Kuishi maisha ya Imani, Katika Ulimwengu Usioamini!!

Kuishi maisha ya imani maana yake ni kuwa kwa kipindi chote cha maisha yetu hapa duniani, kwa kipindi chote cha uhai wetu, na kwa namna yoyote ile inayoashiria maisha kama kuongea kwetu, kutenda kwetu, kuwaza kwetu, kuenenda kwetu, kuvaa kwetu, kula kwetu, kuona kwetu, kukiri kwetu, kutoa na kupokea kwetu, kufanya kazi kwetu, lupigana kwetu, kushinda kwetu, kuomba kwetu na hata namna yote ile ya kuwajibika kwetu kwa watu wengine tunayafanya haya yote kwa imani.

Tunayafanya haya yote kwa uhakika kabisa, kwa kutokuwa na mashaka wala hofu, tunayafanya kama vile tumejua mwisho wake hata kama hatujayaona kwa macho yetu bado. Kama kuna mambo tunatarajia katika kuishi kwetu, basi kuishi kwa imani katika hayo tunayoyatarajia ni kuishi tukiwa na uhakika na udhihirisho ya kuwa hayo mambo yatatokea na kufanyika halisi maishani mwetu bila kujali changamoto zitokanazo na imani yetu katika mambo hayo.

Katika tafsiri ya kitabu cha Waebrania 11:1, Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”. Kwa lugha nyingine naweza kusema, imani ni udhihirisho wa mambo ninayoyatarajia kuyapata, mambo ninayotumaini kuyapata, mambo ninayotamani na kuwa na shauku nayo katika maisha yangu. Kwa hiyo naishi kwa namna inayodhihirisha na kuthibitisha kabisa kuwa kuna mambo ninayoyangojea hapo mbele.

Kama imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, hii inamaanisha kuwa ni muhimu sana kuyajua hayo mambo yatarajiwayo ni mambo gani kwasababu siwezi kuwa na imani na kitu nisichokijua. Kwa mfano, siwezi kuwa na imani kama Yesu Kristo atarudi tena wakati simjui Yesu mwenyewe wala jambo lolote kuhusu yeye, siwezi kusema nina imani Yesu ataniponya wakati hata sijawahi kusikia habari za Yesu na kwamba yeye ana uwezo wa kuponya. Hivyo ni lazima niwe nimesikia habari za jambo Fulani, ni lazima niwe nimeyajua hayo mambo ninayoyatarajia ili niseme sasa nina imani nayo kwamba yatatokea kwangu.

Ninachosema hapa ni hiki, kwa sababu imani chanzo chake ni kusikia, ni muhimu sana kujua unasikia juu ya nini. Kila mtu hujenga imani ya kile anachokisikia na zaidi sana kile achokifahamu na kukijua. Ukisikia sana habari za waganga basi utajenga imani yako kwa waganga lakini kitu cha kujua hapa ni kuwa kama wewe ni raia wa ufalme wa Mungu basi ni lazima imani yako iwe katika mambo yatokanayo na ufalme huo.

Neno la Kristo ndio msingi wa kujenga imani ya kweli kwa kila aaminiye kwa moyo wake na kukiri kwa kinywa chake kwamba Yesu ni Bwana. Kwa hiyo kama nimeamua kuishi maisha ya imani ndani ya Yesu, ni lazima nizidi kumsikia sana Yesu ili nizidi sana kujenga imani yangu kwake kwenye mambo ninayotarajia.

Kabla sijajua kuwa Yesu ni mwokozi nilimdharau na kuwakejeli wote walionambia habari zake, kwa hiyo nisingeweza kuishi maisha ya imani wakati huo.

Nilipomjua Yesu ni nani, kwa kusikia, nikajenga imani yangu na kuanza kutarajia mambo kadha wa kadha yaliyondani yake yeye. Kwa hiyo hakika ya mambo yatarajiwayo inakuja kwa kuzidi sana kuongeza ufahamu katika kuyajua hayo mambo yaliyofungwa ndani yake yeye ninayemwamini.

