Katika sehemu iliyopita tuliangalia tofauti kati ya Imani na Tumaini. Katika sehemu hii ya Tatu [III] ya somo letu tutaangalia Tabia za Imani. Tabia hizi za Imani, katika utendaji kazi wake, hubadilika kutokana na sababu mbali mbali kama vile mazingira, ugumu wa tatizo lililoko mbele, kusudi linalokusudiwa nk.
Aina za tabia za imani katika utendaji kazi wake ni hizi zifuatazo:
1.Huona yasiyoonekana
Mungu aliona ya ulimwengu ndani yake hata kabla hajatamka. Alimuona mwanadamu kabla hajamuumba. Mwanzo 1:27 inasema Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe. Alikuwa na picha ya mtu kisha akamuumba kwa kufuata au ile ramani Paulo aliandika.
Biblia inasema, tusiviangalie vinavyoonekana bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu, bali visivyoonekana ni vya milele. 2Kor 4:18.
Kwa maana twaenenda kwa Imani si kwa kuona. 2Kor 5:7. Paulo anaweka mkazo kuwa mwamini hapaswi kutawaliwa na yale anayoona katika ulimwengu wa asili. Hivyo kuona yasiyoonekana ni moja ya utendani kazi wa Imani.
2.Huona kabla haijatenda
Watu wengi hujaribu kuongea Imani kabla hawajawa na taswira ya kitu ndani ya roho zao kwanza . Kwa sababu hawajauona huo uhalisi kile wanachosema hakiwezi kutimia. Kisha wanasema kuwa kukiri Imani hakutendi kazi, nimeshakiri kwamba nimeponywa lakini bado ninaumwa. Kama bado wanaumwa ni kwa sababu bila shaka hawakuwa wameumbiwa ndani yao taswira ya kujiona wazima kwanza maana aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Mithali 23:7
Wakati akielezea hali katika siku za mwisho, Yesu alisema kuwa mioyo ya wanadamu itavunjika kwa sababu ya hofu ya kile kinachoujilia ulimwengu. Luka 21:26. Usemi huu kwa kawaida unamaanisha kuwa roho za watu ambao hawaishi kwa Imani zitashindwa kuzaa matunda. Ukiri ni muhimu lakini ni sehemu tu ya mduara mzima wa Imani.
3.Hukamilisha kazi
Baada ya kusema taswira unayoona Imani husababisha msukumo wa kuanza kutenda kulingana na taswira hiyo. Petro alijiona katika taswira yake akishuka kutoka kwenye mashua na kutembea juu ya maji kumwendea Yesu. Kilichofuatia ile taswira ni maneno aliyoyasema “ Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Mathayo 14:28.
Yesu aliposema njoo, Petro alianza kutembea juu ya maji. Imani ya Petro iliona, ikanena na ikatenda lakini aliyaruhusu mazingira kubadili taswira yake. Alipoyaondoa macho yake kutoka kwa yasiyoonekana na kuyaelekeza kwa yanayoonekana hapo hapo akaanza kuzama. Mazingira yanapokuwa kinyume nawe unatakiwa uwe jasiri, katika Imani, kwa matendo na kutumnia kile ninachoita Imani ya kung’oa dari.
Hebu tuangalie mfano wa huu katika Biblia, kwenye Luka 5:18-20, ambapo inatuambia juu ya watu wane waliompeleka rafiki yao mgonjwa kwa Yesu ili akaponywe. Baada ya kupokea taswira ya kumfikisha rafiki yao kwa Yesu, walifunga safari wakiwa wamembeba yule mtu kwenye machela. Walipolifikia lile jengo ambamo Yesu alikuwa akihubiri walikuta limefurika watu na hivyo hawakuweza kuingia ndani. Kuna wakati haya mambo ya Imani yanatenda kazi hapo hapo na wakati mwingine hayatendi! Walijitahidi wawezavyo lakini walishindwa kuingia ndani. Walipoona hivyo wakatafuta njia tofauti ya kumpeleka ndani: Walipanda juu ya dari wakampitisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. [Lk 5:19]. Hawakuyaangalia mazingira; Imani yao iliona, ikanena kisha ikatenda!
Watu hao walikuwa majasiri na Imani yao, wakalibomoa dari ili wamfikishe rafiki yao mgonjwa kwa Yesu. Naye Yesu alipoiona Imani yao, alimwambia yule mgonjwa, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. Yesu alipoiona Imani yao na matendo yake [ya Imani] alimponya yule mtu.
Imani inatakiwa kutenda kazi namna hii katika maisha yako. Pale unapoona taswira, usiruhusu chochote kikuzuie. Anza kusema kisha Fanya kitendo, na ukikutana na jambo ambalo ni kama vile linakwamisha wewe ufikie taswira uliyoiona moyoni mwako: Tumia Imani ya aina hii ya kung’oa dari kutafuta mlango. Wakati ukielekea kwenye taswira uliyoiona moyoni mwako na ukakutana na mlango uliofungwa, usikate tamaa. Endelea kubisha hadi utakapofunguliwa! Ni hakika Yesu ataiona imani yako na kukutana na hitaji lako.
4.Husimama
Ni lazima ukusudie kushinda. Unaposema “Nitajaribu” unamwambia Ibilisi kuwa una nafasi nusu-nusu ya kushinda au kushindwa; yaani ni kubahatisha tu. Usijaribu kuishi kwa Imani bali Fanya kabisa. Achana na mipango ya kimwili.
- Basi ndugu zangu nawaarifu ile injili niliyowahubiri ambayo ndiyo mliyoipokea na katika hiyo mnasimama. 1Kor 15:1
-Simamia ile injili mliyoipokea. Simama imara katika Imani. Fanya kiume, ukawe hodari. 1Kor 16:13. Imani husimama, kwa maana nyingine hudumu!
Hatuwezi kufanana na watu wa dunia wanaotegemea mambo ya kawaida ya mwili wanaposhikwa na shinikizo na maadui wakiwaambia hakuna namna ya kujinasua. Watu hawa huwa hawana nguvu.
Mfano: Mtume Paulo alisema, huku akiwa na uhakika kwamba Mungu anaweza kufanya yale aliyoahidi [Warumi 4:21], “Nina uhakika kuwa mtatembea kwa Imani na si kwa kuona [1Kor 5:7] kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini. [2Tim 1:12]. Mtume Paulo alikuwa mtu wa uhakika, jasiri na mwenye kujiamini katika Imani na nguvu.
Baadhi ya watu wanadhani kuwa maisha ya Imani ni kuishi kwa njia ya kujihatarisha. Watu ambao hawajiamini ni wale ambao hawalijuwi neno lake Mungu. Mungu anasema ‘Mimi sitalihalifu agano langu, sitalibadli neno lililotoka mdomoni mwangu [Zaburi 89:34]. Na Mungu si mwongo.
Mfano mwingine: Unapomuona mtu tajiri ambaye ana magari na majumba, kwa akili ni rahisi kusema bila shaka mtu huyo atanipatia pesa nifanye Huduma au kujenga Kanisa. Na hapo ndipo Mungu atakunja mikono yake mpaka utakapoacha kuingilia sehemu inayomhusu yeye. Unapoamua kusema BWANA, NINAKUTWIKA FADHAA ZANGU ZOTE!, ndipo Mungu husema ‘hicho ndicho nilichokuwa nakisubiri’. Anaamua kuchukua sehemu yake na kuleta madhihirisho kwa njia za kushangaza kabisa.
Katika sehemu inayofuata tutaangalia tabia zaidi za Imani katika utendaji kazi wake!
Mwinjilisti David Kimwaga


