Manabii, mitume na magoli ya kuotea

Ni katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia mkanganyiko mkubwa wa kiimani baina ya wakristo wengi hapa nchini. Hali ambayo imepelekea hata washirika wengi kuwakacha viongozi wao wa makanisa na kuanza kutangatanga huku na kule eti wakiitafuta kweli.

Nadhani hili haliwafurahishi watumishi wa Mungu wengi ambao wanatorokwa na washirika wao hao wapendwa ambao wengi walianza nao kazi ya Mungu muda mrefu. Hili linaeleweka, na ndio maana nimeamua kuandika makala hii. Kwani kama mimi nisie mchungaji naweza kujisikia vibaya juu ya jambo hili basi ni dhahiri wachungaji wengi wasingependa washirika wao wapepetwe huku na kule kama makapi. Lakini mambo huwa kinyume kidogo kwa ndugu zetu, si wote, mitume na manabii, kwa hakika wao hufurahia wanapoona watu wanatoka kwenye makanisa yao na kujaa kwenye huduma zao zenye majina mbadala ya kutisha, ‘a.k.a’.

Hapa sizungumzii huduma zinazoalika watu kwenda kuzimu, ila ni huduma zinazomnena Kristo na kutumia Biblia hii hii tunayoitumia sisi wateule wengine. Suala la msingi ninalojaribu kuliweka bayana ni mtindo wa mahubiri ya manabii na mitumehao, dhamira yake, na athari zake kiimani kwa washirika wachanga na hata wale ambao hawajamjua Mungu na wokovu wake bado.

Hivi sasa, kama huna habari, uponyaji wa mwili umekuwa ni biashara ya baadhi ya watumishi wa Mungu. Inashangaza sana pale mtumishi wa Mungu, tena mtume au nabii, anaposema hana sababu ya kuendelea kuwahubiri watu injili ya uponyaji wa roho zao na ondoleo la dhambi zao. Eti kwa sababu watu wamehubiriwa injili ya jinsi jinsi hiyo vya kutosha, hivyo wanahitaji kuhubiriwa juu ya mafanikio. Ni mafanikio gani? Kibiblia, hakuna mafanikio yanayoanzia mwilini. Mafanikio ya ki-Mungu hutokana na ustawi wa roho ya mtu kwanza, 3Yohana1:2 “ Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.” Kutowahubiri watu juu ya kutubu dhambi zao na kuziacha kunafanya uponyaji wa Mungu uwe kama vidonge vya homa. Biblia imeweka bayana kwamba watu wajapohubiriwa na kuziacha dhambi zao ndipo ishara zitaambatana nao kama “bonus”, Marko 16: 15-18

Kimsingi, bado tuko watu wengi ambao tunapata maswali mengi mioyoni mwetu juu ya baadhi ya ndugu zetu wanaojiita mitume na manabii. Suala la unyenyekevu kama tulivyozoea kuwaona wachungaji na wainjilisti wengi kwao halipo. Kitendo cha kuamua kulumbana waziwazi kwenye luninga juu ya mafundisho ya watumishi mbalimbali kimetupa shaka watu wengi kuwa huenda wachezaji hawa wanatafuta kulazimisha magoli yasiyo halali. Mtumishi wa Mungu anaposema ukiwafundisha watu wasitengeneze nywele unataka wenye saluni wale wapi, kwangu mimi hili halina mantiki “non-sense”, maana hakuna makampuni yanayoingiza pato kubwa kwa taifa letu kama makampuni ya pombe na sigara, lakini bado tunahubiri kuwa pombe, sigara, uzinzi ni dhambi, na itabaki kuwa hivyo, hata kama kuna watu wanaishi kwa kuuza sigara, pombe au ukahaba. Tunapokuja kwenye shughuli ya kumnena Kristo na kweli yake, tunamnena kama alivyo, hatujiulizi mara mbili-mbili wala kutazama mazingira, maana neno la Mungu ndivyo lilivyo, ni kali kuliko upanga ukatao kuwili, Waebrania 4:12.

Tena nina hoja juu ya mtumishi mmoja. Bado sijaridhika na dhana nzima ya kusujudiwa miguuni kisha yeye anaendelea kufurahia eti wananishukuru. Wanakushukuru kwa lipi? Kwa wale wanaomfahamu nabii T.B Joshua; Mtu huyu huwa anajitoa mno kuwasaidia watu kimwili “material support”, wajane, yatima na wenye shida mbalimbali lakini mtu yeyote akisema, “asante nabii”, ghafla anamkatisha na kumwambia “mshukuru Mungu pekee”. Sembuse kumsujudia!. Au hamjui kuwa hata Bwana Yesu mwenyewe alikataa kuitwa mwema pamoja na ukweli kuwa alikuwa ni Mungu? Marko 10:17-18 Pia ningeomba atafakari tena ushauri wake ya kwamba mtu akitaka kukuibia mumeo wewe pambana nae hata kumpiga na masufuria. Ushauri huu si wa kiungu hata kama anadai atajibu yeye mbinguni badala ya kanisa. Nasema hivi kwa sababu Biblia haitufundishi kupambana kimwili na wabaya wetu, bali tumeamliwa tuushinde ubaya kwa wema, Warumi 12: 17-19, 21 “ Msimlipe mtu ovu kwa ovu . . . Wapenzi tusijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana . . . Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”

Ieleweke wazi kuwa; Dhumuni langu si kuwanyoshea kidole cha fitina watumishi wa Mungu, la hasha, tunawaheshimu sana. Ila wao pia, kama wanadamu wengine, waliopewa nafasi “favor”, na Mungu kuwa mitume na manabii wanawajibika mbele ya bosi wetu mkuu ambaye ni Yesukama wengine wasio mitume na manabii watakavyowajibishwa kama mistari hii inavyojieleza, Yeremia 23:25 – 32, “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, . . ., Nabii aliye na ndoto, na aiseme ndoto yake; nayeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. . . Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA.”

