Je! Mafanikio yako kifedha yana matatizo?

Mwaka 1997 tulipokea barua na simu nyingi toka kwa watu wa Mungu mbalimbali wakihitaji maombi kwa ajili ya matatizo yaliyokuwa yanawasumbua katika maeneo ya kifedha. Wengine biashara na kazi zao vilikuwa haviendi vizuri – nakadhalika.
Tulikaa na jambo hili katika maombi. Tarehe 24 Septemba 1997 saa kumi na nusu asubuhi tukiwa katika maombi Bwana Yesu alisema nasi katika mioyo yetu ujumbe ufuatao ambao tunaamini utakusaidia hata wewe. Bwana Yesu alituambia hivi:

 • Roho ya mpinga Kristo ndiyo iliyoshambulia mafanikio ya kifedha katika watu  wangu,

 • Imeelekeza mashambulizi katika mafanikio ya roho zao (na nafsi zao) maana nimesema mtafanikiwa katika mambo yote kwa kadri roho zenu zifanikiwavyo,

 • Kufanikikiwa kwa roho zenu kunategemea kufanikiwa kwa nafsi zenu. Mtafanikiwa katika roho zenu kwa kadri nafsi zenu zifanikiwavyo, na matokeo yataonekana katika mambo yote

 • Nafsi zenu zifanikiwavyo zinategemea utendaji wenu wa Neno langu. Ikiwa utendaji wenu wa Neno ukiwa hafifu, na kufanikiwa kwa nafsi zenu kunakuwa hafifu. Kufanikiwa kwa nafsi zenu kukuwa hafifu na kufanikiwa kwa roho zenu kunakuwa hafifu, kwa hiyo kufanikiwa katika mambo yote kunakuwa hafifu pia.

 • Ndiyo maana nasema roho ya mpinga Kristo imeelekeza mashambulizi yake katika kupinga, kuzuia, na kuchelewesha mafanikio yenu katika roho na nafsi zenu.

 • Lakini mnaweza kushinda kwa kusimama katika Neno langu ambalo ni upanga wa Roho mikononi mwenu.

 • Nimesema katika Yoshua 1:8 ya kuwa mtafanikiwa ikiwa mambo matatu yatafanyika juu ya Neno langu:
  (a) Lisiondoke kinywani mwenu
  (b) Mlitafakari wakati wote
  (c) Na kudumu kulitenda

 • Sasa angalia mmesimamaje katika maeneo hayo matatu. Maana hizo ni mbinu za kulitumia Neno langu kama silaha ya kumshinda adui

 • Mkisimama katika Neno langu ninavyotaka mtavuna mafanikio sana kwa wakati wangu msipozimia na kukata tamaa katika mioyo yenu.

 • roho ya mpinga Kristo inawakatisha tamaa kwa kuwaangaliza matokeo ya upungufu mlionao badala ya kuangalia ahadi zangu na matokeo yake.

 • Kwa kadri mnavyoangalia matokeo ya upungufu mlionao, ndivyo mnavyozidi kutafakari juu ya upungufu mlionao. Kwa kadri mnavyozidi kutafakari juu ya upungufu mlionao, ndivyo mnavyozidi kukiri na kushuhudia upungufu mlionao na matokeo yake.

 • Kumbuka mnayafunga mafanikio yenu kwa maneno ya vinywa vyenu yanayotoka katika nafsi zisizotafakari ahadi zangu na matokeo yake.

 • Mimi si mtu hata niseme uongo. Nililolisema katika Neno langu nimesema nitalitimiliza. Napenda kufanikiwa kwenu kuliko nyinyi mnavyopenda kufanikiwa kwa watoto wenu. Msikubali adui ayumbishe macho yenu na mioyo yenu isione uaminifu wangu.

 • Mkisimama katika neno langu na kupigana hivyo vita vizuri vya imani mlivyo navyo;
  – Mtashangilia ushindi wakati kuta hazijaanguka bado,
  – Mtatangaza ushindi wakati bado upinzani wa adui umesimama,
  – Mtaona mafanikio wakati bado mmezungukwa na upungufu,

 • Kumbuka neno langu linatangaza ushindi katika roho kwanza kabla ya haujaonekana kwa nje. Ndicho kilimchomsaidia Ibrahimu wakati anasubiri mtoto wake. Na ndicho kilichonisaidia na mimi pale masalabani – nilishangilia ushindi dhidi ya adui hata kabla sijafufuka. Daudi naye aliuona ushindi wakati bado Goliati amesimama mbele yake.

  Kila mtu atakuja kwangu na kuuliza nimpe Neno la kusimamia katika vita alivyo nayo. Hamuwezi kushinda pasipo Neno.

