Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVIII

 

Somo letu linaendelea. Katika mstari ule wa Luka 13:22 Biblia inaeleza kuhusu mtu mmoja aliyemuuliza Bwana Yesu kuhusu wingi wa watu wanaookolewa. Bwana Yesu akijibu swali hilo alisema kuwa JITAHIDINI KUINGIA KATIKA MLANGO ULIO MWEMBAMBA, KWA MAANA NAKWAMBIA KUWA WENGI WATATAKA KUINGIA LAKINI WASIWEZE. Pamoja na sababu nyingi ambazo nimekwisha kuzieleza katika masomo yaliyotangulia, leo katika Sehemu hii ya Kumi na Nane tunaendelea na sababu nyingine.

23. WATAKOSA MSINGI.

1Kor 3:10-11. “Kwa kadri ya Neema ya Mungu niliyopewa na Mungu, mimi kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake, lakini kila mtu aangalie anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani YESU  KRISTO.”

Wapendwa, leo tutauangalia Msingi. Kila nyumba unayoiona ina msingi, na misingi imetofautiana, msingi wa nyumba ya kawaida ni tofauti na msingi wa ghorofa.  Msingi wa ghorofa Moja ni tofauti na msingi wa ghorofa Kumi. Jinsi  ghorofa linavyokwenda juu  ndivyo msingi unatakiwa kwenda chini, na ndivyo inatakiwa pia wajenzi kuchanganya material kwa kipimo kinachofaa, vinginevyo ghorofa hilo litaishia kuanguka.

Hapo juu tumesoma kuwa hakuna msingi mwingine nje ya Kristo. Maana yake ni hivi ILE SABABU ILIYOKUFANYA USEME UMEOKOKA NI MHIMU SANA SANA.

Wengine waliokoka kwa sababu walikuwa wagonjwa. Walipoambiwa sasa unatakiwa kuokoka, kwa kuwa anaumwa akasema sawa, si kwamba moyo wake ulimpenda Mungu kwa kweli. Wengine walikutwa gerezani, walipoambiwa habari ya kuokoka, na wakaambiwa, ukiokoka Mungu atakutoa jela, na kwa kuwa walikuwa wamebanwa iliwalazimu wakubali na kweli Mungu aliwafanyia hivyo. Wengine walisikia wahubiri wakisema wewe unayeteseka na umaskinu njoo kwa Yesu, atakupa kile na kile, na kwa kuwa walikuwa na hali mbaya wakalazimika kufanya hivyo, na si kwamba mioyo yao ilikuwa kweli imeamua kumfuata Bwana Yesu.

Utakumbuka siku moja Yesu aliwaambia watu waliokuwa wanamfuata kuwa, MSIKITENDEE KAZI CHAKULA  KINACHOHARIKA, AKASEMA MNANIFUATA KWA SABABU  MLIKULA MIKATE MKASHIBA. Mpendwa hebu jiulize: KWA NINI UNAMFUATA YESU?

Tuendelee na somo letu katika kuuangalia MSINGI.

Katika Ebr 6:1-6 kuna maneno ambayo nimeyapanga kama ifuatavyo:

“Kwa sababu hiyo tukiacha, kuyanena mafundisho ya kwanza,  ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu,

1. TUSIWEKE MSINGI TENA WA KUZITUBIA KAZI ZISIZO NA UHAI.

2. NA WA KUWA NA IMANI KWA MUNGU.

3. NA WA MAFUNDISHO YA MABATIZO.

4. NA KUWEKEA MIKONO.

5. NA KUFUFULIWA WAFU.

6. NA HUKUMU YA MILELE.

Ndugu zangu watoto wa Mungu, Maneno hayo hapo juu  ndiyo misingi ambayo kila aliyeokoka alitakiwa kufundishwa. Hiyo ndiyo itakufanya uendelee mbele. Hata kama wewe utakuwa ni ghorofa, hautaweza kuporomoka kamwe!

Sasa tutaendelea kuyapitia moja baada ya jingine ili uweze kuelewa vizuri. Ni ombi langu kuwa Mungu wetu aliyetuokoa atatupatia Neema ya kuweza kuelewa vizuri kwa uongozi wa Roho mtakatifu.

1.Kutubia kazi ambazo hazina uhai. Ni kitendo cha mtu  kutubu dhambi zake kwa mtu. Wengine wanaita Kuungama. Vyovyote utakavyoiita lakini tunapaswa kuungama dhambi zetu kwa YESU, na pia ni kuungama na kuziacha, kutozirudia tena.

Mith 28:13 “Afichaye dhambi zake, hatafanikiwa, bali aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Mpendwa Biblia inajieleza. Tunatakiwa tuziungama na kuziacha tofauti na mafudisho mafu kuwa mtu uende kanisani kila jumapili uungame dhambi kwa mtu. Jumapili hii utaungama kwake, na jumapili ijayo, na ile ijayo, mpaka mwezi, mpaka mwaka, unaanza tena mwaka mwingine! Hapana. Nenda kwa Yesu, ungama na kuziacha, utapata rehema.

Katika Yoh 9:31 tunaona kuwa Mungu hasikii wenye dhambi. Kama utaishi na dhambi, elewa kuwa Mungu hakusikii kabisa wakati unaomba. Atakusikia pale tu ukiziungama na kuziacha, tangu hapo atakuwa anakusikia.

Mith 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu.” Unajua wapendwa, kila mtu anasema “kweli namcha Mungu” au “nampenda Mungu”. Lakini sikia, jipime hapo katika mstari huo unasema kuwa KUMCHA MUNGU NI KUCHUKIA UOVU.

Hebu tuendelee kuona jinsi ya kuungama au kutubu: Ni kutokurudia yale ambayo mtu ameamua kuyaombea msamaha kwa Mungu. Yaani ni kumaanisha kile unachokisema.

Katika Yoh 5:10-14 kuna kisa cha mtu aliyekuwa amelala miaka 38, na wengine walikuwa wanaponywa maji yanapotibuliwa, ila yeye alikuwa haponywi. Siku moja Bwana wa huruma alimkuta amelala, akamuuliza kama anataka kuwa mzima nay eye akasema HANA MTU WA KUMTIA KWENYE BIRIKA.  Nafikiri hakuwa ameelewa swali. Kama wengi wetu tusivyoelewa wakati Bwana ansema na sisi. Utakumbuka Adamu aliulizwa kwa nini UMEKULA TUNDA? AKASEMA NI YULE MWANAMKE ULIYENIPA NDIYE AMENIPA TUNDA. Kumbe kama angeulizwa kuwa “ni nani amekupa tunda ukala?” ndipo angejibu hivyo. Pamoja na kutokujibu swali sawa sawa lakini Bwana akamwambia SIMAMA  JITWIKE GODORO LAKO UENDE. Naye akasimama akajitwika godoro akaenda. Mafarisayo walipomsumbua kuwa mbona amejitwika godoro wakati ilikuwa ni sabato yeye aliwajibu kuwa yule aliyemfanya awe mzima ndiye aliyemwambia ajitwike godoro!

Kama vile wengi wetu tukiishaokoka, watu huwa wanajitokeza kuulizia wokovu wetu, kuwa kwa nini hili, kwa nini umeacha dini yetu, kwa nini hili na lile. Ebu jibu liwe ni kwamba: “YEYE aliyenifanya mzima ndiye ameniambia nijitwike godoro

Yoh 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, angalia umekuwa mzima, usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”

Nimesema kutubu au kuungama ni kuacha, ni kugeuka upande mwingine, ni kuipa dhambi mgongo na kutokuirudia tena. Unaona Yesu alivyomwambia mtu huyu aliyekuwa amelala miaka 38, kuwa akirudia litampata baya zaidi ya hilo la kulala miaka 38. Je, ni lipi hilo baya zaidi?

Biblia inasema pepo akimtoka mtu hurudi tena, akikuta aliyemfukuza hayumo, huendea wengine SABA  walio wabaya zaidi ya yule, na hali ya mtu huyo huwa mbaya zaidi. Hayo yapo katika  Math 12:43

Katika Yoh 8:1-11 tunaona mwanamke mmoja aliletwa kwa Yesu, alikuwa amekamatwa kwenye zinaa, na wanawake wa namna ile walikuwa wanapigwa kwa mawe. Siku hiyo aliletwa kwa Yesu, na Yesu alimhurumia, akawaambia wale washtaki wake kuwa yeyote asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe, na wengine wafuate. Yule mwanamke alijua kuwa amekwisha, pengine alikuwa ameisha wahi kuona wengine wakipigwa kwa mawe, akawa anasubiri mawe. Biblia inasema Yesu akainama akawa anaandika chini, hatuelewi alikuwa anaandika nini, lakini wengine husema alikuwa anaandika dhambi ya kila mtu aliyekuwa pale, na kila mmoja alipoona vile, alikimbia. Mama yule alibaki peke yake na Bwana Yesu, na katika Yohana  8:10-11 “ Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia mwanamke, wako wapi washitaki wako?

2. Kuwa na Imani kwa Mungu. Ni kukubaliana na kile ambacho Neno  la Mungu linasema, hata kama kwa macho ya kibinadamu linaonekana kuwa haliwezekani kabisa. Ndiyo maana mtume Paulo akaandika kuwa: HATUENENDI KWA KUONA, BALI TUNAENENDA KWA IMANI. Hapo ndipo wanapopatikana au walipopatikana mashujaa wa Imani. Walikubaliana na Neno la Mungu bila kujali gharama. Wengine walikubaliana mpaka wakafa bila kubadilisha msimamo wao.

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata, tazama ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani, ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

Yuda 1:5 “Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kuyajua haya yote, ya kwamba Bwana akiisha kuwaokoa watu  katika Nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasoioamini”

Ndugu yangu, wakati mwingine shetani analaumiwa bure. Hapo juu unaona kuwa Bwana akiisha kukuokoa unapaswa kumwamini kuwa anaweza kabisa kukufikisha kule alikokuahidi. Haitakiwi kumtilia mashaka maana mashaka huletwa na uoga. Uoga ukiishaingia, hofu inaingia, mashaka naye anasogea, ndipo kutetemeka nako kunakuja kwenye mwili. Utakumbuka Mungu alimwambia Gidion, katika Waamuzi 7 hivi: “watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israel wakajivuna, juu yangu wakisema, mkono wangu mwenyewe, ndio ulioniokoa, basi sasa nenda  tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema  MTU AWAYE YOTE ANAYEOGOPA NA KUTETEMEKA, ARUDI AONDOKE KATIKA MLIMA  GILIADI. NDIPO WATU ISHIRINI NA MBILI ELFU WAKARUDI, KATIKA WATU HAO, WAKABAKI WATU ELFU KUMI.

Unaona! Mungu haendi na waoga, haendi na wanaotetemeka, hao ndio unasikia wanakufa na pressure, mishtuko. Ukiishaokoka hautakiwi kuwa hivyo. Elewa siku zote kuwa VITA SI VYAKO, ELEWA ALIYEMO NDANI YAKO NI MKUU KULIKO ALIYE KATIKA DUNIA, ELEWA  UNAYAWEZA MAMBO YOTE KATIKA YEYE AKUTIAYE NGUVU.

3. Mafundisho ya Mabatizo. Mpendwa, ninafundisha Misingi au Msingi wa Mkristo, ambao ukiishakuwa ndani yako hakuna kitakachokutikisa kamwe. Kumbuka Biblia inasema kuwa mwenye haki ni jasiri kama SIMBA. Ndiyo maana Bwana wetu Yesu anaitwa  SIMBA WA KABILA YA YUDA. Hata katika Biblia kuna Neno USIOGOPE  mara idadi ya siku za mwaka mzima. Kwa hiyo kila ukiamka asubuhi kuna neno “USIOGOPE” liko hapo kukusalimia.

Kwa nini Biblia inasema MABATIZO?     Haisemi UBATIZO, ni MABATIZO. Hii inaonyesha ni Mengi.

a). Ubatizo wa Maji. Katika Math 3:13 tunamwona Bwana wetu Yesu akienda Yordani kubatizwa. Yohana akambatiza akiwa mtu mzima tofauti na siku zetu unaona watu wanabatizwa wakiwa watoto wadogo, na wanatafuta mtu anakuwa baba yake wa ubatizo. Hiyo siyo Biblia.

Katika Mark 16:14 Biblia inasema AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA. Huyo anayebatizwa anatakiwa kuamini yeye mwenyewe kwa moyo wake, ndipo abatizwe. Kinyume cha hapo tunafundisha mambo yetu wenyewe, wala siyo ya Mungu.

Rumi 6:4 “Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya UBATIZO”. Ubatizo ni ishara ya kuwa mtu amekufa, na anazikwa kwenye maji. Wapo wahubiri wengi wanasema haijalishi ni maji gani, yawe maji mengi au maji kidogo mradi umebatizwa. Mpendwa, ebu sikia maandiko haya hapa katika Math 24:4 “Yesu akajibu akawaambia ANGALIENI MTU ASIWADANGANYE”. Ni juu yangu, ni juu yako, ni juu ya kila mtu kuangalia asidanganywe. Atakayekubali kudanganywa basi atakapofika kwa Yesu, ataulizwa ilikuwaje ukafanya hivyo? Atasema nilidanganywa. Nakuambia ndugu yangu kuwa wala hakutakuwa na msamaha.

Kumbuka Mungu alimuuliza  ADAM “Kwa nini umekula tunda nililowakataza kwamba msilile?” Jibu: Mwanamke uliyenipa. ( Bado alipata adhabu}

HAWA naye akaulizwa: “Kwa nini umekula tunda?” Jibu: Nyoka alinidanganya nikala.  Pamoja na majibu hayo mazuri lakini bado hao wazazi wetu wa kwanza waliadhibiwa tu. Yule aliyepewa na mwanamke, na yule aliyedanganywa, wote waliadhibiwa!.

Hapo nilikuwa nazungumzia ubatizo wa maji mengi, maana kama Biblia inasema ni ishara ya mazishi, basi tuelewe kuwa mtu akifa huzikwa mwili mzima wala sio kichwa peke yake!

Nadhani utaniuliza swali kuwa, Sasa hao wanaobatiza watoto wadogo, wameyapata wapi hayo mafundisho? JIBU: Mark 7:6-7 “Akawaambia Isaya alitabiri vema, juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami, nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu”. Nakushauri kuwa kila unachofundishwa ebu kikague kama kweli kiko kwenye NENO la Mungu, yaani BIBLIA.

b). Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Mdo 1:6-7 “Basi walipokutanika, wakamuuliza, wakisema; Je, Bwana wakati huu ndipo unapowarudishia Israel ufalme? Akawaambia siyo kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilkia juu yenu Roho mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote na Samaria na hata mwisho wa nchi”

Roho ajapo ndani ya mtu ndiye humpa nguvu za kushinda maovu. Ndiye anakupa nguvu za kuwa shahidi.

Rumi 8:26. Hatujui kuomba ila Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Roho wa Mungu alikuwa ndani ya Yesu, ndiye huyo huyo akiwa ndani yako utaishi kama alivyoishi Yesu. Atakuombea kama alivyomwombea Yesu.

Ebr 5:7 “Yeye siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu”. Mpendwa, kama Yesu ndivyo aliishi duniani, kwa kilio kikuu, naye alisaidiwa na Roho Mtakatifu, basi mimi na wewe kama tunataka tushinde tunamhitaji Roho mtakatifu, ndiye atakaye tusaidia.

Gal 4:6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae  mioyoni mwetu, aliaye ABA yaani Baba”. Ndugu yangu pengine umeokoka, au hujaokoka, Ubatizo wa Roho mtakatifu ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo, na huyo ndiye ataendelea kukufundisha Neno la Mungu na kukuweka kwenye kweli yote.

c). Ubatizo wa Mateso. Luka 12:49-53. “Nimekuja kutupa moto duniani, na ukiwa umeishawashwa, ni nini nitakalo zaidi, lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe. Je, mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia la sivyo bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja, watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu wa kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, mwana na baba yake, mama na binti yake na binti na mamaye, mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”

Hayo yote yanaeleza jinsi safari ya Mbinguni inavyomkabili mtu peke yake bila kutegemeana. Kwa hiyo unatakiwa uiangalie Biblia inachokufundisha, kishike, kikumbatie. Wengine wanasema baba kanizuia kuokoka, mama kanizuia kuokoka, kaka, au baba mkwe. Hapana! Kila mtu atasimama mbele za Bwana atoe habari zake mwenyewe.

Bwana akasema anao ubatizo mwingine ambao ni shida kama nini kuutimiz!. Ndugu zangu, Yesu alikuja akatuachia kielelezo hapa duniani. Yaliyompata ndio yatatupata. Kama watu walimpenda, basi watatupenda tu na sisi, kama walimchukia ebu tujue kuwa yaliyompata ndiyo yatatupata. Ndio maana alisema mtu akitaka kumfuata AUBEBE MSALABA WAKE AMFUATE. Kumbuka MSALABA maana yake ni MATESO.

Ni kweli kwamba hatuwezi kusulubiwa kama alivyosulubiwa, ila tunasulubiwa kwa namna moja au nyingine.

Mdo 14:21-22. “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra, na Ikonio, na Antiokia (yafuatayo nimeyapanga mwenyewe kuwa):

    i. WAKIFANYA IMARA ROHO ZA WANAFUNZI.

    ii. WAKIWAONYA WAKAE KATIKA ILE IMANI.

   iii.WAKIWATAARIFU KUWA TUMEPASWA KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.

Ndugu zangu wapendwa, kusudi la Injili ya Kristo tunayoihubiri  linatakiwa  kuwa katika sehemu hizo 3.

Kufanya roho za wanafunzi kuwa imara. Kwa nini zifanywe Imara? Kwa kuwa baada ya kuokoka huwa tunakutana na mambo mazito kiasi kwamba kama mioyo yetu haiko imara kwa Neno la Mungu, hatuwezi kufika popote. Tutaishia kusema tu nimeokoka, lakini mwisho wa siku, unakuta moyo huo ambao haukufanywa imara umebomoka. Ndio maana kwenye milango yetu tunaweka makomeo, na tukiisha funga twaweza kulala. Na mioyo yetu inatakiwa kufanywa Imara. Ndiyo maana imeandikwa katika Mith 4:23 kuwa “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, maana huko ndiko zitokazo chemi chemi za uzima”. Na moyo unalindwa kwa NENO la Mungu. Ndiyo maana imeandikwa kuwa NENO LA KRISTO LIKAE KWA WINGI NDANI YETU.

Kazi ya 3: Kuwataarifu kuwa kuingia mbinguni ni kwa njia ya dhiki nyingi. Ndugu yangu, Biblia vile ilivyoandikwa ndivyo ilivyo. Hatupaswi kuigeuza, wala kuichakachua, au kuigoshi, imeeleza wazi wazi kuwa tutaingia kwa njia ya DHIKI NYINGI. Pata muda soma vizuri Neno katika kitabu cha MASHUJAA WA IMANI, cha Waebrania sura ile ya 11.

1Pt 2:18-23. “Enyi watumishi, watiini bwana zenu, kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wapole tu, bali nao walio wakali, maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki, kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi. Lakini kustahimili mtendapo MEMA NA KUPATA MATESO, huu ndio wema hasa mbele za Mungu, maana ndiyo mlioitiwa, maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake, yeye alipotukanwa hakurudisha matukano, alipoteswa, hakuogofya, bali alijikabidhi kwake ahukumuye kwa haki”.

Ndugu yangu, ebu soma hayo maandiko hapo juu. Mimi na wewe tujipime kwake huyo ambaye tunaambiwa tufuate nyayo zake. Je, tunazikanyaga nyayo zake kweli? Au zetu zimepanuka? Au zimepwaya?

2Timotheo 3:10-12. “Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, makusudi yangu, na Imani na uvumilivu, na upendo na saburi, tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonia, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa wataudhiwa.”

Mistari hiyo inatuonyesha jinsi watumishi wa kweli walivyoishi, ambao Biblia inasema wazi wazi  kuwa TUMEJENGWA KATIKA MSINGI WA MITUME NA MANABII. Kwa kusema hivyo ni kwamba njia waliyoipitia ndiyo tutaipitia, ambayo ndiyo ile  Bwana wetu Yesu aliipitia. Ndio maana walikuwa wakipita na kuwajulisha kuwa wakae wakijua kuwa TUTAINGIA KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.

Ndugu zangu leo nitaishia hapa katika sehemu hii ya Kumi na Nane. Misingi mingine iliyobakia, ambayo ni Kuwekea Mikono, Kufufuliwa Wafu na Hukumu ya Milele nitaielezea katika Sehemu ifuatayo ya Kumi na Tisa.

Ndugu mpendwa, ninakushauri kuwa baada ya kusoma Misingi hiyo niliyoielezea jikite katika kuitafakari na kuitendea kazi ili roho yako ipate kuwa imara katika safari hii, kwa maana ya kwamba dhiki zitakapokuja wala usishangae, na uwe na uwezo wa kupita na upate kuitwa MSHINDI!

Ubarikiwe na Bwana.

Ndugu yenu Mchungaji Samuel  Imori.

 

 

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVII

Wapedwa, leo tunaendelea na mfululizo wa somo hili. Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara nyingi kuwa sipendi nifanye kazi ya hasara, na Neno linasema pia kuwa kazi yetu sio Bure katika Bwana, yapo malipo! Katika Sehemu hii ya Kumi na Saba tutaendelea kuona sababu zaidi zitakazozuia watu kuingia mbinguni na huku wanataka!

22. WATAKUWA CHUMVI ILIYOHARIBIKA.

Math 5:13 “Ninyi ni chumvi ya dunia, lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu”

Ndugu zangu, hapa kwanza tunapewa taarifa kuwa mtu akiisha kuokoka anafanyika kuwa chumvi ya dunia hii. Chumvi ni kiungo kidogo sana lakini ni cha muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Hata mboga zingekuwa nzuri vipi mara zinapokuwa zimekosa chumvi, ukweli zinakuwa haziliki, zinakuwa hazina ladha kabisa!

Neno linaendelea kutuonyesha jinsi ambavyo tunatakiwa kujichunga kama sisi ni chumvi, ili tuendelee kuwa chumvi. Neno limesema kuwa ikitokea chumvi ikaharibika itatengenezwa kwa kuwekwa nini? Neno limesema HAIFAI kabisa!

Neno hili nalilinganisha na lile ambalo wanafunzi wa Yesu walitumwa, wakaenda kazini, mapepo yakawatii, yakawa yanatoka! Waliporudi kwa Yesu walirudi wanafurahi kweli kweli, ila Bwana akawaambia kuwa msifurahie hilo la pepo kuwatii, bali Furahini Kwa Kuwa Majina Yenu Yameandikwa Mbinguni!

Uf 3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika zake”

Bwana Yesu akawaambia wafurahi kuwa majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Na hapo anasema atakayeshinda, JINA LAKE HALITAFUTWA! Kumbe jina laweza kufutwa! Ee Mungu, Tusaidie!

Neno hili ni zito sana! Chumvi ikiharibika haitengenezeki. Zipo gereji za magari, ili magari yakiharibika yakatengenezwe, nguo ikichanika inatengenezwa. LakiniYesu anasema Chumvi ikiharibika haifai kitu!, Sasa kama ni chumvi, basi kazi yetu ni kuunga dunia hii iliyoharibika. Ndiyo maana tumeokolewa ili mahali tulipo tuwe chumvi, tuunge dunia, tulete ladha!

Vyombo

2Timoth 2:20-26 “Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya miti, na vya udongo,  vingine vina heshima na vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, (wepi?) atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa  kwa kila kazi iliyo njema.  Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na Imani, na Upendo na Amani,  pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;  akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu, na kijua kweli;  wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye,  hata kuyafanya mapenzi yake.”

Soma mistari hiyo hapo juu kwa utulivu! Roho wa Mungu atusaidie kujua kuwa tu vyombo. Kila mtu aliyeokoka ni chombo. Lakini swali linakuja hivi, Je! WEWE NI CHOMBO GANI?

Tumeona kuwa tu Chumvi, na kama tukiharibika hatuwezi kutengenezwa tena tukafaa. Na hapo tunaonyeshwa kuwa kila mtu ni CHOMBO. Ili kiwe Chombo kizuri cha kumfaa Bwana chapaswa kufanya yafuatayo:

1.  Kijitakase kwa kujitenga na hao.

2.  Kisafishwe kiwe safi.

3.  Kikimbie tamaa za ujanani.

4.  Kifuate Haki, Imani, Upendo, Amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

5.  Kiyakatae maswali ya upumbavu, yasiyo na Elimu  (ya Mungu) hayo huzaa magomvi.

Biblia inasema kuwa mtu ambaye ni chombo kimfaacho Bwana anatakiwa awasaidie wale walionaswa na Ibilisi hata kufanya mapenzi yake, wapate tena fahamu zao!. Kumbe ukimuona mtu anafanya mambo kinyume hata na ubinadamu, huyo akili zake hazipo, ameshatekwa na yule mwovu, yule mtega mitego, na amemnasa!

Pia Neno linasema chombo hicho kifuate wale wamwitao Bwana kwa Moyo Safi. Kumbe tunaweza kumwita Bwana ikawa siyo kwa Moyo safi! Siku moja Bwana aliwauliza  kuwa KWA NINI MNANIITA BWANA BWANA NA HAMTENDI NIWAAMURUYO?

Zab 119:63 “Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao,na wale wayatiio mausia yako”

Hapo tunaona mwandishi wa Zaburi anasema ni mwenzao wale wanaomcha Mungu. Ebu Jipime na wewe uone kuwa Ni mwenzao na akina nani? Company yako ni akina nani? Rafiki zako ni akina nani?

Kupangwa.   ( Vyombo hupangwa.)

Mwa 7:1-5 “Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika Safina, kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki, katika wanyama wote walio safi jitwalie saba saba, mume na mke, na katika wanyama wasio safi wawili wawili mume na muke. Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na muke, Ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku, na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wan chi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru”

Hapo juu kwanza tunamwona Nuhu akifanya kama vile BWANA alivyomwagiza. Huo ni ushindi. Je, na sisi, tunafanya kama vile tunavyoagizwa?

Tunamwona Nuhu akiingiza viumbe, au kwa sasa tunaweza tukaviita Vyombo. Kulingana na somo letu, ebu tujiulize vyombo hivi vilikubali kupangwa? Siyo kuwa vilikaa jinsi vinavyotaka, au jinsi vinavyosikia kukaa? Kumbuka vingine vinakula vingine, sasa vilikaaje pamoja? Jibu ni VILIPANGWA! Viliwekewa mipaka, paka hakula panya, simba hakula swala,  kwa kuwa Bwana alikuwa amesema kuwa ni mbegu, hivyo zikahifadhiwa!

Hapa inatufundisha nini? Kama tumekubali kuwa ni vyombo, basi tujue tu vyombo gani! Nikupe mfano: Unajenga nyumba, unaweka mlango. Na kazi ya mlango tunaijua wote! Hata tunapoingia kulala tunajua kabisa kuwa ndugu mlango yupo mahali pake. Unaonaje wakati tukiishalala bila taarifa, ndugu yetu mlango anaondoka anaenda nyumba ya jirani; Aseme “najisikia nikafunge kwa jirani”. Anaenda hata bila kuaga. Majambazi wanapita. Wanakuta mlango hayupo, wanaingia kwa ulaini kabisa, na shida zinatokea?

Hayo ndiyo yanatendeka katika Kanisa la leo kwa kuwa watu hawajijui kuwa wao ni Vyombo na ni Vyombo Gani (vya aina gani)!

Chukua hatua muulize Bwana yeye ni mwema. Muulize kuwa “mimi ni chombo gani katika nyumba yako Mungu?”

Kuna mstari mmoja kwenye Biblia Bwana alisema hivi: “WANA WA DUNIA HII WANA HEKIMA KULIKO WANA WA NURU” Inashangaza! Kwa nini iwe hivyo? Na tatitizo hili ukiliangalia sana liko kwenye makanisa yetu yale yanayosema YAMEOKOKA!

Naomba niwape mifano hai:

Haiwezekani hata siku moja mwanafunzi aamue tu kuhamia shule anayotaka. Anaamka asubuhi anasema: “Tangu leo nitakuwa nasoma shule ile” Eti aende kwa kuwa yuko la saba, aende tu aingie la saba aanze kusoma. Kwanza kiti atakachokalia ni cha nani? Nani anamjua?

