Maarifa ya Msingi baada ya Kuokoka

Mpendwa, ubarikiwe! Bwana Asifiwe! Itika, ”Amen“, neno lenye maana, ”Na iwe hivyo“.Mpendwa, umepata neema kubwa kusoma somo hili kwenye tovuti hii. Katika somo hili utapata mafundisho muhimu sana, yatakayokufanya uchote baraka zote za rohoni ambazo Mungu amekusudia kukupa.

Hata hivyo, ili ufuatilie vizuri mafundisho haya, itakuwa vema uwe na Biblia yako karibu, ili ufungue na kusoma mistari inayotajwa, ili upate kuelewa vizuri.

Kwanza kabisa, hongera sana kwa kuokoka. Je, ninajuaje, au wewe utajuaje kwamba kweli umeokoka? Jibu, ni kwamba, kweli tumeokoka, kutokana na jinsi Neno la Mungu linavyotuambia. Wakati ulipotubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, kwa dhahiri Yesu Kristo alikusamehe dhambi zako, maana Neno la Mungu linasema katika

YOHANA 6:37, “……Wala yeyote ajaye kwangu, sitamtupa nje kamwe.“ Hakuna mtu yeyote anayekwenda kwa Yesu na kutubu dhambi zake, akiwa anamaanisha kuziacha kisha Yesu akamtupa nje na  kuacha kumsamehe. Hivyo, ni dhahiri kwamba ulipotubu dhambi zako ulisamehewa dhambi . Dhambi zako zote zimesamehewa  na Mungu hazikumbuki tena (ZABURI 103:12; Isaya 43:25). Sasa baada ya kujua kwamba umesamehewa dhambi zako, ni muhimu kufahamu pia kwamba kupewa msamaha  kunaambatana na kupewa wokovu, maana Biblia inasema katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.

Hivyo basi, kwa hakika umeokoka, na jina lako limefutwa katika kitabu cha hukumu na kuandikwa katika kitabu cha uzima wa milele mbinguni. Kuna furaha na shangwe kubwa mbele za Mungu na malaika zake, kutokana na uamuzi wako (LUKA 15:7,10). Hivyo tangu leo huna budi kuwa na  hakika ya wokovu wako, ili Shetani asikudanganye kwamba hujaokoka. Shetani huweza kutudanganya kwamba hatujaokoka kwa kutumia hisia zetu, na wakati wote tukawa ni watu wa kufuatisha tu sala ya toba na kutaka kuokoka, tena na tena. Hatupaswi kuwa hivyo. Hatuenendi kwa kuona, bali kwa imani (2 WAKORINTHO 5:7). Na imani ni kuliamini Neno la Mungu, na  kulichukua kama lilivyo.

Sasa je, ina maana kwamba huwezi kabisa kufanya dhambi yoyote kuanzia pale ulipookoka? Na kama je, ukifanya dhambi moja baada ya kuokoka, ndiyo wokovu wako umeishia hapo? Ni muhimu sana kufahamu majibu ya maswali haya au siyo ni rahisi kudanganywa na Shetani na kujikuta tumeacha wokovu. Mara tunapookoka halafu tukajikuta tumekasirika au tumesema uongo n.k., Shetani upesi hutudanganya na kutuambia, ”Wewe bado hujaokoka. Kama umeokoka, mbona  asubuhi hii umekasirika na kufanya jambo baya?“ Inatupasa kuwa na maarifa haya tusiangamizwe (HOSEA 4:6).

