Lowassa; “Mungu Yupo Na Mimi Nitayashinda Majaribu”

Askofu Mkuu wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Kati Mch, Eliufoo Sima akitoa mahubiri katika kanisa hilo usharika wa Amani Sabasaba mjini Singida wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo ulioendeshwa na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa.

Askofu wa KKKT Mchungaji Eliufoo Sima akipokea kiasi cha shilingi milioni 10 taslimu kutoka kwa Mhe.Lowasa kama mchango wake katika kufanikisha harambee ya ujenzi wa kanisa hilo.

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mhe.Edward Lowasa amesema kuwa pamoja na kusemwa maneno mengi sana kwenye vyombo vya habari juu yake lakini anamwamini Mungu kuwa anampigania kila kukicha.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka mkoani Singida Hillary Shoo anaripoti kuwa Lowasa ameyasema hayo leo mjini Singida wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa la KKKT usharika wa Amani sabasaba mjini Singida. “Wale wanaofuatilia siasa za nchi yetu kuna maneno mengi saana lakini bwana ni mwema na mwaminifu hatimae tumeshinda”.Alisema. Alisema mara baada ya taarifa hizo siku moja akiwa nyumbani kwake na mkewe huku wakiangalia TV na kutaka kujua magazeti yanasemaje asubuhi kulikuwa na maneno mengi yaliyosemwa ya hovyo hovyo juu yake mengine walishindwa kuyasoma.

“Lakini mke wangu alienda chumba cha pili na kuchukua biblia na kunifungulia maneno ya bibilia kitabu cha Isaya 41:10, usiogope kwa maana mimi niko pamoja nawe tusifadhaike kwa maana mimi ni mungu wako nitakutia nguvu naam nitakusaidia, naam nitakushika mkono wa kuume wa haki yangu.” Alisema na kuongeza kwa maneno hayo niliendelea sana lakini baba askofu nisamehe nichukue hadhara hii kuwashukuru watu wengi sana walioniombea na hatimae kufika hapa nilipo. “Wapo waislamu na mashekhe walifanya dua kwa niaba yangu, nawashukuru sana, pia wapo wakristo walioniombea nao nawashukuru sana, mapadri, mashemasi na watawa, wachungaji na wainjilisti wa madhehebu yote, kwaya mbalimbali na waimbaji wa nyimbo za injili, wanamaombi wote, wanamtandao wao wa ajabu una nguvu kweli kweli na maaskofu wa makanisa yote ya kikristo pia nawashukuru sana.” Alisema Lowasa.

Aidha Mhe Lowasa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli alisema kuwa maneno mengi ya kisiasa yalisemwa juu yake lakini kimsingi hayakuwa ya kweli ya ukweli na siasa zinazoendelea kwa sasa ni za kuchafuana. Pia Lowasa alinukuu maandiko mengine ambayo aliyasoma kutoka kitabu kitakatifu cha Warumi ambayo aliyasoma mwenyewe. “ Lakini ikiwa roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu hataihuisha miili yenu iliyo katika hali ya kufa kwa Roho wake anakaa ndani yenu” alinukuu Lowasa.Aidha alisema kutokana na misukosuko ya kisiasa ambayo amekumbana nayo amekuwa akimwona Mungu akimtetea na utetezi huo ameupata kutoka kwa Mungu, kutokana na maombi ya watakatifu kutoka dini mbalimbali ambao wako pamoja.

Wale wote ambao wanaamini kuwa nafanya kazi kwa kusimamia haki ya Mungu na kazi zote kwa ujumla waliniombea usiku na mchana na kwa hilo Mungu kawasikia na kanifanya kuendelea tofauti na uchafu ambao mimekuwa nikibambikizwa na siasa za kuchafuana. Hata hivyo Lowasa alidai kuwa kama kiongozi hana Mungu ndani yake hawezi kuhimili mikiki ya kisiasa kwani kinachotakiwa ni kumwomba Mungu ili aweze kutetea kazi zinazofanywa na mtu mwenye haki. “Nimekuja kwenye harambee sio kupiga maneno ya kisiasa, nilimwambia baba askofu tuna utamaduni wa kualikwa haramabee nyingi sana, lakini kabla ya kukubali unauliza kwamba hao unaoshiriki nao wamefanya nini, nyie mmefanya kazi kubwa sana nawashukuru na nafurahi kwenye harambee hii.” Alisistiza na kuongeza.

“Kwa sababu ni njia mojawapo ya kuthibitisha kwamba wananchi wanaweza kufanya mambo yao kwani kanisa kama hili miaka ya nyuma lingeweza kujengwa na wafadhili wa nje lakini leo limejengwa na wananchi wenyewe. Mapema askofu mkuu wa KKKT Dayosisi ya kati Mchungaji,Eliufoo Sima anaamini utulivu wa viongozi wa nchi hii ni dhahiri kwamba Taifa hili kwa jinsi ya utamaduni na mapokeo yake , na mambo magumu yanayotokea siku hadi siku, litafanikiwa kutengeneza njia thabiti ya mafanikio ya watu wake. Askofu Sima alisema kumekuwepo na madai mengi kuwa nchi yetu ni maskini lakini angependa viongozi kuyashughulikia kwa umakini mkubwa ili kuondoa manung’uniko miongoni mwao ili yasiharibu tabia njema ya baadhi yao. Hataa hivyo Askofu Sima alimwagia sifa Mhe.Lowasa na kusema kuwa ni tofauti na viongozi wengine ambao unaweza kuwatafuta kwenye simu kwa muda mwingi na wakawa hawapatikani.