Haiwezekani mwalimu aamke tu asubuhi aseme: “Tangu leo nataka kuwa nafundisha shule hii badala ya ile”,jamani,

Mnaona kile Yesu alichosema?  Wana wa dunia wana hekima. Wanajua nani amemwajiri, wanajua akitaka kuhama atafanyaje! Mbona sisi ndio tungetakiwa tujue hayo? Mbona tunasema: “Tunaye Roho wa Mungu”,  Hivyo ndivyo anatufundisha kweli?  Hata kama ni askari polisi aamke aseme “Tangu leo kituo changu cha kazi ni kile, badala ya hiki” Uliona wapi?

Nimalizie Sehemu hii ya Kumi na Saba, nikisema hivi: Elewa wewe na mimi ni Chumvi ya dunia. Pia Elewa kuwa wewe na mimi ni vyombo katika nyumba ya Mungu, hapo Mungu alipokuweka, sio unapotaka wewe!

Nawatakia kutafakari kwema unaposoma ujumbe huu, ili ufike mahali macho yako yafunguke ujue yakupasayo kufanya katika zamani tulizo nazo!

Efeso 1:18-19 “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake, jinsi lilivyo, na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo,na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo, kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake

Amina!

Ndimi ndugu yenu katika Bwana Mch. Samuel  Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVI

Wapendwa leo, kwa Neema ya Mungu, tunaendelea na lile somo la Msitari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia ambapo tunaendelea kuona sababu zaidi zitakazowafanya watu washindwe kuingia mbinguni huku wakiwa wanataka. Tujumuike pamoja katika Sehemu hii ya 16 ambayo inaanza na sababu ya Ishirini na moja (21), ya mambo yatakayosababisha watu wengi wasiingie mbinguni.

 21. WATAFARAKANA NA WAZAZI WAO.

Mal 4:4-6 Ikumbukeni Torati ya Musa, Mtumishi wangu, nilivyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israel wote, naam Amri na Hukumu. Angalieni nitawapelekea Eliya Nabii, Kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya, Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee  baba zao ili nisije nikaipiga dunia kwa laana”.

Neno linasema wazi wazi kuwa Eliya atatumwa, na utakubaliana nami kuwa alipokuja hawakufahamu kama ndiye aliyekuwa ametumwa:

Luka 1:17 – “Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake,ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto,na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa”

Hapo juu anazungumza habari za Yohana Mbatizaji: Kazi kubwa aliyokuja kufanya; kwanza anasema atakuja kwa roho ya Eliya, Ageuze mioyo ya baba iwaelekee watoto, Awatilie waasi akili za wenye haki, (watoto walioasi baba zao, awatilie akili za wenye haki) halafu  Amwekee Bwana tayari watu waliotengenezwa!

Mathayo 11: 13-14, “Kwa maana Manabii wote walitabiri mpaka wakati wa Yohana, Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja, mwenye maskio asikie”

Hapo kuna mambo mazito kweli: “alishakuja”, na “mwenye masikio asikie”. Kumbe twaweza kuwa na masikio na tusisikie!

Efeso 6:1-3, “Enyi watoto watiini wazawi wenu katika Bwana maana hii ndiyo haki,  Waheshimu baba yako na mama yako, amri hii ndiyo amri ya kwanza, yenye ahadi, upate keri, ukae siku nyingi katika dunia.Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, Bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana”

Ndugu zangu, Biblia inasema kabisa kuwa kwa kuwaheshimu wazazi wetu kuna kitu tunapata: HERI pamoja na MIAKA MINGI. Pia wazazi wameambiwa wasiwachokoze watoto wao, ila Wawalee katika adabu, na katika maonyo ya Bwana( Biblia). Wengi wanakataa kulelewa, na wanachofanya ni kukimbia nyumbani; wanatafuta mahali ambapo hawatakemewa, hawataelekezwa; mahali ambapo watafanya wanavyotaka na mtu asiwaulize! Wanakimbia wazazi wao; wanatafuta baba wa kambo! Wengine kwa unafiki wanasema wanawapenda baba zao wa kambo, huku baba zao waliowazaa wapo!

Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa siku tulizo nazo. Biblia inaposema WAZAZI maana yake ni wote wa aina mbili, yaani wa KIMWILI na wa KIROHO pia.

1Kor 4:14-17, “Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha, bali kuwaonya kama watoto niwapendao, kwa maana ijapokuwa mna waalimu kumi elfu, katika Kristo, walakini hamna baba wengi, maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Basi nawasihi mnifuate mimi, kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali, katika kila kanisa”

Hapo juu mtume Paulo anaeleza nini?

Anasema wazi wazi kuwa kumbe naweza kuwa na waalimu 10,000 lakini baba lazima yupo mmoja tu aliyenizaa katika Injili!  Huo ni ukweli usiopingika. Lakini leo hii ukimuuliza mtu Je, Unaye baba yako wa Imani? Wapo wengine watasema “tulikosana naye, nikahama kutoka kanisani, nikajiunga na kanisa lingine!” Wengine waliisha badili mara nyingi tu, sababu walikosana naye, na wako safarini kuelekea Mbinguni! Ndugu zangu, mjue kabisa kuwa tunapambana na shetani ambaye ana sifa zifuatazo: Ni mjanja, ni mkongwe wa vita, anajua namna ya kujigeuza geuza!

2Kor 11:14-15, “Wala si ajabu, shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru, basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza, wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawa sawa na kazi zao?”

Hapa shetani amecheza kweli: mtu aliyekuzaa kwa Injili, akakubatiza, akakulea kwa miaka kadhaa, huyo ni baba yako, ni ukweli usiopingika. lakini baada ya muda, pengine alikukemea, alikukataza hiki na kile, wewe ukaona hapana, yako makanisa mengi mimi nahama! Na kweli ukaondoka, ukaenda mahali, huyo wala hakujui, akakupokea, akakupa na cheo, yeye ati ni mzuri kuliko baba yako? Unaiona roho ya unafki inavyofanya kazi?

Pia mtu anapokuja kanisani, ndugu zangu watumishi wa Mungu, Ebu muulize kama anakotoka ni salama! Usimpokee tu na kumpatia cheo. Mwambie akuletee barua ya anakotoka. Mimi huwa nasema hivi, kama mtoto anataka kuhamia kanisa lingine, hakuna tatizo BALI amueleze baba yake kuwa sasa anajisikia kuhamia kanisa fulani kwa sababu hii na hii na ile. Amuelezee tu! Ninaamini kama  naye ana Roho wa Mungu kweli, na anayoyaeleza yanatosha, naamini atampatia barua nzuri tu, ya upendo, aipeleke kwenye kituo chake kipya! Wala hautakuwepo ugomvi kati ya Mchungaji huyu na yule, wakigombea washirika!

Tukumbuke kuwa wengine ni CHUMVI ILIYOHARIBIKA, haitatengenezeka. Ikikaa hapa kidogo, inaondoka inaelekea kwingine. Wengine wanazunguka tu kama vile Shetani. Maana alipoulizwa na Bwana kuwa anatoka wapi yeye, Shetani, alijibu:  “Natoka kuzunguka-zunguka duniani na kutembea huku na huku humo” Ayubu 1:7

Wengine kazi zao ni kuzunguka tu, hakuna kitu wanafanya . Huwa wanatafuta mahali ambapo hakuna kazi ya kuwabana. Mfano kanisa likianza ujenzi tu, au michango yoyote basi hiyo ni tiketi, wanaondoka, wanatafuta mahali ambapo pameshatengenezwa, wanafika tu ni kukaa, maana kila kitu kipo, jengo, viti, vyombo, n.k!

2Tim 1:15, “Waijua habari hii kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene

Hayo ni maneno ya mtume Paul Mtume akiwataja hawa wapendwa kuwa nao walimwepuka. Yawezekana na Baba yako wa kiroho ndivyo anavyokutaja. Hebu fikiria kidogo: wewe baba yako wa kiroho anakutajaje?

2Tim 1:16-18, “Bwana awape Rehema wale walio wa mlango wa ONESIFORO, maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu, bali alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii akanipata. Bwana na ampe kuona Rehema machoni pa Bwana siku ile, na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso wewe unajua sana”

Ebu jipime mpendwa, umemtafuta baba yako kwa bidii? au yeye ndiye anakutafuta kwa bidii? Wakati mwingine anakupigia simu mpaka inakata, na unasema unampenda Mungu. Unajua kuna wakati Wayahudi walisema wanampenda Mungu, na huku hawamtaki Yesu. Hayo ndiyo yanatendeka leo!

Kumbuka: Kama  YOHANA alikuja kwa Roho ya Eliya, Hata leo watu wanakuja kwa roho ya  FIGELO, na HERMOGENE. pamoja na  ONESFORO!

2Tim 4:10-16, “Maana DEMA aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia, Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yuko hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi. Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso. Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu hasa vile vya ngozi. Iskanda,  mfua shaba, alionyesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake. Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kile neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina!”

Yapo mengi ya kujifunza ndugu zangu. Tusikae tukajidhania tuko salama kumbe matendo yetu ni yale waliyoyafanya hao ndugu zetu waliotajwa hapo juu. Mtume Paulo amewataja wazi wazi. Hata kama nawe baba yako ndivyo anavyokutaja. Hujachelewa! Kumbuka Mwana Mpotevu alipita nyumba nyingi wakati anarudi kwa baba yake, mpaka alipofika kwa baba yake, na baba alimpokea na shangwe, nderemo, vifijo, sherehe, vikafanyika!

Mw 9:20-27, “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu, akanywa divai akalewa, akawa uchi katika hema yake. Hamu , baba wa  Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao, wote wawili, wakaenda kinyume nyume, wakaufunika uchi wa baba yao, nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka, katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea, akasema, Na alaaniwe Kanaani, atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe Bwana Mungu wa Shemu, na Kanaani awe mtumwa wake. Mungu akamnafisishe Yafethi, na akae katika hema za Shemu na Kanaani awe mtumwa wake”

Ndugu zangu, nimeeleza jinsi Moyo wa Mungu siku tulizo naazo unavyolia ili watu waikimbie laana. Lakini wataikimbia kwa njia gani?

Neno linasema katika Malaki 4  kuwa “asijeakaipiga dunia kwa laana”. Napenda tukumbuke kuwa Mungu analitengeneza Kanisa litakalorithi uzima wa milele. Lisilo na ila wala kunyanzi. Kama tunaelekea huko, basi tukubaliane na Neno la Mungu. wako watu hawasemezani, hawasalimiani, hao ni pamoja na baba na watoto wao. Lakini bado kila mmoja anajihesabia haki, wengine wanasema “yeye ndiye aliyenikosea” wengine wanasema “mimi nimemsamehe lakini sitasahau”.

Ndugu zangu turudi kwenye Neno. Mbingu ni ya wale walioshinda. Ebu tuvipige vita vizuri vya Imani, tukiwatanguliza wenzetu. Yale tunayopenda tutendewe na watu nasi tuwatendee na yale ambayo hatupendi kutendewa nasi tusiwatendee wenzetu!

Nuhu alilewa, na akawa uchi. Mtoto wake alipomuona akiwa uchi, alienda kuwaelezea wadogo zake. Mara ngapi washirika wakubwa, wengine wazee, mashemasi, walipouona uchi (madhaifu) wa baba zao waliondoka na kwenda kuelezea wadogo zao? SHEMU na YAFETHI  walikuwa na akili nzuri, walikwenda kinyume cha taratibu, wakatembea kinyume nyume ili kuficha uchi wa baba yao, tena hawakutaka hata kuuona. Wangapi leo wanashangilia kwa kuwa uchi wa baba yao umeonekana??

Napenda nimalize nikisema hivi, ebu tuelewe kuwa aliyetuita ni mmoja, ndiye Amiri jeshi wetu. Tukumbuke kuwa wakati Sauli anatawala, kuna siku vita ilikuwa kali mwisho aliuawa pamoja na mtoto wake, japo alikuwa akimwinda Daud amuue, kwa lugha nyingine alikuwa adui yake. Lakini Daud hakushangilia kifo cha Sauli badala yake alionya akasema jambo lile lisihibiriwe kwa Wafilisti, wangewasimanga! [2Sam 1:20]. Lakini siku tulizonazo hatujui wapi tusemee hili, na wapi tusemee lile!

Ni ombi langu kuwa watoto watajiandaa kurudi kwenda kwa baba zao, na ninaamini kwa Ma-baba hawatakuwa na shida kusema: “MWANANGU KARIBU NYUMBANI!”

Mungu awabariki!

Ndugu yenu, Mchungaji Samuel Imori.

Ufanyeje Ili Maono Uliyoonyeshwa Na Mungu Yatimie?

Habakuki 2:2Bwana akanijibu, akasema, iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye atake kuisoma kama maji, maana njozi hii ni kwa wakati uliomriwa, inafanya haraka, ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; Ijapo kawia ingojee, kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Ndugu zangu, leo tunalo somo lisemalo kuwa, UFANYEJE ILI MAONO ULIOONYESHWA NA MUNGU YATIMIE? Mungu wetu husema nasi kwa njia mbali mbali, kwa ndoto, kwa maono, kwa Neno lake, kwa kutumia Watumishi wake, Malaika, viumbe mbali mbali, hata Punda, n.k. Na akiishasema nasi kuna vitu ambavyo tunatakiwa kufanya ili yapate kutimia yale aliyosema nasi. Kuna wengine akiishasema nao, muda mrefu hupita; wakingojea na  kungojea, na hata wakati mwingine wengine huwa wanakufa bila kuyaona yakitimia. Lakini tunajua kuwa Mungu wetu kamwe hawezi kusema uongo, yeye akiishasema ni lazima atimize yale yote aliyoyasema.

Katika somo hili nitakupatia mambo mbali mbali ambayo unatakiwa kuyafanya ili usababishe yale ulioambiwa yapate kutimia. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

1.Liandike neno hilo ambalo Bwana Mungu amekwambia. Andika kwenye daftari, kitabu au mahali popote ambapo halitapotea. Litunze mpaka hapo litakapotimia. [Hab 2:2].

Dan 9:2  “Katika mwaka wa kumiliki kwake, mimi Daniel kwa kuvisoma vitabu, nilifahamu hesabu ya miaka, ambayo Neno la Bwana lilimjia Yeremiah Nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalem, yaani  miaka sabini

Unaona hapo! Nabii Yeremiah aliandika kile ambacho Bwana Mungu alikuwa amemuonyesha, na Daniel aliposoma alifahamu miaka. Na wakati anasoma kufahamu tayari Israel walikuwa wamekaa utumwani miaka 30 zaidi ya walivyokuwa wametakiwa kukaa. Kwa hiyo tuhakikishe kuwa tunaandika yale Bwana anayosema nasi.

2. Jenga Madhabahu baada ya kuwa Bwana amesema na wewe.

Mwanzo 8:20-21 “Nuhu akamjengea Bwana madhabahu, akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliyesafi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu, Bwana akasikia harufu ya kumridhisha. Bwana akasema moyo moyoni, sitalaani Nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya mwanadamu maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai, kama nilivyofanya.”

Katika Biblia imeandikwa, MHESHIMU BWANA KWA MALI ZAKO. Mungu akiishasema na wewe unafanyaje? Maana unatakiwa ushukuru kwa kile ulichosikia akikuambia, yaani kwa vyovyote utasema asante, sasa unafanya nini ili kuonyesha hiyo asante yako? Nuhu alipotoa sadaka hiyo harufu ilimfikia, na unaona akamfanya Mungu aseme maneno, aahidi kutoharibu dunia tena kwa maji!

Mwz 28:16-22 “Yakobo akaamka katika usingizi, akasema kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua, naye akaogopa akasema, mahali hapa panatisha kama nini, bila shaka hii ni nyumba ya Mungu. napo ndipo lango la Mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake. Akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake, akaita jina la mahali pale Betheli, lakini mji huo hapo mwanzo uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae, nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu, na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe fungu la kumi”

Ninachotaka tujifunze hapa ni kwamba mtu yeyote mwenye akili timamu anaposemeshwa na Baba yake hawezi kukaa kimya tu bila kufanya chochote, bila kusema chochote. Unaona hapo, baada ya Mungu kusema na Yakobo, ilibidi Yakobo asimamishe Jiwe lile, akalimiminia mafuta. Haikutosha hiyo akatamka akitoa Nadhiri kuwa kweli Mungu akinilinda akanipa nguo, akanipa chakula, nikarudi salama, NITAMTOLEA FUNGU LA KUMI KWA KILA ATAKACHONIPA. Pia aliiheshimu mno mahali pale, akapaita LANGO LA MBINGUNI, Nyumba ya Mungu.

Kumbuka, ni mara ngapi watu wengi wanahudumiwa na Mungu katika Madhabahu mbali mbali, na kesho yake yule mtu huondoka na kuendea madhabahu zingine mbali mbali. Nikupe angalizo hapa kuwa angalia madhabahu ambayo BWANA alikutana na wewe, aliyosema nawe.  Wengine hawapo kabisa, Pengine alisema nawe ukiwa  THIATIRA, lakini uliishasonga leo upo  FILADEFIA. Soma vizuri maandiko. Unafikiri ni kwa nini Biblia inasema “kwa Kanisa la THIATIRA Andika. . .! “; “Kwa kanisa la FILADEFIA  Andika. . . .”

3. Usimshirikishe kila mtu hayo Mungu aliyokuambia.

Watu wengi kwa kutokuelewa, tumefikiria kuwa ni sawa kumshirikisha kila mtu tunaye kutana naye, maono au ujumbe aliotuambia Mungu. Hii si sahihi. Kuna madhara makubwa sana kwa jambo hili. Ngoja nikueleze na ninaamini utaelewa:

Zab 69:4  “Wanaonichukia bure ni wengi kama nywele za kichwa changu”.

Naomba nikukumbushe, uwe unajua au hujui, maadui zako ni wengi kama nywele zako.,Huwawezi kuwajua wote. Hivyo ukimwambia kila mtu utajikuta umeshamwambia hata adui yako maana huwajui wote.

Mwanzo 37:5-8 “Yusuph akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia, akawaambia, Tafadhalini sikieni, ndoto hii niliyoiota, Tazama sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama miganda yenu ikazunguka, ikainama mbele ya mganda wangu, Ndugu zake wakamwambia, Je kweli wewe utatumiliki sasa? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake na kwa ajili ya maneno yake”

Fuatilia uone shida zilizompata baadaye. Kwa usalama wako, usimwambie kila mtu maono yako, au jinsi Mungu anavyotaka kukufanyia. Wengine hujifanya rafiki, lakini ukweli ni kwamba ni WACHAWI. Wanakuja kwako kutafuta wakulogeje. Ninaamini kuwa hakuna uchawi kwa mtu wa Mungu! Lakini unapokuwa umemshirikisha mtu ambaye hakutakii mema, mtu ambaye ni adui yako bila wewe kujua, utakuwa unahatarisha maisha yako yote: ya Kiroho, na ya Kimwili pia.

1Kor 4:1-2 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu, hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ni mtu aonekane kuwa mwaminifu”

Hapo juu mtume Paulo anaeleza kuwa Mungu wetu anazo siri zake, ambazo huwafunulia watu kadhaa, si watu wote. Sasa anapokuwa amekufunulia, au ameamua kukufanyia jambo hamwambii kila mtu. Hukuambia wewe tu na unachotakiwa kufanya ni kutunza siri hiyo, maana si kila mtu atakayekuelewa.

Mifano

Mariamu: Malaika alimwambia Mariamu kuwa atazaa mtoto BILA MUME,  Kama Mariamu angeondoka hapo awe anamwambia kila mtu kuwa una habari?mimi nitazaa mtoto bila mume! “. .   Fikiri ingekuwaje?

Petro: Aliitwa na Yesu atembee juu ya maji amfuate na Petro akaweza kutembea. Lakini kama angemuuliza Marko, au Mathayo,  au Yuda, swali kuwa “Yesu ananiita niende kwake juu ya maji, mnanishaurije?” Unaonaje, angepewa jibu gani?  Wengine wangemwambia wala usijaribu, utazama, huwezi! Unaona? Hiyo ni kwa sababu Si wengi wanaojua au wanaweza kujua kile alichokuambia Mungu au kile alichokuahidi. Kwa hiyo kama Mungu hajakuambia umwambie na mtu mwingine basi Tunza siri hiyo!

1Kor 1:26 “Kwa maana ndugu zangu angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye Hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa”

Unaona Biblia inajieleza kuwa si wengi wanaoweza kuelewa kile utakachokisema, wengine mpaka yaje yatokee wayaone ndipo waamini maana hawaenendi kwa Imani, bali wanaenenda kwa kuona, hata kama wameokoka. Wengine ni wakatisha tamaa wazuri kweli. Wengine ukiwaeleza ni kuwafanya watamke kinyume cha vile unavyotegemea kwa kuwa hawawezi kabisa kuelewa unachowaambia. Ukichanganya yote hayo unaweza kuona kuwa matokeo yake hayawezi kuwa mazuri.

Lakini kuna mtu ambaye anastahili au anafaa kuambiwa au kushirikisha jambo ambalo Mungu amekuambia: Gal 6:6 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote” Mkufunzi ndiye mtu pekee ambaye nitakushauri umshirikishe mambo yako. Nasema mkufunzi kwa kuwa hufundishwi na kila mtu. Kama unafundishwa na kila mtu nakuonea huruma maana huyu atakuambia hivi, yule naye atakuambia hivi, na mwingine naye atakwambia vile na mwisho wa siku utatembea kama nyoka!

Malaki 2:7 “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa,tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake, kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi” 

Mpendwa, kuna wajumbe wengi. Wapo waliotumwa na watu mbali mbali, wapo waliotumwa na vitu mbali mbali. Lakini wako WAJUMBE WA BWANA WA MAJESHI. Hao ndio wanatakiwa kutufundisha sheria za Bwana, hao ndio tunatakiwa kutafuta maarifa vinywani mwao. Na hao ndio tunatakiwa kuwashirikisha kile tulichoambiwa na Bwana, na wao watatushauri, watatuelekeza kwa usahihi jambo la kufanya.

4. Mkumbushe Bwana kile alichokuambia kuwa atafanya.

Isaya 43:26 “Unikumbushe, na Tuhojiane, eleza mambo yako, upate kupewa haki yako” Bwana wetu ni Mungu asiye sahau kamwe. Sasa anaposema unikumbushe hana maana kuwa huwa amesahau, huwa anataka kuona kama unajua haki zako, anataka uzitaje, na ukumbuke kuzitaja bila kizidisha, bila kupunguza. Maana ukipunguza basi hawezi kufanya maana hakusema hivyo, ukizidisha hawezi kufanya pia maana hakusema hivyo. Kama vile alivyoweka ulinzi katika Biblia ili mtu asipunguze, wala asiongeze, ndivyo anaangalia kwa bidii kile alichokisema ili kisipunguzwe wala kuongezwa. Ndiyo maana nasisitiza kuwa Mungu anaposema nawe hebu andika vile vile alivyo sema, bila kuongeza wala kupunguza chochote.

Kumb 4:2 “Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu niwaamuruzo” 

Mith 30:6 “Usiongeze neno katika maneno yake, asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo”.

Uf 22:18-19 “Namshuhudiza kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, mtu yeyote akiyaongeza, Mungu atamuongezea hayo mapigo, yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu yeyote akiondoa lolote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamuondolea sehemu yake, katika ule mti wa uzima, na ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki”

Namalizia somo hili kwa kusema kuwa Mungu wetu ni mwaminifu ambaye kamwe hawezi kusema uongo, lolote alilolisema lazima alitimize, ila tunachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wetu. Tukitimiza wajibu wetu yeye atatimiza wajibu wake kulingana na lile alilotuambia kuwa atatimiza au atatufanyia.

Nawatakia kila la heri katika safari yetu ya kuelekea kwetu nyumbani kwa Baba yetu, kwenye raha ya milele.

Ndugu yenu Mch. Samuel  Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XV

“Yesu akawaambia jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze” Luka 13:24

Nimeendelea kueleza somo hili kirefu, jinsi Bwana Yesu alivyosema wengi watataka kuingia wasiweze, kwa lugha nyingine, katika wale watakaojaribu kuingia wapo ambao hawataweza, na wapo ambao wataweza. Leo tena nimeona niendelee kuweka wazi vitu vitavyowafanya wasiweze na huku wanataka.

20. HAWATAHESABU GHARAMA.

Tukisoma katika Luka 14:25-35 tunakuta maandiko yanayosema kuwa “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka akawaambia; “kama mtu akija kwangu, naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake, naam na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ni ninyi, kama akitaka kujenga mnara,  asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia? Asije akashindwa  kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?Na kama akiona hawezi hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.Kadhalika kila mmoja wenu asipoacha vyote alivyonavyo, hawezi kuwamwanafunzi wangu.”

Tumeona mambo mengi ambayo Bwana Yesu akiyataja hapo. Sitaeleza kila jambo ila ona katika mistari hiyo michache ametaja jambo fulani mara 3, na jambo hilo ni “Hawezi kuwa mwanafunzi wangu”. Kuwa mwanafunzi wa Yesu kuna masharti yake mpendwa, wengi wamekataa kuwa Wanafunzi, wamekuwa ni Makusanyiko.

Kuwa mwanafunzi ni kukubali kufundishwa, mpaka umfanane Bwana Yesu. Mtume Petro ni mfano mzuri katika jambo hili. Hata wakati Bwana alipokuwa amekamatwa yeye  alijaribu kujificha asitambulike, lakini waliokuwa pembeni walimwambia Hata kutembea, na kusema kulikuwa kunamtambulisha kuwa ni mmoja wa wanafunzi wake. Je, Kuna jambo gani linalotutambulisha?

Watu wengi waliokoka kama ajali, walijikuta wameamua kumfuata Yesu, na hapo ni baada ya kusikia wahubiri wakisema Njoni mtajirike, Anayetaka gari: nyumba, pesa  aje tumwombee! Kwa hiyo watu wakafuata hayo. Wanapofikia wakae wafundishwe Neno la Mungu, inaonekana wanapotezewa muda, maana kilichowaleta ni vitu vya mwilini.

Mdo 14:21-22, “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra, na Ikonia, na Antokia.

(a).Wakifanya Imara roho za wanafunzi.

(b).Wakiwaonya wakae katika ile Imani.

(c).Wakiwataarifu kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”. [viashirio (a), (b), (c) havipo kwenye Biblia bali ni nimeweka kwa ajili ya kuonyesha ninachotaka ukizingatie]

Napenda usome vizuri andiko hilo hapo juu ili uone kusudi la Injili. Hiyo ndiyo Injili iliyomfanya Paul apigwe mawe. Hakuitia watu pesa, magari, majumba, maana ukiwaitia watu hayo, wanakuwa rafiki zako, wala wasingempiga kwa mawe!

-Alikuwa akifanya roho za wanafunzi kuwa Imara, kwa nini Imara?

Baada ya kuokoka lazima utakutana na dhoruba, mapambano makali, mahali pengine anasema tu wajenzi, wengine wanajenga kwenye mchanga, wengine wanajenga kwenye mwamba. Tofauti ya wajenzi hawa ni pale majaribu yanapokuja, mmoja ataanguka, mwingine atabaki amesimama. Mpendwa unajenga kwenye nini?

-Alikuwa akiwaonya wakae katika ile Imani:

Imani ipi? Ni ile Ya kweli aliyowapandia. Unajua kuna Imani nyingi siku tulizonazo mpendwa, na Paulo aliziona akamtahadharisha kijana wake mpendwa Timotheo katika 2Timoth 4:1 akimwambia kuwa “awe tayari wakati umfaao na wakati usio mfaa, maana utakuja wakati watu watayakataa mafundisho yenye uzima.Watafuata mafundisho mafu, mafundisho yaliyo maagizo ya binadamu”. Mafundisho hayo hayawezi kutufikisha mahali popote.  Ebu tuyaone:

Kolosai 2:20-23, “Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya Amri, kama wenye kuishi duniani? Msishike, msionje, msiguse, mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa, hali mkifuata maagizo, na mafundisho ya wanadamu, mambo hayo yanaonekana kna kwamba yana hekima, Katika namna ya Ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali, Lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tama za mwili

Ndugu zangu kama hatutakubali tuongozwe na Roho wa Mungu, tutaongozwa na mawazo yetu. Hata tungetumia ukali wa mwili, havitatusaidia chochote!

