NINI MAANA YA NENO “KUOKOKA” AU “KUOKOLEWA?”

Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kukupata. Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri. Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika hapo inasemekana umeokoka.

KUZALIWA MARA YA PILI NI NINI?

Nikodemo hakuelewa maana ya kuzaliwa mara ya pili kama jinsi ambavyo wengi hawafahamu leo. Nikodemo aliuliza:

YOHANA 3:4:”Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee! Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?” Jibu ni hapana! Kuzaliwa mara ya pili siyo kurudi tumboni mwa mama yako. Kuzaliwa mara ya pili ni hivi:

Yesu Kristo anaitwa Adamu wa pili au mtu wa pili aliyetoka mbinguni. Adamu wa kwanza alitoka katika udongo na alipojaribiwa na shetani, alifanya dhambi. Adamu wa pili au Adamu wa mwisho, Yesu Kristo, alipojaribiwa na shetani, hakufanya dhambi kamwe. Kama atulivyoichukua sura ya Adamu wa kwanza na tukawa watenda dhambi, basi kwa imani katika Kristo, Yesu, tunazaliwa mara ya pili na kuchukua sura ya Adamu wa mwisho, Yesu Kristo; mwenye uwezo wa kushinda dhambi. [SOMA 1 WAKORINTHO 15: 45, 47-49; WAEBRANIA 4:15]. Tunakuwa tumezaliwa kwa Roho yenye kuhuisha. Hapo mwanzo tumboni mwa mama zetu tulizaliwa katika mwili, tukachukua sura ya yule wa mwili Adamu, sasa tunazaliwa kwa Roho na kuchukua sura ya yule wa Roho; Yesu Kristo. [YOHANA 3:6]. Kwa sababu hiyo, kama jinsi Yesu Kristo alivyokuwa na uwezo wa kushinda dhambi, sisi nasi tunakuwa na uwezo huo pia. Matokeo haya yanatufanya tuishinde dhambi na kuhesabiwa haki ya kuingia mbinguni.

HATUA SITA (6) ZA KUFUATA ILI KUZALIWA MARA YA PILI, KUHESABIWA HAKI, NA KUOKOLEWA KUTOKA KATIKA GHADHABU YA MUNGU

1. UKUBALI KWAMBA WEWE NI MWENYE DHAMBI, UMEMWASI MUNGU, NA
UNASTAHILI HUKUMU
Umekwisha fahamu kwamba wewe ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa na kwa kutenda. Ndivyo ulivyo. Huwezi kukataa. Maisha yako yanakushuhudia mwenyewe kwamba uko mbali na mapenzi ya Mungu. Ukiri wazi jambo hili kama walivyofanya watu hawa katika Biblia:

2 SAMWELI 12:13:
“Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi ……….”

1 SAMWELI 15:24:
“Ndipo Sauli akamwambia Samweli, nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA…”

YOSHUA 7:20:
“Akani akamjibu Yoshua akasema kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA Mungu wa Israeli nami nimefanya mambo haya na haya.”

ZABURI 32:5:
“Nalikujulisha dhambi yangu, wala sikuuficha upotevu wangu. Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA ………….”

2. USIKITIKE KABISA KWA DHAMBI ZAKO, UZIUNGAME NA KUWA TAYARI KUZIACHA KUANZIA SASA NA UWE TAYARI KUOMBA MSAMAHA

ZABURI 38:18:
“Kwa maana nitaungama uovu wangu, na kusikitika kwa dhambi zangu.”

MITHALI 28:13:
“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

LUKA 18:13:
“Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.”

1 SAMWELI 15:25:
“Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu …………….”

2 SAMWELI 24:10:
“Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma ……. Naye Daudi akamwambia BWANA, nimekosa sana kwa haya niliyofanya; lakini sasa, Ee BWANA, Nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.”

EZRA 10:1:
“Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume na wanawake na watoto maana watu hao walikuwa wakilia sana.”

EZEKIELI 18:30 – 31:
“…..Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote …… Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya …….”

