Uumbaji Umerejea “Hapo Mwanzo…”

Kwa Nini Kuwa Na Uumbaji Mpya?
Mw 1&2

Kwa majira na viwango vya Uungu tulivyofikia sasa hivi vya kuamuru vitu kwa kinywa chetu tu na vikatokea kwa uhalisia, nakiri kwa uhakika Mungu Amerejea. Majira ya Mwanzo ambapo Mungu aliongea na watu wake ana kwa ana na akasema angeshuka Yeye Mwenyewe (Lk 20: 16) kulitwaa tena shamba lake la mizabibu akawapa wengine (wanawe) wanaolistahili, ni sasa. Makusudi ya Mungu tangu mwanzo (majira na nyakati) kama yalivyoandikwa katika Mw 1&2, yalichafuliwa na ibilisi na kuibiwa na dunia pamoja na ulimwengu baada ya maanguko. Makusudi ya Mungu ilikuwa ni kila alichokiumba kiwe ni jema. Mwanzo, Mungu aliumba Nuru kwa kutamka. Kitabu cha Injili cha Yoh 1: 1-5 kinasema “1Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu…”–inaendelea kusema, “4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu…” Maana yake ni kwamba ‘Kutamka’ au Neno alikuwa ni Nguvu ya Mungu. Neno alikuwa ni Yesu. Ukioanisha haya maandiko unapata kufahamu kwamba kwa kuwa Yesu ndiye Neno, Yesu alikuwa na Mungu pamoja wote wakiumba mbingu na dunia na vyote vilivyomo. Siyo jambo la ajabu hilo? Jaribu kuvuta picha, Yesu akiwa sambamba na Mungu Baba wakitamka “Hiki kiwepo, kile kiwepo…” na inakuwa! Uuumbaji wa ajabu sana uliokamilika na ambao hauwezi kurudiwa na yeyote wala kulinganishwa na mfano mwingine wowote! Tu kwa sababu hakuna mfano mwingine. Na tizama kwa makini, kila siku katika siku zote saba za uumbaji una mtiririko na mpangilio maalum wa kuumbwa kila kitu Mungu alichokiumba kwa siku yake na kusudi likiwa ni kuumbwa hicho kitu kwa siku hiyo hiyo na siyo siku nyingine yoyote aidha kabla au baada ya siku yake. Ni rahisi kung’amua kwa kutumia mfano wa Mtume Eliya, “hauwezi kuleta mabati na fenicha (ukavipanga ndani) kwenye eneo la ujenzi unapojenga nyumba na kuanza kuezeka paa kabla haujachimba msingi na kujenga ukuta ili nyumba lisimame; kuna hatua”. Naam, mara zote kuna hatua na mpangilio. Mara zote.

Kupitia Nuru, Mungu alifuta ukiwa, utupu na kiza siku ya kwanza ya uumbaji. Akaendelea kufanya uumbaji wa siku sita, akamaliza siku ya saba. Kusudi lake la kuona kila kitu alichokiumba kuwa jema likatimia.

Lakini hebu subiri; siyo kila kitu kiliendelea kuwa jema kama kilivyoonekana. Kumbuka tunaambiwa kwenye kitabu cha Eze 28: 13-19 na Uf 12: 7-9 kwamba majira za zama Lucifer alipotaka kuwekwa mahali pa juu ili atukuke awe kama Mungu, vita vikuu viliibuka mbinguni ambapo marehemu* shetani akiwa na malaika waasi waliomuunga mkono walishindwa vita vibaya sana na Michael mkuu wa malaika wa vita, akatupwa chini huku duniani. Haya yote yalitokea kabla ya uumbaji wa dunia. Kivipi?

Tunaona Mwa 1: 1-2 “1Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya vilindi vya uso wa maji…” (…ibilisi alikuwepo tayari wakati Mungu anaumba); “Roho wa Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” (Roho Mtakatifu naye alikuwepo hata kabla ya Pentekoste na ikawa anaweza kutambua kwamba haambatani na giza wala ukiwa bali tu anapaswa kutulia juu ya uso wa maji ambaye ni Neno/Yesu).

