Viongozi wa Dini wawaonya Polisi

Picha na Tone Media

VIONGOZI wa dini, wamekuja juu na kuonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini, baada ya kudaiwa kumuua Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel TEN Mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, maaskofu hao wamesema tabia ya askari polisi kuhusishwa na matukio ya kumwaga damu, haiwezi kukubalika kwa sababu askari hao wanatakiwa kudhibiti vurugu badala ya kumwaga damu.

Katika mahojiano na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Askofu Msaidizi, Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kuna haja Jeshi la Polisi kuacha tabia ya kuzuia maandamano ya vyama vya siasa kwa kuua raia wasio na hatia.

Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, inatakiwa kujiangalia upya katika kuzuia maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa bila kumwaga damu, “Inasikitisha sana, hali ni mbaya, hivi kweli haiwezekani kuzuia maandamano bila kuua, tujiulize hivi hao wanaozuia maandamano wako ‘trained’ vya kutosha katika kuzuia maandamano? Hivi hawawezi kutumia virungu kuzuia maandamano bila kutumia risasi na mabomu ya hatari, hili liangaliwe kwani kuua siyo vizuri,” alisema Askofu Kilaini.

Pamoja na kutoridhishwa na mwenendo wa jeshi hilo, Askofu Kilaini amewaonya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kujitazama upya ili wasiwaingize wananchi katika hali ya kuuawa ovyo wakati wa kutekeleza siasa zao. Alisema si jambo jema kwa chama hicho, kufanya siasa, huku wananchi wakiendelea kuuawa bila hatia.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste Tanzania, Kanda ya Mbeya, William Mwamalanga, alipozungumza na MTANZANIA jana kwa simu alisema, kuna haja Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmnuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, wajiuzulu kufuatia mauaji ya Watanzania wasio na hatia yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.

Alisema kuwa, viongozi hao wawili, wamepoteza sifa za kuwa walinzi wa raia na kwamba matukio ya mauaji ya kila mara yanayofanywa na askari wa Jeshi la Polisi, yatasababisha nchi kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa tena.

Mchungaji Mwamalanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Jamii wa Kanisa hilo, alisema Tanzania haiwezi kuendelea kuomboleza damu za watu wasio na hatia, huku viongozi waliopewa dhamana wakiwa kimya maofisini.

Alisema Dk. Nchimbi na IGP Mwema, hawana sababu nyingine ya kutowajibika kwa sababu wameshindwa kulinda uhai wa Watanzania.

“Matukio haya yanaendelea siku hadi siku, hii maana yake ni kwamba, polisi wanataka nchi yetu kuingia katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe, hili halikubaliki, ni vema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na IGP Mwema, wawajibike kwa kujiuzulu kwa sababu wamesababisha vifo hivyo. Hatuwezi kuendelea kuomboleza vifo vinavyofanywa kwa makusudi na Jeshi la Polisi, huku viongozi hao wakiwa ofisini bila hata kutoa kauli ya kukemea unyama huo unaofanywa na polisi. Tumeshuhudia vifo huko Iringa, Morogoro, Mbeya, Tarime, Arusha na kwingineko kwa sababu tu watu wachache wanaamua kutoa roho za wenzao kwa sababu wanazozijua wao. Sisi kama watumishi wa Mungu, hatuwezi kuendelea kuombea taifa ambalo watu wake wanaendelea kuuawa kila siku, kwa sababu maombi hayo hata Mwenyezi Mungu hawezi kuyasikiliza,” alisema Mchungaji Mwamalanga.

Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa, kamwe maandamano ya CHADEMA, hayawezi kuwa kisingizio na chanzo cha mauaji ya raia, kwa sababu Dkt. Nchimbi na Kamanda Mwema wamekosa busara za namna ya uendeshaji wa taasisi hiyo nyeti.

“Hata katika nchi zilizoendelea kama Marekani watu wanaandamana, maandamano si uhaini, ni kazi ya polisi kulinda na kusindikiza maandamano hayo na si kuua raia wasiokuwa na hatia, kulikuwa na sababu gani kutumia nguvu kiasi hicho. Hili Jeshi la Polisi ni la Watanzania wenyewe, hatujalikodi kutoka nje, polisi wamepoteza sifa, raia wa Tanzania tungekuwa tumelikodi kutoka nje, tungesema hawana uchungu na nchi yao, lakini hawa ni Watanzania wenzetu, kwa nini wameamua kuwa wanyama?” alihoji.

Mchungaji huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kuna haja ya kufuatilia kwa kina aina ya askari wanaopelekwa katika operesheni mbalimbali, kwani kuna uwezekano wa kuwepo kwa hujuma za makusudi zinaendelea bila uongozi wa juu wa serikali kujua.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, yeye amewataka wananchi kuwa na subira kutokana na kifo cha mwandishi huyo wa habari.

Akizungumza na MTANZANIA, Sheikh Alhad, alisema kifo cha Mwangosi, kimekuwa na utata kutokana na aina ya silaha iliyotumika.

