Kumcha Mungu kuna faida

Malaki 3: 13-18

13Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno magumu juu yako kwa namna gani? 14Mmesema; Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za BWANA wa majeshi? 15Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao maovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. 16Ndipo walio mcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake. 17Nao watakuwa wangu, asema BWANA wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; watakuwa hazina yangu hasa; naami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye. 18Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia”

Kuna watu, na pengine nawe ni mmoja wao, ambaye baada ya kukaa katika maisha ya kumtafuta Mungu na kuona hapati alichotarajia, hugeuka na kuanza kulalamika. Hulalamika kwa kuona kama amejitaabisha bure katika kujiepusha na uovu wa dunia hii. Huona kama amejizuwia kutenda maovu pasipo kuwa na faida. Anaweza hata kushawishika anapowaona watu wakifurahia dhambi akajiona yeye anaishi maisha ya huzuni pasipo na sababu [ingawa kumcha Bwana ni furaha kubwa].

Pengine mtu amekuwa akifunga na kuomba ili jambo fulani litokee. Na kinyume chake akawaona wale ambao hata jina la Yesu halijawahi kutamkwa vinywani mwao ndio wanaofanikiwa. Ndio wanaojenga majumba makubwa, na wengine kuyaita kwa majina yao; akaona wale wanaotoa rushwa maofisini ndio wanaoongezewa mishahara na kupandishwa vyeo, huku yeye akiwa ameishikilia haki, yuko katika nafasi ile ile.

Yawezekana kuna mtu amekuwa anasumbuliwa na ugonjwa fulani kwa muda mrefu, ameomba sana lakini ugonjwa huondoki. Halafu akiangalia upande wa pili anaona kuna mtu ambaye alikwenda mara moja tu kwenye maombezi kisha akapona; na baada ya kupona mtu huyo alirudi tena dhambini, yaani kupona kwake ndio kumempa nguvu zaidi ya kutenda maovu. [3:15]Huyo aliyekuwa anamjaribu Mungu ndiye amepona halafu yeye bado anaumwa!

Sikiliza Neno la Mungu lisemavyo katika ule mstari wa 16 “Ndipo walio mcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake”

Jambo muhimu kulifahamu hapa ni kitu  walichosemezana wao kwa wao, hao wamchao BWANA. Lakini bila shaka hao wamchao Bwana walisemezana juu ya ukuu wa Mungu! Walifarijiana na kutiana moyo kuwa japo wanapita katika mapito bado BWANA Mungu ndiye nguvu yao. Walifarijiana kwamba hata kama walichofunga na kukifanyia maombi hakikutokea bado BWANA Mungu ni tumaini lao!

Ni kama tu walivyosemezana akina Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa hata kama BWANA Mungu asipowaokoa katika lile tanuru la Moto lakini wao hawakuwa tayari kuisujudia ile sanamu ambayo mfalme Nebukadreza aliyokuwa ameisimamisha! [Daniel 3].

Wamchao waliposemezana BWANA alisikiliza na akasikia wakiongea maneno yenye kuelekeza kwake tumaini lao lote. Baada ya BWANA kusikia maneno hayo pale pale kitabu cha ukumbusho kiliandikwa mbele zake wa ajili yao kwa kuwa walisemezana maneno mema huku waliendelea kulitafakari jina lake!

Tusidanganyike! Kumtumikia BWANA Mungu kuna faida. Kuokoka kuna faida. Waache wanaofanikiwa kwa njia za ufisadi wafanikiwe. Waache wanaochekelea katika furaha ya dhambi, ambayo ni ya kitambo kidogo sana, waendelee[Ebrania 11:25]. Waache wanaojiunga katika imani potofu kwa ahadi za utajiri waendelee, maana siku itakapofika utajiri huo hautakuwa na msaada wowote kwao. Waache wanaotafuta uponyaji kwa njia zisizo za ki-Mungu waendelee maana iko siku ambayo itakuwa kama vile magonjwa hayo yamerudi yote kwa wakati mmoja!

Lakini pia iko siku BWANA ataondoa tabu yako. Pengine ameacha shida, ugonjwa au adui huyo aendelee kukusumbua kwa kusudi akufundishe jambo. Pengine ameacha ili akujaribu moyo wako umeweka wapi msingi. Pengine ameacha ili akujaribu unataka mema tu toka kwake au hata mabaya? [Ayubu 1:10]. Yawezekana ameacha ili akuone kama uko tayari kufa kwa ugonjwa huku bado sifa zake zikitoka kinywani mwako na wala hautamkufuru. Pengine amaecha hayo ili uendelee kunyenyekea. [2Kor 12:7]. Pengine ameacha hayo ili akutukuze, akufanye mfano wa Ayubu, ili uwe mfano wa kuigwa katika vizazi na vizazi!

Hebu tuendelee kumtumaini BWANA Mungu. Tuendelee kumuisha yeye. Tuendele kujitia nguvu katika yeye. Tunapokutana tusemezane maneno ya Neema hii aliyotupatia, Neema ya Wokovu. Tunapokuata tuliitie jina lake. Hapo ndipo tutaweka rekodi mbinguni! Loh! Ni fahari iliyoje mcha Mungu kuongea huku duniani kisha mambo hayo yakaandikwa mbinguni!

Kumcha BWANA kuna faida! Tudumu katika hilo kwa kuwa katika siku ile tutakuja kutambulika kama tulikuwa tunamcha BWANA Mungu, kama kweli tutadumu katika kumcha Yeye! Na hapo ndipo kutakuwa na malipo kwa wenye haki, Uzima wa milele na waovu, adhabu ya milele!

Mungu atusaidie!

Advertisements

22 thoughts on “Kumcha Mungu kuna faida

 1. Bwana Yesu asifiwe wapendwa Wangu hakika nimejaribu kufuatilia mada hii nimebarikiwa nimepata maarifa nyingi sana hapa Mimi nafikiri Ndugu Kassim umkubali Yesu Kristo akawe Bwana na Mwokozi wa maisha yako lakini kama utakubali hili neno litimie ndani yako hakika litatimia 2Wathesalonike 2:10-12
  watumishi wa Mungu mliojaribu kumuelewesha huyu ndugu mwacheni kabisa Biblia inasema mzifungiwe nira na wasioamini angalie kuna elimu zingine zinatia najisi masikioni

 2. Ndg Orbi..ukisoma maandiko ya Ndg Albert na kuyatafakari utagundua kitu

  Nanukuu
  ‘Umejaribu kuelezea swala la kumcha Mungu kwa kuangalia biblia inasema nini kwa kuzingatia historia ya maisha ya watu fulani iliyoelezwa katika biblia”.