Jambo hili la watumishi kuhubiri watu ndoto zao limekuwa mtego uliowanasa wengi. Hivi karibuni, huko Nyakato Mwanza, kulikuwa na mkutano wa injili wa mtume mmoja maarufu hapa nchini. Mtumishi huyu alitoa unabii ambao kwa kweli hautofautiani na mfano wa mchezaji kufunga mpira wa kona kwa kutumia mkono. Namnukuu “. . .kuna mtu hapa, na wenzio unawajua. Kazi yenu ni kuchukua watu misukule na kwenda kuwaficha huko. Kama hutajisalimisha leo hapa, nakupa siku saba utaonja mauti . . .” Mpendwa, unabii huu haupimiki kwa mizani yeyote ile “non-quantifiable prophecy”. Utaniuliza kwa nini? Ni rahisi; Hebu tuangalie manabii wengine wanafanyaje kazi ya Mungu; Hivi karibuni nilitazama unabii wa nabii T.B Joshua wa Nigeria juu ya taifa la Pakistan, akasem “I see something like signature . . . one senior government leader in Pakistan saying hey! I’m resigning . . .” Akimaanisha “naona kitu kama sahihi, mtu mmoja wa ngazi ya juu serikalini katika taifa la Pakistan akisema hei! najiuzuru”. Baada ya muda si mrefu, kweli aliyekuwa raisi wa Pakistan Gen. Perves Musharaf akajiuzuru kwa namna ile ile iliyotabiriwa. Hapa watu watauona ukuu wa Mungu na kumpa Yesu maisha yao. Lakini tunapouangalia unabii kama wa Nyakato, utaona una mazingira ya kulazimisha.

Mwisho ningependa tuzungumzie kile ninachokitafsiri kama ni kukosa nidhamu ya kiroho na unyenyekevu wa kitumishi, ama kwa lugha inayoeleweka zaidi kwa sasa hivi tungesema kuleta usanii katika huduma. Zimepita siku kadhaa tangu ufanyike mkutano mkubwa kabisa wa kinabii jijini Mwanza ulioandaliwa na huduma ya ‘Ngurumo ya Upako’ Katika mfululizo wa kuonyesha matukio yaliyotokea katika mkutano huo, nilishuhudia kwa kupitia televisheni moja ya kikristo wafuasi wa nabii huyo, walipokuwa kwenye boti majini, wakisema . . . mheshimiwa nabii, nimewahi kuhudhulia mikutano mingi ya watu kama Moses Kulola na wengine ila sijawahi kuona kitu kama hiki…kicheko. Huu ni ukosefu wa nidhamu na unyenyekevu wa kitumishi. Mimi sijawahi kumsikia Moses Kulola wala Kakobe akitaja jina la mtumishi wa Mungu mwenzie na kumshusha daraja, tena kwenye televisheni. Labda tukubaliane Mungu aliyeianzisha huduma hii ni Mungu wa “Ngurumo ya Upako” na si MUNGU wa Ibrahim, Isaka na Yakobo alieumba mbingu na nchi. Vinginevyo haikuwapasa kunena kwa namna ile kama watumishi.

Na kwa taarifa yenu, waheshimiwa mitume na manabii feki, mnaopenda kuropoka hovyo kwenye runinga na redio, mjue mnatumia sadaka za watu wa Mungu vibaya. Mnawabebesha washirika mzigo wa mamilioni ya fedha kudhamini vipindi ambavyo mnavitumia kurumbana na watumishi wenzenu. Kwa taarifa yenu, leo nataka niwaambie siri; Ustawi wa kanisa la Mungu Tanzania unadhoofisha ufalme wa shetani katika taifa letu. Ila mnapovuruga mambo mjue kabisa mnaustawisha utawala wa shetani katika taifa letu, taifa litalaaniwa, na laana ile itawageukia ninyi. Msitutie ujinga, Mungu mnamjua, na kazi zake ni dhahili, kama mmetumwa kweli na Mungu, fanyeni kazi yake na mtuondolee michezo yenu ya kuigiza madhabauni pa BWANA. Utamkuta mtu yuko bize kweli!. . “ eeh ndio Yesu nakusikia, naam! Unasema tuombee Chalambe eh?. . . ok, sasa Yesu anasema tuombee Chalambe…ah no, ameghaili, anasema tuombee Buguruni”. Huu ni ujinga kabisa, na sipendi watu waifanye madhabahu takatifu ya BABA yangu aliye mbunguni kuwa ni jukwaa la maigizo. BWANA anaposema na mtumishi wake nabii juu ya watu wake hata vitabu huandikwa, tena sauti yake ni ya utisho awapo kazini, Obadia 1:1, Yona1:1-2, Mika1:1, Nahumu 1:1.

Watu wa Mungu na muwe Imara, maana yanakuja makuu kuliko haya tunayoyaona sasa, tumtazame Kristo, aliye muanzilishi na mwenye kuitimiliza imani yetu. Tukichanganyikiwa mapema, tutazimia mioyo na kuchoka njiani hata tukaiacha imani. Amen!

—Kelvin Kahonga, —

Advertisements

25 thoughts on “Manabii, mitume na magoli ya kuotea

 1. Ashaley,

  Kutotaja vibaya vibaya watumishi wengine kwa Nabii Geor Davie sio kigezo cha kuipima kazi yake, Yesu aliwasema vibaya mafarisayo, na pia kufukuza watu waliofanya biashara hekaluni!

  Basi kama kuna kuipima kazi yake,hasa kwa kutumia macho ya kibinadamu basi kutafanyika na anachokihubiri, anachokifundisha, na maisha yake mbele ya jamii kama yanakwenda sababa na Neno lake! Na wala tu hatuwezi kuipima kwa miujiza! Wingi wa watu, au kutowasema watumishi wengine nk.

 2. @ Kelvin: Nimeshuhudia mikutano ya Nabii Geor Davie wa Ngurumo ya Upako, na sijamsikia akiwataja vibaya watumishi wengine, ila huduma yake ndio inayopigwa vita na watumishi wengine. Naamini kuwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ni yule yule wa GeorDavie, anaiwakilisha vema Serikali Tukufu ya Ufalme wa Mungu. Kwa kushuhudia mikutano yake, ndipo utakapojua ukweli kuhusu huduma ya Ngurumo ya upako na Nabii Geordavie.

 3. Imani unatia moyo, maneno yote uliyosema ni mema na haki. Pia asante kwa maandiko. Nadhani Yesu na injili vitaenda mbele ila hizi dini zimetuletea makapi mengi sana.
  Asanteni

 4. Shalom dada Lisa
  Ningependa kuchangia kidogo katika jambo mlilogusia pamoja na kaka Mdoe.

  Mimi nasali Efatha na hiyo taarifa ninayo.Ni kweli kabisa si kila jambo / mchango unamgusa kila mtu kwa wakati mmoja au katika shughuli fulani, Roho wa Mungu anaposema nawe basi unaweza kufanya, na unapoona hupati amani ya Kristo basi hatupaswi kujilazimisha. Mungu anaweza kusema na watu wachache kwa ajili ya kusudi fulani.

