Tuwe na Moyo wa Kujitolea

Bwana Yesu asifiwe sana!

Watu wengi hupiga simu, wengine huandika ujumbe mfupi wa maneno na wengine ujumbe wa barua pepe wakitaka kujiunga na Strictly Gospel kwa sababu za kiuchumi. Wapo ambao huuliza wakijiunga watapata mshahara wa shilingi ngapi. Wapo ambao husema kuwa hali yao ya kifedha ni mbaya sana hivyo wanaona wakijiunga na Strictly Gospel wataboresha kipato chao cha pesa. Hata kuna watu wa karibu ambao hutuuliza kuwa kwa kuendesha blog hii na Strictly Gospel kwa ujumla tunapata nini mifukoni?

Hivi karibuni kuna mtu mmoja ambaye alitaka maelekezo ya namna kujiunga na Freemasons kwa kuwa ameona habari zao katika blog hii. Na sababu kubwa aliyosema inamlazimu ajiunge na Freemasons ni kuwa anataka kuwa tajiri! Baada ya kumhakikishia kuwa sisi si washirika wa Freemasons bali ni wahubiri wa Injili alibadili mwelekeo na kusema basi ajiunge nasi Strictly Gospel kwa sababu hali yake kifedha si nzuri na anaamini akijiunga nasi maisha yake yatakuwa mazuri!

Jumla ya hayo yote ni kielelezo kuwa tunahitaji moyo wa kujitolea ili badala ya mtu kuhitaji au kufanya jambo fulani kwa ajili yake tu tuwe tayari kufanya jambo fulani hata kama faida yake ni kwa mtu mwingine.

Katika kitabu kile cha Mathayo 7:12, Bwana Yesu alisema hivi: “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati yote na manabii”

Ni kweli watu wote tuna mahitaji ya kiuchumi na kila mtu anapambana ili aweze kukabiliana na uhitaji huo. Japo kuna wale ambao walishatoka katika hali ya uhitaji lakini haina maana wamekaa tu na hawajishughulishi tena. Na hata matajiri zaidi nao wako bize wakitafuta kuongeza zaidi utajiri uliopo.

Jambo moja la kufahamu ni kuwa, pamoja na uhitaji uliopo lakini njia mojawapo ya kibiblia ya kupata ni kutoa. Waweza kuwa na uhitaji fulani na ukatamani upate ufumbuzi wa uhitaji huo, kumbe ili upate unatakiwa utoe. Waweza kuwa na uhitaji wa pesa lakini ili uzipate kumbe si lazima uombe au upewe pesa. Waweza toa muda wako kwa ajili ya kushughulikia jambo la mtu mwingine na katika kufanya hivyo ukafungua mlango wa wewe kupata. Si lazima iwe ni kutoka kwa mtu huyo ambaye umetoa muda wako kwa ajili yake. Inaweza kuwa ni kutoka kwa mtu mwingine kabisa ambaye Mungu atakuwa amemgusa kwa ajili yako. Mungu yupo na anatenda hata sasa!

Waafrika na hasa Watanzania tuna kiwango kidogo sana cha moyo wa kujitolea.  Tumenaswa katika mtego wa ubinafsi. Kuanzia maisha ya kawaida ya kimwili hadi katika Huduma za kiroho:.

Ukiingia maofisini hali ni mbaya sana. Kila mwenye nafasi ya “kutengeneza” pesa hutaka kufanya hivyo kwa ajili yake tu. Watu hutafuta marupu rupu kwa njia hata zisizo halali; mfano anaweza kujiongezea masaa ya OT (Over-time). Anaweza kulazimisha safari za kikazi ili tu apate traveling allowance, hata kama safari hizo hazima maslahi kwa umma. Walio katika sehemu za manunuzi nao hali ni mbaya. Risiti nyingi za uongo huandikwa na zingine zinaongezwa kiasi cha pesa ili kinachozidi kiingie katika mfuko binafsi. Mikataba mingi huingiwa kwa hila na asilimia kumi, (teni pesenti) ikipotosha lengo la mikataba hiyo pasipo kujali hasara yake kwa umma. Wako mabosi ambao huendelea kuchukua mishahara ya watu ambao walishakufa. Loh!

