Nilioa Muathirika wa HIV

Bwana Yesu asifiwe watumishi. kwanza naomba niwaombe radhi kwa kutokuweka jina langu hadharani kutokana na nafasi niliyonayo katika jamii. pili nimevutiwa sana na michango ya watumishi wa Mungu juu ya ndoa na talaka.

naomba nianze hivi, Haya ninayoyaandika hapa ni maisha yangu halisi. nilikutana na mke wangu miaka 10 iliyopita. wakati wa uchumba wetu sikuwahi kumgusa. wakati uchumba unaendelea tuliamua kwenda kupima H.I.V. bahati mbaya yeye alikutwa postive na mimi negative. kutokana na kuwa nilishamuhakikishia kumuoa na kutokana na IMANI yangu kuwa kubwa niliamua kumuoa. Wakati wa uchumba zilipatikana tetesi kwa ndugu zangu lakini niliamua kuwadanganya kwamba ni uongo. na kweli tulioana baada ya miaka minne. Baada ya mwaka ndani ya ndoa tulibahatika kupata mtoto. kwa sababu ailijifungua kwa operation kinga ya mwili ilishuka sana. Ndipo akaanza kuugua na hapo ndipo ndugu walipofahamu ukweli na ya kwamba niliwadanganya tokea mwanzo.

tulipopimwa mimi na mtoto tulionekana hakuna aliyeathirika. hapo kinga ya mke wangu CD4s zilishashuka mpaka chini ya 20. Ndipo akaanzishiwa ARV na kwa kweli yuko vizuri kwa sasa,ila shida yangu ilikuwa kwa sababu sikuweka imani kwenye ARV bali kwa Yesu Kristo niliona nisikutane nae tena mpaka Mungu aniambie kwa nini muujiza ulitendeka kwa mimi na mtoto lakini hakuamua kumponya mke wangu (kwenye mahusiano yetu ya kindoa hatukuwa tunatumia kinga kwa maana niliamini yeye ni Mzima katika Jina la Yesu.. Babu wa samunge alipoanza japokuwa mimi sikumuamini nilimwambia aende labda angekutana huko na Mungu.

Sasa kumbe wakati anaumwa si mnajua wapendwa maisha yetu ya kiafrica maneno mengi, sasa yeye kumbe akawa anaweka mambo moyoni na kujenga chuki kwa watu. Kwa bahati mbaya baada ya hali yake kuimarika uchumi wangu uliyumba sana. ilibidi niachie nyumba kubwa tuliyokuwa tumepanga na kuchukua nyumba ndogo kwa sababu familia yangu bado ni ndogo ili tuweze kuendana na uhalisia wa maisha. lakini yeye alikataa kuja nyumbani kwa sababu hakupenda kuishi katika nyumba hiyo ndogo tena yenye mkusanyiko wa wapangaji wengine(mwanzo tulikuwa tunaishi peke yetu). kwa hiyo akaamua kwenda kwa ndugu yake. Nilimshawishi mara sita lakini alikataa kuja mpaka nitafute nyumba ingine. Baada ya kuchoka nikaamua kuachana nae. kwa hiyo nikawashirikisha watu wakaribu na wakaona ni sawa.

Msaada ninaohitaji
1. Ndoa yangu na imani yangu vilikuwa sahihi?
2. Kwa matendo anayonifanyia mke wangu kumuacha ni sawa?
3. Kama sifanyi nae tendo la ndoa je hapo kuna ndoa?
4. Je? nikifanya nae tendo la ndoa imani yangu ni sahihi au namjaribu Mungu.
5. Kama uchumi wangu ukiimarika akija atanipenda kweli?
6. Kuna watu wanaamini kwamba ushirikina ulitumika kunifanya nimuoe akiwa HIV positive lakini mimi mpaka leo naamini nilikuwa timamu, hivi kama ni kweli alitumia ushirikina kulikuwa na ndoa hapo?

Watumishi samahani kwa kuwachosha na maelezo marefu lakini kwa kweli mchango wenu utanibariki sana. tunavyoendelea mbele nitajitambulisha kwa jina halisi.

Mungu awabariki sana.

–Chitu

Advertisements

18 thoughts on “Nilioa Muathirika wa HIV

 1. Ombeni kwa pamoja kwa ajili ya hekima na ujasiri na amueni kwa pamoja, kwa msaada wa Mungu, kuwa waaminifu wenyewe kwa wenyewe. Ili kuzuia maambukizi ya HIV kwa wewe Bwana, unaweza kuamua kutohusiana naye kingono, au KAMA ni lazima, daima tumia mipira ya kondomu wakati unafanya ngono. Tunaambiwa inazuia maambukizi ya VVU.

  .Amueni kwa pamoja, kwa msaada wa Mungu, kuna na mtoto mwingine. Mkiamua ndiyo, muongee kuhusu ni lini mtafanya hivyo na jinsi ya kumweka mtoto bila HIV.
  Mkiamua hapana, muongee kuhusu njia nzuri, salama za kuwa na uhakika hapati mimba.