“Ninachojua ni kwamba, Mwandishi wa Habari anapaswa kufanya kazi yake katika mazingira yoyote sambamba na kulindwa kwa usalama wake. Kwa kifo cha Mwangosi hivi sasa ninaiomba jamii ivute subira ili kuweza kubaini ukweli juu ya chanzo cha kifo chake. Hakika kifo cha ndugu yetu huyo kinapaswa kuwa ni somo tosha, bado ninasisitiza kuwa, tunahitaji kujua nini kilichopelekea kupigwa na hadi kupoteza maisha yake,” alisema Sheikh Alhad.

soma zaidi habari hii kwenye gazeti la MTANZANIA

Source: Wavuti 

 

Advertisements

10 thoughts on “Viongozi wa Dini wawaonya Polisi

 1. ACHENI MUNGU AITWE MUNGU KUMBE MAASKOFU NAO NI WATU WA KAWAIDA TU NA INAELEKEA WENGI HAWANA UPAKO KWANINI NAZUNGUMZA HIVYO MBONA NI MUDA MFUPI MAKANISA YAMECHOMWA MBAGALA,ASKARI AMEUAWA ZANZIBAR,KAMANDA WA POLISI AMEUAWA MWANZA HIVI MATAMKO YENU MAASKOFU MULIKUWA MUNAONGOZWA NA ROHO WA MUNGU NI VEMA MUFUNGE MUJIHOJI KULIKONI LEO MAASKARI TULIOWALAUMU LEO TUNAOMBA MSAADA WAO KUNA TATIZO ROHO WA MUNGU ANATUKIMBIA TUFANYE NINI ISIJE IKAWA MUNGU KATUKABIDHI KWA SHETANI ATUADHIBU KAMA ENZI ZA AYUBU ,AYUBU ALIKUWA NA UPAKO JE SISI?????????????

 2. Wachungaji na maaskofu kukaa pamoja na kuamua kutoa tamko la kulaani mauaji au matendo mabaya ya polisi au serikali sidhani kama ni kitu sahihi kibiblia au kinaweza kubadili chochote.

  Ukiangalia vizuri sura nzima ya kanisa utagundua lina mamluki wengi sana wa serikali na mfumo wa usalama. Hivyo hakuwezi kukawa na sauti ya Mungu katika matamshi ya maaskofu na wachungaji wanapokemea serikali maana katika kuandaa hayo makemeo kunakuwa na serikali ndani yake.

  Ukisoma vizuri maandiko utangundua kuwa mara nyingi Mungu amekuwa akitumia mtu mmoja tu au watu wachache sana kukomboa nchi.

  Kanisa la Tanzania mimi naona halina tofauti na serikali, in fact halina tofauti na chama tawala. Ndio mana huwa ukifika muda wa kuombea uchaguzi tunaambiwa “usiombee chama bali omba Mungu atupe mtu safi kutoka chama chochote”

  Safari hii nisisikie mchungaji au mtumishi yeyote ananiambia hivyo. Maana haiwezekani katika kanisa moja wengine wachague mashetani na wengine wachague watenda haki halafu tukasema wote waliongozwa na Roho mtakatifu.

  Safari hii naombea chama tena kwa sauti ya juu sio ya kunong’ona. Labda kama kutakuwa na wagombea binafsi.

  Kuna maaskofu mamluki wengi tu, halafu ati wanatoa tamko la kulaani!!

  Maaskofu hawa ambao kila leo wanakwenda kunywa chai ikulu, na kupewa posho,ati waweze kukemea serikali inapokosea!

  Hicho ni kiini macho!

 3. Mimi siwezi kulaani polisi, nailaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chama tawala – CCM; Serikali na CCM ni kama mwenye mbwa anapoamua kumwamulisha mbwa wake kwamba Kamata huyo – hata kama sio mwalifu, Hivyo lawama kuzipeleka kwa mbwa badala ya kwa Mwenye Mbwa ni uvivu wa kufikiri.

 4. Kitakachofuatia ni police kuhamisha familia zao kutoka uraiani ili wakaishi nazo kambini, kwa maana siku si nyingi mauaji ya makusudi yakiendelea wananchi watataka polisi nao wasikie huo uchungu wa kuondokewa na jamaa/ndugu kinyama kiasi hicho. Maana wanajenga uhasama kati ya familia zao na wananchi

  Hapo kinachotetewa ni chama tawala ambacho kimsingi kimeshindwa kutawala. Anguko lao linakuja kwa kasi kuliko lile la shetani alipooanguka toka mbinguni.

  Kanisa tuchukue nafasi yetu.

 5. inasikitisha sana kwa kweli hiki kitendo kimeumiza watanzania wote tunaopenda amani
  hawa watu nchi imewashinda sasa wameamua kumwaga damu za watu wasio na hatia

 6. hawa maaskari watakua wametumia vyeti vya watu kusomea upolisi ndo mana hawajui wajibu, wao mwenzio hana silaha utatumiaje silaha kha. Nakilaaani sana kitendo hiki ewe polisi uliyeua utajibu nini mbele za Bwana.

