Mambo ya Kuzungumza na Mchumba Kabla ya Ndoa

Baada ya kuvishwana pete ya uchumba, wasichana wengi huona kwamba kilichoko mbele yao ni kupanga harusi tu. Hujishughulisha kwa hali na mali kuhakikisha harusi inakuwa sawa na ile anayoiwaza siku zote, na kusahau kuwa baada ya harusi kuna maisha ambayo ndiyo haswa yanayopaswa kupangiliwa kwa umakini. Baadaye wanajikuta wameingia kwenye ndoa huku mambo mengi yakiwa hewani na hivyo kupelekea migogoro isiyoyalazima mara tu baada ya ndoa.

Kuna mambo muhimu sana ambayo wachumba wanapaswa wayaongelee na kufikia muafaka kabla ya kuunganika na kuwa mwili mmoja. Yanaonekana ya kawaida sana lakini yanaweza kuleta msuguano na kuharibu kabisa furaha ya ndoa. Tuyaangalie kwa uchache:

1. Mahali pa kuabudu.
Binti anaabudu katika kanisa kubwa na ndiye kiongozi wa sifa na muongozaji wa nyimbo karibia zote za kwaya, na kijana anaabudu kwenye kanisa dogo linaloanza na ndiye mwenyekiti wa vijana na mwalimu wa shule ya jumapili. Hapa nani anamfuata nani? Bila kukaa chini na kujadiliana kwa pamoja jambo hili linaweza kuleta mvutano. Ni vyema mkaangalia kwa mapana na marefu option zote kisha kwa pamoja mfikia muafaka kulingana na huduma ya kila mmoja wenu.

2. Jinsi ya Kuishi
Waafrika ni kawaida yetu kuishi pamoja na ndugu zetu na kusaidiana katika mambo mbalimbali ya maisha. Sio jambo geni kumkuta kijana au msichana anaishi na wadogo zake na kuwasomesha. Linapokuja suala la ndoa ni vyema jambo hili likawekwa sawa mapema. Je mtaweza kuishi na ndugu wangapi? Na wa upande upi na kwa kigezo gani? Je wataanza kuishi nanyi muda gani baada ya kuoana? Pale tu mtakapooana au lini? Hili si jambo dogo na linaweza kuharibu amani kabisa ndani ya nyumba. Ni vyema mkaliweka sawa mapema na wale mnaoishi nao wajue hawaishi tena na kaka au dada bali Mr & Mrs hivyo heshima iwe kwa wote. Pia sishauri kuishi nao mara tu baadavya kuoana, ni bora wakaenda kwa ndugu wengine angalau mwezi mmoja wa kwanza muweze kuwa na wakati wenu wa faragha wa kufahamiana vizuri na kuizoea nyumba yenu mkiwa wenyewe.

3. Mapato na Matumizi
Hili ni eneo nyeti sana. Wasichana wengine wanapoolewa huambiwa kuwa ‘usimwambie mumeo unapata kiasi gani na uwe na akaunti yako ya siri.’ Mmh hapa pana tatizo, maana nijuavyo mimi mwili mmoja ni katika kila idara, hamna siri. Sasa wewe ukificha na mwenzio akaficha, kuna maendeleo kweli hapo? Ni muhimu sana kwa wachumba kukaa na kupanga jinsi ya kuyatumia mapato yenu mtakapooana. Muwe wawazi kila mmoja anachokipata na muainishe matumizi yenu na kuangalia ni kwa jinsi gani mtaweza kuyafanikisha.

Baada ya kuoana, kila kitu kitakuwa ni chenu wote. Kama ulikuwa na nyumba, gari, viwanja, shares, bank accounts n.k vyote vinakuwa mali ya familia, hivyo ni vyema mkaangalia hili mapema ili asije mmoja wenu akajenga nyumba kwa siri bila mwenzie kujua. Pia muangalie ni ndugu gani wanahitaji msaada kifedha na jinsi gani mtaendelea kuwasaidia, mfano ada, matibabu, n.k. Hapa panahitaji hekima kubwa sanabya kiMungu kuamua nani asaidiwe kulingana na kipato chenu kwa wakati huo. Maana ndugu wa kuhitaji msaada wenu watakuwa ni wengi kuliko uwezo wenu. Hapa ndipo mstari wa mithali 14:1 unapoleta maana.
Mithali 14:1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