  Kuhusu Efatha kuna ujenzi wa chuo wanatarajia kufanya pale kibaha kwa ajili ya taaluma mbalimbali kwa ajili ya watanzania na mipango mingine ya kuongeza huduma kwa jamii. Kuna madhehebu mengi sana kama wakatoliki, walutherani n,k wamekuwa mtari wa mbele kujenga mahospitali, vyuo, e.t.c hata sisi pamoja na kazi kubwa ya kueneza injili tunaweza kuamua kuchangia kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Na pengine wenzetu wamekuwa wakipata misaada toka kwa wafadhili nje ya nchi, lakini sisi mfadhili wetu ni Yesu kupitia kazi za mikono yetu.

  Pia naomba nikusahihishe kuwa kwa case ya Efatha si kweli pesa za vijijini huwa zinaenda makao makuu kila mara, almost makanisa yote ya mikoani yamejengwa kwa michango ya watu wa makao makuu kwa asilimia kubwa na kabla sijahama DSM nilihudhuria mipango na mikakati hiyo na tutakuwa tukiendelea kufanya hivyo kadiri tutakavyopata neema. Na saa nyingine tunazikusanya halafu kamati kuu ya makao makuu wanapanga namna ya kuzigawanya kwa shughuli zinazohusu ujenzi, mahitaji ya vituo mbali mbali kwa kuzingatia ukubwa na uhitaji wa vituo. Kiongozi wa huduma hagusi kabisa pesa za huduma, iwe sadaka, fungu la kumi e.t.c na wala hapokei mshahara. Yeye anaweza kutangaza, kuhamasisha, na kuongoza kadiri Bwana alivyosema naye lakini kamati na accounts na wanahuduma ndo wanaohusika na pesa hizo kwa mikakati na malengo ya mwaka tuliyopanga. Hagusi unless watu wakiamua / ukiamua kumbariki wenyewe.

  Kwa case hii ya nusu mapato watachangia watu vituo vyote ambao watapata neema, ‘SI LAZIMA’. Si kweli kuwa vituo vyote nje ya DSM wanaishi watu maskini, hapana. Kuna branches za mikoani ambazo pia wanaweza kuchangia kwa ajili ya vijiji vya mikoa hiyo. Mimi naishi Mwanza na kituo chetu cha Efatha Mwanza kinaendeleza kusaidia kujenga makanisa ya ndani ndani zaidi.

  Pia kutoa ni moyo si umaskini wala utajiri,nafikiri ukiwa unatambua thamani ya wokovu na kutamani watu waokolewe basi kuwasaidia watu kupata injili ni kitu cha thamani mbele za Mungu kuliko utajiri wa kibinadamu. Cha muhimu ni kujua unatoa kwa kusudi lipi. Kama kipindi cha matendo ya Mitume (Mdo 5) waliweza kuwa na makubaliano yao kama kanisa.

  Ni kweli kuna manabii wa uongo, matapeli , wenaotumia pesa za watu kujinufaisha n.k wala sikatai, lakini si sawa kupoteza imani kwa watumishi wote si kila jambo huwa linafanyika kwa nia mbaya. Na kuna wakati inawezekana watumishi wetu wakawa na mapungufu lakini pia tuna nafasi ya kumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze katika mapenzi yake na ni muhimu kuwaombea na kuliombea kanisa (mwili wa Kristo kwa ujumla bila kujali huduma ili wasitoke nje ya kusudi na hata panapotokea lengo la kupotosha basi aingilie kati au afanye njia nyingine .

  2Nyakati7:14
  Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao

  Binafsi nawapenda / nawasikiliza na kutii matamko ya watumishi hata kama ni nje ya huduma yangu kadiri Roho Mtakatifu anavyoniongoza na ninapokuwa nina doubt basi naingia magotini ili Bwana aongoze sawa sawa na mapenzi yake

  Wafilipi 4:7
  Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  Zab 32:8
  Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.

  Isaya 48:17
  Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata

  Nawapenda, tuendelee kuombeana na kusaidiana. Tukiomba kwa bidii kuomba kwa ajili ya kanisa (mwili wa Kristo)
  Napenda kuendelea kujifunza toka kwenu.

 5. Kwa vigezo hivyo Lisa nadhani ni sahihi kwa biashara za kihindi maana wafanya biashara hujali pesa ziinge wala hawajiulizi zinatoka wapi au kwa nani, lakini si kwa vigezo vya kibiblia. Kuhusu Sulemani, wafalme walipeleka fedha na mali kwa sulemani (siyo maskini waliopeleka fedha) ingawa wote walifaidika kwa hekima za Sulemani. Pili kama mwenye makosa ni mtoaji na siyo mlaji basi ina maana kwamba huyo mlaji si muungwana. Mungu ni mwaminifu (siyo dhalimu) na siku zote anatetea maslahi ya maskini.

 6. Bwana Yesu asifiwe sana!!
  Hivi mbona Mfalme Sulemani mteule wa Bwana alipokea zawadi nyingi tu?? unataka kuniambia kwamba wafalme waliomletea Suleman mali nyingi hawakuwa na Maskini katika falme zao??. Kama maskini walikuwepo mbona walichukua mali na kuzipeleka kwa Sulemani na Sulemani alipokea bila kipingamizi?. Mali zile zilipelekwa kwa Sulemani kwa sababu ya hekima Mungu aliyomjalia.Soma 1Wafalme10:1-Mwisho. Kwa upande wangu silaumu saana hawa wanaopeleka sadaka zao makao makuu huenda kuna kitu kimejificha hapo na mtu wa kijijini hajagundua bado ndio maana wakisikia kutoa sadaka kwenda makao makuu wanazikimbiza haraka kweli. Nimesali Efatha wiki mbili sasa zimepita wanatakiwa kutoa fedha nusu ya kipato chako/mshahara wako uende makao makuu lakini moyo wangu haunitumi kupeleka, ila nilicheka sana. Na sadaka hiyo itapelekwa Machi mwanzoni ila watabarikiwa walio wake. Wakati mwingine tunahitaji kuomba ili mambo haya yabatilishwe badala ya sadaka kupelekwa mijini makao makuu, zikusanywe na kujenga nyumba ya Bwana kijiji hadi kijiji. “Ombeni lolote kwa Jina la Yesu mtapewa” Watumishi huenda wanakula lakini kosa si lao ni kosa la mtoaji.
  Tunajifunza

 7. Sasa naona ukweli unajitokeza. Vijijini hakuna watenda kazi kabisa, hata makanisa haya ya kipentekoste ukienda vijijini wanachangishwa sadaka ya kupeleka makao makuu (darisalamu) wakati hao wanakijiji wanasalia ndani ya kikanisa cha makuti. hiyo sadaka darisalamu, wakuu wa dini na rafiki zao wananywea soda na kuku. Mimi naona dini dini hizi pamoja na wachungaji/manabii/miume wengi wanatumikia matumbo yao badala ya watu. Wewe utaonaje maskini wakibarikiwa kwa kukuletea wewe pesa badala ya kuwa kinyume cha hapo?
  Angalia hao viongozi wa dini wote watoto wao wanasomea huko ng’ambo marekani au Uingereza! Yaani kweli wapendwa kweli akili zetu zimechukuliwa msukule au tumekuwa wavivu wa kuona na kufikiria?
  Samahani kama naonekana kuwa wazi sana.

