE ndiyo jina lake, aliyesema na Musa katika mlima wa Sinai, YUPO karibu mno kuliko mavazi uliyoyavaa. Hapendi atuone jangwani mahali palipo na ukame, hofu, kiu, kifo,kudhoofika nk. Ila anatupitisha ili tuweze kufisha/kuua kila kinachotufanya tusimsikie anaposema nasi, anatupitisha ili jina lake likatukuzwe kutoka Jangani hadi hadi kwenye eneo lenye rutuba! anataka ubaki wewe na yeye tu, mkiwa jangwani, Ili Akunyunyuzie maji  na kukunyeshea mvua ya baraka!

Basi siku ya leo ninayo habari njema kwako, Mungu anao uwezo wa kufanya njia kwenye bahari, anaweza kutoa maji jangwani na kutoa mito nyikani. Kwamba akidondosha maji yake kidogo tu! hauwi mapooza tena. Anakujaza utoshelevu!

Akikunyunyizia maji kidogo tu kwenye ndoa yako itakuwa ni amani, akinyunyizia maji kidogo tu kwenye afya yako utakua mzima mwenye afya njema, akinyunyiza maji kidogo kwenye tumbo lako utasa na kuharibika mimba unaondoka, Cancer inakimbia, HIV inaondoka, kwenye masomo yako unakua kichwa sio mkia tena, biashara yako mafanikio, kwa watoto wako wataacha njia zao mbaya.

Mkono wake sio mzito hata ashindwe kufanya sasa, anaweza kunyesha mvua kubwa ya baraka nyingi, lakini atakuonesha uweza wake Mkubwa kwa jinsi atanyunyiza maji kidogo kwako ukapokee uzima tele. Hautabaki jinsi ulivyo.

Sasa, weka kando wasiwasi wako na futa machozi yako…Mahali penye Ukame ndio mahali Mungu anataka kukutana nawe, akudondoshee maji yake ya uzima, ukachanue tena, Amka sasa ukamsifu Bwana! AMEN

Ishi toka ndani ya Moyo wako, Uwe halisi!

Mungu ametuita tuishi maisha halisi, ishi kama wewe siyo kama mwingine, ISHI KUTOKA MOYONI MWAKO, unajionaje? U Mdhaifu? U Mshindi? Inabidi uone mambo ya  kitukufu ndani yako sio mambo manyonge, jiambie, mimi nimebarikiwa. Uzima wa Mungu uko ndani yangu, toka ndani ya moyo wangu kuna chemichemi ya uzima, dunia iko moyoni mwangu, iko mikononi mwangu, Neno la Mungu linasema katika Isaya 12:3-4 “Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu. Na katika siku hiyo mtasema, mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; yatangazeni matendo yake kati ya mataifa; Litajeni jina lake kuwa limetukuka”

Neno linasema Utateka maji  kwenye visima vya wokovu..hakusema atakupa maji ila utateka maji!!

Sasa Ikiwa Bwana Yesu yuko ndani yako…NDANI YAKO..kwenye chemchemi yako unateka furaha, unateka, kupata na kutangaza amani, unateka kicheko, unatawala maisha yako kutoka ndani yako!!  UNANG’ARA!! Mungu anaiondoa aibu yako. Neno la Mungu linasema katika mithali 4:18 “Bali nija ya mwenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu”

Tamka sasa vitu vilivyo ndani yako, viachilie, vifanyie kazi. Utavifikia na kuvigusa..Uta-shine!!

Mfungulie Bwana Yesu Mlango

Tumekua na maswali mengi kuhusu maisha yetu, kwenye mahusiano yetu, kazi zetu, watoto wetu, biashara zetu na kila hali tunayopitia tumekua na maswali na kuyaancha yajae kwenye akili zetu na kupiga kelele kwenye ufahamu wetu. Lakini ninayo habari njema kwako, yawezekana umeisikia mara nyingi kuhusu kumfungulia Yesu mlango aingie moyoni mwako, fungua moyo wako mkaribishe Bwana Yesu kwenye tatizo lako. Wewe mwenyewe unajua huwezi kulitatua kwa nguvu na akili zako, basi Mwambie Bwana Yesu sasa yatosha naomba ushughulike na tatizo langu!!

Bwana Yesu yupo tayari kuingia ndani ya moyo wako, ndani kabisa ya maisha yako -NDANI YETU- ili atakapoingia NDANI afanyike msaada wako, afanye baraka kwako, ayafute machozi yako, akuponye afya yako, atakutibu majeraha yako na kukupa majibu ya maswali yako. Sasa mtakua marafiki, mtaongea pamoja na mtakula pamoja. Utakua pamoja naye na yeye pamoja nawe!! Unachotakiwa kufanya ni kuisikia sauti yake, na kukubali kumfungulia mlango, aingie NDANI katika kila eneo limekuzunguka mwambie Bwana Yesu Karibu. Ufunuo 3:20

Bwana Yesu, Ataondoa mizigo yetu!