Sasa hebu fikiria hiyo aibu ya kushindwa vita marehemu shetani, kupondwapondwa tikitiki hadi kutupwa kutoka katika himaya yake au nyumba yake hadi uhamishoni kwenye mazingira ambayo hakuizoea. Marehemu shetani ikawa anategea kusubiri mda wake alipize kwa uovu. Alivyoona tu Mungu amekamilisha uumbaji usiokuwa na waa wala mfano wa chochote kingine kile, akaanza kupanga mikakati yake michafu!

Mlango alipouwacha wazi Adamu kidogo, marehemu shetani hakupoteza mda, alitumia mwanya huo uliojitokeza akaupata mlango na kumuingia Adam na Hawa, ikawa ndio basi tena! Kila kitu kikachafuliwa. Kukatokea maanguko makubwa, Adam na Hawa ikawa hawaweziruhusiwa na Mungu kuona tena kwa macho ya Uungu waliopewa tangu mwanzo kwa sababu walihiari kuchangamana na adui, ikabidi Mungu auzime Nuru, awanyang’anye thamani (yaani Uungu), akarudisha kiza. Shetani naye akawa amepata utatu wake alioukusudia; yaani kiza, utupu na ukiwa! Mara kadha utamsikia mtu akitamka “maisha yangu ni jehanamu duniani…” hayo majira ya anguko ndiyo majira ambayo ‘maisha kuwa jehanamu duniani’ yalipomwingia binadamu; binadamu alipohiari kumsikiliza na kuwa na mahusiano na marehemu shetani. Na hali hii hujirudiarudia pale mtu anapohiari na kuchagua kufanya kile ambacho anakijua dhahiri kuwa ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Lakini hebu tusitoke nje ya mada yetu. Swali tunalojaribu kujibu ni “kwa nini Uumbaji Mpya?” …na kwa nini Sasa?
Ili kuweza kupata majibu mwafaka ya hayo maswali, hebu tutizame kwanza ni nini hasa kilichoharibiwa na kuibiwa na marehemu shetani kwenye kila mojawapo za siku sita ambazo ndizo siku zote za maisha yetu sisi kushirikishwa kuumba na ambazo ndizo Mungu alifanya uumbaji, na katika siku ya saba Mungu alipomaliza kazi ya kuumba mbingu na nchi na jeshi lake lote, akapumzika, na ambayo ni siku yetu pia ya kupumzika na kustareheshwa maisha yetu yote.

Siku ya I
Mw 1: 1-5
Hii ilikuwa ni siku ya KUONA.
Tunajifunza pale Mungu aliposimama na kusema “Iwe Nuru” (Mw 1: 3), alitaka kiza, utupu na ukiwa uliokuwepo utoweke. Mw 1: 2(a) anasema “2nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na kiza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji…” vuta taswira ya utupu unaotisha, nchi isiyo na chochote kitambaacho wala kiotacho; hakuna maisha wala chochote kipumuacho; mawimbi makubwa yakitupwa-tupwa huku na kule na kibaya zaidi, juu ya yote kuna lindi kuu la kiza kinene ile haujawahi kuona! Halafu “…Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji…” (Mw 1: 2[b]) Aha, sasa tunajifunza kitu hapa, Mungu alikuwa na upendo. Na Roho Mtakatifu naye alikuwepo wakati wa uumbaji… Alikuwepo Mungu Baba, Mwana (maji, ambayo kwayo juu yake R.M ikatulia), na Roho Mtakatifu, wote wakifanya kazi pamoja, kwa kushirikiana (kumbe ili kufanikisha kila jambo kuna umuhimu wa kufuata kanuni ya Mungu ya uumbaji ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wana wa Mungu wengine eeh? Siyo kuwa mbinafsi na kujitakia sifa za peke yako).