Ni kweli, ni mapenzi ya Mungu kabisa baada ya kuokoka tusitende dhambi tena. Hata hivyo tunapokuwa bado watoto wachanga kiroho, bado tunaweza tukajikuta tunafanya dhambi hapa na pale. La msingi ni kwamba, mara unapojikuta umetenda dhambi, unatakiwa kutubu mara moja kwa nia ya kuacha dhambi  hiyo na utasamehewa palepale, na wokovu wako unaendelea nao. Biblia inasema katika 1YOHANA 2:1-2, ”Watoto wangu wadogo nawaandikia haya ili kwanba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote“. Hata hivyo, mtu aliyeokoka hawezi kutenda dhambi kwa kukusudia, yaani anajua kwamba kufanya hili ni dhambi, halafu yeye analifanya  kwa kusudi kabisa eti atatubu! Mtu anayetenda dhambi kwa kukusudia hivyo, huyo bado hajaokoka maana kufanya hivyo, Biblia inasema ni kumtukana Mungu (HESABU 15:30-31). Mtu aliyeokoka anaweza kujikuta amefanya dhambi bila kukusudia na hilo litamkosesha amani sana, na vilevile anaweza kufanya dhambi fulani kwa sababu ni mtoto mchanga kiroho, hivyo hajajua sana nenola haki; yaani hajajifunza sana Neno la Mungu, na kuyafahamu mapenzi ya Mungu kuhusu janbo hilo (WAEBRANIA 5:12-13).

Baada ya kupata maarifa haya, sasa tupige hatua zaidi katika mafundisho yetu. Baada ya kuwa umeokoka sasa, hupaswi kuona haya au aibu kuwaambia ndugu na marafiki zako kwamba umeokoka. Ukiona haya, Yesu Kristo atakuonea haya katika utukufu wa Baba yake (MARKO 8:38). Yaani hatakubali uingie mbinguni. Mtu anayemuonea haya mtu mwingine anakuwa kama hamjui kabisa, na anakuwa hataki hata kumtazama, ili asije kushawishika kumwonyesha upendo au huruma.

Vivyo hivyo, sisi nasi kama tunaona haya kuwaeleza wengine kwamba tumeokoka, siku ya mwisho Yesu atakuwa kama hatujui kabisa. Tukumbuke kwamba tunapookoka na kuwahi kuwaeleza watu wanaotufahamu kwamba tumeokoka, hilo linatupunguzia hatari ya kuvutwa dhambini. Mapema kabisa, mwanzoni tu mwa mazungumzo yetu, na marafiki wa kiume au wa kike wa zamani katika uasherati na uzinzi, ulevi, dansi, ushirikina n.k.; hatuna budi kusema, ”Mimi nimeokoka, hivyo siwezi tena kufanya mambo yale tuliyokuwa tunayafanya pamoja“. Vilevile hatuna budi kuvunja urafiki wa pete na kidole na watu wale tuliokuwa tunafanya dhambi pamoja, maana kama tutaambatana nao kwa karibu sana, kama mwanzo; wataturudisha tena dhambini. Ni vema sasa kuwa na urafiki wa pete na kidole na wenzetu waliookoka (ZABURI 119:63; MITHALI 22:24-25). Hata hivyo hatupaswi kuwachukia au kuwadharau watu ambao hawajaokoka, bali tunapaswa kuwapenda, kuwaombea na kuwaalika kusikia mahubiri, ili wao nao waokoke kama sisi. Bado tutashirikiana nao vizuri ofisini n.k. Ila, wale tuliokuwa tunafanya nao uasherati au uzinzi, tujiepushe nao kabisa maana ni rahisi sana kurudia uchafu wa mwanzo.

Ni muhimu pia kukumbuka kwamba tukiwaambia ndugu na marafiki kwamba tumeokoka, upesi watasema kwamba tumepotea. Tusijali maneno hayo. Hawajui walisemalo. Kabla ya kuokoka, ndiyo tulikuwa tumepotea, lakini sasa tumepatikana, maana Yesu alikuja kutafuta na kuokoa  kile kilichokuwa kimepotea (LUKA 19:10). Furaha na shangwe zilifanyika  baada ya mwana mpotevu kurudi kwa babaye, na inatajwa kwamba alikuwa amepotea, lakini sasa ameonekana (LUKA 15:32). Hivyo waliopotea yaani wana wapotevu, ni watu ambao hawajaokoka, siyo sisi tuliookoka!

