Wa mabondeni warudishwe kijijini – Mchungaji

MCHUNGAJI wa Anglikana jijini Dar es Salaam, Obedi Ntigogozwa, amesema Serikali inapaswa kuwasafirisha kwa mabasi waathirika wa mafuriko waliojenga mabondeni na kuwapeleka vijijini kwao kama ilivyofanya kwa ombaomba wakati Mkuu wa Mkoa akiwa Yusuf Makamba.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Ntigogozwa alisema huruma ya Serikali imepitiliza kwa kuwa mara kadhaa wamepigiwa kelele ya kuhama katika maeneo hayo lakini wamekaidi amri hiyo.

Mchungaji huyo ambaye ni Msimamizi wa Makanisa ya Anglikana ya mapokeo ya Low Church (Waanglikana Wakiinjilisti), alisema kwa ukaidi wao, suluhisho pekee ni kuwarejesha vijijini mwao kuendeleza shughuli za kilimo walizozitelekeza na si kung’ang’ania mjini.

Aliishauri Serikali kutengeneza miundombinu bora na kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana huko vijijini ili watu hao watekeleze azma ya Kilimo Kwanza kwa vitendo na kuongeza uhakika wa usalama wa chakula nchini kuliko kuendelea kuhatarisha maisha yao mabondeni.

“Fursa zipo vijijini walikokimbia na kuja mjini na kujenga katika maeneo ya hatari kama ilivyoelezwa na wataalamu.

“Serikali miaka kadhaa iliyopita wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwa Makamba, ilivalia njuga suala la ombaomba wakarejeshwa vijijini mwao na wengi walikuwa wakitoka Dodoma, inashindwaje kwa hawa?” Alihoji Mchungaji huyo.

Alishauri waliogoma kuhama licha ya kupewa maeneo bure huko Mabwepande, wilayani Kinondoni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam waondolewe kwa lazima kwa kupandishwa kwenye magari yatakayokodiwa na Serikali hadi vijiji wanakotoka kwa kuwa hata kupewa
viwanja ni huruma iliyopitiliza.

“Wapelekwe vijijini kuendeleza kilimo, sasa Serikali ina dhana ya ‘Kilimo Kwanza’ wakaitekeleze kwa vitendo huko, wawekewe tu miundombinu sambamba na vifaa vya kilimo na kuimarisha masoko.

“Wakalime tuepuke njaa badala ya kung’ang’ania mahali ambako si salama kwa maisha yao, Mungu kasema kwa njia hii (mafuriko), wanataka nini tena,” alihoji Mchungaji Ntigogozwa.

Aliyataja maeneo yenye rutuba nzuri kwa kilimo ambako alidai baadhi ya waathirika wanatoka huko ni pamoja na maeneo ya Kusini mwa nchi, Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini na kuongeza kuwa mashamba mengi yametelekezwa huku watu wenye uwezo wa kulima, waking’ang’ania mabondeni na baadhi wakijihusisha na utapeli.

Alisema ikiwa Serikali itaona gharama kubwa kukodi mabasi, ifanye harambee kama ilivyofanyika kwa vyakula na mahema sambamba na huduma za maji kwenye makambi ya dharura kwa kuwa anaamini kwamba baadhi ya waathirika waliopewa maeneo hayo mapya, watauza siku si nyingi na kurejea mabondeni.

Hata hivyo Serikali ilishatoa msimamo kuhusu suala hilo kuwa, watakaorudi au kugoma kuhamia Mabwepande, haitahusika na jambo lolote litakalowapata na kwa wanaoishi eneo la Bonde la Msimbazi, watalazimika kuhama kupisha ujenzi wa mradi wa eneo la kisasa la mapumziko.

Ujenzi huo uliwahi kuelezwa bungeni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ingawa alipingwa vikali na baadhi ya wabunge wa Dar es Salaam wakigoma wapiga kura wao kuhamishwa.

Hata hivyo msimamo huo wa wabunge ilikuwa kabla hawajashuhudia gharika hiyo ya mafuriko ya mwishoni mwa mwaka 2011 iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 40 na wengine zaidi ya 5,000 kukosa makazi.

