Salaam za maaskofu wa KKKT kwa watanzania wote kuhusiana kuchomwa kwa makanisa ya kikristo Mbagala

Wapendwa Katika Bwana,
Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla.

Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.

Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika eneo hili la Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimissioni vya Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili kufika hapa Mbagala. Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu:

 1. Tumekuja kuwapa pole na kusimama pamoja nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu ni machozi yetu. Machozi yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33).
 2. Tumekuja kuonyesha majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani, kuporomoka kwa umoja na mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa, na wenye msiba ni watanzania wote, wenye dini na wasio na dini.
 3. Tumekuja kushiriki pamoja nanyi kupokea matumaini ya Tanzania mpya. Katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa. Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo na dini.

Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa kufanya haya yafuatayo:

 1. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na ruhusa kutoka mamlaka zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
 2. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu ya dini; wawe wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi wao binafsi ili kupata kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini.
 3. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali za makanisa kwa kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo tunamwachia Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.

Wapendwa wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa Tanzania ya Julius Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni kebehi kwetu sisi wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala baada ya kazi njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania aliyoijenga.

Kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari, yaani mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa matunda machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa. Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:

 • Uchochezi wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili.
 • Ubishi usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa nchini na hata kudiriki kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania. Lengo la ubishi huu ni mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya kimbari na mateso ya kanisa.
 • Matumizi mabaya ya baadhi vyombo vya habari, vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini miongoni mwa watanzania
 • Ukimya wa vyombo vya dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya matumizi ya vyombo vya habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari, mateso kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache dhidi ya wengi.
 • Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama:

 1. Kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala katika mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi?
 2. Madai yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa nchini. Madai haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa nchini.
 3. Madai na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini
 4. Mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria.
 5. Mashinikizo ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma,
 6. Kuhoji na kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini

Wapendwa wana KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama wanaofanya mambo haya ya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana harakati”, tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na watanzania walio wengi, tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao usitumike kuvunja nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.

Kwa macho na masikio yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na waoga, hufika wakati wakasema “sasa basi” pale wanapodhalilishwa kupita kiasi. Hatuombei wakristo wafikishwe hapo.

Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa sababu ya zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu?

Sisi tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana waumini wa dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii na wasiolazimika kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake. Kamwe hawezi kuliacha liangamie.

Kwa Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine.

Katika mateso haya, kanisa litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo wote kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya kuomba na kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa, imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16).

Daima tukumbuke kuwa, “KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO” (Waefeso 6: 12).

Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu,

 1. Askofu Dr. Alex G. Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani
 2. Askofu Dr. Stephen Munga –Mkuu, D/Kaskazini Mashariki
 3. Askofu Dr. Martin Shao – Mkuu, D/Kaskazini
 4. Askofu Dr. Thomas Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati
 5. Askofu Dr. Benson Bagonza- Mkuu, D/Karagwe
 6. Askofu Isaya J. Mengele – Mkuu, D/Kusini
 7. Askofu Levis Sanga – Mkuu- D/Kusini Kati
 8. Askofu Elisa Buberwa – Mkuu –D/Kaskazini Magharibi
 9. Askofu Andrew Gulle – Mkuu, D/Mashariki ya Ziwa Victoria
 10. Askofu Michael Adam –Mkuu, D/Mkoani Mara
 11. Askofu Renard Mtenji – Mkuu, D/Ulanga-Kilombero
 12. Askofu Dr. Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde
 13. Askofu Job Mbwilo – Mkuu, D/Kusini Magharibi
 14. Askofu Dr. Owdenburg Mdegella- Mkuu, D/Iringa
 15. Askofu Jacob Ole Mameo- Mkuu, D/Morogoro
 16. Askofu Zebedayo Daudi – Mkuu, D/Mbulu
 17. Askofu Paulo Akyoo – Mkuu, D/Meru
 18. Askofu Charles Mjema – Mkuu, D/Pare
 19. Askofu Mteule Amon Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma
 20. Askofu Mteule Dr. Alex Mkumbo- Mkuu, D/Kati