Tuendelee tena sasa. Ni muhimu tena wakati huu wa mapema, baada ya kuokoka, kufahamu jinsi ya kuukulia wokovu. Maneno mengine yanayotumika badala ya kuokoka, ni kuzaliwa mara ya pili (YOHANA3:3). Hivyo kwa maneno mengine, umezaliwa mara ya pili, kwa Roho. Ulizaliwa mara ya kwanza, pale ulipozaliwa kwa njia ya kawaida ya kimwili. Wakati huo ulizaliwa kwa mwili, lakini sasa umezaliwa kwa Roho, kama Yesu alivyozaliwa, kutokana na mimba iliyopatikana kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (YOHANA 3:6-7; MATHAYO 1:20-21). Wewe sasa ni mtoto mchanga wa kiroho. Sasa basi, hebu tafakari jambo hili. Je mtoto mchanga anapozaliwa katika hali ya kawaida ya kimwili, anaweza kuendelea kuishi bila kunyonya maziwa? Jibu ni kwamba atakufa baada ya muda mfupi kwa  sababu ya kukosa chakula. Vivyo hivyo hakuna mtoto mchanga wa kiroho anayeweza kuendelea katika wokovu kama hapati maziwa yasiyoghoshiwa yaani yasiyochanganywa na maji. Tunasoma katika 1PETRO 2:2,” Kama watoto wachanga waliozaliwa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu“. Maziwa haya yasiyoghoshiwa ni nini? Ni mafundisho ya Neno la Mungu yanayofundishwa kwa kuzingatia Biblia inavyosema, bila kuchanganywa na taratibu tu za kibinadamu. Neno la Mungu ni chakula cha roho zetu (MATHAYO 4:4; KUMBUKUMBU LA TORATI 8:3; YEREMIA 15:16).

Baada ya kuokoka, haikupasi kuzungukazunguka huko na huko kwenye mahubiri yanayozungumzia tu kutubu dhambi na kuokoka. Hayo pamoja na jinsi yalivyo mazuri, umekwisha yasikia, na tayari umekwisha okoka. Unachokihitaji sasa ni mafundisho ya kina ya Neno la Mungu ya kukuwezesha kufahamu yanayokupasa kufanya na yale yasiyokupasa kufanya, na hatimaye wewe nawe uwe mwalimu wa wengine (MITHALI 12:1 ; HOSEA 4:6; MAMBO YA WALAWI 5:17: MATHAYO 22:29; WAEBRANIA 5:11-14). Kabla ya kuokoka, tulikuwa katika mafundisho manyonge yenye upungufu, ndiyo maana hayakutufanya tuokoke. Baada ya kuokoka, Neno la Mungu linatuonya  kutoyarejea mafundisho hayo manyonge, kama tunataka kuukulia wokovu. Tuwe tayari hata kuwaacha ndugu zetu huko na kutafuta Kanisa lenye watu wenye imani moja na sisi yaani waliookoka kama sisi, ambapo mafundisho yote ni ya wokovu (Soma WAGALATIA 4:9; HOSEA 4:17; 2 PETRO 1:1). Vilevile, kama tunataka kuukulia wokovu, tusitosheke na ibada moja tu ya Jumapili kwa wiki, au kwa mwezi. Miili yetu inakula mara mbiliau tatu kwa siku. Roho zetu ni za thamani zaidi, hivyo hatuna budi kuhudhuria ibada zote za Kanisa kwa gharama yoyote, ili tuukulie wokovu, hata kama Kanisa tuliloliona linatufaa, liko mbali kiasi gani! (Soma MATHAYO 12:42; MITHALI 2:3-5; AYUBU 23:12; ZABURI 119: 72).