  “kitabu chochote kinachofuatwa na waumini wanaojali utu, hicho ni kitakatifu. Vilevile, wazo lolote linalojali utu, linalofanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi”

  Ndg Orbi, Ni roho…inataka kutuhubiria injili ya imani ambazo binadamu wamejitengenezea, roho hii mara nyingi ujiona kuwa inajiweza, Hawamtegemei Mungu(JEHOVA) na badala yake ujiona bora na kiburi. Wanaamini mambo kwa uwezo wao mwenyewe.Biblia kwao ni historia inayozungumzia watu fulani. Wao kitabu chao kinazungumzia Haki za Binadamu,kwa mfano ndoa za jinsia moja,Dunia kuwa sehemu salama ya kuishi na vitu vinavyofanana na hivyo,uko ndio kujali utu,Na ndio utakatifu na si rahisi kukileta hapa, kuna bwana alipita hapa na injili yake alipoambiwa alete kitabu cha injili yake akuonekana tena mpaka leo.Habari ya Ufalme wa Mbinguni na kuzaliwa mara ya pili(wokovu) ni upuuzi kwao,Ndipo pale Bwana alinena usimtupia Lulu nguruwe…….
  Tofauti nyingine wao maskani yao ni hii(Dunia/Mwili)inayoharibika,Wakati sisi(Waokovu) tuna amini kuwa maskani hii ikiharibiwa tunayo maskani nyingine isiyoharibika,sis(Waokovu)i ni wageni tupitao ,Wao wamefika.
  Asante John Paul kwa kweli umeandika yote, Bwana Akuruzuku, Neema na iwe kwako na Amani iongezwe kwako katika kumjua Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo

  Orbi …..
  “Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?’
  (Ayub 38:36)

  “Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi?”(Ayub 40:2)

  Amen.

 3. Ndugu Albert Kissima,

  Naona maswali yangu unayaepuka, Naona labda nije na swali jingine…..labda yale ya awali yamekuzidi uwezo………Na swali langu ni hili; unaporudia rudia katika mjadala wako na ndugu John hasa unaposema ” Vitabu vingine VITAKATIFU vinaweza kuzingatiwa” Ni vitabu vipi hivyo? Labda tukivifahamu vitabu hivyo vinaweza kutupa maana halisi ya kumcha Mungu……….!

 4. Ndg Albert,

  Nitakujibu hoja zako kukuonyesha jinsi ZINAPINGANA na Neno la Mungu. Na hapo ndipo nilipouliza kwa kama tutapata mbadala wake kwenye Biblia utaamini kipi?

  Sasa tuangalie hoja zako na jinsi zinapingana na Neno la Mungu:

  1. Suala la Kumcha Mungu.

  Biblia inasema kuwa Kumcha Mungu ni Kuzishika Amri zake zote na Sheria zake zote, Kumpenda na Kumtumikia. Kumb 6:2; Kumb 18:19; Kumb 10:12.
  Kwa hiyo hoja yako kuwa kumcha Mungu ni TAKING CARE OF HUMAN KIND ni wazo linalopingana na maana ya Biblia ya kumcha Mungu!

  2. Sala ya TAKING CARE OF HUMAN KIND.

  Biblia inasema katika Luka 11:2-4 hivi, Akwaambia, Msalipo semeni Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani, kama huko mbinguni, Utupe siku kwa siku ridhiki yetu, Utusamehe makosa yetu kama sisi nasi tunavyowasamehe waliotukosea, Na usitutie majaribuni lakini utuokoe na yule mwovu”

  Huo ndiyo mwongozo wa KUSALI kama inavyoelekezwa katika Biblia. Kusali ni Kuongea na Mungu. Hiyo ndiyo maana ya Sala. Kwa hiyo TAKING CARE OF HUMAN KIND siyo SALA! Ni udanganyifu!
  NB: Prayer = The act of communicating with a deity (especially as a petition or in adoration or contrition or thanksgiving)

  3. Suala la wewe Kupinga Kuokoka.

  -Katika Mathayo 1:21 Biblia inasema, “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”
  -Yohana 10:9 “Mimi ndimi mlango, mtu akiingia kwa mimi ataokoka…..”
  -Luka 18:26-27 “Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Akasema Yasiyowezekana kwa wanadamu, yanawezekana kwa Mungu”

  Maandiko hayo machache hapo juu yanaonyesha kuwa kusudi la Yesu kuja duniani ni ili kuwaokoa watu kutoka katika dhambi zao. Huo ni mpango wa Mungu. Sasa huoni wewe KUKATAA kuwa kuna KUOKOKA Unapingana na Mungu?

  4. Suala la VITABU VITAKATIFU.

  Biblia inasema katika maandiko kuwa suala la Utakatifu ni la Mungu. Utakatifu asili yake ni UUNGU, yaani Utatu MTAKATIFU. Mungu Baba ni Mtakatifu. Yesu Kristo ni mtakatifu pamoja na Roho wa Mungu aliye mtakatifu! Mahali palipo na Uungu mtakatifu hapo ndipo palipo na Utakatifu. Mtu anayemcha Mungu naye ni mtakatifu. Mahali anapokaa Mungu napo ni patakatifu. Na Biblia ni takatifu kwa kuwa ni Neno la Mungu Mtakatifu.
  Luka 4:34; Luka 3:16; Ufunuo 4:8; 1Cor 3:17

  Kwa hiyo kule kusema kuwa KILA kitabu chochote kinachofuatwa na waumini wanaojali utu, hicho ni kitakatifu SI KWELI. Huo ni uongo na ukengeufu! Hata kama waumini hao watajali utu kwa kiwango gani LAKINI kama Mungu hayupo hapo, HAPO HAKUNA UTAKATIFU.

  Kwa hiyo hivyo unavyoviita ni vitabu vitakatifu unajidanganya kwa kuwa HAKUNA KITABU CHOCHOTE kilicho kitakatifu zaidi ya Biblia, kwa kuwa Biblia ndiyo Neno la Mungu, Yehova, aliye MTAKATIFU!

  5.Dunia kuwa mahali SALAMA PA KUISHI

  -Biblia, katika Isaya 24:19, inasema “Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya waya kama machela, na mzigo wa dhambi zake utailemea, nayo itaanguka na wala haitainuka tena.
  -Biblia inasema katika 1Pet 5:8, “Muwe na kiasi na kukesha kwa maana mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye huzunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze”
  -Luka 10:18-19 inasema “Akasema, nimemuona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama nimemewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitakachowadhuru”

  Kutokana na maandiko hayo tunaweza kuona kuwa DUNIA HAIWEZI KUWA MAHALI SALAMA PA KUISHI IKIWA DHAMBI BADO IPO maana shetani ataendelea kuelekeza watu katika kumuasi Mungu na kuuharibu uumbaji wa Mungu maana kazi yake shetani ni kuua, kuchinja na kuiba na kuharibu! Kwa hiyo hakuna namna ya kuifanya dunia iwe mahali salama pa kuishi ikiwa dhambi bado iko mioyoni mwa watu. Kwa hiyo ili kuifanya dunia mahali salama pa Kuishi kinachotakiwa ni Kuhubiri Injili ili watu Wamkubali Yesu aondoe dhambi.

  Siasa haiwezi kufanya dunia mahali salama pa kuishi. Sheria kali haziwezi kifanya mahali salama pa kuishi maana sheria huleta hofu. Kinachoweza kuleta usalama duniani ni watu watakapomcha Mungu!

  Sasa hebu tuone harakati ulizonazo wewe katika kuifanya dunia iwe mahali salkama pa kuishi:

  “Vilevile, wazo lolote linalojali utu, linalofanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Hilo ni takatifu, ni safi, halina doa”

  “Maneno haya nimeyapata kwa kuangalia uhusiano wangu na wanadamu wengine. Ni kwa namna gani nitaishi nao katika kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Nimeyatafakari sana maneno haya. Sijapata mwisho wake, sijapata ugungufu wake. Ni sahihi kwa mtu wa kila imani. Maneno haya yanatukumbusha namna bora ya kuishi”
  ……hapa ulikuwa unatetea TAKING CARE OF HUMAN KIND!