Mungu akasema ‘Iwe Nuru’, kama tulivyokwishaona kwenye Mw 1: 3. Alitaka Nuru iwepo na idumu katika majira yote hadi mwisho wa dahari. Lakini sasa hivi angalia mazingira yaliyowazunguka watu. Isipokuwa kwa wana wa Mungu tu, hakuna nuru tena baada ya maanguko; baada ya adui shetani kuiba nuru kwa binadamu na uumbaji wote.
Yakupasa uelewe ni kwa nini ilibidi Yesu afe na afufuke tena; uelewe kuhusu Vizazi vyote Vinne (na maana halisi ya Vizazi Vinne kama vile Mungu alivyomaanisha na sio vile imekuwa ikichukuliwa na watu kwa uelewa wa kibinadamu) na nafasi ya kila kizazi katika uumbaji na ndani ya majira na nyakati zote; ni namna gani haya matukio yote yameunganishwa na hatua ya Mungu kulijaza dunia na Nuru yake kwa mara nyingine tena.

Tutafahamu pia namna wana wa Mungu wana uwezo wa kuamrisha uumbaji ndani ya majira na nyakati na uumbaji ukatii. Kwa sababu baada ya ufufuo, sisi wana wa Mungu tunajidai kwa Mungu wetu kwa kuwa ameturejeshea tena Nuru na kushirikishwa umbaji kwenye kizazi chetu, kizazi cha IV.
NURU (Mwa 1: 1-4) inakupa NAFSI HAI (Mwa 2: 7)

Siku ya II:
Mwa 1: 6-8.
Siku ya pili, “6Mungu akasema, na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji… 8…Mungu akaliita lile anga mbingu…”

Hii ilikuwa ni siku ya KUONA FURSA.
Fursa ya kuenda juu na kushika Neno kwani maji ni Neno la Mungu. Tunamwona Yesu pale kwenye kisima cha Yakobo mjini Sikari anamwambia mwanamke wa Kisamaria kwamba “14walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele” – Yn 4: 14.

Kwa hiyo kilichoibiwa na adui hapa na ambacho Yesu alikusudia kukirejesha kilikuwa ni kuona fursa za vitakavyokuhakikishia kwamba hakuna vizuizi kwenye kila kazi utakayofanya na yale utakayoumba. Kwa kuwa binadamu alikuwa kipofu baada ya Nuru ya siku ya kwanza kuibiwa, hakuweza tena kuona nafasi zinazojitokeza na kuweza kumuinua kwa kwenda juu na kwa upana usio na kikomo huku kazi hizo zake zikimtukuza, kumuenzi na kumuinua Mungu kwa shukrani na utukufu katika kila ujuzi, karama na sanaa.
Hapa ndipo ilipo hatma yako.
KUONA (Ef 1: 18) inakupa BUSTANI YA EDENI (Mwa 2: 15)

Siku ya III:
Mw 1: 9-13
Hii ilikuwa ni siku ya KUPANDA MBEGU na KUVUNA FAIDA.

Mungu alitenga maji ya bahari na ya nchi kavu, akaumba miche na mimea aina yote, miti ya matunda kwa kusudi lake. Na ndani yake akaweka mbegu ili miti hiyo izae zaidi.
Kusudi la Mungu, -kusudi ambalo lilikuja likaibiwa na adui ilikuwa ni kwamba mbegu hii iweze kuzaa zaidi na zaidi, kwa uzao na kwa faida. Maana yake ni kwamba kila ambacho ungepanda wewe, kiwe ni kwenye biashara, elimu, mifugo, wanyama wa kufuga na wa mwituni, mbegu za nafaka, misitu, viwanda, kilimo, uvuvi, uongozi; yote yaweze kuzaa kwa faida kubwa. Lakini hiyo haikuja kutokea hivyo.

