Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVI

Wapendwa leo, kwa Neema ya Mungu, tunaendelea na lile somo la Msitari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia ambapo tunaendelea kuona sababu zaidi zitakazowafanya watu washindwe kuingia mbinguni huku wakiwa wanataka. Tujumuike pamoja katika Sehemu hii ya 16 ambayo inaanza na sababu ya Ishirini na moja (21), ya mambo yatakayosababisha watu wengi wasiingie mbinguni.

 21. WATAFARAKANA NA WAZAZI WAO.

Mal 4:4-6 Ikumbukeni Torati ya Musa, Mtumishi wangu, nilivyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israel wote, naam Amri na Hukumu. Angalieni nitawapelekea Eliya Nabii, Kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya, Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee  baba zao ili nisije nikaipiga dunia kwa laana”.

Neno linasema wazi wazi kuwa Eliya atatumwa, na utakubaliana nami kuwa alipokuja hawakufahamu kama ndiye aliyekuwa ametumwa:

Luka 1:17 – “Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake,ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto,na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa”

Hapo juu anazungumza habari za Yohana Mbatizaji: Kazi kubwa aliyokuja kufanya; kwanza anasema atakuja kwa roho ya Eliya, Ageuze mioyo ya baba iwaelekee watoto, Awatilie waasi akili za wenye haki, (watoto walioasi baba zao, awatilie akili za wenye haki) halafu  Amwekee Bwana tayari watu waliotengenezwa!

Mathayo 11: 13-14, “Kwa maana Manabii wote walitabiri mpaka wakati wa Yohana, Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja, mwenye maskio asikie”

Hapo kuna mambo mazito kweli: “alishakuja”, na “mwenye masikio asikie”. Kumbe twaweza kuwa na masikio na tusisikie!

Efeso 6:1-3, “Enyi watoto watiini wazawi wenu katika Bwana maana hii ndiyo haki,  Waheshimu baba yako na mama yako, amri hii ndiyo amri ya kwanza, yenye ahadi, upate keri, ukae siku nyingi katika dunia.Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, Bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana”

Ndugu zangu, Biblia inasema kabisa kuwa kwa kuwaheshimu wazazi wetu kuna kitu tunapata: HERI pamoja na MIAKA MINGI. Pia wazazi wameambiwa wasiwachokoze watoto wao, ila Wawalee katika adabu, na katika maonyo ya Bwana( Biblia). Wengi wanakataa kulelewa, na wanachofanya ni kukimbia nyumbani; wanatafuta mahali ambapo hawatakemewa, hawataelekezwa; mahali ambapo watafanya wanavyotaka na mtu asiwaulize! Wanakimbia wazazi wao; wanatafuta baba wa kambo! Wengine kwa unafiki wanasema wanawapenda baba zao wa kambo, huku baba zao waliowazaa wapo!

Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa siku tulizo nazo. Biblia inaposema WAZAZI maana yake ni wote wa aina mbili, yaani wa KIMWILI na wa KIROHO pia.

1Kor 4:14-17, “Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha, bali kuwaonya kama watoto niwapendao, kwa maana ijapokuwa mna waalimu kumi elfu, katika Kristo, walakini hamna baba wengi, maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Basi nawasihi mnifuate mimi, kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali, katika kila kanisa”

Hapo juu mtume Paulo anaeleza nini?

Anasema wazi wazi kuwa kumbe naweza kuwa na waalimu 10,000 lakini baba lazima yupo mmoja tu aliyenizaa katika Injili!  Huo ni ukweli usiopingika. Lakini leo hii ukimuuliza mtu Je, Unaye baba yako wa Imani? Wapo wengine watasema “tulikosana naye, nikahama kutoka kanisani, nikajiunga na kanisa lingine!” Wengine waliisha badili mara nyingi tu, sababu walikosana naye, na wako safarini kuelekea Mbinguni! Ndugu zangu, mjue kabisa kuwa tunapambana na shetani ambaye ana sifa zifuatazo: Ni mjanja, ni mkongwe wa vita, anajua namna ya kujigeuza geuza!

2Kor 11:14-15, “Wala si ajabu, shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru, basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza, wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawa sawa na kazi zao?”

Hapa shetani amecheza kweli: mtu aliyekuzaa kwa Injili, akakubatiza, akakulea kwa miaka kadhaa, huyo ni baba yako, ni ukweli usiopingika. lakini baada ya muda, pengine alikukemea, alikukataza hiki na kile, wewe ukaona hapana, yako makanisa mengi mimi nahama! Na kweli ukaondoka, ukaenda mahali, huyo wala hakujui, akakupokea, akakupa na cheo, yeye ati ni mzuri kuliko baba yako? Unaiona roho ya unafki inavyofanya kazi?