 8. Bwana Yesu asifiwe!!!!
  Uswege
  Nukuu “””Nakubaliana na wewe Lisa, lakini kama kuna mkristo haoni umuhimu wa Kununua Biblia huyo kweli ni Mkristo?”””
  Watu hawa kweli ni wakristo!!! Lakini tatizo ni msingi walionao kwenye swala la biblia. Madhehebu mengine nikitoa mfano Catholik ni dhehebu la kikristo, lakini msingi wa neno la Mungu hawana. Hawa mara nyingi hutumia Miongozo ya Vitabu ikiwemo Misale ya Waumini. Ni watu wachache ndani ya kanisa hili tena kwa baadhi ya maeneo wameweza kwenda na Biblia kanisani vinginevyo ni vitabu vya misale vyenye miongozo ya ibada na neno la siku hiyo kutoka kwenye biblia basi. Watu kama hawa wasipopata changamoto ya hawa watumishi wa Mungu watasidikaje??.Na Katholik ni wengi sana mijini na vijijini.
  Kuna Muslim nao Biblia hawaijui hata kama wanaijua ni kwa ajili ya challenge kwa watu fulani, hawa nao wasaidiweje kama siyo through watumishi??.
  Watu wengi ni wakristu lakini msingi wa neno la Mungu hawana wanahitaji msaada kwa yeyote yule mwenye uwezo wa kufundisha, kuhubiri na kusisitiza kuhusu kusoma neno. Ndio maana nasisitiza kwamba watumishi tunawahitaji sana.
  Nukuu “”””Na hao mitume unaowazungumza hawajajazana vijini unakosema kwenye shida ya Biblia! bali wapo Mijini tena ile miji Mikuu wakitumia gharama kubwa kuwa hewani kwenye Luninga!””””
  Ni kweli watumishi wengi wako mijini lakini wale ambao kwa kiasi fulani wako mbele wameanzisha huduma vijijini. Na huko vijijini kuna watumishi ambao husaidia kutoa huduma kule. Na mtumishi anapoonekana kwenye TV au akatengeneza videos hii husaidia kusambaa zaidi kwa habari ya neno la Mungu. Kwa jinsi ninavyoona mimi Mtumishi wa Mungu akifanya semina mjini, ni rahisi kwa semina hii kupenya hata kijijini kwa sababu kuna watu wa vijijini watahudhuria semina ile au kusikikiliza na kuona vilevile na watapata kitu fulani na kuwasidia wale wa vijijini. Wakati mwingine huwa ni vigumu kwa mtumshi kuzunguka mikoa yote au wakati mwingine ni jinsi alivyoongozwa na Roho wa Mungu.
  Nukuu“”””””Ulokole wa leo hauna tofauti na uganga?”Manabii wa leo hatuoni wakilia juu ya Utakatifu, kuteseka na kudharaulika kwa ajili ya Kristo!Una mkosi, una madeni! umekosa Mchumba! Biashara zinakwenda Kombo! Una jini Mahaba! “”””” Manabii hawa si kwamba wanamtangaza Yesu mwingine au vinginevyo wawe manabii wa nguvu za giza. Lakini kama yale yale watu wanayoendea kwa waganga, ndiyo hayo hayo tunayapata kwa Yesu tena bure kwa nini usimtangazie hivyo hivyo ili aende kwenye njia iliyo sahihi. Utajiri unatoka kwa Yesu, Majini mahaba yanatimua kwa Jina la Yesu, Kazi unapata ukiwa ndani ya Yesu kwa nini usimtangazie mtu direct kwamba haya yote unayotafuta kwa mganga kwa Yesu utapata bure??? Kwangu mimi sioni shida hapo. Ifike wakati Yesu tuliemfungia kanisani,mifukoni, kwenye cover za biblia tumtoe sasa waziwazi aonekane na watu wajue kwamba kile wanachokifuata kwenye nguvu za giza hata kwa Yesu kipo halafu BURE””””. Tusiwaangalie kama vile wako kibiashara zaidi ila wako kwenye huduma lakini shida ni kwamba;HEKIMA, BUSARA, MAARIFA, YA KUFANYA HUDUMA INAKUWA NA UTATA. Tuzidi kuwaombea wasimamie zaidi sauti ya Roho wa Mungu na si kufanya mambo bila kuomba na kufuata sauti zao wenyewe. Pole pole tutafika. Ila kwa sasa Tanzania kuna mwamko sana pamoja na mapungufu ya watumishi tulionao ni kuzidi kuwaombea ili tuweze kung’oa roho ya dini na badala yake sasa iwe ni habari za Mungu aliye hai na si huduma ya kanisa au ministry fulani. Tukishaokoka tunakuwa watoto wa baba mmoja.
  Tunajifunza.

