Ufanyeje Ili Maono Uliyoonyeshwa Na Mungu Yatimie?

Habakuki 2:2Bwana akanijibu, akasema, iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye atake kuisoma kama maji, maana njozi hii ni kwa wakati uliomriwa, inafanya haraka, ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; Ijapo kawia ingojee, kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Ndugu zangu, leo tunalo somo lisemalo kuwa, UFANYEJE ILI MAONO ULIOONYESHWA NA MUNGU YATIMIE? Mungu wetu husema nasi kwa njia mbali mbali, kwa ndoto, kwa maono, kwa Neno lake, kwa kutumia Watumishi wake, Malaika, viumbe mbali mbali, hata Punda, n.k. Na akiishasema nasi kuna vitu ambavyo tunatakiwa kufanya ili yapate kutimia yale aliyosema nasi. Kuna wengine akiishasema nao, muda mrefu hupita; wakingojea na  kungojea, na hata wakati mwingine wengine huwa wanakufa bila kuyaona yakitimia. Lakini tunajua kuwa Mungu wetu kamwe hawezi kusema uongo, yeye akiishasema ni lazima atimize yale yote aliyoyasema.

Katika somo hili nitakupatia mambo mbali mbali ambayo unatakiwa kuyafanya ili usababishe yale ulioambiwa yapate kutimia. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

1.Liandike neno hilo ambalo Bwana Mungu amekwambia. Andika kwenye daftari, kitabu au mahali popote ambapo halitapotea. Litunze mpaka hapo litakapotimia. [Hab 2:2].

Dan 9:2  “Katika mwaka wa kumiliki kwake, mimi Daniel kwa kuvisoma vitabu, nilifahamu hesabu ya miaka, ambayo Neno la Bwana lilimjia Yeremiah Nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalem, yaani  miaka sabini

Unaona hapo! Nabii Yeremiah aliandika kile ambacho Bwana Mungu alikuwa amemuonyesha, na Daniel aliposoma alifahamu miaka. Na wakati anasoma kufahamu tayari Israel walikuwa wamekaa utumwani miaka 30 zaidi ya walivyokuwa wametakiwa kukaa. Kwa hiyo tuhakikishe kuwa tunaandika yale Bwana anayosema nasi.

2. Jenga Madhabahu baada ya kuwa Bwana amesema na wewe.

Mwanzo 8:20-21 “Nuhu akamjengea Bwana madhabahu, akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliyesafi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu, Bwana akasikia harufu ya kumridhisha. Bwana akasema moyo moyoni, sitalaani Nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya mwanadamu maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai, kama nilivyofanya.”

Katika Biblia imeandikwa, MHESHIMU BWANA KWA MALI ZAKO. Mungu akiishasema na wewe unafanyaje? Maana unatakiwa ushukuru kwa kile ulichosikia akikuambia, yaani kwa vyovyote utasema asante, sasa unafanya nini ili kuonyesha hiyo asante yako? Nuhu alipotoa sadaka hiyo harufu ilimfikia, na unaona akamfanya Mungu aseme maneno, aahidi kutoharibu dunia tena kwa maji!

Mwz 28:16-22 “Yakobo akaamka katika usingizi, akasema kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua, naye akaogopa akasema, mahali hapa panatisha kama nini, bila shaka hii ni nyumba ya Mungu. napo ndipo lango la Mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake. Akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake, akaita jina la mahali pale Betheli, lakini mji huo hapo mwanzo uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae, nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu, na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe fungu la kumi”

Ninachotaka tujifunze hapa ni kwamba mtu yeyote mwenye akili timamu anaposemeshwa na Baba yake hawezi kukaa kimya tu bila kufanya chochote, bila kusema chochote. Unaona hapo, baada ya Mungu kusema na Yakobo, ilibidi Yakobo asimamishe Jiwe lile, akalimiminia mafuta. Haikutosha hiyo akatamka akitoa Nadhiri kuwa kweli Mungu akinilinda akanipa nguo, akanipa chakula, nikarudi salama, NITAMTOLEA FUNGU LA KUMI KWA KILA ATAKACHONIPA. Pia aliiheshimu mno mahali pale, akapaita LANGO LA MBINGUNI, Nyumba ya Mungu.