Mbagala, Dar es Salaam,
Oktoba 18, 2012

Source: http://www.wavuti.com/4/post/2012/10/salam-za-maaskofu-wa-kkkt-kuhusiana-na-uchomwaji-moto-makanisa.html#ixzz29efShGsl

Advertisements

13 thoughts on “Salaam za maaskofu wa KKKT kwa watanzania wote kuhusiana kuchomwa kwa makanisa ya kikristo Mbagala

 1. INAPOFIKIA KIONGOZI WA CHAMA TENA MAARUFU MSONI ANASHUTUMU SERIKALI KWAMBA IMEWAONEA WANAOJIITA VIONGOZI WA DINI HIVYO WAPATIWE DHAMAMA MARA MOJA NA KUWE NA MJADALA WA KITAIFA KUHUSU AMANI NA USALAMA WA TANZANIA HAPA TUNAKUWA NA WASIWASI IWAPO WACHOMAJI WA MAKANISA WAMETUMWA NA WANATUMIA MWAVULI WA DINI KUFANYA SIASA.KAMA WABUNGE WATASHINDWA KUZUNGUMZIA HOJA HII KWENYE KIKAO CHA SASA WABUNGE WACHUNGAJI WALIOKO BUNGENI WATAMTANGAZIA MUNGU KUWA UPAKO UMEWAKIMBIA HIVYO WAACHE KAZI HIYO TUSIPOKUWA WAANGALIFU YALE YANAYOTOKEA NIGERIA BOKO HARAM KWETU ITAKUJA SIJUI NINI IKUMBUKWE HATA NIGERIA WANASALI BADO MAKANISA YANACHOMWA INAPOFIKIA IMANI YA DINI FULANI UKIUA KAFIR UNAPOKELEWA AHERA KWA VIGELEGELE BASI TUTATOLEWA KAFARA WENGI NDIO SABABU KUNA KIGUGUMIZI KATIKA KUSHUGHULIKIA MAUAJI NA UHARIBIFU WA MALI ZA MAKAFIR SI RAHISI KUZALIWA NYERERE MWINGINE

 2. INAUMA SANA WAMA MBG TUMEUMIA LAKINI KISASI SI JUU YETU,TUTAENDELEA KUWAPANGISHA KTK NYUMBA ZETU ,KUWAVISHA NA KUWALISHA BWANA ATATENDA.

 3. Mungu awabariki sana Maaskofu wetu kwa wito huo mlioutoa.Ni imani yangu kuwa wahusika wote yaani ,Serikali,Viongozi wa dini zote ,Wanasiasa na Watanzania kwa ujumla watayazingatia yote yaliyo semwa na Maaskofu wetu.Pia tujifunze kutoka kwa maaskofu wetu has ROHO YA UMOJA.MUNGU ATUBARIKI .

 4. MANENO YA WATUMISHI WA MUNGU,YANAONYESHA KWA WAZI KUWA,UTULIVU NI TUNU NA MUNGU HATAIACHA TANZANIA IAIBISHWE NA WATU WACHACHE WASIO PENDA AMANI.MUNGU AWABARIKI WATUMISHI,

 5. Duniani hapa tunaongozwa na katika kutenda HAKI. HAKI ndiyo inampa binadamu AMANI ya kweli. MUNGU aliye juu, atujalie katika kutenda haki ya kweli ili AMANI tuliyojengewa na Waasisi wa Taifa hili la Tanzania isipungue hata chembe,bali izidi kuongezeka. AMENI

 6. Mungu wetu ni Mwema sana,hakika Mungu hataliacha taifa la watu wake waangamie.Mungu ibariki Tanzania

 7. Tunaamini kuwa Mungu atatupigania, maana anasema katika neno lake kuwa macho yake huzunguka zunguka duniani kuangalia wamchao ili ajionyeshe kuwa ni mwenye nguvu