  Kwa vile familia yako ni ndogo, si lazima ukodishe jumba kubwa na la kifahari, mueleze huyo mama na aelewe kwamba hata lishe yake itabadirika, hivyo, nilazima aangalie afya yake na siyo nyumba kubwa.

  Kumbuka, siku ya harusi uliahidi utamtunza hata wakati ni mgonjwa au maskini. Kumbuka ahadi mlizofanya. Ila asing’ang’anie jumba kubwa maana hilo halikuwamo katika covenant ya ndoa.

 2. Oooh, Wewe kamanda wa jeshi la Bwana. Mimi naona tatizo lako ni kwamba imani uliyokuwa nayo tangu mwanzo, imeanza kupungua!! Umeanza kuwa Petro baada ya kutembea hatua chache majini, akaanza kusahau alikotoka na huyo aliyemwita atembee majini…
  Ushindi wako kwa Ibilisi ni mkubwa mno, hupaswi hata kidogo kumpa nafasi yule adui. Ushauri wangu kwako ndg yangu.
  1. Usimwache mke.
  2. Mtafute huko aliko halafu mtenge siku 7 za kufunga ninyi wawili tu peke yenu(ikiwezekana nendeni milimani-faraghani) mkamlilie Mungu huko ili aondoe tatizo kabisa. jiwekeni sawa kwanza kabla ya kwenda kukutana na Munmgu huko milimani. Imani ilikuokoa wewe na virusi, ndiyo imani hiyohyo itakayoondoa virusi hivyo ndani ya mwili wa mkeo.
  NB: Kumbuka kuwa Mungu halazimishwi kumponya mkeo. Kwa uzoefu wangu, Mungu anaweza kurespond papo hapo, baada ya muda fulani kupita au asitende chochote kabisa kwa yale anayoyaona YEYE kuwa ni sahihi. Lakini hupaswi kufa moyo kwa maisha haya ya kitambo, bali furaha yako ikaongezeke kwa Bwana Mungu wako.
  3. Ongeza bidii ya kumtafuta Mungu zaidi.
  Binafsi, naungana na wewe ktk kukuombea.
  Ubarikiwe wewe pamoja na famlia yako

 3. Aise! yaani wewe unahitaji msaada wa kutosha. kumbuka hakuna aliyetabibu bingwa na mashuhuli duniani kama Yesu. …MUNGU huyu aliumba mbingu, nchi , milima mirefu na masayari (unirvese) yote yaliopo anaponya UKIMWI….

 4. Usijaribu hata kidogo kumwacha Mungu wako na wala usije ukamujaribu hata siku moja na Mungu wa neema na akubariki sana.

 5. Nakupa pole ndugu kwa yaliyokupata. Ushauri wangu kwa wanaokushauri utumie kondom si sahihi tena wanasema wameokoka wakati kutumia kondom ni kushiriki mauaji kabisa kabisa.Nenda kanisani kwako kaa kwa kina na mchungaji wako akushauri kwa undani swala hili si la kujadili kwa juu juu.Mungu akutie nguvu ushinde.

 6. UPENDO HAUNA KIKWAZO WALA SABABU.

  Kwanza nakupongeza kwa kuamua kuoa mke huku ukijua udhaifu wake kiafya katika mfumo wake wa damu (yaani Ulemavu wa chembe za damu usababishwao na HIV au VVU).

  Watu wengi hawawezi kuushinda mtihani wa kumwoa mke mwenye ulemavu kama ulivyofanya wewe. Kuwa na HIV ni ulemavu anaokuwa nao mtu na huwezi kuuona mpaka kwa kutumia vipimo vya kisasa vinavyotambua ulemavu huo (VVU). Huu ni ulemavu kama ulemavu mwingine ulivyo mfano; albinism, upofu, uziwi, ukoma, kiwete, nk ingawa aina hizo huwa zinaonekana kwa macho.

  Ni watu wachache sana, hata wale wanaodai kuoteshwa na Mungu kuhusu Mke mwema, wanaoota kumpata mke mwema mwenye ulemavu. Wengi hudhani mke au mume mwema ni yule asiyekuwa na ulemavu wowote, mzuri kwa maumbile ya mwili, sura, elimu, nk. Kama mtu akija na maono ya kuoteshwa na Mungu akawaambia watu ameoteshwa na Mungu kuhusu mwenza lakini kumbe anao ulemavu fulani, ndoto au unabii huo utaonekana kama wa uongo na bandia (fake prophecy).

  Nikirudi kwenye mada yangu ya “UPENDO HAUNA KIKWAZO WALA SABABU” ni kwamba watu wengi huwa wanachanganya “UPENDO KATIKA NDOA” na, “MAELEWANO KATIKA NDOA”. Haya mawili yamekuwa yakitumika katika kutaka kumaanisha kitu kimoja wakati siyo hivyo.