“Kwa kweli wewe ni kiongozi wa pekee,tofauti na wengine,unaweza ukamtafuta kwenye simu hata mara tano na hapatikani, lakini wewe kila ninapokupigia unapokea simu yangu,na hata katika harembee hii nilipokupigia nikakuomba uje Singida ukasema upo njiani unaenda Dodoma,”. “Lakini na mimi nikakwambia nipo njiani naenda Morogoro,ukasema basi tukutane njiani,mtu mkubwa kama wewe kukutana njiani hiyo ni ajabu.”alisema Askofu. Katika harambee hiyo Mhe.Lowasa amechangia kiasi cha shilingi milioni kumi ambapo makusanyo yote yaliyopatikana katika ujenzi wa kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Amani zilipatikana zaidi ya shilingi milioni 138. Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini liliko Kanisa hilo Mohammed Dewji (MO) alichangia shilingi milioni 10, Mfanya biashara maarufu hapa nchini aliyemtaja kwa jina moja tu la Patel amechangia mabati ya kuezekea kanisa hilo yenye thamani ya shilingi milioni 50. Kanisa hilo la usharika wa amani linatarajiwa kukamilika mapema hapo mwakani kwa gharama ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 480.

–MJENGWA BLOG—

Advertisements

15 thoughts on “Lowassa; “Mungu Yupo Na Mimi Nitayashinda Majaribu”

 1. Bila kutaja chama wala dini, tuone tu ktk hayo ambayo hata mbele za Mungu si mema kuwafanyia watu wake, kuwatoza kodi kubwa, kuwatumikisha (sasa hivi kodi kwenye kila kitu ili tuweze kulipa mishahara ya hii serikali likiwamo bunge)
  1. Kuna wabunge wangapi ambao sio chama tawala walipinga au kujitolea posho yao ili tu kupunguza makali ya uchumi kwa wananchi? ni Zitto tu!
  2. Wabunge wote wamekubali kuongezwa posho na wanalilia kabisa, je wale wapendwa wenzetu kule mbona hawapingi hili, mnaweza sema ohhh hata wale wanaopinga ni wanafiki lakini tunajuaje?
  3. Je tunaona kuna kitu kikubwa ambacho ‘Wakristo’ walio serikalini wanachangia ktk kupunguza makali ya maisha kwa wananchi? kupinga ufisadi? kusema na kukemea wazi maovu hata tu kuhatarisha hivyo vibarua vyao?
  4. Msahara wa mbunge huyu asiye waziri ni karibia milioni 7 na wanaruhusiwa na wote karibu wamechukua mikopo zaidi ya milioni 100 wangapi wanajitolea kwa masikini, kwa kueneza injili? hasa hao tunawaita Wakristo au hata hao wasio ktk chama tawala?
  TUKUBALIANE JAMANI MTAWALA YEYOTE KUTOKA TAIFA HILI SIO MTUMISHI WA WATU ILA NYIE MTAMTUMIKIA….KIKUBWA NI KUMWOMBA MUNGU AINUE TAIFA HILI LIWE KTK HAKI, HAPO NDIO LITASTAWI VINGINEVYO NI KUPOKEZAANA VIJITI TU…MBARIKIWE

