Mchungaji Gwajima akana maelezo ya Kova

Aidan Mhando na Patricia Kimelemeta
HATUA ya kukamatwa mtu anayetuhumiwa kuhusika na tukio la kumteka na kumshambulia Dk Stephen Ulimboka limezidi kuibua mkanganyiko,  baada ya  Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kusema raia huyo wa Kenya hakwenda kanisani hapo kutubu,  bali alitaka kumuona kiongozi huyo wa kiroho.

Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kwamba jeshi hilo lilimkamata raia huyo wa Kenya, Joshua Malundi wakati akitaka kuonana na mchungaji Gwajima ili atubu dhambi zake za kumteka Dk Ulimboka.

Hata hivyo jana, Mchungaji Gwajima licha ya kukiri mtuhumiwa huyo kufika kanisani kwake lakini alieleza kwamba haikuwa kwa nia ya kutaka kutubu kosa la kumteka Dk Ulimboka kama ilivyodaiwa katika taarifa za polisi.

Alisema mtu huyo alikwenda kuonana na mchungaji huyo kiongozi lakini kabla ya kuonana naye walinzi wa Kanisa hilo walimkamata na kumtaka aeleze shida yake, ndipo alipodai kwamba yeye ndiye aliyehusika na tukio la kumteka Dk Ulimboka na kwamba yupo na wenzake 12.

Mchungaji Gwajima alisema pia kwamba, raia huyo anayedaiwa ni Mkenya katika mahojiano na polisi mbele ya walinzi wa Kanisa hilo, alisema ana tatizo la kuropoka.

“Tarehe 26/27, mwezi uliopita mtu mmoja alikuja hapa kanisani na kuomba kuonana na mimi lakini, baada ya walinzi kumtaka aeleze shida yake kabla hajafika kwangu ndipo alisema kwamba yeye ndiye alihusika na tukio la kumteka Dk Ulimboka na kwamba yupo na wenzake 12 kutoka Kenya,” alisema Gwajima na kuongeza;

“Baada ya walinzi kuona jambo hilo ni kubwa waliamua kumpeleka katika kituo cha polisi Kawe, ambako alihojiwa na baadaye akatakiwa kueleza wapi anapoishi, ndipo alidai kwamba anaishi katika nyumba ya wageni inayojulikana kwa jina la Maifea iliyopo Kawe,” alisema.

Mchungaji Gwajima alifafanua kwamba, baada ya hapo walinzi wa Kanisa hilo waliamua kuondoka na kumuacha mtuhumiwa huyo katika kituo cha polisi Kawe kwani waliona kazi yao imeishia hapo.

“Walinzi wetu baada ya kumpeleka katika kituo cha polisi Kawe waliondoka lakini baadaye mtu huyo alipelekwa Makao Makuu ya polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema.

Gwajima alifafanua kwamba, baada ya kufikishwa Makao Makuu ya Polisi alihojiwa ambapo baadaye  walinzi wao walipigiwa simu na kutakiwa kwenda  kuhojiwa na kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo la kumkamata mtu huyo.

Alisema baada ya walinzi wa Kanisa hilo kwenda kufanya mahojiano na polisi, baadaye mtu huyo aliitwa na kutakiwa kueleza kama anawafahamu ndipo alipokiri kuwafahamu na kuhusika na tukio la kumteka Dk Ulimboka.

Aliongeza kwamba, baada ya kukubali kuhusika na tukio hilo, mtu huyo muda mchache baadaye  alikana na kudai kwamba hahusiki na yeye ana ugonjwa wa kuropoka.

Mchungaji Gwajima alisema kwa sababu mtu huyo amekamatwa katika Kanisa hilo na kudaiwa kwamba alikwenda kutubu kosa la kumteka Dk Ulimboka, angependa ifahamike wazi taratibu za imani yao zinakataza kumtangazia mtu kufanya toba na pia  haipaswi kutangazwa katika vyombo vya habari.

Serikali iunde Tume huru.
Mchungaji huyo alisema kwamba ni vema Serikali ikaunda Tume huru kuchunguza tukio hilo kwani, nayo ni miongoni mwa chombo ambacho kinalalamikiwa kuhusika na tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka.

Alisema msimamo wa Kanisa hilo ni kwamba, madaktari waache kugoma na Serikali haipaswi kuwafutia leseni madakatari kwani wametumia fedha nyingi kuwasomesha.