 9. Nakubaliana na wewe Lisa, lakini kama kuna mkristo haoni umuhimu wa Kununua Biblia huyo kweli ni Mkristo? na kama haaoni umuhimu ka kuwa na Biblia kwa nini anaona umuhimu basi wa kusikiliza hata hao manabii, ambao wengi wako kwenye Luninga! kama si uvivu wa Kiroho! nini basi. Na hao mitume unaowazungumza hawajajazana vijini unakosema kwenye shida ya Biblia! bali wapo Mijini tena ile miji Mikuu wakitumia gharama kubwa kuwa hewani kwenye Luninga! Kwa hiyo sidhani kama hao Mitume na Manabii wako kwa sababu watu wameshindwa kulisoma Neno na wao wamesimama badala ya maskini! Kwa kifupi Nenda kijijini kama utakuta Mtume na Nabii! Mmoja wa hao mitume ameona credibility yake imeshuka mkoani Arusha kaamua kuja kubanana hapa hapa Dar!
  Kwa kifupi sijasema watu wasiende makanisani! Neno la Bwana linasema “msiache kukutanika pamoja madamu iitwapo leo” Tunapokutanika pamoja inabidi tujengwe na kukuwa na kuwa watu wazima! sio kunywa maziwa tu ! na kuwa wachanga tukiyumbishwa na kila upepo wa elimu!
  Kwa kifupi kuvuma kwa hawa Manabii, Mitume ni Ishara kamili kwamba kwa sehemu hali ya waumini wengi ni bado changa sana! Nimeona baadhi ya watu Waliookoka na Wakiokokeshwa yena na hao manabii, watu waiobatizwa ubatizo wa maji mengi, wakibatizwa upya na hao mitume! Kila kitu ni sarakasi ambayo hujii kesho italeta nini! Leo Msukule! Kesho njoo peperusha kitambaa cheupe kwa ajili ya utajiri, kesho kutwa nenda kwenye makaburi ya babu zako kuondoa laana ya umaskini, Mtu mmoja asiyeokoka aliuliza mbona “Ulokole wa leo hauna tofauti na uganga?”Manabii wa leo hatuoni wakilia juu ya Utakatifu, kuteseka na kudharaulika kwa ajili ya Kristo! Tofauti ya manabii hawa na Sheikh Yahya au zamani Profesa Vulata ndogo mno! Una mkosi, una madeni! umekosa Mchumba! Biashara zinakwenda Kombo! Una jini Mahaba! Haiitaji kuwa Mwanafunzi mkuu wa Biblia kugundua hii iNJILI ya manabii wengi ni Injili Nyingine! Ni Roho Nyingine, na ni Yesu Mwingine!

 10. BWANA YESU ASIFIWE SANA!!!

  WATUMISHI WA MUNGU NI MUHIMU SANA KATIKA JAMII.
  MTU ASIYEJUA KUSOMA ATAAMINI KWA KUWA AMESIKILIZA, AKAFUNDISHWA, AKAELEWA N.K.
  WATU WENGINE HAWANA HATA UWEZO WA KUNUNUA BIBLIA. WATU HAWA WAPO NA WATASIDIKAJE KAMA SI THROUGH MTUMISHI ATAKAYEFUNDISHA, AKAELIMISHA, N.K. WATU HAWA WAPO TUNAISHI NAO KATIKA JAMII NA TUNAWAONA WATASAIDIKAJE KAMA SI KWA KUFUNDISHWA THROUGH MTUMISHI WA MUNGU???
  WATU WENGINE HAWAONI UMUHIMU WA KUNUNUA BIBLIA ASIPOFUNDISHWA AKAJUA UMUHIMU WAKE ATASAIDIKAJE?
  WAKATI TUNAPOSEMA TUSIMAMIE NENO NA KUJARIBU KUONA WATUMISHI SI WA MUHIMU SAAAAANA TUANGALIE MAKUNDI YOTE. MARA NYINGI TUNAJADILI TUKIANGALIA KUNDI LILILOKO MJINI LENYE UWEZO WA KUBOFYA KEYBOARD,KUPATA BIBLIA KIRAHISI KABISA, KUNDI LILILOFUNGUKA AKILI!!! NA KUSAHAU KUWA KUNA WENGINE WAKO VIJIJINI HATA BIBLIA HAWAJUI KAMA KUNA AGANO JIPYA NA LA KALE. HAWA WASAIDIWE VIPI??? KAMA WATUMISHI SI MUHIMU KWAO.
  PAMOJA NA KUWA NA SHERIA NYINGI LAKINI MUNGU ALIMWEKA YOSHUA KUWAVUSHA ISRAEL PALE YORDANI.
  TUKIJARIBU.
  TUSILAUMU WALE WANAOMWENDEA MUNGU KANISANI KILA JUMAPILI NA KUWAONA WANATAFUNIWA NENO, TUTAFUTE NAMNA YA KUWASIDIA; MOJAWAPO KUSOMA NENO; LAKINI HUYU MTU ATAELEWAJE NENO WAKATI HANA MSINGI MZURI WA KUSOMA NENO???
  HAPA NABII,MTUME, MWANAMASIFU ATAHITAJIKA KUMWELEWESHA HUYU MTU. SI WOTE WENYE MSINGI MZURI WA KUSOMA BIBLE HAWA WANAHITAJI USAIDIZI SAMBAMBA NA NEEMA YA MUNGU ILI TUWE PAMOJA.
  TUWATIE MOYO WATUMISHI WA MUNGU WAZIDI KUSAIDIA WATU WA KUNDI HILI ILI NAO WAFIKE PALE TULIPO SISI, PAMOJA NA MAZINGIRA MAGUMU WANAYOPITIA TUTAFIKA .
  TUNAJIFUNZA

 11. Biblia iko wazi “Chachu kidogo huchachua donge zima” na kuwa “Chemchemu itoayo maji mbaya haiwezi kutoa maji mazuri” Ni kweli kila mtu kapewe karama yake yake, lakini kila karama iko katika “Wigo” wa neno la Mungu! Kitabu cha ufunuo kiko wazi kabisa! Juu ya hatari ya kuongeza na kupunguza maneno ya Mungu.

  Watakatifu, Neno la Bwana linasemaje….” hata wataeule” wanaweza kupotea! Wakristo wengi wa leo wanataka kutafuniwa Neno la Mungu, hawana muda wa kukaa na Bwana, kulisoma na kulitafakari Neno, wengi wa wakristo Neno la Mungu katika maisha yao wanalipata masaa machache siku ya jumapili! Wanalielewa Neno kwa kupitia miwani ya mtu mwingine!
  Tusisoma Neno la Mungu kama Waasemblies Of God, Walutheri, Wasabato, Wapentekoste, Waanglikana wanavyofundisha! Soma neno la Mungu kama Mtu unayetaka Bwana aseme na wewe! naye atasema na wewe! na kila kitu kitakaa mahali pake! Utamfahamu Huyu Mungu kuwa ni mkuu kuliko Dhehebu, Manabii na wanaojiita Mitume nk.Kwani anasema nanyi mtaifahamu Kweli nayo Kweli itawaweka Huru!

  Jambo jingine la kukumbuka ni kuwa Manabii wa uongo hawatakuja na kusema kuwa ” Nimekuja kuwapotosha” au “Kuwapeleka Jehanamu” kwani hata wao hawajui kuwa wamepotoka na ndio maaana wanaitwa “Mbwa Mwitu waliovaa mavazi ya Kondoo” Tukea tukijua si Kila mtu anayesema “Yesu” “Roho Mtakatifu” anatumiwa na Bwana! Shetani toka awali alitumia maneno ya Mungu! na Paulo anasema hujuigeuza kawa mfano wa wana wa Nuru!
  Tusipime kazi ya Mungu kwa wingi wa kundi la watu, kwani ni wengi watakaokwenda Jehanamu! na wala matendo ya miujiza, kwa Biblia imeonya kabisa katika hilo. Kila jambo litapimwa na Mizania ya Neno la Mungu, Paulo anasema kila kazi itapimwa! Hebu tuwe kama watu Waberoya! Tusimeze kila kila kitu kutoka kwa kila mtu anayeibuka na kujiita “Mtume” “Nabii” nk!