–Habari Leo

3 thoughts on “Wa mabondeni warudishwe kijijini – Mchungaji

 1. BWANA ASIFIWE!Mimi nadhani unapotoa wazo ktk maafa kama haya ukiwakama mtumishi uweumeomba MUNGU akupehekima kwanza iliutoe ushauri sahihi!kwamfano siorahisi namnahiyo kupeleka watu vijijini wengine niwafanyakazi maeneo mbali mbali je ajirazao itakuwaje?nawengine niwatuwaliozaliwa hapahapa mjini hata kijiji hawana asiliyao nihapa hapa miaka nendarudi!nawengiwao utakuta pia ndio waumini wa makanisa kama ya mtoawazo la kupeleka waumini vijijini je vipi waumini wa makanisa waishio maeneo kamahayo!nadhani wazo la serikali limekaa kiakili zaidi wapatiwe maeneo waendelee na shughuli kupeleka kijijini watu wenye shugulizao ningumu kidogo hapa wana vyanzovyao wana watotowao ktk shulembalimbali sijamborahisi sana kwa mtu ambaye hanalolote kule aende kule kutamshinda kabisa!hutakuwa umemsaidia.Halafu kwa sisi watumishi wa MUNGU tukitoa wazo lakienyeji enyeji linaweza likatukosanisha na waumini bila kujua unaweza ukakuta kanisa linapungua kumbe ni jinsi ya uongeaji wako hauna mvuto kwa jamii na usisahau bila kujua hukohuko wapo waumini toawazo lakujenga / kuboresha maisha yao usiwakanyage wengine kesho ndio wauminiwako!umewapeleka kijijini na wewe hutaki kuhudumu kijijini itakuwaje!?na maranyingine tukitoa wazo lisilo sahihi lina tuondolea imani na heshima mbele ya kondoo tunao wachunga!watatukimbia!lamsingi wacha pale ambapo MUNGU ameona wapewe waende na tuwaombee awapeuwezo wajenge na tuwashauri wauminiwetu wajenge viwanja vilivyo pimwa kwawale ambao bado hawajanunua viwanja au walau maeneo ya miinuko,bilakusahau haya ya awamu hii ilikuwa nimaafa hata baadhi ya balozi fulani ziko mjini maji yaliingia au nyumbani kwa REGINALD MENGI sasa wale nao utawaambia waende vijijini?usisahau unapotoa wazo kwamba kuna maafa na kuna hali ya kawaida maafa hataukiwa tambarare utakumbwa tu!MUNGU atusaidie!

 2. Dada Rose,

  Achana na mtazamo huo. Kurudi vijijini siyo suruhisho kwa wakazi wa mabondeni. Katika Jiji la Dar es salaam ambako kila aina ya matatizo hupatikana ni vigumu kuwaondoa watu wakarudi vijijini.

  Hivi tunaposema vijijini kwanza tuna maanisha nini. Mimi naona hata kule Mabwepande walikohamishimiwa ni vijijini. Kijiji kwa tafsiri yangu ni mji mdogo wenye watu wachache labda wasiozidi laki moja. Ni mji mdogo wenye watu wanaoweza kujuana kwa sura. Wanaweza kusaidiana wakati wa misiba au sherehe kwa umoja. Hiki ndicho huitwa kijiji.

  Watu wengi wanadhani kwamba vijiji ni maeneo yasiyokuwa na umeme, barabara za lami, shule na vyuo vikuuu, hakuna magari mengi. Kumejaa wafugaji na wakulima tu.

  Dada Rose anasema ni muhimu tukawa wazalishaji na si kupenda kuwa wauzaji tu na kwamba tuwaombee wafumbuke macho.

  Napenda kuwakumbusha wapendwa kwamba watanzania wengi ni WALAJI na wala SIYO WAZALISHAJI.

  Asilimia zaidi ya 60 hapa Tanzania ni WALAJI (Consumers) na asilimia 40 hivi ndiyo wazalishaji (Producers). Tatizo hili lipo kote mijini na vijijini.

  Ukitaka kulielewa hilo tembelea nyumba za wapendwa wengi na wasiokuwa wapendwa wako pia. Utakuta nyumba moja ina watu wapatao 8 au 10 na wote wanamtegemea mtu mmoja tu katika kupata mahitaji yote ya msingi; chakula, mavazi, matibabu, elimu, malazi. Baba au mama huyo anayezalisha(mfanyakazi wa mshahara au biashara) ndiye anayehangaika kila siku ili walioko nyumbani mwake wapate kula. Hali hii iko sana mijini kote na hasa Dar es salaam. Tatizo hilo haliko kwa wale waishio mabondeni pekee. Hata ukienda kwa Mchungaji huyo anayetaka watu watimuliwe warudi makwao vijijini unaweza kukuta ana watu kwake ambao siyo wazalishaji bali ni WALAJI TU.

  Napenda kumkumbusha Da Rosemary kwamba kule vijijini hakuna fursa nyingi kama anavyodai yeye katika maelezo yake. Fursa pekee iliyopo vijijini ni ardhi ya kuweza kutumia kulima. Kilimo siyo deal tena kwa watu wa kisasa. Hakuna hoja ya Kilimo KWANZA. KILIMO KWANZA NI SIASA SIYO UHALISIA WA MAISHA KIJIJINI.

