Tunamuhubiri Bwana Yesu!

Utukufu kwa Bwana Yesu! suala la mijadala, maswali na mada zote tunazoziweka hapa vinavyohusiana na suala la IMANI KATIKA YESU KRISTO, ni kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo ili kuweza kumsaidia mtu ambaye ameokoka lakini hakuwa na ufahamu wa jambo fulani na yule ambaye alikuwa hajaokoka aweze kumfahamu na kumpokea Yesu. Tunaamini katika michango inayotolewa hapa yako mengi ya kujenga na wengi wamesaidika. Tunaamini pia kwamba kati ya wanaotoa michango hapa wengine ni watumishi wa Mungu [wachungaji, wainjilisti, manabii, mitume, waalimu n.k] ambao wana uhakika na wamethibitisha yale wanayoyasema ya kuwa hayo ndiyo kweli ya Neno la Mungu. Lakini pia wapo wengine ambao wamekutana na Yesu Kristo katika maisha yao na wanachoandika hapa ni uzoefu halisi ambao hauhitaji mjadala ili kuutetea kwamba wanachoandika ni kweli. Kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba kila mtu anayechangia kwa msukumo wa ROHO NJEMA iliyoko ndani yake mchango wake si bure. Maana yuko shambani mwa Bwana Mungu akiitenda kazi.

Michango inayotolewa hapa kwa nia ya kuujenga mwili wa Kristo mingi ina maneno mazuri ambayo yakizingatiwa yanaweza kumsaidia mtu kuweza kuimarika katika wokovu wake na kuwa balozi na shahidi mzuri wa Bwana wetu Yesu Kristo katika ulimwengu, ambalo pia ni kusudi la Yesu Kristo. [Matendo 1:8]; Na yule ambaye hajaokoka aweze kuufahamu ukweli wa Injili na kuokoka.

Pamoja na michango inayotolewa hapa wapo wachangiaji wengine ambao michango yao haiko katika kusudi la blog hii na kibaya zaidi haiko hata katika kusudi la Injili ya Yesu Kristo. Wapo wanaoleta michango yao kueleza kwamba ni vizuri watu wajadili mambo ya maendeleo kama vile kuanzisha miradi fulani, au kufundishana mbinu za kujikomboa kutoka katika umasikini, wakidai kwamba kujadili mambo yasiyoleta maendeleo ya kiuchumi ni kupoteza muda. Michango ya namna hii huwa hatuiruhusu hapa [labda kama imetolewa chini ya mada inayohusiana na mambo hayo na yakipimwa na Neno la Mungu (Biblia)] kwa sababu zipo blog na mitandano mingine mingi sana inayozungumzia mambo ya mwilini, ni mingi mno! Hivyo kama mtu ana msukumo wa kusaidia mwili zaidi kuliko roho tunamshauri kutoa maoni yake kwenye blog zinazohusiana na mambo hayo. Wapo pia ambao katika michango yao hutumia lugha chafu ambayo haiwapasi wana wa Mungu kuitumia. Michango ya namna hii pia hatuwezi kuirihusu hapa.

Kwa hiyo mtu ambaye alituma mchango wake katika mada yoyote lakini hakuuona ukitokea basi aelewe kwamba mchango wake haukuwa ndani ya kusudi la blog hii.

Kwa maneno hayo machache tunakuomba ndugu msomaji unapochangia hakikisha mchango wako una lengo la kujenga. Hata kama ni swali hakikisha ni la kujenga ambalo likijibiwa majibu yake yanaweza kumsaidia mtu katika kuukulia wokovu.

Mungu azidi kukubariki unapoendelea kutembelea blog hii na kuchangia michango mbali mbali yenye kuujenga mwili wa Kristo.Amen!

4 thoughts on “Tunamuhubiri Bwana Yesu!

 1. Just  curious ; Heading mliyoiweka chini ya column ya “Recent Comments” imeandikwa : MTILILIKO au mlikuwa mnamaanisha MTIRIRIKO?

  Mbarikiwe!

 2. Ndugu Joel WM,

  Bwana Yesu afisiwe!

  Ushauri wako ni mzuri sana. Hata hivyo huo utaratibu wa kuwasiliana na watu ambao wanatuma maoni/michango yao ambavyo havikubaliki kutokana malengo ya blog upo. Kilichoandikwa kwenye mada hapo juu kuhusu mtu aliyetuma ujumbe halafu asiuone kilikuwa ni kwa ujumla. Lakini pia huwa kuna matatizo ya kiufundi ambapo maoni/hoja hufutika hata kabla havijasomwa; na haya hayaepukiki. Ikishatokea hivyo hata anuani ya email ya mtu aliyetuma ujumbe huo nayo hupotea na hivyo kuwa haiwezekani tena kuwasiliana naye.