Baada ya adui kuiba Nuru ya macho ya Rohoni, kila ambacho binadamu aliona ilikuwa ni viunzi na vizuizi kila sehemu na wala sio fursa! Utajiri, faida, mitaji ya kukua na kuvuna sana ulimezwa na upofu. ‘Kila ambacho watu sasa wakawa wanaona kotekote kwa herufi zote 21 ikawa ni -OPPORTUNITIES ARE NO WHERE’. Adui akaingiza masharti yake kwamba ukitaka kupata hayo yote mambo mazuri hapo juu ambayo Mungu alikusudia tokea mwanzo yawe ya kwako kumiliki na kutawala wewe uliyeokoka (Mw 1: 26 –kumbuka aliyepewa kumiliki na kutawala ni Nafsi Hai, sio mtu), ni lazima utambike, uuwe, uloge, uende kwa wanajimu, utabiriwe kwa karata na kusomwa viganja, uchanjwe chale, utembee juu ya kaa la moto, uzini na ndugu yako, uabudu wanyama, ujiunge na makundi ya ajabu kama ‘scientology’ au ya waabudu shetani, ‘free-masons’ na kadhalika. Lakini tunamshukuru Mungu kuwa kila kitu kimerejea kama Mwanzo ndani ya kibanda cha IV na Mungu wetu yuko juu ya wote na miungu yao katika Jina la Yesu!
BUSARA/FAIDA/THAMANI (Mit 3) inakupa CHAKULA (Yn 6)

Siku ya IV:
Mw 1: 14-19
Hii ilikuwa ni siku ya UTAMBUZI wa majira ya utendaji.

Kuweza kutofautisha majira na nyakati, Mungu aliumba mianga mikuu miwili, yaani jua na mwezi; “14…Na iwe mianga katika anga la mbingu na itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;…”
Na Mungu alikuwa hasemi “…ikawa saa sita na dakika moja usiku au ikawa saa tano na dakika hamsini na tisa na sekunde hamsini na tisa usiku, siku moja”. A-ah! Anasema kila akimaliza kuumba majira yale aliyotumia, “…ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya…” Oh, sasa unaelewa eeh? Sasa haya majira yanayofanana na majira ya kufanya mambo machafu ya kuanza kuhesabu mwanzo wa siku usiku wa manane yalianzia wapi? Huwa wajiuliza na kutafakari hayo?

Ili kuweza kupanga shughuli zetu zinazomtukuza Mungu, tungehitaji kufanya hizi kazi kwa kuishi katika mwanga, au nuru! Unapokaa katika Nuru, wewe ndio sasa unakuwa ‘Nuru Mwenyewe!’ -unakuwa ni taa kwa ulimwengu. Na ili kupata baraka na kuongozana na baraka ya siku hiyo, anza siku yako kwa kukaa katika malango ya majira mazuri ya kuanza siku vizuri, yaani kaa katika mwanga/Nuru. Bila nuru, tunaweza kufanya chochote kikafanyika tukafanikiwa? Jibu ni kwamba hatuwezi.

Lakini kuna zaidi. Nuru hii ingekusaidi kuelewa mzunguko mzima wa majira unamoishi na kuendeleza kazi zako kwa kuwajibika na kutekeleza kusudi la Mungu kwako ndani ya maisha yako kwa kipindi ambacho umepewa. Kwa kutumia nuru hii ungeweza kutambua dalili za maumbile au uumbaji na kuweka kumbukumbu za siku na miaka, na kupanga hizo shunguli zako zioane sambamba na vipindi na majira fulani ya uumbaji ili huo mtiririko-sare uweze kuleta uumbaji uliokamilika wa kazi zako, uweze kumpendeza Mungu sawasawa na kusudi lake yeye mwenyewe kwamba kila alichokiumba kimpendeze! Uumbaji si wa ajabu bwana!

Lakini ni nini kilitokea mbele ya safari? Kwa sababu kwa kadiri unavyofahamu, kila ‘ulichokiumba’ ukiwa mtu au kuona kikiumbwa kwa ajili ya kazi zako aidha haikufanikiwa au ilikuwa ni kazi ya manyasi (I Kor 3: 10-15) ambayo ikipitishwa kwenye gombo la chuo la moto iliteketea kabisa. Maana yake ni kuwa adui alichokiiba ni wewe kutoweza kuona na kutambua uwiiano huu wa majira na matukio. Kwa mfano, unaweza kukuta mtu ikifika mda fulani umepanga kitu au safari ambayo matokeo yake yangekuwa ya faida kwako, basi kutatokea kisirani au ya ugonjwa au hali ya namna yoyote ya kupelekea kukwamishwa kwa zoezi hilo zima lisitokee au lisitimie. Mikakati miovu ya adui ndivyo ilivyofanya kazi. Inakubidi mwana wa Mungu ujikinge, na kila ajitokezapo umlenge na umpige adui umuangamize kabisa kwa jina la Yesu!