 2. Naomba nikujibuni kwa kifupi tu, hivi huyu ni mwanasiasa tuseme ni mtawala, kwani huyu anatakiwa aweje? mie sidhani kama huyu anataka uongozi kanisani, zaidi anatafuta kuongoza nchi na kwa kanuni zetu nchi haina dini, ndiyo maana yoyote anaweza kutawala. Na ndio maana napinga mtu kumnyooshea kidole kwani hatujui nani anafaa zaidi na hata tukiangalia woote tu ni watawala!
  Tukija ktk Biblia kihistoria Mungu hakuwapa watoto wake watawala ila aliwapa manabii na makuhani ambao alisema nao na wao walipeleka ujumbe kwa watu, kuanzia Musa kule Misri tunaona wakiwa hivyo hadi wenyewe kutokana na kutokutii na kuona mara nyingine Mungu hasemi nao wala kuwasaidia wakimkosea walimtuma nabii Samweli ambaye alikuwa akiwaongoza wakati huo amwambie Mungu awape na wao “Mfalme” …. (1Samweli 8:5-20) kwanza Samweli alisikitika na kuona wamemkataa na wanamkaidi Mungu na kutaka kuwa kama wa mataifa, hivyo Mungu aliwajibu…. mmeomba mfalme nitawapa, ila mjue atawatawala na kuwatumikisha watoto wenu na kuwatoza kodi, na kuwanyang’anya mashamba yenu….hivyo hawa wooote ni watawala. wanaweza kutoka kwa Mungu au kujileta wenyewe kikubwa ni kumsihi Mungu hilo kongwa lao lisiwe kubwa kwetu injili iendelee kuenezwa, pili watuache tumwabudu Mungu wetu kwa amani, la Mungu atatupigania kama kwa Farao.
  Kuwa na mtawala asiyemjua Mungu sio laana maana tukiangalia Biblia hadi Agano jipya Yesu mwenyewe alizaliwa kipindi waisraeli wakiongozwa na utawala wa Rumi hawa warumi hawakumjua Mungu, ila ajabu Pilato alitaka hata kusema makuhani wale wamsikilize Yesu pengine anasema kweli ila ni makuhani (kanisa) ndio waliona anawanyang’anya haki yao ya kupata ukuhani na mafao yake, ndo maana nasema kanisa ndio linapaswa kuwa takatifu na kuwa kioo kwa taifa,
  Kanisa pia lina kosea kumwachia mtu bila kumwonya huyu kama mtawala si kuhani huyu! Anapaswa kuwa chini ya kuhani kama Daudi alivyomtii Samweli, hata nabii Nehemia aliweza kulijenga tena hekalu la suleimani kwa msaada wa mfalme wa Babeli ambaye hakuwa wala akimjua Mungu. Danieli na wenzie, nabii Esta wote hawa walitumika na kuokoa taifa la Mungu wakiwa chini ya watawala wasio mjua Mungu kabisa.
  Hatujui ni kwanini tuko chini ya watawala wa imani nyingine, injili bado haijaenea Tanzania? kanisa bado vuguvugu kusimama na kueneza injili kufikia taifa la Kikristo? Ni Mungu ameamua kutupitisha ktk kipindi fulani cha mpito? hatujui? hatujauliza? na kikubwa nadhani hatujaomba kwa dhati kwa ajili ya hilo, kila mtu anapenda tu Mungu asikie chama au fulani atawale kwa vigezo vyake, ndio ninapopinga kuwa tunajuaje?
  ukiwaangalia wote hawa ni watawala wa mwili sio wa kiroho, mradi hawatufungi ktk kueneza injili, kuabudu ktk Mungu wetu ni juu yetu kumwambia Mungu tunataka taifa la namna gani na hivyo watawala pia watakuwa hivyo hivyo vinginevyo haiwezekani kwa watu wachache (Wakristo) kutawala taifa lisilomjua Mungu, tafuteni kwanza ufalme wa Mungu ….huu utakatifu uanzie kanisani uenee nchini hata watawala watakuwa ni watu wa Mungu pia. Ni maoni yangu

 3. Ndugu wana SG
  Kwa kweli mjadala wa sasa ni mgumu maana wengine hata manifesto ya nini Lowassa atafanya akiwa Rais wanao wanatumwagia ili tuwe na AMANI.
  Lowassa ni mtu mmoja tu ambaye hawezi kubadili NCHI hii kwa kuwa mifumo ya serikali zilizopita( ambazo na yeye kashiriki kama kiongozi mtiifu hata kiasi cha kujiuzulu kulinda heshima ya Serikali na Chama chake) imelalia DHAMBI nyingi ambazo watendaji wa dhambi hizo hawako tayari kutubu wala kuchukuliwa hatua wanazostahili
  Msijedanganywa kuwa Lowassa ana MORAL AUTHORITY ya kupambana na uovu maana uovu wa karibuni umejengwa na MTANDAO ULIOMWINGIZA JAKAYA KIKWETE IKULU na LOWASSA ndiye king maker pamoja na ROSTAM AZIZ

  MSIJEDANGANYWA KUWA CCM INAWEZA LETA MAENDELEO TENA HAPO NDO MWISHO WA MFUMO HUO KIFIKIRI NA KUTENDA

 4. wana SG
  Kwa watu wanaotafuta fedha hawa hata wakiwa Maaskofu wetu tunajua kuwa OMBAOMBA HANA UCHAGUZI,WAENDELEEE KUNTUMIKIA KAFIRI WAPATE MRADI WAO!Usishangae hata wewe ukijipeleka pale watakuinua binadamu wale hata utoe wanachotaka
  Lowassa aseme kila kitu kama Zakayo wa Biblia na atubu kweli na aachane na ndoto za Urais atamani kutumika kama mzee wa kanisa wa mtaa kwanza kwa miaka mitano akiwa ameuza vyoote na kuwapa maskini!Hizo anazotoa yeye na kina Patel na Mohamed Dewji ni jana ya nyani tu!

 5. Heee! “Mchapa kazi kuliko mchapa majungu”; Hii ni kali ndugu Mligo.
  Ni kweli hakuna anayependa mchapa majungu lakini MCHEZA MPIRA ALIYETOKA UWANJANI kwa kupumzishwa na refa kwa KADI NYEKUNDU halafu akiwa nje anawalaumu timu yake kuwa “HAWAFANYI MAAMUZI MAGUMU” “ili kuboresha mchezo”, inaleta maswali mengi kuliko majibu. Kumbuka tunasherekea 50yrs toka Uhuru wa Tanganyika.