  Kuna watu (hasa wanaume) wanadhani kwamba kama hali yao ya uchumi ni nzuri basi mke atampenda zaidi. Napenda kuwaambia kwamba hii siyo kweli. Kama mke unasema anakupenda kwa sababu unayo mali au pesa huo siyo “UPENDO” ni “UELEWANO” katika ndoa.

  Sifa za Upendo katika ndoa ni kama zifuatazo:

  1. Unampenda mwenza wako kama alivyo pamoja na ulemavu alio nao hata kama ni HIV.

  2. Uko tayari kumsamehe saba mara sabini kwa kila kosa alitendalo hata kama amefanya zinaa saba mara sabini (7 x 70= 490) kwa siku.

  3. Hauweki orodha ya makosa yake aliyokutendea siku ya jana au siku kadhaa zilizopita. Yaani “UPENDO WA KINDOA” hautakabari bali hustiri wingi wa dhambi. Hata angetenda dhambi gani, “UPENDO” hautamkana na kumtenga wala kumnyanyapaa.

  4. Mume mwenye upendo wa kindoa yuko tayari kufa kwa ajili ya mke wake ampendaye kama Kristo alivyokubali kufa kwa ajili ya mke wake yaani “Kanisa. Hata kama mkeo ana ulemavu wa vipi wewe kama unasukumwa na “UPENDO” ninaousema hapa hautamwacha kamwe. Upendo wa Ndoa ya Kikristo huwa hauna lugha ya kusema, “NAMWACHA” mke wangu au mume wangu kwa sababu eti hii , hii, hii, au ile, ile na ile. Lugha ya “KUACHANA” haipo mahala penye “UPENDO” hata siku moja. Ukiona mtu ameachana na mke wake au mume wake, “KWA SABABU YOYOTE ILE” ujue waliooana kwa msukumo wa “UELEWANO” siyo kwa msukumo wa “UPENDO”. Sema Ameeen.

  5. “Upendo wa kweli” tofauti na “Maelewano ya kweli” unamjali mwenzako katika “RAHA” au “SHIDA”, Unastahimili majaribu yote na kuvumilia hali zote zitakazojitokeza mbele ya safari. NDOA ni sawa na “safari” tuzifanyazo kila siku kwa mabasi au treni au meli au ndege. Je, hujawahi kusafiri na ukakutana na matatizo njiani ikiwemo kupata ajali, kupata pancha, kulala porini, kupata mawimbi makubwa ziwani/baharini au hewani kama unasafiri kwa ndege? Je, ulipokutana na hayo uliamua kurudi nyuma kwa sababu tu umekutana na misukosuko njiani? Bila shaka wengi wanaendelea mbele na safari hadi wafike kule waendako. Hata Ndoa nayo iko hivyo. Haifai kumwacha mke kwa sababu yoyote ile hata kama ungegundua kwamba ana ulemavu wa chembe za damu yaani ana VVU au Kansa au Ugumba, nk. Kama “ULIMPENDA” na siyo kwamba “MLIELEWANA” kuishi pamoja hadi kifo kije kuwatenganisaha basi utaendelea kuishi naye bila malalamiko wala huzuni moyoni. Tena utamfurahia mkeo katika ulemavu wake. Tena uko tayari kuishi naye kama alivyo siyo kama wewe utakavyo au watu wengine watakavyo.

  6. Kuhusu VVU na tendo la ndoa, mimi nina uhakika kabisa kwamba wewe hutapata VVU hata kama mkeo anavyo. Hii ni kwa sababu huo ni “ULEMAVU” wake na wala siyo wako. Pamoja na ushauri huu, mimi sitakushauri kutumia “mpira wa kiume” kwa hoja ya kujilinda wewe usiambukizwe. Sikushauri hivyo kwa sababu eti mimi napingana na hoja ya “Kondom” kwa wakristo kuzitumia. Ukipenda kutumia “Kondom” naomba wewe na mkeo mkubaliane tena kwa “UPENDO”. Hoja yangu hapa ni kwamba kabla ya kukutana katika tendo la ndoa hakikisha kwamba mkeo umemwandaa vya kutosha hadi sehemu yake ya uke iwe laini sana na majimaji ya kutosha ili unapomwingilia kusiwepo musuguano mkali unaochubua uke wake au uume wako. Kama mtakutana mara moja tu kwa kila wiki yaani mara 4 kwa mwezi nakuhakikishia kwamba hautapata VVU hata siku moja. Haikikisha kwamba mkeo anakula vyakula vyenye kuleta “mafutamafuta laini yaani “vagina lubricants oil” kama vile korosho, karanga, matunda, dagaa wa kigoma, samaki, ndizi za kupikwa, nyanyachungu, biringanya na mboga za majani. Chochote kati ya vyakula hivyo huongeza “vagina lubricating oil” ili kuzuia michubuko isitokee wakati wa tendo la ndoa. Kumbuka kwamba, VVU humshika mtu pale tu afanyapo “ngono zembe” yaani kukutana kimwili bila kufanya zoezi la kumwandaa mwezio. Kwenye ndoa mara nyingi hili huwa lipo. Wanandoaa wengi wana tatizo la kutoandaana ili kusisimua “mafuta ya uke” yatiririke kwanza ndipo wakutane. Ukifanya hivyo hata kama hutatumia “Kondom” bado hutapataa maambukizi ya VVU.