Tukiwa ukingoni sasa mwa somo letu, hatuna budi pia kufahamu juu ya Shetani. Neno ”Shetani“, kwa lugha ya asili, maana yake Adui, Mshindani, Mpinzani, na pia Yeye aletaye vizuizi kwa watu wa Mungu au watu waliookoka katika hali ya uadui kabisa, ili ikiwezekana, waiache njia ya kweli ya wokovu ya kumfikisha mtu mbinguni. Shetani anaweza kutumia mawazo yako mwenyewe au ndugu zako wa kimwili, kukuvunja moyo na  kukukatisha tamaa kuendelea na kweli yote ya wokovu uliyoipokea. Utashangaa siku ya ibada ndiyo magonjwa yanaanza, ndiyo wageni wanakuja kukutembelea n.k., ujue vyote hivyo ni vizuizi vya Shetani, mpinge kwa kutokuruhusu lolote lile kukutoa katika ibada (YAKOBO 4:7). Mateso na maudhi mbalimbali kwa mume, wazazi, ndugu n.k; yanaweza kuja kwako baada ya kuokoka. Hii si ajabu, ni kazi za upinzani za Shetani. Yalimpata Yesu. Wewe songa mbele tu bila kujali yatakayokupata (WAFILIPI 1:29-30; 1 WATHESALONIKE 3:3; 1 PETRO 3:14; MATHAYO 5:11-12; YOHANA 5:16; 7:19-20; 8 :48 ; 15 :24-25 ; MARKO 3:21; 2 TIMOTHEO 3:12; WAGALATIA 4:29; 1 PETRO 4:12-16). Kwa vyovyote vile, usigeuke nyuma na kuacha wokovu. Vipige vita vizuri vya imani, imani uilinde (WAEBRANIA 3:14; 2 PETRO 2:20-22; 2 TIMOTHEO 4:7). MUNGU AKUBARIKI!!!

Kwa msaada zaidi muone Mchungaji wa Kanisa linalohubiri wokovu.

*****************

–Askofu Zakaria Kakobe

Advertisements

7 thoughts on “Maarifa ya Msingi baada ya Kuokoka

  1. Asante Askofu,

    Mafundisho ni mazuri na yenye kutia moyo sana, kadiri ya jambo la Wokovu na Kuokoka lilivyo mbele yetu.

    Jambo ambalo ninahitaji kulijua zaidi ni kule ‘Kuukulia Wokovu’. Nanukuu kutoka ulichotufundisha, “Tunasoma katika 1PETRO 2:2,” Kama watoto wachanga waliozaliwa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu“. Maziwa haya yasiyoghoshiwa ni nini? Ni mafundisho ya Neno la Mungu yanayofundishwa kwa kuzingatia Biblia inavyosema, bila kuchanganywa na taratibu tu za kibinadamu.” Pia umetushauri kutokuzunguka zunguka kwenye mahubiri manyonge yenye upungufu.

    Kama nimekuelewa vizuri katika hiki ulichokihubiri, kipimo kizuri cho kuukulia wokovu ni mafundisho yanayozingatia Biblia inavyosema. Maana unyonge wa mahubiri huzalisha watu wanyonge. Nayo Maandiko yanasema hakuna kinyonge kitakachoingia Mbinguni! Basi, katika kuukulia wokovu, kanisa lako likiwa ndicho kigezo, nimewaona wanawake wote wakifunga vitambaa vichwani, tofauti na makanisa mengine yanayokiri wokovu, kwao silioni jambo hilo likitimizwa; Je hiyo siyo Ishara tosha ya unyonge na upungufu wa mafundisho iwapo jambo hilo ni fundisho la Biblia? Maana umetushauri twende huko!

    Ubarikiwe Askofu.

  2. nimefurahia sana mafundisho haya, ni ukweli uliotolewa kwa ufahamu mkubwa na mpangilio mzuri sana. Mungu akubariki Askofu Kakobe!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s