4. Mipango ya Mbeleni
Shule, ujenzi, kuanzisha familia, kufungua biashara, kuanzisha huduma n.k yote haya yanahitaji kuzungumziwa mapema na kuwekewa misingi. Mfano wewe unahitaji baada tu ya ndoa utafute scholarship ukasome ulaya wakati mwenzio akifunga macho tu anajiona anaitwa baba, hapo lazima shida itatokea. Lazima mjue vipaumbele vyenu kama familia ni nini. Mkishafahamu hilo ni rahisi kujua muanzie wapi na wakati gani. Mume hawezi tu kuamka asubuhi na kusema anaacha kazi na kuanzisha kanisa, sasa familia itakula wapi? Ni lazima mkae chini mpange mjue mume akiacha kazi familia itaishije, mke je atakuwa tayari kubeba majukumu yote?

Mwisho huu ndio wakati muafaka kumweleza mwenzio kama uliwahi kuchumbiwa hadi kutolewa mahari lakini mambo yakaharibika. Pia kama unamtoto ni lazima narudia LAZIMA umweleze mwenzi wako. Usiingie kwenye ndoa na siri yoyote, itakuwa ni bomu la kuwasambaratisha.

Nakutakia ndoa njema yenye baraka, amani na furaha tele.

–Magreth Riwa

Advertisements

24 thoughts on “Mambo ya Kuzungumza na Mchumba Kabla ya Ndoa

 1. Bwana Yesu asifiwe, Awali ya yote, na penda kuwasalimu katika jina la bwana na mwokozi wetu Yesu kristo. Kwanza ningependa kuelewa kiongozi ktk famila ni nani.
  Pili: Biblia inasemaje kuhusu wana ndoa.
  Na Tatu: Mipaka ya mwanaume na mwanamke ni ipi? naomba majibu BWANA AWABARIKI

 2. Shalom

  Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa na pia mtu anayemwamini na aliyeokoka yampasa kuomba mchumba na kupokea kutoka kwa Mungu. Kumbuka sisi ni wanadamu na tunamambo mengi sana tumepitia katika maisha kila mmoja kwa jinsi yake. Unapompata mwenzi wa kufanana naye haimaanishi mtakuwa mmepitia mambo sawa au mna ufahamu unaofanana. Mazungumzo ni msingi wa ndoa na hayaishii kwenye uchumba tu, hadi mnapooana. Lazima kila kitu kijadiliwe na wanandoa wote wawili kuanzia malezi ya watoto, shule ya kupeleka watoto, kiasi cha kuahidi kanisani, ujenzi, nini cha kununua n.k

  Ni muhimu kufahamu kuwa unapomuoa mwanamke unamuoa mtu mwenye akili timamu na maranyingine anaweza kuwa na hekima na burasa kuliko wewe, mfano hai ni nabali na mkewe abigaili. Kumbuka mkioana si wawili tena, hivyo kila kitu lazima kifanyike kwa umoja maana mmekuwa mwili mmoja.

  Zaidi nitembelee katika blog ya women of christ.

  Mbarikiwe

 3. Asante mtumishi kwa kutupa hizi funguo za muhimu sana ,,,,Mungu akubariki naomba endelea mtumishi.

 4. Hiyo ni njema sana.Bwana akupake mafuta zaidi uwasaidie vijana wavuke salama ghambo ya pili.

 5. Kama kuna mtu anadhani kuwa mambo aliyosema dada Magie siyo ya muhimu, tehee.. dawa ni ndogo, wewe achana nayo kisha ingia kwenye ndoa. Maana yakiwa ya muhimu au ya kipuuzi mziki wake mwenye kuucheza ni wewe mwenyewe.

  Ni vizuri kusikiliza maneno ya wenye hekima, yaani kusikiliza maneno au ushauri wa wenye uzoefu.