  NB: Ndoa yoyote haitaitwa NDOA kama hakuna kukutana kimwili. Tendo la ndoa ndiyo NDOA yenyewe. Ndio “muhimili Mkuu” wa ndoa. Ndiyo “uhai wa ndoa” ndiyo “moyo wa ndoa”. Huwezi kupata “faraja ya moyo” bila kufanya “tendo la ndoa”. Huwezi kupata “utulivu wa akili” bila ya kupewa “Tunda” la ndoa. Mkeo kuwa na HIV siyo mwisho wa maisha. Watu wasiokuwa na HIV wataendelea “kufaariki” ukiwaona huku mkeo akiendelea kuishi tena maisha ya raha. Hakikisha mnapokula “tunda” la ndoa usiwe na “fikra” potofu kichwani mwako kwamba ……hivi akiniambukiza itakuwaje…..? au kwa nini ………nisimwache….? Lugha ya KUACHANA isitamkwe kabisa kinywani mwako wala kwake.

  7. Mwisho kabisa, ili niachie wengine kuchangia hoja hii, napenda kukuambia kwamba maswali yote uliyouliza katika kujenga hoja zako baadhi nimeyajibu hapo juu katika maelezo yangu. Labda swali lako la 1 na la 6 ndiyo sijajibu.

  Swali la 1: Umeuliza, je Ndoa yangu na imani yangu vilikuwa sahihi?

  Jibu ni kwamba NDOA YAKO ILIKUWA SAHIHI kwa mujibu wa sheria ya Ndoa ya 1971 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa Maandiko (Math. 19:1-10) mstaari mmoja wa 6 unasema, ……basi alichokiunganisha Mungu, HIV isikitenganishe…….. Soma vizuri sheria hiyo ya Ndoa ya mwaka 1971 uone tafsiri ya ndoa. Haipishani na Maandiko Matakatifu. Kwa hiyo vyovyote ilivyokuwa wakati unataka kuoa, bila kujali maaneno na vijimambo vya ndugu na wazazi NDOA YAKO NI HALALI KIBIBLIA na KISHERIA.

  Swali la 6: Umeuliza: Kuna watu wanaamini kwamba ushirikina ulitumika kunifanya nimuoe akiwa HIV positive lakini mimi mpaka leo naamini nilikuwa timamu, hivi kama ni kweli alitumia ushirikina kulikuwa na ndoa hapo?

  Jibu lake ni kwamba, kama mtu ana umri zaidi ya miaka 18 na hajalewa pombe anaruhusiwa kuingia mkataba wowote kisheria. Ndiyo maana hata sheria inaelekeza kwamba mtu chini ya umri wa 18 haruhusiwi kuingia mkataba wowote. Wewe kama ulikuwa na miaka 18 au zaidi na hukuwa umelewa pombe na wala hukushinikizwa na upande wowote huku ukiwa hujui unalotenda basi NDOA HIYO NI SAHIHI NA HALALI. Hata kama ungekuwa na ushahidi kwamba alitumia ushirikina kukushinikiza kumuoa, au hata kama angetumia chochote kukutaka umuoe (ingawa yote hayo hayana ushahidi ni hisia tu) bado NDOA HIYO NI HALALI KABISAA. Kwa hiyo hata kama angetumia ushirikiana bado hapo kuna NDOA HALALI KIBIBLIA NA KISHERIA.

  Nakutakia maisha marefu (above 75 years).

  Ndimi nduguyo katika Bwana Mr. Milinga.