-Akiwataarifu wateule kuwa Tutaingia mbinguni kwa njia ya dhiki nyingi.

Hilo katuwezi kukwepa! Kama tumebeba Injili ya Bwana Yesu, Injili aliyoibeba Paul, Injili ambayo haijachakachuliwa,  Tujue tutapita kwenye dhiki, ambayo Bwana alisema wazi wazi kuwa, “Duniani mnayo dhiki lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu.”

Wengi tuko kwa Yesu bila  kupiga gharama. Ndiyo maana kila siku utasikia maombi kama haya: Mungu nifanyie lile, na lile, na lile, nifanyie, maana ulisema, nifanyie lile, nifanyie na lile! Nk. Ni vigumu sana kusikia mtua akiomba kama: Mungu nataka nikifanyie lile, na lile, nami nitafanya na lile, na lile, nitafanya na lile! Jipime unavyoomba. Kuomba kwako kunaweza kuonyesha  kama ulipiga au hukupiga hukupiga gharama.

Siku mmoja watu walinong’ona nyuma ya Yesu wakisema “mikate leo ni kama amesahau kututengenezea!” Ndipo aligeuka akawaambia: “Msikitendee kazi chakula kinachoharibika!”

Rais mmoja wa Marekani alipotawala, aliongea na wafanyakazi osifini mwake akisema: Mtu asiulize kuwa Amerika itamfanyia nini!  Ila kila mtu ajiulize Nitaifanyia nini Amerika! Kiongozi yeyote anapoteuliwa kuwa Kiongozi wazo la kwanza ni hili: Sasa Nitapewa gari, nyumba nzuri ya kuishi, mshahara mnono, nk.

Kwa upande wa kanisani: Wengi wanakuja Kanisani maana wametumainishwa kuwa kuna kile, kuna kile na kile! Lakini sasa watu inabidi ufike wakati  tumwambie Mungu kuwa Bwana nataka nikufanyie kile, na kile. Sasa inatakiwa itoshe kumuagizi tu  Mungu. Tumemwagiza Mungu kiasi cha kutosha!

Tena imeandikwa katika Biblia “Tafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, hayo mengine mtazidishiwa”. Yawezekana hata hatujui Ufalme wa Mungu ni Nini! Lakini imeandikwa katika Biblia kuwa Ufalme wa Mungu siyo kula na kunywa, bali ni Furaha, Haki na Amani katika Roho Mtakatifu!

Mpendwa, yawezekana kabisa hukupiga garama mpaka ukajikuta umeingia kwenye wokovu. Ndiyo maana unapoelekezwa jinsi ya kutembea kama mwanafunzi wa Yesu, unashindwa, mpaka unakuwa kama Mgalatia ambaye akiambiwa ukweli anakasirika! Ndivyo Wagalatia walivyokasirika na mtume Paul akawambia yafuatayo katika Gal 4:16. Je nimekuwa adui wenu kwa kuwaambia yaliyo kweli?

Wakati umefika sasa tusimfanye Mungu kama mtoto wa shule wa kutuma tuma; nipe kile; niletee kile!  Sisi tumemfanyia nini? Tunalo wazo la kumfanyia nini?

Mahali pengine anasema hivi: Mnawaza nini Juu ya Bwana? Wengine wanawaza kumtuma tu, kumuelekeza vile wanataka awafanyie, mwisho mpaka hata mistari muhimu kwenye Biblia kama ule wa kukufanya “Umpatie Mungu nafasi” wengi hawautumii siku hizi, hata ule wa “Mapenzi yako yatimizwe, Si kama nipendavyo”, ni wachache sana wanaoitumia siku hizi!

Hebu leo niishie hapo; nikisema kuwa kama hujapata kukaa chini ukapiga gharama: mpaka uhesabu vitu vyote kuwa hasara, mpaka uvione kama mavi [Filipi 3:8], nakusihi hebu fanya hivyo!

Nawatakia kila la kheri wakati tunaendelea kujifunza Neno la Mungu. Ni ombi langu kuwa macho ya mioyo yetu yatatiwa Nuru, tupate kuona vitu vya Rohoni!

Ni ndugu yenu, Mtumwa wa Kristo,  Mchungaji  Samuel Imori.

Mstari unaoniliza Kuliko Yote katika Biblia – XIV

Kila ninaposoma mstari ule wa Luka 13:22 huwa ninamuona, mtu huyu aliyemuuliza Bwana Yesu kiasi cha watu wanaookolewa, kuwa alikuwa na busara. Aliuliza kutaka kujua idadi kama ikiwezeka asipoteze muda wake. Jibu alilopewa na Bwana ni: Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba kwa maana nawambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze. Ndio maana mstari huu hunifanya nilie kuliko mistari yote: Watu kutaka kuingia mbinguni lakini wasiweze! Hata Bwana Yesu aliwaambia wamama kuwa WASIMLILIE, bali wajililie wenyewe na watoto wao, kwa ajili ya yale yanayokuja mbele yao.

Luka 23:27-31 “Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakimuombolezea, Yesu akawageukia akawaambia, enyi binti za Yerusalem, msinililie mimi, bali jililieni ninyi wenyewe, na watoto wenu, kwa maana tazama siku zinakuja, watakaposema, heri walio tasa, heri matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watapoanza kuiambia milima  tuangukieni, na vilima tufunikeni, kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwa katika mti mkavu?”

Mpendwa, maelezo hayo juu ni mazito kweli kweli, na marefu. Unatakiwa uyasome kwa utulivu na kutafakari, uelewe yana maana gani.

Msitari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia, unanifanya nilie kwa ajili ya nafsi yangu na kwa ajili ya watoto wangu wote wa KIMWILI na KIROHO pia. Paulo alisema mahali fulani hivi: “Vitoto vyangu,, nawaonea utungu mpaka Kristo auimbike ndani yenu”

Hadi sasa tumeshaona sababu mbali mbali ambazo zitafanya wengi washindwe kuingia mbinguni wakati wanataka. Leo, katika sehemu ya Kumi na Nne (14) ya somo hili, tutaendelea kuona tena sababu nyingine:

19. WATAMALIZA  VIBAYA.

Mhubiri 7:8, ”Heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo wake” Hapo Biblia inatufundisha kabisa kuwa makini na namna tutakavyomaliza. Watu wengi wanafurahia mwanzo wa jambo lolote, bila kujali mwisho utakuwaje. Ndiyo maana Sulemani aliomba hivi: “Uniwezeshe nijue kuingia na kutoka”. Watu wengi hujali tu namna ya kuingia/kuanza, ila hawaangalii namna ya kutoka/kumaliza. Swali linakuja: Tutamalizaje safari tuliyoianza.?

Katika Zaburi 30:6-7 Daudi anasema hivi: “Nami nilipofanikiwa nalisema sitaondoshwa milele, nawe Bwana uliuficha uso wako nami nikaaibika”

Ndugu zangu watu wengi huwa tunaanza vizuri sana, tunakuwa na bidii kweli kweli. Mara tunapoanza kufanikiwa, hapo ndipo mambo yanaanza kuwa vingine; tunafikiri tumefika, hata wakati mwingine tunaridhika kabisa. Tunaweza kuangalia mwenendo wa Yusufu kama mfano wa kuigwa: Ysufu  alipokuwa nyumbani kwa Potifa, angeweza kudhani amefika, kuwa sasa mambo yamekuwa mazuri, akae ale anywe. Nakuambia kama angewaza hivyo ingekuwa rahisi kwake hata kuanguka dhambini na yule mama Potifa. Angefikiri kuwa sasa maisha yamemnyookea. Kumbe bado nyumbani kwa Potifa hakukuwa na chakula cha kuwatosha na ndugu zake; na hatujui kama alikuwa analipwa mshahara kwa kuwa alikuwa mtumishi tu wa ndani. Bado alikuwa na safari ndefu. Ndiyo maana akasema: Nifanyeje Dhambi Nimkose Mungu?

Hebu endelea na safari! Usijifikirie wewe tu, kama tulivyo wengi wetu leo: mtu ukiishajenga nyumba, ukanunua gari, unasema ‘sasa nini tena?’ Hebu nikukumbushe kuwa ndugu zako bado wako Misri, wanatakiwa kuja hapo ulipo ukawahudumie.

Tukisoma mistari katika 2Nyakati 26:1-15 tunaona jinsi mfalme Uzia alivyo fanikiwa, lakini  mwisho akafanya vitu vya ajabu na utaona yale yaliyomkuta, ni marefu kidogo sitayakopi ila soma ujionee. Lakini kwa ajili ya somo letu tutaangalia mstari wa 16 ili tuende pamoja:

“Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia”

Mfalme Uzia alipofanikiwa moyo wake uliinuka, akafanya mabaya: akaamua atoe kafara, kinyume cha utaratibu, wakati ilikuwa ni kazi ya makuhani. Lakini kwa kuwa yeye  alishafanikiwa hata hakuwaheshimu tena waliokuwa na jukumu la kufukizia.  Hivyo alimaliza vibaya:  alimaliza na ukoma, alimaliza na kutengwa!

Ndivyo ilivyo kwa wengi wetu: wanakuja makanisani, wengine hawana kitu, na kwa kuwa Mungu ni mwema, watumishi wa Mungu huomba, humlingana Mungu, na Mungu huitika na humbariki mtu huyo. Baada ya hapo huwaoni tena wakiendelea na Mungu. Wengine hurudi nyuma kabisa, hurudi hadi kufikia hatua kuvunja ndoa zao, wengine hurudi tena vilabuni. Ndugu yangu, inatisha!

Na kwa sababu hiyo, kupitia somo hili mimi naomba upokee angalizo ninalokupatia kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 8:11-18:

Mistari 11-14 inasema: Jihadhari usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga  nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoogezeka, na kila kitu ulichonacho kitakapoongezeka, basi hapo moyo wako usiinuke ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa”

Mistari ya 15-18 inaendelea kusisitizia matemdo makuu ambayo BWANA, Mungu wetu, aliwatendea Wana wa Israel na kwa mfano wa hayo anatutendea nasi leo. Na anamalizia katika ule mstari wa 18 kwa kusema kuwa BWANA, Mungu wetu, ndiye atupaye nguvu ya kupata utajiri. Hivyo hatutakiwi kabisa kumsahau!

Mungu atusaidie! Maana najua atatubariki, kwa kuwa imeandikwa “Anatuwazia mawazo mema, kutupatia mema katika siku zetu za mwisho.”

Ee Mungu, tusaidie tumalize safari yetu vizuri! 

Mbarikiwe nyote mnapoendelea kuvipiga vita vizuri vya Imani.

Ndugu yenu Mch. Samuel Imori

Kuachana


Luka 16:1 8  “Kila amwachaye mkewe na kumuoa mke mwingine azini naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.”

Wapendwa katika Bwana, nawasalimu wote katika Jina la Yesu Kristo Mwokozi wetu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa. Nimesukumwa leo kulizungumzia suala hili zito: Suala la kuachana watu wawili waliokwisha kuoana, waliokwisha kukubaliana kuwa MKE na MUME. Maandiko yamesema hapo juu kuwa kila amwachaye na kuoa mwingine AZINI, na yule amwoaye yule aliyeachwa AZINI. Nimekuwa nikisuluhisha ndoa za watu wengi zenye machafuko, zenye shida, na baada ya hayo yote, nikasukumwa kuwa niandike ujumbe huu, ili uwasaidie wale ambao tayari wamekwisha kuoana, na wale ambao wataoana.

Efeso 5:33 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe, na mke asikose kumstahi mumewe”

Mpendwa, hebu tuendelee kujifunza kutoka kwenye Neno la Mungu. Wajibu wa MUME ni kumpenda mke wake kama nafsi yake. Suala hili ni gumu; ni agizo gumu, lakini aliyetuagiza anajua kuwa wanaume wataweza kumpenda mke KAMA mtu apendavyo nafsi yake. Mtu anapojikwaa mguu, kwa kuwa anaupenda mguu wake, haupigi, wala haukati, anaupuliza, anaushughulikia kama umeumia, hawezi kuuliza kuwa ‘ulikuwa unatembeaje mpaka ukajikwaa?’. Na MKE ameambiwa asikose KUMSTAHI mumewe. KUMSTAHI ni KUMHESHIMU MUMEWE. Kumheshimu kwa njia gani?

Efeso 5:22 “Enyi wake watiini waume zenu, kama kumtii Bwana wetu, kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa, naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile kanisa limtiivyo Kristo, viyo hivyuo nao wawatii waume zao katika kila jambo”

Naomba twende pole pole tukijifunza, ili ndoa zipone maana nyingi zimeoza, hazifai. Wamama wameambiwa wawatii waume kama kumtii Kristo. Hapo napo huwa kuna matatizo, maadam wote wameokoka, basi wanajihesabu kuwa wako sawa. Hapana! Soma vizuri: MUME NI KICHWA. Sasa kama mume ni kichwa, ndiye anatakiwa kuongoza nyumba, kwa kuwa kichwani kuna- MACHO, MASIKIO, UBONGO, MDOMO, n.k

Nazungumzia mambo ya rohoni: wamama wengi wamebomoa nyumba zao kwa mikono yao, pale walipojaribu kuongoza, wakidhani wanaweza. Kumbuka neno hili kuwa Adamu aliishi bila Hawa lakini Hawa hakuwahi kuishi bila Adamu.  Hawa alipoishi bila Adamu kwa dakika chache tu aliondoka akakutana na nyoka, wakati Adam hayupo pamoja naye, akajitahidi kuzungumza na nyoka akijibu maswali aliyokuwa anaulizwa, lakini hakufua dafu!

1Tim 2:13-14 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudangaywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa, akaingia katika hali ya kukosa

Biblia inaeleza wazi wazi kuwa Adam hakudanganywa. Aliyedanganywa ni Hawa. Sasa tuendelee kujiuliza: kama Adam hakudanganywa, ilikuwaje Ale tunda? Je, Alilazimishwa?; Kwa nini alikula?

Nilipokuwa natafakari mambo haya niliyaona kwa ndani zaidi. Utakumbuka wakati Bwana alipokuja ili akutane nao Bustanini, hakuwakuta, akamwita Adam na  kumuuliza alikokuwa! Adamu akasema “nimejificha, kwa kuwa niko uchi”; akamuuliza “nani amekwambia kuwa uko uchi?” [au umekula tunda nililokukataza?] Adamu akasema “Mwanamke uliyenipa ndiye amenipa tunda nikala”.

Sasa ona hapa, Je, Hawa alimlazimisha?  Kwa nini alikula?  Watu wengi wanasema kuwa Adam aliposema kuwa ni huyo mwanamke uliyenipa, alikuwa anamlaumu Mungu kwa kumpatia mwanamke. Hapana!  Hebu leo nikuonyeshe kitu hapo: Biblia inasema “Apataye mke apata kitu chema, tena hujipatia kibali kwa Bwana

Sasa Adam alipojibu kuwa “ni huyo mwanamke uliyenipa” alikuwa akisema hivi: “Huyu mwanamke uliyenipa, najua hukunipa kitu kibaya, ulinipa kitu chema kabisa, na mimi kama mimi hajanikosema, amekukosea wewe. Na kawa kuwa wewe Mungu wangu ulinipa kitu chema basi sitakiacha, nitaongozana nacho kokote kitakakokwenda, sitakiacha. Wewe Mungu una uwezo, kwanza unajua kuwa ni chombo dhaifu, wewe ungeweza kukizuia kabisa kisile tunda lakini ukakiacha kikala, basi nakufa nacho!”.

Alipomaliza kusema hayo akalipokea tunda kwa hiari yake, akala  na akajua sasa hawawezi kumuona Mungu wakiwa na hali hiyo; wakakubaliana waondoke  shambani.

Sababu nyingine iliyofanya ale ni kuwa alijua kuwa yeye Adam aliishi bila Hawa  na wala hakuomba Mungu ampe mke, ni Mungu tu alisema “si vema sasa uwe peke yako nitakufanyia msaidizi”, na akamfanyia  wa kufanana naye, yaani alimfanyia mwili wake, sasa mwili wako utaukataje uutupe? Akajua kuwa UBAVU wenyewe hauwezi kuishi  bila kichwa, ndio maana alisema basi nitaendelea kuwa na ubavu huu.

Ruth 1:16-17 “Naye Ruth akasema, usinisihi nikuache, nirejee nawe, maana wewe uendako nitakwenda, nawe ukaapo nitakaam watu wako watakuwa watu wangu, pale utakapokufa nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa. Bwana anitende hivyo na kuzidi, ila kufa kutatutenga wewe na mimi”

Huyo ni Ruth alipokuwa anamwambia mama mkwe wake, wakati amemsihi aondoke kama Olpa alivyofanya. Ndugu zangu nazungumza habari za KUACHANA, siku tulizonazo, limekuwa ni tatizo kubwa katika maisha ya wana ndoa wengi, wengine maombi yao yamekwama hayajibiwi kwa sababu ya ndoa zao.

1Pt  3:7 “Kadhalika nanyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke heshima, kama chombo ksicho na nguvu, na kama warithi pamoja na neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”

Neno linasema wazi wazi kuwa mume ukae na mke wako kwa akili. Unaona hiyo? Kukaa na mke inatakiwa akili itumike. Je, Ni akili ya namna gani? : Kuwa ni chombo kisicho na nguvu, japo wakati mwingine wanajitutumua kana kwamba wana nguvu, lakini Biblia inabaki pale pale kuwa ni chombo kisicho na nguvu, ya kwamba mume umpe mke Heshima. Kumpa heshima ni kufanyaje?

Hayo yote tuyaangalie vizuri maana ndiyo yanayoleta matatizo iwapo mmoja atashindwa kutimiza wajibu wake. Unajua kama madereva wote wangefuata sheria za barabarani, nakwambia hakungekuwa kunatokea ajali barabarani, pale pa “keep left”, mwendo gani unatakiwa hapo, wakati gani umpite mwezako aliye mbele, wakati gani usimame n.k!

1 Pt 3:1-6 “Kadhalika nanyi wake watiini waume zenu, kusudi, ikiwa wako wasioliamini Nneo, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile neno. Wakiutazama mwenendo wenu safi na wa hofu. Kujipamba kwenu kusiwe kujipamba kwa nje, yaani kusuka nywele, na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi, bali uwe utu wamoyoni, usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika, yaani roho ya upole, na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumikia Mungu, na kuwatii waume zao,kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana. Nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yoyote”

Soma kwa makini hayo yote hapo juu, utaelewa. Je,  wewe mama unamwitaje mumeo?

Unajipambaje? Wengi wamesoma wakaelewa vibaya kuwa Biblia imetukataza kujipamba, hapana. Inakueleza jinsi unatakiwa kujipamba, usidhani ukiisha vaa nguo nzuri, ukasuka nywele zako, ufikiri kuwa hapo umemaliza; hapana. Kumbuka Bwana anaangalia MOYO, na jambo hili Yesu aliliweka hivi:

Math 23:27-28 “Ole wenu waandishi na mafarisayo wanafiki, kwa kuwa mmefanana na makaburi, yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivi ninyi kwa nje mwaonekana na watukuwa wenbye haki bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”

Unaona alichosema Bwana Yesu hapa? Wala hakusema makaburi yasipakwe chokaa, hapana! Kama ambavyo hakusema watu wasivae mavazi mazuri, ila pamoja na kuvaa, tuelewe kuwa kuna cha zaidi ya kuvaa: mioyo ni muhimu kuliko kuvaa! Hapo inabidi tuelewe vizuri, maana wapo watu wanasema kuwa Biblia inasema haturuhusiwi kuvaa mavazi ya thamani. Hapana hiyo siyo maana yake!Mtu akikwambia kuwa uanajeshi wako usiwe wa kuvaa buti, hapo hajasema usivae buti, ila anasema ukiisha vaa buti, usije ukadhani umemaliza, kuna zaidi ya hapo!

Biblia inasema kuwa katika siku za mwisho watu watakuwa na tabia fulani, ambapo mimi nimechagua mambo matatu ambayo hayo ni mabaya mno! Hebu jipime:

1.Wenye kuvunja maagano.

2.Wasiotaka kufanya suluhu.

3.Wasio na shukurani.

Tafakari hayo mambo hapo juu. Mtume Paulo aliona siku za mwisho kuwa watu watakuwa wanavunja maagano. Katika kuoana huwa kuna maagano, wengine wanavalishana pete, wanasema maneno mbele za Mungu na mbele za watu, vigelegele vinapigwa, Neno linasomwa na watumishi wa Mungu.! Lakini baada ya siku si nyingi, hayo maagano yanavunjika; unasikia ndoa hiyo imekwisha wala haipo tena! Ni wengi wamevunja, na tayari wameshaoa tena. Lakini wanasema bado wanasonga kuelekea Mbinguni! Hivi ni kweli kuna kuelekea mbinguni hapo? Endelea kutafakari!

Wengine hawataki kabisa kufanya suluhu. Biblia imesema kuwa “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Wapo wana wa Mungu, wazuri kabisa katika kuwapatanisha wapendwa wanapokoseana. Lakini kwa sababu siku za mwisho watu hawatakubali kufanya suluhu, basi hakuna kinachofanyika isipokuwa kuachana tu. Endelea kutafakari!

Watakuwepo watu watakaovaliwa na roho ya kukosa shukurani. Hivi kweli, mkeo/mumeo ambaye mmekaa naye miaka kadhaa unayoijua wewe; Hakuna hata jambo moja tu ambalo aliwahi kukufanyia zuri? Ukilikumbuka hilo, naamini kuwa litageuza hasira yako na utaumba roho ya kushukuru, na mwisho msamaha utaumbika na utamsamehe, na utajikuta mnasameheana.

Kol 3:12 “Bsi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusahemeana; mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake, kama Bwana alivyowasamehe ninyi; vivyo nanyi”

Napenda nimalizie kwa kusema kuwa Mungu atusaidie: ndoa ziponywe; talaka zisitajwe kwetu kamwe; vinginevyo tunaelekea kwa wenzetu wan chi zilizoendelea hasa za Ulaya na Marekani ambao wanaoana kwa mkataba, ukiisha wanaongeza. Hiyo siyo Biblia.

Nawatakia kila la kheri katika ndoa zenu. Amina!

Mchungaji Samnuel Imori.

 

Kuabudu Sanamu

Walawi 26:1 “Msifanye Sanamu yoyote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lolote lililochongwa katika nchi yenu ili kulisujudia, kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu”

Maandiko haya yanaonyesha Mungu anavyotuambia kuhusu Sanamu kuwa tusiiabudu.

Lakini sanamu ni nini? Wengi tukiulizwa tutasema ‘Sanamu ni picha”, na kwa maana hiyo tutajua kuwa Mungu anasema kuwa tusiabudu picha. Je, huo ndio ukweli?

Tuendelee kuangalia: tumeambiwa tusichonge sanamu yoyote, mahali pengine anasema “usifanye sanamu yoyote kwa mfano wa kitu chochote kilicho mbinguni, au duniani ili kukiabudu”.

Swali langu kuu katika ujumbe huu  ni JE SANAMU NI NINI?

Zaburi 97:7; “Na waaibishwe wote waabuduo Sanamu, wajivunao kwa vitu visivyofaa, Enyi miungu yote msujuduni yeye”

Hasara inayopatika kama mtu akiabudu sanamu, ni kuaibishwa. Katika hao (wanaoaibishwa) ni pamoja na wale wanaojivuna kwa vitu visivyofaa, vitu vinavyopita. Pia taarifa inatolewa hapo kwenye Zaburi 97:7 kuwa miungu yote imsujudie Yeye (Mungu).  Hapo tunaona kumbe kuna miungu, ambayo si picha, au sanamu zilichongwa. Tunatakiwa kuwa makini tunapoabudu, kwamba tunaabudu nini! Tumeona kumbe sanamu si ya kuchonga tu. Hebu tuendelee kujifunza maana swali letu linasema   SANAMU NI NINI?

1Falme 18;27—29; “Ikawa wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, mwiteni kwa sauti kuu maana ni mungu huyo, labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe, wakapiga kelele, wakajikata kata kwa visu, na nyembe kama desturi yao, hata damu ikawachuruzika,  ikawa wakati wa adhuhuri walitabiri, hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia”

Fuatilia kwa makini maneno hayo hapo juu, utaona vitu ambavyo pengine hujawahi kuviona. Hawa watu walikuwa wanaabudu, walimwita mungu wao mpaka wakatabiri. Lakini Biblia inasema hapakuwa na sauti, wala aliyeangalia. (Jiulize: walitabiri wakisemaje?).  Bila shaka walikuwa wakisema “BWANA ASEMA!”, lakini Biblia inasema hapakuwa na sauti. (Maana yake Mungu hakuwaambia chochote, hakuwaelekeza chochote). Anaendelea kusema hakuna aliyeangalia, yaani Mungu hakuwajibu, wala hakuwaangalia.

Mpendwa kumbuka swali letu SANAMU NI NINI?

Ebu tutafakari pamoja kisa hiki cha kutisha katika Biblia. Mimi najifunza kuwa Eliya alimjua Mungu aliyemwabudu. Vitu vilitokea; tunaona upepo ukivunja miamba, ukitikisa milima, wala Eliya hashtuki, wala haondoki pale pangoni!

1Falme 19:11-13; “Akasema, toka usimame mlimani mbele za BWANA, na tazama BWANA akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja vunja miamba mbele za BWANA, lakini BWANA hakuwemo katika upepo ule. Na baada ya upepo tetemeko la nchi na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto, lakini BWANA hakuwemo katika ule moto, na baada ya moto sauti ndogo ya utulivu. Ikawa Eliya alipoisikia alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka akasimama mlangoni mwa pango, na tazama sauti ikamjia kusema Unafanya nini hapa Eliya”  

(Ndipo Eliya akaanza kujibu, na mwisho akapewa maagizo ya kufanya)

Tunaona upepo ukitokea na kupasua miamba, lakini Eliya aliendelea kungojea. Tunaona tetemeko la nchi linatokea lakini yeye bado aliendelea kungoja apewe maagizo na MUNGU. Mpaka moto ukatokea, bado Eliya alinyamaza kimya; mpaka Biblia inasema SAUTI NDOGO YA UTULIVU. Mpendwa siku tulizo nazo watu wanaabudu: Upepo, wanaabudu Matetemeko, wanaabudu mioto.  Ndiyo maana unaona hawana maagizo kutoka kwa Mungu. Hawawaelekezi watu watafanyaje ili waingie Mbinguni; wanawaambia habari ya MIUJIZA tu, hiyo ni mioto; ni upepo; ni matetemeko maana hayasemi. Kila leo watu wanayaona, wanaangushwa nayo, lakini kwa kuwa hayawaelekezi watu wafanye nini, basi hawabadiliki. Ndipo baada ya yote hayo Mungu akaja akamwelekeza Eliya atakavyofanya kazi, tena kwa sauti ya utulivu, ya kueleweka kuwa afanye nini!

Siku tulizonazo, kwa kuwa watu wamekutana na matetemeko, mioto, upepo, hawakungoja SAUTI YA UTULIVU isiyo na ugomvi, isiyo na wivu, isiyo na chuki, isiyo na mashindano, basi tulipokutana na hayo mengime tukakimbia kuwa Mungu ametuita, na ukweli ni kwamba hatukumgoja aje na sauti ya utulivu, ndio maana unaona siku zetu ni kuumana, kulana, kuangamizana!

Yeremia 46:12; “Mataifa wamesikia habari ya aibu yako, nayo dunia imejaa kilio chako, maana shujaa amejikwa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili pamoja”

Mpendwa sikia msitari huo hapo juu! Kumbuka kuwa Mungu wetu ni mmoja, Mbingu ni moja, tutaishi Mbinguni pamoja milele, lakini unasikia msitari huo unasema aibu imesikiwa, Dunia inalia kuwa SHUJAA AMEJIKWAA JUU YA SHUJAA MWENZAKE, WOTE WAMEANGUKA CHINI. Hii ni kusemaje?: Wewe mtumishi wa Mungu, na mtumishi mwingine wa Mungu hatusalimiani. Tumechukiana, tunapambana kwenye Runinga kushambuliana, huyu anamshurishia huyu, huyu anamrushia huyu. Neno limeiita hiyo ni aibu, Neno limesema dunia inalia, WOTE WAWILI WAMEANGUKA CHINI.