 12. BWANA YESU ASIFIWE SANA!!
  KWA UPANDE WANGU NAVYOONA KILA MTUMISHI WA MUNGU ANAFANYA KAZI YA MUNGU KWA JINSI ALIVYOITWA.
  MWINGINE ANAWEZA AKAFUNDISHA NENO LA MUNGU VIZURI NA ASILIMIA KUBWA YA WATU WAKAELEWA VIZURI KWA KIWANGO CHA KUWEZA KUYATENDEA KAZI. WAKATI HUO HUO MWINGINE HATA AFUNDISHE KUANZIA ASUBUHI MPAKA JIONI WATU WACHACHE SANA WATAELEWA LAKINI AKIINGIA KUSIFU NA KUABUDU WATU WENGI WATAOGELEA NDANI YA UWEPO WA MUNGU. LAKINI WOTE NI WATUMISHI WA MUNGU KILA MTU KWA NAMNA ALIVYOJALIWA.
  WENGINE WANAWEZA SANA KUHUBIRI INJILI NA WATU WENGI WAKAPONYWA NA MIUJIZA IKATENDEKA NA WATU WENGI SANA WAKAAMINI. LAKINI MTUMISHI HUYO HUYO HAWEZI KUSIMAMA KAMA MWALIMU NA AKIFUNDISHA WATU SI AJABU WASIMWELEWE.
  KWA HIYO UTUMISHI WA MUNGU WAWEZA KUKUJIA KWA NJIA YOYOTE, UIMBAJI, UFUNDISHAJI, UHUBIRI, UNABII, N.K NA WENGINE HUPEWA YOTE KWA JINSI MUNGU ALIVYOAMUA. LAKINI SISI KAMA BINADAMU TUNAWAKOSOA NA KUTOA CHANGAMOTO WAKATI MWINGINE KIMAKOSA BILA KUJUA KWAMBA MUNGU ANAWATUMIA HAWA WATUMISHI KWA JINSI ALIVYOAMUA.

 13. Nimesoma nakala yako na nashukuru Mungu kuwa bado kuna watu katika nchi yetu wenye macho ya rohoni wanaona matatizo ya “Kanisa” Tanzania. Kama utatumia vigezo halisi vya neno la Mungu kazi nyingi tunazoziona sasa hizi nchini mwetu hazina kabisa mkono wa Mungu! Watu wamekuwa wakitafuta mafanikio na baraka kuliko kumtafuta “Mtoa Baraka” wengi wamekuwa wakitafuta uponyaji “Kuliko kujisalimisha kwa “Mponyaji” Ishara na miujiza imekuwa kama alama ya uwepo wa Mungu!Ndio maana Mtume au Nabii akisema wokovu si kitu, bali “Power” bado maelfu watamiminika kama wamfuatao mpiga filimbi wa hamelini.Mtu Paulo alisema wazi, kama mtu atawahubiria “Yesu” mwingine “Injili” nyingine na hata mkipokea “Roho” nyingine ……!! taratibu pasipo wengi manabii na mitume wengi leo wanachohubiri si kile kilichoko katika maandiko! Hakikuhubiriwa na Yesu wala Paulo haya Mitume wengine! Mwandishi mmoja alisema kwamba ni rahisi sana kukemea mafundisho potofu nje ya kanisa, lakini ndani ya kanisa ni vigumu mno! Mara utasikia usihukumu! Usimnenee mpaka mafuta wa Bwana! Lakini je ndivyo yanenavyo maandiko!
  Yesu alifanya nini juu ya mafundisho ya uongo? Paulo je? Kama alidiriki kumkemea Petro alipoona haendi sawa na Injili ya Kristo sembuse sisi!
  Wale waberoya hawakupokea na kumeza mafundisho mazima mazima toka kwa Paulo, waliketi wakayachunguza! wakaona kama yanaendana sawa na “Neno” hai la Mungu, na Biblia ikawaita Waungwana! Hebu ndugu zangu tusimeze kila kitu maadamu kinatoka kwa “Mtenda miujiza” “Mtume” au “Nabii” Bwana Yesu aliisha tuonya siku nyingi. Mwandishi mashuhuri Tozer anasema ” Si dhambi kutilia shaka mafundisho yoyote yanayokuja mbele yako, lakini ni hatari ya kufisha kuamini na kumeza kila fundisho linajitokeza mbele yako”
  Bwana na Awabariki!

 14. Ndugu Anna Mango,

  Ni kweli tunafundishwa kuonyana kwa upendo na kuangalia boriti zetu kabla ya kunyooshea wengine kwa kuwa kipimo tunachopimia wengine hicho hicho kitatumiwa kwetu pia.

  Sibishani nawe, naomba unielewe,lakini nataka kuongeza tu changamoto ili tuzidi kutafakari.

  Neno linalotufundisha tuonyane kwa upole ndilo hilo hilo linatufundisha Kukemea inapolazimika. Kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwa na full package ya Neno la Mungu wakati wote ili kuepuka kuelemea upande mmoja.

  Ninakubaliana nawe kabisa kwamba kama kuna ujasiri wa kuwaambia live ni heri kufanya hivyo. Lakini inawezekana mtu mwingine akasoma hapa na isiwe rahisi kwake kufika Dar es Salaam au Tanzania kwa ujumla kwa ajili ya kupeleka ujumbe wake. Lakini kwa kupitia hapa anaweza kuandika, kwa upendo tu, na mtu mwingine aliye karibu na watu hao [watumishi wenye tabia zisizokuwa nzuri] akawafikishia. Ninaamini kati ya watu wanaosoma hapa yawezekana kabisa akasoma mtu mmoja kutoka huduma fulani na ambaye kama ataongozwa na roho ya upendo anaweza kuufikisha ujumbe huo kwa muhusika. Hivyo mimi siamini kwamba kuandika hapa ni kuzungumzia chini chini.

  Na ninavyofikiria mimi kuandika hapa inaweza hata ikawa ni rahisi zaidi kufikisha ujumbe kuliko kumtafuta mtumishi uso kwa uso. Ninasema hivyo kwa sababu watumishi wengi wakishafikia hali fulani, kwa maneno mengine wakiinuliwa hadi level fulani, huwa ni vigumu sana kuonekana uso kwa uso. Ili umuone unahitaji appointment ya muda mrefu sana. Na pengine kama wewe hufahamiki yawezekana usipate kabisa nafasi ya kuonana na mtumshi. Lakini ukiandika hapa yawezekana mtu wake wa karibu akasoma na akampelekea ujumbe mara moja.