Mambo yatarajiwayo, kwa tafsiri niliyoiweka hapo juu, inamaanisha mambo ninayotumainia ndani ya imani yangu katika Kristo na haya mambo ni kama:

 • Uzima

 • Uponyaji

 • Baraka za mwilini na za rohoni

 • Mafanikio na maendeleo

 • Maisha ya ushindi

 • Ulinzi

 • Uzima wa milele

 • Masomo

 • Chakula

 • Mavazi

 • Nguvu

Kwa kuchukua mfano mmoja hapo juu, mimi nimeokoka ingawa nimekuwa naishi maisha ya hali ya chini kiasi kwamba hata mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na hata mahali pa kulala sina, kuishi maisha ya imani katika hali hii ni kuwa na hakika juu ya hayo mambo ninayoyahitaji kuwa nitayapata kutegemeana na imani yangu katika yeye ninayeamini, yaani Kristo, kuwa anaweza kunipa hayo yote sawa sawa nay ale ninayoyafahamu na kuyajua, yale niliyoyasikia amesema kuwa atanifanyia.

Ingawa mwili wangu utaonekana kuchakaa lakini imani yangu inanipa nguvu na tumanini kwani ninajua kabisa kuwa ipo siku Yule ninayemwamini atayabadilisha maisha yangu kwa kadri ya imani yangu, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yangu na zaidi sana kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake.

Kwa upande mwingine, kuna mambo yasioonekana ambayo nayo tunatakiwa tuishi kana kwamba tumeyaona na hapa Neno la Mungu linasema, Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Neno bayana ni sawa na kusema halisia, imani ni uhalisia, waziwazi au inayooneka kabisa kwa macho ya nyama na damu. Umesubiria mtoto kwa muda mrefu, imani inakupa nguvu na tumaini la kuendelea kuishi maisha yako kila siku kama mama aliyepata mtoto tayari. Bayana.

Halisia. Inayoonekana. Kama kuna jambo lolote lile ninalolingojea na bado sijaliona, ninatakiwa niwe nalingojea kama vile nimeshaliona kama vile Babu Ibrahimu, habari zake zinasema alitarajia yasiyoweza kutarajia, alitarajia mambo yasiyoonekana kana kwamba yameonekana, alimtarajia Isaka wakati hali yake na ya Bibi Sara haikuwa na uwezo wa kuwapa motto.Lakini yeye alisubiri katika kutarajia kwake mambo yasiyoweza kutarajiwa kabisa. Nguvu ya imani yake aliipata kwa kumjua anayemwamini.

“Mjue sana Mungu, ili uwe na amani na ndivyo mema yatakavokujia”, ndivyo utakavyozidi kupata ushindi maishani mwako, ndivyo utakavyozidi kushinda vita na makwazo ya duniani hapa na ndivyo utakavyozidi kuishi maisha yenye utulivu na usalama kwa maana unamjua yeye akupaye nguvu za hata kupata utajiri.

Kwa hiyo kuishi maisha ya imani ni katika hali zote kwa maana pasipo hiyo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima, sio ombi, lazima aamini (awe na hakika wa mambo anayotarajia toka kwake) kwamba yeye Mungu yuko na zaidi ya hayo huwapa thawabu, huwapa Baraka, huwapa mambo mema, huwapa mafanikio, huwapa hazina njema wale wote wanaomtafuta. Katika hali zote, kufanikiwa au kutokufanikiwa, kupata au kukosa, raha au mateso.