Mfano mzuri wa namna adui na maajenti wake waliweza kupindisha majira na kusudi la uumbaji wa siku ya IV, siku ya majira na nyakati (Zab 19: 1-6) ni namna Wamisri, Wagiriki, Wayunani na makabila mengi ya mataifa ya mbali walitenga siku ya Mungu ili kuiabudu jua, mwezi, nyota, milima; na kila siku na majira ikawa na mungu wake!

Rum 12: 1-2 inaashiria kwamba ili kutompa adui nafasi ya kujibadili sura akajipenyeza miongoni mwa wana wa Mungu, Mungu anataka wana wake wafuatishe njia zake tu na sio njia za dunia, na Mungu hakutaka kila mtu ajue siri ya Majira na Nyakati ila kwa wachache wateule ambao ni wana wa Mungu waliokamilika ili waweze kutambua vya uungu, wamiliki na waitawale uumbaji wote –ili adui asiweze kuiba hiyo siri sawa-sawa na –I Kor 2: 6-10.
Kilichokuwa kimeibiwa ni siku ya IV:
Majira na Nyakati za Kanisa
Unabii wa Kanisa
Kutembea na wingu la Mungu

MAJIRA NA NYAKATI (Mwa 1: 14; Mh 3) inakupa MADHABAHU YA KWELI (Rum 8: 4)

Siku ya V:
Mw 1: 20-23
Siku ya kuumba VIKUBWA, VIPANA na VINGI
“20Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. 21Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao…”
Hii ilikuwa ni siku ya vikubwa. Mungu aliamua kujiachia! Aliumba vitu vikubwa, vitu vipana, uumbaji ambao hauwezienea ndani ya mizani yoyote ya kibinadamu; papa na popo -viumbe vya kutisha ajabu; vingine vyenye uzuri usio kifani, -mtizame kipepeo, kisha mkabili nyangumi; mgeukie samaki-milia, halafu mshangae tai– haiba yenye upekee kwa kila kiumbe! Kwa uweza wake mkuu ambao haujawa na mfano na hautakuwa na mfano kamwe, Mungu aliumba hivyo vyote siku ya tano.

Lakini adui kama kawaida yake alitaka kuhakikisha anaiba utukufu kwa Mungu, akaingiza uwongo na kuiba kwetu akili ya Kiungu ya kuweza kuumba vikubwa, vidumuvyo, kwa wingi, na akaiba pia nafsi ya kushirikishwa kwenye uumbaji, ya kuona fursa, kutambua majira na kumtukuza Mungu kwa kuumba vingi na vikubwa katika majira yale ambayo tunapaswa kuumba hayo yaliyokusudiwa na Mungu na yawe ndiyo yenyewe sahihi. – Mw 2: 19.
KUZAA NA KUONGEZEKA (Mwa 1: 22) inakupa NAFASI YA NENO (Yos 1: 8)

