MAOMBI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU, VYA KATI, SHULE ZA SEKONDARI, NA SHULE ZA MSINGI NA CHEKECHEA.


Kuna umuhimu mkubwa, kuomba kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo na mashule, kwa sababu shetani anafanya kazi bila kulala, ili kupofusha akili zao na macho yao ili wasione wala kuelewa wanachofundishwa. Wakati wanapokuwa darasani, anaondoa uwezo wa kumwelewa mwalimu au wanamwelewa kinyume na mafundisho yake. Wanapokuwa katika kujisomea, anaondoa uwezo wao wa kukumbuka. Anawafanya kuwa wazito wa kuelewa yale wanayoyasoma. Hata wakisoma sana, mara yale waliyosoma huondolewa mioyoni mwao na hivyo, kusahau walichosoma. Hali hii huwakatisha tamaa na kuwafanya kuwa na hofu ya kushindwa mitihani. Wanapoingia kwenye chumba cha mitihani, shetani huwatia hofu zaidi ya kushindwa mitihani. Hofu hii ya gafla inapowajia, wanashindwa kabisa kufikiri na majibu yote hupotea.

Haya ni mashambulizi ya shetani. Wakati mwingine mawakala wa shetani, huiba ufahamu wao na kuutumia kwa faida yao. Wakati mwingine, shetani huwanong’oneza na kuwaongoza kujibu maswali visivyo. Wanadhani wanaandika jibu halali, kumbe hawakuelewa swali na hivyo, wanajibu swali ambalo halipo na kuacha swali ambalo lipo. Hivyo, tunahitaji kuwaombea sana wanafunzi. Haipendezi kuachishwa masomo, lakini inapendeza kushinda na kumpa Mungu utukufu hasa watoto wake wanaposhinda mitihani. Ni mapenzi ya Mungu kuishika elimu na kushinda.

Neno linasema: Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; umpende, naye atakulinda (Mithali 4:5-6). Tena: Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako (Mithali 4:13). Hivyo, ni mapenzi ya Mungu kwetu sisi kumshika elimu na kujiendeleza.

Maombi: Baba, Mungu wa Mbingu na Nchi, Jina lako litukuzwe milele. Baba, wewe ndiyo sababu ya sisi kukutana hapa leo ili tupate kuhudhuria mbele zako. Baba, tunapenda kusemezana na wewe siku zote na kuleta hoja zetu kwako. Leo Baba, pamoja na kuleta hoja zetu mbele zako, tunaomba kukusikia pia ukituelekeza ili tujue yatupasayo kufanya. Baba, leo tunawahudhurisha vijana wetu wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, shule za sekondari, msingi na chekechea, mbele ya kiti chako cha rehema. Baba kama neno lako lisemavyo, tunaamini tutapata nguvu na uwezo wa ushindi kwa ajili na wanafunzi hao. Neno lako linasema: Basi, na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili kupewa rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji (Waebrania 4:16) Baba, tunaomba uwape uwezo wa kuelewa. Uwape hekima na maarifa, ujuzi na roho ya ufunuo, ili wapate kujua siri zilizojificha katika kila somo na kila swali. Baba, uwape uwezo wa kufumbua kila fumbo lililofumbwa katika maswali ya mitihani yao.

Baba, kama neno lako lisemavyo: Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; alioutenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina utajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya minguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote (Waefeso 1:17-23).

Baba, Mtakatifu, wanapokuwa katika masomo yao darasani, maktaba, au vyumbani wakijisomea, au wakifanya mazoezi ya nyumbani au wakiandika mada mbalimbali walizopewa na walimu wao; Roho Mtakatifu uwafundishe na kuwatia katika kweli yote, kama Yesu alivyotuahidi hapo aliposema: Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote …….; na mambo yajayo atawapasha habari (Yohana 16:13).

Uwaelekeze sehemu muhimu za kusoma na kuelewa ili waweze kujibu maswali kwenye mitihani yao. Baba, watakapoketi katika mitihani yao, Roho Mtakatifu awakumbushe yote waliyosoma na yale yote waliofundishwa, ili waweze kujibu vyema mitihani yao. Bwana Yesu ulituambia katika neno lako kwamba: Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia (Yohana 14:26).