  Mungu huzungumza nasi kwa njia nyingi sana wapendwa, mojawapo ni kupitia watu wengine, na nyingine ni kupitia taabia za watu. Hatuhitaji kuwekwa darasa fulani ili tufundishwe mtu wa aina fulani anatakiwa kufanya nini na nini na anafaa kufanya nini au kupewa kazi gani. Hili Mungu ameliweka ndani ya watu kuwa kama msingi; KUMJUA ANAYEKUFAA KWA WAKATI UTAKAOMHITAJI.

 6. Shalom ni kweli Mengi yamesemwa juu ya Lowasa,lakini ya wengine hatujayasikia au tunayapuuza.Shilingi inapande mbili sawa na kwa Lowasa, nampenda huyu jamaa kwa sababu ni mchapakazi upande wa mabaya sitazungumzia sababu sina uhakika,vilevile siasa ni “mchezo mbaya”.Bora tupate mchapakazi kuliko mchapa majungu.

 7. shalom ndg John Paul na wengine, asante kwa mchango wako, sijakataa na ninakubaliana kabisa kuwa hawa watawala wetu ni mafisadi hata yule ambaye tunaweza semaa hahusiki na mkataba wowote kwanini? kwasababu kuanzia mishahara wanayojipangia na posho zao ukilinganisha na mishahara na kodi wanazowatoza wananchi ni ufisadi tosha mbele za Mungu. Tofauti kubwa ya maisha iliyopo inatengenezwa na wao ndio maana nimesema tayari nchi yetu ni ya kibepari, kila kiongozi anazo, hivyo kama anaguswa kutoa sio unafiki au dhambi, Tukubaliane hawa wote wanazo sana tu, hat mbunge anazo, kumbuka huyu alikuwa waziri mkuu analipwa mshahara na stahili zake zote. Miiko ya wafanyakazi kutofanya biashara haipo wanaruhusiwa kukopa na kufanya biashara yoyote. Tukubali kuwa hawa sio wenzetu wana kipato kikubwa mno hivyo kutoa milioni kumi au ishirini baada ya miezi miwli sio kitu cah ajabu ni sawa na wewe kutoa laki tano au moja kwa kipindi hicho. Unafahamu kuna viongozi wangapi ambao ni wamiliki wa majumba UK, US au SA? ni wengi sana na sio mojamoja. Hivyo usione mtu anatoa kitu ukachukulia kirahisi na kusema anazo! wenzie wanazo na zaidi na bado wagumu na wanatamaa ya kupoka na kupeleka nje, kuhonga wanawake nk. Hayo yaliyo moyoni mwake na nia yake kisiasa si juu yetu, Mungu ndiye anayesoma ndani ya kila mmoja wetu. Pia sifurahii mtu kujihurumia maana kama mapiato lika mtu anapitia na wengine ni zaidi sio vizuri kusimama mimbarini na kusema hayo. Tatizo siku zote watumishi wetu wanaotulea wanashundwa kumwandaa mtu aseme nini. wewe toa sadaka yako, na kiri wokovu wako, mengine ni juu yao kuku judge kama uko sawa au. Kwa vile kila kmtu anafahamu kwa sehemu yake. ninachopinga ni watu kumkashifu anapotoa misaada au sadaka kwa kusema ni mnafiki au hafai ka hiki au kile, msimkatishe tamaa, wokovu ni safari ndefu anahitaji pia walezi wazuri wasio na woga na mtu. Ni hayo tu kwakweli tuko pamoja.

 8. “MUNGU YUPO NA MIMI NITAYASHINDA MAJARIBU”…..

  Ninavyofahamu mimi Majaribu ni mitihani au mitego ambayo shetani anamtegea mtu ili amkosee Mungu. Kutokana na maana hiyo MIMI SIJAELEWA NI MAJARIBU YAPI AMBAYO MPENDWA LOWASA AMEJARIBIWA KUMKOSEA MUNGU? Yaani na baada ya kujaribiwa hivyo HAKUMKOSEA MUNGU? Na kama kweli “kuna majaribu anapitia” Je!, ni ya KISIASA au ni ya KIIMANI?

  Kwa dada yangu mpendwa Rose,

  Kwa watu walioko CCM, kama kwa ndugu Lowasa, HAKUNA AMBAYE SI MNAFIKI NA MWOGA. Ni sasa hivi baada ya KUONA MAJI YANAELEKEA SHINGONI ndiyo wanaanza kutoa siri, japo kwa tahadhari kubwa, kubwa sana! Maana akishaongea mahali kama hapo baadaye utawaona wanacheka, hao hao wanaorushiana maneno kwenye mikutano na vyombo vya habari, na meno yote nje wakipanga mikakati mingine ya kichama…… Kama siyo unafiki ni nini?