Haya ndiyo machache tuliyoyapokea kutoka kwa Bwana Yesu tulipofanya maombi ya kuuliza kwa nini watu wengi wa Mungu wamekuwa hawafanikiwi vizuri katika eneo la fedha. Ingawa Bwana alisema nasi mwaka 1997 tunaamini bado ujumbe una nguvu ndani yake ya kukusaidia. Tafakari maneno ya ujumbe huu, weka katika matendo yaliyomo – na Mungu atakusaidia!

            Ahsante,

Christopher na Diana Mwakasege

Advertisements

8 thoughts on “Je! Mafanikio yako kifedha yana matatizo?

 1. Bwana Yesu Asifiwe Wapendwa Naomba Kuuliza Hairusiwi Kumwabudu Mungu Na Mali !

 2. Watakatifu tu ndio watakao ingia mbinguni; Pamoja na mambo yote kikubwa unatakiwa kutenda wema na kusimama katika nafasi yako vizuri. Mungu akubariki.

 3. Tunapozungumzia masuala ya imani ni lazma watu tuwe makini sana sababu ni kwamba watu walio weng wanapenda sana kuvuruga iman za watu jambo ambalo halimpendez Mungu…. Mungu yupo sana ila unamuamini kwa njia gan?

 4. Shetani mara zote ni muongo, ni Baba wa huo, ni muuaji, alikuwa hivyo tangu kale! Alimwambia Bwana Yesu niabudu, ‘nitakutajirisha’ Hajabadilika yuko hivyo, Haoni taabu kukuhonga Mali, fedha na ukwasi wa kila aina ili aiuwe Roho yako, ni muuaji! Kwanini tusumbukie sana pesa?

  Mtu apatapo wigi wa mali ndipo huwa amebarikiwa sana? Ninani kati yetu mwenye kibari cha kuomba kuliko mwingine? Neno linasema “Ombeni lolote kwa jina langu (jina la Yesu)…….” Kwanini Mtu anakuwa na mawazo ya kuombewa tuuuu? kwa nini?

  Kwani, Mtu akiomba mwenyewe hawezi kupokea kwa nini, wakati neno la Mungu linasema Ombeni nanyi mtapewa…….tena mkisha kuomba aminini ya kwamba mmekwisha pokea navyo vimekuwa vyenu. Kutoamini ndicho chanzo cha kutopokea, Dhambi ni kutoamini neno la Mungu!

  Jambo lingine la kujiuliza, kwanini Wachungaji wanapoanza uombeaji tu wanakuwa matajiri kwa ghafla sana? kwa nini waombeaji hawa hawatangazi kwa bidii kusudi kuu la Injili (Toba na ondoleo la Dhambi) “Strongli wanastiki katika utajirisho tu”? Jambo lolote lisilo la Biblia si la Mungu.

  Kaa chonjo!

 5. YESU WA NAZARETH/ SIJAMSIKIA AKIWAHUBIRIA WATU NAMNA HII. LABDA MNISAIDIE NI BIBLIA IPI MAHUBIRI YA SIKU HIZI YALIYOJAA MALI/FEDHA HUTUMIA.

  “Apendaye fedha hatashiba fedha, wala apendaye wingi hatashiba nyongeza” (Mhubiri 5:10)

  “mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu chochote kwa nafsi yake,katika yote anayoyatamani walakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo” (Mhubiri 6:2)

  “akawakataza wasichukue kitu njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za kibindoni;” (Marko 6:8)

  “msiwe na tabia ya kupenda fedha;mwe radhi na vitu mlivyonavyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, sitakupungukia kabisa, wwala sitakuacha kabisa.” (Waebrania 13:5)

  “Maana shina la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine wakiitafuta hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi” (1 Timotheo 6:10)

  Yesu mwenyewe anasema “Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” (Luka 16:13)

  Yesu anajua uzima wa milele una thamani kuliko fedha ndio maana katika mahubiri yake hakuwaasa namna gani watapata mali kwa maana alijua wataacha kumtumikia Mungu na hata wakimtumikia watapenda mali zaidi.

  Watu waliohubiri na kuleta toba ya kweli kwa ajili ya ujio wa Yesu hawakuhubiri fedha,hata mitume hawakuwapa fedha.

  Batolomayo alikuwa kipofu na ombaomba akaomba kitu chema na si fedha.
  Dunia ya leo tu vipofu wakiroho tuombe uzima wa kiroho si fedha, tuwe na busara kama Batolomayo.

  Petro alitaka pia watu wapate uponyaji na si fedha “Lakini Petro akasema, mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho.”Matendo 3:6

  Kanisa la Laodikia ni moja ya makanisa ambalo watu wake walikuwa na mali na kujiona wamepata kila kitu na kusahau kumtumikia Mungu, Yesu anawaambia ni vipofu hao.

  Yesu akizungumzia mali hazungumzii mali zinazoharibika wahubiri igeni mfano wa Yesu.
  Injili ya Biblia gani hii mnaileta?