Watu wengi imani kwa Mungu inapotea, wengine wamebeba matatizo yao ndani ya mioyo yao na kuona ni mengi sana kiasi kwamba pakitokea muujiza sehemu fulani hukimbilia kule, wengine wamewaza pengine wameumbwa kwa ajili ya kupata matatizo. Sio kweli hapo ni shetani anakuhubiria! Tatizo ni wewe mwenyewe.

Shetani ametengeneza maswali ndani yako, na jinsi mtu anavyowaza na kujiuliza maswali mengi ndio matatizo yanaongezeka na kumuelemea sana. Neno la Mungu linasema hakuna tatizo kubwa ambalo yeye hawezi kuliondoa. Hakuna ugonjwa usiopona kwa kumwamini Bwana Yesu, Hakuna lolote la kumshinda, Mungu anachotaka kuona kwetu ni uvumilivu na kukaa katika mpango wake. Huku tukimuamini Yeye anayeweza kuhamisha milima yetu!Wapenzi, neno la Mungu linasema, duniani tunayo dhiki lakini tujipe moyo maana Kristo aliushinda ulimwengu, ulimwengu wote ameubeba, ni jambo dogo sana kushughulikia tatizo lako, anaangalia moyo wako umebeba nini?

Je umebeba kutokuamini? umebeba matatizo yako? sasa inabidi moyo wako uwe mtupu! Ili yeye aingine na kuondoa yale yaliyokua yamekukosesha furaha na amani. Jipe moyo Mkuu. Mungu yupo kwa ajili yako atafanya kitu kipya kwako!

Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Mat. 11:28

Shetani ni mwizi wa mipango na malengo yetu!

Yeremia 28:11-12 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho, nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza” 

MIPANGO na MALENGO!

Bwana Yesu asifiwe wana wa Mungu, Tukisoma Neno hapo juu tutaona jinsi Mungu anavyotujali na kutuwazia mambo mema juu ya maisha yetu na ametupa uhuru kumwendea, kumuita ili yeye atusikilize. Hii ni juu Maisha yetu…kwamba anatuwazia mawazo ya amani wala si mabaya!

Kama kawaida shetani hakosi kujihudhurisha kwenye baraka zetu, anataka aibe yale Mungu amewaza kwetu. Yale unayowaza kufanya, biashara, huduma, kazi, familia yako, vipawa nk…kile Mungu ameweka kwako…shetani naye anataka akiharibu ili usifikie kwenye mpango sahihi Mungu aliokuandalia.

Lakini kama utaangalia na kulinda kile Mungu amekupatia, ile mipango na malengo yako, adui hawezi kukushinda. Maana utajua hila zake utamshinda, hatakupata. Shika sana ulichonacho!!

–Mary D–

Kwa nini tunalisoma Neno la Mungu, Neno la Mungu ni nini?

Neno la Mungu, Biblia. Ni kitabu kilicho hai! “Kwa maana neno la Mungu ni hai tena lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili, linachoma kabisa na kutenganisha nafsi na roho, viungo vya mwili na mafuta yaliyomo ndani yake; na kutambua nia na mawazo ya mioyo ya watu.” (Waebrania 4:12)

Neno la Mungu linafanya kazi kwenye roho na nafsi ya mtu anayelisikiliza na kuliamini!

Lina Nguvu, inamaana liko kazini, linafanya kazi kwa kila anayeliamini. Paulo aliwaambia Wathesalonike “Nasi tunamshukuru Mungu bila kukoma pia kwa sababu mlipo lipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu. Bali mlilipokea kama lilivyo hasa, yaani, neno la Mungu, ambalo linafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.” 1 Wathesalonike 2:13. Kwa hiyo Neno la Mungu lilifanya kazi kwenye maisha ya Wathesalonike kwa sababu walilipokea kama sio neno la mwanadamu, Kama Mungu ndio amesema nao, wakaliamini na likawa kama walivyolipokea na kuamini!!

Ni kali kuliko upanga Ukatao kuwili, linagawa nafsi na roho, kwamba linapenya kabisa na kuondoa takataka, linatenganisha kilicho cha kimungu na kisichotoka kwa Mungu, kilicho cha kweli na kisicho cha kweli, kinachotoka kwa Mungu na kisichotoka kwa Mungu. Neno linatupa uwezo wa kuhukumu mawazo ya mioyo yetu, tunapima maisha yetu na misimamo yetu kwa kutumia Neno!