  Kuna wimbo fulani nilitunga, wenye beti mojawapo lenye maneno yafuatayo:

  Haki itakufukuzisha kwenye vikundi vya biashara,
  Kwa sababu hufanyi magendo wa la hutoi rushwa,
  Utafukuzwa kazini kwa kusema ukweli,
  Halafu waongo wanazidi kuongezewa vyeo”

  Hakuna mtu mkweli anaweza kukaa CCM, sasa! Hakuna mtu jasiri anaweza’kaa CCM. Hakuna! CCM ukisema ukweli huwezi kubakia. Yupo mbunge wa Mbarali ameingia kwenye misuko suko mingi hadi kuwekwa ndani, kwa sababu tu ya kusema ukweli. Yupo Luka Seleli, kule Nzega, baada ya kuanza kusema ukweli akaonekana hawezi KUKISAIDIA CHAMA, akawekwa pembeni. Kwa kifupi kila mtu ambaye anayeonekana KUFUATA HAKI na KUKATAA UOVU huyo huonekana ni ADUI na HAWEZI KUKISAIDIA CHAMA cha Mapinduzi!

  Wanapopata nafasi ya kuongea kwenye mikusanyiko ya kidini ni mafundi sana wa ku-quote maandiko. Wengine hu-quote kutoka kwenye quran na wengine kwenye Biblia. Tulishuhudia sana mheshimiwa Makamba aki-quote mara nyingi sana kutoka katika Biblia. Inashangaza halafu kwa upande mwingine inatia huruma! Maana wanayajua maandiko lakini wanachagua ya kwao yanayowatetea wao na kuyatumia hayo.

  Kinachoniuma mimi KIWANGO CHA UWAJIBIKAJI TANZANIA NI KIDOGO SANA! Umakini katika jambo lolote ni mdogo mno! Taifa linalia. Kila kona ni kilio. Ikulu inapitisha maamuzi ya ajabu. Wizarani kunakubaliwa mikataba yenye maangamizi kwa wananchi. Mikoani kunafujwa pesa ambazo zingekwenda kwa wananachi zingebadilisha maisha yao. Wilayani kuna mbinu nyingi za kudanganya kuwa kilichopokelewa toka mkoani kimetumika. Kwenye Kata na Tarafa kuna upotoshaji mwingi wa haki. Kwenye vijiji kuna madudu mengi ambayo viongozi wa vijiji wanafanya kwa kujua au kutokujua.

  Majuzi, katika kuzunguka zunguka nchini, nilikutana na mtendani mmoja wa Kijiji fulani katika Mkoa wa Singida, Nikawa namuulizia ulizia kama anafuatilia mambo ya nchi yanavyokwenda. Nilimueleza kama anataarifa kuwa Nape Nnauye alipatwa na “presha” siku ya kesi yake kule Arusha ilipofika? Yule mtendaji kwa mshangao aliniuliza… “Nape ndiye Nani….?” Nilimwangalia kisha nikamhurumia. Nilimjibu lakini nikampa somo kuwa Atafute muda awe anasikiliza/tazama taarifa za habari kwenye TV badala ya muziki tu, kama ambavyo watu wengi Tz wanavyofikiria TV ni kwa ajili ya kuangalia muziki tu.

  Sasa kama mtendaji wa Kijiji, serikali ya Chama Tawala hajui Katibu Mwenezi wa Chama Tawala chake, Je! Kuna matumaini tena kwa wanakijiji? Cha kusikitisha hawa viongozi ndio huwa mstari wa mbele kuwashawishi watu WACHAGUA CCM kwa kuwa Ni cha Makini, Chama cha Enzi na Enzi. Kumbe wao wanachofukuzia pale ni shilingi mbili-tatu walizowekewa mifukoni mwao. Si viongozi wa wananchi bali ni viongozi wa matumbo yao.

  Hali hiyo imedumaza waTz wengi, hasa waliokata tamaa ya maisha. Wako tayari kubebwa na kimbunga chochote cha kisiasa ili mradi tu kimbunga hicho ndani yake kimebeba japo pesa ya kununulia vipande kadhaa vya sabuni ya mche na vibaba vichache vya mafuta ya taa!

  Kutokana na hali hiyo, WATU WENYE FEDHA NYINGI, ambao kwa sasa siyo siri tena kuwaita MAFISADI, wanapotoa michango kama vile alioutoa mheshimiwa Lowasa HAO HUONEKANA KAMA MIUNGU. Hata wanapotumia maandiko ya Biblia si wengi wanaweza kutafakari kama maandiko hayo yaliyonukuliwa yanaendana na hoja hiyo iliyozungumziwa. Ni watu wanaoheshimwa, watu wanaoonekana kama vile Pesa ya Tanzania NDIYO HAKI yao na wengine hawana Haki ya kumiliki pesa au utajiri huo wa Taifa!

  Lakini jambo linalosahaulika na muhimu sana kama waTz wangetafakari ni hili kuwa Mtu mmoja anatoa shilingi milioni 10 kwenye harambee moja na kwa mwaka utakuta anafanya hivyo mara kadhaa, Je hiyo pesa inatoka wapi? Je, ni kweli anatoa kwa kuwa ANAUCHUNGU NA KAZI YA MUNGU ANATOA KWA KUWA ANAZO?