1. UKIRI KWAMBA HUWEZI KUACHA DHAMBI KWA NGUVU NA UWEZO WAKO NA UOMBE MSAADA WA YESU KRISTO MWENYE NGUVU.

Huwezi kuacha dhambi kwa nguvu zako au uwezo wako! Dhambi ina nguvu na uwezo juu ya mwanadamu. Kwa nguvu zako, utajaribu kuacha sigara na kutafuna pipi au peremende lakini siku mbili tatu unajikuta unarudia tena kuvuta sigara. Kiu ya sigara huwezi kuishinda kwa uwezo wako. Kwa nguvu zako utajaribu kuacha uasherati na uzinzi kwa kuogopa magonjwa ya hatari kama UKIMWI, kisonono au kaswende; lakini utajikuta baada ya muda mfupi tamaa iko palepale. Utajitahidi kuacha pombe na kuanza kunywa kahawa lakini muda mfupi unashindwa kabisa kuishi bila kunywa pombe. Ni lazima ukiri kwamba huwezi. Dini haiwezi kumfanya mtu aishinde dhambi. Tangu uwe na dini, hujaweza kushinda dhambi. Watu wenye dini ndiyo ambao wamejaa magerezani wakiwa ni wahalifu wakubwa. Unachotakiwa kufanya ni kusalimu amri na kuanguka miguuni pa Yesu Kristo aliyeshinda dhambi, yeye atakupa msaada na uwezo wa kuishinda dhambi.

AYUBU 26:2:
“Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo! Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu!”

4. MWAMINI BWANA YESU

MATENDO 16:31:
“….. akamwambia, mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

INAKUPASA KUYAAMINI YAFUATAYO

(a) YAAMINI MANENO YOTE YA BWANA YESU
Kumwamini mtu maana yake ni kuyaamini maneno yake. Kuyaamini maneno ya mtu, kunathibitishwa pale tu unapochukua hatua ya kuyatenda. Mtu akikuelekeza kwamba njia hii ndiyo inayokwenda Nairobi, ishara ya kuyaamini maneno yake ni kuanza kuifuata njia hiyo. Kumwamini Bwana Yesu ni kuyaamini maneno yote ya Bwana Yesu yaani Biblia na kuwa tayari kulitii na kulitenda kila neno ambalo anatuagiza tulifanye bila uasi wa namna yoyote. Tunaokolewa kutoka katika uasi.

ZABURI 119:6:
“Ndipo mimi sitaaibika, nikiyaangalia maaagizo yako YOTE”.

(b) UAMINI KWAMBA YESU ALIKUFA MSALABANI KWA AJILI YA
DHAMBI ZETU NA KUCHUKUA HUKUMU YETU
Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Baraba ambaye alikuwa ahukumiwe kifo, aliachwa huru na Yesu akachukua nafasi yake. Aliposulibishwa, tulisulibishwa pamoja naye na kuisulibisha asili ya Adamu inayotufanya tutende dhambi. Tulizikwa pamoja naye na kufufuka naye na kupata upya wa uzima.

WARUMI 5:8:
“………. Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”

ISAYA 53:5:
“Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu.”

WARUMI 6:5-6:
“Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; tukijua neno hili, ya kuwa utuwetu wa kale, (utu wa Adamu) ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.”

(c) UAMINI KWAMBA DAMU YA YESU ILIYOMWAGIKA MSALABANI INA UWEZO WA KUSAFISHA DHAMBI ZOTE. UAMINI KUWA HAKUNA WOKOVU NJE YA DAMU YA YESU.
Mpango wa Mungu, tangu mwanzo kabisa ni damu. Mungu anapoiangalia damu, ndipo ukombozi unapotokea. Habili alihesabiwa haki kwa sababu Mungu aliiangalia damu iliyotokana na dhabihu yake [WAEBRANIA 11:3; MWANZO 4:4] ili mwana wa Israeli aweze kuwa salama wakati wana wa Misri walipokuwa wanapata pigo la kufiwa na kila mzaliwa wa kwanza, sharti lililokuwapo ili kuokoka; ni kwamba BWANA alitaka kuona damu katika kizingiti cha juu na miimo miwili ya mlango. Bila damu, hakukuwa na wokovu. [KUTOKA 12:5-7, 12-13, 22-23]. Katika Torati pia karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu, hakuna ondoleo la dhambi [WAEBRANIA 9:22]. Sasa, kwa jinsi hiyo hiyo, hakuna kusamehewa dhambi na kupata wokovu nje ya damu ya Yesu.

MATHAYO 26:28:
“Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”Amini sasa kwamba damu ya Yesu ikinyunyiziwa kwako leo, dhambi zote zitaondolewa na utawekwa huru mbali na dhambi. Utakuwa na uwezo wa kuishinda dhambi.

5. MKIRI YESU KUWA BWANA WAKO:

WARUMI 10:9:
“Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa Kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”

WARUMI 10:13:
“Kwa kuwa, kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka.”