Imani inahitajika na hivyo wakati wa Furaha wewe furahi kwa imani na wakati wa majaribu ya imani yako usiseme hii sio imani kwani ni vema

kuhesabu ya kuwa ni Furaha tupu tunapoingia katika majaribu mbali mbali tukijua kuwa kujaribiwa kwa imani yetu huleta saburi maishani mwetu. Kwa hiyo neno imani lina maneno matano ambayo ni:

 1. Hakika-kutokuwa na shaka wala hafu, thabiti

 2. Mambo-ahadi za Mungu unazozijua kama Neno lake linavyosema

 3. Yatarajiwayo-tumaini la kungojea na kusubiri

 4. Bayana-halisia, inayoonekana

 5. Yasiyoonekana-kwa macho ya nyama na damu

Kwa hiyo, ninapomalizia ukurasa huu, napenda kusema kuwa kuishi maisha ya imani ni kuishi maisha tegemezi katika kile anachokisema Mungu. Ni kuishi maisha ya mtu wa haki, mwenye haki anaishi kwa imani, anaishi kwa kuwa na ujasiri na uhakika wa mambo yote anayoyatarajia hata kama hajayaona kwa macho yake. Tunawaza kwa imani, tunaongea kwa imani, tunakula kwa imani, tunatembea kwa imani, tunafanya kazi kwa imani, tunaomba kwa imani, tunaangalia kwa imani, tunaenenda kwa imani na kwa ujumla wake yote tunayoyafanya iwe ni kwa neno au kwa tendo tunayafanya yote kwa imani katika jina la Yesu tukizidi sana kumshukuru Mungu Baba.

Kwa maana tunajua ya kuwa pasipo imani, haiwezekani kumpendeza Mungu kwani sisi kama wenye haki imetupasa kuishi kwa imani. Kuna uhusiano kati ya kuwa mwenye haki na kuishi maisha ya imani. Haiwezekani mtu akaishi kwa imani bila kuhesabiwa haki katika Yesu Kristo aliye mwanzilishi wa imani yetu. Na huu uhusiano ndio tutakao uchambua na kujifunza juu ya kwa nini mwenye haki aishi kwa imani. Umebarikiwa katika jina la Yesu Kristo!

–Sehemu ya kitabu cha Mtumishi wa Mungu, Mwinjilisti Raphael Joachim Lyela

Mawasiliano zaidi kuhusu kitabu chake wasiliana nae

Email: annointedkaka@yahoo.com

Simu: 0787 110 003

Advertisements

11 thoughts on “Kuishi maisha ya Imani, Katika Ulimwengu Usioamini!!

 1. Mungu akubari sana kwa kukupa mafunuo ya kuandika ujumbe mzuri ambao kwakweli nimejifunza kitu chatofauti sana.

 2. Docta Lightness, utukufu kwa Mungu.

  Efeso 4:11… inaonyesha wazi wazi jinsi mwili wa Kristo unavyotakiwa kuwa na lengo lake, kila mmoja wetu ni kiungo ili kkukamilisha mwili wa Kristo na tena kila mmoja wetu amepewa au amefuniliwa kwa kiwango chake hivyo nimefurahi kusikia kuwa tuko pamoja katika kuisema kweli ya Neno la Mungu,mimi naamini kuwa bila kujali idadi ya watu unaweza kufanya kitu mahali popote ulipo hata kama ni ni ofisini au njiani, tuungane pamoja katika kuhubiri injili na kulisema Neno kwa ujasiri mkuu, haya ndio mapenzi ya Mungu

 3. ni kweli ulimwengu tunaoishi sasa ni ulimwengu usioamini kutokana na changamoto mbalimbali yeyote atakaeweka maneno haya katika matendo kwa msaada wa Roho mtakatifu atakuwa mshindi songa mbele mtumishi na endelea kupanda mbegu hii nzuri kwa maisha ya watu siku moja zitaota

 4. nimebarikiwa na somo lako mtumishi wa MUNGU mimi pia huwa naandika makala za imani kwa blog hii asante sana ni kama kwa ulimwngu wa roho tupo pamoja sababu unayoyasema na mimi nimeyasema pia ingawa atujuani ni kweli mungu anataka kanisa litoke kwa level moja na kwenda kwa level nyingine nakutia moyo endelea kueleza kweli ya MUNGU sababu siku izi watu hawaamini neno tena bali wanawaamini sana maneno ya wanadamu mtu anaamini neno la nabii kuliko hata neno la Mungu lazima tufike mahali tuishi kama neno linavosema na sio kama watu wanavyotaka.Hili somo linaitajika sana haswa kwa hizi siku za mwaisho mambo ni mengi na changamoto za maisha ni nyingi lazima tuamue kuishi kama MUNGU anavyosema ili tutoboe otherwise tutakuwa watu wa kumlaumu MUNGU kila siku