 7. MUNGU HUNGOJA WAKATI KUJIBU MAOMBI YAKO

  Biblia inasema katika Yohana 11:1……..Palikuwa na mtu mmoja jina lake Lazaro, mtu huyu aliugua sana ndugu zake wakatuma ujumbe kwa Yesu wakimwomba Yesu akamponye, lakini Yesu hakwenda kumponya. Lazaro akafa, na baada ya siku nne ndipo Yesu akaenda kwa Lazaro akakuta amekwisha kufa siku nne zilizopita. Martha dada yake Lazaro akamwambia Yesu “Bwana kama ulingelikuwepo asingalikufa” Kauli hii ya Matha inaonyesha wazi kabisa kwamba maombi ambayo alimwomba Yesu aende amponye nduguye kabla hajafa hayakujibiwa. lakini yesu akamwambia Amini Lazaro atafufuka, Yesu alikwenda Kaburini alikozikwa Lazaro akamfufua.
  Ndugu zangu kunawakati unaweza kuwa umeomba kitu katika majira uliyayotumai kwamba Bwana atakujibu lakini ukajikuta kwamba yamepita bila kuona majibu ya maombi yako. unaweza kukata tamaa, lakini kumbe leo tunapata kujifunza kwamba Mungu hujibu kwa majira ambayo yeye anaona yanafaa kwaajili ya utukufu wake ili kwamba Atukuzwe Duniani. kwa sababu hiyo Yesu alisema ugonjwa huu wa Lazaro si wa kufisha ila ni kwa ajiri ya utukufu wa Mungu. yatupasa tuwe na imani ambayo aliambiwa Martha awe nayo ya kwamba Tuamini tu hata kama tunaona haiwezekani tena, ghafla mambo yatakuwa sawa. na siku zote ukiona umefika sehemu ambapo hakuna msaada kabisa basi Mungu yu-mahala pale kujionyesha katika utukufu wake. Wana wa Israel walipofika ukingoni mwa bahari hapakuwa Meli wala Boti ya kuwavusha wakigeuka nyuma wanayaona majeshi ya Farao yakiwafuata kwa kasi, walipoteza tumaini,hapo hapo Mungu akajitokeza katika utukufu wake ili atukuzwe, akayagawa sehemu mbili maji ya bahari wakavuka pakavu.
  Nakumbuka siku moja niliwahi kukosa pesa hata ya kununulia chakula, nikawa nimelala usiku njaa ikawa kali nguvu zikaondoka, nikakumbuka kwamba kulikuwa na mfuko wa pipi ambazo nilitakiwa kuwapa watoto Nikiwa katika Huduma. nikamwambia Mungu, Daudi alikuwa na njaa akala mikate ya hekaluni kinyume cha sheria, na mimi nachukua pipi hizi kama Daudi. nikataka nichukue pipi niziponde kisha nichukue maji nitengeneze kama juice walau ninywe nipate nafuu. nikainuka kitandani nichukue maji kwenye ndoo, ghafla nikaona mfuko wa plastic kwenye ndoo nikautwaa nikaona ni mzito, nilipoangalia ndani nikakuta kuna chips na na chupa ya juice! kisha nikakumbuka kwamba kulikuwa na rafiki yangu alikuwepo pale ndani kwangu labda atakuwa alileta yeye. lakini nikagundua kwamba Mungu amemuokoa mtumishi wake na njaa. kwa hiyo nikajifunza kwamba kumbe ukiona sasa mambo hayawezekani tena muujiza uko karibu mahala hapo usijikwae shetani akachukua nafasi utakuwa na hasara kubwa kuja kuupata tena muujiza huo itakupasa gharama upya ya majaribu mapya.

  Bwana akulinde mtu wa Mungu.

 8. kaka pole sana kwa yaliyo kukuta, kwani mimi naamini kuwa kila linalofanyika chini ya jua ni mungu amepanga.Hivyo huna budi kuendelea kumuomba Mungu akupe majibu ya maswali yako kwani mimi binafsi nashindwa kujua nianzie wapi kukushauri maana yote uliyosimulia naona kama maajabu ya dunia kweli imani yako ilisimama katika bwana.Na katika ushauri wa watumishi waliotangulia kukushauri inabidi pia utafakari kwa undani zaidi kwani wao pia ni mitazamo yao,kumbuka wewe uliamini katika bwana hivyo jaribu kufanya maombi mara kwa mara na mungu atasikia kilio chako na hapo ndipo majibu sahihi ya maswali yako yatakapopatikana.Pole sana na mungu akujaze roho ya ujasiri katika hili.

 9. Bwana Yesu asifiwe.

  Pole kwa yote yaliyokupata. Nadhani ulipata jaribu la size yako kabisa, kama ni kutoka kwa Mungu au kwa shetani sijui, ila ushauri wangu kwako ni huu. Kaa kitako na Mungu umuulize nini cha kufanya. Usichukue mawazo ya kila mtu atakayokupa, ila pia kuna mawazo mengine ni mazuri. Kwamba ni mawazo gani mazuri au mabaya huwezi kuchuja kirahisi ukiwa peke yako, unahitaji msaada wa Mungu. Soma Isaya 48:17 na Zaburi 32:8, Mungu anasema atakufundisha ili usipate hasara. Tafuta uso wa Mungu kwa maombi hata ya Kufunga, nina hakika Mungu alikuwa anajua kuna siku utapita kayika hali kama hiyo, na nina hakika kuna wazo aliwaza kwa ajili yako.

  Mungu akutie nguvu umalizie vizuri.