Nikuulize swali: Unafikiri ni nini kimesababisha? Jibu ni hili hapa kuwa wengine walisikia Upepo wakaondoka, wengine walisikia Miamba ikipasuka wakaondoka, wengine waliona Moto ukiwaka wakaondoka. Hatukusubiri tupewe maagizo na Amiri jeshi wetu mkuu. Halafu kinachotumaliza sasa ni Kiburi kuwa mimi ni bora kuliko yule, kwa hiyo nitaingia tu mbinguni. Hapana ona Biblia inavyosema: “Wote wawili wameanguka chini”

Hii inatuonyesha jinsi ambavyo wengi wetu tunaabudu sanamu, wengine wanaabudu upako wa  Mungu wala siyo Mungu,  wengine tunaabudu ngurumo, radi, tetemeko, wala siyo Mungu. Wapendwa tuache sanamu tumpate Mungu, naye atatufundisha vizuri kuwa  Hakuna Dhambi Itakayopenya Kuingia Mbingu Takatifu.

Yer 17:5-6; “Bwana asema hivi amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema bali atakaa jangwani palipo na ukame, katika Nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu”

Hapa  tunaendelea kujifunza kuhusu Sanamu. Ndugu zangu leo hii tuko kwenye kona mbaya, watu tumemwacha Bwana tayari tunaabudu sanamu, tunaabudu wanadamu, viumbe walioumbwa na Mungu, na viummbe hivi navyo vimekubali kuabudiwa. Mchungaji ninakuwa na mshirika mwenye mshiko, hata angefanya dhambi gani haguswi, nitamgusaje na yeye ndiye anayenifanyia kila kitu? Kwa kuwa anao mshiko imebidi nimweke kuwa mzee wa kanisa, hata kama hana sifa yoyote tofauti na mshiko.

Tembelea makanisa ya leo utaelewa ninachosema, hamia kanisa lolote, toa senti yako vizuri siku mbili tatu, utasikia tayari mzee wa kanisa, hata kama hujajazwa na Roho, na wewe unakubaliana tu kuwa ni sawa!

Ndugu zangu tusikubali kuabudiwa, nasi tusikubali kuabudu mtu awaye yote, hizo ni sanamu, nazo zimejaa sana, kila mahali. Na shetani ni mjanja, wengine wala Mungu hajawaleta, ila wamechongwa na shetani na akatuletea.

Mdo 8;18-24; “Hata Simioni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemwekea mikono yangu apokee Roho mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja na wewe kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali, huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili kwa kuwa moyo wako si mnyoofu mbele za Mungu basi tubia uovu wako huu ukamuombe Bwana, ili kama yamkini usamehewe fikra hii ya moyo wako kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo na tena u katika kifungo cha uovu, Simioni akajibu; niombeeni ninyi kwa Bwana yasinifikilie mambo haya mliyoyasema hata moja”

Simioni Mchawi alikuwa kanisani, Mtume wa kweli akatembelea kanisa hilo, akamkuta.Unaona! Akataka ampatie pesa ili ampatie kipawa, tena Mtume hakumuomba kama hawa wa siku zetu tulizo nazo, ambazo mtu anaingia kwenye Runinga dakika 10  anawapatia watu  namba ya M-Pesa, pamoja na Acount Namba kuwa tumeni hela humo;  tofauti na Mtume Petro: Simioni mchawi mwenyewe alijipeleka kwa  Petro kuwa “nataka kukupa hela”! Unaona Petro alivyomkemea kuwa yeye na pesa hizo apotelee mbali!, Akamwambia kuwa hana fungu katika Ufalme wa Mungu.

Kisha mtume Petro akaendelea kumwambia kuwa alikuwa katika uchungu kama nyongo na kumshauri atubie uovu wake. Na kweli kumkemea huko kukamletea kufikia toba ya kweli! Mpendwa, kama ingekuwa siku zetu pengine Petro angeweza kumwambia kuwa yeye ,Simion mchawi, anaweza kupotea lakini cheki amwachie!

Hebu jaribu kufanya utafiti, wakati watunzi wa nyimbo wanapotunga nyimbo huwa kuna kitu kinaitwa korasi (CHORUS). Sijui kama umewahi kufanya utafiti kuwa hata kama wimbo una beti 10, baada ya kila beti huwa tunarudi kwenye CHORUS, kwa nini?  Hapo ndipo kiini cha wimbo kilipo, na inalazimika kurudia rudia ili kiini kiingie na kieleweke. Hicho ndicho kiini cha wimbo.

Sasa tazama  tunavyohubiri siku zetu, kusudi letu la kuhubiri ni nini?:

Naingia kwenye Runinga, napiga Injili wakati nahubiri nimeweka CHORUS ambayo ni M-Pesa na/au Acount No, tena inacheza cheza, inaendelea kupita kwa kujirudia rudia! Mimi naona tugeuze utaratibu ndugu zangu tuweke YESU jina hilo liwe linapita, liwe linacheza cheza, lijirudie mara nyingi kwenye Runinga. Hiyo iwe ndiyo  CHORUS watu waishike hiyo! Siyo M-pesa, wala Acount No.  Mungu anajua kuwa tuko kazini hivyo sio lazima tuombe ombe kama maskini. Unapotumikia Mungu unatakiwa ujue tumeajiriwa na Mbingu, na Mbingu itawajibika juu yetu. Mbingu sio mataahira mpaka tukaombe ombe kwa wale tunaowahudumia, wengine mpaka tuwatoze hela ndio tuwaombee; Je kama kweli Yesu angefanya kazi kwa njia hiyo, yule mama wa senti mbili angeonekana kuwa ni kitu??

Math 9:13 “Lakini nendeni mkajifunze maaa yake nini maneno haya, nataka rehema wala si sadaka. Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki wenye dhambi.”

Math 12:7; “Lakini kama mngalikua maana yake maneno haya, Nataka rehema wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia”

Pitia mistari hiyo hapo juu pole pole uone Bwana anasema kusudi lake si pesa, ni REHEMA ( HURUMA). Utakubaliana na mimi kuwa Yesu alikuwa na mtunza hazina, kwa hiyo siyo kwamba alikuwa hachukui sadaka, ila hapa anaonyesha kuwa sadaka halikuwa  CHORUS, ila CHORUS ilikuwa REHEMA.  Nasi wapendwa tunafundishwa kuwa hebu sadaka isiwe CHORUS.

Yatubidi tuwe na huruma kwa watu wenye shida, ambao hawana kitu; wengine wanakuja makanisani tunawaambia watoe tu watabarikiwa, kwa hiyo wanatoa kwa Mungu ili wabarikiwe, hilo ndilo linakuwa kusudi la kutoa kwao, tunashindwa kuwaambia watu kuwa vyote walivyo navyo ni vya Mungu, hata wanapomtolea wanarudisha tu sehemu ya vile alivyowapa. Ndio maana  katika kitabu cha Ayubu imeandikwa kuwa “Nani aliyetangulia kunipa na ananidai?” Wakati mwingine tunawaambia kuwa watatajirika; Je ni kweli watu wote watatajirika? Mbona Neno linasema “Maadamu nchi idumupo masikini hawatakoma katika nchi”?

Mdo 14:14-18; “ Walakini Mitume Barnaba na Paulo walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema akina Bwana mbona mnafanya haya,  Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi, twahubiri habari Njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili, na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi, na bahari na vitu vyote vilivyomo, ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote yaende katika  njia zao wenyewe, lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shinda wasiwatolee dhabihu!”

Katika maandiko hayo hapo juu tunaendelea kujifunza jinsi Mitume waliotutangulia walivyofanya kazi waliyotumwa na Mungu, kwa maana Neno linasema TUMEJENGWA KATIKA MSINGI WAO. Ukisoma maandiko kabla ya hayo niliyonakili, utaona walivyopewa majina makubwa makubwa, mazito, mmoja akaitwa  ZEU, mwingine HERME, Lakini hawakukubaliana na kile kilichokuwa kinafanywa na wafuasi wao. Unajua wafuasi huwa hawajui kitu, wanasema lolote linalokuja katika mawazo yao. Wengine wakitaka kukudhihirishia jinsi ulivyo wa maana, ulivyo muhimu, ndio maana wanaweza kukupa majina ya ajabu.

Nilisikia mahali mtu anajiita MJUKUU WA YESU!.  Ndugu zangu hebu twende na Biblia tuache mbwembwe! Mjukuu wa Yesu maana yake nini? Na tunawaangalia tu hatuwasaidii, tusinyamaze kusema. Tuseme tu ili wakisikia watapata msaada! Na hata kama hawatabadilika lakini watakuwa wameshaambiwa!

Mitume hawakukubali majina hayo makubwa. Wewe wasikie wahubiri wanaoitwa mashuhuri. Sikia tu majina, wengine utafikiri ni Mungu mwenyewe. Hayo yatatufanya tuwe sanamu; yatatufanya tuonekana wa maana kuliko wengine. Kumbuka Bwana alisema anayetaka kuwa mkubwa awe mtumishi wa wote. Sasa mtumishi wa nyumbani kwako huwa unamlipa nini?

Mungu atusaidie turudi kwenye Biblia, kama tunata kumuona Mungu wetu. Mahali pengine anasema, “mmalizapo semeni kuwa TU WATUMWA TUSIO NA FAIDA TUMEFANYA TU YATUPASAYO”

Nahitimisha kwa kurudia Swali letu- SANAMU NI NINI?

Sanamu ni kitu chochote tutakachokipenda kuliko Mungu. Hiyo tayari ni Sanamu! Ni maombi yangu Mungu atusaidie tuepuke Sanamu katika maisha yetu yaliyobakia hapa Duniani kabla hatujaenda kwetu mbinguni kwa Baba, mahali ambapo hakuna kilio tena.

Amani iwe kwako na ubarikiwe!

Mchungaji Samuel Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko yote katika Biblia – XIII

Ndugu msomaji, baada ya mstari huo wa Luka 13:22 kushika nafasi kubwa katika moyo wangu, ilibidi nitafute sana SABABU zitakazowafanya watu washindwe kuingia mbinguni huku wao wakiwa wanataka. Baada ya kuchukua uamuzi wa kutafuta sababu hizo Mungu alindelea kunionyesha, kwa hiyo kupitia somo hili, nami ninakuwekea sababu hizo ambazo ukizisoma, naamini kabisa utapata kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya Ukristo. Ninakusihi tu usichoke kufuatilia somo hili!

Leo katika Sehemu ya Kumi na Tatu (13) ya somo hili tutaona sababu nyingine itakayowafanya watu washindwe kuingia mbinguni huku wao wakiwa wanataka.

18. WATAJENGA TENA YALE WALIYOYABOMOA.

Gal 2:18 “Nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji”.

Mpendwa msomaji, hapo tunaona Mtume Paulo anasema na Wagalatia kuwa kama wakiishaokoka, ni vizuri waangalie ili wasije wakajenga tena yale waliyoyabomoa. Ni wazi kuwa mtu anapookoka huwa kuna vitu anabomoa, kuna vitu anaviacha, mpaka unasikia shuhuda mbali mbali kuwa mimi nilikuwa hivi, nilikuwa hivi, lakini sasa nimeacha! Ndiyo maana Petro yeye aliliweka hivi katika 2Pet 2:20-22:

“Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia, kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza, maana ingekuwa heri kwao, kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapishi yake mwenyewe, na Nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaagaa matopeni”

Ndugu mpendwa hebu shikilia kwa bidii kile ulichokipata, maana yapo madhara kama utashindwa tena kuendelea na safari yako ya Mbinguni. Wapo watu wanaokoka, kisha wanaamua kwenda likizo, wanapumzika kwanza kisha wanaanza tena. Tafadhali usifanye hivyo!  Kumbuka Bwana alisema hivi: Mtu aliyetia jembe lake kulima kisha akaangalia nyuma hafai katika ufalme wa Mungu. Pia Neno linasema kuwa sisi ni chumvi ya ulimwengu, na chumvi ikiharibika itatiwa nini ili ikolee? Haifai, ila kutupwa na kukanyagwa. Yapo maandiko yanayotisha, lakini hatuna budi kuyafundisha.

Math 5:13; “Ninyi ni chumvi ya dunia, lakini chumvi ikiwa imeharibika, itatiwa nini hata ikolee, haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu”

Hebu tujiulize kidogo, je tumewahi kukutana na chumvi? Maana kama Biblia inasema kuna chumvi iliyoharibika, tukubali kuwa ipo, wakati mwingine wachungaji wanahangaika na chumvi zilizoharibika, wanapoteza muda wao kuombea chumvi zilizoharibika!

Mungu atusaidie ili tusijenge tena yale tuliyoyabomoa, maana imeandikwa kuwa pepo amtokapo mtu, hurudi tena kuja kucheki alimotoka.

Math 12:43; “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo na maji akitafuta mahali pa kupumzika asipate, halafu husema nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka, hata akija aiona tupu imefagiwa na kupambwa, huenda akachukua pamoja naye pepo wengine walio wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo, na mtu huyo hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa katika kizazi hiki kibaya”

Ndugu zangu, ni ombi langu kuwa wewe uliyeokoka usiangalie nyuma tena, usirudie matapishi tena, usijibatize kuwa NGURUWE au MBWA. Songa mbele, tufike kwenye uzima wa milele!

Mungu awabariki.

Ndugu yenu   Mchungaji Samuel   Imori.

 

Maadui ni Wazuri

“Mmesikia kwamba imenenwa jicho kwa jicho na jino kwa jino, lakini mimi nawaambia msishindane na mtu mwovu, lakini mtu akupigae shavu la kuume mgeuzie na la pili, na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili, akuombaye mpe, naye atakayekukopa kwako usimpe kisogo.Mmesikia kwamba imenenwa mpende jirani yako, na uamchukie adui yako, lakini mimi nawaambia wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mabinguni, maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki nawasio haki.”  Mathayo 5:38-45.

Maneno hayo ni sehemu ya hotuba aliyoitoa Bwana Yesu pale mlimani akizungumza kuhusu ADUI . Jambo hili la kumpenda adui kibinadamu ni gumu, ndio maana aliwaambia wanafunzi wake wasitoke Yerusalem mpaka awaletee msaidizi.

Tunapotamka maadui zetu, nadhani kila mtu anaelewa nini maana ya adui :  adui yetu ni mtu au  kitu chochote kilicho kinyume nasi, na kikipata nafasi ya kutudhuru mara moja kinadhuru. Nyoka, kwa mfano, siku zote ni adui wa mwanadamu kama Bwana alivyomwambia kuwa ameweka uadui kati yetu, na yeye, kwa kuwa alikubali kutumiwa na shetani.  Kwa maana hiyo tunafahamu kabisa kuwa yupo adui yetu mkubwa ambaye ni shetani, na hapa Bwana hasemi juu yake kuwa tumuombee, bali anasema kabisa juu ya WATU, wala hasemi juu ya  vitu vingine.

Daud anasema katika Zaburi 55:12-14 kuwa aliyegeuka kuwa adui yake ni mtu waliyesali naye, waliyepeana shauri pamoja. Tuone yanavyosema  maandiko hayo:

“Kwa maana aliyetukana si adui, kama ndivyo ningevumilia, aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye, kama ndivyo ningejifucha asinione. Bali wewe mtu mwenzangu, rafiki yangu niliyejuana nawe sana, tulipeana shauri tamu, na kutembea nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.”

Maandiko haya yanaonyesha jinsi rafiki yako anavyoweza kugeuka na kuwa adui yako mkubwa, ndio maana nikasema adui ni mzuri, amewekwa kwa makusudi kabisa.  Kumbuka kuwa Yesu asingekuwa na maadui wala asingesulubiwa, naye alikuja ili asulibiwe, nani angemsulubisha? Petro asingeweza kumsulubisha, wala Marko wala Mathayo. Sasa ni nani angemsulubisha Yesu? Ni dhahiri kuwa ilikuwa ni sharti awepo adui ndiye atomize kusudi la Yesu kusulubiwa.

Nimesema adui ni mzuri kwa kuwa yeye aweza peleka habari zako mbaya, tena yeye mwenyewe atapeleka habari zako nzuri, maana maandiko yanasema Bwana anatuwazia mema. Mema hayo adui atatumika kuyatangaza. Hebu nikuelezee ninamaanisha nini ili uweze kuelewa  vizuri:

Katika Mwanzo 37:29-36 kuna habari ya Yusufu na ndugu zake. Yusufu alichukiwa sana na ndugu zake hadi wakaamua wamuue. Lakini Mungu akamtetea akamtumia kaka yake kumnusuru na kifo. Badala ya kumuua walimuuza kisha wakaleta habari kwa baba yao kuwa amekufa,  ameraruliwa na mnyama mkali. Baba yake alilia mpaka akatamani kufa. Biblia inasema mpaka akakataa kutulizwa. Alilia sana mwishowe yakaisha.

Lakini tukisoma Mwanzo 45:25-28 kuna  habari inayoonyesha kuwa wale wale waliotangaza kifo cha Yusufu ndio hao hao walitangaza pia kutawala kwake Misri. Kila alipokuwa akipata habari Baba yake Yusufu alizimia: Alizimia mara ya kwanza aliposikia amekufa na mara ya pili alizimia aliposikia kuwa Yusufu anaishi na tena anatawala!

Mpendwa kwa somo hili fupi tunajifunza kuwa hebu tuwaombee maadui zetu maana hao hao ndio Mungu atawatumia kutangaza baraka zetu na ndio hao hao Mungu atawatumia katika kuinuliwa kwetu. Tusipowaombea, nani atatutangaza?,

Ubarikiwe na Bwana wakati unaingia kuwaombea na kuwabariki maadui zako. Siku moja watakuwa watangazaji wa habari za kuinuliwa kwako!

Ndugu yenu   Mch Samuel Imori

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote katika Biblia – XII

Mtu mmoja alimuuliza Bwana Yesu, “Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache?”Bwana Yesu akawaambia: “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia kuwa wengi watataka kuingia, wasiweze”. Luka 13:23-24

Huwa nasema siku zote kuwa huo ndio mstari unaoniliza kuliko mstari wowote katika Biblia. Nilipata shida sana nilipousoma na baada ya kupata shida hiyo nikachukua muda kumuuliza Mungu kuwa ni nini kitakachozuia watu ingawa wao wanataka! Tayari nimeshaeleza sababu nyingi katika sehemu zilizotangulia kwenye somo hili.  Somo bado linandelea na katika Sehemu hii ya Kumi na mbili tutaendelea kuona mambo zaidi ambayo ndiyo sababu itakayowafanya wengi washindwe kuingia mbinguni huku wao wakiwa wanataka. Fuatana nami:

17. HAWATAKUWA NA MSINGI.

Ebr 6:1-2. “Kwa  sababu hiyo tukiacha kuyanena  mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu, tusiweke MSINGI tena kwa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na Imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele

Ndugu zangu msingi ndio nyumba, bila msingi nyumba yoyote iko hatarini; na ukitaka kujenga ghorofa, utakubaliana nami kuwa lazima msingi uende chini sana, na pia uchanganyaji wa vifaa vya ujenzi ufanyike kwa utaalam ( simenti, mchanga, kokoto, n.k.)

Katika Ebr 5:11na kuendelea mtume Paulo aliandika akiwaamboa Waembrania kuwa alikuja akiwa na mengi ya kuwaambia, lakini akashindwa kuyasema kwa kuwa walikuwa WAVIVU, yaani hawakuwa na msingi. Akawaambia walikuwa wanahitaji mtu awafundishe mafundisho ya kwanza, ya  MSINGI.

Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wakristo wa siku za leo, kwa kuwa baada ya kuokoka hawakai chini wakafundishwa MSINGI, Msingi wa Wokovu. Baada ya kuokoka tu mtu anakuwa anadhani tayari amejua kila kitu, na ndiyo maana unaona vituko vinavyoendelea katika kanisa. Ukweli ni kwamba mtu anapokata shauri ni mtoto, anatakiwa kulelewa, kuelekezwa kwanza! Chukua mfano wa mtoto mchanga anapozaliwa: Kwanza anapewa maziwa, ndipo uji, baadaye chakula laini, na mwisho huweza kula pamoja na wengine. Anapozaliwa, anaanza na kukaa, kutambaa, kusimama, kisha kutembea, na mwisho hukimbia.

Turudi kwenye somo: Misingi hiyo ni ipi? Misingi hiyo ni:

1.Kutubia kazi zisizo na Uhai.

Hapa anazungumzia TOBA, kitu ambacho wakristo wengi hawakifahamu. Kutubu ni kuacha, kughairi, kugeuka, kutokurudia tena. Lakini kuna wakristo huwa wanakwenda kutubu kila jumapili, au kila wakikutana kanisani, au kila wakitaka kusali. Tuone maandiko yanavyoeleza kuhsu TOBA:

Yoh 5:14; Usitende dhambi tena.

Yoh 8:11;Usitende dhambi tena.

1Yoh 5:18;Aliye wa Mungu hujilinda.

Mw 4:6-7; Dhambi ipo mlangoni inakuotea, lakini unapaswa uishinde.

Ndugu zangu, dhambi ziko za aina mbali mbali, na zina nguvu mbali mbali. Inahitaji mtu kuamua kama anataka kushinda dhambi, kwa kuwa anashindana na kitu chenye nguvu.

Mith 5:22; “Ameshikwa kwa kamba za dhambi zake” kumbe dhambi zina kamba. Na tukisoma katika Zab 107:10, 14,16 tunaona maneno: taabu na chuma,  milango ya shaba, na mapingo ya chuma. Ndio maana BWANA akasema kuwa atayavunja. Isaya  45:2-3. Maandiko hayo kielelezo mojawapo kinachoonyesha nguvu ya dhambi na ambavyo inatakiwa kuvunjwa.

Kupitia somo hili napenda kukujulisha kuwa toba ni kujutia na kuacha yale tuliyoyafanya. Ni kumwambia Mungu kuwa sasa basi nimeacha, siyo kumwambia mtu kila jumapili, mpaka jumapili nyingine tena. Wengine wanaficha dhambi wakidhani hakuna ajuaye. Hebu soma mstari huu kwa makini katika Mith 28:13 usemao:    “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema” Ndugu mpendwa, usifiche dhambi yoyote katika maisha yako. Kumbuka kuwa dhambi ni roho, ikemee, ipeleke mahali ambapo itakemewa na kwa kuwa ina masikio itasikia, na ukiionyesha kabisa kuwa umeikataa, itakuacha!

Katika Mith 8:13 tunasoma: “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu”, Hivyo kama tutasema tunamcha Mungu, na huku bado tunapenda uovu, hapo ujue mambo bado. Tukimcha Mungu twatakiwa kuacha kabisa uovu. Siyo kuutubia na kuurudia tena kwa lengo la kuja kuutubia tena siku zijazo!

2.Imani kwa Mungu.

Ndugu zangu Mungu wetu anapenda Imani yetu tuiweke kwake, na si kwa kitu kingine chochote. Unajua ukimwamini Mungu hakuna kitakachokutikisa. Hapo ndipo walipotokea akina Shadrack, Meshack, na Abednego. Ni kwa sababu walimwamini Mungu.

Ukimwamini Mungu utamngojea kwa kila jambo; maana wako watu wanaokwenda mbio, hawamsubiri Mungu. Kumbuka Neno linasema kuwa aaminiye hatafanya haraka. Isaya 28:16. Aaminiye hatafanya haraka, hatafanya haraka: kuchoka, kukata tamaa, kuchoka kusubiri. Na hata kuna misemo ya Kiswahili isemayo; Subira yavuta heri; Haraka haraka haina mbaraka na Mwenda pole hajikwai! Watu wamefanya haraka, mwisho wakaingia hata katika huduma kabla hawajaiva, wengine walifanya haraka  wakapindua baba zao kutoka kwenye viti wakakaa wao. Hiyo ni mifano ya hasara za kufanya haraka na haraka hizo ni haraka za kuelekea katika kupotea. Mith 20:21 inasema:

“Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake lakini hautabarikiwa” (Kuna wengine huua wazazi wao ili warithi!)

3.Kuwekea mikono.

Hili suala la kuwekea mikono, ni suala ambalo linatakiwa watu wafundishwe kabisa; waelewe kuwa mtu yeyote anayekuwekea mikono, kuna kitu kinatoka kwake kinakuja kwako. Wengi wamewekewa mikono na watu wasiowajua, na madhara yakawapata. Roho mbali mbali huwaingia watu kwa kuwekewa mikono.

Katika 1Tim 5:22 mtume Paulo anasema, “Usimwekee mtu mikono kwa haraka…..” na kinyume chake ni sahihi kuwa “ Usiwekewe mikono kwa haraka” Mkristo anapaswa kufundishwa jinsi ya kutunza kichwa chake, siyo kichwa cha kujifunzia kuomba kwa wahubiri. Hiyo yote ni misingi ya mkristo. Maandiko yafuatayo yatakusaidia kujifunza zaidi kuhusu kuwekewa mikono. 1Tim 4:14; 2Tim 1:6; Mdo 6:6; Mdo 8:17.

Kila unapowekewa mikono jiulize ni kwa nini ananiwekea mikono? Siyo suala la kutega-tega kichwa kwa kila umwonaye mbele yako, ili akuombee. Ndiyo maana Mungu alitoa vipawa hivyo, akatoa WACHUNGAJI. Wapo wakristo ambao hawana mchungaji, wao husema kila mtu ni mchungaji wake, huo ni upotofu. Biblia inasema Mchungaji wako atatoa hesabu yako mbele za Bwana, wewe unasema WACHUNGAJI watatoa habari zako.

4.Mabatizo.

Kuna mabatizo ya aina 3: i).Ubatizo wa Maji. ii).Ubatizo wa Roho mtakatifu na iii). Mateso. Sitaweza kuyaelezea hayo yote kwa mistari yake, lakini ukinitaka kufanya hivyo nitafanya, ila ninaelezea kidogo huo wa MATESO.

Katika Luka 12:50 Bwana Yesu alisema “nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!”

Ukipata muda soma Ebr 11:35-39. Lakini ukipata muda pitia kitabu hiki kinachoitwa kitabu cha mashujaa wa Imani.

Efeso 2:20 inasema tumejengwa juu ya msingi wa MITUME na MANABII. Maana yake nini? Tutaipitia njia waliyoipitia; Yatatupata yale yaliyowapata wao.

Mdo 14:21-22. “Imetupasa kuingia katika ufame wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” Pata muda usome maandiko haya machache uone yale ambayo mitume waliyafanya: Mdo 14:8; 2Falm 5;25.

Mungu atusaidie tuipite njia waliyoipitia wenzetu waliotutangulia katika huduma hii ya kumtumikia Mungu.

5.Kufufuliwa wafu

Tunatakiwa kufundishwa vizuri tujue kuwa mtu  yupo katika nafsi 3 ambazo ni MWILI NAFSI na ROHO.Tunatakiwa tuelewe kuwa mtu anapokufa huwa ni nini kimemtokea; kuwa roho yake imemtoka pamoja na nafsi yake na viko mahali alipovichagulia vikae milele, na mwili tunaurudisha mavumbini uliko kuwa. Na pia tufundishwe kuwa siku moja  utafufuliwa ama upate UZIMA WA MILELE, au AIBU NA KUDHARAULIWA MILELE. Dan 12:2; “Tena wengi wa hao walalao katika mavumbi ya ardhi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, na wengine kudharauliwa milele”.

Tukielewa hiyo wala hatutangoja siku ya kufa ndio tuombewe, na kumwambia Mungu kuwa sasa MUWEKE  MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI!

6.Hukumu ya milele.

Ni vizuri tufundishwe ili tuelewe kuwa kuna hukumu ya milele; ambayo watu wataingia motoni  milele. Na hapa inabidi uelewe kuwa SIYO watu peke yake. Hapana! Kuna mpangilio wa kuingia humo kwa wale watakaokwenda huko. Ngoja nikupangie:

Ufunuo 19:20; “Yule mnyama akakamatwa, na yule Nabii wa  uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wake, walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake, hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto. Liwakalo kwa kiberiti

Ufunuo 20:10; “Na yule ibilisi mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku, hata milele na milele

Ufunuo 20:14; “Mauti na kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto

Ufunuo 20:15; “Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameameandikwa katika kitabu cha uzima,  alitupwa katika lile ziwa la moto”

Ndugu zangu msingi ndiyo nyumba kama nilivyokwisha sema, kama uliokoka na hujawahi kufundishwa mambo hayo, ambayo ndio msingi wa mkristo, usijifariji. Hebu amua jifunze hayo, uyafahamu na uyafanye ndipo utasimama katika wokovu wako, ulioamua kuushika.