 5. Kaka yangu Samuel,

  Nimesoma comment zako na kuzielewa fika, asante kwa namna ulivyoiweka. Lengo langu halikuwa kutafsiri kinyume na biblia bali kumfanya Ibrahim babu yangu pasipo kuleta uelewa watu wanaosema Yesu alioa au kuzaa na vitu kama hivyo. Najua Ibrahimu ni baba yangu wa imani.

  Vinginevyo,asante kwa kuwa makini na ushauri wako. Nimeuelewa kabisa. Na kuhusu maswali yaliyoulizwa najua kila mmoja ana ufunua na uelewa wa mambo kwa kadri ya neema ya Mungu kwake, kwahiyo sote kwa pamoja tutashirikiana kuelewa hayo maswali kwani yana umuhimu na nguvu sana hasa kwa nyakati tulizo nazo leo.

  Yes,mawasiliano yatapatikana mapema baada ya kuwekwa wakfu.

  Kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.
  Jesus Up!
  Raphael

 6. Ubarikiwe,mpendwa Joachim kwa mafundisho mazuri naomba pindi kitabu kitapokuwa kimewekwa wakfu tayari usisite kutujulisha namna ya kukipata,Mungu akubariki sana.

 7. ht mimi nmebarikiwa sana na somo la imani. watu wengi wanapenda kuombewa swali je mna imani? ahsante kaka Raphael, Mungu akubariki

 8. Ninachojaribu kukionyesha hapa ni kwamba twapaswa kuwa makini na kila kinachotoka vinywani mwetu, maana imeandikwa TUTATOA HESABU, Mfano nilioutoa kwa ndugu mhubiri MJUKUU WA YESU, akikutana na watu wanaopotosha ambao wanasema kuwa Yesu alioa, akazaa watoto, hata nao wakazaa, yaani wajukuu wapo, atawasaidiaje? Naye ni mjukuu, Yesu ni BABU yake? Ukisoma katika Biblia, Paul alikuwa BABA yake Timotheo, na bado tunaamini Timotheo naye alizaa watoto ktk Imani, bado walikuwa watoto wa Paul, siyo wajukuu wake. Nashukuru kwa somo lako la Imani, tunangoja maswali ya Mr Milinga yajibiwe. Barikiwa.

 9. Ndugu Joachim Shaloom, asante kwa makala yako kuhusu Imani, pamoja na maswali ambayo Mr Milinga ameyauliza, ambayo yanangoja majibu, ama kutoka kwako, au kutoka kwa waalimu wengine wa Imani, ili tuendelee kujifunza, maana pia itatusaidia kupambanua hata IMANI POTOFU, ZA MASHETANI, Ambazo nazo pia zinatenda MIUJIZA. Na kwa kuwa tunajifunza, nikuombe usome mistari ifuatayo katika Biblia. LUKA 1.73 Imeandikwa BABA YETU IBRAHIMU, YOH 8.39, 56 Hapo utaona wakati wa Yesu, wakisema. WAKAJIBU WAKAMWAMBIA BABA YETU NDIYE IBRAHIM, na 56 anasema IBRAHIM BABA YENU, Ninachotaka kukuonyesha hapa ni kuwa kwa mujibu wa Biblia, Ibrahim ni BABA yetu wa Imani, siyo BABU yetu, mmoja katika mafundisho yake akasema hivi…PALE AMBAPO BIBLIA IMENYAMAZA TUNYAMAZE, PALE AMBAPO IMEPIGA KELELE TUPIGE KELELE. Nilikuwa napita mahali katika Jiji letu la Dar, nikaona tangazo la mkutano, nilikwenda kuliso nilishangaa, mhubiri ameandika jina lake, mbele ameweka :. -( MJUKUU WA YESU ). Sikumpata anieleweshe maana yake. Any way tunajifunza. Barikiwa.