  Tatizo jingine lililopo ni baadhi ya wachangiaji kuandika kwa kutumia anuani za email zisizo sahihi/feki. Tunapokuwa tukitaka kuwasiliana na mtu aliyetumia anuani feki huwa tunashindwa kwa kuwa anuani feki hazitambuliwi na mtandao. Tunashauri basi kila mtu unapochangia uhakikishe anuani ya email unayotumia ni halisi.

  Tunakuomba ndugu Joel umfikishie ujumbe huu huyo ndugu aliyetuma lakini hakuona mchango wake na hakupata maelezo yoyote kwamba anaweza kuandaa na kutuma tena. Asikate tamaa na wala asiwe na maswali yasiyo na majibu. Blog hii iko wazi kwa watu wote.

  Ushauri tunaotoa kwa msomaji ni kwamba kama imetokea mtu ulituma maoni yako halafu hayakuonekana kwenye blog na hujapata maelezo yoyote kwa nini maoni hayo hayakutoka tunakusihi, kwa upendo, kuchukuwa hatua ya kutuma tena ikiwezekana unaongeza na maneno kwamba ulishatuma maoni hayo. Hii itatusaidia kupata tena maoni ambayo yalifutika kutokana na matatizo ya kiufundi lakini pia kutukumbusha kama kuna mtu alituma maoni yake ambayo hayakukubaliwa halafu tukawa hatukuwasiliana naye kwa ajili ya ufafanuzi ili tuweze kufanya hivyo.

  Kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo hutokea na kisha maoni na michango kufutika tunakuomba ndugu msomaji kama umeandaa mchango wako na kuutuma kwenye blog ni vema ukauhifadhi kwanza hadi utakapoona umetokea kwenya blog. Hii itaepusha kupoteza maoni yako mazuri ambayo mengine yanachukuwa muda mwingi kuyaandaa na pia pengine si rahisi kuyakumbuka yote na kuokoa muda wa kurudia kuandaa kama italazimika kufanya hivyo.

  Hakuna upendeleo kwa msomaji wala mchangiaji ye yote. Kila mchangiaji ana haki sawa na mwingine. Kwa hiyo wote tushirikiane katika kuhakikisha maoni na michango yetu inaonekana kwenye blog kwa kuandika michango mizuri na ikiwezekana kurudia kutuma tena mchango wako ambao ulikuwa umeutuma lakini haukuonekana na hukuwa umepata ufafanuzi wowote. Lakini jitihada za Strictly Gospel ni kuwasiliana na kila mtu ambaye alituma mchango wake lakini kwa namna moja au nyingine ukawa nje na malengo ya blog ili aweze kutambuwa tatizo lilipo na kurekebisha mchango wake.

  Strictly Gospel tunaamini kila mtu anaweza kuchangia mchango ambao ni wa manufaa. Iwe ni kuuliza swali; kujibu swali; kufundisha; kueleza jinsi mtu anayofahamu kuhusu jambo husika nk. Tunaposhiriki katika kutoa michango ndivyo tunavyoongeza wigo wa kujifunza.

  Mungu azidi kukubariki unapoendelea kutembelea blog hii na kuchangia michango mbali mbali yenye kuujenga mwili wa Kristo. Amen!

 3. Nashauri, kama mkiona vema, kuwasiliana na wanaotuma mada za kiroho lakini mkaona hazipaswi kutolewa katika blogu, mkiwafafanulia ni kwa vipi wameenda nje ya malengo ya blogu. Hiyo itasaidia siku nyingine wasitoke nje ya mstari. Vinginevyo, wanaweza kubaki na maswali na kukata tamaa ya kutuma mada huku. Mimi ninamfahamu mmoja ambaye alituma na hajaona mada yake kutoka, na mpaka sasa hajajua kama haina sifa za kutoka katika blogu hii au la.

  Mbarikiwe.

 4. Asante sana kwa kazi nzuri, binafsi nimebarikiwa sana na blog hii, nimejifunza mengi ya kunikuza ktk safari yangu ya wokovu. Bado mgeni na bado mchanga ktk wokovu ninashukuru kuwa mnaipitia na kusahihisha michango yetu, asante.
  Ni kweli nadhani mambo mengine ambayo si ya kuujenga mwili wa Kristo yasiwekwe hapa kwani itakuwa vigumu kudhibiti nidhamu vitu vitakuwa vingi sana. Tunaweza kujiunga kwenye blogs au forum nyingine zenye mambo tunayohitaji kama elimu, biashara nk zipo nyingi tu.
  Mungu wetu azidi kuwabiriki na kuwatia nguvu ktk kazi yenu hii ninawaombea ktk Jina la Yesu.Amen.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s