Nimekuonyesha misingi ya wokovu; na mahali pengine Biblia inasema “kama MISINGI ikiharibika mwenye haki atafanya nini?”

Kumbuka kila unapofanya chochote kwa Mungu unajenga, ndio maana imeandikwa habari ya wajenzi wawili katika Mathayo 7:24-27. Hapo anaeleza kuwa wapo wajenzi wawili, mmoja amejenga juu ya MWAMBA, na wa pili amejenga juu ya MCHANGA.

Nyumba zote zinaonekana zimesimama lakini kinachowatofautisha ni pale majaribu yatakapotokea: ndipo aliyejenga kwenye mwamba nyumba yake itasimama lakini aliyejenga kwenye mchanga haitaweza kusimama, itaanguka tu!

Mpendwa msomaji kwa leo naishia hapo nikisema maombi haya kuwa Mungu atusaidie tunapojenga kwenye MSINGI aina ya mwamba ambao ni Yesu Kristo, na mchanga ni pale utakapojenga Imani yako juu ya kitu chochote kile tofauti na Imani katika Kristo Yesu. Hebu tukubali kujufunza na kifahamu Misingi ya mkristo ili tuweze kufanikiwa katika safari yetu ya kwenda mbinguni.

Ni mimi ndugu yenu, Mchungaji Samwel Imori.


Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia -XI

Luka 13:22 - Mtu mmoja akamuuliza Bwana Yesu Je! Watu wanaookolewa ni wachache? Bwana akamjibu akamwambia jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze.

Si nia yangu kumkatisha mtu yeyote tamaa ya safari ya mbinguni, ila niko hapa kukuonyesha jinsi inavyohitajika kuamua katika safari hii. Mahali pengine maandiko yanasema  tangu enzi za Yohana mbatizaji habari njema ya ufalme inahubiriwa, na wenye nguvu wauteka huo ufalme. Nimekuwa nikizungumzia sababu mbali mbali zitakazowazuia watu kuingia wakati wanataka. Na leo tunaendelea kuona sababu zaidi katika Sehemu Ya Kumi ya somo hili.

16. HAWATAELEWA FAIDA YA WOKOVU ( KUMTUMIKIA MUNGU).

Katika Mathayo 19:27 tunaona maneno ambayo mtume Petro alimuuliza Bwana Yesu kuwa walikuwa wameacha vitu vyote na kumfuata Yesu, Je! Watapata NINI? Mara nyingi napenda kusema kuwa hakuna mtu yeyote duniani mwenye akili timamu anayependa HASARA. Petro alitaka kujua atakachokipata, baada ya kuwa ameamua kuacha vyote na kumfuata Yesu. Kama ingetokea Bwana Yesu amjibu kuwa fanya kazi maana UNAJITOLEA, nadhani hapo ndipo ingekuwa mwisho wa Petro. Lakini kwa kumjibu alimwambia atapata mara mia, katika ulimwengu huu na uzima wa milele baadaye.

Habari hii pia tunaiona katika Marko 10:28-31 huku tofauti ikiwa ni kuongezwa maneno PAMOJA NA DHIKI katika Marko. Ndiyo maana katika Galatia 6:9 mtume Paulo aliandika maneno fulani ili kuwaambia Wakristo waendelee kufanya kazi ya Mungu bila kuchoka, maana malipo yapo baada ya kazi hii katika dunia hii. Maneno hayo ni:

Tena tusichoke katika kutenda mema, kwa maana tutavuna kwa wakati wake tusipozimia roho.

1Kor 15:58; “Basi,ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana”.  Yaani kazi ambayo italipwa ni ile iliyofanywa katika Bwana,( sio kazi yoyote, katika Bwana. Ndiyo maana anasema ni wale tu wafanyao MAPENZI YA BABA YANGU). Kumbe unaweza ukafanya kazi ya Mungu, lakini yakawa siyo mapenzi ya Mungu.

Katika Ebrania 6:10 tunaona kuwa Mungu si dhalimu hata aisahau kazi ya mtu. Hii ina maana kuwa Mungu hawezi kudhulumu mtu yeyote. Ndio maana imeandikwa “kila mtu atavuna kile alichokipanda”.

Faida ya Kumtumikia Mungu.

Leo ninakupatia baadhi ya faida utakazozipata kama ukiamua kumtumikia Mungu kwa dhati. Faida hizi ni zile utakazopata ukiwapo hapa hapa duniani. Najua tutalipwa pia na mbinguni, lakini leo naongelea faida za hapa hapa duniani.

-Mithali 11:31 – Mwenye haki atalipwa duniani, na mkosaji pia.

-Mithali 11:25 – Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa. Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. Maana yake ni chochote unachofanya kwa watu, ujue na watu pia watakufanyia. Ukifanya ubaya, ndivyo utafanyiwa; Ukifanya wema ndivyo utafanyiwa.

-Mith 12:14 – Utavuna chochote utakachokipanda.

-Mith 20:7 – Chochote utakachokifanya, kizuri au kibaya, utawaachia watoto wako. Wakati mwingine unaweza kudhani uko salama, kumbe utawaachia watoto wako ama BARAKA, au LAANA.  Ukiangalia kwa makini katika 1Falme 4:24-25 kuna maandiko maneno yanayosema kuwa Sulemani alistarehe pande zote. Swali ni kwa nini alistarehe? Hii ni kwa sababu baba yake alikuwa amepigana vita vya kutosha, alikuwa amesukumia mbali maadui kiasi cha kuwa mbali sana na Ufalme wake Sulemani.

-Mith 13:22 – Huwaachia WANA WA WANA–

Unaona sasa imekwenda kwa  WAJUKUU. Ndiyo maana tunasema  Mungu wa IBRAHIM, ISAKA, na YAKOBO. Leo hii watu wengi wanahangaika kwa sababu ya yale ambayo baba, babu zao walifanya; Wao wanahangaika leo, au wanafurahia leo.

-Luka 7:2-5 -Kuna maneno yanayoonyesha jinsi Wazee walivyomwambia Yesu kumtendea jambo jema mtu ambaye aliwajengea sinagogi. Hivyo kwa kuwa alijenga SINAGOGI basi alistahili kutendewa jambo hilo. Kumbukumbu ni muhimu sana. Leo hii kuna watu wameshapita lakini hakuna kumbukumbu lolote. Walikuwa na mali, walikuwa na uwezo, lakini leo hakuna kumbukumbu lolote kuwa walikuwepo duniani.

-Mith 10:27-Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu. Mpendwa Neno linasema wazi wazi kuwa kama utakuwa ni mcha Mungu miaka yako itaongezwa, mahali pengine inasema AKASHIBA SIKU.

-Zab 90:10-Miaka yetu ni sabini, themanini tukiwa na nguvu.

Anaposema tukiwa na nguvu, anasemaje? Anamaanisha KAMA TUKIWA NA SABABU YA KUWEPO DUNIANI.

-Katika Isaya 54:12-17 tunaona faida tupu kama ukimcha Mungu, sitaikopi hapa, tafadhali tafuta muda uisome uone. Waweza soma pia faida tele katika Isaya 43:2 na uone kuwa hakuna hasara yoyote katika kumcha Mungu.

-Ayub 5:19-27. Ayubu alikuwa ni mzee wa siku nyingi hivyo alijua faida tele za kumtumikia Mungu. Ndiyo maana aliandika namna hiyo hapo, ebu soma uone!

Nimalizie kwa kukuachia mifano mbali mbali ya watu waliomtumikia Mungu na kuona faida zake, ambao habari zao tunazipata katika Biblia. Pata muda usome maandiko kuhusu mifano hii:

-Mdo 9:36-Dorkas.

-Isaya 38:1-Hezekiah.

-Esta 3:12-Mordekai.

-Mdo 10:1-Cornelio.

Nakutakia kila la kheri wakati unajiandaa kulipwa na Mungu wako unayemtumikia katika ulimwengu huu na ule ujao.

Mbarikiwe.

Ndugu yenu  Mchungaji Samweli Imori..

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – X

Bwana Yesu alisema “wengi watataka kuingia lakini wasiweze..” Neno hili limeendelea kuimba ndani ya moyo wangu kuwa niwaambie watu, niwaelekeze yale yatakayowazuia kuingia wakati wanataka.

Kuishi motoni milele ni jambo baya sana. Watu hawataki kusikia kuwa kuna wengine wataishi motoni milele. Ndio maana wamejitungia kuwa wakati utakuja watu wengine watawekwa mahali ambapo watateswa kwa muda,  wakati huo wakisafishwa kisha waingie Mbinguni. Wanasema kuna mahali panaitwa PARAGATORI. Lakini ukitafuta katika Biblia yote hakuna kitu hicho, kuna mahali pawili tu: Mbinguni katika raha ya milele na Motoni kwenye mateso ya milele. Mtu anatakiwa kuchagua lakini wengi wanasema Mungu ndiye atakuchagulia pa kukaa milele. Hapana! Hivyo sivyo lisemavyo Neno la Mungu.

Tukisoma Biblia katika Kumb 30:19-20 Neno la Mungu linasema hivi:

“Nazishuhudia Mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako, Uzima na mauti, baraka na laana, basi chagua uzima ili uwe hai wewe na uzao wako, Kumpenda Bwana Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye, kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako, upate kukaa katika Nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahim na Isaka, na Yakobo kuwa atawapa.”

Unaona! Uchaguzi ni wangu na wako: Tunatakiwa kuchagua katika ya kuishi Mbinguni milele au Motoni milele.

Leo, katika kuendelea na somo letu kwenye Sehemu hii ya Kumi, tutaona sababu nyingine itakayowazuia watu kuingia mbinguni huku wakiwa wanataka. Sababu hii ni:

15. HAWATAJUA MAANDIKO WALA UWEZA WA MUNGU.

Marko 12:24 “Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?”

Kumbe waweza kujua MAANDIKO lakini usijue UWEZA wa Mungu!  Na waweza kujua UWEZA wa Mungu lakini usijue MAANDIKO.

Katika 2Tim 3:16-17 Biblia inasema kuwa kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. Hii inatufundisha kuwa tukubali kila tunapoonywa na Neno la Mungu, kila tunapokatazwa chochote na Neno la Mungu, tukubali, tutii.Vinginevyo tutakasirika, na tutakuwa adui za wale wanaotumiwa na Mungu kutuonya na kuturudi. Ndiyo maana mtume Paulo akasema katika Gal 4:16, Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?

Kuna msemo wa Kiswahili usemao: MSEMA KWELI NI MPENZI WA MUNGU. Lakini nataka nikuambie kuwa wasema kweli wote wanakutana na vipingamizi vingi mno! Kusema kweli kwao huwasababishia mateso mengi sana. Hao ndio kama akina MIKAYA. Mikaya alisimama katika kweli, mpaka Mfalme akasema atiwe jela, ale kwa shida, anywe kwa shida mpaka atakaporudi. Mikaya hakujali na akaendelea kusema ukweli kwa kuongeza kuwa Kama mfalme angerudi salama, basi Bwana hakusema naye! Na  akamalizia kwa kusema: sikieni watu wote! 1Wafalme 22:28

Wasema kweli hawaogopi. Wasema kweli hawapendwi maana hawapendezi mtu bali wanapendeza Mungu. Hutawasikia wanasema kuwa WATU WATANIELEWAJE?  Bali wao wakati wote husema MUNGU ATANIELEWAJE?

Tunatakiwa kuyajua maandiko! Kijana alimuuliza Bwana Yesu swali, akiuliza kuwa mwanamke aliyeolewa na wanaume saba, hapa duniani, na wote wakafa, na tunaelekea Mbinguni, Je mwanamke huyo atakuwa wa nani? Unaona! Yeye alitaka kuhamisha vita vya duniani vya kugombea wanawake na wanaume apeleke Mbinguni. Ndipo Bwana Yesu akamwambia anapotea kwa kutojua Maandiko wala Uweza wa Mungu. Wakati mwingine watu wameuita uweza wa Mungu kinyume cha maandiko, na hapo Mungu atakaa kimya kwa kuwa Mungu hutembea katika Neno lake.

Yoh 18:37-38, “Pilato akamwambia wewe u mfalme basi? Yesu akasema wewe wasema kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajilibya haya mimi nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mstari wa 38, Pilato akamuuliza Kweli ni nini?”

Unaona jinsi Pilato alikuwa hajui kweli maana yake nini. Watu wengi leo wanafanana na Pilato. Hawajui kweli ni nini. Neno linasema nanyi mtaifahamu kweli nayo kweli itawaweka huru. Kweli ni Neno la Mungu. Ndilo linaweka mtu huru. Sasa mtawala mzima hajui kweli, eti anauliza kweli ni nini!

Wakati Bwana Yesu akiwa pale msalabani, habari inayopatikana katika Math 27:45-50, kuna maneno yasemayo: “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? yaani, Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema Huyu anamwita Eliya. Mstari wa 49: Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.”

Andiko hili linaonyesha jinsi watu wanavyoshindwa kuelewa kile maandiko yanamaanisha. Ndiyo maana vituko katika mambo ya imani vimekuwa vingi katika kizazi chetu. Kama ambavyo watu wale walitafsiri Eloi kuwa ni Elia hata leo wako wanaotafsiri maandiko kwa namna wanavyoona wao na kusababisha watu wasipate kile ambacho maandiko yanamaanisha!

Katika Mathayo 26:31-32 Kuna maneno aliyoyasema Yesu: “Ninyi nyote mtachukizwa wa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa nitampiga mchungaji na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu nitawatangulia kwenda Galilaya”. Kwa hiyo, kama wangeyaelewa maneno hayo sawa sawa, walipaswa kwenda Galilaya, ndiko wangemuona. Lakini wao walikwenda kukaa kaburini!

Hata siku za leo watu wako makaburini, wakidhani bado yumo kaburini. Wako kwenye matambiko.  Lakini Bwana hayumo  kaburini, yu hai anaishi milele na milele na wala hafi tena!

Katika Math 26:57-61, wakati Bwana Yesu akiwa mbele ya Kayafa na ushahidi wa kumshaki unatafutwa, hata kama ni wa uongo, tunaona maneno ya kushangaza katika ule mstari wa 61: “Hata baadaye wawili wakatokea wakisema, Huyu alisema, naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu” Huo ni uongo mkubwa maana Yesu alikaa duniani miaka yote mitatu na hakuwahi kusema hivyo hata kidogo. Ngoja tuone Isemavyo Biblia:

Yohn 2:19, “Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha”.

Yesu aliposema HEKALU wao moja kwa moja walidhani ni JENGO maana wao ndilo walikuwa wanafahamu kuwa ndilo hekalu la Mungu. Na hata leo hii  wengi sana bado wanadhani hekalu ni JENGO. Ndiyo maana wanapokuwa kanisani: Wanajitahidi, wasivute sigara, wasilewe, wasiseme mabaya. Wakiwamo kanisani, hata wanatembea kwa mwendo wa pole wakimaanisha ndiko kutembea kitakatifu, wanaimba kitakatifu kabisa. Lakini wakiishatoka humo, na ukawakuta nje ya jengo/hekalu hutaelewa kabisa kuwa ndio wale walikuwa wanaimba kitakatifu katika jengo lao la kuabudia .

Biblia inasema Kanisa ndilo litakalonyakuliwa.  Je! Ni kweli kuwa ni JENGO ndilo litakalonyakuliwa?

Tukisoma maandiko katika 1Kor 6:19-20 na 1Kor 3:16-17 tunaona wazi wazi kuwa kumbe hekalu la Mungu ni watu; watakatifu aliowaokoa, akawahesabia haki. Hao ndio wanaitwa KANISA au kwa maneno mengine Hekalu la Mungu, Roho mtakatifu anakaa ndani yao. Ndivyo Yesu alimaanisha aliposema kuwa: “livunjeni hekalu hili, nami nitalisimamisha  kwa siku tatu”. Wao walishangaa sana kusikia maneno hayo maana hekalu lile lilikuwa limejengwa kwa miaka mingi sana. Ndiyo maana walishangaa sana aliposema kuwa atalisimamisha kwa siku tatu tu! Kauli hiyo iliwachanganya kabisa. Kumbe Yesu alikuwa anasema habari ya mwili wake. Unaona hapo walivyopotea, kwa kutokujua Maandiko?

Katika Efeso 5:27 maandiko yanasema: “apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo, bali liwe takatifu lisilo na mawaa” Pale penye kusema “Kanisa takatifu, lisilo na ila wala kunyanzi” ndipo watu wengi wanapotea, wakisema hakuna watakatifu hapa duniani. Mpendwa, ebu soma vizuri, labda ukatae tu, lakini Biblia imeeleza wazi kabisa:

Zab 16:3, Watakatifu waliopo duniani hao ndio waliobora.

1Pt 1:15-16, Kama yeye aliyewaita alivyo mtakat8ifu, nanyi iweni watakatifu kama yeye.

Math 5:48, Nanyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu alivyo mkamilifu.

Uf 21:27, Ndani ya mji huo wa Mbinguni hakitaingia kamwe kilicho kinyonge.

Uf 22:15. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi . . . .

Ndugu yangu mpendwa, ebu soma Biblia. Pata muda wa kusoma Biblia kwa Bidii ili upate kuyajua maandiko. Pia mtafute Bwana na nguvu zake.

Yesu alisema: “Mnapotea kwa kuwa hamyajui MAANDIKO wala UWEZA wa Mungu”. Mpendwa, kumbuka Biblia ina mistari 31,173. Ni ujumbe wa Mungu kwa wanadamu. Tukubali kujifunza. Twahitaji muda wa kutosha ili kujifunza yale yaliyoandikwa katika mistari hiyo ya Biblia.

Naomba kwa Mungu ili kila atakayesoma ujumbe huu aelewe jinsi anavyowiwa kujifunza Neno la Mungu pamoja na kuufahamu Uweza wa Mungu.

Tuonane Sehemu ijayo ya somo hili.

Ndugu yenu: Mchungaji  Samwel  Imori.

 

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – IX

Wapendwa, tunaendelea na mfululizo wa somo letu la Mstari Unaoniliza kuliko yote katika Biblia. Nirudie kidogo kuwa katika Biblia kuna mistari 31,173.Yote ni muhimu sana na yote ina maelekezo. Lakini mstari wa 13 katika kitabu cha Luka Sura ile ya 24 wenye maneno haya: “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze” ni mstari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia. Na katika mfululizo huu nimeweka na ninaendelea kuweka sababu ambazo zitawazuwia watu wengi kuingia mbinguni huku wao wakiwa wanataka. Na leo tutaendelea kuona sababu zaidi.

14. HAWATAJUA MAANA YA NEEMA.

Tito 2:11-14. Maana Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa…..!

Nilikuwa nafundisha mahali fulani na nikauliza maana ya Neema. Kulikuwa na majibu tofauti kama vile: Ni Huruma za Mungu, Ni upendeleo wa Mungu, Ni msaada wa Mungu, nk. Mimi niliasema vema kwa kila mtu aliyejaribu kutoa mawazo yake, pengine na wewe una mawazo yako kuwa Neema ni nini?? Mimi nilitoa mawazo yangu kuwa Neema ni AJIRA. Turudi tena kwenye mstari wetu:

Nayo yatufundisha…..

i.KUKATAA UBAYA.

ii.KUKATAA  TAMAA ZA KIDUNIA.

iii.TUPATE KUISHI KWA KIASI, KWA HAKI, na KWA UTAUWA, KATIKA ULIMWENGU HUU WA SASA.

Mistari inayoendelea inasema: “Tukilitazamia tumaini lenye baraka, na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu, ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe”  Kaama tunataka kupona tukubali tusafishwe!

iv. WALE WALIO NA JUHUDI KATIKA MATENDO MEMA.

Kwa nini nimesema kuwa NEEMA NI AJIRA?

Neema ikiishakuita ili iwe Neema kuna mafundisho inakufundisha, kuna AJIRA inakupatia, endelea kufuatana nami utanielewa.

Katika Luka 1:26-34 kuna maandiko yanayosema kuwa malaika alipeleka taarifa kwa Binti, Bikira aliyeitwa  Mariamu, akamwambia kuwa umepata Neema. Kwa kuwa umepata Neema sasa unapewa AJIRA: UTACHUKUA MIMBA NA UTAZAA MWANA. Mariamu alijitetea kuwa hamjuwi mume. Hapa alikuwa anasema nini? Unajua msichana yeyote aliyepata mimba akiwa nyumbani kwao, kabla ya kuolewa, katika Taifa la Israel, alikuwa akipigwa kwa mawe na kufa. Biblia inasema ndivyo walivyouondoa uovu katika Israel. Mariamu alijua sasa hataishi, ni hatari. Si huyo tu. Yusufu naye alipogundua kuwa huyu binti tayari ana mimba, na hajaolewa, yeye hajakaribiana naye, akajua huyu hataishi, atapigwa mawe. Akajisemea mwenyewe: “Ili nisione haya yakitukia natoroka, nimuache!” Biblia inasema malaika alimtokea Yusufu akamwambia usiogope. Angeweza kusema, “Yusufu usiogope, Mariamu ameajiriwa na Mungu!”

Katika Mwanzo 6:7-34 Mungu alimwambia Nuhu kuwa “mwisho wa wanadamu wote, wanyama wote, ndege wote, umefika. nitawaua kwa maji, LAKINI WEWE UMEPATA NEEMA”. Kwa maneno mengine “LAKINI WEWE NAKUAJIRI”. Ndipo akamwelekeza jinsi ya kutengeneza SAFINA, akasikiliza maelezo, na yeye akayafuata. Alimbiwa Urefu, Upana, Mahali pa kuweka mlango, Miti ya kutumia na kisha aipake Safiina kwa Lami . Mwanzo 6:22 inasema “Ndivyo alivyofanbya Nuhu, sawa sawa na vyote alivyimwamuru Mungu. Hivyo ndivyo alivyofanya”. Mwanzo 7:5; Nuhu akafanya kama vile BWANA alivyomwamuru. 

Tukisoma Yak 2:14-26 tunakuta maandiko yanayoelezea habari ya Imani na matendo. Soma kwa makini maelezo hayo kuwa Imani bila matendo imekufa nafsini mwake.

Mwandishi wa kitabu hicho anasema; Mmoja aonyeshe Imani bila matendo, na mwingine aonyeshe Imani yake pamoja na matendo. Watu wengi wameokoka kwa maneno, kwa midomo. Ukiwauliza mbona hivyo? wanasema hatukuokolewa kwa matendo, bali ni kwa NEEMA. Sijakataa kabisa, na sitakataa, ila nasema Baada ya NEEMA kukuokoa imekwambiaje?. Imekufundisha kufanyaje?

Yak 4:17;Yeye ajuaye kutenda mema wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi. Yeye anayeikubali NEEMA kisha NEEMA IKAMFUNDISHA, NA ASIFANYE KILE NEEMA INAMFUNDISHA KWAKE HUYO NI DHAMBI. Wangapi leo wako dhambini? kwa kwa wanafundishwa kila leo, wanakatazwa hiki na hiki kila leo, lakini hayo ndiyo wanayoyafanya?

Math 7:21-23; Si kila mtu anayeniambia Bwana Bwana atakayeingia katika Ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni. Wengi wataniambia siku ile Bwana, Bwana hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.  Inatisha ndugu yangu, Neema iliwafundisha, Neema iliwakataza, Neema iliwaagiza, lakini hawakufanya!

Yoh 13:17; Mkiyajua hayo kheri ninyi mkiyatenda. Tukigeuza mstari huu utasomeka hivi; Ole mkiyajua hayo kisha msiyatende!. Hebu nikuelekeze mpendwa: Kusema tu “nimeokoka” hakutakusaidia kitu chochote. Wengi leo ni  WAZURURAJI. Nisamehe kwa kuwa nitatumia neno hili kuelezea kile ninachotaka kukuelezea. Wakati mwingine msako hutokea mjini, polisi wanapita, wanauliza VITAMBULISHO wanaokutwa hawana wote wanakamatwa, wanaambiwa ni WAZURURAJI.  Maana kama ungekuwa umeajiriwa ungekuwa na kitambulisho! Wengi ni wazururaji. Hakuna kitu wanafanya. Hutembea kanisa hadi kanisa. Wakikuta hapo Kanisa limejengwa, viti vipo, speaker, nk, wao ni kufika na kukaa, basi! Jumapili anafika anakaa. Anahubiriwa, anaambiwa omba. Wengine wanalia, wanaenda nyumbani. Wiki ijayo tena anakwenda kwingine. Wiki nyingine kwingine. Mwezi unaisha. Anaanza tena. Akiulizwa “unafanya nini?” Utasikia anajibu: “Tumeokolewa kwa neema!”

Wengine ni WASHANGILIAJI. Katika mpira wachezaji ni kumi na mmoja (11),  wengine wote wanakaa kwenye jukwaa, kazi yao ni kushangilia, kukosoa jinsi wengine wasivyojua kucheza.

Soma kwa makini 2Petro 1:3-11 ili ujue kuwa unachotakiwa kufanya baada ya kukutana na NEEMA:

i.   Tumekirimiwa Tabia ya Uungu.

ii.  Tunaokolewa na uharibifu uliomo duniani.

iii. Tukijitahidi kwa upande wetu, katika Imani yetu- TIENI WEMA.

iv.  Katika wema wetu  tutie MAARIFA.( Maarifa ni Neno la Mungu)

v.   Katika Maarifa yetu– KIASI.(self controll)

vi.  Katika Kiasi chetu  tuweke  SABURI- (  saburi ni kungojea, kutokuwa na haraka)

vii. Katika Saburi yetu-   UTAUWA ( Utakatifu)

vii. Katika utauwa wenu- UPENDANO WA NDUGU. ( upendo wa kweli)

ix. Katika upendano wa ndugu- UPENDO.   ( upendo ni Mungu mwenyewe hata muimbaji mmoja   aliimba kuwa MUNGU NI PENDO). Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele yawafanya kuwa siyo wavivu, wala sio watu wasio na matunda kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. MAANA YEYE ASIYE KUWA NA HAYO NI KIPOFU, HAWEZI KUONA VITU VILIVYO MBALI. AMESAU KULE KUTAKASWA DHAMBI ZAKE ZA ZAMANI.

x. Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu, na uteule wenu; maana MKITENDA HAYO HAMTAJIKWAA KAMWE. (2Petro 1:10)

Ndugu yangu, nilikuwa nakuelezea kuwa kwa upande wangu mimi niliiita NEEMA kuwa ni AJIRA. Hebu jikague tangu umepata NEEMA hii ya Wokovu, umefanya nini? Sasa hivi unafanya nini? Unajipanga kufanya nini? Wewe ni mshangiliaji?  Wewe ni mzururaji?  Mkaguzi wa  makanisa?  Unakagua ya nani aliyekujengea? Kumbuka umeajiriwa, na malipo yapo mbele yako! Kazi yako itapimwa. Kama hayo yote unayasubiri, Je! Kazi yako itakaa au itateketea?

Nakutakia kila la heri katika AJIRA yako.

Nduguyo Mchungaji  Samuel  Imori

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – VIII

Wapendwa, leo tunaendelea na somo letu lisemalo Mstari unaoniliza kuliko yote katika Biblia. Hadi sasa tumekwisha ona sababu kumi na mbili (12) zitakazofanya watu washindwe kuingia mbinguni huku wakiwa wanataka. Katika Sehemu hii ya Nane (8) tunaendelea kuona sababu zaidi:

13. HAWATAKUWA WATU WAZIMA.

Kusudi la Mungu kutuzaa mara ya pili kwa njia ya Neno lake ni ili tukue tuwe watu wazima.

Ebrania 5:11-14; Ambaye tuna maneno mengi ya kusema katika habari zake, na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia, kwa maana iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita) mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu, nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana Neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga, lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na  mabaya..

