Mwaka Mpya ni Roho??

Ndugu zangu katika Kristo kwa mara nyingine Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali tuutazame mwaka mpya kwa jicho la tofauti ili kuzijenga nafsi zetu kisha kumrudishia sifa Mungu Baba kupitia kwa Mwana wake wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu aliye ndani yetu atushuhudiaye mambo yote sawasawa na Yeye apendavyo kwa majira haya. Huwa ni mazoea kusheherekea kuingia kwa mwaka mpya lakini leo imempendeza Bwana Yesu Kristo tufungue macho yetu tujadili kwa pamoja nini hasa maana ya mwaka mpya. Uumbaji wa Mungu ulifanyika kwa namna mbili, namna ya rohoni na kwa namna ya mwilini. Namna ya rohoni ni ya uumbaji wa ulimwengu wa roho na namna ya mwilini ni uumbaji wa ulimwengu wa mwili. Hivyo kuna vitu vya ulimwengu wa roho na viumbe vya ulimwengu wa roho vile vile kuna vitu vya ulimwengu wa mwili na viumbe vya ulimwengu wa mwili. Basi kwa mtazamo huo mwaka mpya unagawanyika katika namna mbili, naam namna ya mwilini na namna ya rohoni.

Wakati wa uumbaji Bwana Yesu Kristo, alipewa maelekezo ya kufanya mianga ili iwe dalili za majira na siku na miaka. Mwanzo 1: 14 – 15 MUNGU [BABA] AKASEMA, NA IWE MIANGA KATIKA ANGA LA MBINGU ILI ITENGE KATI YA MCHANA NA USIKU; NAYO IWE NDIYO DALILI NA MAJIRA NA SIKU NA MIAKA; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Na Bwana wetu Yesu Kristo aliyefanya vyote wala pasipo Yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika akayachukua yale maagizo ya Mungu Baba na kuifanya mianga katika anga. Mwanzo 1: 16 – 17 MUNGU [MWANA, BWANA WETU YESU KRISTO] AKAIFANYA MIANGA MIWILI MIKUBWA, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi… Hivyo mianga iliumbwa ili kutia nuru lakini zaidi ya hapo iliumbwa ili kutenga siku, dalili, majira na miaka. Ukitazama kwa wepesi mianga ni vitu vya mwilini lakini vimepawa uwezo wa kutenga siku, dalili, majira na miaka ndio maana wanajimu (‘astrologers’) kwa uwezo wa kipepo wanaweza kutazama mianga ambayo ni vitu vya mwili vilivyo angani na kubashiri siku, dalili, majira na miaka. Hivyo mianga iliyoumbwa imepewa uwezo wa kutenga mchana na usiku, kutenga dalili, kutenga majira na kutenga miaka juu ya viumbe vilivyo ulimwenguni. Viumbe vilivyo ulimwenguni vipo vya namna mbili, viumbe vya rohoni na viumbe vya mwilini.

Sisi wanadamu tupo pande zote mbili maana tuna roho ambazo ni viumbe vya rohoni na tuna miili ambayo ni viumbe vya mwilini. Hivyo mianga iliyoumbwa inatuathiri kwa namna mbili, inatuathiri kwa namna ya mwilini na vile vile inatuathiri kwa namna ya rohoni. Inatuathiri kwa na mna ya mwilini kwa kuwa hiyo ndiyo inayotutengea mchana na usiku na pale mchana unapoingia mwili huathirika maana inapasa kuamka na kutoka ndani kwa shughuli za kawaida wakati usiku unapoingia mwili huathirika maana inapasa kuingia ndani na kupumzisha miili kwa kulala. Athari za mwilini haziishii hapo maana siku moja  na nyingine hutengwa na hiyo mianga na vile vile mianga hiyo hutenga majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi … (Mwanzo 8: 22). Hii mianga huathiri viumbe vilivyo ulimwenguni kwa namna ya rohoni maana roho zipo ndani ya miili na miili inapoathirika kwa njia moja au nyingine roho nazo huathirika. Mafano miili inapokuwa na shughuli nyingi roho zinakuwa na uwezo mdogo wa kufanya mambo yake hasa zile roho changa na pale miili inapopumzika roho zinakuwa na uwezo mkubwa hata kusikilizana na Mungu wakati wa usiku mtu alalapo kitandika katika usingizi mzito. Ayubu 33: 14 – 16 KWA KUWA MUNGU HUNENA mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali (naam hajasikia kutokana na kusongwa na shughuli za mchana) KATIKA NDOTO, KATIKA MAONO YA USIKU, USINGIZI MZITO UWAJILIAPO WATU, KATIKA USINGIZI KITANDANI; NDIPO HUYAFUNUA MASIKIO YA WATU NA KUYATIA MUHURI MAFUNDISHO YAO. vile vile mianga huathiri viumbe wa rohoni kwa kuwa katika siku, majira na mwaka kuna makusudio fulani ambayo yamepangwa na Mungu kutokea ulimwenguni, hivyo pale mianga inapotenga siku majira na mwaka hutenga mambo ya rohoni yaliyokusudiwa kutendeka Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.

Katika ulimwengu wa roho ili jambo litendeke huwa kuna nguvu ya rohoni maalumu huachiliwa ili kutimiliza jambo husika. Nguvu hizo zinaweza kuwa zimetoka kwa Mungu juu mbinguni au zinaweza kuwa zimetoka kwa Shetani chini ya nchi. Shetani na malaika zake ni viumbe wa rohoni na walipotupwa makao yao makuu ni chini ya nchi Ufunuo 5: 3 WALA HAPAKUWA NA MTU MBINGUNI, WALA JUU YA NCHI, WALA CHINI YA NCHI (wakaapo Shetani na malaika zake), aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nguvu zinazotoka juu mbinguni zinaweza kuwa nguvu za Roho Mtakatifu au nguvu za malaika watakatifu na nguvu zinazotoka chini ya nchi ni nguvu za malaika wa Shetani (mapepo). Katika kila majira na mwaka kuna nguvu maalumu inaruhusiwa na Mungu kuingia ulimwenguni na kufanikiwa katika mambo yake. Inawezekana nguvu fulani ikawepo kwa muda kitambo lakini isifanikiwe katika mambo yake ila katika mwaka fualni itapewa kibali cha kufanikiwa ili kutimiza makusudi ya Mungu juu ya nchi katika majira hayo, naam katika mwaka huo. Hivyo watu tumekuwa na shahuku kuuona mwaka mpya kwa kuwa ndani ya mioyo yetu ipo tafsiri isiyotafsirka katika utashi wetu kuwa yapo mabadiliko katika mwaka ujao japo hatuyafahamu. Watu tunasheherekea kuuona mwaka tukiwa na shauku kwa kupanga malengo ya mwaka mpya bila kufahamu kuwa ipo nguvu ya rohoni iliyokwisha kupangwa juu yetu katika mwaka huo, mpya. Vile vile wengine hushindwa kuuona mwaka mpya kwa kuwa makusudi ya rohoni ya mwaka huo hayawahusu
hao hata wakazimishwa ili wasiingie huko.

HAKIKA MWAKA MPYA NI ROHO KAMILI

–Elineema Kavuta

Advertisements

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s