Pia mtu anapokuja kanisani, ndugu zangu watumishi wa Mungu, Ebu muulize kama anakotoka ni salama! Usimpokee tu na kumpatia cheo. Mwambie akuletee barua ya anakotoka. Mimi huwa nasema hivi, kama mtoto anataka kuhamia kanisa lingine, hakuna tatizo BALI amueleze baba yake kuwa sasa anajisikia kuhamia kanisa fulani kwa sababu hii na hii na ile. Amuelezee tu! Ninaamini kama  naye ana Roho wa Mungu kweli, na anayoyaeleza yanatosha, naamini atampatia barua nzuri tu, ya upendo, aipeleke kwenye kituo chake kipya! Wala hautakuwepo ugomvi kati ya Mchungaji huyu na yule, wakigombea washirika!

Tukumbuke kuwa wengine ni CHUMVI ILIYOHARIBIKA, haitatengenezeka. Ikikaa hapa kidogo, inaondoka inaelekea kwingine. Wengine wanazunguka tu kama vile Shetani. Maana alipoulizwa na Bwana kuwa anatoka wapi yeye, Shetani, alijibu:  “Natoka kuzunguka-zunguka duniani na kutembea huku na huku humo” Ayubu 1:7

Wengine kazi zao ni kuzunguka tu, hakuna kitu wanafanya . Huwa wanatafuta mahali ambapo hakuna kazi ya kuwabana. Mfano kanisa likianza ujenzi tu, au michango yoyote basi hiyo ni tiketi, wanaondoka, wanatafuta mahali ambapo pameshatengenezwa, wanafika tu ni kukaa, maana kila kitu kipo, jengo, viti, vyombo, n.k!

2Tim 1:15, “Waijua habari hii kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene

Hayo ni maneno ya mtume Paul Mtume akiwataja hawa wapendwa kuwa nao walimwepuka. Yawezekana na Baba yako wa kiroho ndivyo anavyokutaja. Hebu fikiria kidogo: wewe baba yako wa kiroho anakutajaje?

2Tim 1:16-18, “Bwana awape Rehema wale walio wa mlango wa ONESIFORO, maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu, bali alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii akanipata. Bwana na ampe kuona Rehema machoni pa Bwana siku ile, na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso wewe unajua sana”

Ebu jipime mpendwa, umemtafuta baba yako kwa bidii? au yeye ndiye anakutafuta kwa bidii? Wakati mwingine anakupigia simu mpaka inakata, na unasema unampenda Mungu. Unajua kuna wakati Wayahudi walisema wanampenda Mungu, na huku hawamtaki Yesu. Hayo ndiyo yanatendeka leo!

Kumbuka: Kama  YOHANA alikuja kwa Roho ya Eliya, Hata leo watu wanakuja kwa roho ya  FIGELO, na HERMOGENE. pamoja na  ONESFORO!

2Tim 4:10-16, “Maana DEMA aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia, Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yuko hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi. Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso. Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu hasa vile vya ngozi. Iskanda,  mfua shaba, alionyesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake. Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kile neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina!”

Yapo mengi ya kujifunza ndugu zangu. Tusikae tukajidhania tuko salama kumbe matendo yetu ni yale waliyoyafanya hao ndugu zetu waliotajwa hapo juu. Mtume Paulo amewataja wazi wazi. Hata kama nawe baba yako ndivyo anavyokutaja. Hujachelewa! Kumbuka Mwana Mpotevu alipita nyumba nyingi wakati anarudi kwa baba yake, mpaka alipofika kwa baba yake, na baba alimpokea na shangwe, nderemo, vifijo, sherehe, vikafanyika!

Mw 9:20-27, “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu, akanywa divai akalewa, akawa uchi katika hema yake. Hamu , baba wa  Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao, wote wawili, wakaenda kinyume nyume, wakaufunika uchi wa baba yao, nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka, katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea, akasema, Na alaaniwe Kanaani, atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe Bwana Mungu wa Shemu, na Kanaani awe mtumwa wake. Mungu akamnafisishe Yafethi, na akae katika hema za Shemu na Kanaani awe mtumwa wake”

Ndugu zangu, nimeeleza jinsi Moyo wa Mungu siku tulizo naazo unavyolia ili watu waikimbie laana. Lakini wataikimbia kwa njia gani?

Neno linasema katika Malaki 4  kuwa “asijeakaipiga dunia kwa laana”. Napenda tukumbuke kuwa Mungu analitengeneza Kanisa litakalorithi uzima wa milele. Lisilo na ila wala kunyanzi. Kama tunaelekea huko, basi tukubaliane na Neno la Mungu. wako watu hawasemezani, hawasalimiani, hao ni pamoja na baba na watoto wao. Lakini bado kila mmoja anajihesabia haki, wengine wanasema “yeye ndiye aliyenikosea” wengine wanasema “mimi nimemsamehe lakini sitasahau”.

