Kikombe cha `Babu` chazidi kupoteza umaarufu

  Wabunge wataka kipigwe `stop`

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, wameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kumfungia Mchungaji Ambilikile Masapila ‘Babu’, kutoa huduma kwa madai kwamba, amekuwa akisababisha vifo vingi tangu alipotangaza dawa yake.

Ushauri huo ulitolewa na wajumbe hao jijini Dar es Salaam, wakati kamati hiyo ilipotembelea TFDA, ambako walitumia fursa hiyo kujionea utendaji kazi wa maabara pamoja na maeneo mengine muhimu ya mamlaka hiyo.

Walidai ‘Babu’ alipotangaza kutibu magonjwa sugu matano, kikiwamo kisukari na Ukimwi, wagonjwa wengi walishawishika na kutoka hospitalini kwenda kupata kikombe chake.

Walisema matokeo yake vifo vingi vimetokea, hivyo wakaihoji TFDA sababu ya kutomsimamisha ‘Babu’ kuendelea kutoa huduma yake.

Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge

wa Chaani (CCM), Ali Juma Haji, ambaye alisema ‘Babu’ amekuwa akiwaumiza watu, hivyo akashauri kusimamishwa kwa huduma yake ili kuondokana na tatizo hilo.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zarina Madabida.

Alisema ‘Babu’ alitangaza kutibu magonjwa makubwa na dunia nzima ilishamjua anayatibu, lakini tayari watu wengi wamekwishakufa kwa kuacha dawa za hospitali.

Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vipodozi, Mitangu Fimbo, alisema TFDA haitoi vibali vya dawa kama anazotumia ‘Babu’ kutibu.

Fimbo alisema vibali vya dawa za aina hiyo hutolewa na Baraza la Dawa Asilia.

Alisema kazi ya kumchunguza ‘Babu’ hadi kusimamishwa inaweza kuchukua mwaka mmoja.

Fimbo alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini tatizo hilo na kwamba, katika uchunguzi huo wanashirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia.

Alisema utafiti huo unasimamiwa na NIMR na kwamba, utakapokamilika, majibu yatatolewa na wananchi watapewa taarifa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margareth Sitta, alisema kuna haja kwa Serikali kuendelea kuwekeza katika masuala yanayohusu maabara, kwani ni sehemu muhimu.

Alisema maslahi ya wafanyakazi katika maabara ya TFDA, yanatakiwa kuboreshwa na kusema usalama wao sio mzuri kiafya kwa kuwa wanapokea harufu tofauti katika kazi ya uchunguzi.

Aliwataka wananchi kuacha kuingiza dawa kwa njia za panya kwani hali hiyo ni hatari kwa afya.

Sitta, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, alisema dawa hizo hazina kiwango cha ubora unaotakiwa na matokeo yake ni madhara kwa binadamu.

Mkurugenzi wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni wananchi kutokuwa na uelewa juu ya matumizi ya dawa, ambazo zina viwango kwani wengi wao wamekuwa wakijinunulia dawa katika maeneo yasiyohusika.

—IPP

Advertisements

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s