  Pia mwanaume au mwanamke anayedhani kuwa mwanamke ni kama roboti kazi yake ni kutii tu anayosema mwanaume, na penyewe jibu ni rahisi; ingia kwenye ndoa au kama umo tayari, wewe mwamrishe tu, maana muziki wa matokeo ya kufanya hivyo utaucheza mwenyewe pia

  Nimetumia hiyo lugha hapo juu kwa sababu sioni sababu ya kubishana sana wakati matokeo mazuri au mabaya ya kufanya ambacho Magreth anatushauri ni wa mtu binafsi. Yeye kwa uzoefu alionao ameamua kutupa ushauri wa bure,Kuuchukua au kuukataa ni ridhaa ya kila mmoja wetu, lakini mimi naamini wengi wana matatizo kwenye ndoa kwa sababu waliyapuuza mambo kama haya.

  Kazi ya Mungu ni kukupa mke/mume. Lakini kazi ya jinsi ya kuendesha familia yenu si yake kukupangia, ila ni ya kwako. Hawezi kuja kukwambia fungueni a/c ya pamoja, pangeni hivi mipango yenu ya mbele. Atafanya tu hivyo kama kuna kusudi maalumu,na hiyo hutokea kwa uchache sana na kwa watu wachache pia.

  Yesu hakusema mwanamke atamwacha baba na mama yake nae atamfuata mume wake, bali mume ataacha baba na mama yake nae ataambatana na mke wake. Ukiangalia vema maneno haya utagundua kuwa suala la wapi kwenda kuishi ni makubaliano ya mume na mke, wala hakuna shuruti kuwa mwanamke lazima aende anakoishi mwanaume.
  Mimi nitajadiliana na mchumba wangu,wala sintampeleka kama roboti. Nimesema “mimi” na wewe fanya unavyoona ni vema kwako wala hulazimiki kufanya kama mimi.

  Isaka alimtoa Rebaka kwao akampeleka kwake (kwao- nyumbani kwa mzee Ibrahim), lakini Yakobo aliishi na wake zake Leah na Recho kwao( nyumbani kwa akina Leah). Kwa hiyo hakuna mfumo maalum,ispokuwa fanya kama utamaduni wa jamii yenu ulivyo. Wewe kama ni mhindi fanya kama mhindi, mwarabu fanya kama mwarabu, mswahili fanya kama mswahili,mnyakyusa fanya kama mnyakyusa n.k

  Fikiria kwa nini Mungu alituumba tukiwa na akili, halafu fikiria kama ni halali kuzitumia hizo akili au kama ni kosa. Kudhani kuwa kutumia akili zetu ni udhaifu kila kitu tunatakiwa kumsubiri Roho mt. atuambie ndo tufanye ni kutokuelewa kwa kiwango kikubwa maana ya kuongoza na Roho.

  Kumradhi kwa hiki ninachokwenda kusema: Kuwaza kuwa kila kitu lazima tuambiwe na Roho mt. ndio maana ya kuongozwa nae, basi hata mtindo wa kujamiana na mwenzi wako na wenyewe utasubiri akuongoze

  Nasema hivi: Anaeona ushauri wa Magreth haumfai, aachane nao si lazima!

 6. Shalom wapendwa
  ni mafundisho mazuri ila naomba kuongeza kuwa hivi vitu ambavyo unapomuomba Mungu akupe mtu ulipaswa kuwa navyo moyoni na vinatakiwa viwepo na sio vya kujadiliana
  Kwa nini kwa sababu hata kama wote ni wakristo kweli ila kihuduma kama ulivyotaja mwingine anaona yupo juu hasa mwanamke kuliko mwanaume sijui hata mkijadili akakubali inakuw ani utii tu lakini atashindwa kuendelea na kile alichokusudiwa na Mungu, kumbe yupo ambaye labda Mungu alimchagulia angeendana na huduma yake.
  Maswala kama kuficha mishahara, watoto, mali ni vitu vya kidhaifu vinavyoongozwa kimwili zaidi na sidhani kama umeokoka utafanya hivyo. Kama mmoja ana watoto, mali, au kazi anayoona kuwa inaweza kuwa tatizo kwa mwenza wake basi unapoomba Mungu akupe atakayeweza kuchukuliana nawe kwa hali ya kipato chako, familia utakayo, watoto wako na mengineyo. Hata mkijadiliana na mkashindwa kuafikiana iweje mnaachana na kisha uaanza majadiliano na mwengine?
  Ni vizuri kumshirikisha Roho mt na uwe na amani huyu kweli ndiye ubavu wangu hayo mengine mtayaweza tu ktk Yeye awatiaye nguvu, leo mfano una kazi, ni mzima, huna ndugu anayekutegemea ghafla unapooza, kazi unaachishwa, mali inaisha majadiliano yenu yakikaziwa itakuwaje???
  ndg Mabinza ukianza mwenyewe bila kumshirikisha Mungu utegemee matatizo ambayo mengine ni magumu na kukufanya ushindwe kufanya kusudi la Mungu au kwa viwango visivyokusudiwa.
  Sio kila ‘Mkristo’ anafaa kuwa mke au mume, kila mtu amepangiwa wake kwa kusudi maalum, tatizo tunakuwa tayari na vigezo vyetu vya mwilini tukijibiwa huyu ndiye tunakataa au hatuoni na tunarudi tena kuomba, au tunaanza kuomba tukiwa tayari na watu wetu tunawapeleka mbele za Mungu….sasa utakapoitwa utumike ndipo utauona moto mke au mume hatambui kabisa hili na anageuka adui namba moja wa huduma yako hata kusababisha kusambaratika familia na wewe ukibaki aidha kuacha kutumika au uikose familia. Ndoa bila chaguo la Mungu ndiyo chanzo cha kuudumaza mwili wa Kristo kwasababu kanisa linakuwa na nguvu likianzia ngazi ya familia kwa hiyo shetani anahakikisha anaharibu chanzo halafu anakaa aone kama kusudi ulilopewa litatimia!
  Mbarikiwe