  Mwl. Peniel S Sarakikya

 10. Pole sana mtumishi wa Mungu kwa suala hilo gumu.
  Mimi ninaamini kwamba, hakuna linalomshinda Mungu kabisa. Kwa habari ya maswali yako naamini ifuatavyo:
  1. Ndoa na imani yako ilikuwa ni sahihi kabisa. Usipoweka mashaka, Mungu atamponya na kumleta tena muwe pamoja. kwa kuwa uliamini na siyo kwamba kuna mtu alikupa mawazo ya kukushawishi basi uko sawa. Ndoa yako ni sahihi, hujamjaribu Mungu.
  2. Kumuacha mke wako sio sawa maana ni mke wako na ni kifo tu kinatakiwa kiwatenganishe. Kama kweli ulianza na Mungu kama unavyodai, unapaswa kuendelea na Mungu na uachane na mashauri yasiyo ya Mungu yanayokufanya uchukue maamuzi mengine. Maamuzi mengine kama ya kumuacha si ya Mungu na sikubaliani nayo hata kama una uhakika kwamba anafanya uzinzi.
  3. Kutokufanya naye tendo la ndoa ni uamuzi wako. Lakini ulishasema kwamba uliendelea na tendo la ndoa kwa kuamini kwamba yeye ni mzima. Ina maana sasa umeamua kuamini kwamba ni mgonjwa na kwamba hawezi kupona kabisa? Kwa nini unaacha? Ujue kwamba kama unaanza kuingiza mashaka unamzuia asipone maana Biblia inasema, “Mwenye shaka… asitegemee kupokea kitu kwa Bwana” (Yakobo 1:6).
  4. Ukifanya naye tendo la ndoa kwa kuamini kwamba ni mzima ni sawa kwa sababu “imani bila matendo imekufa”. Ila nakuona kama mtu ambaye mara kadhaa unapata mashaka. Acha kusikiliza maneno ya watu na ndugu wasiomwamini Mungu kama unataka uuone uponyaji wa Bwana kwa mkeo. Hebu msifu na kuutafakari ukuu wa Mungu ili uuvute uwepo wa Mungu na uponyaji utadhihirika.
  5. Suala sio atakupenda, je wewe unampenda? Na kama upendo wenu umejengwa na uchumi kuimarika inabidi mwangalie kwa upya kama mnajua nini maana ya upendo wa kweli. Zungumzeni mwelewane.
  6. Kuamini ushirikina ni uamuzi wa mtu. Mwamini Mungu na Mungu peke yake, huna sababu ya kuitafakari dunia, ushirikina, shetani au watu.
  Soma Neno la Mungu
  Tafakari,
  Iambie nafsi yako unachoamini
  Tenda

  Utafanikiwa hakika.
  Ubarikiwe

 11. Ahsanteni sana kwa maoni yenu watumishi.
  1. kuhusu afya yake kwa kweli kwa sasa yuko vema kabisa. ambacho kinamsumbua ni kile kinyongo alichowawekea watu wakati anaumwa. kwa ufupi amekuwa mgomvi sana na hapa ndipo mahusiano yetu yanapozidi kuwa magumu.Lakini pia mahusiano yake na watu wanaomzunguka ni magumu sana anaweza akaamua kujibu watu (bila kujali umri) kwa dharau na kashfa
  2.kuhusu familia mathalan mtoto ni yeye anaishi nae na ninajitahidi kumtunza kadiri niwezavyo.
  3. kuhusu kuokoka kwa kweli tuikutana tukiwa tumeokoka na kwa kweli wakati wa uchumba mda mwingi tuliutumia kwa kusoma neno.
  4.kuhusu maombi amefanyiwa maombi na watumishi wakubwa tofautitofauti ambacho sielewi ni wakati gani atapokea muujiza wake.
  5. kuna mtumishi ameshangaa juu ya kuokoka na kusema uongo (kwamba ameathirika na mimi nikawaambia ndugu kwamba hajaathirika) hapa labda watumishi mnisaidie mimi siwezi mjibu

  nitajitahidi kuzidi kuweka mambo mengi bayana kadiri maswali yanavyojitokeza.

 12. Ndugu,
  NAKUPONGEZA KWA IMANI KUBWA NAMNA HII.

  Ninaomba nichangie japo kidogo;

  1. Ndoa yangu na imani yangu vilikuwa sahihi?

  Niseme kwa mtizamo wangu vilikuwa sahihi, kwa sababu wewe ulikuwa unaamini ktk Uponyaji wa Mungu. Lakini uponyaji wa mke wako MUNGU ALIKUWA ANASUBIRI IMANI TOKA KWA MKEO AMBAYO BADO MKE WAKO HAKUIGUSA NA KUIFIKIA. Naamini angeigusa hiyo imani angeponywa. Kuna kesi ya mtu mmoja kanisani kwetu ambaye alikuwa na mke muathrika(WALIOANA KABLA YA KUOKOKA) wakapata mpaka watoto wawili lakini Yule kijana hakuathrika hadi leo ila Yule mke alifariki mwaka jana, Yule kijana na watoto wote ni wazima hawajaathrika. Yule mke alishikilia dini yake kubwa, sijui kama huko alikuwa ameokoka.