 7. ka inauma sana jamani roho gani ya kumuuwa mwenzako bila kosa tena kwa risasi e Mungu mtetee mja wako msamehe uovu wake na umpumzishe kwa amani inauma sana da.

 8. Kwa kweli jeshi letu la polisi limekosa mwelekeo kabisaaaaa!kwanza kabisaa elimu hawana ya kutosha ndio maana wao wakiamua jambo lazima litekelezwe!kifupi kitendo hiki cha mauji tunaweza kukiita ni “TORTURE”ambacho kimataifa hakikubaliki hata kidogo,kwa nini wao wanakialalisha?kwa vitendo hivi vya mauaji ya kinyama?Tunavyofahamu kazi ya polisi is to keep “peace and order”sasa uuaji unatokana katika aya mambo mawili?kwa kweli hatuna jeshi la polisi nchini kwetu ambao wameisomea kazi yao na kuizingatia.Bado elimu ya kuwalinda raia wake wanaiitaji,yaaan imefikia wanaboa kabisaaaaa!subiri dawa yao hipo jikoni,mungu hawezi kuwaacha huku wanazimwaga damu zisizo na hatia!

 9. Inatia kinyaa sana nchi hii wakati mwingine.

  Wanajitokeza Polisi na makamanda wao wanaanza kutoa taarifa za uongo mchana kweupe wakidhani kwamba wao wako juu ya sheria. Hivi ukiwa polisi FFU Tanzania unakuwa juu ya sheria?

  Unajua hawa vijana wa jeshi la kutuliza ghasia (FFU) huwa wanajiona wako juu ya sheria. Haiingii akilini Kamanda wa Polisi RPC anaambiwa uongo naye anakurupuka kuutangaza uongo huo mbele ya kamera za TV na magazeti na redio. Ujinga gani huu.

  Hivi wewe unaweza kuambiwa kwamba aliyefariki amefariki kwasababu ya “kitu kizito kilichorushwa” kichwani mwake au tumboni mwake wewe kama RPC unakubali kuitisha wanahabari na kuwaambia huo upuuzi? Are you serious? Ina maana kwamba Polisi wawapo eneo la kazi na macho yao yanakuwa mapofu hawaoni tena. wanashindwaje kuona kwamba kilichorushwa ni JIWE, RISASI, BOMU, CHUPA YA BIA, CHUPA YA PETROLI, nk? Hivi nchi hii hatuna polisi wenye akili zenye akili?

  Naomba niungane na wengine kulaani vitendo vya polisi letu linaloofanya vitu vya kijinga hadi mtu ambaye hajasoma hata darasa la saba anaona kabisa kwamba polisi ndio wametekeleza mauaji halafu wao wanajiosha kirahisi eti hawakuhusika. Mjini Morogoro walisema eti yule kijana muuza magazeti alirushiwa kitu “kipepeacho” au kwa kimombo “flying object” halafu hicho kitu hadi leo hawakijui eti, HUU UJINGA GANI TUNAENDEKEZA.

  Mwandishi wa habari wa Chanel 10, ameuawa kisha tena wanakuja na porojo zilezile kama siku ile alipopigwa Dr. Ulimboka wakaja na filamu ya kutisha hadi kanisani kwa mzee Gwajima!. Maajabu ya Musa haya bado hatujaona yale ya Firauni!!!!!

  Nalaani tabia hizi chafu za polisi. Mungu awaponye maofisa wa polisi kwani bado mwahitaji hekima za Mungu. Hivi inawagharimu nini kuacha watu wakaandamana au wakafanya mikutano yao ya hadhara kisha wakaongea weeeeee mpaka mate yawakauke na usiku ukifika wataenda kulala, ninyi polisi mwakosa nini? Hivi kama Mkuu wenu kaagiza kwamba mikutano yote ya siasa isendeshwe kama ikiendeshwa na ikalindwa vyema kwa amani ninyi mwakosa nini? Ninyi mwataka kila siku mlaaaniwe tuuuuuu na wananchi kila kukicha? Hebu tafuteni hekima zaidi.

  POLISI, TUNAOMBA TABIA HII IKOME KABISA, NA MATUKIO KAMA HAYA YAWE YA MWISHO HADI UCHAGUZI WA 2015 OKTOBA UTAKAPOISHA.

 10. nami naungana na maasikofu hawa nalaani vikali tabia hii mbaya ya polisi, vinginevyo polisi hatuwahitaji katika jamii yetu. kama wanataka kumwaga damu waende Bagdad, Iran na kwingineko lakini sio hapa Tanzania. mimi sio mwanasiasa lakini nina hasira na vitendo vya polisi kumwaga damu katika mikutano ya siasa. najua mnatetea maslahi kama alivyodai yule kamanda wa Iringa kwamba amekaribia kusitaafu! so kwa kuwa amekaribia kusitaafu anataka aache damu imwegwe na vijana wake. ?

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s