 8. Mungu wetu na atukuzwe. Kufika kwa Baba zetu Maaskofu wote wa KKKT huko Mbagala kunaonyesha jinsi Dayosisi zetu zilivyo viungo katika mwili mmoja yaani KRISTO. Niseme pia ya kwamba maneno na matamko yaliyotamkwa na Mababa hawa ni mafundisho tosha yenye msingi imara; si kwetu Wakristo tu bali kwa watu wote hata wenzetu waliofanya matendo haya ya uvunjaji na uchomaji wa makanisa.
  Nawapongeza Mababa hawa kwa hekima hii yenye chimbuko la Umoja ili kuonya na kukemea mabaya na kuwa wazi katika kuyaweka maswali muhimu peupe. Nina hakika hatua ya juu kuliko hata kumwona Rais, Mababa wamekwisha ifanya, maana “wamezungumza na kuyaweka haya kwa MUNGU wetu. Nampongeza na kuheshimu pia Rais wetu kwa kutembelea Mbagala na kujionea yeye mwenyewe hasara kubwa zilizotokea kwenye makanisa yetu. Aliahidi ya kwamba vyombo vya sheria vitahakikisha haki inatendwa katika hili.
  Maaskofu wetu wametuomba sote wakasema hivi “Kwa Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi
  ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine.”
  Maneno haya ni mazito basi sote na tushikamane katika yote.
  MUNGU IBARIKI TANZANIA na WATU WAKE
  Amina

 9. Asanteni maasikofu wa Tanzania kwa kwa Faraja.

  Ila Najiuliza wanaharakati wa haki za Binadamu, Baadhi ya vyama vya Kisiasa, Wana habari, Vyombo vya habari na Wapenda maandamano ya Kisiasa Mbona katika hili la kuonewa kwa Wakristo hatuwaoni au kuwasikia? Tuseme tatizo lenu ni kati ya Serikali inapopishana na Chadema tu ndipo mnapoona kukiukwa kwa Sheria na haki za msingi za kibinadamu? au mpo Kisiasa zaidi?!

  Tunataka matamko yenu Kulaani vitendo vya vikundi vya uvunjaji amani. Vinginevyo nashindwa kuwaelewa kama mpo kwa ajiri ya kusimamia Haki, Sheria na Amani!

  Elewekeni tujue moja!

 10. Amen maaskofu na ni kweli vita yetu si juu ya damu na nyama.. Tuendelee kuomba Mungu as Visasi si juu yetu ni vya Mungu mwenyewe. Wakisto siku zote tumekuwa wavumilivu sana kwani ni mara ngapi imekuwa ikifanywa mihadhara ya kutukashfi lakini hatujawahi ht siku moja kuchoma misikiti. Hicho kitu wanachokitaka juu ya nchi hii kimeshindwa na kitaendelea kushindwa kwa jina la YESU na ndio maana kwa hasira wanachoma makanisa. Lets just keep on praying

 11. Nashukuru sana maaskofu wetu kutoa matamko yenye wito mzito na wajibu mkubwa kwa wananchi na viongozi wetu. Pia niwashukuru wananchi wote wa Tz wenye mapenzi mema na nchi yetu. Ikumbukwe kuwa ukiwa katika nyumba ukachoma chumba kimoja usifikiri uko salama kwa sababu tu eti uko chumba kingine!!. Naomba sana sana maaskofu wetu muungane na mkamuone raisi, waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani. Nafikiri kama tutatoa matamko tu na maombi, haisaidii kwani tangu 2001 mmemkua mkifanya hivyo bila mafanikio yoyote. Nafikiri ni vyema mkachukua hatua ya juu zaidi kuliko kuendelea na hizo approaches 2 (maombi na kutoa matamko). Hii itaifanya serikali yetu isilale na kuwaogopa watu au jamii fulani huku jamii nyingine ikidhulumiwa kila kukicha nje nje. Pia ndg zangu kutokuwepo kwa muungano kati ya watoto wa mama ndio unafanya somehow tuonewe. Katika masuala kama haya ni vema tuungane watoto wote na kushughulikia jambo hili kwa umakini ninauhakika huku tukifanya mengine kama Kristo alivyoagiza tutumie pia akili zatu ili ktka nyumba nzima kisiungue hata chumba kimoja. hatima yake taifa letu litapona na hakuna atakayeonewa na kudhulumiwa.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s