  Bahati nzuri Yesu, mwalimu wa Kweli na wa Haki, alishatuhakikishia kuwa linapokuja suala la Utoaji kwa Mungu, Mungu huwa haangalii WINGI WA KILICHOTOLEWA bali NIA iliyoko nyuma ya utoaji huo na kilichotolewa ni kiasi gani ya anachomiliki mtu!

  Watu wachache Tz wamemiliki fedha na utajiri ambao kama ungegawia kwa haki nchi isingekuwa hapo ilipo. Kwa hiyo wanapoitwa kwenye harambee hivyo WANATOA AMBACHO WALISHAFICHA SIKU NYINGI. Kile ambacho kingefanya, mfano kanisa hilo liwe limeshakamilika siku nyingi, kama kila mtu angekuwa analo fungu lake lililofichwa, anakitoa kwa JINA LAKE lakini kumbe kilikuwa ni cha wote! Wanachukua sehemu kidoooogo na kurudisha kwenye umma kupitia harambee kama hizo na kuendelea kujenga UTUKUFU WAO.

  Kama mheshimiwa Lowasa angekuwa jasiri, ANGEYASEMA HAYA ANAYOYASEMA SASA wakati alipojiuzu [sijuwi ni kujihudhulu…., kiswahili tu lakini]. Mwingine alipohojiwa kwa nini hakusema aliyayosema kama mwezi uliopita alisema “alikuwa anaogopa kufukuzwa kutoka katika chama”. Wengine walisema “kama tungesema kila kitu, Serikali yote ingekufa…” Maana yake ni Kuwa hakuna MSAFI CCM!

  Niiishie hapo kwa upande huo….

  NIkirudi kwenye suala la Mh. Lowasa, kama kweli ametubu basi Mungu ameshamsaheme. Kusamehe ni kazi ya Mungu. Lakini kama amesema hayo kwa unafiki Mungu pia anajua. Kwa hiyo ni kazi kwake yeye mwenye kama ameamua kutengeneza maisha ya rohoni ki kweli kweli au anatangaza maneno hayo ili AJISAFISHE KISIASA…anajua mwenyewe. Maana shahidi wa mambo ya mtu ni mtu mwenyewe! Nafsi yake inafahamu.

  Na si lazima kama ameamua kutubu AWE RAIS, Suala la toba kwa Mungu halihusiani na urais. Kama ingekuwa hivyo basi wote watatubu ili kila mtu awe rais. Kutubu ni muhimu tu hata kama mtu hagombei japo ubalozi wa nyumba kumi!

  Ni maombi yangu kuwa Mungu afungue macho ya viongozi wote wa kitaifa, KWELI na Nuru iingie ndani mwao ili ILETE HAKI, HAKI ambayo italiinua taifa hili kwa kuwa Raslimali za Taifa zitagawiwa kwa wananchi wote kwa HAKI!

  Namalizia mchango wangu na maandiko hayo kutoka katika Isaya 55:6-7

  Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana,
  Mwiteni, maadamu yu karibu.
  Mtu mbaya na aache njia zake,
  Na mtu asiye haki aache mawazo yake,
  Na amrudie BWANA,
  Naye atamrehemu,
  Na arejee kwa Mungu wetu,
  Naye atamsamehe kabisa!

  Amina!

 9. Kampeni zinaendelea, nami naendelea kujifunza. Utabiri haujawahi kuwepo nami nina mashaka na kutumia “madhabahu kujisafisha” badala ya “kutubu”.

  Swali moja naomba kuuliza. Je mtoto wako wa kumzaa akiwa jambazi na amewahi kufanya ujambazi nyumbani kwako. Siku ya siku anakuambia ametubu na kuacha kabisa na anaomba arudi hapo nyumbani; JE UTAMRUHUSU KURUDI? Na kama jibu ni ndiyo JE UTAISHI NAE KWA KUMCHUKULIA KAMA VILE ZAMANI KABLA HAJAWA JAMBAZI?

  Tujadiliane.

 10. Ndugu Johanes,

  Naomba kukuuliza maswali yafuatayo, Je Yesu alichukua mwili huu wa nyama na damu kwa ajili ya nini na kwa ajili ya nani? (Waebrania 2:14-15).

  Je Mungu amekueleza wewe kuwa kwa dhambi za Lowasa hawezi kumsamehe kamwe?

  Nini maana ya Yesu kuja hapa duniani kwa ajili ya dhambi zetu kama hata tukitubu hatusamehewi?

  Nini maana ya neno ufisadi? Je limefungwa kwenye mambo ya siasa tu? Na je dhambi hii ya ufisadi haisameheki hata kama yule aliyeifanya atatubu?

  Haya ni baadhi tu ya maswali mengi sana ambayo nimejiuliza baada ya kusoma comment yako.

  Barikiwa na Bwana.