  2. Kwa matendo anayoyafanya kumuacha?

  sio sahihi kwa sababu ulikubali kumwoa ukiwa unajua kama ameathrika, japo kuna matendo mengine yaziada ambayo yanaonyesha kwamba anafanya huyo mwenzio, haya yanatokana na kuchoka kwa imani yake na Marathi yake, hivyo kazi kubwa unatakiwa umtiie moyo na kumwombea na kuingiza ile imani ya kwanza japo ni kazi kubwa sana lakini jaribu kupata msaada wa maombi kutoka kwa watumishi mbalimbali ili kusudi la Mungu litimie.

  3. Kama hufanyi nae tendo la ndoa hapo kuna ndoa?

  Ndoa ilishakuwepo hivyo haijavunjwa na kumbuka ahadi yako wakati wa KUFUNGA NDOA TAKATIFU A.K.A. PINGU ZA MAISHA. ——-WAKATI WA SHIDA NA RAHA—-????

  4. NIKIFANYANAE tendo la ndoa imani yangu sahihi au namjaribu Mungu?

  Kwa sababu imani yako imeanza kuteteleka kwa mashaka, nashauri sasa uwe na subira, kwani ninyi nyote(ME/KE) mmeanza kupatwa na wasiwasi na mashaka makubwa, hivyo uwe mvumilivu mpaka Mungu akupe jibu sahihi nini la kufanya ktk hilo. La sivyo unaweza kuingia ktk mtego mkubwa.

  5. Kama uchumi ukiimarika atanipenda kweli?

  Kweli upendo wakati ukiwa na pesa tu, si upendo wa kweli kabisa. Labda na pengine ninaweza kuwa sahihi, kwamba saa ya kuimarisha zaidi imani yako sasa, UNAJUAJE PENGINE NDIO MUNGU ANAKUEPUSHA AU NDIO MAJIBU YA MUNGU MKE KUONDOKA, AU UNAJUAJE PENGINE MUNGU AMEAMUA KURUHUSU YEYE AONDOKE BAADA YA WEWE KUBOMOKA KIUCHUMI ILI AKUONYESHE KWAMBA HUYU MKE MUDA WOTE ALIKUJA AKAKUPENDA KWA SABABU YA MALI? Sorry ndugu labda nitakuumiza ila tafakari zaidi hatika kipengele hiki, mtegemee Mungu zaidi, usiwe na haraka kuoa mwingine utamuudhi mungu.

  6. HAPA HAKUNA USHIRIKINA, UNGEMUOAJE MSHIRIKINA HUKU UKIWA NA IMANI YA NAMNA HIYO? HAYO NI MAWAZO YA KIMWILI ZAIDI.

  NAISHIA hapo nitarejea baadae nipo harakaharaka njiani.
  Barikiwe
  Anthony Mwenda

 13. (1)Ndoa ilikuwa sahihi,sababu ulishafunga nae ndoa (2)Ulipataje uhakika kwa Mungu kwamba huyo ndiye mke chaguo la Mungu kwako (3)Huwezi kumuacha labda kwa yeye kufanya dhambi ya uzinzi (4)Hata kama hufanyi nae tendo la ndoa,huyo bado ni mkeo kwa kuwa tu ulifunga nae ndoa (5)Tumia kondom kama imani imeshuka (6)Kama hujaokoka,nakushauri uokoke maana maana utajazwa Roho Mtakatifu na atakusaidia na kukuongoza veme juu ya mambo ambayo kwako hayana majibu maana yeye anashauri zaidi ya binadamu yeyote

 14. Mi sijaelewa inakuwaje unakuwa na imani kubwa kwa Mungu….na unasema uongo( Unaamua kumdanganya mtu/ndugu juu ya huyo mwanamke). Naomba yeyote mwenye kuelewa anieleze.

 15. Hakika unae Mungu aliyekutetea akakuponya katika hilo, ki ukweli ulionyesha upendo wa ajabu sana nahisi hii ni kutokana na imani yako, kwa vijana wa leo wasiona imani yeyote asingeweza kuoa muathirika.Mshukuru sana Mungu kwa hilo na mtumikie yeye aliyekuponya.
  Sidhani kama kuna mtumishi yeyote atakuambia au atakubali kwamba kuna ushirikina ulitendeka wewe kuoa,ila ninachojua ni upendo wa kweli uliokua nao kwake na hukutaka kuvunja ahadi uliyoiweka kwake, ulifanya jambo jema sana mbele za Mungu ndo maana mkono wa Bwana ulikua na wewe na akakulinda mpaka mwisho.
  Kwa sasa kwa kuwa kuna mashaka yamejengeka kati yako na yeye na ameshaamua kuwa mbali na wewe, sikushauri uendelee kumbembeleza arudi kwako ila kitu cha msingi kujua ni kwamba ni mke wako na atabaki kuwa mke wako na Mbingu zinalitambua hilo, kwa hiyo endelea na majukumu ya kumtunza hakikisha hutendi dhambi kwa kuwa Bwana ana kusudi na wewe.
  Lea zawadi uliyopewa na Bwana kwa upendo wote na usithubutu kumtakia neno lolote mtoto wako juu ya ugonjwa wa mama yake ila penda kucheck afya zenu mara kwa mara kwani muda mwingine vipimo hunganya.