Ukienda kwa wafanya biashara hali ni mbaya sana. Mizani na vipimo vya uzito vimekazwa au kulegezwa ili visipime kihalali (hili nalo ni chukizo kwa Bwana Mithali 20:23). Vipimo vya ujazo vimepunguzwa kwa kukatwa au kuwekwa vitu vingine ndani ili vipime kidogo. Vipimo vya urefu vimefutwa alama zisionekane vizuri ili kipimo kiwe kifupi kuliko inavyotakiwa. Kuanzia mfanya biashara mkubwa hadi mdogo kabisa, kila mmoja hutafuta namna yoyote ya hila ili apate faida isiyo halali kwa kuharibu vipimo!

Kwa ujumla hali ya ubinafsi ni mbaya. Inatafuna nchi kuanzia Ikulu hadi mitaani, kwenye ngazi ya mwanzo kabisa. Maana hata muuza mafuta, anayeuza kwenye vibaba vya shilingi 50-50 za kitanzania naye hujitahidi afanye litakalowezekana ili apime mafuta kidogo kuliko alivyomwambia mteja wake.  Hata muuza nyanya, anayeuza nyanya za mafungu, hujitajidi apate njia ya “kumzunguka” mteja kwa kupanga nyanya kubwa juu katika chombo halafu chini anaweka zile ndogo na pengine mbovu!

Mambo ni mengi mno na tukisema tuyaandike yote hapa inaweza ikawa ni usumbufu kuyasoma maana itabidi yasomwe kwa siku nyingi. Lakini hayo machache hapo juu yanaonyesha kuwa hali ya ubinafsi iko juu sana. Na hiyo ndiyo sababu watanzani wengi ni wezi au wana wasi wasi wa kuibiwa. Hakuna kuaminiana kwa kuwa si rahisi mwizi kumwamini mtu mwingine kwa kuwa anajua kuwa naye ataiba tu kama ambavyo yeye huiba. Tunaishi maisha ya kuogopana, maisha yaliyofarakana. Maisha yaliyomeguka!

Katika mambo ya kiroho, yaani makanisani na katika Huduma mbali mbali za kiroho hali nako si nzuri. Watumishi mbali mbali huingia katika migogoro kwa sababu za maslahi ya binafsi. Ni mara nyingi inapofanyika mikutano ya Injili ambayo bajeti yake ni pesa nyingi na ambazo hutolewa na wafadhili au wahubiri wageni, wachungaji hubaki katika mtafaruku wakigombea kile kilichobakia maana kila mmoja hutaka apate zaidi kuliko mwenzake. Matangazo katika television, redio pamoja na magazeti hufupishwa muda au nafasi kuliko makubaliano na kinachobakia huingia katika mifuko binafsi. Vifaa vya matangazo kwa njia ya vipaza sauti pamoja na magari kwa kazi hiyo huandikiwa kiasi tofauti cha pesa kuliko makubaliano na kinachobakia huingia mfukoni. Na wakati mwingine hali huwa ni mbaya sana kiasi cha wachungaji kupigana ngumi kwa kuwa muafaka wa namna ya kugawana ‘nyara’ unashindikana! Sasa hii ni kujitakia laana, tena ni kuivuta kwa kamba!

Vikundi vingi vya muziki wa injili huanzishwa lakini mara tu husambaratika. Ukiuliza sababu utaambiwa kuna pesa fulani ilipatikana lakini viongozi wakaitumia kibinafsi. Kwaya nyingi nzuri zimekwama kabisa kwa sababu tu ya kugombania mapato. Zipo ambazo baada ya kupata mafanikio viongozi walichota pesa na kuacha uongozi na uanakwaya kabisa. Mifano hai tunayo!

