Umuhimu wa kwaya kanisani

HISTORIA YA UIMBAJI NA MUZIKI

Uimbaji asili yake ni mbinguni (Eze 28:13-15). Tutakapofika mbinguni tutaendelea kumwimbia Bwana (Ufu 15:2-4; Ufu 5:9-10).
Hapa duniani nyimbo na muziki vilianza zamani sana baada ya kuumbwa kwa Adamu na Hawa “…na jina la nduguye  aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.”(Mwa 4:1-21).

UMUHIMU WA KWAYA KATIKA KANISA

Kwaya ni kikundi cha watu wanaoimba pamoja(na kupiga vyombo vya muziki). Kwaya ni kiungo muhimu katika Kanisa kinachofanya huduma ya uimbaji. Wapo wanakwaya wenye vipaji vya uimbaji, sauti za kuvutia na uwezo wa kutunga nyimbo  mpya. Kanisa ni mwili wa Kristo wenye viungo vingi; na kila kiungo kina kazi. Kiungo hiki (Kwaya) kikitimiza vizuri wajibu wake, Kanisa litahudumiwa (1 Pet 4:10-11).

Kwaya ni muhimu ndio maana hata katika Agano la Kale walikuwepo watu maalum waliowekwa kufanya huduma ya uimbaji (1Nya 6:31-32). Maneno ya nyimbo yana nguvu kubwa. Yanaweza kubadili hali ya huzuni kuwa ya furaha na moyo mgumu kuwa laini. Mtu mwenye udhaifu anaweza kusikia nguvu na uzima kwa nyimbo. Daudi alipopiga muziki roho mbaya ilimwacha Sauli (1 Sam 16:23).  Tunasoma pia kwamba siku moja Sauli aliingiwa na ghadhabu, chuki na kumwonea Daudi wivu baada ya kusikiliza maneno ya nyimbo (1 Sam 18:6-9).

Nyimbo tunazosikiliza (redioni, katika kanda,  nk) kama hazina maneno yenye maadili mazuri, mioyo yetu inaweza kuchafuliwa na kutufanya twende kinyume na mapenzi ya Mungu.

Nyimbo zinavuta nguvu na uwepo wa Mungu (2 Nya 20:21-22; 2 Fal 3:15-16). Paulo na Sila waliomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, hatimaye milango ya gereza ikafunguka (Mdo 16:25-26).

AINA ZA NYIMBO

Nyimbo nyingi zinaangukia katika makundi yafuatayo:

 1. Nyimbo za mafundisho/maonyo (Kol 3:16).

 2. Nyimbo za faraja

 3. Nyimbo za mahubiri (Isa 48:20).

 4. Nyimbo za sifa/shukurani/maombi

 5. Zipo pia nyimbo za upuzi (Amo 6:5). Mungu hapendi nyimbo za upuzi.

Biblia inatuagiza kuimba “kwa akili”  yaani tuimbe huku tukiwa na ufahamu wa nyimbo tunazoimba (Zab 47:6-7; 1 Kor 14:15). Kwa sababu hiyo, wanakwaya wanapaswa pia kujua nyimbo wanazoimba zina maana gani au lengo lake ni nini. Zinahubiri au zinafariji? Zinajenga au zinabomoa? Vinginevyo wanaweza kujikuta wanaimba nyimbo za upuzi au zisizokuwa na maana.

Kama wewe mwenyewe huelewi yale unayoimba, unafikiri wale wanaosikiliza wimbo wako wataelewa? Sio rahisi.

MADA ZA NYIMBO
Wimbo unaweza kuwa na mada (topic) moja au zaidi. Lakini wimbo wenye mada moja ni mzuri zaidi. Kwanini?

 1. Wimbo wenye mada moja mara nyingi unaanza kwa utangulizi, baadaye unaelezea mada yenyewe na kisha unatoa hitimisho, kwahiyo ni rahisi kukumbuka ujumbe wa wimbo huo.