Mpendwa kama nilivyosema hapo juu, kusudi la Mungu la kutuzaa kwa njia ya Neno lake ni kuwa tukue, tuwe watu wazima katika Imani. Hata mzazi anapolea mtoto pia hilo ndilo kusudi lake kuwa mtoto yule akue, siku moja aache kunyonya, akae, atambae, asimame, atembee, akimbie, mwisho siku moja awe mtu mzima.

Paulo anasema alikwenda kwa Waebrania, amebeba mafundisho mazito ya Neno la Mungu akidhani atakuta watu wazima awafundishe, awaelekeze, kumbe akakuta ni watoto wanaohitaji maziwa. Na ukumbuke kuwa wakristo tuko vitani, tunapigana na adui yetu shetani, kitakuwa kichekesho kama kuna vita kati ya Nchi na Nchi, kisha Nchi moja ipeleke watoto wa darasa la pili, la tatu, kupigana kitakuwa kichekesho kabisa!

Efeso 4:13-15; Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani, na kumfahamu sana mwana wa Mungu,  hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli, katika pendo na kukua , hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

Ukisoma mistari hiyo vizuri inaeleza Mkristo anatakuwa akue, awe mtu mzima. Unajua mtu mzima kwa kusema kweli, haanguki hovyo hovyo. Watu wazima hawagombani hovyo hovyo, lakini watoto waweza kuanguka chini hata peupe, mpaka unashindwa nini kimemwangusha mtoto huyu. Mtoto aweza kugombana na mtoto mwingine kwa ajili ya toi, au kwa ajili ya nyumba ya mchanga, ambayo hata hawezi kulala ndani yake, akisema ‘umenikanyagia nyumba yangu!’

Efeso 4:11-12; Naye alitoa wengine kuwa Mitume, na wengine kuwa manabii, na wengine kuwa wainjilisti, na wengine kuwa Wachungaji na Waalimu kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.

Ndio maana tunasisitiza kuwa ili kanisa likue, liwe watu wazima, wanahitaji huduma zote hizo tano, lazima tukubali Yapo makanisa hayatambua huduma hizo, mengine yanatambua mbili, mengine tatu, lakini nasema tujifunze kwenye vidole vyetu 5 vyote! Ili mkono uwe mkono vyote vinatakiwa, hata kale kadogo kaweza kuonekana hakana maana sana, lakini ebu jaribu kutoa uchafu katika sikio lako! Lazima utumie kakidole kadogo, vinginevyo utadhuru sikio lako. Nyoosha mkono wako uone kuwa vidole vyote vinalingana. Pamoja na kutukulingana huko lakini vinahitajiana, na vyote ndipo huitwa mkono, kikipungua kidole kimoja ni KILEMA tayari.

2 Tim 3:7; Wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.

Unaona kuwa wapo watu ambao wanajifunza kila leo, lakini hawafikii ujuzi wa ile kweli. Kumbuka Biblia inasema, NANYI MTAIFAHAMU  KWELI, NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU. Na akisema hivyo tufahamu kuwa  Biblia yote ni KWELI, lakini ni kweli gani itakayotuweka huru??? NI KWELI TUNAYOIFAHAMU.

Hata ungeshikilia Biblia, ukawa unatembea nayo, hata ungeishona ikawa nguo, hata ungeinywa ikakaa tumboni mwako, hata ungeifanya kuwa mto ukalalia, bado haitakusaidia, itakuwa tu kama hirizi zingine, hirizi za ngozi za kenge, vitambaa vyeusi n.k.

Ndio maana unaona mtu anapewa kitambaa, mafuta, wala hana Imani juu ya Mungu, ila anakaa na mafuta hayo yamsaidie, wengine wanakunywa, imani inakuwa juu ya vitu hivyo wala si juu ya Mungu,

Gal 4:1-4; Lakini nasema kuwa mrithi wakati wote  awapo mtoto hana tofauti na mtumwa, angawa ni  bwana wa yote, bali yu chini ya mawakili, na watunzaji, hata wakati ulioamriwa na  baba. Kadhalika na sisi tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia, hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma mwanae ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.

Huo ndio utoto, unaona hata kama mtu ni tajiri kiasi gani, akitokea amekufa, kama mrithi wake ni mtoto, hawezi kukabidhiwa mali ile japo ni ya baba yake, mpaka awekewe watunzaji, wamtunzie, mpaka atakapokuwa mtu mzima ndipo atakapo kabidhiwa mali ya baba yake. Hiyo ndiyo hali ya Kanisa letu la leo, Mungu wetu anatupenda sisi tu warithi, warithi wa ahadi zake, lakini utakubaliana na mimi kuwa ni wachache wanaoweza kukabidhiwa mali ya baba yao.

Nikupe mfano, tunafundishwa kuwa kila tunapopata kipato, tunatakiwa kumtolea sehemu ya 10 Mungu kuwa hiyo ni mali yake. Mfano- anakupa laki 2  unatakiwa kumtolea 20,000.  Hilo ndilo fungu la kumi, la laki mbili. Na tukubaliane kuwa Mungu wetu siku zote anasema atatuinua, toka imani hata imani, utukufu hata utukufu. Sasa huyu wa laki mbili, anashindwa kutoa 20,000. Anasimama kuomba, na kuombewa kuwa Mungu mbariki, Mungu nibariki! unaweza kujua kuwa huwa anasemaje?:

Huyo anasema hivi: MUNGU KWA SASA UNANIPATIA LAKI 2,  NA HUWA NAKUIBIA  ELFU 20, NAKUOMBA UNIBARIKI, UNIINUE, UNIPANDISHE NIWE NAPATA LAKI 4,  ILI NIWEZE KUKUIBIA ELFU 40. Mpendwa Mungu ananyamaza kimya, maana bado  mtu huyu katika ile hela kidogo ameshindwa kuwa mwaminifu, na hata Mungu akimpa zaidi ndivyo ataendelea kuiba.

Hebu tukue, tuwe watu wazima! Na tunakuwa kwa njia gani?

Kusoma Biblia, kuomba, kuendelea kumfahamu Mungu wetu, kuendelea kumtafuta Mungu kila inapoitwa leo, bila kuchoka, bila kudhani tunajua, maana Neno linasema kuwa yule anayedhani kuwa anajua bado hajui kama inavyompasa kujua:

IKor 8:2 Mtu akidhani kuwa anajua Neno, hajui Neno lolote bado kama impasavyo kujua. 

Mpendwa tukubali kukua, tukubali kujifunza. Kama ule msemo usemao ELIMU HAINA MWISHO.

Mbarikiwe! Tuonane tena katika Sehemu ijayo, ya Tisa (9), ya somo hili la MSTARI UNAONILIZA KULIKO  YOTE KATIKA BIBLIA.

Ndugu yenu, Mchungaji  Samuel Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – VII

Wapendwa katika BWANA, Namshukuru Mungu atupaye uzima na kutuweka salama hadi leo hii ambapo tunaendelea na somo letu. Katika somo hili tunaangalia sababu zitakazowafanya watu wengine wasiingie mbinguni japo wanataka sana kuingia humo. Tumeshaangalia sababu Kumi na Moja (11) na leo tunaendelea kuangalia sababu zaidi. Naomba Mungu akupatie, wewe ndugu unayesoma hapa, moyo wa kuelewa na kisha kuyafanyia kazi yale unayojifunza hapa:

12. Hawatamjua Mungu wa Kweli. Katika Yoh 17:1-3 tunaona Bwana wetu Yesu aliomba maombi haya akisema, UZIMA WA MILELE  NDIO HUU WAKUJUE WEWE, MUNGU WA PEKEE, NA YESU KRISTO ULIYEMTUMA. Hapo ni kusemaje? kumbe kuna miungu wengi katika uso wa dunia. Biblia imesema kuwa wengine  mungu wao ni TUMBO, wengine mungu wao ni mungu wa dunia hii, yaani SHETANI.

1Nyak 28:9. Daudi aliyekuwa mcha Mungu alimuusia mwanae akisema, “Nawe Sulemani  mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali, kwa kuwa Bwana hutafuta tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote na fikra, ukimtafuta, ataonekana nawe ukimwacha atakutupa milele” Hapo yapo mengi ya kujifunza,  Mungu hutafutwa, naye hutafuta watu, kama tukimwacha yeye atatutupa milele. Daudi aliyekwenda na Mungu, ilimlazimu amshauri mwanae amjue, yeye binafsi, sio kupitia kwa mtu mwingine.

Ayub 42:5-6, “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio, bali sasa jicho langu linakuona, kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu, katika mavumbi na majivu”. Ayubu alisemezana sana na Mungu kabla hajamuona, lakini mwisho wake anasema anatubu na kugalagala katika majivu na mavumbi, anasema amejichukia. Mpendwa dhambi isiyotubiwa inauficha uso wa Mungu, na hawezi kusikia.

Ukisoma Isaya 6:1-5 utaona kuwa Isaya anasema alipokufa mfalme Uzia hapo ndipo alipomwona Bwana, na alipomwona, mahubiri yake yalibadilika. Mwanzoni alihubiri akisema OLE WA TAIFA LENYE DHAMBI. Lakini alipomuona Bwana aligeuka, akasema maneno yafuatayo, Mstari 5, “Ndipo niliposema Ole wangu, kwa maana  nimepotea, kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, na macho yangu yamemwona mfalme, Bwana wa majeshi” Baada ya toba hiyo ndipo alipotakaswa. Katika Biblia mahali pengine imesema, wewe unayekiona kibanzi cha mtu mwingine, ebu kwanza utoe boriti iliyoko ndani yako. Tunapaswa kujikagua vizuri.

Katika Math 16:13-20 tunajifunza jambo muhimu sana. Bwana Yesu aliuliza swali kwa wanafunzi wake, kuwa watu wanamwita kuwa yeye ni nani? Katika kujibu swali hilo tunajifunza mengi: Wengine wanasema wewe ni Eliya, Yeremiah, mmoja wa manabii, Yohana mbatizaji. Ndipo akawageukia kuwa ninyi je? Au kwa lugha nyingine MLIWASAIDIAJE? Hapa tunajifunza mengi, kuwa Bwana wetu hakuwa anajitangaza, kama angekuwa anajitangaza, basi alipouliza kuwa watu wanamwitaje Wangemwita jina alilokuwa anajitangaza kwalo, pia wangemjibu kuwa huwa wanakuita kama ulivyotuambia na tukawaambia. Petro alikomboa jahazi akasema, WEWE NDIYE KRISTO, MWANA WA MUNGU ALIYE HAI na baada ya jibu hilo, Yesu akamwambia hujajua hayo kwa akili zako, ila Mungu amekufunulia, na akaendelea kusema kuwa katika Mwamba huo uliougundua Nitalijenga kanisa langu na milango ya kuzimu haitalishinda. Hapo ndipo wengine wananakiri vibaya kuwa alisema atalijenga kanisa juu ya Petro.

Maandiko katika Mark 4:35-41 yanasema kuwa siku moja Yesu aliwaambia wanafunzi wake wavuke kwenda ng’ambo, na walipokuwa wakienda, wakiwa kwenye mtumbwi, upepo mkali ulitokea, ukakipiga chombo, bahari ikachafuka, na wakawa katika hatari. Mmoja wa wanafunzi wake akamwendea akamwambia, Bwana si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka akaukemea upepo, akaikemea bahari, vyote vikatulia, Biblia inasema KUKAWA SHWARI KUU. Mstari 40-41, “Akawaambia mbona mmekuwa waoga?  hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana-  NI NANI HUYU, BASI, HATA UPEPO NA BAHARI HUMTII?” Unaona! Walikuwa wanatembea na Bwana Yesu, wakati wakiwa na uoga, hofu, mashaka, kutokuamini na wanaulizana NI NANI HUYU? BAHARI INAMTII, UPEPO UNAMTII? Yawezekana kabisa, mimi na wewe tuko hivyo, tuko kwenye mawimbi makali, msuko suko mkali wa bahari. Lakini hatujui tuliye naye kuwa ndiye aliyeviumba hivyo, vinamjua, tukimwambia atavituliza kabisa, kutakuwa shwari kuu.

Dan 11:32.Sifa kubwa ya watu wamjuao Mungu wao ni kuwa:

HAWATADANGANYWA.

WATAKUWA HODARI.

WATATENDA MAKUU.

Hapo ndipo walipopatikana akina Shadrack, Meshack na Abednego, kwa kuwa Mungu wao ni Moto waliingizwa katika moto, na ule moto haukuweza kuchoma Moto halisi ambao ndiye Mungu wa kweli, muumba mbingu na Nchi.

2Tim 1:12, “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya,wala sitahayari, kwa maana  NAMJUA YEYE NILIYE MWAMINI. NA KUSADIKI YA KWAMBA, AWEZA KUKILINDA KILE NILICHOKIWEKA AMANA KWAKE, HATA SIKU ILE” Paul mtume alipata mateso mengi sana, ikiwemo kupigwa kwa mawe, bakora, na mengine mengi, lakini sikia anavyosema kuwa anamjua yeye aliyemwita, unajua ndio maana wakati mwingine utasikia tunalaumu watu, kwa namna yoyote, wakati mwingine wachungaji tunalaumu wakristo, pengine kwa sababu mbali mbali kama vile oh hawatoi!, oh hawanitunzi! Ngoja leo nikwambie mpendwa, mwamini aliyekuita, wala usilazimishe mtu yeyote kukupa chochote, wala tusiwe omba omba, ila tumwangalie yeye aliyetuita,

Katika Zab 78:41 Biblia inasema Israel walirudi nyuma wakampa mpaka mtakatifu wa Israel. Usimpe mpaka, yeye anaweza kufanya zaidi ya yale tuyawazayo, na yale tuyaombayo. Katika kumalizia sehemu hili naomba nikutajie sifa nne za Mungu wetu, ili uweze kufunguka zaidi katika kumjua.

YUKO KILA MAHALI-    Zab 139:7-10.

ANA UWEZA WOTE -  Zab 135:5.

ANAJUA KILA KITU -   Zab 147:3-4, Zab 139;23-24.

HANA MWANZO WALA HANA MWISHO –  Zab 90:1-4.

Mpendwa, akili zetu haziwezi zikamwelewa Mungu kikamilifu, ila yale yaliyofunuliwa ni yetu, yale yaliyo sirini ni yake yeye mwenyewe. Ndio maana mtume Paul akasema mahali hivi sisi tu uzao wake, na kama tu uzao wake, hatupaswi kumlinganisha na  vitu vilivyochongwa kwa mikono ya wanadamu yaani kumlinganisha na fedha, dhahabu, mawe ya dhamani n.k. Ebu tuendelee kumuomba atufungue macho ya ndani ili tuweze kumjua yeye aliye Mungu wa Kweli, wa pekee, na Yesu Kristo aliyemtuma, huo ndio uzima wa milele.

Nawatakia kujifunza kwema.

Ndugu yenu Mchungaji Samuel   Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – VI

Wapendwa,

Katika Sehemu zilizotangulia nimeeleza wazi wazi kuhusu jibu lile Bwana wetu Yesu alilolijibu kuwa WENGI WATATAKA KUINGIA WASIWEZE. Nimeeleza sababu mbali mbali zitakazofanya wasiweze kuingia japo wanataka. Leo tunaendelea katika sehemu ya Sita ya somo hili, kujifunza sababu nyingine zitakazofanya watu wasiingie mbinguni.

10. Hawatashinda.

Katika Yohana 16:33, Bwana alisema duniani mnayo dhiki lakini jipeni moyo, MIMI nimeushinda ulimwengu. Mpendwa, kuna vita kali kati yetu na ulimwengu huu unaokwenda kuangamia, na ndimo tunakaa, unapambana uende na watu, na watu wanapambana wasichukuliwe nao.

1Pt 2:21, Biblia inasema Bwana wetu aliteswa akatuachia KIELELEZO, yaani sampuli  ili tufuate nyayo zake. Kuja kwake duniani ilikuwa ni kufanya demostration, kutuonyesha sisi kama wanadamu tunapaswa kutembeaje. Ndio maana Neno linasema kuwa alijaribiwa kama sisi bila kutenda dhambi. Ebr 4:15. Alijaribiwa kwa mambo yote ambayo tunajaribiwa kwayo, bila kutenda dhambi, ndio maana akasema, nitalijenga kanisa langu katika mwamba na milango ya kuzimu haitalishinda. Na katika kusisitizia hili la kushinda kuwa ni muhimu ebu tuone jinsi makanisa yale aliyoonyeshwa Yohana alivyotumwa kwao: Uf 2;7; Uf 2:17; Uf 2:25; Uf 3:5 Yote hayo yanasema YEYE ashindaye…….. na Tukigeuza kinyume cha hapo tutasema YEYE ASHINDWAYE…..!

Tunatakiwa kupigana vita vizuri vya Imani, wala tusiogope kwani Biblia inasema wazi wazi kuwa tu WASHINDI na ZAIDI YA WASHINDI. Biblia imesema wazi wazi kuwa yeye aliye ndani yetu ni mkuu kuliko aliye katika dunia. Kwa hiyo ushindi ni wetu. Japo maadui zetu ni wengi mno, mmoja aliwataja katika Biblia kwenye Zaburi 69:4 kuwa kuwa ni wengi kuliko nywele zake, “Maadui zangu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu”. Hata ungekuwa na upara, usijifariji ebu cheki nywele za jirani yako, ndivyo adui zako walivyo wengi na kuzidi!

Katika 1Kor 16:9 Paul alisema amefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, lakini wanaompinga ni wengi. Ujue hivyo kuwa milango yako iko wazi kabisa, ila wanaokupinga ni wengi mno, unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa unaye Bwana wa Vita, ndiye pekee atakayeweza kukushindia. Pambana ushinde, pigana ukilinda Imani, kwani Bwana aliuliza swali kuwa Je! ATAKAPOKUJA MWANA WA ADAMU ATAIKUTA IMANI?

Imani yako inawindwa ili ipigwe. Kinyume cha Imani ni Hofu, Mashaka na Kutokuamini.

11.Hawatajua Wakati.

1Nyak 12:32 katika Biblia inasema kuwa katika Taifa la Israel kulikuwa na kabila moja liliitwa WANA WA ISAKARI, wenye akili ya kujuwa WAKATI. Hao ndiwo Taifa la Israel liliwategemea. Ndugu zangu, katika kiswahili kuna methali inasema WAKATI UKUTA. Kuhesabu wakati tunaanza na sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, mwaka, miaka. Ni muhimu sana kujali wakati. (Jambo hili la wakati kwa Afrika ni tatizo kubwa sana).

Kwenye Kutoka 8:8 Kuna somo la kushangaza kidogo, Musa alipokuwa anachukua Wana wa Israel kutoka Misri, kuna mapigo mengi Mungu aliipiga Misri kwa mkono wa Musa, pigo moja wapo lilikuwa VYURA. Ukisoma mstari huo hapo juu, Pharaoh alichoshwa na vyura, maana kila kona kulikuwa na chura. Angepewa maji hata ya kunywa, angekaa kitandani kote huko ni vyura tupu na akawaita Musa na Haruni, wakaja wakasimama mbele yake, akawaambia waombe kwa Mungu wao ili vyura watoke katika nchi wakae mtoni tu. Musa akamuuliza swali Je unataka tukuombee lini? Kwa lugha nyingine: Je! unataka tuwatoe lini?

Ndugu yangu swali zuri sana hilo. Naamini kwa mtu mwenye akili timamu halitamsumbua kulijibu. Maana, waombaji ni MUSA -Wapo. Wanaoondolewa ni vyura, nao wapo. Anayeombwa ni Mungu- naye yupo. Faraoh akatoa jibu la ajabu – Akasema KESHO! Wapo wapendwa wengi ambao ni wa kesho wala si wa leo. Ndugu yangu ya kesho wala huyajui, wewe na mimi ni wa leo ndiyo yetu, kesho si yetu.

Luka 19:41 inaonyesha jinsi Bwana alialia akisema mngejua yanayokuja, lakini sasa yamefichwa. Ebu tumuulize Mungu hata yajayo, ili tujue jinsi ya kujiandaa kukabiliana nayo, wala tusibweteke kwa ajili ya leo; kumbuka ushindi wa kesho unaandaliwa leo. Mith 1:24. Wakati mwingine Mungu anatutaka leo, sisi tunamwambia kesho, au tunakaa kimya, halafu tunaamua kuitika kesho. Soma utaona Biblia inasema kwa kuwa nimewaita mkakataa, na mimi mtakaponiita nitacheka.

Soma Ebr 12:16-17 na ufuatilie vizuri, utaona kuwa kijana huyo (Esau) hakuona kuwa uzaliwa wa kwanza ni kitu cha maana, akaudharau, akafikiri kirahisi tu kuwa wakati wowote akiutaka atauchukua tena. Hapana, haiko hivyo! Wakati Mungu anatutaka ni vizuri tumkubalie, vinginevyo wakati tutakapomtaka na yeye atakaa kimya.

Luka 23:27-31 inaonyesha Bwana alipokuwa akielekea msalabani. Wamama walimfuata nyuma wakimlilia kwa ajili ya mateso aliyokuwa anayapata siku ile: kupigwa, kutukanwa, kudhihakiwa nk. Lakini yeye alisimama akawaambia wawalilie watoto wao. Kumbe watoto tunao wazaa twapaswa kumlilia Mungu sasa kwa ajili yao, vinginevyo wakikua watatufanya tulie. Watatuliza! Maana mtoto wako akiwa jambazi, akapigwa mawe mbele yako, akavalishwa taili mbele zako, hutaweza kumsaidia kama hukumsaidia akiwa mtoto.

Tujitahidi kuujua wakati wetu na tukishaujua tuutumie vizuri.

Mbarikiwe!

Mch Samuel Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – V

Ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Biblia inasema Yesu alipouona mji aliulilia, akisema ‘laiti ungejua hata wewe yapasayo amani, lakini sasa yamefichwa kwako’. Luka 19:41-44. Pata muda  usome maandiko hayo ili uone Yesu alivyokuwa analia, akisema kuwa kwa sababu hukujua wakati wa kujiliwa. Ni vizuri tujue kinachokuja mbele yetu, tutafute Biblia inasema nini kuhusu siku za mwisho, ili tujue jinsi ya kuweza kupenya.

Nimesema kuna msitari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia. Katika Sehemu nne (4) zilizotangulia nimeelezea mambo mbali mbali yatakayozuia watu kuingia mbinguni huku wakiwa wanataka. Mambo hayo ni:

1.Hawataelewa.

2.Madeni.

3.Watampa Ibilisi nafasi.

4.Yaliyoifanya Israel isiingie Kanaan.

5.Hawatakubali kutengenezwa.

6.Watabakiza kitu.

7.Watakataa mafundisho yenye uzima.

8.Watakosa uvumilivu.

Vyote hivyo nimevielezea katika sehemu zilizotangulia. Nakuomba uyasome kwa makini, kisha tuendelee na safari yetu.

9. Mwili. Katika Rum 8:5-8 Biblia inasema mwili unashindana na roho, na hata hauwezi kutii kile Mungu anasema. Sasa kama mwili hauwezi kutii, nasi ndimo tunakaa, sasa itakuwaje? Wenzetu wanaojua jinsi ya kusafiri kuelekea Mbinguni waliandika mengi na katika 1Kor 9;25-27 mtume Paul aliandika kuwa hapigi hewa, anapambana kuutesa mwili na kuutumikisha, asije akaelekeza wengine namna ya kuingia Mbinguni kisha yeye awe wa kukataliwa. Unaona, mpendwa ebu jiulize. Unautesa mwili wako? Kuutesa maana yake kuuzuia vitu ambavyo unataka, kuunyima, kutokuukubalia. Unautumikisha mwili wako? Kuutumikisha maana yake kufanyiza yale ambayo hautaki kuyafanya, maana kwa hiari ya mwili huwezi kufanya yale ya rohoni.

Katika Rumi 7:14 mtume Paulo anasema yale anayotaka kuyafanya wala hayafanyi, anajikuta anafanya kinyume kabisa. Yaani anafanya yale asiyoyataka kufanya, mwisho akasema amegundua kuwa ndani ya mwili wake inakaa dhambi, lugha nyingine angesema ndani ya mwili wake yanakaa MAPEPO, maana dhambi ni pepo. Kwa hiyo tunamhitaji mwokozi. Ndiyo maana mahali pengine amesema mwili wangu umekufa kwa habari ya dhambi. Tunatakiwa tuiue miili yetu kwa Neno la Mungu, vile Neno linataka tunatakiwa tufanye bila kujali gharama.

Kwenye 1Thes 4:3-5 Biblia inasema kila mmoja wetu ajue kuuweza mwili wake. Kama hatutaiweza miili yetu, basi tujue kuwa miili yetu itatuweza. Na miili yetu ikituweza basi kule inakoelekea ndiko itakwenda na sisi, maana mwili kwao ni hapa hapa duniani. Ndio maana Mungu akaweka mshale wa kukukumbusha mwili unakoelekea. Ebu tazama PUA yako, kama inaelekeza kwenda chini basi elewa huko ndiko mwili unaelekea, na kama inaelekea juu mwenzetu umepona.

Mwili unatamani ukishindana na roho. Mwili unatamani vitu vya duniani; majumba, magari, fedha, nguo, vyakula, n.k. Ebu uangalie mwili usikuvute kukupeleka kwao. Ebu kubali roho ikuvute kukupeleka kwao, maana roho inatoka juu kwa Mungu wetu na itarudi huko. Mwili umetoka chini mavumbini na unarudi huko, na wewe na mimi ni NAFSI. Waweza kuwa upande wa mwili au waweza kuwa upande wa roho.

Chagua ni upande gani uwe. Nani utamuunga mkono? Chagua leo. Lakini uelewe kuwa wengi miili yao itawaweza na kuwapeleka kubaya kwa kuwa ya mwili wanayataka, ya roho wanayataka, wanataka yote, haiwezekani!

Ebu tuiue miili yetu!

Tuonane tena katika Sehemu ijayo na Mungu awabariki.

Ndugu yenu katika Kristo Mchungaji Samuel  Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – IV

Luka 13:24, Yesu akajibu akasema jitahidini kuingia katika mlango uliomwembamba, kwa maana nawambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze.

Kama nilivyotangulia kusema katika Sehemu ya 1, 2 na 3  kuwa mtu huyo ambaye jina lake halikutajwa, alimuuliza Bwana Yesu swali, kuhusu idadi ya wale wanaookolewa, ndipo Bwana akajibu kwa kuutumia mstari huo. Mpendwa hakuna mtu anayeweza kufanya biashara akapata hasara kisha akafurahia.

Efeso 5:26-27. Biblia inasema Yesu alikuja alisafishe kanisa, lisiwe na waa, kunyanzi wala lolote kama hayo. Nilieleza katika sehemu zilizotangulia kuwa vitu vifuatavyo vitasababisha wengi wasiweze kuiingia Mbingu.

1.Hawataelewa.

2.Madeni.

3.Watampa Ibilisi nafasi.

4.Yaliyoifanya Israel isiingie Kanani.

5.Watabakiza kitu.

6.Hawatakubali kutengenezwa.

7. Watakataa mafundisho yenye uzima.

Nakuomba urejee katika masomo hayo hapo juu, ili uweze kuona vile yatakavyozuia wengi kuingia mbinguni. Na leo tunaendelea Sehemu hii ya Nne.

8. Watakosa uvumilivu.

Math 24:13, Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Mpendwa mwenda Mbinguni, sikia mstari huo unavyosema, ni kweli tumeokoka, tuliokoka lini, pale tu tulipomkiri Yesu kwa kinywa, na tukaamini mioyoni mwetu, tangu hapo tulipata HAKI, na WOKOVU. Hilo halipingiki kabisa, tumeokoka, pamoja hayo yote, sasa anasema atakayevumilia mpaka mwisho, huyo ndiye ataokoka.

Mhubiri 7:8, Heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo wake, hii inasema TUTAMALIZAJE? Ndio maana Biblia imeandika juu ya watu mbali mbali, wapo walioanza vizuri sana, lakini walimaliza vibaya. Wapo wengine walianza vibaya sana, mpaka watu wakasema huyu bure, lakini walimaliza vizuri sana.Biblia inasema ATAKAYEVUMILIA MPAKA MWISHO, Ebu jiulize atakayevumila NINI?