  KILIMO KWANZA VIJIJINI hakiwezekani kwa sababu kubwa zifuatazo:

  1. Wakazi wa vijijini hawana mitaji ya kuweza kulima mashamba makubwa. Huwezi kulima mashamba makubwa kwa kutumia jembe tu la mkono.

  2. Hali ya hewa inayoweza kutegemewa kwa kilimo siyo ya kuaminika tena. (Uncertainity rain seasons). Mvua zikinyesha zinakuja na mafuriko au zinakuwa haba kabisa.

  3. Huwezi kurudi kijijini KULIMA KILIMO KWANZA wakati huna utalaam. Nani arudi kulima mashamba ambayo hana utalaam nayo. Labda dada Rose na Mchungaji wao wana utalaam wa kilimo. Hata watalaam wetu toka SUA wamejazana mijini ambako hakuna mashamba.

  4. Sababu nyingine ni kwamba miundo mbinu ya kusafirisha mazao toka vijijini ni duni au hakuna kabisa. Nani akalime nyanya kule Rorya, Nyamongo, Kasulu, Kibondo, Rufiji au Loliondo ambako hakuna baraabara ya kumsaidia kuwahisha mazao yake sokoni.

  5. Hakuna masoko. Masoko ya bidhaa hizo watakazo zalisha yako wapi Nani akalime bidhaa ambazo zitaozea shambani au kudoroa sokoni. Dada Rosemary wewe waweza?? Hata mchungaji hawezi kwenda kulima kwa mfano, viazi, maharage, mahindi, mpunga, kahawa, chai, nk wakati hajui soko la bidhaa hiyo atalipataje. Thubutu yako. Nani aende kijijini? Mbona wachungaji wenyewe hawaendi kufungua makanisa vijijini. Mbona wanapenda kuanzisha makanisa kibao mijini.

  Namaliza kwa kuwakumbusha kwamba, Miaka kama 30 ijayo kama Yesu atakuwa hajarudi, zaidi ya asilimia 50 ya watanzania watakuwa wako Mijini. Kwa sasa kasi ni kubwa na zaidi ya 20% wako mijini kwa sasa wakati wa uhuru Tanganyika ni chini ya asilimia 5 waliokuwepo mijiji. Umoja wa Mataifa ulikuwa umetabiri kwamba ifikapo mwaka 2008 nusu ya watu ulimwenguni ingekuwa inaishi mijini na wala siyo vijijini.

  Inaonekana Mchungaji huyu na dada Rosemary hawajatafiti sababu zinazowafanya watu wakimbilie mijini hadi kuamua kutafuta viwanja maeneo ya hatari kiafya.

  Katika miji ya Tanzania, Dar es salaam ni JIJI mimi nisilopenda kuishi kabisa. Jiji la Dar lisilipendi hata kidogo kwa maisha kwani nimeishi humo zaidi ya miaka 10. Nashangaa kwa nini watu wanabanana Dar wakati kuna miji mizuri inakua kwa kasi sana kama MBEYA, MWANZA, DODOMA, ARUSHA, MOSHI, MOROGORO, GEITA, KAHAMA, na TANGA.

  Nimalizie kwa kukueleza sababu za Kwa nini watu wengi bado wanang’ang’ania DAR au mijini na hawataki kwenda vijijini:

  1. DAR kuna viwanda vya kila aina ambapo miji mingine na vijijini hakuna.

  2. Wizara zote za Serikali ziko DAR tena maeneo ya Posta Mpya.(Foolish City Plan).

  3. Ofisi zote za balozi za nje (foreign embassies) ziko DAR.(another foolishness in Dar)

  4. Mashirika yote makubwa ya serikali kama vile TBC, EWURA, SUMATRA, NSSF, PPF, PSPF, GEPF, TRA, TANESCO, nk yako DAR (a big stupidity again).

  5. Makanisa makubwa sana hapa Tanzania yako DAR. (Roman Catholic, Anglican, Lutheran, Moravian, FGBF, RGC, nk, nk, nk. (Huu nao ni ulimbukeni wa hatari).

  6. Makampuni mengi ya binafsi yako DAR. Hebu tazamaa: IPP Media Group, Clouds Media Group, New Habari Corporation, Magazeti yote, TV zote kubwa, nk, nk taja yote uyamalize utayakuta Dar.

  7. Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na Binafsi ziko Dar. Taja UDSM, IFM, DIT, DUCE, USTAWI, ARDHI, OPEN UNIVERSITY, nk, nk. Juzijuzi tu ndipo serikali ikaona aibu ikaanza UDOM mjini Dodoma angalau UDOM kimepunguza msongamano Dar maana watanzania wengi walikuwa wanadhani usiposoma UDSM hautaitwa MSOMI. Kila mzazi na vijana walikuwa wanakimbilia chuo kikuu cha mlimani. Huu ni ulimbukeni tu.