 7. mpaka siku watu watakapokubali kuwa Yesu kristo ni bwana wao na mwokozi wao na kuacha kuzitegemea akili zao ndipo Mungu atakavyoingilia kati na kuongoza maisha yao na matatizo hayo yote ndio yatakapo kwisha. unaposema umekuwa mcha Mungu alafu eti hata sehemu ya kuabudu ni lazima muanze kujadiliana ni ishara tosha kuwa kati yenu ninyi wawili hakuna mwanamke bali kila mmoja ni mwanaume yaani anaweza kuamua lolote lile lifuatwe na mwingine. mi ninachojua kuoa ni jambo la furaha sana kiasi kwamba kila kitu unajisikia kumwambia mkeo hata kama hajakuuliza na kwa mke yeye kwanza furaha yake ni kukusimulia yote aliyofanya kwa siku hiyo hata kama hukuwa na muda wa kumsikiliza ila tu ilimradi wewe ujue leo kafanikiwa wapi na kashindwa wapi ili umsifie na kumshauri zaidi. huyo ndio mke kweli kweli hata mumewe humwamini. Mi ninachojua iwe kwa lugha kiingereza au kiswahili au kiyunani anayeposa ndio muoaji iwe ni mwanamke au ni mwanaume na ndio maana nikasema baadaye tutaanza kujadiliana hata nani amuoe mwenzake. Jambo la kulielewa kwa wadada ni kwamba kuolewa ni kukubali kuwa chini ya mwanaume mmoja tu maisha yako yote na kwamba japo yanaweza yakawepo mambo Usiyopenda kuyafanya lakini kwa ajili ya mume wako kwa moyo radhi kabisa utafanya na mume wako akishaona submission ya jinsi hiyo ndipo anaposema kweli nimepewa mke na Mungu na hivyo upendo wake hukua zaidi na kuanza kujishughulisha sana ili alinde hicho kitu chake chenye thamani. kuanza kujadiliana juu ya wapi kwa kuabudu na juu mapato kuwa tushirikishane au tusishirikishane ni matokeo ya mioyo ya ujeuri na kujiinua miongoni mwa wanandoa kwani upendo unapokuwepo utajikuta tu ukishirikisha mwenzako hata kama hajakuuliza juu ya hayo mapato yako. shida kubwa ni akina dada kujiinua sana juu ya waume zao. lakini pamoja na hayo yote bado yako mabaki ya akina Sara na Rebeka ambao waliita waume zao bwana kwa ukweli na sio kwa unafiki. Tatizo jingine ni mafundisho potofu yanayoendelea ya kuwafundisha mabinti kuwa wao sio watu wa kutii tu bali nao wanauamuzi wa lolote ndani ya nyumba zao hasa hizo movement za kudai haki sawa na upendeleo kwa wanawake , hii haina tofauti na wanawake wa korintho!! mi nafikiri wangefundishwa wanaume namna ya kuto nyanyasa wake zao badala ya kuwafundisha wanawake namna ya kuwa betray waume zao ambao wengi wao tayari wao wameshajua kuwa ni viongozi ndani ya nyumba zao. hii imepelekea wanawake wengi ambao wanaendesha hizo harakati za haki sawa waachike na waume zao na wamebaki kama maganjo tu na sasa wanatafuta waumini nao akina dada kabla hawajaolewa tayari sumu hii mbaya imesha waingia na ndio maana kunakuwa na mijadala kama huu wa kwetu eti muanze kujadili ni wapi tutaabudu huku ni kupungikiwa ufahamu mi sijaona msichana alipoolewa alafu akamwamisha mkaka kutoka kanisani kwake na kuamia kwa mdada ila dada ndio aliyeolewa na anaaga kwao rasmi yaani kanisani na kwenye familia yake kuwa yeye sasa sio wa huko tena bali ni wa kwa mumewe. BADO NINGALI NINA MENGI LAKINI KWA SASA NIISHIE HAPO KWANZA LAKINI NITARUDI TENA!!!!