  Tatizo jingine ninalolifahamu kwetu binaadamu ni kiburi. Watu wengi wakiwa katika hali ya uhitaji ili wainuliwe na Mungu kimaisha, kihuduma au namna yoyote ile huwa wako tayari kupokea ushauri na kufanyia kazi ule unaofaa. Lakini mtu huyo huyo akishainuliwa inakuwa kama yeye hahitaji tena ushauri wa binaadamu mwingine. Huwa tuna tabia ya kusahau tulikotoka na kudhania tumefikia level fulani kwa nguvu zetu. Ndiyo maana Mungu akawaonywa wana wa Israel katika Detronomy 8:10-18.

  Ninamfahamu ndugu mmoja ambaye alikwenda kumshauri mtumishi fulani ambaye yeye injili yake ni kuombea watu wapone magonjwa tu pasipo kuwahubiria habari ya toba iletayo wokovu ili awe na kipindi cha mafundisho ya wokovu ili ambao hawajampokea Yesu wapewe nafasi ya kufanya hivyo. Yale majibu kutoka kwa mtumishi huyo yalikuwa ya kukatisha tamaa maana yeye alisema ‘hakuna mwanadamu ye yote anayeweza kumshauri lolote’. Kwa hali ya namna hii ni vigumu mtumishi huyo [na anayefanan na huyo] kushauriwa kwa sababu ameshajipandisha sana juu.

  Hili ni tatizo letu sote. Yawezekana kuna mtu unasoma hapa na wakati huu bado uko katika hali ya uhitaji wa kuinuliwa, kwa namna yoyote ile. Ushauri wangu kwako ni kwamba Mungu atakapokuinuwa usijepoteza moyo wa unyenyekevu. Binaadamu tunategemeana. Mungu anaweza kuweka neno kwa ajili yako kinywani kwa ndugu au rafiki au mtu ye yote. Kwa hiyo moyo wa unyenyekevu na utayari unahitajika ili kushauriana na kuonyana kuweze kufanya kazi.

  Faida ninayoiona mimi ya kuweka mambo kama haya hadharani [wewe umeita ‘kunyooshea vidole] ni kwamba inaleta changamoto kwa watu ili kila mtu aweze kuwa na kiu ya kulifahau Neno la Mungu yeye binafsi, kama alivyoandika ndugu Paul maneno haya: “”Inabidi Kanisa sasa lianze kujifunza namna ya kupima roho chafu zidanganyazo na kutenda ishara za Uongo, ambazo si lazima kwamba zimetokana na Mungu…””. Kwa kuwa ni kweli kabisa si kila muujiza unatokana na Mungu.

  Ninakubaliana nawe kwamba hakuna mwanadamu aliye mkamilifu. Lakini matatizo yanatofautiana. Mgonjwa wa malaria akimuona jirani yake anakula chakula kwenye mazingira machafu akiwa ni mwenye upendo na roho njema atamtahadharisha na kumshauri asafishe mzingira yake ili asipate kipindupindu. Lakini akisema kwamba kwa sababu yeye naye anaumwa malaria kwa hiyo hawezi kumshauri jirani yake kwa habari ya kipindu pindu hiyo haitakuwa ni hekima maana atakuwa anamwangamiza ndugu yake.

  Kutokukamilika kwetu kunatupatia sababu zaidi ya kuombeana, kuonyana, kushauriana, kuelekezana na hata ikibidi kukemeana ikiwa tu kwa kufanya hivyo unaweza kumsaidia nduguyo. Na mtu anayeonywa, kushauriwa, kuelekezwa au kukemewa anatakiwa atambuwe kwamba anafanyiwa hivyo kwa nia njema ili awe katika sehemu salama.

  Upendo wa Mungu ukitufunika tutafanya yote kwa faida ya kila mmoja!

 15. wapendwa
  napenda kusema wazi kuwa tumefundishwa kuonyana kwa nyimbo na zaburi na kuangalia boriti zetu kabla ya kunyooshea wengine maana kipimo tutumiacho kwa mwingine kitatumika hichohicho kwetu.
  ninachokiona hapa ni hasira na uchungu juu ya manabii na mitume waendeshao huduma. itakuwa vema kuwafuata na kuwaeleza bayana ikiwa upo ujasiri huo kuliko kuyazungumzia kichinichini like this.

  tukumbuke pia ya kuwa waongozwao na Roho hao ndio wana wa Mungu na Mungu hutoa uwezo wa kupambanua Roho. neema ya Mungu imemwagwa kwa watu wote sambamba na uelewa na ufahamu maana Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa. cha msingi ni kuwaombea watumishi wote wa Kanisa la Bwana maana ametoa wengine kuwa Mitume na wengine Manabii, waalimu, mashemasi na wainjilisti kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu na kuujenga mwili wa Kristo, jambo lolote linalofanyika kinyume ni kuomba neema ya Mungu iwafunike maana kuwanyooshea vidole haisaidii ndio kwanza kujitia unajisi.kwa kuwa hakuna mwanadamu aliye mkamilifu basi na tusaidiane na kuombeana

  Amina

 16. Tudumu kuwaombea watumishi wa Mungu.Tukumbuke kuwa wao wako front line hivyo wanapata mashambulizi mengi sana ya Shetani.
  Tusipoteze muda mwingi kuwakosoa bali tuwaombee.Hebu mkumbukeni Petro, yeye alidhani kuwa yu imara sana kumbe alikuwa dhaifu kiasi cha kumkana Yesu.Bwana Yesu alimwombea,hakupoteza muda kumsemasema sana!
  Mungu anajua ndani yetu hakuna chochote cha kufanya makusudi yake! Ndiyo maana akasema tuisubiri ahadi ya Roho. HEBU TUWAOMBEE WAVISHWE UWEZA WA BWANA TOKA JUU! (mdo 1:8)

 17. I believe there are Prophets and Apostles in this era. I personally know one who is aired on the Emmanuel channel, he is called Prophet T. B. Joshua of the synagogue church of all nations, Lagos – Nigeria.

 18. Shallom wapendwa,

  Naomba kuuliza kwenu watumishi wa Mungu kwamba kwa dunia hii tuliyonayo sasa tunayo ngazi ya mitume na manabii? nimeuliza hivyo kwa sababu kuna mtumishi mmoja alikwishawahi kuniambia kwamba siku hizi mitume na manabii hawapo na kusema kwamba hawa waliopo kwa sasa kibiblia siyo sahihi.