  Wazo linalojali UTU PASIPO KUMJALI MUNGU haliwezi kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi. Kuishi kwa kuangalia UHUSIANO WA MTU NA MTU hakuwezi kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi bali Kuishi kwa KUANGALIA UHUSIANO kati ya MTU NA MUNGU. Uhusiano SAHIHI kati ya Mtu na Mungu ndiyo huleta MWONGOZO BORA NA THABITI wa namna gani mtu AISHI KWA UHUSIANO MZURI NA MTU MWINGINE.

  Kw ahiyo harakati zako hizo ni batili maana haziko katika Mungu, bali zimejenga msingi wake JUU YA UTU na wala si JUU YA MUNGU!

  6.Maarifa, Akili na Hekima!

  Nasikitika kwa kuwa hukunielewa na kisha kwako umeoona ni jamo la kuchekesha. Hapa ninanukuu tu kile ambacho tayari nilishakiandika:

  “Na kwa sababu hiyo suala la “kufikiri” huwa halina hafasi inapotokea kuna jambo ambalo kwa akili linashindwa kupata maelezo. Ikishafikia hapo inabidi mtu ‘AAMINI’ ingawa kwa akili zake HAJAELEWA”

  “Nimeandika hayo kwa masikitiko kwa kuwa HUKUELEWA KUWA HAPA TUNAWEKA MWONGOZO WA BIBLIA MBELE. Ni blog ya Kikristo…Ni blog ya Injili….! Biblia mbele, Akili, Utashi na Maarifa ya kila mtu tunaviweka Nyuma….”

  Lakini pamoja na kuandika hivyo wewe ukajibu hivi: “Hata maandiko ya BIBLIA ili kuyatafakari na kuyafundisha yanahitaji maarifa, utashi, elimu, ibada, akili, hekima n.k.”

  Katika hilo mimi nakubaliana nawe lakini kwa lengo kuu kuwa hivyo ulivyovitaja vinatakiwa vitumike katika kulielewa Neno la Mungu na kisha kulikubali. Sasa huoni kuwa wewe unavitumia KUPINGANA NA MUNGU? Hayo si matumizi SAHIHI ya akili, ni matumizi HARAMU. Tunatakiwa kutumia mambo hayo katika kujifunza na kuelewa kile ambacho Mungu amesema na si KUPINGA KILE AMBACHO MUNGU AMESEMA kwa kudhani kuwa tunaweza badilisha jambo la Mungu kwa kutumia vitu hivyo.

  -Neno la Mungu linasema hivi katika Isaya 55:9, “Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”

  Narudia tena haya yafuatayo:

  Biblia inasema hivi: HEKIMA YA DUNIA HII NI UPUZI MBELE ZA MUNGU (1Cor 3:19)

  na kuhusu Maarifa Biblia inasema;

  KUMCHA BWANA NDICHO CHANZO CHA MAARIFA (Mithali 9:10)

  Hivyo hakuna Hekima wala Maarifa SAHIHI pasipo kumcha Mungu wa Biblia.

  Hakuna hekima sahihi ya namna ya kujali utu pasipo kumfahamu Mungu wa Biblia. Hakuna maarifa salama kwa ajili ya watu pasipo maarifa yaliyojenga msingi katika Mungu!

  Nimalizie kwa kujibu hoja zako mbili za mwisho:

  -Kuhusu maarifa ya hospitali ni kuwa kama ungekuwa unasoma kwa makini ungeshaelewa kuwa ninachozungumza ni kuwa Tunaweza kutumia akili na maarifa na hekima na chochote chema ambacho Mungu ametujalia, kwa ajili ya kuendesha maisha yetu. Lakini hatuwezi tumia vitu hivyo kwa ajili ya kumdadisi Mungu, kama ulivyosema wewe “kumchabua”. Hatuwezi kumchambua Mungu kwa akili tunayotumia kutengeneza Dawa ya Kutibu Malaria; hatuwezi kumchambua Mungu kwa akili tunayotumia Kuoka Mikate! Hatuwezi kumchambua Mungu kwa akili tunayotumia kuruka angani na kwenda mfano, mwezini. Hapana! Hatuwezi kumchambua Mungu kwa namna hiyo. Hiyo ni akili kwa maisiha yetu!

  Linapokuja suala la Mungu, ni lazima tuangalie Neno lake linasemaje na kisha tunaliamini! Hapo ndipo mioyo yetu itaungana na Uungu na kisha tutafahamu Yeye ni Nani na yeye ni Nini! Mungu anasema katika Yer 3:33 “Niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyojua”. Hakuna namna yoyote ya kutumia akili ili kumwelewa Mungu bali twahitaji KUMUAMINI na tukishafanya hivyo Yeye atatufunulia ili tuweze kumfahamu! Tunaweza kutumia AKILI zetu katika KUCHAGUA LIPI NI NENO LA MUNGU na tukilipata ndipo mengine yanaendelea!

  Suala la Galileo umeuliza hivi:

  “Wapo waliokuwa na mtizamo kama wako, walimwambia kuwa alikuwa akienda kinyume na maandiko, alimkosoa Mungu. Kwa nini basi waamini hili la Dunia kuzunguka Jua pamoja na kuwa lilikuwa ni wazo la Binadamu tuu? Kama ni mwalimu wa jografia (labda) ungekuwa unawakaririsha wanafunzi kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote na kwa uwezo wako wote dhana hii ambayo ni wazo la mtu”

  Jibu langu ni hili: Mungu ndiye aliumba kila kinachoonekana na kisichoonekana. Mungu ndiye aliumba na kuweka mfumo wa Sayari na Anga kama vilivyo leo. Dunia kuzunguka jua SI WAZO LA BINADAMU bali ni Uumbaji wa Muungu ndivyo ulivyo. Si wazo la Galileo lililofanya dunia ianze kuzunguka Jua!Yeye aligundua tu jambo ambalo tayari lilikuwa hivyo hata kabla hajakuwepo! Kwa hiyo mimi Ninaamini dunia inazunguka jua kwa kuwa ndivyo Mungu alivyoumba mfumo wa Anga na wala siamini hivyo kwa kuwa ni Galileo alisema. Na zaidi sana niamini au nisiamini, sitaweza kubadilisha kile Mungu alichoumba. Kwa hiyo hapa si suala tu la kuamini au kutokuamini bali NI ULE UHALISIA WA JAMBO husika! Hata kama Galileo naye asingegundua jambo hilo na dunia yote tukaendelea kuamini hadi leo kuwa jua ndilo linazunguka dunia, hilo nalo lisingebadilisha uumbaji huo wa dunia kulizunguka jua!

  Kadri siku zinavyoendelea maarifa ya kisayansi yanaongezeka. Mambo mengi yanaendelea kugunduliwa. Wanadamu sasa wanaweza kuona sayari au kitu katika anga kilicho umbali wa ajabu. Wanaweza kupima na kuratibu mzunguko wa sayari, jua na mwezi na hata kuweka katika table, tarehe ambazo jua litapatwa, mwezi utapatwa, na lini sayari zote zitajipanga katika mstari mmoja nk. Haya yako hivyo SI KWA SABABU YA MAWAZO YAO lakini ni kwa sababu HIVYO NDIVYO ULIVYO UUMBAJI wa ajabu wa Mungu!