Kumbuka, ni mara ngapi watu wengi wanahudumiwa na Mungu katika Madhabahu mbali mbali, na kesho yake yule mtu huondoka na kuendea madhabahu zingine mbali mbali. Nikupe angalizo hapa kuwa angalia madhabahu ambayo BWANA alikutana na wewe, aliyosema nawe.  Wengine hawapo kabisa, Pengine alisema nawe ukiwa  THIATIRA, lakini uliishasonga leo upo  FILADEFIA. Soma vizuri maandiko. Unafikiri ni kwa nini Biblia inasema “kwa Kanisa la THIATIRA Andika. . .! “; “Kwa kanisa la FILADEFIA  Andika. . . .”

3. Usimshirikishe kila mtu hayo Mungu aliyokuambia.

Watu wengi kwa kutokuelewa, tumefikiria kuwa ni sawa kumshirikisha kila mtu tunaye kutana naye, maono au ujumbe aliotuambia Mungu. Hii si sahihi. Kuna madhara makubwa sana kwa jambo hili. Ngoja nikueleze na ninaamini utaelewa:

Zab 69:4  “Wanaonichukia bure ni wengi kama nywele za kichwa changu”.

Naomba nikukumbushe, uwe unajua au hujui, maadui zako ni wengi kama nywele zako.,Huwawezi kuwajua wote. Hivyo ukimwambia kila mtu utajikuta umeshamwambia hata adui yako maana huwajui wote.

Mwanzo 37:5-8 “Yusuph akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia, akawaambia, Tafadhalini sikieni, ndoto hii niliyoiota, Tazama sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama miganda yenu ikazunguka, ikainama mbele ya mganda wangu, Ndugu zake wakamwambia, Je kweli wewe utatumiliki sasa? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake na kwa ajili ya maneno yake”

Fuatilia uone shida zilizompata baadaye. Kwa usalama wako, usimwambie kila mtu maono yako, au jinsi Mungu anavyotaka kukufanyia. Wengine hujifanya rafiki, lakini ukweli ni kwamba ni WACHAWI. Wanakuja kwako kutafuta wakulogeje. Ninaamini kuwa hakuna uchawi kwa mtu wa Mungu! Lakini unapokuwa umemshirikisha mtu ambaye hakutakii mema, mtu ambaye ni adui yako bila wewe kujua, utakuwa unahatarisha maisha yako yote: ya Kiroho, na ya Kimwili pia.

1Kor 4:1-2 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu, hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ni mtu aonekane kuwa mwaminifu”

Hapo juu mtume Paulo anaeleza kuwa Mungu wetu anazo siri zake, ambazo huwafunulia watu kadhaa, si watu wote. Sasa anapokuwa amekufunulia, au ameamua kukufanyia jambo hamwambii kila mtu. Hukuambia wewe tu na unachotakiwa kufanya ni kutunza siri hiyo, maana si kila mtu atakayekuelewa.

Mifano

Mariamu: Malaika alimwambia Mariamu kuwa atazaa mtoto BILA MUME,  Kama Mariamu angeondoka hapo awe anamwambia kila mtu kuwa una habari?mimi nitazaa mtoto bila mume! “. .   Fikiri ingekuwaje?

Petro: Aliitwa na Yesu atembee juu ya maji amfuate na Petro akaweza kutembea. Lakini kama angemuuliza Marko, au Mathayo,  au Yuda, swali kuwa “Yesu ananiita niende kwake juu ya maji, mnanishaurije?” Unaonaje, angepewa jibu gani?  Wengine wangemwambia wala usijaribu, utazama, huwezi! Unaona? Hiyo ni kwa sababu Si wengi wanaojua au wanaweza kujua kile alichokuambia Mungu au kile alichokuahidi. Kwa hiyo kama Mungu hajakuambia umwambie na mtu mwingine basi Tunza siri hiyo!