Katika mambo ya kiroho pia mambo ni mengi sana ambayo kuyaandika yote itakuwa ni kukosekana kwa kiasi. Lakini kwa ujumla hali ni mbaya mno, mno!. Na yote hii ni kwa sababu ya ubinafsi. Kila mtu hutaka kujinufaisha yeye tu kabla ya mwingine au huyo mwingine asipate kabisa.

Lakini katika Biblia tunafundishwa kuwatanguliza wengine. Na pia kila mtu kutokuangalia mambo yake tu bali ya wengine. Kila mtu anahimizwa kumhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Wafilipi 2:3-5.

Maana ya maneno hayo ni kuwa wewe unapomtanguliza mtu mwingine na yeye akakutanguliza itafika mahali wote mtakuwa mbele. Hakuna atakayekuwa amebaki nyuma. Utakapoanza kuangalia mambo ya wengine: wanapata shida gani uwasaidie, wanahitaji nini ili ufanyike sababu ya wao kufanikiwa au japo kufurahi na kisha mtu mwingine akafanya hivyo kwa ajili yako utakuta jamii nzima tumekuwa kila mtu ni mtaji kwa mwingine. Wewe utafanyika mtaji kwa mwingine na yeye atafanyika mtaji kwako na hatimaye wote tutajikuta tumefanikiwa! Hiyo  ndiyo Biblia na Ukristo kwa ujumla!

Tuhahitaji kubadilika. Jamii nzima inahitaji kubadilika. Tukibadilika nchi itapata amani ya kweli. Watu watajisikia salama maana anajua kuna mtu anahangaika kwa ajili yake kama yeye anavyohangaika kwa ajili ya wengine. Uadui utaondoka. Kila mtu atapenda awe chanzo cha furaha kwa mwingine kama ambavyo yeye amefurahishwa na mwingine. Tutatamani kumuona ndugu yako, mwajiri/mwajiriwa wako,dereva au mfanyakazi wako wa nyumbani,  jirani yako nk akitabasamu kwa kuwa amekuona! Na kinyume chake naye atajitahidi akufanye utabasamu. Maisha yatapata nuru mpya na maana mpya!

Katika Huduma ya kazi ya Bwana Mungu, kazi itasonga mbele kwa kuwa Mungu ataruhusu Baraka kwa kuwa tumeandaa mazingira ya Yeye kufanya hivyo. Watu wengi wataokoka kwa uwepo uwepo wa Haki ya Mungu itakuwa kati kati yetu. Tutabarikiwa na Bwana kwa kuwa tunawapa na wengine. Siyo rahisi kwa mchoyo kubarikiwa. Siyo rahisi kwa mbinafsi kubarikiwa. Kinachoonekana kwa wabinafsi na wachoyo ni Mafanikio tu na siyo Baraka maana mafanikio yanaweza patikana hata kwa kuiba na kuua!

Tukiwa na moyo wa kujitolea tutatamani kila mtu awe sababu ya kuwezesha jambo fulani lifanikiwe. Mfano badala ya  mtu kupiga simu hapa na kuuliza akijiunga atapata mshahara kiasi gani atapiga simu na kuuliza afanye nini ili achangie kufanikisha Huduma hii. Kila mtu akifanyika sababu ya jambo au mtu mwingine kufanikiwa, kinyume chake ni kuwa yeye atajikuta amefanikiwa kupitia mtu mwingine aliyejitahidi ili amfanikishe!

Tunahitaji kuwa na moyo wa kujitolea. Kila mtu akiwa na moyo wa kujitolea ufisadi hautakuwepo; wizi hautakuwepo. Tutaishi pamoja. Tutagawana sawa kwa sawa kilicho cha umma. Maisha ya kila siku mitaani yatabadilika. Watu hawataogopa kuwatuma watoto wao madukani kwa kuwa hata mtoto atapimiwa sawa sawa na mtu mkubwa. Wakaguzi wa mahesabu hawatakuwa na kazi kubwa maana mahesabu yote maofisini yako sahihi, hakuna kilichoghushiwa. Maendeleo katika nchi yatashamiri. Hata wale wasiojiweza, ambao wana matatizo katika maumbile yao watakuwa na matumaini mapya kwa kuwa pesa inayotolewa na wahisani kwa ajili ya kuwasaidia itawafikia kwa kadri ya makubaliano.