 2. Unakuwa na ufafanuzi wa kutosha. Beti 3 au 4 zinazungumzia mada moja tu kwa kuifafanua.

Mada ya wimbo inaweza kumlenga mtu mmoja au watu kadhaa:

 • Waliobatizwa

 • Mvulana na msichana waliotangazwa kwamba ni wachumba

 • Maharusi – waliofunga ndoa (Zab 78:63) nk.

 • Watu ambao hawajaokoka (wanaosikiliza mkutano wa Injili).

“KUMECHISHA”

Neno hilo linatumika kuelezea jinsi mtu alivyovaa mavazi yanayofanana rangi. Mtu anaweza kumwambia rafiki yake: “Aisee, leo umependeza! Umemechisha vizuri sana – kuanzia kichwani hadi miguuni!”

Wakati wa ibada, kwaya inaweza pia “kumechisha” nyimbo zake na mahubiri au tukio la siku hiyo. Kwa mfano, kama mada ya mahubiri ni “Faida za wokovu”, kwaya itafute wimbo unaozungumzia wokovu na kuuimba kabla au baada ya mahubiri. Wakati wa mkutano wa Injili, ili “kumechisha,” pambio kama hii inafaa kuimbwa” “Akina baba njoni, akina mama, njoni, nanyi vijana njoni, mje muokolewe…”

Wimbo kama huu ufuatao haufai kuimbwa na kwaya wakati mwinjilisti anapokuwa amemaliza kuhubiri mkutano wa Injili: “Sio kila mtu asemaye ameokoka, ataingia mbinguni. Siku ile watasema, ‘tulikuwa wahubiri’, watakataliwa.”

Siku moja mahali fulani kwaya ilikaribishwa iimbe wimbo ili kukamilisha mahubiri  ya siku hiyo. Mahubiri yalikuwa mazuri sana lakini bahati mbaya kwaya ile iliimba wimbo “usiomechi” na mahubiri yale: “.. toa kwanza boriti katika jicho lako mwenyewe ndipo utoe kibanzi katika jicho la ndugu yako.” Tuimbe kwa akili na pia  “tumechishe”!

Ili kwaya iweze kila mara kufaulu kumechisha inahitaji kuwa na nyimbo nyingi, zenye mada mbalimbali. Ni vizuri kila somo katika Biblia liwe na wimbo wake. Yaani ziwepo nyimbo zinazozungumzia wokovu, utakatifu, amri za Mungu, neema, msamaha, ubatizo, ndoa, watoto, utumishi, uinjilisti, maombi nk, nk. Je, kwaya ya Kanisa lako ina nyimbo ngapi? Sulemani alikuwa na nyimbo zaidi ya 1000 (1 Fal 4:29-32).

JINSI YA KUPATA WIMBO/MADA MPYA

Watu wengi wanapenda vitu vipya. Kiatu kipya, gauni jipya, nyumba mpya, vyombo vipya nk. Vivyo hivyo watu wanapenda kusikia nyimbo mpya. Lakini je, ni rahisi kwaya au watunzi wa nyimbo kupata nyimbo mpya kila mara?

Mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata nyimbo au mada mpya.

 1. Ukisikia sauti ya wimbo (melody) moyoni mwako fanya haraka kuirekodi kwenye kanda (kama una radio cassette na microphone) ili usisahau.

 2. Soma Biblia, soma vitabu vya Neno la Mungu. Hudhuria vipindi vya mafundisho. Mada unazozipata zitungie nyimbo. Nyimbo zinazotungwa kwa njia hii ni nzuri kwa sababu zinalingana na Neno la Mungu.  Sio rahisi watu kuzikosoa kwamba haziendani na Biblia.

 3. Unaposafiri, unapokuwa sokoni nk, sikiliza yale yanayosemwa, tazama yanayofanyika kisha uyatungie nyimbo (za maonyo, za ushauri nk) kulingana na Neno la Mungu.