  Lakini la kukumbuka hapa ni kuwa AKILI HIYO YA KUJUA mwenenendo wa sayari, jua na mwezi HAIWEZI KUTUMIKA Kufanya UTAFITI WA MUNGU NI NANI na Yuko wapi! Hakuna!.

  Hiyo ndiyo maana yangu ya kusema kuwa kwenye mambo ya Mungu Maarifa yetu, akili zetu na hekima zetu sharti zikae nyuma! Narudia tena nilipoandka hivi:

  Nimeandika hayo kwa masikitiko kwa kuwa HUKUELEWA KUWA HAPA TUNAWEKA MWONGOZO WA BIBLIA MBELE. Ni blog ya Kikristo…Ni blog ya Injili….! Biblia mbele, Akili, Utashi na Maarifa ya kila mtu tunaviweka Nyuma…

  Nasubiri kutoka kwako, MUHIMU ni katika zile HOJA ZAKO SITA (6).

  Karibu!

 5. SALAMU NDUGU ALBERT KISSIMA NIMESOMA MAANDISHI ENYE UNAPOANDIKIA NDUGU JOHN PAUL . NA MIMI NA KUULIZA KWA UPOLE SANA TUSAIDIE JUU YA MAMBO TUNAYOANDIKIANA JUU YA MCHA MUNGU INAMAANISHA NINI? UPIME KUTUSAIDIYA KAMA TUKO MBALI NA NENO LA MUNGU ? NA ZAIDI UNIONESHE KATIKA BIBLIA PALE ILIPOANDIKWA ? KAMA NIKI SOMA NENO VIZURI SISI WOTE TUNAPIGA MBIO JUU YA KUINGIYA KWENYE MULANGO MWEMBAMBA NDIO SEHEMU AMBAYO AMANI ITAKUWA YA MILELE

  UNISAIDIYE

 6. Hahahahahaha! Kwa hakika ndugu John Paul wanifurahisha sana. Hata maandiko ya BIBLIA ili kuyatafakari na kuyafundisha yanahitaji maarifa, utashi, elimu, ibada, akili, hekima n.k. watu wanashinda kutumia mapaji haya ya roho Mtakatifu na ndio maana wanatumia mistari ya biblia kuanzisha makanisa yao (ministries zao) kisha wanaanza kukashifu kule walikotoka. Hii ndio hali halisi, wala hain mjadala.

  Ndugu John Paul, naomba nikuulize swali moja. Je, unaamini katika dawa za hospitalini, kuwa unapoumwa na ukaenda kutibiwa na dokta ( ambaye mbali na kutumia maarifa yake, akili yake, utashi wake, elimu yake) na kisha ukapewa dawa ambazo zimegunduliwa na mwanadamu aliyetumia akili yake, elimu yake, utashi wake, maarifa yake? au umeshatibiwa hospitalini na ukapona? Imekuwaje hadi ukawaamini madaktari hawa kama umeshawahi kutibiwa nao?

  Achana na hilo la madaktari, bila shaka unaaamini/unafahamu kuwa Dunia inalizunguka jua na inazunguka katika mhimili wake. Miaka mingi iliyopita, watu walikuwa na ufahamu tofauti. walikuwa wakijua kuwa Jua ndio linazunguka na Dunia iko stationery. ndugu Galileo Galilei alikuja na wazo tofauti. aliushawishi ulimwengu kuwa sio Jua linalozunguka bali dunia, jua lipo stationery. alifanikiwa kuushawishi ulimwengu, watu walikubali na ndio maana hata sasa wewe unatambua hivyo. Waspo w3aliokuwa na mtizamo kama wako, walimwambia kuwa alikuwa akienda kinyume na maandiko, alimkosoa Mungu. Kwa nini basi waamini hili la Dunia kuzunguka Jua pamoja na kuwa lilikuwa ni wazo la Binadamu tuu? Kama ni mwalimu wa jografia (labda) ungekuwa unawakaririsha wanafunzi kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote na kwa uwezo wako wote dhana hii ambayo ni wazo la mtu.

  Ni ukweli ulio wazi kuwa Ndugu yangu John Paul unataka kufunga mjadala. Ni vyema kama ungejadili kwa hoja kuliko kuweka vitisho. Ingekuwa vizuri sana kama ungejitetea kwa kutumia upande wako na si kuweka vikwazo. Leta hivyo vinyume katika Biblia halafu tuvijadli. kama vitakuwa na ushawishi, tutakubaliana. Kumbuka pia, kama utajibu maswali yangu hapo juu, pengine utakuwa katika mazingira mazuri zaidi ya kuleta au kutoleta vifungu hivyo kanushi kutoka katika biblia. pia nakukumbusha kujibu swali langu hili, “Labda nikuulize kama hata vitabu vingine vitakatifu navyo vinaweza kuzingatiwa”.

  Kumbuka kuwa humu kuna mijadala ya Ukristo na Uislamu. Sasa kama huwa inajadiliwa, sijui ni kwa unafiki ama.

 7. Ndugu Kissima,

  Umejibu maswali ya wengine……naomba pia ujibu yangu ikiwezekana……kwangu mimi itaniwezesha kuchangia hoja yako……..nanukuu tena

  ” Labda utupe msingi wa hayo mafundisho yako yanatoka wapi? Ni ndani ya Biblia? Au wewe unaielewaje Biblia? Na Kwako Yesu ni nani hasa? Unaichukuliaje kazi ya Yesu Msalabani? Je Yesu ni Njia ya Pekee ya kumjua Mungu Kama alivyosema Yesu Mwenyewe? Au kuna Njia Nyingi tu! Na Ukristo ni mojawapo katika hizo nyingi? Au “Taking Care to Human being” is the one of a way to God…..?”

  Kwangu mimi huu ndio msingi wa Kujua Ukristo ni nini? Au ni lipi la Msingi katika Imani ya Kikristo……Nasubiri

 8. Ndg Albert,

  Kumbuka katika mchango wangu wa tarehe 14 niliandika maneno haya yafuatayo:

  “Karibu sana hapa ambapo mijadala yetu imejengwa juu ya Maandiko Matakatifu yaani Biblia. Na kwa sababu hiyo suala la “kufikiri” huwa halina hafasi inapotokea kuna jambo ambalo kwa akili linashindwa kupata maelezo. Ikishafikia hapo inabidi mtu ‘AAMINI’ ingawa kwa akili zake HAJAELEWA. Mtu akiamini vile inavyosema Biblia, kitu hicho huumbika na kuwa halisi. Na asiye amini, basi, hubakia gizani huku akishangaa ni nini kinaendelea!

  Hivi ndivyo watu walivyomwamini Mungu kupitia Neno lake, na sasa wanaendelea kumwamini. Na hao wanaomwamini Mungu kupitia Neno lake, Uwepo wa Mungu hujidhihirisha kwao, nao wanathibitisha walichokiamini kuwa ni Kweli!”

  Nasisitiza lifuatalo: Na kwa sababu hiyo suala la “kufikiri” huwa halina nafasi inapotokea kuna jambo ambalo kwa akili linashindwa kupata maelezo”

  Ungelisoma kwa makini na kulizingatia hilo wala tusingefika hapa tulipo ambapo wewe UNAANDIKA KWA KUTUMIA MAWAZO YAKO na unataka mtu aamini MAWAZO YAKO yaliyo KINYUME NA NENO LA MUNGU. Hapa HAKUNA ELIMU NYINGINE INAYOWEZA KUPATA NAFASI ISIPOKUWA ni ELIMU YA NENO LA MUNGU TU! Yaani Mungu anasemaje na si ALBERT anasemaje! ….Tafakari sana maneno haya.