 11. Shalom
  naweza onekana vingine kabisa, si kwasababu sijui ametabiriwa, ni Mkristo au nini ila mie kwa upande wa CCM naona bora huyu! Maana kukataliwa na Myerere ilikuwa anaamini ujamaa na alihoji utajiri (mifugo mingi) aliyokuwa nayo Lowassa. ajabu ni kuwa alipomweka Mwinyi alitangaza azimio la Zanzibar na kufuta ujamaa… Sasa Tanzania ni ubepari kila kiongozi analipwa hela nyingi sana na je anafanyia nini? kwa vile huyu hana kuoa kila kukicha na anaubunifu wake kumiliki sio sababu kwamba wengine hawaibi, na je hela yao mbona ngumu kuitoa kwa masikini? na je huyu kasema wazi alivyohusika na kila hatua je wengine mbona hawasemi? kuna kamati zilificha ukweli ila wanaitwa mashujaa na watu ndio wanasema wanafaa kuwa raisi! Tuwe wakweli na tuache kumnyooshea kidole, kama ni dhambi kuna isiyooshwa kwa damu ya Yesu? wakati wa uongozi wake tumeshuhudia maamuzi mengi magumu akifanya bila woga, hawa wengine ni wanafiki tu na waoga, tunahitaji mtu shujaa sasa, labda nimwone mwingine baadae, lakini hawa wanaosema tupokee misaada na Kurani tutupe mmmm. Tumuombe Mungu tu na tusimtweze Roho Mt kwa kupinga bila sababu. Ni mtazamo wangu tu.

 12. Lowasa Edward Ngoyayi akiwa Rais wa Tanzania mambo 10 yafuatayo yatatokea:

  1. Mfumko wa Bei utashuka kutoka 17% ya sasa hadi 5% ndani ya miaka 5 ya mwanzo

  2. Thamani ya Shiilingi ya Tanzania itaimarika zaidi dhidi ya sarafu za nje hasa Dollar ya marekani na Yuro ya Ulaya.

  3. Shule za Sekondari zote za Kata alizoziasisi zitapata mabweni, Maabara, Vitabu, Walimu, Mdawati na Vifaa vyote muhimu ndani ya Miaka 2 ya mwanzo.

  4. Uchumi utakua kwa kasi kama ya ndege inayotaka kupaa angani kama enzi za Mkapa. Kumbukeni wakati ule wa Mkapa uchumi ulitaka kupaa ila baada ya Mhe. Kikwete kuingia Ikulu, ile ndege iliyotaka kupaa kama alivyosema Mkapa iliamua kuahirisha safari.

  5. Lowasa akiwa Rais wa Tanganyika na Zanzibar muungani wetu utaimarika zaidi. Natamani tuwe na Serikali Tatu. Kama serikali 3 haziwezekani basi Bora tuwe na Serikali MOJA yenye nguvu kiuchumi. Tuwe na Rais aliye na nguvu pande zote visiwani na Bara.

  6. Lowasa akiwa Rais wa nchi hii, Reli ya Kati toka DAR – KIGOMA/MZA itatengenezwa kwa kasi ya hali ya juu. Ndani ya miaka 3 ya mwanzo Reli itakuwa iko saaaafi sana.

  7. Lowasa akiwa Rais wa Nchii hii, uwajibikaji katika ofisi za umma, serikali na Binafsi utaongezeka kwa kasi. Sasa hivi Bara na visiwani uwajibikaji wa kazi umepungua sana. Watu wengi wanafanya dili za fedha tu bila kuchapa kazi. Lowasa si unamjua anavyowaka hapo hapo na kuwawajibisha wazembe bila kusubiri maamuzi ya vikao na taratibu na kanuni za kazi. Ukivurunda hapo ulipo anakuwasha vibao na kibarua kinaota miguu.

  8. Lowasa akiwa Rais, waislam na wakristo wataheshimiana na wataweza kufuata maadili ya dini zao. Rais akiwa Lowasa Makamu wake atakuwa Mwislam na Waziri Mkuu atakuwa Mwanamke mama Anna Tibaijuka (Professor).

  9. Lowasa akiwa Rais, ufisadi utaendelea lakini kazi mahala pa kazi zitaonekana na maendeleo yataonekana kwa haraka na uwajibikaji utaonekana kwa haraka. Kwa sasa ufisadi upo, uwajibikaji hakuna, kuwajibika au kuwajibishwa hakuna. Lowasa akiwa Rais watu siyo kwamba hawatafanya ufisadi wa mali za umma ila naamini nidhamu itakuwepo. Hata kama yeye anasemwa kuwa ni fisadi, lakini kazi zake kama waziri Mkuu tuliziona. Tatizo ni kwamba wengine ni mafisadi tuuuu ambao kazi yao ni kufukuzia dili za pesa kila kukicha, kazi za maendeleo hawafanyi. Kumbuka Mkapa alivyokuwa mchapa kazi. Kuchapa kazi hakumwondoi kuwa fisadi. Lakini watu hawatamsahau kamwe kwani aliweza kuushusha mfumko wa bei kutoka asilimia 40% mwaka 1995 hadi 5% mwaka 2005. Lowasa akiwa Waziri Mkuu Maamuzi magumu ya kuwajibisha wazembe aliyatekeleza na ndiyo maana na yeye aliamua kujiuzuru ilipotokea kashifa ya Richmond.