Ndugu zangu turudi kwenye Neno. Mbingu ni ya wale walioshinda. Ebu tuvipige vita vizuri vya Imani, tukiwatanguliza wenzetu. Yale tunayopenda tutendewe na watu nasi tuwatendee na yale ambayo hatupendi kutendewa nasi tusiwatendee wenzetu!

Nuhu alilewa, na akawa uchi. Mtoto wake alipomuona akiwa uchi, alienda kuwaelezea wadogo zake. Mara ngapi washirika wakubwa, wengine wazee, mashemasi, walipouona uchi (madhaifu) wa baba zao waliondoka na kwenda kuelezea wadogo zao? SHEMU na YAFETHI  walikuwa na akili nzuri, walikwenda kinyume cha taratibu, wakatembea kinyume nyume ili kuficha uchi wa baba yao, tena hawakutaka hata kuuona. Wangapi leo wanashangilia kwa kuwa uchi wa baba yao umeonekana??

Napenda nimalize nikisema hivi, ebu tuelewe kuwa aliyetuita ni mmoja, ndiye Amiri jeshi wetu. Tukumbuke kuwa wakati Sauli anatawala, kuna siku vita ilikuwa kali mwisho aliuawa pamoja na mtoto wake, japo alikuwa akimwinda Daud amuue, kwa lugha nyingine alikuwa adui yake. Lakini Daud hakushangilia kifo cha Sauli badala yake alionya akasema jambo lile lisihibiriwe kwa Wafilisti, wangewasimanga! [2Sam 1:20]. Lakini siku tulizonazo hatujui wapi tusemee hili, na wapi tusemee lile!

Ni ombi langu kuwa watoto watajiandaa kurudi kwenda kwa baba zao, na ninaamini kwa Ma-baba hawatakuwa na shida kusema: “MWANANGU KARIBU NYUMBANI!”

Mungu awabariki!

Ndugu yenu, Mchungaji Samuel Imori.

Advertisements

2 thoughts on “Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVI

 1. Pastor Imori,

  Asante sana kwa mafundisho na maonyo. Kwa kweli kulingana na wakati tulionao, ni wakati ambao kanisa linapaswa kukaa na kukomaa katika mafunzo na maonyo yatakayo lifikisha katika ujuzi wa Neno la Mungu ili kuwa tayari kwa kazi yake. Ubarikiwe sana Mchungaji kwa kuutoa wakati wako na kutuletea mafundisho haya.

  Pamoja na hayo, katika sehemu mojawapo ya mafundisho hayo, nimetatizika kidogo, lakini naamini kuwa utanielekeza vizuri zaidi katika hilo kwa ajili ya utukufu wa Bwana.

  Kuna Unabii uliounukuu kutoka kitabu cha Malaki, halafu ukaendelea kuutolea ufafanuzi na kuutafsiri. Ninakinukuu kifungu hicho kilichonitatiza :

  “Hapo juu anazungumza habari za Yohana Mbatizaji: Kazi kubwa aliyokuja kufanya; kwanza anasema atakuja kwa roho ya Eliya, Ageuze mioyo ya baba iwaelekee watoto, Awatilie waasi akili za wenye haki, (watoto walioasi baba zao, awatilie akili za wenye haki) halafu Amwekee Bwana tayari watu waliotengenezwa!”

  Shauku yangu kubwa ni kufahamu zaidi kuhusu kutimia kwa huo unabii wa Malaki kama ulivyokirejea kifungu cha Luka 1:17, haswa katika sehemu hii ambayo umeitolea tafsiri; “…Awatilie waasi akili za wenye haki, (watoto walioasi baba zao, awatilie akili za wenye haki).”

  Naomba, kutoka tafsiri/fundisho ulilotupa, niulize maswali haya:-
  1. Akina ‘baba’ walikuwa ni akina nani katika siku hizo za ujio wa Yohana Mbatizaji ?
  2. Akina ‘baba’ hao walikuwa na tatizo gani lililompelekea Mungu kuigeuza mioyo yao?
  3. Je, hao watoto walio waasi baba zao nao ‘kutiliwa akili za wenye haki’ walikuwa ni akina nani katika siku hizo?
  4. Je, kulikuwa na aina mbili mbili za makundi, yaani akina baba waliogeuzwa mioyo yao kuwaelekea watoto, ni watoto wepi hao, maana hawa watoto wengine ndiyo kwanza wanatiliwa akili za wenye haki? Na hao watoto waliotiliwa hizo akili waliwageukia baba zoa wepi, maana hawa baba wengine ndio kwanza wanageuzwa mioyo kuwaelekea watoto?

  Ubarikiwe Pastor!

 2. Huu ni ukweli usiopingika kimwil na kiroho. MUNGU akubariki na akutumie zaidi katika huduma hii.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s