Tumeanza na Mungu, tutamaliza na Mungu – Joshua Nasari

“Cha kwanza kabisa namshukuru sana Mungu ambaye alinipa maono ya kuwa mbunge wa Arumeru mashariki, nimekuwa nikiyasema kwa muda mrefu watu walifikiri natania, lakini vilevile nikishukuru chama changu cha CHADEMA ambacho kilinipa ridhaa ya kusimama kuwakilisha kwenye uchaguzi mdogo wa Arumeru mashariki, kwakweli niwashukuru sana watu wa Arumeru mashariki ambao hawakujali umri wangu, hawakujali uwezo wangu kifedha, hawakujali historia ya familia yangu katika siasa, hawakujali kila mapungufu ambayo nilikuwa nayo, lakini wakaamua kunichagua…..napenda niseme  na kama nilivyosema tangu mwanzo kwamba tumeanza na Mungu na tutamaliza na Mungu na siyo kwenye kupata kura peke yake, tutaendelea kumtumikia Mungu na kumuweka Mungu mbele, tutamtanguliza yeye na tutaongozwa na yeye siku zote”

Haya ni maneno ya mbunge wa CHADEMA mtumishi wa Mungu, Joshua Nasari (26) aliyeshinda Jimbo la Arumeru mashariki kwa kura 32972 ambazo ni sawa na asilimia 54 na kufuatiwa na mgombea wa chama cha mapinduzi, Sioi Sumari aliyepata kura 26,757 sawa na asilimia 42.

“Shetani ameshakufa, tangu tarehe 4/11/2008″ – Nabii Elia

Ni ajabu na kweli kusikia maneno hayo toka kinywani mwa mzee wangu wa kanisa wa siku nyingi aliyenilea nilipookoka miaka ya 80′s. Leo niliamua kuamka asubuhi na mapema nikaenda kwenye morning glory ya kanisa mojawapo kati ya makanisa jirani. Maombi yalikua mazuri na kwa bahati ndipo nikakutana na mzee wangu huyo wa kanisa. Naye amekua muumini wa kanisa hilo.

Akaanza kunishuhudia ndipo nikaanza nami kujifunza mambo mapya ya upande mwingine wa imani ya kikristo. Kwanza mzee alikua na jina lake la ukoo tulilomtambua kwalo, ameliacha na kupewa jina lingine. Kitabu chake cha neno la Mungu kina gamba la juu jipya na hakiitwi “Biblia” akitaka kuomba anatumia majira, siku na nyakati ili kufanikiwa. Lililoniacha mdomo wazi ni pale aliponiambia kuwa “Shetani ameshakufa, tangu tarehe 4/11/2008 na ameuawa na nabii wetu mkuu. Hata wapunga pepo wanajua hilo, ukiwauliza wanasema ameuawa na nabii Elia…” Nikajiuliza kama wapunga pepo wanajua hilo, wewe Mtakatifu unajua shetani ni marehemu? Kazi kwako!

–EK–

Wachungaji Msitangazie washirika dhambi ya mtu mwingine!

“Mchungaji unapotangaza dhambi/makosa ya mtu kwa washirika/waumini kinachotokea ni kwamba yule mtu hata kama ameshatubu kwa Mungu wale washirika watabakia wakimhukumu “fulani alitenda dhambi hii”. Kwa kufanya hivyo watu hao wanabakia na dhambi hiyo hadi siku yao ya kufa. Maana mtu akitubu Mungu humsamehe lakini watu ni vigumu sana kusahau.

Na wewe mtu uliyeokoka, mtu akitenda dhambi achana naye, usiweke dhambi yake moyoni mwako bali songa mbele katika kumwangalia Yesu”

Mwinjilisti Obadia alipokuwa akihubiri katika mkutano wa Injili mjini Arusha tarehe 22, June, 2011.

Kupata mafanikio ni vita ya kiroho

Watu wasiookoka ambao wamezama katika ushirikina pia wanatambua kwamba mafanikio yao huanzia katika ulimwengu wa roho kabla hayajadhihirika katika ulimwengu unaoonekana. Wanachofanya ni kuwaleta waganga wa kienyeji kuziweka wakfu biashara zao au miradi yao kwa nguvu za mapepo.

Hii ndiyo njia inayowawezesha kupenya kwa kuingia katika ulimwengu wa roho kwa kunuizia nguvu za kishetani. Nawe mwana wa Mungu, Unaweza kupenya na kuingia katika ulimwengu wa roho kwa kuomba katika Roho kwa kutumia mamlaka yako ya kimungu iliyopo nyuma ya Jina la Yesu Kristo. Unapaswa kuchukua mamlaka dhidi ya nguvu za kipepo ambazo zinapingana na mafanikio yako. Ili ushinde inabidi uingie katika vita ya kiroho, uyaone mafanikio yako!

Mtume Prosper K. Ntepa