Faida za Moyo wa kujitolea ni nyingi. Hata wewe msomaji unaweza kuendelea kuziorodhesha na ukishafanya hivyo Omba Mungu akuwezeshe uwe na moyo wa huo ili Uwe sababu ya furaha au mafanikio kwa mtu mwingine; kwa kazi ya Mungu na kwa jamii nzima.

Na wewe unayeiba ofisini kwako, au una kipimo batili katika biashara yako au pengine unatumia mali ghafi zilizokwisha muda wake (expired) katika kutengeza mfano chakula hotelini/mgawahawani kwako; Pengine unauza madawa ya binadamu yalipo-expire maana yali-expire kwenye makabati dukani kwako, [na unaona ukitupa itakuwa hasara] geuka! Badilika leo. Baada ya kusoma ujumbe huu gundua kuwa kwa kufanya hivyo unakuwa sababu ya huzuni kwa wengi na Mungu anakuona kuwa wewe ni mkosaji na atakuhumu. Geuka. Rudi katika haki! Mwamini na kumfuata Yesu. Yeye ndiye kielelezo cha Moyo Wa Kujitolea. Alijjitolea kwa ajili kwa ajili ya uzima wa milele. Nasi twaweza kujitolea kwa ajili ya furaha na mafanikio ya mwingine.

Mungu akubariki unapochukua hatua ya kufanyia kazi ujumbe huu! Na endelea kutembelea blog hii pia mfahamishe na mtu mwingine ambaye hajaifahamu.

 

 

Advertisements

5 thoughts on “Tuwe na Moyo wa Kujitolea

 1. Asante kwa mafundisho ambayo yanatupasa ktk viungo mbali mbali na hasa ututoaji. Bwana akubariki na azidi kukutumia sawa na mapenzi yake. Amina.

 2. Ni kweli kwamba Mungu humpenda mtu yeyote atoaye kwa uaminifu. Kutoa ni muhimu sana kwani hiyo ni njia ya kukua katika imani. Lakini pia kuna baraka nyingi ukimtolea MUNGU. Kheri mkono utoao kuliko upokeo.

  Soma (Malaki3:10, Mwz.8:20-21, 1Nyak.29:14,17, 2Wakorintho8:3-5, 1Wakorintho 16:2)
  Wakristo wengi sana hutoa kwa shetani kuliko kumtolea Mungu, kwa sababu shetani amewakandamiza macho wasipate kutambua faida ipatikanayo juu ya kumtolea Bwana.
  Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, kuna nini Bwana?
  Akamwambia,’’sala zako na sadaka zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu’’ (Matendo 10:1-4). Kumbe nasi tukimtolea Bwana tutabarikiwa, kwani si mpango wa Mungu mwanadamu awe masikini.
  Ni lazima tutoe mali, muda na hata nguvu zetu kwa Bwana. Mungu wetu ni mtoaji yeye alitoa kwanza, kwani ukisoma Yohana 3:16 inasema, ‘’Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele’’.
  Nasi ni lazima tukumbuke kumtolea Mungu mali zetu na usiwe miongoni mwa watu wanaoshawishi kutomtolea Mungu.

  Kazi ya Sadaka:-

  -Kulisha au kutunza watumishi wa Mungu (Hesabu 18:8, 21, 31, Luka 10:7)
  -Mahitaji ya Kanisa (2Wakorintho 8:1-5, Hagai 1:9-11)
  -Kupeleka Injili (1Wakorintho 9:14)
  -Msaada kwa wajane, yatima na wengine wasiojiweza n.k
  Kwa yeyote anayemtolea Bwana ameahidiwa baraka (Kumb.28:1-14) na yeyote asiyetoa atapokea Laana (Kumb.28:15-29).
  Mithali 3:9-10 inasema, ‘’Mheshimu Bwana kwa mali yako, na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi na mashinikizo yako yatafurika divai mpya’’.
  Bwana akupe mafunuo mapya.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s