  10. Lowasa akiwa President wa URT wanafunzi wa elimu ya juu wote watapewa mikopo bila ubaguzi wala bila hata mmoja kubaki kwa visingizio vya bajeti ya serikali kuwa ndogo. Unakumbuka alivyoshawishi mabenki mwaka 2007 yafute vikwazo vya utoaji mikopo kwa wajasiliamali waliokuwa wanaomba mikopo ile ya mabilioni ya JK? Mabenki yalikuwa yamegoma yakitaka DHAMANA ZA MIKOPO hiyo iwe viwanja vya nyumba, Lowasa akakataa kwani kulikuwa na dhamana ya serikali. Lowasa akiwa Rais, atashawishi Mifuko ya Pensheni, LAPF, PSPF, NSSF, PPF, GEPF, ZSSF iweke utaratibu wa kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu kama alivyoishawishi yote kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma -UDOM. Kile chuo kimejengwa kwa fedha za kutoka Mifuko hiyo ya pensheni nchini na siyo wafadhili. Aidha, atashawishi mabenki yote ya biashara kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wanafunzi wote wanaokidhi vigezo vya kusoma elimu ya juu.

  Hayo ni baadhi tu ya yale yanayotarajiwa ikiwa Lowasa atagombea kuwa Rais na akashinda wapinzani wake wa kisiasa. Lowasa hata kama anatafsiriwa kuwa mchafu ni kwa sababu tu aliamua kujiuzuru. Hii haina maana kwamba wale ambao hawakujiuzulu walikuwa WATAKATIFU. Hivi kuna mtu wezaye kuwa Mtakatifu huku akiwa mwanasiasa?

  LOWASA EDWARD NGOYAYI, SONGA MBELE, MUNGU IBARIKI TANZANIA. HATA KAMA HUTAKUWA RAIS WA NCHI HII, WENGI TUTAKUKUMBUKA KWA MICHANGO YAKO YA MAENDELEO KWA NCHI HII NA WATU WAKE HASA MAKANISA/MISIKITI HATA KAMA UNGEKUWA FISADI WA VIPI?

  LOWASA EDWARD NGOYAYI WEWE NI POOA SANA. UNYENYEKEVU WAKO SIYO TU KWAMBA UTAKUKWEZA BALI PIA UTAKUOKOA MILELE.

  WATU WA KIGOMA TUNAKUKUMBUKA SANA ULIVYOSAFIRI KWA GARI TOKA BIHARAMULO-KIBONDO-KASULU, NGURUKA- UVINZA TABORA ILI KUANZA MCHAKATO WA KUTENGENEZA BARABARA YA LAMI TOKA KIGOMA HADI DODOMA. SONGA MBELE.

 13. ”Niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua”Yeremia 33:3.
  Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache, Math.22:14

  MUNGU IBARIKI NCHI YETU TANZANIA.

 14. Fedha ni shetani mkubwa tena anaweza hata kusababisha Mungu akasahaurika kwa watumishi wake na kukalia kumwabudu aliyemchafu mwenye kutumia jina la Bwana vibaya ili tu apate madaraka,mithili ya maskoofu wa kitanzania kupenda fedha na kuwanza kumsujudu Lowassa kwa kusema yeye ni ni msafi eti ana Mungu moyoni mwake na wakati hata kichanga(MALAIKA WA MUNGU) wanamfahamu Lowassa si msafi toka enzi za kale hata nyerere alimyoshea kidole,ndugu maskoofu mmefikia hatua mfananishwe na Mwanafunzi aliyemsaliti Yesu na hatimae kumtia mikononi mwa wayahudi!! Acheni unafiki nyie watumishi wa Mungu mtaingiza Taifa kwenye machafuko makubwa kama mtakalia kujifanya mmetumwa na Mungu kusafisha waliolitia Taifa kwenye umaskini na kutengeneza matabaka!KAENI NA KUJUA KAZI YENU NI KUOMBEA TAIFA AMANI WALA SI KUFANYA MIKUTANO YA KISIASA, MUMEPOTOKWA NA MISINGI YA KAZI YENU,WAHURUMIENI WATANZANIA NA MSIDHANI FEDHA MNAZOPEWA NI BORA ZAIDI YA AMANI…Dhahiri nimeamini maneno matakatifu yasemayo si wote waniitao Bwana Bwana watauona ufalme wa mbingu!hata nyie maskoofu kaeni mjitathmini vizuri, siwatukani bali uchungu wa kuona amani inavyoelekea kupotezwa nanyi imebidi niwakumbushe wajibu wenu,MUNGU NIBARIKI,MUNGU IBARIKI TANZANIA,MUNGU IBARIKI AFRIKA. AMENI

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s