Roho Mtakatifu, wanafunzi hawa, watakapokuwa wanajibu maswali ya mitihani yao, uwape uwezo wa kujieleza vizuri, uwezo wa kuandika vizuri. Uwape kuwa na ujasiri, wala wasiwe na uwoga na wasiwasi. Neno la Bwana linasema: Katika pendo hakuna hofu; lakini pendo lililokamilika hutupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo (1 Yohana 4:18). Tena: Nasi twajua kuwa Mwana wa Mungu amekwisha kuja naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye kweli, nasi tumo ndani yake aliye kweli, yaani, ndani ya mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele (1 Yohana 5:20). Tena: Hatukupokea roho ya dunia na roho wa hofu bali neno linasema: Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi (2 Timotheo 1:7)

Roho mtakatifu, useme nao na kuwaelekeza wanapoandika mitihani yao, hasa pale wanapoandika majibu ambayo sio. Neno linasema: Na masikio yao yatasikia neno nyuma yako, likisema Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto (Isaya 30:21). Baba, Roho wako ahuishe fahamu zao, na uelewa wao zaidi ya wote, nao wawe mara kumi bora kuliko wote katika masomo yote kama neno lako lisemavyo: Basi kwa habari za hao vijana wane, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima …. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu aliowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake (Danieli 1:17,20).

Baba Mtakatifu, Mungu wa Mbingu na Nchi, kwa mamlaka ya Jina la Yesu Kristo, tunakwenda kinyume na roho yule wa uasi na uharibifu, anayeharibu ufahamu wa wanafunzi, anayepotosha fahamu zao, anayewasahaulisha, anayewatia uwoga na mashaka, anayewatetemesha akiwaambia kwamba watashindwa. Anayetanga-tangisha mawazo yao wakati wanaposoma au kujisomea. Tunakufunga katika Jina la Yesu Kristo, na kukukaza kwa minyororo, na kukutupa katika shimo lisilo na mwisho, hata siku ya Hukumu. Achia fahamu zao, achia akili zao. Achia hisia zao.

Kwa Jina la Yesu Kristo, pepo unayewaondolea kibali kwa walimu wao, tunakuamuru kurejesha kibali chao kwa walimu wao. Pepo unayeweka uzito katika akili zao, hata wasielewe masomo, tunakuamuru kuondoa mkono wako juu ya fahamu zao, ondoa mawe ya uzito wa mizani, uliouweka katika fahamu zao. Tunakuamuru wewe roho wa kusitasita wakati wa kujibu maswali, uondoke kwao tangu sasa, ondoka katika fahamu zao. Tunakuamuru wewe roho wa kutetemesha mikono, wakati wa kuandika, ondoka katika mikono yao. Tunakufunga kwa jina la Yesu na kukutupa katika giza la nje.

Tunafunga pepo, unayeondoa amani ndani yao na kusababisha mahangaiko. Pepo wa mahangaiko ya moyo unayesababisha moyo kwenda mbio wakati wa mitihani, na kusababisha mwanafunzi achanganyikiwe. Ondoka katika mioyo yao tangu sasa. Moto wa Roho Mtakatifu ukuteketeze. Katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tunakufunga pepo unayetatanisha wakati wa mitihani hata mwanafunzi anatatanika katika kujibu maswali; ondoa mikono yako juu yao. Tunakufunga kwa jina la Yesu na kukutupa katika giza la nje. Pepo la kushindwa mitihani, pepo la uoga, tunawafunga tangu leo, na kuwatupa katika giza la nje. Tunawazuia ili kwamba msiwaguse hao wanafunzi tangu leo, katika jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

Tunajenga wigo wa Damu ya Yesu Kristo na moto wa Roho Mtakatifu, kuzunguka miili yao, viungo vyao vyote, ubongo wao, mifumo yao ya fahamu, mifumo yao ya kupumua, mifumo yao ya damu, mifumo yao ya chakula, uzazi, mifumo yao ya haja ndogo na haja kubwa, figo zao, maini yao, mapafu yao, bandama zao. Miguu, mikono, vichwa, vywele, macho, ngozi, meno, pua, nyuso zao na kila kilicho chao katika miili yao. Mavazi yao, kalamu zao, vifutio, madaftari, viatu, soksi nguo za ndani, kucha zao. Alama zote zilizochukuliwa kwao na kufungwa na wachawi, moto wa Roho Mtakatifu unaziteketeza sasa katika jina la Yesu wa Nazareti – Amen.

Baba, wanafunzi hao watakuwa vichwa na sio mikia. Watakua juu tu na sio chini, maana Roho wako aliye bora anakaa ndani yao. Baba Mtakatifu, wewe unastahili kupewa sifa na utukufu, kwa kuwa Bwana, ulitununua kwa damu ya thamani, ukatufanya kuwa ufalme na makuhani, na ukatupa kumiliki katika nchi. Wastahili wewe kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na Baraka – Amen.

Tunakushukuru kwa kuwa umetusikia na kutupatia haja zile ambazo tumekuomba – Amen.

Pastor Zephaniah Ryoba, Morogoro

Advertisements

7 thoughts on “MAOMBI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU, VYA KATI, SHULE ZA SEKONDARI, NA SHULE ZA MSINGI NA CHEKECHEA.

  1. Hakika yatupasa kukesha zaidi na zaidi! Ubarikiwe Pastor kwa kutushirikisha jambo hili.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s