  8. Hospitali zote zenye watalaam na vifaa vya kisasa zipo Dar. Kila kona utakuta kuna hospitali ama ya serikali au binafsi. Kigamoni ambako mimi nina nyumba maeneo ya Vijibweni kuna Hospitali kubwa ambayo wakati najenga pale haikuwepo. Miaka hiyo ya 2003 kulikuwepo kituo cha Afya tu kigamboni. Temeke, Kinondoni, Ilala kote kuna hospitali za rufaa kwa sasa.

  9. Redio nyingi za Kikristo ziko Dar. Tunashukuru Mungu kwamba angalau na Mwanza kuna redio za Injili zaidi ya 3 (HHC FM, KWA NEEMA FM, na LIVINGI WATER FM) Miaka kama 6 iliyopita redio hizo hazikuwepo hewani. Angalau wakristo wa Mwanza nao wanaweza kujaribu kujifaninisha na wale wa Dar ambako kuna vituo vingi vya TV , Redio, magazeti ya Kikristo ambayo hata kuyataja siwezi.

  Kutokana na miundombinu iliyomo mijini watu hulazimika kujazana mijini kwa hali zozote zile. Mimi nimeishi Kigamboni tangu mwaka 1999. Wakati ule wakazi wa Kigamboni tulikuwa tunajuana kabisa. Hata kama umevuka kwenda mjini au hujavuka, kila mtu alijua kwamba fulani kavuka mjini au yupo. Wakati natafuta kiwanja cha kujenga mwaka 2003 nilipata kiwanja eneo la Vijibweni tena mbali kabisa. Enzi hizo vijibweni, Gezaulole, Kimbiji, Mwasonge na Kibada ndizo zilionekana kama kijiji ndani ya Jiji. Hebu nenda leo ujionee watu walivyofurika. Vijibweni ya mwaka 2003 siyo ya sasa kabisa. Mimi nyumba yangu iko vijibweni karibu na plots za NSSF wakati ule nikiwa najenga watu walinishangaa kwa nini nimeamua kwenda kuishi maporini vile. Ukienda leo hata pa kukanyaga utapakosa. Hii ndiyo hali halisi. Kwa sasa mimi ninaishi Jijini mwanza. Nimenunua eneo la kuishi maeneo ya Mkolani-Buhongwa. Wakati pia nanunua eneo hilo mwaka 2007 kulikuwa ni maporini ambako wanaishi wafugaji na wakulima. Nenda sasa uone Buhongwa na Mkolani palivyo. Pamejaa watu na viwanja havijshikiki tena kama huna zaidi ya Tshs 5,000,000 hupati kiwanja.

  Dada Rose na Mchungaji, katika Jiji lenye miundombinu kama hiyo michache niliyotaja ni dhana potofu kuhubiri madhabahuni tena kwa ujasiri kanisani kwamba waliokumbwa na mafuriko watimuliwe kurudi vijijini. Hii ni dhana mbaya kuipandikiza kwa watu.

  Nani aende kijijini ambako hakuna vitu hivyo nilivyovitaja. Nani HAPENDI KUISHI JIJI LA MARAHA (Ingawa mimi huyaona kama KARAHA)??

  Hivi wewe ukitumwa ukaishi kijijini sasa hivi unaweza kwenda kuishi kabisa baada ya kukaa mjini na kuonja RAHA zake? Wachungaji na Mitume na Maaskofu wengi wanakwepa hata kwenda kuhubiri mikutano ya Injili vijijini. Kule kijijini utalala wapi hakuna hata Guest House? Utalala kwa wapendwa gani wenye kulala katika nyumba za nyasi na vitanda vya makuti na kunguni juu.

  Weeee. Nani aende huko?. Labda wewe uanze.

  Asante kwa kunielewa na kunisoma.

 3. Shalom
  samahani naweza nikaonekana siwajali lakini mie naona wakipewa eneo kijijini kuna fursa nyingi kuliko kuwaacha walivyokuwa hapo jangwani wakisubiri kifo kwa mafuriko, daima ni magonjwa maana hamna vyoo au vinafurika. wanapita na kuzungukwa na maji machafu daima. Ni bora waondolewe na kijijini ni kitu pekee ninachoona kinafaa kwa mtazamo wangu. taratibu hata sie wafanyakazi tumeanza kurudi vijijini kutafuta ardhi na kulima, ajira na biashara ndogondogo haziwezi kukidhi mahitaji yote.
  Ni muhimu tukawa wazalishaji na si kupenda kuwa wauzaji tu.
  Tuwaombee wafumbuke macho.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s