  “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona” (Ufunuo 3:18)

  “Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; (Isaya 55:1)

  YESU ANATAKA TUWE NA MALI ISIYOHARIBIKA TUSIWE KAMA WALIVYO WA ULIMWENGU HUU WENYE MALI ZA KUHARIBIKA. UZENI KISHA MUMFUATE.

  “HAMWEZI KUMTUMIKIA MUNGU NA MALI” (LUKA 16:13)

 6. Wanyondo,

  Si wewe tu unayetatizika na huduma ya ‘Utajirisho’ Mimi nami ni kama wewe, ila baada ya kujiuliza, kama ambavyo unajiuliza wewe, nimeamua kuigeukia Biblia maana hata ukiwauliza hawa wachungaji wetu huwa hawajibu! Wapo kinyume kabisa na yule aliyewapa “Kazi” Maana wanajiita (watumishi wa Bwana) Bwana nimjuaye ni Yesu, na yesu alijibu kila swali aliloulizwa na mtu aliyekuwa na nia ya kweli ya kujifunza, ndiyo maana aliitwa ‘Mwalimu’!

  Ukihudhuria makanisani humo utashangaa, kwanza kunaubaguzi wa ajabu, upendeleo kwa “wenye nazo” Ukabila na udini vimetanda. Usipokuwa mwangalifu unaweza kuacha kusali, maana karibu kila “Mtumishi” akikupita karibu, waliowengi wamejaa uchu, uchoyo, ubinafsi, unyonyaji, hawana huruma,watu wafitina, mawazo yao ni pesa tu,hawana huruma hata kidogo nani WAONGO! unaweza kuyaona waziwazi hayo, ninashawishika kusema kama Yesu akishuka sasa hivi kwa jinsi ya kwanza, angeweza kusema pasipo shaka kuwa, “Sioni Mwisraeli wa kwelikweli humo, hawa wote WAMEJAA ila ndani yao!”

  Samahani kama kunaaliyekwazika kwa maneno haya,

  Ila kama yupo Ndugu analo la kuniambia KARIBU!

 7. Mafundisho ya mafanikio kiuchumi yamekua ndio msingi mkuu wa mahubiri ya sasa,nashindwa kujua kwa nini yameshika kasi kubwa kipindi hiki kuliko hata miaka kumi iliyopita?Na kama ni maono Mungu anawapa watumishi wake,je hapo nyuma watu walikua hawahitaji mafanikio?leo hii ni vigumu kutofautisha matangazo ya mganga wa kienyeji na mchungaji,yote yanafanana,mafanikio kiuchumi!!!!Nashindwa kujua je matatizo makubwa yanayosumbua watu wa Mungu sasa ni uchumi(umaskini)?lakini masikini wamekuepo toka mwanzo!!Napata mashaka sana na mafundisho ya sasa ya mafanikio kiuchumi!msaada tafadhali!

 8. Wapendwa Christopher na Diana Mwakasege;

  Kwanza nikubaliane nanyi kwa moyo wangu wote kwamba maandiko ndivyo yasemavyo,kama mlivyoyanukuu! Lakini naomba niulize nami hivi:-

  1.kwanini watu wafikilie sana juu ya ufanisi wa kimwili kwa kipindi hiki kuliko wakati wa mwanzo wa historia ya kanisa?

  2. Je, uhitaji hautokani na roho ya uchoyo na ulafi waliyonayo watu wenyewe?

  Enzi ya kanisa la kwanza, Waongofu ama waumini walikusanya mali au sehemu ya mali zao na kuzikabidhi kwa mitume ili zitumike shirika! Sasa tunasikia na kuona katika ama kupita Luninga au watu wakitoa ushuhuda waziwazi kanisani kuwa, baada ya maombezi wamefanikiwa kiuchumi n.k. Lakini pia yesu alipata kusema kuwa ‘yafaa nini nduguyo akikujia anahitaji, wewe ukamwambia nenda nyumbani ukaote moto na Mungu atakubari! Sasa,

  3. Je, ni wangapi kati yao wametoa sehemu ya hizo mali ambazo wanadai kupewa na Mungu, kuwapa wajane, yatima, Masikini na au wahitaji walau hata kwa wanao sali nao?

  Biblia inasema moja ya masharti aliyoambiwa Yesu, ili akabidhiwe MALI na fahari yote ya hii Dunia, AMWABUDU SHETANI!

  4. Je, huoni kuwa kunamahusiano makubwa kati ya Mali za kimwili na Shetani, japo watu wengi wanadai kuzipata kwa Mungu kwa njia ya maombezi? (najiuliza kama kweli wamepewa na Mungu, je kwanini wawe wachoyo? pili, mali yao hiyo inamtukuzaje Mungu iwapo hawasaidii yatima, wajane au masikini? – {Maana Yesu alimwambia yule mtu tajiri ‘nenda kauze mali yako uwape masikini (yaani siyo apeleke kanisani kwa mchungaji!), kisha uje unifuate’}

  Nitafurahi kupata majibu ya maulizo yangu hayo machache ili nijifunze kitu.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s