Kauli ya Kova
Kwa mujibu wa DCP,  Kova alisema raia huyo alikamatwa katika kanisa la ufufuo na uzima na akiwa na kitambulisho cha utaifa wa Kenya namba 29166938, kilichotolewa Octoba 11 mwaka juzi katika Wilaya ya Nyeri, nchini humo.

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kinchojulikana kama GunStar chenye Makao yake  Iwiru, Wilaya ya Thiaka nchini Kenya na kwamba kinaongozwa na mtu mmoja anayejulikana kama Silencer akisaidiwa na Pft.

Alisema baada ya kuhojiwa raia huyo alisema alikuja nchini Juni 23, mwaka huu kwa ajli ya kufranya tukio lilitokea juni 25 mwaka huu na kwamba baada ya kuhojiwa alisema alikodiwa na mtu ambaye ni mtumishi wa serikali ambaye hakumtaja jinakwa lengo la kuja kumduru Dk, Ulimboka.

Mwananchi 

Advertisements

3 thoughts on “Mchungaji Gwajima akana maelezo ya Kova

  1. Moyoni mwangu ninaumizwa na kitendo cha kumteka na kumfanyia kilichotokea kwa Dr Ulimboka. Kwanza si jambo la kibinaadamu tena kiuungwana wala kistaarabu iwe kisiasa au vinginevyo. Na hili nalisema si kwa huyo tu bali kwa mtu yeyote akitendewa hivyo. Siungi mkono uovu wa mtu yeyote hata kama ni wangu mwenyewe. Ila katika “mkano” niliousoma kwenye magazeti wa Mtumishi mwenzangu hakukunibariki, kwani kwa mamlaka aliyopewa na Mungu ndiyo aliyoyatumia kuwaruhusu walinzi wake baada ya mtu huyo kukiri ya kwamba yeye ndiye aliyefanya kitendo hicho ambacho ni kibaya. Je walimpeleka kituoni kwa madhumuni gani basi; kama si kumtambulisha mtu huyo ili uchunguzi na sheria ichukue nafasi yake? Malumbano kati ya Mtumishi huyu wa Mungu na POLISI yanatoka wapi? Kama toba ya mtu huyo ilikuwa ni siri basi wasingelimpeleka polisi. Mchungaji angelinyamaza. Hivyo basi serikali naichukue nafasi ya kuchunguza na kama atabainika ana hatia-sheria ichukue nafasi yake. “Tiini kila mamlaka maana kila mamlaka yatoka kwa Mungu” alisema Mtume Paulo. Ninamwombea uponyaji wa ajabu Mungu Dr Ulimboka; apone ili yeye na madaktari wenzake waendelee kutuhudumia sisi wengine kwa kile kipaji cha Udaktari ambacho Mungu amewapa kupitia serikali yetu. Schalom!

  2. Bwana Yesu asifiwe, mimi nadhani haikuwa na haja kwa mtumishi wa Mungu kubishana na serikali kwani hakukuwa na umuhimu wa yeye kukanusha au kutokukanusha. Tatizo sasa hivi watumishi wa Mungu tunaishi kimwili zaidi ya kiroho. Mungu peke yake ndie anaweza kumsafisha mtu awe msafi. Mungu atusaidie sana dunia isituhadae

  3. Shaloom wapendwa, kila kazi ina miiko yake, ukifuatilia, Wachawi wana miiko yao, Madaktari wana miiko yao, Askari wana miiko yao. Hata Wachungaji nao wana miiko yao, Daktari hawezi kabisa atoa siri za mgonjwa, au akatoboa siri kuwa mgonjwa anaumwa ugonjwa gani. Sasa hata kama huyo kijana amekuja kanisa kwa Gwajima kwa kutubu, na kweli ametubu maana yake amesamehewa, na anayesamehe ni Mungu, ambaye kwa kupitia Mtumishi wake Gwajima, atakuwa amemsamehe kijana huyo, na kwa kuwa amemsamehe dhambi zake zote, basi Mch Gwajima akikana ni sawa, maana huyo kijana ni mpya siyo yule wa jana na juzi, na kwa kuwa hiyo toba ilifanyika ofisini basi Gwajima ana haki ya kukanusha, hapaswi kumchongea, au kumtolea ushahidi kwenye vyombo vya dola, anajua Mungu amemsamehe, na Mungu akisamehe amesamehe, vyombo vya dola vina vigezo ambavyo vinatumia kufanya kazi zao hata bila Mchungaji. Mungu awasaidie,Asante. .

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s