  Lakini kama kweli UNAFAHAMU na UNAAMINI kuwa IMANI BILA MATENDO IMEKUFA kwa nini USIFAHAMU NA KUAMINI KUWA KUNA KUOKOKA? Maana ndivyo inavyosema BIBLIA!

  Ni mambo mengi huyajui au uliyajua UKAAMUA KUASI na KUANZA KUTUMIA MAWAZO NA KUFIKIRI KWA AKILI ZAKO UNAWEZA UKAFANYA HATA YALE YA MUNGU.

  Kauli kama hii: “Sijui, lakini sikubadili mfumo kwa shinikizo la imani yoyote ya kidini, nilitumia tu akili, utashi na maarifa. Nilijiona nilikuwa chukizo kwa jamii. Sikuijali jamii, sikuutendea utu haki” inakudhihirisha kuwa HUNA HATA DINI kwa kuwa MUNGU HANA NAFASI KWAKO! Wewe unachoamini ni UWEZO WA AKILI, UTASHI na MAARIFA YAKO KATIKA KUENDESHA MAISHA YAKO. Lakini maarifa YASIYOMWELEKEZA MTU KWA MUNGU ni maarifa BATILI!.. . Ni janga la Kiroho!

  Nifupishe tu hivi kuwa; Kama ni Akili, Utashi na Maarifa KILA MTU ANAYO YA KWAKE. Na mimi ninayo ya kwangu….na Msomaji anayesoma hapa naye ANAYO YA KWAKE! Sasa kila mtu akisema aandike ANAVYOWAZA YEYE tutaishia Kugombana kwa kuwa kila mtu ATATAKA WATU WOTE waamini ANAVYOWAZA KICHWANI MWAKE. Sasa hapo itakuwa ni balaa…..!

  Nimeandika hayo kwa masikitiko kwa kuwa HUKUELEWA KUWA HAPA TUNAWEKA MWONGOZO WA BIBLIA MBELE. Ni blog ya Kikristo…Ni blog ya Injili….! Biblia mbele, Akili, Utashi na Maarifa ya kila mtu tunaviweka Nyuma….

  Sasa kabla sijandelea sana, pengine kujibu maswali na hoja zako, nahitaji jibu kutoka kwako. Ninahitaji jibu la swali hili:

  Je, Kama tutapata katika Biblia kinyume cha hayo uliyoyaandika UTAKUWA TAYARI KUACHA MAWAZO YAKO NA KUAMINI BIBLIA au UTAENDELEA NA MSIMAMO WAKO WA KUAMINI akili, utashi ma maarifa yako?

  Jibu la swali hilo litaamua kama nikujibu hoja zako au niache kwa kuwa sina muda wa kupoteza kusikiliza ushawishi wa kulazimisha toka kwa mtu anayefikiria kuwa Mawazo yake yanaweza Kuwa Juu ya Neno la Mungu!

  Hata sijuwi hiki kiburi umekipata wapi……..!

 9. Ndugu zangu, ninawashukuru kwa kuendelea kuguswa na mchango wangu ktk mada hii. Nimepitia maoni yenu na nitajaribu kueleza na kujibu maswali niliyoulizwa kwa kadiri ya niwezavyo na kwa ufahamu wangu. Mniwie radhi kwa kuchelewa kujibu (kwa upande mwingine).

  Ndugu Daniel, mimi ninaamini kuwa si kosa kutaka kumjua Mungu zaidi na kwa kila sekunde na dakika. Ninawaza ni nani aliyekupa uwezo wa kujua kuwa siwezi kummaliza Mungu na kumuelewa. Ni Mungu amekutuma au wasema kwa kuwa tayari una imani? Binafsi sioni vibaya kumchambua na kumjadili Mungu. Siogopi hata kidogo. Ili mradi ninafanya hivyo katika harakati za kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Ndio maana huwa ninawakumbusha watu kuwa “ni vyema wakajiuliza Mungu ni nini kuliko Mungu ni nani” maana hili la Mungu ni nani ni swali rahisi na pengine linalozuia watu wasiijue dhana ya Mungu barabara.

 10. 2 (i). Kuokoka tafsiri yake ni kuepukana na jambo ambalo lingeleta madhara. Hii ni tafsiri ya kawaida ya kiswahili kwa namna nilijuavyo neno “Okoka” kama mtumiaji wa Kiswahili. Sasa katika swala la imani, tafsiri yake ni kuacha maovu au yale yote yatafsiriwayo au kuonekana wazi kwenda kinyume na matendo ya Mungu. Tafsiri ya imani ndio iliyonisukuma kutambua ama kuamini kuwa kuokoka ni hali ya kubadili tu mfumo wa maisha. Nitoe mfano halisi. Mimi kipindi cha nyuma nilikuwa mnywaji mzuri wa pombe. Ilifika mahali nikaamua kuacha pombe kabisa. Nilitafakari, nikaona pombe haina faida kwangu, nikaiacha. Sasa sijui hapa niliokoka kwanza ndipo nikaamua kubadi mfumo wa maisha au nilipoacha pombe nikawa ktk kundi la waliookoka? Sijui, lakini sikubadili mfumo kwa shinikizo la imani yoyote ya kidini, nilitumia tu akili, utashi na maarifa. Nilijiona nilikuwa chukizo kwa jamii. Sikuijali jamii, sikuutendea utu haki. Nina miaka zaidi ya kumi sasa situmii kilevi cha aina yoyote mbali na chai ama kahawa.

  3 (i ) Ndugu John Paul, niliandika hivyo ili kukupa na kukushawishi wewe na wengine kujaribu kuitafakari hoja hii. Kujipa nafasi ya kupata ukweli ama usahihi wa SALA uiitayo yangu. Ingekuwa vyema sana kama ungesema hii si Sala yenye nguvu kuliko nyingine yoyote kwa kutoa hoja mbadala. Mimi nimeonesha hili kwa kukueleza maana ya kuokoka na namna nisivyokubaliana na kuokoka.
  (ii) Mazingira ya kawaida nina maana ya maisha ya sasa ya Mwanadamu, utaratibu wa kila siku wa maisha. Fananisha mafundisho na simulizi za vitabu vitakatifu na maisha ya sasa ya Mtanzania/ya mwanadamu katika maisha ya sasa.

  4(i) Nianze kwa utangulizi huu. Ndugu John Paul, nilikuuliza swali, hujalijibu na badala yake ukaniuliza swali. Ok. Ni namna mojawapo ya kujibu swali, yaani kwa kuuliza swali. Ninaamini (kwa uzoefu) mimi ningefanya hivi kwenye maswali yako uliyoniuliza, bila shaka usingeridhika kabisa. Huu ndio ukweli.

  Nianze kujibu maswali yako.
  4 (i) kitabu chochote kinachofuatwa na waumini wanaojali utu, hicho ni kitakatifu. Vilevile, wazo lolote linalojali utu, linalofanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Hilo ni takatifu, ni safi, halina doa. Swali la nne na vipengele vyake nimejibu. Kwa nini vitabu ni Vitakatifu na kama mawazo yanaweza kuwa matakatifu.