 4. Mwombe Mungu akupe wimbo mpya. Mungu anaweza yote.

Unapokosa maneno ya kuweka katika wimbo sio vizuri kujaziajazia tu maneno au sauti zisizo na maana ili wimbo uimbike!

UPIGAJI WA VYOMBO VYA MUZIKI

Maneno ya nyimbo yanavutia sana yanapoambatana na upigaji mzuri wa vyombo. Biblia inatuagiza tupige kwa ustadi (Zab 33:3). Kila inapowezekana tuwe tayari kujiunga na shule za muziki au kujifunza kwa wale wanaojua ili tuweze kupiga vyombo kwa ustadi. Siku hizi kwenye mtandao kuna masomo mengi ya muziki yanayotolewa bure kuhusu jinsi ya kupiga gitaa, kinanda, jinsi ya kusoma noti za muziki(notation) nk. Tuwe tayari kuyatafuta.

Biblia inasema tusiifuatishe namna ya dunia hii (Rum 12:2a). Hata katika uimbaji na upigaji wa vyombo hatuna haja ya kuifuatisha namna ya dunia hii. Haimpi Mungu utukufu ukisikia mtu anasema: “Kwaya hii imeimba wimbo unaofanana na wimbo wa yule msanii wa muziki kule Marekani (ambaye hajaokoka).” Tunaye Mungu anayeweza kutusaidia kupiga vyombo kwa ustadi. Tumtegemee.

Vyombo vya muziki vinasaidia kubeba ujumbe. Kwahiyo fundi mitambo wa Kwaya ni vizuri ahakikishe kwamba sauti za vyombo hazizidi zile za waimbaji. Vinginevyo watu watasikia tu vyombo na kukosa ujumbe.

MITINDO YA UIMBAJI

Kuna mitindo mbalimbali ya uimbaji. Wengine wanaimba huku wamesimama wima, wengine wanaimba huku wamekaa, na wengine wanaimba huku wakionesha ishara mbalimbali kwa mikono na miguu yao. Mitindo ya uimbaji ni mizuri iwapo tu inasaidia kufikisha ujumbe kwa wahusika. Huduma ya uimbaji sio “show.” Hatuimbi ili kuwaonesha wengine kwamba sisi tuna mitindo mizuri ya kuimba. Kwahiyo kwa mfano, kama wimbo una maneno yafuatayo: “Dunia inaangamia. Watu hawamchi Mungu, asubuhi mpaka usiku watu wanakunywa pombe, wanafanya uzinzi, wanapigana. Tuwaombee wasiangamie…” sio vizuri kuuimba wimbo huo kwa mitindo ya shangwe na nyuso zilizojaa furaha. Sio vizuri kwa sababu sio jambo linalofurahisha kuona watu wanaangamia.

UTAKATIFU KATIKA UIMBAJI

Huduma ya uimbaji ni muhimu iendane na maisha ya utakatifu. Mizaha wakati wa mazoezi ya nyimbo haifai. Mizaha ni dhambi (Mit 26:19, 19:29; Zab 1:1).
Kuimba bila utakatifu ni kelele mbele za Bwana (Amo 5:12, 22-23).

Wanakwaya ni walimu. Wanalifundisha Kanisa. “Basi wewe umfundishaye mwingine, je! hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe?…” (Rum 2:21-24).

UMUHIMU WA KUIOMBEA KWAYA

Ni muhimu kuiombea kwaya bila kukoma. Pasipo Mungu Kwaya haiwezi kufanya hayo tuliyojifunza katika somo hili (Yn 15:5). Kwahiyo basi tuwaombee viongozi wa kwaya, walimu wa kwaya, wapigaji wa vyombo nk. Tukemee roho ya kiburi na mafarakano isipate nafasi katika kwaya. Tuwaombee watunzi wa nyimbo, Bwana awape nyimbo mpya zenye ujumbe mzuri. Tuviombee vyombo vya kwaya visiharibike. Tuwaombee wanakwaya wawe na bidii ya kumtumikia Mungu kwa uimbaji (Rum 12:11).

Mwl Christopher Frank

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s