Vazi Lililotobokatoboka

Katika Biblia, kuna watu ambao walifundishwa habari za Injili ya Yesu Kristo, wakazingatia mafundisho yale. Baada ya kuyazingatia, wakaanza kuyaishi hivyo wakafanyika WANAFUNZI wa Yesu, kweli kweli. Watu ambao hawakuwa wamejifunza habari za Injili, walipoona jinsi wanavyoishi wale Wanafunzi wa Yesu, walishangaa sana kwa kuwa walikuwa wanaishi sawa sawa na walivyofundishwa, na maisha yao yalibadilika yakafanana na Kristo. Jambo hili liliwafanya, wale wanafunzi, waitwe WAKRISTO. Walikuwa wamelivaa Vazi la Ukristo. Ukristo ikawa ni Matokeo ya Vile mtu alivyo.

Miaka iliendelea, Watu wakiwa wanaitwa Wakristo, kutokana na vile walivyokuwa wanaishi. Mwenendo wa maisha yao uliwatetea na kuwatambulisha kwa jamii inayowazunguka kuwa wao ni Wakristo. Lakini kadri miaka ilivyozidi kusonga ile hali ya mtu Kuitwa Mkristo kutokana na alivyoishi nayo iliendelea kubadilika. Kukatokea watu ambao pamoja na Kuitwa waKristo, lakini walianza kutenda mambo ambayo yanatofautiana na mafundisho ya Kristo. Hali hii ilisababisha baadhi ya watu kutumia “Ukristo” kama njia moja wapo ya kujitetea kuwa Yeye ni “Mtu mwema”.

Katika siku zetu, hata sasa unaposoma maneno haya, kuna mahali kuna mtu ambaye anajiita Mkristo lakini anatenda tofauti na Mafudisho ya Kristo. Miaka kadhaa iliyopita, wakati badiliko hili la Ukristo kutoka katika kuwa Matokeo ya mtu anavyoishi na kuwa ni Mtu anayetazamiwa kuwa hivyo, Wachungaji wengi waliibiwa na kupoteza malizao nyingi kwa kuwa watu walikuwa wanajitambulisha kuwa yeye ni Mkristo, kwa hiyo anahitaji msaada wa kulala japo kwa usiku huo tu ili kesho aendelee na safari yake. Na mtu akipewa hifadhi alikuwa anatumia mwanya huo kuiba na kutokomea kabla jua halijachomoza. Vazi la Ukristo likawa limetobolewa tobolewa. Ikawa ni lazima mtu avae vazi jingine ndani ya vazi hilo ili kukinga yale matundu ya vazi la Ukristo.

Baada ya kuona hivyo, wale walioendelea kuishi kwa kadri ya Mafundisho ya Yesu, ilibidi waweke vazi jingine ndani ya Vazi la Ukristo. Wakawa wanaitwa kuwa Mtu aliyeokoka. Kwamba kule kusema tu ni Mkristo ikawa haitoshi tena, ni lazima kuwe na kingine zaidi ya hapo. Wakawepo Wakristo Waliookoka. Ndani ya Wakristo wakawepo Wakristo wanaoishi kidunia kabisa na Wale wanaoishi Kikristo. Hivyo kukaja na Vazi jipya la “Kuokoka”.

Miaka imekwenda, huku vazi la Kuokoka likiwa linatumika kuziba yale matundu ya Ukristo, lakini inaonekana kuwa Vazi la “Kuokoka” nalo linaonekana Kuchakaa,na pengine tayari limeshaanza kutoboka. Kule kusema mtu “ameokoka” nayo inakuwa tu ni mtu anayetazamiwa kuwa hiyvo! Wengi wametapeliwa kwa jina la “kuokoka”. Wasichana na wavulana wengi wamejikuta katika misiba ya ndoa kwa kuwa wakati wa uchumba, mmoja wapo alivaa vazi la Ukristo lililotoboka, kisha akavaa na vazi la ‘Kuokoka” ambalo nalo kumbe limetoboka pia….! Na mifano mingine mingi ya yakuonyesha jinsi hali hii ilivyo.

Nimetafakari, nimewaza sana kuwa baada ya hivi vitambulisho viwili, au mavazi mawili kutobokatoboka, yaani Ukristo na Kuokoka kutokutosheleza kuwa ni Jina la Mfuasi wa Kristo, ni jina gani jipya litafuatia baada ya haya mawili? Ikiwa wakristo wa kwanza, waliookoka katika mapambazuko ya Injili, walistahili Kuitwa Wakristo kwa kuwa waliishi kama Kristo alivyofundisha, nadhani bado kuna uzuri kwa Wafuasi wa Kristo kutambulika katika jamii inayowazunguka kwa kuwa Ni Mabalozi wa Kristo. Je, hao wanatambulika au watatambulika kwa jina gani jingine?

Naendelea kuwaza…..