  5. Sijajichanganya hata kidogo. Nimeamua kutumia upande unaousimamia wewe(biblia) katika kukupa mfano halisi wa mapaji ya Roho mtakatifu na pia kukukumbusha kuwa nina uhuru wa kutumia chanzo chochote cha maarifa, kufikiri na kutumia vitabu kama misaafu ikiwa ni mifano.

  Ndugu yangu, unapoandika “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa”, na “hekima ya Dunia hii upuzi mbele za Mungu” na ukaishia hapa, mimi ninaona ni matumizi ya mistari hii yanayoleta mashaka. Mistari hii kama hutotoa tafsiri yake kwa kuhusianisha na maisha ya kawaida ya mwanadamu, basi mistari hii inakosa msaada kabisa. Yaani, kile ulichokusudia kukifundisha kupitia mistari hii, kinakosekana.

  Kwa leo niishie hapa. Nitaendelea kutoa ufafanuzi wa muliyoyauliza.

 11. Ndugu John Paul, ninajibu maswali yako kama ifuatavyo.

  Swali la kwanza.
  Maneno haya nimeyapata kwa kuangalia uhusiano wangu na wanadamu wengine. Ni kwa namna gani nitaishi nao katika kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Nimeyatafakari sana maneno haya. Sijapata mwisho wake, sijapata ugungufu wake. Ni sahihi kwa mtu wa kila imani. Maneno haya yanatukumbusha namna bora ya kuishi.

  ii. Maneno hayo ndio sala, “taking care of humankind”. Sala hii ni ya kutenda kuliko kuliko kunena. Tofauti na sala nyingine ambazo hunenwa tu. Sala hii msingi wake ni Upendo. Inazingatia sana maneno ya imani bila matendo, si hai, imekufa.

  iv. Taking care of Humankind ni Prayer, kama nilivyotangulia kusema. Yeyote awezaye kuisali sala hii, nionavyo mimi, ndiye amchaye Mungu. Ninaamini maana ya Taking care of human kind ni wazi waifahamu. Hili sio tatizo. Nitapenda pia kujua ni kwa kiasi gani waikubali sala hii ndugu John Paul.

 12. Nawasalimu ktk Jina la Yesu Kristo,

  Ndg Albert umeandika..
  “Mimi kama ni Mwislamu ama M-Romani mkatoliki, ninapaswa kuokoka na kujiunga na kundi fulani la waliookoka na walio na misimamo yao inayowaongoza.
  Kusema ukweli, mimi siamini ktk kuokoka kabisa, na kamwe sitakaa kuamini dhana hii, sasa sijui kama hapa nitakuwa katika nafasi gani ya kumcha Mungu. Lakini bado ninaomba mnifafanulie vizuri”

  Nami naomba nafasi ktk moyo wako Nikufafanulia kwa kutumia maaandiko

  Yohana 3
  Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.
  Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.
  Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. (UOKOVU)

  ”Yoh3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ULIMWENGU, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.
  Bwana anamwambia Nikodemo kuwa mtu asipozaliwa mara ya pili ktk Roho(Wokovu)hawezi kuuona Ufalme wa Mungu.na anasisitiza kuwa kilichozaliwa kwa Roho ni roho,na kilichozaliwa na mwili ni mwili,HIYO NI CHANGAMOTO KWAKO

  Napenda ujue kuwa Wokovu Sio swala la DINI, wala Misimamo au Dhana,Kabila,Rangi,Taifa,Wokovu ni kwa ajili ya Ulimwengu haubagui Mkatoliiki au Muislamu n.k, Ebu fikiri nami ktk miaka 200 baada ya Kristo kulikuwa hakuna Ukatoliki wala Uislamu/Madhehebu lakini Wokovu ulikuwako,

  Nabii Isaya ameandika” Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana” Isaya11:2

  Unaona hapo Roho saba za Mungu ambazo Bwana wetu Yesu kama Binadamu zilimjilia juu yake ,Ukishazaliwa mara ya pili ktk Roho(WOKOVU)ambao si kwa mapenzi ya damu au mapenzi ya binadamu ila kwa mapenzi ya Mungu, Hizo Roho saba za Mungu zinamjilia juu yake mtu huyo

  Tunasoma hapo nakuona Roho ya kumcha Bwana,hakuna swala la maisha gani yawe ya kawaida yawe ya tajiri,Mtanzania au sio ,kama kusingekuwa na Roho ya kumcha Bwana isingeandikwa,

  Paulo anandika kwenye “1koritho2: 11-15 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo”.

  Anaendelea…..”.Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda KUWAOKOA waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa…… Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa…….. Bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu;” “1Koritho1:20,26,27

  Nakubaliana na yale waliyoandika Ndg Monga,Daniel na John Paul,kumcha Bwana ni Kuamini ,Utii,Kushika Amri zake , Kuzitenda,Kuisikia Sauti yake kwa Bidii na Unyenyekevu,Kuishi maisha yasiyo na Mawaa,Kiasi yaani Utauwa n.k.

  …………”Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu Yohana6:44,45.
  Kwa Mapenzi ya Bwana ipo siku Ataliita Jina lako nawe utazaliwa mara ya pili(Wokovu) utajua kumcha BWANA kwa haya maisha yetu ya kawaida ya Mtanzania

  Ashukuriwe Bwana Wetu Yesu Kristo.

 13. Ndugu Kissima,

  Labda utupe msingi wa hayo mafundisho yako yanatoka wapi? Ni ndani ya Biblia? Au wewe unaielewaje Biblia? Na Kwako Yesu ni nani hasa? Unaichukuliaje kazi ya Yesu Msalabani? Je Yesu ni Njia ya Pekee ya kumjua Mungu Kama alivyosema Yesu Mwenyewe? Au kuna Njia Nyingi tu! Na Ukristo ni mojawapo? Au “Taking Care to Human being” is the one of a way to God…..?

  Ukisaidia kujibu haya utasaidia majadiliano na kufundishana! Naogopa hata kusema UBARIKIWE Maana Baraka nazoziamini zimejengwa juu ya Yesu Mwana wa Mungu aliye HAI! Aliyeketi Mkono wa Kuume wa Mungu Baba Akituombea…..na Aliyesema nje ya yeye ni wezi na wanyang’anyi…..Utazipokea Baraka zake ndugu Kissima? Baraka zake zimefungwa katika Kasha la Wokovu!

 14. SALAMU SANA NDUGU ALBERT KISSIMA

  NIMESHUKURU TENA MUNGU KUNIPA NA FASI YA KUSAIDIANA JUU YA MASWALI YAKO.

  NDUGU KWA KWELI ATA MIMI NALIKUWA KAMA WEWE NA MASWALI KAMA IYO NA KATIKA UPENDO YA WANA WA MUNGU WAKANIFAHAMISHA . NJIA ZURI YA KUMWAMINI YESU KAMA BWANA MUOKONZI WAMAISHA YANGU .NDIPO TAYARI NIMEOKOKA NAMUTUMIKIYA MUNGU.

  KAMA UKO NA BIBLIA SOMA MUHUBIRI 12 : 13-14
  MATAYO 12 : 36-37

  AO TAFUTA KANISA MOJA YA KIROHO IKUSAIDIYE KARIBU NAWE

  UBARIKIWE

 15. Ndg Albert Kissima,

  Nimesoma maoni yako na kuna mambo mengi sana ambayo ningeandika lakini nimefupisha ili tuende hatua kwa hatua. Baada ya kusoma maoni yako nimeandika pamoja na maswali na ninakuomba usome taratibu kisha uyajibu kwa uangalifu maswali niliyokuuliza uli tuweze kupiga hatua. Ukiyajibu haraka haraka tunaweza kujikuta tunazunguka hapo hapo!