1Kor 1:26 “Kwa maana ndugu zangu angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye Hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa”

Unaona Biblia inajieleza kuwa si wengi wanaoweza kuelewa kile utakachokisema, wengine mpaka yaje yatokee wayaone ndipo waamini maana hawaenendi kwa Imani, bali wanaenenda kwa kuona, hata kama wameokoka. Wengine ni wakatisha tamaa wazuri kweli. Wengine ukiwaeleza ni kuwafanya watamke kinyume cha vile unavyotegemea kwa kuwa hawawezi kabisa kuelewa unachowaambia. Ukichanganya yote hayo unaweza kuona kuwa matokeo yake hayawezi kuwa mazuri.

Lakini kuna mtu ambaye anastahili au anafaa kuambiwa au kushirikisha jambo ambalo Mungu amekuambia: Gal 6:6 “Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote” Mkufunzi ndiye mtu pekee ambaye nitakushauri umshirikishe mambo yako. Nasema mkufunzi kwa kuwa hufundishwi na kila mtu. Kama unafundishwa na kila mtu nakuonea huruma maana huyu atakuambia hivi, yule naye atakuambia hivi, na mwingine naye atakwambia vile na mwisho wa siku utatembea kama nyoka!

Malaki 2:7 “Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa,tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake, kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi” 

Mpendwa, kuna wajumbe wengi. Wapo waliotumwa na watu mbali mbali, wapo waliotumwa na vitu mbali mbali. Lakini wako WAJUMBE WA BWANA WA MAJESHI. Hao ndio wanatakiwa kutufundisha sheria za Bwana, hao ndio tunatakiwa kutafuta maarifa vinywani mwao. Na hao ndio tunatakiwa kuwashirikisha kile tulichoambiwa na Bwana, na wao watatushauri, watatuelekeza kwa usahihi jambo la kufanya.

4. Mkumbushe Bwana kile alichokuambia kuwa atafanya.

Isaya 43:26 “Unikumbushe, na Tuhojiane, eleza mambo yako, upate kupewa haki yako” Bwana wetu ni Mungu asiye sahau kamwe. Sasa anaposema unikumbushe hana maana kuwa huwa amesahau, huwa anataka kuona kama unajua haki zako, anataka uzitaje, na ukumbuke kuzitaja bila kizidisha, bila kupunguza. Maana ukipunguza basi hawezi kufanya maana hakusema hivyo, ukizidisha hawezi kufanya pia maana hakusema hivyo. Kama vile alivyoweka ulinzi katika Biblia ili mtu asipunguze, wala asiongeze, ndivyo anaangalia kwa bidii kile alichokisema ili kisipunguzwe wala kuongezwa. Ndiyo maana nasisitiza kuwa Mungu anaposema nawe hebu andika vile vile alivyo sema, bila kuongeza wala kupunguza chochote.

Kumb 4:2 “Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu niwaamuruzo” 

Mith 30:6 “Usiongeze neno katika maneno yake, asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo”.

Uf 22:18-19 “Namshuhudiza kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, mtu yeyote akiyaongeza, Mungu atamuongezea hayo mapigo, yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu yeyote akiondoa lolote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamuondolea sehemu yake, katika ule mti wa uzima, na ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki”

Namalizia somo hili kwa kusema kuwa Mungu wetu ni mwaminifu ambaye kamwe hawezi kusema uongo, lolote alilolisema lazima alitimize, ila tunachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wetu. Tukitimiza wajibu wetu yeye atatimiza wajibu wake kulingana na lile alilotuambia kuwa atatimiza au atatufanyia.

Nawatakia kila la heri katika safari yetu ya kuelekea kwetu nyumbani kwa Baba yetu, kwenye raha ya milele.

Ndugu yenu Mch. Samuel  Imori.

Advertisements

9 thoughts on “Ufanyeje Ili Maono Uliyoonyeshwa Na Mungu Yatimie?

 1. Amen, Ubarikiwe na Bwana Mtumishi kwa Ujumbe mzito wenye kutosogeza kutoka tulipo kwenda hatua nyingine.Jina la Bwana LITUKUZWE

 2. Ubarikiwe mtumishi ni kweli jambo hili linawasumbua wengi kwakuto fahamu! Lakini nadhani umetufungua macho

 3. Amen, ni somo zuri sana

  Tatizo linasumbua wengi hatuna utulivu au hatuombi hekima na uongozi wa Roho wa Mungu jinsi ya kutendea kazi maono au ufunuo uliopewa,

  Mfano;
  1) Umepewa kuonyeshwa fulani hakufai atakuharibia jambo in future, basi utakuta mtu anaanza vita ya mwilini, anamchukia mtu n.k

  2) Umeonyeshwa madhaifu ya mtu unaanza kumtangaza, badala ya kumuuliza kwa nini Mungu kakuonyesha? Inawezekana kakuona upo katika nafasi nzuri ya kusimama na kuomba kwa ajili yake, lakini wewe badala yake unaanza kutangaza.