Yak 5:7-11,Kwa hiyo ndugu vumilieni hata kuja kwake Bwana, tazama mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya dhamani, huvumilia kwa ajili yake, hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho, nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu msinung’unikiane, msije mkahukumiwa, Angalieni mwamuzi amesimama mbele ya milango, Ndugu watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni twawaita kheri waliosubiri, mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana, ya kwamba Bwana ni mwingi wa Rehema, mwenye huruma. Mpendwa yasome maneno hayo juu, uone wenzetu walivyopita katika safari ya kwenda kwa Mungu.

Katika Ebr 6:13-15 Biblia inasema Mungu alimpatia Ibrahim Ahadi, na kwa kuvumilia akaipata ile ahadi, wapendwa, tunahitaji kufundishwa Neno la Mungu kwa usahihi, mfano mtu anahubiri kuwa NJONI NIWAOMBEE  MTAJIRIKE. Lakini Biblia inasema MAADAM NCHI IDUMUPO MASKINI HAWATAKOMA KATIKA NCHI. Ukisema watu wote watatajirika wawe mamilionea, utakuwa unapingana na Neno la Mungu. Mpendwa Biblia inasema- Tutaketi kuhukumu pamoja na Kristo, tutakuwa tunahukumu watu walioshindwa kumcha Mungu kama sisi, kwa kusema hivyo. Yako mambo ambayo hata ungeombaje hayatabadilika, hayatakaa vile unataka, ndio maana kuna mstari unasema hivi – SI KAMA NITAKAVYO MIMI BALI KAMA UTAKAVYO WEWE. Yesu hakutaka kabisa apitie Msalabani, ila ona anasema Baba ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke. Si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe, Malaika kutoka Mbinguni akaja akamtia nguvu kuwa hakuna njia nyingine ni hiyo tu.

Wengi hukata tamaa haraka, wengi hukata tamaa kwa kuwa wametumainishwa kitu ambacho siyo mapenzi ya Mungu kwa mtu huyo. Na hapo ndipo watu hukata tamaa, watu huanza kujihukumu kuwa naona Mungu hanisikii mimi, wakati mwingine Mungu husema hapana. Lakini kwa kuwa maamuzi yetu tuliishayafanya tayari, jibu tumeishalitengeneza tayari, hata hatusikii anaposema, na hapo hatuwezi kuvumilia zaidi.

Katika Kumb 3:23-28 tunapata habari ambapo Musa alikuwa ametembea na Taifa la Israel, ameliongoza kwa muda mrefu, wamemzoea, mwisho Mungu akamwambia hutaingia Kanaani. Alimwendea Mungu tena akamuomba amruhusu aingie Kanaani aione, Nchi aliyokuwa amesema mno habari zake, Nchi ijaayo maziwa na asali, lakini Bwana akamwambia wazi wazi kuwa ‘nisikusikie tena ukisema nami jambo hilo’, mpendwa Musa aliendelea kufurahi tu na kumwambia Yoshua kuwa yeye hataingia, maana Mungu amemzuia. Unaona?  Alimsikia, akamwelewa vizuri.

Katika 2Kor 12:7-1 tunapata habari za mtumishi wa Mungu mtume Paul, ambaye alikuwa amefanya kazi kubwa katika maisha yake ya utumishi, akisema kwa wingi wa mafunuo aliyopewa, mjumbe wa ibilisi alitumwa kwake MWIBA, ili umchome asijivune kupita kiasi; akasema kwa ajili ya kitu hicho alimsihi Mungu mara 3  kimtoke, ila Mungu akamwambia NEEMA YANGU YAKUTOSHA, wisho anasema anajisifia hayo. Mpendwa ebu ujue namna ya kumsikiliza Mungu wako aliyekuokoa, tatizo watu wanakusikilizia, ndio maana wanakudanganya, na unadanganyika, masikio unayo, macho unayo, mwambie Mungu akufungue upate kusikia na kuona.

Batmayo alikuwa kipofu kabisa na alikaa kando ya njia. Hilo ndilo lilikuwa tatizo lake: KANDO YA NJIA. Alikaa pembeni mwa Neno la Mungu. Lakini alikuwa na sifa moja kuwa hakuogopa watu. Hata walipomwambia anyamaze asipige kelele, hapo ndipo alipiga kwa nguvu, mwisho Yesu akasimama, akawaambia mwiteni aje hapa kwenye njia, Wakamwambia jipe moyo inuka anakuita. Unaona! Watu wale wale waliokuwa wanamwambia unampigia kelele, ndio hao wanamwambia simama anakuita. Ukisoma vizuri, alipoinuka alitupa koti lenye mavumbi, hakuna aliyemwambia atupe, alielewa tu. Na leo usitegemee mtu akwambie tubu, acha dhambi, Wewe ni jiwe?   Ndiyo maana Daudi alimwambia Suleman Mwanangu mjue Mungu wa Baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu.

Pia unaona Yesu hakuwauliza wale waliomwambia kuwa anataka nimfanyie nini? Alimuuliza yeye Batmayo kuwa unataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana nipewe kuona! Naye akaona. Mungu amekuita, amekuokoa, yeye yuko tayari kusema na wewe, wala usifanye haraka kukata tamaa, mngojee, yeye ni mwaminifu.

Ebr 11.35. Kitabu cha Waebrania kinaitwa kitabu cha mashujaa. Kwa nini kiliitwa kitabu cha mashujaa? Je ni wote waliomba na Mungu akawatokea akawatoa kwenye shida zao?

Je ni wote waliingizwa kwenye moto wakatoka kama kina Shadrack, Meshack, na Abednego? Je ni wote waliingia kwenye tundu la simba wakatoka salama? Je ni wote waliugua wakaombewa wakapona? Ukisoma vizuri watu kama akina Elisha walikufa kwa jipu. Usiige fulani, fulani ni fulani, wewe ni wewe. Mtu anaandika posters kuwa LETENI VIWETE, VILEMA, VIPOFU, VIZIWI. Je wanapoletwa wote wanapona?     Umewaita wa nini? Yesu aliwatangazia kuwa njoni viwete sasa? Yesu alipofika makaburini alimwita Lazaro, wengine walibaki wamelala makaburini, wewe unataka makaburi yote yabaki  matupu?

Kiwete aliyekuwa akiomba katika mlango mzuri, elewa Yesu alipita akamwacha pale. Kwa nini? Alijua huo ni mtaji wa Petro, wewe unataka umalize mitaji yote?  Wanaokuja wataanzia nini? Mdo 16:6-10. “Wakapita katika Nchi ya Frigia, na Galatia, wakikatazwa na Roho mtakatifu, wasilihubiri Neno katika Asia.Walipofika kukabili Misia, wakajaribu kwenda  Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa. Wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paul akatokewa na maono usiku, alimwona mtu wa Makedonia,amesimama akimsihi, na kumwambia, vuka uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri habari njema”.

Watu watakosa UVUMILIVU. Mpendwa ebu vumilia, katika hali uliyonayo wakati unamgoja Bwana. Usiyumbishwe na kila upepo, na kila elimu. Watu wanakusikilizia Mungu anasemaje. Yeye yuko tayari kusema na wewe, pata muda, mpe muda. Wakati mwingine kaa kimya mbele zake, tafakari juu yake, mpe moyo wako, mfanyie Ibada yenye maana, hakika utaisikia sauti yake!

Ni ombi langu kuwa  utakuwa na UVUMILIVU mpaka mwisho ili uweze kuingia katika ule uzima wa milele.

Mbarikiwe na Bwana.

Ndugu yenu  Mchungaji Samuel Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – III

Namshukuru Mungu, Muumba Mbingu na Nchi, anayetuwezesha kuendelea kujifunza kila iitwapo leo, kadri tunavyoona kuwa siku za kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo zimekaribia. Unajua Biblia inasema hata yeye (Yesu) hajui siku hiyo ila Baba peke yake. Ni ukweli usiopingika kuwa kama Mungu angemjulisha Yesu siku ya kuja, kwa kuwa anatupenda sana, Biblia inasema alitupenda UPEO, Angetubonyeza! Na kama angetubonyeza, basi watu wangemsubiri tarehe na saa ile aliyosema. Wangemsubiri jioni yake kama angesema anakuja kesho, na huo usingekuwa upendo kabisa. Hata hivyo alijitahidi kutujulisha dalili na majira, vitakavyotujulisha kuwa kuja kwake kumekaribia.

Katika sehemu ya  kwanza na ya pili kwenye somo hili lisemalo Mstari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia nilieleza baadhi ya mambo yatakayo wazuia watu kuingia mbinguni wakati wanataka. Luka 13:24, Bwana akawaambia jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze. Sababu ambazo nimeshazieleza hadi sasa ni:

1.Hawataelewa.

2.Madeni.

3.Watampa Ibilisi nafasi.

4.Yale yaliyoifanya Israel isiingie Kanaan.

5.Hawatakubali kutengenezwa.

6.Watabakiza kitu.

Maelezo ya sababu hizo yanapatikana katika Sehemu ya Kwanza na ya Pili ya somo hili. Hivo unaweza ukarejea kusoma sehemu hizo mbili zilizotangulia ili uweze kuelewa zaidi. Soma kwa makini utaona jinsi hayo yaliyotajwa hapo juu yatakavyo wazuia wengi. Lakini sasa tunaendelea na Sehemu ya Tatu.

7.Watakataa mafundisho yenye uzima.

Biblia haisemi WATAKATAA MAFUNDISHO, bali inasema Watakataa mafundisho yenye UZIMA. Kumbe kuna mafundisho mengi, mengine yana UZIMA na mengine ni kinyume cha uzima, yana MAUTI. Ndio maana Biblia imesema mahali kuwa ANDIKO LINAUA ila ROHO ANAHUISHA.

2Tim 4:1-7 Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu waliohai na waliokufa, kwa kufunuliwa kwake na ufalme wake, lihubiri Neno, uwe tayari wakati unaokufaa, na wakati usiokufaa. Karipia, Kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote, na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima, ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe, watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti, nao watajiepusha, wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.Bali wewe uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya muhubiri wa Injili timiliza huduma yako.

Mpendwa, kuna mengi sana ya kujifunza katika mistari hiyo hapo juu, Mtume Paul alimwelekeza kijana wake Timotheo namna ya kufanya kazi. Akamwambia, KARIPIA, KEMEA, ONYA. Hayo ndiyo watu siku hizi hawataki kusikia, wanatakiwa HANDLE WITH CARE,  watu wamekuwa  CHUPA ZA CHAI – Thermos! Pia akamwambia watu watakavyojipatia waalimu wale wanaowataka, maana watawaambia kile wanachotaka. Kumbuka tunapokwenda hospitalini, anayejua dawa ni Daktari. Huwezi kumwambia Daktari dawa unayotaka, kama ni sindano, vidonge, dawa ya maji nk, anayejua dawa unayohitaji ili upone ni Daktari. Watu watakataa mafundisho yenye uzima, watataka mafundisho yasiyo na uzima, mafundisho mafu, na kama utafundishwa mafundisho mafu, imani yako itakuwa kwa watu. Utawategemea watu, na ukiwategemea watu, utaishi katika laana, na mtu huyo akiisha kufa, basi huo ndio utakuwa mwisho wako.

Mdo 5:34-37, Lakini mtu mmoja  Farisayo, jina lake Gamaliel, mwalimu wa Torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika Baraza, akaamuru Mitume wawekwa nje kitambio kidogo,akawaambia- Enyi waume wa Israel, jihadharini jinsi mtakavyo watenda watu hawa, kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda,akijidai kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye, naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda mgalilaya, siku zile za kuandikwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea, na wote waliomsadiki wakatawanyika

Unaweza kuona kazi isiyojengwa katika msingi wa Kristo, hiyo haidumu, hiyo inapita, itayeyuka, itabaki historia tu kama zile zingine zilizopita. THEUDA na YUDA MGALILAYA, baada ya kuondoka kwao, kila kitu kiliondoka. Lakini ujue walikuwa na mafundisho, watu waliwaamini, watu waliwasikiliza, watu waliwasifia. Wengine waliwaita majina mbali, wengine waliringa kwa ajili yao, wakisema eeh  wewe acha tu ndugu yangu,  sisi sio kama watu wengine,Tunaye Theuda siyo mchezo, tunaye Yuda Mgalilaya sio mchezo! Yawezekana ndivyo unashuhudia kuwa ebu twende kwa Mtume wetu, twende kwa Mchungaji wetu, akikuombea tu shida yako imeisha. Mpendwa unampeleka huyo kwa Theuda, unampeleka huyo kwa Yuda Mgalilaya. Tunapaswa tuwapeleke watu kwa YESU, ndiye mwenye uzima, wengi wamekwenda makanisani kuona miujiza ambayo Mitume wao wanafanya, wao kazi ni kuiangalia na kuishangaa miujiza hiyo, Na mitume hawawafundishi kuwa miujiza hii hata wao wanatakiwa waifanye kwa jina la Yesu maana ndivyo ilivyoandikwa Mark 16:17, Na ishara hizi zitafuatana na wale waaminio, Kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa Lugha mpya, watashika nyoka, hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya.

Yoh 14:12, Amini amini  nawambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa  kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Wapendwa mstari ule wa Marko 16:17, unasema ishara hizi zitafuatana na hao waaminio, na aaminie ni nani? Wapendwa mstari wa Yohana hapo amesema kuwa yeye amwaminiye Yesu, kazi zote ambazo Yesu alizifanya yeye atazifanya. Ndugu zangu sio kazi ya mitume, sio kazi ya Manabii, wala Wachungaji, ni kazi za WAAMINIO.

Tumesikia watu watakataa mafundisho yenye uzima, watakimbilia mafundisho mafu, nasema ni mafu kwa sababu, kama uko kanisani, kazi yako ni kuja kuangalia jinsi mtu mmoja anavyofanya miujiza, hata ungemuita jina gani, mimi halinishtui, maana Paul anasema mna waalimu kumi elfu. 1Kor 4:15, Japo kuwa mna waalimu kumi elfu, lakini hamna baba wengi. Kwanza hapo tujifunze kuwa twapaswa kuwa na baba wa kiroho, ambaye atatusaidia wala tusiwe yatima. Pili hata wangekuwa walimu kumi elfu kama wanafundisha mafundisho mafu, hao waalimu watatupoteza, hata wangeinuka na majina makubwa makubwa. 2Kor 11:13-14 Wapo Mitume wa Uongo. 2Kor 2:17. Wengi wamelighoshi Neno la Mungu, kughoshi ni kufanyaje, WAMELICHAKACHUA, kwa msemo wa kisasa.

Ufunuo 2:2,Umewachunguza hao wajiitao Mitume, ukakuta sio, wanasema uongo.

Mtumishi wa Mungu wa kweli, anafanya kama Yesu, kwa njia gani?  Hata angekufa leo kazi ile itaendelea. Ndio maana alikuwa anawatuma waende watoe pepo, na wakirudi wanafurahi kweli kweli, wakisema hata pepo wanawatii. Kinyume chake  watumishi wesio wa kweli, wanajua kuwa wao ndio tu wanaweza kutoa pepo, kufundisha, kutenda miujiza, wengine wote ni wa kuja kukaa tu na kujionea miujiza, na hawafundishwi kuwa kazi hii ni yenu, kama mnaamini, wao wanakaa tu kama misukule, hawawezi lolote,  hayo ni mafundisho mafu. Ndio maana unasikia matangazo yote ni kuwa njoni muone miujiza, njoni muone miujiza!

Math 24:24-2. Ma-Kristo wa uongo watatokea. Kama hufanyi yale Bwana Yesu aliyoyasema katika Biblia, usishangae, na hutakataa ukiambiwa wewe ni Kristo wa uongo. Na Manabii wa uongo watatokea, watafanya ishara kubwa, watafanya maajabu, ili wapate kuwapoteza hata wateule. Yesu akasema nimekwisha kuwaonya mbele.

Utawatambua kwa matunda wanayoyazaa, watu wanaowazaa katika Imani. Ebu  angalia maneno haya katika Yoh 15:16, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua, nikaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yakae.

Hili ni Neno zito ambalo kila mhubiri anatakiwa aliangalie kwa makini sana, kama utakwenda uhubiri Injili mahali, watu waje, uwatoe mapepo, uwaombee magonjwa waliokuwa nayo yawatoke, Kisha uwatoze sadaka, ufunge mkutani baada ya siku zile za mkutano, ziwe 10,  8 au zozote, kisha utoweke. Umezaa matunda, unakusanya sadaka unaondoka, Mungu akikujalia utarudi tena mwakani, majira kama hayo. Ebu sikia mstari huu ufuatao, utaukwepaje? Math 23:15, Ole wenu waandishi na mafarisayo wanafiki, kwa kuwa mnazunguka katika bahari, na nchi kavu, ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu, na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanam mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.

Nikufungue macho hapa, anasema nini. Katika Math 12:43, Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo na maji, akitafuta mahali pa kupumzika asipate, halafu husema, nitarudi nyumbani kwangu niliko toka, hata akija aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa, mara huenda akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo, na hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyo kuwa katika kizazi hiki kilicho kibaya.

Huyu mtu uliye mhubiri kisha ukamwacha hewani, wengine wanasema tafuta kanisa la kiroho uwe unaabudu humo. Ndugu zangu huyo aliyekata shauri leo, anajua kanisa la kiroho ndio lipi? Hata ungemwambia kanisa la kiroho, au kanisa la kimoyo, au la kimwili, haelewi. Anachojua alikuwa na pepo umemtoa, na ukweli unabaki kuwa umemzaa katika Imani, unawajibika katika maisha yake. Lakini utashindwa kumwelekeza kwa kuwa Mchungaji wake ndiye amekuandalia mkutano huo, ambaye hata haamini wokovu, mwisho mtu yule anarudi kule kule ulikomkuta anasali na ana pepo, na sasa tazama kinachompata: anafanyika kuwa mwana wa Jehanam mara mbili; mapepo yanamrudia, hata mhubiri wa kweli akimshuhudia, wengine wanasema aa! niliokoka katika mkutano wa mhubiri mkubwa, wewe utaniambia nini? Umemfanya kuwa mwana wa Jehanam. Heri usingemhubiri, angebaki na pepo mmoja, ila sasa anakuwa na SABA.

Napenda kumaliza Sehemu ya Tatu  ya somo hili la Mstari unaoniliza kuliko yote katika Biblia kwa kusema kuwa Kwa kuwa sababu moja wapo ni kuwa watu watakataa mafundisho yenye uzima, ebu tukubali kufundishwa, hata kama tu wahubiri wakubwa, tukubali kusikiliza ushauri, maana imeandikwa. 1Kor 8:2, Mtu akidhani ya kuwa anajua Neno, hajui Neno lolote bado kama impasavyo kujua.

Mungu atusaidie. Biblia inasema mahali pengine IKO NJIA INAYOONEKANA SAWA MACHONI PA MTU, LAKINI MWISHO WAKE NI NJIA ZA MAUTI. Tufanane na Apolo, tuwe na  mioyo ya kufundishika, kushaurika. Mdo 18:24-28. Soma jinsi Apolo alikuwa mhubiri mzuri, alipokutana na wamama hao waliotajwa, walimchukua, wakamfundisha vizuri, hakukataa, hakusema anajua, kama wengi wetu tunavyodhani kuwa tunajua kila kitu. Hata Musa mtu mkubwa kabisa, Mkwe wake alimpatia ushauri na akamsikiliza. Unajua mpendwa unaweza ukajihesabia haki kuwa unafanya kazi kubwa, hiyo ni kwa macho yako ya kibinadamu, je Mungu anaionaje?

Jiulize-

1. Mafundisho ninayofundisha ni yenye uzima?

2. Mafundisho ninayofundishwa ni yenye uzima?

3. Ninaowafundisha, kama nikiondoka leo watadumu?

4. Anayenifundisha kama akiondoka leo nitadumu?

Majibu unayo wewe, na ni ombi langu Mungu atufungue macho tupate kuona, tupate kuelewa. Tutaendelea katika Sehemu ya Nne ya somo la Mstari unaoniliza kuliko yote katika Biblia.

Mbarikiwe mnapoendelea kushirikiana nami katika mafundisho haya.

Ndugu yenu, Mchungaji    Samuel   Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – II

Bwana Yesu asifiwe! Leo tunaendelea na Sehemu ya Pili ya somo lisemalo MSTARI UNAONILIZA  KULIKO MISTARI YOTE KATIKA BIBLIA na Mungu, Muumba mbingu na Nchi, awabariki wote tunapoendelea na somo hili.

Ndugu zangu mimi binafsi sipendi kitu kinachoitwa HASARA. Nadhani hata wewe hupendi pia, na Mtume Paulo naye pia hakupenda ndio maana aliandika ujumbe huu katika kitabu cha 1Kor 9:26-27 akisema, Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye, napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha, isiwe, nikiishakuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. Ndugu yangu wahubiri  tunatakiwa tuseme hivyo. Tujiandae, ya kwamba yale tunayowaelekeza watu wafanye, kwanza sisi tujielekeze kufanya; vinginevyo tutaingiza wengine na sisi tuwe wa kukataliwa. Katika somo lilopita nilisema kuwa msitari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia ni ule usemao YESU AKAMWAMBIA JITAHIDINI KUINGIA KATIKA MLANGO ULIOMWEMBAMBA, KWA MAANA NAWAAMBIA WENGI WATATAKA KUINGIA WASIWEZE.

Mpendwa, kwa upande wangu, lolote ninalolifanya kwa Mungu ni ili niingie Mbinguni siku moja, nipate kupumzika milele, mahali ambapo hakuna kilio, hakuna magonjwa tena, ndio maana tuliamua kumfuata Yesu. Katika sehemu iliyopita nilieleza mambo matatu (3)  ambavyo vitafanya watu wasiingie mbinguni, na leo nitaendelea na yanavyofuata. Lakini kwa kujikumbusha tu ni kuwa mambo matatu ambayo nimeshayasema tayari ni 1.Kutokuelewa, 2.Madeni na 3.Kumpa Ibilisi nafasi. Nimeshaeleza kwa undani kuhusu mambo haya katika sehemu ya kwanza kwa hiyo sitayaelezea tena hapa. Kama ulikuwa hujasoma ile sehemu ya kwanza ni vema ukaisoma ili uweze kupata mtiririko kamili wa somo hili.

Nasema mstari huu unaniliza kwa kuwa watu watafanya kazi ya hasara, wataumia, watatoa hela zao, watafanya mambo mengi kwa ajili ya Mungu, lakini eti mwisho wa siku wanaikosa Mbingu. Mbaya sana! Hata Bwana Yesu alisema mahali fulani kuwa wengine watakuja na kusema BWANA TULITOA PEPO KWA JINA LAKO, NA TULITOA UNABII KWA JINA LAKO, NA KWA JINA LAKO TULIFANYA MIUJIZA MINGI. Soma habari hii katika  Math 7:22-23, Ndipo nitawaambia dhahiri sikuwajua ninyi kamwe, ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.  Soma haya kisha utafakari.

Tuendelee na jambo jingine kati ya yale yatakayofanya watu wasiingie mbinguni huku wakiwa wanataka:

4. 1Kor 10:1-13.

Ni yale yaliyolizuia Taifa la Israel kuiona Nchi ya Kaanan. Mpendwa ebu tuangalie kwa makini somo hilo. Ule umati wa watu waliotoka Misri utumwani, Mungu alisema anawapeleka katika Nchi ya Ahadi Nchi ijaayo maziwa na asali. Waliona miujiza tele kwa macho yao ambayo siwezi kuyaeleza hapa, ebu isome mwenyewe uone. Wataalam wanasema walikuwa watu kama milioni 4 bila kuhesabu watoto na wanawake. Lakini utakumbuka ni watu WAWILI tu waliiona Kaanani. Ni yapi yaliwafanya wasiione Kanaani?: a).Wengi Mungu hakupendezwa nao. b)Walitamani mabaya. c). Ibada ya sanamu. d). Uasherati. e). Kumjaribu Mungu. f).Manung’uniko.

Mstari wa  11  unasema hivi, Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na misho ya zamani. Mambo niliyoorodhesha hapo juu ndizo dhambi zilizofanya taifa lile liishie jangwani. Mpendwa Ebu jikague. Jiulize maswali yafuatayo na ujijibu mwenyewe:

-Je! Ninampendeza Mungu?

-Je! Nitamani mabaya (yaani yale ya Misri)?

-Je! Ninaabudu sanamu? Kumbuka sanamu ni chochote unachopenda kuliko Mungu, hiyo ni sanamu, maana imeandikwa mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote. Pia mahali pengine amesema watoto wadogo jihadharini na sanamu.

-Je! Uasherati nimeushinda? Kumbuka Neno linasema atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani amekwisha zini naye.

-Je! Ninamjaribu Mungu? Kumjaribu ni kutokumuamini kama kweli anaweza kukutetea, kukupigania, mpaka wengine wanakwenda kuaguliwa kwa wapiga ramli.

-Je! Ninayo manung’uniko yoyote moyoni mwangu? kuhusu wazee wa kanisa, Mchungaji wangu, Mchungaji mwenzangu nk. Manung’uniko!

5.Watabakiza KITU.

Watu wengi wanadhani kuna dhambi kubwa, na dhambi ndogo, dhambi nyingi.

Kumb 23:14, Bwana huzunguka katika kituo akuokoe, angalia kiwe safi asije akaona kitu ( KITU) akageuka na kukuacha.

Ebr 12:1- Tuweke kando kila mzigo mzito na ile DHAMBI  ituzingayo kwa upesi.  Kagua ni dhambi gani imebaki inayokuzinga kwa upesi, inayokuangusha mara kwa mara, ambayo hujaishinda, upambane nayo uishinde, ndipo utasema uko salama. Ni vita. Ni mapambano. Pia uje dhambi imezidiana nguvu, mahali pengine anasema umekamatwa kwa kamba za dhambi zake. Kumbe dhambi zina KAMBA. Mith 5:22.

Zab 107:10 Waliokaa kaika giza na uvuli wa mauti wamefungwa katika taabu na CHUMA.

Zab 107:16, Ameivunja milango ya shaba, ameyakata mapingo ya CHUMA.

Yawezekana kabisa umeshikwa na kamba za dhambi, au shaba, chuma. Ndio maana tunahitaji Damu ya Yesu ihusike kuvunja kila aina ya dhambi ndani yetu. Tusijifariji, wakati tunajua kuwa bado.

Mith 28:13, Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, ila yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

Dawa ya dhambi ni kuitubia na kuiacha, siyo kuificha. Ukiificha hautafanikiwa kamwe, hautafanikiwa nini? Chochote katika maisha yako, ya kimwili na kiroho pia. Hata ungeombewa, ukapewa na mafuta, na vitambaa ukavifanya kuwa hirizi, hutafanikiwa. Hata ukiona kama unafanikiwa, sio mafanikio yatokayo kwa Mungu, yaweza kutoka kwa yule adui yetu. Ukumbuke alimwambia Bwana Yesu amwinamie, kisha ampatie mali ya dunia hii, na wengi wamemwinamia amewapa. Ndio maana wengine kila mwaka wanatoa kafara, wanatoa watoto wao, wake zao, hata waumini wao.

Katika 1Tim 5:24 Biblia inasema, wengine dhambi zao zi dhahiri, hazikujificha, wengine zinawafuata, wengine zinawatangulia.Unaona! Zinazotangulia zina nguvu ya kukuvuta, zinazokufuata bado unazipenda zikija nyuma yako unazikaribisha.

Zab 51:10-12 Ee Mungu uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu, usinitenge na uso wako, wala roho yako Mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako, unitegemeze kwa roho ya wepesi. Zaburi hiyo ni ile ambayo Daudi aliiandika akitubu dhambi zake. Isome kwa makini. Daudi alijua Roho wa Mungu hatakaa na dhambi, Alijua kuwa amepoteza furaha ya wokovu, na mengine mengi.

Mark 1:1-3. Kama kweli mtu anataka Mungu akutane naye, ni lazima atengeneze njia zake, ayanyoshe mapito yake, ndipo Bwana atapita. Mpendwa umeme unatembea kwenye nyaya zake ulizotengenezewa na Mungu siku zote hutembea kwenye Neno lake. Batmayo alimwita Yesu akiwa kando ya njia. Yesu akasimama, akawaambia wanafunzi wake mwiteni,  maana alikuwa kando ya njia. Ebu tukae kwenye Neno la Mungu.