  Binadamu ana uhuru wa kuchagua. Ana uhuru wa kuamini au kutokuamini jambo fulani. Ndiyo maana Biblia inasema “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa…” na wala halisemi kuwa NI LAZIMA KUAMINI. Hapana!

  Kwa hiyo suala kwamba huamini katika kuokoka na KAMWE hutaamini hilo ni la kwako. Una uhuru wa kuamini au kutokuamini. Lakini lazima ufahamu kuwa mwisho wa yote utapata malipo yanayostahili sawa sawa na KUAMINI au KUTOKUAMINI kwako. Uchaguzi ni wako!

  Wakati ukisisitiza kufafanuliwa mtu aishi vipi ndiyo iwe anamcha Mungu, hapo mbele umeweka sharti kuwa BILA KUSHAWISHIWA KUWA KUSALI SALA FULANI (ambayo hata hivyo mimi sijaiona hapo) NDIYO KUMCHA MUNGU, HUTAKUBALI.

  1. Ulichoandika wewe ni hiki: “Binafsi huwa ninaamini kuwa, THE MOST POWERFUL PRAYER ON EARTH IS TAKING CARE OF HUMAN KIND”. Labda kama mtaweza kunishawishi kuwa kuisali sala hii ndio kumcha Mungu nitaelewa”

  Naomba ufafanuzi kupitia maswali yafuatayo;

  i. Sasa wewe huwa unaamini jambo hilo kutokana na NINI? Ulipata wapi maneno hayo kisha Ukayaamini?

  ii. Ni SALA ipi iliyoko kwenye maneno hayo ambayo unasema kuisali hiyo ndiyo kumcha Mungu?

  iii. Je, TAKING CARE OF HUMAN KIND, kwako ina maanisha ni PRAYER?

  iv. Je, kuna uhusiano gani kati ya TAKING CARE OF HUMAN KIND, PRAYER na Kumcha Mungu?

  2.”Hili la kuokoka moja kwa moja siliafiki kwa kuwa maana ya kawaida ya kuokoka ni kubadili tu namna ya maisha, jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wa mwanadamu yeyote kuanzia mpagani, Mkristo Mromani, Mchawi, n.k.”

  i. Je, maana ya kawaida ya KUOKOKA kuwa ni KUBADILI TU NAMNA YA MAISHA uliipata wapi?

  ii). Naomba ufafanue ni kwa vipi MTU ANAWEZA KUBADILI TU NAMNA YA MAISHA, KWA UWEZO WAKE na kwa kufanya hivyo AKAWA AMEOKOKA?

  3.”Labda kama mtaweza kunishawishi kuwa kuisali sala hii ndio kumcha Mungu nitaelewa. Kusema hivi sifungi milango hata kidogo ya kuelimishwa nini Maana ya Kumcha Mungu kwa kuzingatia mazingira ya kawaida ya binadamu tunamoishi”

  i. Ndg Albert, kwanza umeshafunga milango ya kuelimishwa kwa kuwa hutaki kusikia lolote ila isipokuwa KUSHAWISHIWA KUHUSU KUSALI SALA YAKO KUWA NDIYO KUMCHA MUNGU. Yaani hakuna namna yoyote nyingine ya kukufanya UELEWE isipokuwa kupitia hicho ulichokiita wewe kuwa ni SALA, japo mimi sijaona sala yoyote hapo!

  ii). Unaposema MAZINGIRA YA KAWAIDA unamaanisha nini?

  4. “Labda nikuulize kama hata vitabu vingine vitakatifu navyo vinaweza kuzingatiwa. Pengine hata na mawazo mengine matakatifu lakini yakiwa ni mitizamo”

  i).Vitabu gani vingine ambavyo unavifahamu kuwa ni VITAKATIFU?
  ii). Kwa nini ni vitakatifu?
  iii) Je, mawazo na mitizamo yavyo vinawezaje kuwa ni VITAKATIFU?

  5.”Wazo lako hili ndugu yangu John Paul siliafiki kwa kuwa litanikosesha uhuru wa kueleza yale ninayowaza na pia kuenda kinyume na andiko kutoka ktk biblia linalosema kuwa Roho Mtakatifu ametoa uwezo wa kuchambua mambo ambapo, mbali na mambo mengine lkn tumepewa uwezo wa kutumia hekima, akili na maarifa katika mazingira yetu”

  Hapo ndipo unapojichanganya! Mwanzo wa maelezo yako umepinga kuhusu kuokoka na kamwe hutaamini! Labda jambo ambalo ulikuwa hulifahamu ni hili {ni haki yako kutolifahamu maana unapinga kuokoka} Roho mtakatifu anakaa ndani ya Mtu ALIYEOKOKA. Hawezi kaa ndani ya mtu ANAYEPINGA KUOKOKA. Roho mtakatifu huingia ndani ya mtu baada ya KUMWAMINI NA KUMPOKEA YESU na KUMFANYA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKE.

  Sasa wewe unayepinga kuokoka, huku dunia inashuhudia, UTAPATA WAPI HAKI YA KUWA NA ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO? Kwa kuwa umeshakataa kuokoka, forget about the Holy Spirit working in you! Roho mtakatifu si haki yako kwa kuwa Umeshamkataa! Lakini pia WEWE UKIPINGA KUOKOKA haina maana HAKUNA KUOKOKA. Vinginevyo MUNGU/YESU ni Muongo na wewe NDIYE MKWELI?

  Pamoja na kupewa uwezo wa kutumia hekima, akili na maarifa lakini Hekima yetu haiwezi kupindisha Mpango wa Mungu; Akili zetu ni ndogo mno kulinganisha na akili za Mungu. Na hata Hekima unayoisema, hekima ya kibinadamu ni ndogo mno kulinganisha na hekima ya Mungu. Na hata hayo maarifa unayosema tuko nayo ni madogo mno.

  Biblia inasema hivi: HEKIMA YA DUNIA HII NI UPUZI MBELE ZA MUNGU (1Cor 3:19)

  na kuhusu Maarifa Biblia inasema;

  KUMCHA BWANA NDICHO CHANZO CHA MAARIFA (Mithali 9:10)

  Hivyo hakuna Hekima wala Maarifa SAHIHI pasipo kumcha Mungu wa Biblia.

  Nilipoandika niliandika kuwa huwezi tenganisha kati ya KUOKOKA na KUMCHA Mungu wa Biblia. Sasa wewe ambaye hutaki KUOKOKA utajua mwenyewe utamcha vipi Mungu. Lakini inawezekana una Mungu wako asiye wa Biblia. Huo ni uamuzi na hiari yako.