 8. asante dada kwa ujumbe mzuri! ila mie nadhani mambo mengine ni nadharia zaid kuliko uhalisia, kwa mfano suala la kutokuwa na siri kwa mwenzako ni gumu sana….nafikiri!

 9. Asante sana dada Magie kwa ujumbe wako mzuri na wenye mafundisho kwetu. Mungu akubariki mpendwa!!


 10. Nikweli Magreth kasema mambo ya Msingi sana, hata mimi nayakubali yote, lakini sijajua bado, kuwa ukitimiza hayo aliyoyasema Magreth, ndiyo ndoa itapona? Hakuna suruhu ya jambo mpaka mzizi upatikane. Je, Migogoro ya Ndoa chanzo chake kikuu ni nini hasa?

  Maana si wachamungu, si wapagani na hata wale ambao hawakuoana kwa ndoa wote wamo katika taabu hii, Kwanini hasa? Wanawake wanasema chanzo ni akina Baba, na akina Baba nao wanasema chanzo ni akina Mama, ali mladi kusingiziana, kutupiana lawama na kubebeshana zigo hili baya!

  Mwenye kujua atupe chanzo watu tufurahie Ndoa jamani, Mwaka wa kwanza hadi wanandoa wanapopata kitoto cha kwanza (Kwa wasio na matatizo katika uzazi) huwa Furaha tupu, lakini baada ya hapo nisikilizie, wengine hudiliki hata kuomba Mungu makanisani wakitaka heri wabaki wajane, hawataki tena aina hiyo ya ndoa, wanataka waanze mahusiano na wengine upya, wanasema mimi, sikujua, nilikosea au nilidanganywa nk. Naomba jamani mawazo!

 11. Yeah, of course ni muhimu kujadiliana hayo mambo. Na suala la nani amuoe nani lenyewe linapatikana katika lugha baadhi tu, hususani za kibantu Kiswahli kikiwemo, ambapo mwanaume huoa na mwanamke huolewa.Na kuolewa kwa wanaume wa kibantu ni kama tusi.

  Na sijui sana mwanaume kusema ameoa ina maana gani nzuri ambayo mwanamke akisema ameoa atakuwa ameiharibu.

  Lakini nafikiri wengi wetu tunajua katika Kiingereza kuna neno moja tu “marry” ambalo hutumiwa na jinsia zote.

  Yaani Sungura(+me ) husema “I am married to Xyz(+ke), na Xyz husema I am married to Sungura.

  Lakini kwa Kiswahili Sungura husema “Nimemuoa Xyz, na Xyz husema nimeolewa na Sungura.

  Dada Magreth kasema mambo ya msingi sana.

  Abarikiwe.

 12. kama hata mahali pa kuabudu na penyewe tunaanza kujadiliana hii ni hatari baadaye tutaanza kujadiliana hata nani amuoe mwenzake.

 13. Hivi, ni jukumu la nani kuchagua Mwenza wa ndoa, Mungu au mhusika mwenyewe? maana husemwa “Mke mwema atoka kwa Bwana” Neno hilo linamaana gani? Nina hofu kuwa huenda migogoro katika ndoa hutokana na kutojua maana ya Neno hilo la Mungu!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s