 16. Shalom mpendwa
  pole na kuuguza, naomba tu nikuulize haya
  umeokoka?
  umepokea au kujazwa Roho mt? kama ndio:
  je wewe ulipoamua kumuoa uliuliza kwa Mungu kama ndiye chaguo lake?
  kama ulijibiwa ndio na ukaamua kwa utashi wako kujifunga hapo kwa kiapo nadhani rudi kunsihi Mungu akutie nguvu ustahili yote, si uliapa hadi kifo kiwatenganishe? labda ni majaribu shetani anakupitisha maana kufa sio kwa ukimwi tu, waweza wewe kufa kwa ajali leo hii ukamwacha yeye akaishi miaka 10 zaidi
  kama hujaokoka basi unawajibika pia kumtunza na kuwa nae maana hukuwa na roho wa Mungu kuweza kusikia na kuuliza nani ni mwenza wako, sasa kumwacha huyu mgonjwa na hali yake kwa sasa naona ni dhambi, mvumilie na muombee apate amani ya moyo.
  Watu wengi tunachoogopa ukimwi ni
  1, kifo cha ujanani
  kabla ya kufikia uzeeni
  2, magonjwa nyemelezi yanayosumbua kila kukicha na kukufanya ushindwe kumudu kufanya kazi au kutofanya sawasawa.
  3. kuambukiza wenza na kurithisha kwa watoto hadi wajukuu ni kama kuua kizazi chako
  4. gharama kubwa ili kukuwezesha kujitibia magonjwa nyemelezi, wewe, mwenza watoto na bado kuweza kumudu gharama nyingine za maisha

  sasa kwa upande wako nadhani ulikuwa umeingia kwenye haya mahusiano ukijua nini gharama yake, nafikiri hapa ndio umuhimu wa wazazi na ndugu kuhusishwa unapokuja wao wangeweza kukushauri hayo niliyoweka hapo juu ambayo nadhani wewe hukuyajua.
  Kwa kifupi nimewauguza na nilkuwa ktk huduma ya maombezi, wagonjwa wa ukimwi mara nyingi wanajihisi kunyanyapaliwa na wanapenda sana kuwa na usiri na hivyo wewe kumpeleka huyo mwenzio ktk nyumba ya wapangaji wengi ni ngumu sana kwake. Hawa hasa wakishuka CD4 kiasi hicho magonjwa nyemelezi kama kuharisha, homa zisizoisha ni kawaida hebu pata picha huyu mgonjwa kwenye choo cha watu wengi inakuwaje? Kama kweli ulimpenda mwanzo nakushauri kaa naye sasa umsikilize na kama uwezo huna wa nyumba ya pekee mwache akae tu hapo alipo na fika kila leo kumjulia hali. Unawajibika kwasababu hadi ukajiaminisha kumuoa ukiwa tayari unajua hali yake, naye alikuamini na kuridhia lakini kitendo hicho ni hatari kwake na kwako pia. Kwa kuingia ktk ndoa na kulazimika kuzaa ndio kama hivyo imemshushia CD4 zake hadi kufikia hapo alipo. Sikulaumu ila hawa watu ni bora wasizae maana mama yeyote mjamzito kinga hushuka sana, hivyo hawa wagonjwa kama inaepukika wanashauriwa wasishike mimba kabisa sijui nyinyi nani aliwashauri kuzaa na wewe kutotumia kinga?
  Samahani lakini kama umempokea Yesu, tafadhali rudi ktk magoti msihi Mungu akupe macho na masikio ya rohoni kuhusu hili, kama bado umpokee Yesu na utulie uukulie wokovu wako utaelekezwa na watumishi nini cha kufanya kuhusu mkeo. Ubarikiwe na Mungu akutie nguvu.

 17. kuna watu ambao hawapati HIV. lakini utajijuaje? usichukulie granted?
  kwa kweli una bahati, na bahati uliyoipata usiichezee.
  hapa ni kama mtu aliyeanguka kutoka ghorofa ya 7 hadi chini na hakupatikana na jeraha lolote. mtu kama huyu akirudia kwenda kwa mara ya pili kujitupa tena chini mara nyingine haponi anaweza kusagika na kuwa unga. nimeona wengi wanaofikiri kuwa bahati ni kila siku. tunza bahati yako kama unapenda kuishi. na huyu dada anautu wa kukaa mbali na wewe, kwani hataki uathirike kama yeye, ili uwepo umlee huyo mtoto. mambo mengine mke wako hawezi kukuambia direct. kama anajitenga ,shukuru kaa kimya na mshukuru Mungu. ikiwa atahitaji msaada wa kimaisha mpe haraka kama huna nenda kakope mahali.
  ubarikiwe na pole na hilo mpendwa.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s