 16. Kwako Ndg. Albert Kissima.
  Tunapozungumzia suala lolote la MUNGU; ni vema kabisa kujiandaa kumuelewa kama MUNGU. Na nikukumbushe tu kuwa; ufahamu wetu una kikomo lakini SI MUNGU. Jaribu kujiandaa kwanza kuelewa kwa kuwa MUNGU hatakulazimisha kuelewa ila ataeleza UKWELI kama ilivyo katika NENO lake na una uhuru wa kuchagua kufuata ama la. …….Lakini, kumbuka kuwa unapochagua kutofuata, kubali pia matokeo yake. …….Jambo lingine la MUHIMU tunaloweza kusaidiana ni kuwa; HUWEZI KUMCHUKUA MUNGU UKATAKA KUMLINGANISHA NA UWEZO WAKO WA KUELEWA. ANABAKI KUWA MUNGU HUWEZI KUMALIZA KUMUELEWA, NDIO MAANA UNATAKIWA KUAMINI TU. Maana wokovu ni halisi ndani ya neema ya MUNGU. Huwezi hata mara moja kusema kuwa unaweza kubadilika au kuamua maisha yako ukayabadilisha mwenyewe, kuna kikomo, na ndipo tunapomhitaji sana MUNGU (Kitu ambacho nadhani hujakipa nafasi stahiki). Ahsante.

 17. Ninawashukuru nyote mliotoa maoni yaliyotokana na mchango wangu.

  Nimeyasoma na bila shaka nimeyaelewa mawazo yenu. Kikubwa ninachokiona hapa ni kuwa ili nimche Mungu, ninapaswa kuokoka. Mimi kama ni Mwislamu ama M-Romani mkatoliki, ninapaswa kuokoka na kujiunga na kundi fulani la waliookoka na walio na misimamo yao inayowaongoza.

  Kusema ukweli, mimi siamini ktk kuokoka kabisa, na kamwe sitakaa kuamini dhana hii, sasa sijui kama hapa nitakuwa katika nafasi gani ya kumcha Mungu. Lakini bado ninaomba mnifafanulie vizuri, ili Kumcha Mungu Mwanadamu aishi vipi. Hili la kuokoka moja kwa moja siliafiki kwa kuwa maana ya kawaida ya kuokoka ni kubadili tu namna ya maisha, jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wa mwanadamu yeyote kuanzia mpagani, Mkristo Mromani, Mchawi, n.k.

  Binafsi huwa ninaamini kuwa, THE MOST POWERFUL PRAYER ON EARTH IS TAKING CARE OF HUMAN KIND. Labda kama mtaweza kunishawishi kuwa kuisali sala hii ndio kumcha Mungu nitaelewa. Kusema hivi sifungi milango hata kidogo ya kuelimishwa nini Maana ya Kumcha Mungu kwa kuzingatia mazingira ya kawaida ya binadamu tunamoishi.

  Ndugu John Paul, ninakushukuru kwa kunikumbusha kuwa hoja zote msingi wake lazima uzingatie kitabu kitakatifu yaani Biblia. Labda nikuulize kama hata vitabu vingine vitakatifu navyo vinaweza kuzingatiwa. Pengine hata na mawazo mengine matakatifu lakini yakiwa ni mitizamo.
  Wazo lako hili ndugu yangu John Paul siliafiki kwa kuwa litanikosesha uhuru wa kueleza yale ninayowaza na pia kuenda kinyume na andiko kutoka ktk biblia linalosema kuwa Roho Mtakatifu ametoa uwezo wa kuchambua mambo ambapo, mbali na mambo mengine lkn tumepewa uwezo wa kutumia hekima, akili na maarifa katika mazingira yetu.

 18. Mpendwa wangu, kama dunia ukaayo inafananishwa na mlevi na inawayawaya kama machela, wewe umebana wapi au umejisalimisha kwa nani? Hebu kabidhi maisha yako kwa Yesu na mshirikishe Mungu katika kila jambo; Nakusihi sana mpendwa wangu, Uchukue hatua kabla haujaja wakati mbaya kwani kuokoka ni faida, tena kuokoka ni kuuchukia uovu! Mwamini Yesu sasa nawe utaokolewa.

 19. Ndugu Albert Kissima,

  Nashukuru kwa maoni yako na kuhitaji ufafanuzi kuhusu suala la ku-mcha Mungu na kuokoka!

  Karibu sana hapa ambapo mijadala yetu imejengwa juu ya Maandiko Matakatifu yaani Biblia. Na kwa sababu hiyo suala la “kufikiri” huwa halina hafasi inapotokea kuna jambo ambalo kwa akili linashindwa kupata maelezo. Ikishafikia hapo inabidi mtu ‘AAMINI’ ingawa kwa akili zake HAJAELEWA. Mtu akiamini vile inavyosema Biblia, kitu hicho huumbika na kuwa halisi. Na asiye amini, basi, hubakia gizani huku akishangaa ni nini kinaendelea!

  Hivi ndivyo watu walivyomwamini Mungu kupitia Neno lake, na sasa wanaendelea kumwamini. Na hao wanaomwamini Mungu kupitia Neno lake, Uwepo wa Mungu hujidhihirisha kwao, nao wanathibitisha walichokiamini kuwa ni Kweli!

  Sasa nikirudi kwenye yale uliyohitaji, napenda kuongezea juu ya yale ambayo ndugu Monga ameelezea:

  1. Kumcha Mungu ni kuamini na kutii kile anachosema. Kutii likiwa na maana ya KUTEKELEZA au KUTENDA yale ambayo Mungu anasema kupitia Neno lake, yaani Biblia, kwa sasa. [Zamani Mungu alisema wazi wazi na watu kupitia Manabii au moja kwa moja kwa mhusika]

  2. Biblia ni mjumuisho wa Agano la Kale na Agano Jipya. Kwa hiyo Neno la Mungu ni pamoja na Injili, ambamo ndani yake kuna habari za Yesu, Mwokozi. Kwa hiyo mtu anayemtii Mungu, the Bible way, huyo ndiye aliyeokoka! Kwa hiyo haiwezekani kutenganisha KUMCHA MUNGU wa Biblia na KUOKOKA: Mtu aliyeokoka ndiye Mcha Mungu, na Mcha Mungu ni yule aliyeokoka!

  Kwako, ndugu Kissima!

 20. Bwana asifiwe……..

  salamu kwako ndugu ALBERT KISSIMA kama vile unapouliza juu ya KUMCHA MUNGU tafisiri yake ni wazi mpendwa.
  MCHA MUNGU NI MTU MWENYE KUMUOGOPA MUNGU NA KUMUPENDEZA MUNGU NA TAYARI UMEOKOKA

  MCHA MUNGU SI MTOVU

  WARUMI 10 : 9-11 jaribu kuisoma roho ya Mungu atafsiri ndani yako.

  Bwana awe nasi

 21. Nianze kwa kukushukuru ndugu kwa uchambuzi wako wa neno la Mungu kutoka katika biblia.

  Umejaribu kuelezea swala la kumcha Mungu kwa kuangalia biblia inasema nini kwa kuzingatia historia ya maisha ya watu fulani iliyoelezwa katika biblia.

  Kama hutojali, naomba unifafanulie sasa (kwa kuzingatia maisha ya kawaida ya Mtanzania na ya mtu mwingine yeyote kokote kule) maana ya KUMCHA MUNGU. Nini tafsiri yake katika maisha ya kawaida ya binadamu, mtu aishije. Unafikiri ili um-MCHE MUNGU ni lazima uwe ume-OKOKA?

 22. Bwana Apewe sifa zake

  Kweli na mimi na shukuru Mungu sana juu ya fundisho iyi yakutu kamilisha kwa IMANI yetu kwa Mungu kupitiya Emmanuel Mungu pamoja nasi YESU

  Ndio iyi kipindi ninapopitia kwa sasa Mungu ni mwema kweli tuko pamoja

  Mungu awabariki sana azidi tena kunipa nguvu ya zaidi

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s