6. Hawatakubali kutengenezwa.

Rumi 8:29, Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili, wafananishwe na mfano wa Mwana wake.

Mpendwa, tuaitwa watu wa lugha, taifa, kabila na mila mbali mbali. Na Neno linasema kuwa huwa tunaitwa ili tufananishwe na Yesu. Je! Umewahi kujiuliza ni kwa njia gani tunafananishwa?  Je ni kwa kupakwa rangi? Au Ni kwa kufanyaje?

Katika Yeremia 23:29 Biblia linasema kuwa Neno ni  NYUNDO,  MOTO.

Ebr 4:12 – Neno ni upanga ukatao kuwili. Sasa tuangalie nyundo hiyo inavunja nini?   Moto huo unachoma nini?  Upanga huo unakata nini? Wapendwa tusipokubali Neno la Mungu litutengeneze, lipasue mioyo yetu iwe ya nyama, lituchome mioyo yetu ilainike,

Kuingia mbingu ni kitendawili. Tafakari hili: Walikuja watu wanamtafuta Yesu akasema ni mimi, walirudi nyuma wakaanguka, huku akijua kabisa wanakuja wamkamate na kumtesa, mbona aliwangoja wakainuka tena wakamkamata?

Mathayo 5 Inajulikana kana Hotuba ya mlimani – Adui yako akiwa njaa mlishe, akiwa na kiu mnyweshe, mbariki anayekuudhi. Hayo hakuna anayeyaweza ila yule aliyekubali kutengenezwa.  Mtu akikushtaki akitaka kukunyang’anya kazi mwachie na joho pia. Aliyetengenezwa na Jiwe kuu la pembeni, yaani Yesu, ndiye pekee anayeweza kufanya hayo, maana imeandikwa hivi katika Mathayo 21:42-44 Yeye ni jiwe kuu la pembeni, litakayemwangukia linamsaga tiki tiki, atakayeliangukia atavunjika vipande vipande. Hivyo ni kusemaje? Yule atakayekubali kufanya vile Yesu anavyomwambia, hata kama ni vigumu vipi lakini  akafanya, huko ndiko kusagwa. Yule atakayefanya vile anavyotaka mwenywe wakati Yesu amemwambia vingine, huko ndiko kuliangukia jiwe, unavunjika vipande vipande, na si rahisi kuunga tena. Ndio maana Bwana mwenyewe akasema, Kwa nini mnaniita Bwana Bwana na hamfanyi niwaamuruyo?

Wapendwa katika Bwana, katika toleo la tatu tutaendelea kuona sababu zaidi zitakazofanya wengi watake kuingia lakini wasiweze. Nawatakia kila la kheri katika kujisomea hayo.  Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa akupe kuelewa na akupe kufanya yale tunayoagizwa katika Neno lake.

Ndugu yenu katika Kristo, Mchungaji Samuel Imori.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – I

Namshuku Mungu aliyeumba Mbingu na Nchi, yeye atupendaye kiasi cha kumtoa mwanae wa pekee, aliyetufia msalabani. Nimesukumwa moyoni mwangu kuuandika mstari unaoniliza katika Biblia kuliko mistari yote. Inawezekana wewe usikulize, au ukakuliza lakini shauku yangu ni kuwa mstari huu ukufanye upige mbio za dhati kuelekea kwetu Mbinguni.

Mstari wenyewe ni Luka 13:24, usemao “Jitahidini kuingia katika mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watataka kuingia wasiweze

Mpendwa, wewe unayesafiri kuelekea mbinguni, ebu fuatana nami, uweze kuona kile nilichokiona baada ya kusoma mstari huo. Hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu ambaye anapenda afanye kazi ya HASARA, au afanye kazi isiyo na faida kwake.

Yesu alisema WENGI watataka kuingia lakini wasiweze. Tunajua kuwa kuokoka ni kile kinachosemwa katika Rum 10:9-10 kuwa  UKIAMINI, UKAKIRI   unapata HAKI na unapata WOKOVU. Hakuna mjadala kwa hilo ndivyo mtu anafanya na anasema NIMEOKOKA. Na anaposema nimeokoka, maana yake ni kwamba ameokoka na Jehanam ya moto, ndivyo Biblia inavyosema katika kitabu cha Yoh 5:24 kuwa “Amini amini nawambia, yeye alisikiaye Neno langu, na kumwamini yeye aliyenipeleka, yuna uzima wa milele, wala haingii hukumu, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani”. ALISIKIAYE NENO LANGU ( Lipi?)

Nilipokuwa natafakari mstari huu, moyo wangu uliniuma sana, sikutaka nifanye kazi ya hasara. Sikutaka niwaingize wengine mbinguni kisha mimi niwe mtu wa kukataliwa. Ni wahubiri wachache wawezao kusema hivi, kama ilivyo katika 1Kor 9:26-27, “Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye, napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa, bali nautesa mwili wangu, na kuutumikisha, isiwe, nikiishakuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”. Ni ukweli usiopingika kuwa wahubiri wengi tusipoangalia tutaingiza wengine mbinguni kisha sisi tuwe watu wa kukataliwa.

Ninataka nikueleze vitu mbali mbali ambavyo Bwana alianza kunionyesha kimoja kimoja miongoni mwa vile vitakavyowazuia watu kuingia wakati wanataka:

1. Hawataelewa. Katika Marko 4:10-12 Biblia inasema watakuwa na masikio ila hawatasikia, watakuwa na macho ila hawataona. Ni kweli tumesikia kuwa Yesu ni Bwana, ni mwokozi, tukamwamini, tukaanza kwenda makanisani. Swali, Je! Yale tunayoagizwa tunayafanya?

Yak 4:17 Yeye ajuaye kutenda mema na hatendi kwake huyo ni dhambi. Ndio kusemaje hivyo, tunayofundishwa yote kama hatuyatendi, tujue tuko dhambini, na ndio maana Bwana Yesu akasema MBONA MNANIITA BWANA BWANA NA HAMTENDI NIWAAMURUYO? Hatutendi ama kwa kutokuelewa, ama kwa makusudi tu. Mifano iko mingi, hakuna mchungaji yeyote atakayefundisha watu kuwa WAWE WANACHELEWA IBADA, kuwa WAWE WANAKOSA IBADA. Hayo ndiyo tunafanya nani anatufundisha? Kwenye Luka 24:44 Biblia inasema alikaa na wanafunzi wake miaka mitatu (3) ndipo akawafungua akili zao wapate kuelewa na maandiko, aliwaambia akifufuka atawatangulia kwenda Galilaya, Walipaswa kwenda Galilaya, ila walikwenda Kaburini. Tuombe Mungu atuwezeshe kila tunaloambia tuelewe na atusaidie tutende.

2. Madeni.  Rumi 13:8; Mith 22:7; Kum 28:12. Nikisema madeni inaweza kuonekana kama ni jambo geni kabisa, maana madeni yamekuwa ni kawaida kwa wateule. Warumi niliyokupa inasema kuwa MSIWIWE na MTU chochote,  maana yake tusidaiwe na mtu. Mithali  niliyokupa inasema akopaye ni mtumwa wa yule amkopeshaye. Sisi tu watumwa wa Bwana Yesu, sio watumwa wa mtu, ila kama wewe ni mdaiwa elewa yule anayekudai  wewe ni mtumwa wake. Na ile Kumbukumbu la Torati niliyokupa imesema hatutakopa sisi, bali tutakopesha. Mpendwa usiwe na haraka kukopa, mwisho unashinwa kurudisha, unajifariji kuwa utarudisha. Yesu anarudi wakati wowote, akikukuta una deni hawezi kukunyakua kwa maana atakuwa amekusaidia kumdhulumu mtu. Wengine walikopa wake, wakapewa mpaka leo hawajafanya vile vinywa vyao vilivyosema – UMETEGWA KWA MANENO YA KINYWA CHAKO NA UMEKAMATWA.

3. Watampatia Ibilisi Nafasi. Efeso 4:27,”Wala msimpe Ibilisi nafasi”. Kabla hatujaangalia mstari huo kwa ndani, ebu tujue kwanza kazi za shetani, ndipo tutajua kuwa mara tukimpa nafasi atafanya nini:

Yoh 10:10, Mwizi haji ila aibe, achinje na kuharibu.

1Pt 5:8-10 Mshitaki, Mzungukaji, mmezaji.

Mshitaki – Yeye siku zote hutafuta makosa tunayoyatenda na kisha huenda kwa Mungu wetu kutushitaki, na Mungu ni mwenye haki.

Mzungukaji - Wapo wakristo wengi kazi yao ni kuzunguka toka kanisa hili kwenda lile. Kesho yuko lile kesho kutwa yuko lile, hana mchungaji, hana mahali maalumu anapowajibika. Kumbuka Mungu alimuuliza Ibilisi unatoka wapi, Ayub 2:1-2;Ayub 1:6-12, Shetani akamjibu natoka duniani, kuzunguka zunguka huko na huko humo. Sasa ujue kama unazungukazunguka, basi yupo anayekuzungusha. Acha. Tafuta kanisa, tafuta mchungaji ukae chini, ufundishwe, atakayetoa hesabu yako mbele za Mungu.

Mmezaji – Yeye kazi yake ni kumeza, na amemeza wengi. Ukiweza waweza muuliza Yona alimezwa na Nyangumi bado akaendelea kuishi. Wengi adui yetu amewameza. Wamo ndani ya miliki yake, hawana hiari, wanafanya kile anataka. Ebu kubali tumuamuru akutapike kwa jina la Yesu. 2Tim 2:25-26.

Mtega mitego – Ni mtaalaam wa kutega mitego. Ametega wengi, akawatupia mahindi kama vile tunavyotupia kuku wakati tunapotaka kumkamata. Kuku haoni mtu anayetupa, yeye huona mahindi, na huendelea kufuata mahindi, mwisho hujikuta miguuni mwa mtu na mwisho mikononi mwake, amekwisha! Mtume Paul anasema ‘wala hatukosi kuzijua hila zake’.

Leo nimekupa vitu vitatu vitakavyozuia watu wanaotaka  kuingia mbinguni na wasiweze. Katika sehemu linalofuata nitaendelea kukuonyesha vingine zaidi ambavyo vitawafanya wengi wanaotaka kuingia washindwe. Si nia yangu kukuvunja moyo. Tunaposafiri katika barabara huwa kuna alama za barabarani. Ukikaribia mlima unaikuta inayokuambia MLIMA MKALI. Hii haina maana urudi. Hapana! Ina maana tafuta gia ya kupandia mlima unaoukabili.

Yesu anarudi, ebu jiandae, jitengeneze, tuonane katika sehemu ya pili ya somo hili la Msitari unaoniliza kuliko mistari yote katika Biblia.

Nduguyo Mchungaji  Samuel Imori.

KIBURI

Ziko dhambi nyingi ambazo inatulazimu kupambana nazo, na inatubidi tuzishinde.  Mungu alimwambia Kaini Kama ukitenda vema hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe,  walakini yapasa uishinde”. Hayo tunayasoma katika  Mw 4:7. Lakini leo nitazungumza juu ya dhambi inayoitwa kiburi.

Mith 16:18-19, “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabali hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi”.

Dhambi hii ni silaha mbaya anayotumia adui yetu shetani kumaliza watu wasafirio kwenda Mbinguni. Biblia inasema wazi wazi kuwa moyo ni mdanganyifu, una ugonjwa wa kufisha. Tunatakiwa kuwa makini kabisa; tunatakiwa kujiangalia kabisa; maana imeandikwa kuwa tuulinde moyo kuliko yote tuyalindayo, maana huko ndiko zitokazo chemi chemi za uzima.

Zaburi 30:6-7, “Nami nilipofanikiwa, nalisema sitaondoshwa milele.  BWANA, kwa radhi yako wewe uliuimarisha mlima wangu.  Uliuficha uso wako nami nikafadhaika”. Utakumbuka kuwa Daudi ni mtu ambaye Mungu alijisifia, hata akasema ‘nimeona mwana wa Yese ambaye moyo wake ni kama wangu‘.

Lakini sikia, alipofanikiwa akasema HATAONDOSHWA MILELE.

Mpendwa hapa tunaona kiburi kinafanya mtu anajisahau, anadhani ni wa kudumu, hata hakumbuki kuwa ataondoka duniani.  KAZI UNAYOFANYA KAMA NI YA MUNGU ITADUMU,UTAANDAA MTU WA KUMWACHIA UKINGALI HAI. ILA KAMA NI YAKO, UKIFA NAYO ITAISHIA HAPO.

Mdo 5: 34-37, “Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamaliel, Mwalimu wa Torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo; akawaambia, Enyi waume wa Israel, jihadharini jinsi mtakavyo watenda watu hawa.  Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai kuwa yeye ni mtu wa mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika, wakawa si kitu. Baada ya hapo mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea, na wote waliomsadiki wakatawanyika.”

Yesu alisema  PASIPO MIMI NINYI HAMWEZI KUFANYA LOLOTE.

Ninakuonyesha jinsi kiburi kinavyomwingia mtu, maana ni roho, hata mtu hawezi kujua kuwa kimemwingia. Unajua mwanzilishi wa kiburi ni LUCIFER. Katika Isaya 14:13-15 tunasoma, “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu Nami Nitaketi juu ya mlima wa Mkutano Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye aliye juu”

Kiburi kinamfanya mtu asiridhike na nafasi aliyo nayo. Mungu alimpatia Lucifer kiti chake, na alikuwa ni kiongozi wa sifa, lakini hayo yote hakuona kuwa ni kitu, ndipo akasema mambo hayo hapo juu, kwamba lazima afanane na yeye aliye juu, yaani naye AABUDIWE, na unaona alifanikiwa. Leo watu wanamwabudu, ingawa hana Mungu tena!

Hapa nataka nikuonyeshe kitu: Mungu ameita Watumishi mbali mbali, kama alivyomwita Paul, akampatia mtoto wa kiroho Timotheo.  Ukisoma vizuri, Paul alibaki kuwa baba yake Timotheo, na Timotheo alibaki kuwa mtoto wa Paul.

Siku tulizo nazo Timotheo wengi wamepindua baba zao, wamekalia madhabahu, na watu wanashangilia tu wanaona ni sawa sawa. Acha kujifariji mpendwa!

Nazungumza habari za KIBURI. Soma kwa makini katika Dan 4:28-37. Nebukadneza alitawala, na siku moja akadhani ni kwa akili zake, akadhani ni kwa uweza wake. Hakujua kuwa ni Mungu alikuwa amemuweka. Kiburi kikampata. Akatamka kuwa amefanya makuu kwa uweza wake. Bwana akampeleka porini kwa miaka saba, mpaka akili zilipomrudia. Kumbe kiburi kikimpanda mtu, akili zake huwa hazipo tena!

Mith 27:2, “Mwingine na akusifu, wala si kinywa chako mwenyewe, mtu mgeni wala si midomo yako wewe”. Unaonaje siku tulizonazo, Je! Tunangoja watu watusifu? au tunajisifu wenyewe kuwa sisi ni watu maarufu?

Mith 11:2, “Kijapo kiburi, ndipo ijapo aibu”.

Mith 8:13, “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu, kiburi na majivuno, na njia mbovu, na kinywa cha ukaidi pia nakichukia”.

1Pt 5:5, “Mungu huwapa wanyenyekevu neema, huwapinga wenye kiburi.”

Soma pia kwa makini 2Nyak 26:1-23; Kuna mfalme aliitwa UZIA, alitawala vizuri, alimtafuta Bwana, na Bwana alionekana kweli. Bali katika ule mstari wa 16 Biblia inasema hivi, “Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi Bwana, Mungu wake, kwani aliingia Hekaluni mwa Bwana ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia. Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini, wa Bwana, mashujaa, wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia si haki yako Uzia, kumfukizia Bwana  uvumba, ila ni haki ya makuhani, wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba, toka katika patakatifu. Kwa kuwa umekosa, wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa Bwana Mungu. Akagadhibika Uzia, naye alikuwa na chetezo mkononi na alipowagadhabikia makuhani kukamtokea ukoma.”

Pata muda usome mwenyewe, napenda niwaambie kitu, sio kuwa kila mtu anaweza kuwa  Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji, Mwalimu,  HAPANA.

Efeso 4;11- Naye alitoa wengine kuwa  mitume, na wengine kuwa Manabii, wengine kuwa wainjilisti, na wengine kuwa wachungaji, na waalimu”

Ni Mungu anawaweka, sio ujuzi wa mtu. Waweza kuwa kanisani, ukawa umejaliwa kuwa na pesa, na mchungaji wako hana pesa, na kwa kuwa unatoa pesa kanisani, adui akakuambia una uwezo kabisa kuwa Mchungaji. Na unachofanya, ni kumobilize watu, kwa kuwa una kapesa, mapinduzi yanafanyika, na unakalia kiti, mchungaji anatupwa nje! Baada ya hapo mnaendelea mbele huku mkiambiana  kuwa ‘tunaelekea Mbinguni‘ mnafika mahali hata baba yako huyo hamsalimiani!

Mpendwa ebu shituka. Unajua siku moja Absalom,mtoto wa Daudi, aliweza kabisa kumobilize watu, na Daudi akapinduliwa. Kwa siku zile chache akiwa kwenye kiti, alidhani ni mfalme. Watu walimwita hivyo na yeye akadhani hivyo, ila hakuwa lolote, wala chochote!

Mal 4:4-6, “Ikumbukeni Torati ya Musa, mtumishi wangu, nilivyomwamuru huko Horebu, kwa ajili ya Israel wote, naam amri na hukumu, Angalieni nitawapelekea Eliya Nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na ya kuogofya, Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee  baba zao, ili nisije nikaipiga kwa laana”

Naomba nikusaidie:  Panapo muda kumbuka ni wapi ulipoanguka, urudi. Kama unajua ulipindua madhabahu, waumini wakakuunga mkono, maaskofu wakakuunga mkono, na sasa unamiliki, isikie sauti ya Mungu leo. Geuka, nenda kwa baba yako mwambie, baba nimerudi. Hata kama alifanya nini, atakayemhukumu ni Mungu, ndiye aliyemwita!

Namalizia nikisema kiburi kimenyemelea wengi, utawajua kwa jinsi wanavyoongea- “Nita….!”,  “Nita….!”,  “Nita…..!”

Yohana  15:5, “Mimi ni mzabibu nanyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana,  maana pasipo mimi, ninyi hamwezi kufanya lolote

Ili tuepuke kunaswa na kiburi, ebu tukubali kuwa sisi hatuwezi kufanya neno lolote kama Bwana wetu Yesu alivyosema, ni yeye atendaye ndani yetu. Tukilikubali hilo kujisifu kutafungiwa nje, tutapona na kiburi hakitatupata.

Mungu nisaidie, wasaidie watumishi wako tuweze kuepukana na kiburi, tuambatane na unyenyekevu katika utumishi wetu. Amina!

Mungu awabariki.

Mchungaji Samuel Imori

Baraka na Namna ya Kupokea

Leo tutakuwa tunaangalia maana ya neno BARAKA. Watu wengi tumezoea kulitumia,  limezoeleka, limekuwa  neno la kawaida, na rahisi  kulitamka. Mtu ukimfanyia chochote, kikubwa au kidogo, utasikia ‘Mungu akubariki‘!.  Sielewi kama huwa tunaelewa kile tunachomaanisha, na pia sielewi kama huwa tunaelewa kile wale wanaotuambia huwa wanamaanisha..

Sasa tuanze somo hili kwa maandiko katika Mwanzo 12:1-3, yasemayo:

“Bwana akamwambia Abram, toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha, nami nitakufanya wewe kuwa Taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka, nami nitawabariki, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa“.

Mungu alimwambia Abram, [wakati hajawa Ibrahim] mambo mengi mno, na kama angekuwa hana bidii katika mambo ya Mungu, basi nadhani angeishia kusikia sauti ya Mungu tu, halafu hakuna matokeo yoyote ambayo yangetokea.

Isaya 1:19-20, “Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi, bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga, maana kinywa cha Bwana kimenena haya”

Mstari huu ni muhimu sana, una maelekezo muhimu sana hata kuweza kufikia kile kinachoitwa Baraka: anasema kama tutakubali, halafu tutii.  Ndugu mpendwa,  hakuna anayemkataa Mungu muumba wake, labda kichaa;  labda mpumbavu ndiye husema hakuna Mungu. Lakini kila mtu anakubali, kwenye mikutano wanakubali.  Wahubiri wanapomaliza kuhubiri huuliza wangapi wanamkubali Bwana Yesu  katika maisha yao, karibu uwanja wote, wanakubali, hata kama hawainui mikono, lakini mioyoni huwa kuna sauti inasema ‘lakini ni kweli’, hiyo wanakubali. Tatizo liko wapi? . . . KUTII! Hapo ndipo penye matatizo, na wala shetani hahangaiki kukuzuia usikubali, hilo anasema wewe kubali tu, tena pengine hata hatujui pale tunapoambiwa BWANA asifiwe, tunasema, “Amina!”. Maana yake “Amina” ni “iwe hivyo”. Kwa hiyo kukuacha ukubali hilo ni sawa, lakini tatizo ni hatakubali UMTII   MUNGU.

Ibrahim pamoja na maneno mazuri aliyoambiwa na Mungu wake, ilikuwa lazima afanye kazi ya ziada kupokea kile alichokuwa amekisema Bwana.

Ebr 6:13-15, ” Kwa maana Mungu alipompa Ibrahim ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na kwa hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi“.

Tumeona Mungu akimsemea Ibrahim  mambo mazito, kama vile ambavyo Mungu amesema mambo mazito kwa ajili yetu, maana wote walio katika Kristo ni warithi wazirithio ahadi za Ibrahim. Wengi wetu tunazifahamu ahadi zilizoko kwenye Neno lake, wengi huzikariri katika kuomba, nyingi tu nzuri nzuri, hata zingine huwafanya watu ambao hawajaokoka waamue kuokoka ili wazipate.

Mpendwa, naomba unipe masikio yako;  Hapo juu tumeona neno zito kuwa Mungu aliapa kwa nafsi yake. Hii ina maana hawezi kusema uongo kama neno lisemavyo mahali fulani, kuwa Mungu si mtu aseme uongo, wala si mwanadamu ajute. Kujuta ni tabia ya watu;  tena ni tabia  ya watu kusema uongo, ndio maana tunatakiwa tuishi rohoni, tuache tabia za kiutu za ubinadamu.

Biblia inasema IBRAHIM KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.

Hapo napo pana matatizo.  Kwa kuvumilia nini? Hakuna kitu kizuri kinachovumiliwa, mtu akiniambia “vumilia tu unywe chai hii!”;  mara moja nitajua chai ina matatizo hii, mara ninajua haina sukari.

Sitaingia kwa ndani kukuambia kuwa alivumilia nini? Ebu fikiri hili: Wataalam wanasema tangu Mungu alipomwambia atampatia mtoto kutoka katika viuno vyake ilimchukua miaka 25. Je! Ni mangapi yalisemwa wakati huo wa kusubiri?   Watu walisema walivyoweza, kila aliyeweza kusema alisema, huwa nawaambia watu kuwa kusema hakuhitaji fedha za kununulia betri, wala kuweka umeme, hapana. Ni pale mtu anapokula chochote akashiba, inaweza kuwa mhogo, ugali, mhindi, n.k.

Ni ombi langu kwako; ebu vumilia, tulia mngojee Bwana aliyesema ni mwaminifu, kile alichokuambia atatimiza tu!

Mwanzo 22:15-18, “Malaika wa Bwana akamwita Ibrahim mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki, nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani, na mzao wako utamiliki mlango wa adui zao. Na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia, kwa sababu umeitii sauti yangu.”

Bwana hakumwambia kuwa “nitakubariki kwa kuwa unaisikiliza sauti yangu”, hakumwambia kwa kuwa “nimekuchagua tu ili nikubariki”, hakumwambia “kwa kuwa umeamua kuwa na dini kubwa ya pili, au ya tatu”….! Hakumwambia “kwa sababu umeomba usiku kucha”, “kwa kuwa unanena kwa lugha kama cherehani”. Hapana. Bali ni “Kwa kuwa UMETII SAUTI YANGU“.

Nimesema kuwa hapa kwenye Kutii ndipo penye matatizo makubwa.  Na Isaya amesema kama tukitii tutakula mema ya Nchi, hakusema “kukitafuta mema ya nchi kwa kuombewa tutayapata”, hakusema “tukiwekewa mikono tutapata mema ya nchi”, hapana. Bali ni “kama mkikubali na kutii“.

Nilipokuwa natafakari maana ya BARAKA, niliona kwa ndani zaidi kuwa Kubarikiwa ni:

“Kukubaliwa na Mungu”.  “Kuitikiwa na Mungu”. “Kushughulikiwa na Mungu”. “Kupiganiwa na Mungu”.  “Kutetewa na Mungu”.  “Ni kukingwa na Mungu”. “Kulindwa na Mungu”.  “Ni kulikuza jina Lako”.  “Ni kukufanya wewe mwenyewe uwe baraka”.

Wanaokubariki, utawafanya wabarikiwe. Wanaokulaani, yeye atawalaani. Kwa lugha nyingine vita si yako, ni yake. Wewe utakuwa sababu ya watu wengine kubarikiwa, kunzia kwa watoto wako, wajukuu zako, na majirani zako, hata Taifa lako pia.

Dan 4:10-12, “Njozi  za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi, naliona na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana, mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, , na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia, majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote, wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.”

Ebu  tuendelee kuona baraka maana yake nini, ambayo hailetwi kwa kutabiriwa tu, kisha tukae tukingojea maadamu watumishi wa Mungu wameshatutabiria, hata wangetuwekea mikono yote miwili, kisha waongeze na miguu yote miwili, kama hatutakuwa WAVUMILIVU,  na WATII, Nasema kwa ujasiri wote kuwa tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu!

Yakobo 5:7-11,  “Kwa hiyo ndugu vumilieni hata kuja kwake Bwana, Tazama mkulima hungoja mazao ya nchi, yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake, hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya  mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu msinung’unikiane, msije mkahukumiwa, angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake  Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

Maandiko hayo yanaendelea kuonyesha wazi kuwa uvumilivu ni jambo la muhimu kabisa katika safari yetu ya kuelekea Mbinguni. Pale tunapokosa uvumilivu kuna jambo hutokea.Tunaposhindwa kumngojea Bwana huwa tunashawishika kutafuta na kushika njia nyingine. Hapo manung’uniko mengi na kulaumiana kwingi hutokea.

Wafilipi 2:12-13, “Basi wapendwa wangu kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi  nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema”.

Bado neno linaendelea kukazia kuhusu utii, neno linasema “tutimize”. Kuna kitu tunatakiwa kutimiza. Bila hivyo hatuwezi kuziona ahadi za Mungu tulizoahidiwa, au tunazozisoma katika Biblia. Paulo anasema wakati alipokuwepo  pamoja nao, walitii, lakini sasa anasema asipokuwapo, wao watii zaidi na kutetemeka. Wako watu wanaomtii Mungu wakati Mchungaji wake yupo, wakati kiongozi wa kanisa yupo. Lakini mtu huyo akiwa peke yake, hakuna utii wowote anaouonyesha kwa Mungu. Kumbuka Yusuph alikuwa peke yake kule Misri, tena wakati mke wa Potifa alipomtaka hakuwepo mtu mwingine, ila yeye alikataa kabisa kumtenda Mungu dhambi!

Ndugu zangu Baraka tele tumeahidiwa na Mungu wetu, ama kwa unabii, ama kwa Neno lake, ni za kwetu kabisa,.Lakini zitakuwa za kwetu pale tutakapomtii Mungu wetu; Pale tutakapofanya kile Mungu anatutaka tufanye. Naomba Bwana atupatie roho ya utii, ili tuweze kumtii Mungu wetu.

Namalizia nikikutakia baraka tele, juu yako mwenyewe, juu ya watoto wako, juu ya majirani zako, kiwe chakula nyumbani mwako, cha kimwili na cha kiroho, cha kuwatosha watu wote walio pamoja na wewe.

Nitaendelea kukuombea mpaka baraka zilizotamkwa katika Biblia zikufikilie, pamoja na maombi yangu, lakini nawe umeona unachotakiwa kufanya:

Uwe Mtiifu, Uwe Mvulivu!

Mchungaji Samuel Imori