Neno “BWANA” maana ya “MTAWALA”. Kumkiri Yesu kuwa ni Bwana wako au kuliitia jina la BWANA wako; maana yake kukubali Yesu akutawale katika mambo yote. Mtu mwenye dhambi anakuwa ni mtawala wa maisha yake. Anafanya analolitaka. Huu ni uasi. Kulielezea jambo hili vizuri, ni kwamba mtu mwenye dhambi, amekalia kiti katika moyo wake na kuushika usukani wa moyo. Yeye mwenyewe ndiye dereva. Anakwenda popote anapotaka mwenyewe. Iwe ni dansini, kwenye sinema, katika baa ya pombe n.k. Sasa, kumkubali Yesu kuwa Bwana wako, ni kuwa tayari kuondoka katika kukikalia kiti cha moyo wako na kumpisha Yesu akikalie. Yeye awe dereva wako. Akupeleke anakotaka na wewe umfuate bila ubishi wowote. Ukubali kwenda sawasawa na neno la Mungu. Linakokupeleka, na wewe ulifuate mara moja. Ukubali kuwa mtumwa na ukubali kuwa huna haki yoyote ya kujitawala. Je uko tayari kumfanya Yesu awe BWANA wako? Tazama, yuko katika mlango wa moyo wako leo anabisha. Anataka kuingia akikalie kiti cha moyo wako. Je uko tayari kumpokea na kumfungulia mlango wa moyo wako aingie? Ukimfungulia, utakula pamoja naye katika Ufalme wa Mungu.

UFUNUO 3:20:
“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha, mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.”

6. CHUKUA MANENO PAMOJA NAWE, MWENDEE HAKIMU:

Hii ndiyo hatua ya mwisho: Yesu Kristo ndiye Hakimu atakayeuhukumu ulimwengu
[SOMA YOHANA 5:22; MATENDO 17:31]. Hata kabla ya hukumu ya mwisho, mtu yeyote asiyemwamini Yesu katika hatua hizi ulizozifahamu, amekwisha hukumiwa tayari. Ghadhabu ya Mungu inamkalia, na hata akifa sasa kabla ya kutubu, anakwenda Jehanum moja kwa moja.

YOHANA 3:18, 36:
“Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.”

Kwa hiyo ili ukwepe hukumu au uokolewe, njia ni rahisi tu! Ukiwa umeyaamini na kuyakubali haya yote, chukua maneno yote haya kwa ufupi na mwendee Hakimu ukamwambie akuondolee maovu yako yote. Unafanya hivi kwa kutoa sadaka ya mdomo wako au kinywa chako. Kwa kinywa chako unakiri kwamba ni mwenye dhambi na kuhitaji kusamehewa na kumpokea Yesu awe BWANA wako. Maneno haya tunayoyatamka katika sala kwa Hakimu, ndiyo yanayojulikana kwa jina “SALA YA TOBA”.

Ni muhtasari wa haya yote tuliyojifunza. Siyo lazima yawe sawasawa kwa kila tunayemwabia ayatamke, maana yake ni kwamba hakuna sala maalum ya kukariri ambayo lazima itumike kwa kila mmoja. Ila ni kwamba misingi ya sala hiyo inabidi iwe ni hatua hizi sita tulizojifunza.

HOSEA 14:2:
“Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie BWANA, mkamwambie Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe.”
Ungeweza kuomba mwenyewe ingekuwa pia ni sawa, lakini kwa sababu hujui kuomba, fuatisha maneno haya na kuyatamka. (Huu ni mfano wa sala ya toba inavyopasa kuwa).

S E M A M A N E N O H A Y A

“Mungu Baba, nakuja mbele zako na mbele ya Hakimu wa Ulimwengu, Yesu Kristo. Nakiri kutoka moyoni kwamba mimi ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa na kwa kutenda. Nimekutenda dhambi mno, nimeasi na kuwa mbali na mapenzi ya Mungu. Mimi ni mchafu mno, kwa dhambi hizi nastahili ghadhabu au hukumu yako kali, lakini sasa nakusihi unisamehe dhambi hizi. Narudi kwako na kughairi kabisa na sitaki tena kuyafanya yote yaliyo kinyume na mapenzi yako, lakini kwa nguvu zangu na uwezo wangu siwezi. Nahitaji kukupendeza lakini sina uwezo wangu mwenyewe wa kuweza jambo hili. Nahitaji msaada wako. Ninaamini maneno yako yote na kuwa tayari kuyatenda. Ninaamini kuwa uliteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zangu. Naamini ulimwaga damu yako ili nipate ondoleo la dhambi. Nahitaji damu sasa inisafishe na kuniosha uovu wangu wote. Naamini kwamba katika damu yako kunanguvu ya kushinda dhambi. Nipe nguvu hiyo sasa ili nikutii katika mambo yote. Nizaliwe mara ya pili kwa Roho wako. Nakukubali Yesu uwe BWANA wangu. Karibu moyoni mwangu unitawale. Niongoze popote kuanzia sasa. Lifute jina langu katika kitabu cha hukumu, liandike katika kitabu cha uzima. Asante kwa kunisamehe na kuniokoa. Napokea wokovu huu kwa shukrani katika jina la Yesu. AMINA

–Anin-Gift

Advertisements
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

21 thoughts on “NINI MAANA YA NENO “KUOKOKA” AU “KUOKOLEWA?”

