Utii Kwa Mume

Kiswahili kina mameno machache, tafsiri ya ‘obey’ na ‘submit’ yote ni utii kwa Kiswahili, lakini kwa uhalisia ‘submit’ ni zaidi ya ‘obey’.’Submit’ ni kukubali kwa unyenyekevu kuwa chini ya mamlaka fulani, kuiamini hiyo mamlaka na bila kujaribu kuwa juu yake, na ‘obey’ ni kufanya kile unachoambiwa na mamlaka iliyo juu yako. Hivyo utii wa submit ni zaidi ya utii wa obey. Ni kuamua kuwa chini ya mamlaka hiyo na sio kusubiri kuambiwa kitu ndipo utii. Utii wa mke kwa mume ni ‘submit’, kuamua kuwa chini ya uongozi wa mume wako, kuuheshimu na kumwamini kuwa anaweza kuwaongoza bila kutaka kuingilia nafasi yake kama kiongozi.

Jambo hili limekuwa ni gumu sana kwa wanawake wengi hasa wale ambao wana kipato, wlimu, huduma au nafasi katika jamii zaidi ya waume zao. Biblia inawataka wake wote kuwatii waume zao bila kujali hali zao wala nafasi zao au kama wameokoka ama la.

Waefeso 5:22-24 Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo na wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Mistari hii katika biblia inatuonyesha jinsi gani inavyotupasa kuwatii waume zetu. Paulo amefananisha utii huu na utii wa kanisa kwa Kristo, utii wa kuamua toka moyoni kunakosukumwa na upendo na wala sio utii wa kulazimishwa. Ni utii katika kila jambo, dogo hadi kubwa kama vile kanisa linavyomtii Bwana Yesu. Ila tunapewa angalizo, “kama ipendezavyo katika Bwana”. Hivyo hatupaswi kutii pale ambapo tunaelekezwa kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Kolosai 3:18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.

 Unaweza kusema kuwa mume wako hajaokoka na wewe umeokoka hivyo ni vipi sasa utajiweka chini ya uongozi wake? Biblia inalojibu kama tunavyoona hapa katika mistari hii ifuatayo.

1 Petro 3:1-2 Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;

Kumbe utii wako kwa mume wako kunaweza kumfanya akaokoka bila hata mahubiri ya maneno mengi. Kutii sio utumwa, ni kuitambua nafasi ya mume wako na nafasi yako kama mke kwenye ndoa yenu. Unapoitambua nafasi ambayo Mungu amekupa utashangaa utii unakuja bila hata kujisukuma. Wewe ndiwe mlezi wa familia, mfariji wao, muangalizi, mfundishaji watoto na mengine mengi. Soma Mithali 31:11-31

Katika biblia tunaona jinsi Sarah alivyokuwa mtii kwa mume wake Abrahamu. Mume wake alipomuambia kwamba Mungu amesema watoke katika nchi yao na waende katika nchi atakayowaambia wasipopajua wao, sarah alimtii bila kubishana naye. Alikuwa tayari kuondoka mahali alipopazoea na kuenda na mume wake asipopajua kwa sababu alimuamini Mume wake na kuwa tayari kuongozwa naye. Mwanzo 12:1-9

Mume anajukumu kubwa sana la kumpenda mke wake kama Kristo kwa kanisa, upendo usio na sababu, upendo wa kujitoa kwa ajili yake, upendo wa kumtanguliza. Mume anapofanya haya ni rahisi sana kwa mke kumtii bila kuona uzito, ila hata kama mume wako bado hajafikia kiwango hicho cha upendo, wajibu wako wa kumtii upo pale pale na hapo utaziona Baraka za Mungu katika ndoa yako.

Ubarikiwe na Bwana Yesu.

WADADA – Muonekano wa Nje

1 Samweli 16:7 “Lakini BWANA akamwambia Samweli, usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje,bali BWANA hutazama moyo”

Mungu pekee ndiye anayeweza kuuona moyo wa mwanadamu, mwanadamu hawezi kuona moyo hivyo yeye yupata majiby yake pale anapoangalia mwonekano wa nje. Kutokana na hili basi ni vema wanawake wa kikristo tukawa na muonekano mzuri ili uwe ushuhuda mwema kwa wale wanaotutazama. Moyo mnyenyekevu na mwema huonekana katika muonekano wa nje, ni vyema tukajitahidi kuvaa vizuri, nadhifu na maridadi bila makwazo wala kujishushia thamani.

Muonekano mzuri ni muhimu sababu wewe ni kielelezo kwao waaminio na kwa wale wasioamini na kwa familia yako pia. Kwa wale walioolewa hakikisha muonekano wako haumfanyi mume wako akakosa heshima, vaa vile mume wako anavyopendezwa kuliko kuvaa ili kuwapendeza watu wengune.

2 Korinto 11:7b..Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.

Pia kumbuka kuwa muonekano wako unaonyesha jinsi ulivyo, kama upo rafu rafu basi inaonyesha kuwa hata katika mambo yako mengine haujali, haipendezi mdada kwa na nywele zimefumuka au kuchakaa bila kuzitengeneza vizuri, au kuvaa nguo inayoonyesha sehemu kubwa ya mwili wako mfano kifua, mgongo au mapaja. Kwanza unajivunjia heshima na kumdharaulisha Mungu wako wa wale wanaokuona.

Vaa nguo inayokutosha vizuri, sio kubwa sana sio ndogo sana, hakikisha nguo ipo katika hali nzuri, sio unavaa sketi zipu imefungwa na pini au blauzi isiyo na baadhi ya vifungo. Pia ujue nguo ipi ni ya kuvaa mahali gani na kwa wakati gani, sio nguo ya kwenye sherehe ya usiku wewe unaivaa kanisani. Jitahidi kuuweka mwili wako katika hali nzuri, usiwe na harufu ya jasho wala nywele zisiwe na harufu yoyote mbaya. Tunza mwili wako maana ni hekalu la Roho mtakatifu. Jipende kwanza mwenyewe ili watu wengine nao waweze kupendezwa nawe.

Ubarikiwe.

–Magreth Liwa–