 10. My brother,

  Asante sana kwa comment zako zilizojaa hekima na kuleta changamoto za kiufahamu. Nami kwa sehemu yangu nitayafanyia kazi hayo maswali maana yanasaidia sana, laiti kama ningeyapata kabla ya kukitoa kitabu hiki. Lakini pia yananipa fursa ya kufikiria kuendelea kuandika kwa wakati mwigine juu ya somo hili.

  Kuhusu kukipata kitabu, nitakweleza kwa njia ya email yako uliyonitumia. Kitabu hicho kinawekwa wakfu rasmi ijumaa hii na ndipo kitaanza kuuzwa,kwa hiyo usijali tutaliweka vizuri hilo.

  Mungu akubariki sana mwana wa Mungu.

  Raphael-Jesus Up!

 11. Mpendwa Joachim,

  Ubarikiwe sana kwa kitabu kizuri ingawa umetumegea tonge dogo tu kupitia Meza hii hapa ya duara la majadiliana SG, somo la IMANI bado ni somo pana na gumu sana.

  Nimeshasoma vitabu vingi sana vya Imani, kaseti nyingi za mahubiri ya Imani zimesikika toka kwa watumishi wengi wadogo na wakubwa, mahubiri kuhusu imani yamehubiriwa sana kiasi kwamba watu wengine husema kwamba, kama huna imani huwezi kupata muujiza wa mungu wakati huo huo kuna mtu unamwona anapokea muujiza toka kwa Mungu huku akiwa hana hata imani yoyote ya Ukristo.

  Somo la Imani bado naliona gumu au halijapata walimu wenye mawanda mapana ya maandiko na ufafanuzi wa kuelewweka kwa kila mtu.

  Bado kuna mambo mengi huwa hayapatiwi majibu somo la Imani linapofundishwa. Mambo hayo huwa ni:

  1. Imani ni nini?

  2. Je, kuna mtu anaishi bila Imani? Mbona karibu 99% wanaamini kwamba Mungu yupo hata kama hawatendi yale yasemwayo na maandiko ya Mungu?

  3. Nifanyeje ili nami niwe na Imani hata kama ya chembe ya haradali? Je, nifunge nakuomba kwa siku 40? Je nisome Biblia kila siku? Je, niende chuo cha Biblia? Je, nikae kanisani kila siku au kila Jpili?

  4. Watu wenye Imani na wasio na imani ya kweli utawatofautishaje katika dunia hii?

  5. Imani ya kweli ni ipi? Uislam, Ukristo, Uyuda, Ubudha, Ukomunisti? Upagani?

  6. Kama Ukristo ni Imani ya kweli; sasa nani mkweli hapa? Mpentekoste? Mwangilikani, Mu-EAGT, Mrutheri, Mkatholiki, Mu-orthodox, Mu-sabato? Mujehova witness, ?

  7. Imani ya kweli hapa ni ipi? Wale wanaohubiri hadi miujiza ikatoke? au wale wanaohubiri Neno kwa kina sana bila kuwa na miujiza? au ni wale wanaohubiri Neno kwa kina naa miujiza kufuatana nao? Au ni wale wasiobadilika kufuatana na mabadiliko ya tamaduni za dunia au taifa? Imani ya kweli iko je hapa?

  8. Imani ya kweli ni ipi? Je, ni kule kubarikiwa sana kimasomo, kifedha, kiuchumi, teknolojia, kijeshi, kisiasa, au ni vipi?

  9. Imani ya kweli, ni ipi? Je, ni kule kusali sana, kuimba sana, kutoa sana sadaka, kusaidia wenye uhitaji? Au ni vipi?

  Maswali haya yanaweza kutusaidia wengi sana endapo wapendwa wataweza kujitolea kufafanua zaidi.

  Anyway, where can I get your book in Kigoma region? Mimi niliyeko hapa mwisho wa reli napataje kitabu chako? (0767285417).

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s