 1. Kuokoka kwa waanadam hili haliwezekani pia hakuna mwanaadamu aishie dunian atende mema na asitende dhambi.
  Somen bible tena

 2. Mungu Yesu akubariki sanaa.
  napata shida kumueleza msabato habari za Yesu kwani watu hawa huwa wabishi saana. Wakati mwingine natamani niwe na uwezo wa kufungua vichwa vyao na kuweka akili yangu kwao, vile mimi namjua Kristo.
  Watumishi wa MUNGU aliye hai, naombeni msaada katika hili Ili tumleetee kristo bikira safi
  asanteni saana.
  Yesu awabariki nyote.

 3. Barikiwa ndugu mpendwa mtumishi hakika “sawa na matendo”kila mmoja atalipwa.

 4. Mko vizuri
  mungu aendelee kuwabariki ili muendelee kufanya kazi yake.

 5. ee mwenyezi Mungu pokea sala zangu na unisamehe mimi mwenye dhambi.nipate fulaya uzima wa milele na furaha siku zote amina.

 6. Hapo ndipo penyewe umelonga mtumishi wa MUNGU , Mungu wa mbinguni akubariki.

 7. Hata mimi nimefurahia ulivyochambua maandiko yanayohusu kila hatua ya wokovu.

  Lakini kwa mtazamo wangu ilitakiwa iishie hataua ya tano tu ya kumkiri Yesu kuwa ni Bwana. Ile hatua ya sita mimi huwa naiona ni ya kimapokeao zaidi ambayo hata ktk biblia mitume hatuwaoni wakiifanya.

  Maana ya kumkiri Yesu ni kama hivi:
  Mwinjilisti: Sungura unakubali kwamba Yesu ni Bwana
  Sungura: Ndiyo nakubali
  Mwinjilisti: Je unaamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua katika wafu?
  Sungura: Ndiyo naamini

  Kwa kufanya hivi Sungura tayari anakuwa ameokoka. Hayo maneno mengine ambayo ndiyo yanatumika sana mimi siyaoni kama ndiyo maana halisi ya kumkiri Yesu ambako kunaleta wokovu

  Pia sidhani kama ni sahihi kusema kuwa mtu anapokuwa hajaokoka (mwenye dhambi) anakuwa amekikalia yeye mwenyewe kiti cha moyo wake, na yeye ndiye dereva.

  Maisha ya dhambi ni maisha ya utumwa mbaya sana ambao mtu hutumikishwa na shetani. Na ndio maana hufika wakati mtu hafurahii kutenda dhambi, anataka kutenda mema lakini bado anajikuta anatenda tu hayo mabaya asiyoyapenda hata yeye mwenyewe. Paul anasema hapo si yeye bali ni ile dhambi itendayo kazi ndani yake.

  Asante.

 8. Naomba kueleimishwa kama kuna aya yoyote ndani ya Biblia inayosisitiza juu ya sala za kukaririshana. Mungu huangalia hitaji la moyo wa mdhambi au kutamka maneno yaliyotengenzwa na mwanadamu na kuonekana kama ni maneno mazuri mbele za Mungu? Kuna fomula ya kuomba toba?

 9. Yesu ainuliwe kwa kipawa ambacho mungu amekujalia kulichambua fundisho la wokovu kwa kina na kwa upako wa roho mtakatifu kazi yako sibure bwana atakulipa usipo zimia roho.usichoke maana nikusudi la mungu kuruhusu utanda wazi ili kila moja hukumu iwe ya haki kwani neno lipo kiganjani mwake ili asipate nafasi ya kujitetea.Bwana akubariki na azidi kukufanya taa na ukombozi kwa kila atakaye soma makala hii.akawenae msaada kwa mwingine ili injili ya kristo yesu isonge mbele.Amina.

 10. Mtumishi wa Bwana,

  Nimebarikiwa na Neno hili la uzima. Ni mafundisho yaliyochambuliwa kwa kina na kwa uelewa mpana wa maandiko. I like a well analysed teachings like this. Non biased doctrines can save peaople from sin. Keeeeeep it up man of God.

  Bring more and more logical and analysed word of God so that many can receive healing and salvation

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s