Hapo mwanzo, kabla ya kuwapo kitu kingine cho chote, alikuwapo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo Neno amekuwa na Mungu. 3Vitu vyote viliumbwa na yeye, wala hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho hakukiumba. 4Uzima ulikuwa ndani yake na uzima huo ndio ulikuwa nuru ya watu. Yohana” 1:1-4

Tunajifunza, Neno alikua pamoja na Mungu naye ni Mungu “Neno akawa mwanadamu akaishi kati yetu akiwa amejaa utu kufu na kweli. Tuliona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba.17Musa alitule tea sheria kutoka kwa Mungu, lakini Yesu Kristo ametuletea neema na kweli.” Yohana 1:14,17

Kwa maana hiyo Yesu Kristo ndiye Neno la Uzima, tunamsoma Yesu, Bwana Yesu ndiye NENO!

Mungu awabariki sana.

Dhamiria Kubadilika 2011

Mambo ya zamani yaliyokukatisha tamaa, kukurudisha nyuma, kuachwa na kuumizwa moyo (2010) yaache yapite, kubali kusamehe na kuanza upya maisha yako. Pania kuwa MPYA mwenye maono MAPYA, Mabadiliko siku zote yataanza kama ukikubali kubadilika na kuchukua hatua.
 

Kila silaha itaakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utahukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, kwa jina La Yesu natamka kila silaha itakayoelekezwa kwako kukuchinja, kukuharibu na kuuua MAONO yako, MIPANGO, MAWAZO na kitakachoinuka kwa ajili ya maisha yako kishindwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakolosai 2:14

Amani Itawale!!

Hakuna kitakachozuia amani yako…ruhusu shauku ya kukaa kwenye uwepo wa Mungu, wakati mwingine tafakari ukuu wa Mungu kwenye maisha yako, usitafakari yote yanayokukosesha amani..mtafakari BWANA, kumbuka matendo makuu aliyokutendea, kumbuka shuhuda na maajabu anayoyatenda kila siku kwa watu wake…Muda wako binafsi na Mungu hata kama ni dakika chache, unabadilisha maisha yako yote, AMANI INATAWALA moyoni, unafurikwa na ukuu wa Mungu, Unajaa sifa na kila utakalofanya ni shuhuda tu, utakuwa mwepesi…Hautakumbuka yale yote, utayadharau, na kuona ulipoteza muda wako bure…Ikiwa Mungu akiangalia mkono wake, analiona jina lako pale, ikiwa ameyatanda mawingu kama pazia, na mbinguni ni kiti chake cha enzi, anayo AMANI TELE anagawa bure… Ile milima, bahari, yale mawingu yalivyokaa kwa AMANI na utulivu yeye ndiyo ameviweka, na kwavile wewe u wa thamani kwake…..AMANI ITAWALE kwako kuanzia saa hii, nyumbani kwako na ndugu zako Natamka AMANI, kazini, shuleni na kila eneo utakanyaga ni AMANI tu. Ruhusu ile shauku ya kukaa na Mungu, ile kiu…itawale. Itakuwa AMANI DAIMA…Smile as you are going through your day!!

Wafilipi 4:7 “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu

Tuombe Mungu Atupe Moyo Safi – Zaburi 51:10

“Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu”

Leo Ni Siku Njema Ambayo Bwana Ameifanya, Ni Siku Mpya…Jana Imeisha Na Kupita, Na Mambo Ya Jana Na Zamani Zile Yamepita, Na Leo Mungu Yupo Tayari Kufanya Kitu Kipya Katika Maisha Yetu. Yupo Tayari Kutufinyanga Na Kutupa Mioyo Safi, Iliyotulia! Nina Imani Wengi Tunatamani Mungu Afanye Kitu Kipya Katika Maisha Yetu Kila Eneo Linalotuzunguka!

Tunafinyangwa Kila Inapoitwa Leo, Mwambie Bwana Yesu Akufinyange, Akuumbie Moyo Safi, Akuwezeshe Katika Mambo Yako Yote, Akupe Tumaini… Ya Kale Yote Yamepita, Tazama Yamekuwa Mapya…Usikumbuke Maumivu Ya Moyo Uliyoyapata, Mateso, Magonjwa Uliyoyapata Jana Na Miaka Ilee Iliyopita… YOTE AMEPITA. Tengeneza Leo, Uwe Mpya, Mawazo Mapya, Nuru Mpya Itaingia Katika Maisha Yako. Mwambie Mungu Aumbe Moyo Safi Ndani Yako Leo. Amen!

NENO LA FARAJA – Yeremia 17:7

Mara nyingi tunaona kama matatizo yetu hayaishi, magonjwa, ndoa, kazi n.k…tunaona kama ndio yanaongezeka na hakuna dalili ya kuisha…Wakati mwingine tunajiuliza kuna uwezekano wa kupata baraka za Mungu katikati ya Hayo Matatizo? Kuna uwezekano wa kuinuliwa tena? maswali yamekuwa mengi sana kuhusu maisha yako na jinsi ya kupita katika hayo!