Maandiko ya rejea: Mdo 11:26; Lk 11:39; Math 23:25-28

John Paul

Advertisements

4 thoughts on “Vazi Lililotobokatoboka

 1. Jina zuri na la kibiblia ni kuitwa wa-kristo. MIMI NI MALI YA KRISTO ‘christian’, KIMAUMBILE na kisaikolojia, jina kama ilivyo sura si mali yangu, NI MALI YA WATU WENGINE KUNITAMBUA MIMI, mimi sina namna ya kujiita mwenyewe. KOSA lililipo ni kuwa kuwa WATU WANAJIITA wenyewe WAKRISTO, ‘WALIOOKOKA, nk.
  Hata Bw. YESU hakuwahi kujiita majina: mimi ni MWANA WA MUNGU, au mimi ni MUNGU lakini watu walioona kazi zake walisema “HAKIKA HUYU NI MWANA WA MUNGU.
  Kumbe sisi wakristo tukishaanza tu KUJIITA: mimi mkristo, MIMI nimeokoka, Mimi MTOTO WA MFALME, tunakuwa tunatafuta SIFA badala ya KUTOA HUDUMA ZA UKRISTO. Tumeshazoea MIMI NAITWA ………. nimeokoka nampenda Yesu. KOSA LA KUJIITA. Hata shetani ameshaanza kujiita, maana hilo ni rahisi.
  KOSA la pili baada ya kujiita, ni KUWATENGA WATU WENGINE: Hawa hawajaokoka (Hii si kazi yangu mimi kutenganisha waliookoka na ambao hawajaokoka) hiyo ni kazi ya Mungu.

  Inabidi watu watutambue kwa MATUNDA. Watu waone uvumilivu tulionao, Upendo tulionao, upole, kiasi nk. Watu waone uvaji, lugha tunzotumia watamtukuza Mungu na kusema huyu mtu anaonekana ni MKRISTO au AMEOKOKA.
  Na matunda haya YATADUMU TU kama yanatokana kweli na NGUVU YA KIMUNGU na UHUSIANO WETU NA MUNGU.
  Mungu awabariki

 2. Bwana asifiwe!Jina sio kitu japo asilimia fulani linabeba uzito lakini angalia sifa za jina na matendo ya mtu mwenye jina hilo Bony mwaitege alisema utanitambuaje kama nimeokoka tazama MATENDO.

 3. Nasema jina si kitu, nilipokuwa natafakari kwa undani, nikawakumbuka watoto wangu, mimi ni kabila tofauti na mke wangu, sasa tumezaa watoto wetu, hawajui cha kwetu wala cha kwao mama yao. Mashuleni waliposoma, wakiulizwa wanasema kabila ya baba yao, wengine wanasema ya mama yao, lakini akiongeleshwa hicho kilugha, anaumbuka, anaishia kusema nilikulia mjini, kwa Walokole wengi, Wakristo wengi, wanaposemesha Kikristo wanaumbuka, wanasema wamekulia mjini, kwetu hatufanyi hivi na vile. Iko siku ya kuumbuka. Niwashauri, wazazi wa Wakristo -.yaani Wachungaji wa kweli wajitahidi kuwafundisha watoto wao ( yaani washirika kikristo, kilokole) wasije wakajitetea kuwa walikulia mjini watakapoumbuka. Asante.

 4. Shaloom, nadhani jina kama jina halimfanyi mtu awe kile kijana linamtaja. Kumbuka Yesu alisema kulikuwa na WANAWALI 10. Wote waliitwa WANAWALI, Ila akasema 5. Walikuwa wenye busara, na 5 walikuwa wapumbavu. Lakini wote waliitwa WANAWALI. Hata Wakristo nao, wapo wapumbavu na wenye busara. Pia akasema, walikuwepo WAJENZI wenye busara, na WAJENZI WAPUMBAVU. Wote waliitwa WAJENZI, Wote walijenga, tofauti ni wapi walikuwa wanajenga. MWAMBANI na MCHANGANI, zote zilitw a nyumba, zote zilijaribiwa, matokeo ndio yaliyo sema Mpumbavu ni yupi na mwenye busara ni yupi, WANAWALI wote walikabiliana na giza, wote walihitaji mafuta ya kumulikia, hapo ndipo ilijulikana Mwenye busara ni nani na mpumbavu ni nani. . Ndio maana wataalam wakatengeneza mashine ya kupimia fedha, iko noti ya elfu 10. Zote zinafanana kabisa, kwa macho unashindwa kutambua ipi ni ipi, lakini mashine inazitenganisha ka bisa, nimalize kwa kusema hivi, JINA kama jina, hata mtu angeitwa Mlokole, au Mtume, Nabíi, Mwinjilisti, Mch, au Mwalimu, hamfanyi awe hivyo. Mmoja akasema, siku moja wanyama walialikwa kwenye sherehe wote wakavalishwa sut, pamoja na punda, saa ya kuwika ilipofika aliwika tu pamoja na suti. Jina si kitu. Ndani. Asante.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s