Tamko la Maaskofu wa Anglikana kuhusu Waumini kumzuia Askofu Kasagara kuhudumu

TAMKO LA MAASKOFU WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA KUHUSU KUNDI LA WAUMINI WA KANISA LA WATAKATIFU WOTE LA MJINI SUMBAWANGA AMBALO LIMEKATAA KUMRUHUSU ASKOFU MATHAYO KASAGRA KUTOA HUDUMA KWENYE MTAA HUO

Kikao cha Maaskofu kilichokutana tarehe 26 Septemba 2012 huko Mtumba, Dodoma kilitafakari kwa pamoja juu ya fujo zilizojitokeza katika kanisa la Watakatifu Wote huko Sumbawanga tarehe 23 Septemba 2012 zilizosababishwa na kundi lisilotaka kumtambua Askofu Mathayo Kasagara kwamba ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa na kutoa tamko lifuatalo:

KWAKUWA kundi la waumini wanaowakilishwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera wanaojitambulisha kuwa ni viongozi wa Kamati ya Usimamizi wa Kanisa la Watakatifu Wote katika mji wa Sumbawanga iliyo ndani  ya Dayosisi ya Lake Rukwa ya Kanisa Anglikana Tanzania inayowakilishwa na John M. Mahinya ambaye amekuwa akiandika barua kwa niaba ya Kamati wamekataa kumtambua Askofu Mathayo Kasagara kuwa ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Ziwa Rukwa.

NA KWAKUWA viongozi hawa wa kundi hili la waumini walifikisha suala hili kwenye Mahakama ya serikali ya Wilaya ya Sumbawanga kupinga uhalali wa Uaskofu wa Askofu Kasagara na kuomba azuiliwe kutoa kuhudumu yake ya kiaskofu

NA KWAKUWA Mahakama hii ya Wilaya ilikwishatoa uamuzi wake uliomo kwenye Deed of Settlement uliokubaliwa na pande zote mbili mbele ya Hakimu Mkazi Mheshimiwa M. W. Goroba tarehe 17 Januari 2012. Makubaliano ambayo yalitiwa saini na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera kwa upande wa walalamikaji na Askofu Mathayo Kasagara kwa upande wa walalamikiwa. Upande wa malalamikaji ukiwakilishwa na kampuni ya uwakili ya S. Mawalla Law Consultants wa Sumbawanga na upande wa walalamikiwa ukiwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Albert Msando Legal Consultants ya Arusha ambao wote walitia saini zao,

NA KWAKUWA uamuzi huo wa Mahakama kwa kuzingatia kwamba Kanisa la Watakatifu Wote la mjini Sumbawanga ni mali ya Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania (Maaskofu) na uliitaka Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania itoe uamuzi utakaohitimisha suala hili,

NA KWAKUWA Nyumba la Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania linaheshimu maamuzi ya Mahakama za Serikali ingawa viongozi wa kundi hili la waumini walivunja Katiba ya Kanisa kwa kukimbilia mahakamani kabla ya kupitia hatua mbali mbali zilizomo kwenye Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania, Maaskofu waliona vyema wasikilize kwanza hoja za waumini hao kabla ya kutoa uamuzi wao na hivyo kutuma tume iliyokwenda Sumbawanga tarehe 23 Machi 2012 na kuwasikiliza

NA KWAKUWA kundi hilo lilishindwa kutoa vielelezo vya kuthibitisha kwamba Askofu Mathayo Kasagara alitoa rushwa ili achaguliwe kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Lake Rukwa na hivyo kuifanya Nyumba ya Maaskofu itoe uamuzi wa kuendelea kumtambua Askofu Kasagara kwamba ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa,

NA KWAKUWA tarehe 23 Septemba 2012 kundi hili la waumini lilipinga uamuzi wa Nyumba ya Maaskofu wa kumtambua Askofu Kasagara kuwa ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa uliosomwa kwao na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Rev Canon Dr Dickson Chilongani, mbele ya Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, The Most Rev Dr Valentino Mokiwa na Askofu wa Dayosisi ya Ruaha The Rt Rev Dr Joseph Mgomi, ndani ya Kanisa la Watakatifu Wote,

KWA HIYO BASI NYUMBA YA MAASKOFU WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA INATOA TAMKO KUWA:

  1. Kulingana na Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, kifungu cha 14 (8) Nyumba Ya Maaskofu imeridhika kabisa kwamba Askofu Kasagara ni Askofu halali wa Dayosisi ya Lake Rukwa. Kifungu hicho kinasomeka hivi: “Matokeo ya uchaguzi huo ni ya mwisho, hayatapingwa popote na taratibu za kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule zitafuata.”Kifungu kinamaanisha kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania hakuna pingamizi lolote linalokubaliwa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa. Kwa hiyo pingamizi la kundi hili la Watakatifu wote linakiuka Kifungu hiki cha Katiba kwavile liliibuka baada ya matokeo kutangazwa na tena halina uthibitisho wowote kwahiyo halina nguvu yoyote ya kisheria. Pia kifungu hiki kinazuia matokeo hayo kupingwa mahali popote. Hivyo basi masuala ya uchaguzi wa Askofu hayawezi kupelekwa katika mahakama za kidunia. Anayefanya hivyo au anayekusudia kufanya hivyo, kama ni Mkristo au Mhudumu anavunja Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania.
  1. Viongozi wa kundi hili la Waumini wanatakiwa wawasiliane na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania ili wafanye utaratibu wa kukabidhi mali zote za Dayosisi ya Lake Rukwa kwa Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania kama zilivyoorodheshwa kwenye makubaliano yao na Mahakama (deed of settlement) ambayo walitia saini. Mali hizo ni pamoja na Kanisa la Watakatifu Wote, Ofisi ya Mchungaji, Nyumba mbili za Wachungaji, uwanja wa Kantalamba ulio na Nyumba ya Askofu na Chapel ya Askofu, jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya kanisa vilivyopo eneo la Majumba Sita pamoja na St. Matthias English Medium School. Kukaidi kukabidhi mali hizi ni kukiuka maamuzi ya Mahakama, na Kanisa Anglikana Tanzania halitasita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kundi hili.
  1. Nyumba ya Maaskofu inalitaka kundi hili la Wakristo wanaompinga Askofu Kasagara waelewe kwamba muumuni kuwa Mwanglikana ni suala la hiari na kama hakubaliani na mafundisho ya kanisa na maamuzi ya Maaskofu amejitenga yeye mwenyewe na kanisa na hivyo ni vyema akajitoa maana machoni mwa Kanisa yeye ni mwasi na si muumini tena wa Kanisa Anglikana.

Lukwangule

 

Advertisements

One thought on “Tamko la Maaskofu wa Anglikana kuhusu Waumini kumzuia Askofu Kasagara kuhudumu

  1. Hahaa..mbona tamko linajikanganya lenyewe? Mara masuala ya kanisa hayawezi kupelekwa kwenye mahakama za kidunia (tamko kifungu na. 1). Alafu kifungu namba 2 kanisa halitasita kuwachukulia hao waumini wa ‘watakatifu wote’ hatua za kisheria, sasa hizo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa fasiri ya mahakama gani kama si hizohizo za kidunia? Kwa maana hiyo viongozi wa kanisa ndo wana haki ya kuchukua hatua za kisheria, ila waumini wakichukua hatua za kisheria wanakuwa waasi! hii si sawa, hata kama tamko limeshapitwa na wakati ila naliponda kwamba halina weledi wala upako!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s