Mungu Anasemaje? Katika Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, ambaye BWANA ni tumaini lake”

Hivyo jambo la busara na lenye kuleta majibu, sio kumwamini mwanadamu, au akili zako au kuzama kwenye maswali yako yasiyo na majibu!…Maana kila siku utajiuliza na hautapata majibu, utaishia kukata tamaa na moyo wako kuinama.

Jibu ni kubadilisha mfumo wako wa kufikiri… fikra iamini kwamba Mungu anaweza, kwamba hakuna jambo linalomshinda, kwamba yeye ni jibu la mambo yote..unaamini kwamba yeye ndio nguvu zako. unaondoa yale mawazo yako ya kushindwa na maswali mengi..unapanda ushindi na majibu ya Neno la Mungu, unahakikisha vinapenya sana ndani yako!

Utaona badiliko, maana hautakuwa aliyeshindwa tena, bali mshindi, hautakuwa mgonjwa tena bali mwenye afya..maana umeweka tumaini lako kwa BWANA…kwa Jehova Rapha aliye mponyaji wako, kwa Jehova Shalom aliye amani yako!

Utaanza kuonekana katika hali halisi, utachangamka na kufurahi tena, tutaona tabasamu lako, …..watakushangaa. Utakuwa na nguvu mpya! utasahau taabu yako maana umeyaona majibu yako tangu zamani ulipobadili mawazo yako manyonge! ukayaona majibu yako.

Wapenzi, Kumtegemea Mungu Kuna Faida!

YESU ANAKUPENDA

Hapo mwanzo alikuwepo ROHO MTAKATIFU hata kabla ya uumbaji! Siku Mungu anaiumba dunia alitamka kwa NENO lake kila kitu kikatokea, Aliposema na iwe jua nalo likawa, Wawepo Samaki Watawale  bahari vyote vikawa!! Mwanzo 1:1-31

Kwa vile Mungu yupo pamoja nawe anaishi ndani yako. Usiogope maana tangu mwanzo hujazaliwa Mungu alikujua, roho yako ilikuwepo hata kabla ya mwili, Hivyo Basi, Roho yako iambatanishe na ROHO wa Mungu! uwe connected kwake ili afanye  njia kwako uwe halisi kwa hali ya mwilini kama Mungu alivyokukusudia. “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nilikujua, kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalumu, nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.’’ Yeremia 1:5

Ndugu, Bwana Yesu Hawezi Kukuacha, ANAKUPENDA kwa KINYWA chako umba baraka palipo na laana, amani pasipokuwa na amani uzima palipona ugonjwa shwari palipo na dhoruba.Utaona matokeo mazuri katika maisha yako.

Hauko Peke Yako, Mungu Yu Pamoja Nawe!

Ile Bidii I Wapi Kwetu? – Warumi 1:16

Pastor Paul Steven, Akiwa Mitaa Ya Posta, Dar es salaam, Akihubiri bila woga!

Nakumbuka zamani Watu Walihubiri Injili Kwa Nguvu na Mali  zao. Ulikua Ukienda  Sokoni, Mashuleni, stendi ya mabasi, kona ya njia unaona watu wanahubiri Injili, Pia watu walikua jasiri kusema wazi kwamba wameokoka. Hawaoni aibu! Hata watukanwe vipi walisimama kwenye msimamo wao kwamba wameokoka.

Lakini Siku Hizi Sioni sana hii bidii, zaidi ni mabango na habari mbaya mitaani. Na Injili Ya Kweli Imepotoshwa Na Kwa Vile Watu Wengi Hatusomi Neno La Mungu, Tunatekwa! Inasikitisha, Katika Wagalatia 1:6-10 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo…..”

Wapenzi, Tusione aibu Kusema Tumeokoka, Majirani, marafiki, Wafanyakazi wenzetu, Tunaoishi Nao wajue umeokoka, Na Matendo Yako Yakawe Ushuhuda Kwao Ili Nao Wampokee Bwana Yesu! tukiona aibu tunampa shetani nafasi ya kutushambulia na kupata mlango wa kuturudisha “Misri” Kwa sababu hatuna ujasiri wa Kumkiri Bwana Yesu Mbele  Za Watu, Atafanikiwa Kututeka Kwa Hila Zake Mbaya! Mbarikiwe.

Muite Bwana Yesu Katika Shida Yako!

“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao”. 2 Nyakati 7:14

Swali: Umemuita Bwana Yesu Katika Shida Yako? Kama Umemuita Je Unaamini/Umeamini Atakujibu?

Matokeo Ya Kumuita Yesu; Magonjwa Yanaondoka, Huzuni Huondoka, Familia Inarudishwa na Upendo,Watu Wanaokoka, Vipofu Wanaona.

Jina La Yesu Linamaanisha “NGUVU”, Muite Naye Anasikia!