  Je ni kweli? naomba mchango wa majibu kutoka kwenu.

 19. Shalom,
  Hii hoja ni pana sana na nionacho mimi wakristo wengi wanaogopa kuchangia,
  Mathayo 7:15-23 Bwana YESU anatuonya juu ya habari hizi kwa umakini sana, Tutawatumbua kwa matunda yao,
  Kwa kila Born again Christian kuna matunda ya aina mbili tunatarajia kwake 1. Tabia (character) za KIMUNGU sawasawa na Wagalatia 5:22…..tunda la Roho upendo …… na 1kor 13 :1-8 hizo ni tabia hutokana na Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu au kutuzaa mara ya pili kwa ufalme wa Mungu, 2. ni utendaji kazi wa KIMUNGU … ndio Bwana YESU alipo waambia wanafunzi Matendo 1:8 , saasa huu utendaji kazi wa Mungu kama hizi karama , huduma adui aweza kuiga kabisa kabisa hapa ni lazima kanisa lianze kuwa makini sana soma ufunuo 2:2 uone kanisa la efeso lilivyo weza kuwabaini mitume wa uongo……. maana wanaweza kuja watu wakitenda kazi kama watumishi wa Mungu lakini sio, ambacho adui hawezi kuiga ni Tabia ya KIMUNGU ndo maana BWANA YESU alisema tutawatambua kwa matunda yao……ni haki ya msingi ya member wa mwili wa kristo yaani kanisa; Biblia inatutaka tuhakikishe mambo yote na tushike lililo jema, maaana kabla hatujawapokea hawa jamaa ni lazima tuwahakikishe 1Yoh 4:1,
  vile angalia sifa za Mtumishi wa MUNGU hapa MT Paulo anaandika 1Tim 3:1-7 toa neno askofu weka Mtumishi,
  Shida yetu kwetu sisi ni kwamba utakuta tunamuona kabisa anayejiita MTUMISHI yuko nje ya upendo wa MUNGU ila kwa sababu anafanya miujiza basi tunakubali kirahisi kwamba ni mtumishi wa Mungu,

  Angalia sana mtumishi anayejiaminisha YEYE badala ya neno la MUNGU
  Mtume mmoja nilimuangalia kwenye luninga alinipa shida sana kuhusu maono yake. Katika kuelezea maono yake alisema maneno yautayo, nanukuu ” Mbingu zikafunguka nikasikia sauti ikisema njoo hata huku” …[kwa wanaojua Biblia inatoka ufunuo 4:1] … akaendelea “nikaona ngazi ikishuka” [ hii inatokana Mwanzo pale Yakobo alipolala Bethel akaota ngazi ndefu ikipanda kutoka juu mpaka chini] ..halafu akaendelea… “malaika akaja akaniambia Wewe mtu upendwaye sana” …[hii inatoka daniel 9]. Sasa pima mwenyewe ushuhuda huu

  Tutawatambua kwa matunda yao na siyo shuhuda zao, kama hawafundishi upendo na kuweka msingi mkuu kwenye utakatifu inabidi tuwaogope!

  Inabidi Kanisa sasa lianze kujifunza namna ya kupima roho chafu zidanganyazo na kutenda ishara za Uongo, ambazo si lazima kwamba zimetokana na Mungu….
  MUNGU awabariki sana naishia hapa kwa leo.

 20. Shallom!!

  Ndugu tumeipata hoja uitoayo katika bidii yako ya kulitahadharisha kanisa lake Mungu ambako KRISTO YESU ndie kichwa. Angalizo ulitoalo….” nafikiri binafsi hili ni angalizo na sio shutuma”, ni jema na la kujenga ambapo jamii ya watoto wa Mungu katika uso huu wa dunia la paswa kulifanyia kazi.

  Watakatifu lazima watambue hizi nyakati na wakati tulionao sasa na ni nini kusudi la Mungu Muumba tangu mwanzo hata ufikapo mwisho wa dahari. Tangu mwanzo wa kanisa hata mwisho wake yatokanayo yote yapo chini ya mamlaka Mungu mwenyewe alichokikusudia ndicho kinachokua.

  Hawa ndugu wanasema ni watumishi wa Mungu kwa nafasi zao, wametumwa kuwatumikia watakatifu wake Mungu, hivyo tuseme KAZI hiyo ni yake Mungu

  Kwa kweli ni ngumu sana tena sana kuifahamu na kuielewa kazi zake Mungu isipokuwa mtu kafunuliwa sawasawa na Alivyopenda Mungu mwenyewe maana tu kazi yake Mwenyewe.

  La msingi tuombeane kwa kadri tunavyo shirikishwa naye Baba, huwezi kujua hao watumishi wamekutana na Mungu wapi na wametumwa nini……. nafsi zao mbele zake ni zipi?

  Ni vizuri pia kama unauhakika juu ya Muongozo wowote ulionao kwa mpakwa mafuta ni hekima umtafute na kumshirikisha.

  Siri ya Kristo ni KUU…… twaweza kusema mengi lakini Baba awajua walio wake toka mwanzo habahatishi siku ile itajulikana.

 21. Kweli kaka nakuunga mkono kwa hoja zako, siku hizi tunashindwa kutuelewe yupi lakini ashukuliwe Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu tunawatambua watumishi wa kweli na tunawaombea.

  Kwa ufupi watumishi wengi ni waganga njaa na hawana hata chembe ya unyenyekevu!

 22. Shalom,
  Kuhusu hawa watumishi nashauri tuwaombee ili Mungu awasaidie kusimama katika nafasi zao za kiutumishi.

  Pia na sisi wapendwa tuwe makini kusoma neno la Kristo, wapendwa wengi wanakimbilia upako, sijui kupewa unabii n.k. Wengi pia wanapenda injili za mafanikio kuliko utakatifu. Biblia imeshatamka tufanikiwe kama vile roho zetu zifanikiwavyo.(3 john 1:2).

  Pia tusipende malumbano, ikiwa kiongozi wako (mfano; mchungaji,nabii, mtume n.k.) akimsema mtumishi mwingine, usifurahie wala kukubaliana na jambo kama hilo. Sana sana mwombee rehema kwa Mungu.

  Pia nasi humu kwenye hii blog nawashauri tusiyataje majina ya watumishi “live”, binafsi naona haipendezi. Hata Yesu wakati akimkemea Petro hakusema “wewe Petro…… ila alisema “rudi nyuma yangu shetani”…….

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s