  3) Umeonyeshwa fulani ni mke wako au mume, unaanza kukurupuka na kuanza kusumbua watu ambao Bwana hata bado hajasema nao.

  Ndio maana wengi leo wamepoteza neema yao ya kupokea maono kama zamani, sababu hawatafuti hekima na uongozi wa Roho Mtakatifu kwanza. Vinywa vinatuponza wengi, hatujui kutunza siri za Mungu.

  Nina amini kabisa miongoni mwa vitu vinavyodhihirisha ukaribu wako na Mungu ni kiwango ambacho Mungu anakupa maono juu ya mambo fulani ya kutokea mbele, hataacha kila jambo liwe kama suprise kwako.

  Mbarikiwe

 4. Bwana asifiwe ndugu Mch Samuel Imori

  Kweli nimesoma fundisho lako juu ya neno ama Ndoto ama maono ulipoona itimilike . mimi niko na ndoto ni ndefu sana na taka kukueleza kupitia Simu kama unaweza kunipa Namba yako ya Simu mimi nikupigiye na nikujulishe vile Ndoto yangu adi kufikiya Maono na niko na liya juu ya neno fulani

  Mungu akubariki

 5. BWANA ASIFIWE

  Akisat sana Mch Samuel Imori Kwa somo iyi ya kunichenga kiroho.Kweli kufatana vile unapohandika juu ya madui zetu wako kama nywele za kicho zetu . Sasa juu yangu mimi niko na Ndoto na Ikafika maono ile ile usiku na bibi niko karibu yangu iko na sikiya vile niko NALIYA juu ya jamaa yangu . mambo iyi inepopita karibu miaka 15 zaidi Nililota nimeona jamaa yangu iko kunyumba yetu iko wazi ata mutu iko na lala ukipita barabarani unamuona wasi Malaika akanishika mukono akasema nami acha wao kuja apa tuende kanisani tukabishana naye sana na niko NALIYA juu ya kupoteya ya jamaa langu kisha Malaika akanipeleka kwa Kanisa enye nalikuwa na shiriki akasema apa ndio kwako acha wao. Ile Ndoto na ginsi ili geuka kuwa Maono kabisa ata wakati ninapoandika iyo mambo yote yana kuja kwa akili yangu siwezi ata siku moja kusahau.Kweli ile siku naliliya sana mupaka ikaonekana wazi kimwili na Bibi yangu akashangaha sana na nikamueleza.sasa leo Mch Samuel kila siku niko na omba juu ya jamaa yangu miaka iyi bibi ya mzee kama vile mama mdogo siri ikatoka ndani ya kama iko MUCHAWI sio mimi nilisema mtoto moja alimupa Dawa akuje karibu na mimi na nika mutuma kwa Pasta moja achunge pale apo ndio dawa iyo ilipoteya mambo iyi ilipita miaka 2010 na mimi mwenyewe nika muona mama ule tuka fanya baraza juu ya mambo iyo akasema kweli mimi sio muchawi lakini na juu mbele ya kukamatana na baba yenu nalimufanyiya Dawa ya mapenzi juu anipende sana ile alisema mbele ya watoto wake wanaposikiya na Mzee pamoja . sasa swali langu ni iyi kila maombi na oombe jamaa lango ama nifanye nini juu BIBLIA inasema Ombea ata wadui zako. naomba ushauri kwako

  Mungu akubariki

 6. shalom mtumishi
  ni somo zuri sana maana wengi tunaomba na tunaonyeshwa kweli maono ila kutunza haya maono hadi yatimie ni kazi sana au tunakuwa tumekosea ktk kufasiri hayo maono. Ngoja niipitie vizuri hii na kuifanyia kazi nitarudi tena, Barikiwa

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s