Siku ya VI:
Mw 1: 24-31

Mtu aliumbwa. Siku ya KUTAWALA NA KUMILIKI, UPEKEE.
Siku hii, Mungu alisema “nchi izae kiumbe hai kwa jinsi yake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.” Mw 1: 26 –“26Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu: wakawatawale…” kusudi la Mungu kumuumba binadamu kwa sura yake, yaani tabia zake na sifa zake ilikuwa ni tuwatawale viumbe vingine vyote alivyoviumba kwa namna ambayo italitukuza Jina lake yeye Mungu.“27Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”. Mw 2: 7 “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai”. Kwa hiyo mtu ambaye ni mavumbi aliumbwa kwa mfano wa Mungu kwa kupuliziwa pumzi ambalo ni nafsi ya Mungu. Nafsi Hai ndilo lilimuwezesha Adam kumiliki na kutawala kila kilichowekwa chini ya himaya yake kwa sababu alikuwa punde kidogo awe Mungu -Zab 8: 5. Nafsi Hai ndilo linaniwezesha na kukuwezesha wewe kuamrisha, kutiisha, kumiliki na kutawala uumbaji wote. Mungu anachokuambia hapa ni kwamba alikuumba kwa sifa hizo hizo alizo nazo yeye. Kabla ya anguko kuu, ulikuwa na kila alivyonavyo Mungu, ingawa punde kidogo. Tunamwona Mfalme Daudi akitafakari; (Zab 8: 4-6 “4Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? 5Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima;6Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake…” -mtu mwenye nafsi hai ulikuwa na uwezo Wake mkuu, uwepo Wake mkuu, na hekima Yake kuu; haukuwa na doa. Hadi pale Adamu alipoacha mlango wazi.

Unajifunza nini kutokana na ukiwa huu? Ni kwamba kilichoibiwa ni uwezo wako wa kumiliki na kuitawala uumbaji wote. Kitabu Mungu alichokishika wakati Adamu anaibiwa mkoba na marehemu shetani kilikuwa na mihuri saba – Uf 5: 1. Ni kitabu ambacho kinawezesha kukaa kwenye kiti cha enzi ili kumiliki na kutawala uumbaji wote na ambao funguo zake angeweza kupewa na ukafunguliwa tu na yule ambaye anazo Roho saba za Mungu zilizotumwa katika nchi yote na ulimwengu pia. Ni Yesu Kristo pekee, simba na Mfalme Mkuu kutoka katika kabila la Yuda ndiye anazo roho zote saba za Mungu -funguo za malango ya Kitabu – Uf 5: 12. Je hapo sasa nafasi yako inakuwa wapi, wewe uliye mrithi wa Ufalme? Lile pumzi la Mungu alilokupulizia kwenye uumbaji ambayo ndiyo ina sifa zote za uungu na macho Saba ya Rohoni ya kuweza kuona kama Mungu, ilitoweka baada ya anguko. Alichoibiwa Adamu kikafa ni nafsi hai na ndio maana hauoni akiwa amekufa mwilini pale pale, bali alifungua malango ya kufa kwa vitu vyote ambavyo yeye na wewe mngeumba, na akapitia ‘jehanamu duniani’ kama mwengine yeyote yule aliyefuatia. Hakuwa tena wa kipekee. Haungetamani kuwa yeye.
Kwa kifupi utendaji wa Adamu ulikuwa wa kilegevu. Mungu mwenyewe anajua vizuri sana kwamba ulegevu ndio unaleta tofauti kati ya mtumishi bora na huduma iliyokufa. Na ndio maana unaona hakuna chochote Mungu alichokiumba kimekaa kilegevu-legevu. Yeye ndiye anayeweka viwango vya utimilifu. Hatarajii pungufu ya hivyo viwango kutoka kwako. Mungu alisikitika sana na utendaji wa binadamu na ndio maana siku hizi (Kum 8: 2-3) Mungu hakupi huduma hivi-hivi ya kumtumikia, lazima ampitishe mtumishi aliyemchagua kwenye ‘gombo la chuo’ ngangari la moto na kaa ya mawe.
UUMBAJI (Mwa 1 & 2) inakupa UPENDO WA AGAPE (Yn 3: 16)

Siku ya VII
Mw 2: 1-3
Hii ndiyo siku Mungu alipopumzika. Siku ya KUSTAREHESHWA.

Mungu alimaliza kazi ya wiki nzima ya uumbaji, akatizama kushoto na kulia, kaskazini na kusini, akafurahi sana kwa kuona kila kitu alichokiumba kilikuwa ni jema. Alistahili kupumzika. Akae tu, kutulia na kufurahia kazi zake.
Rum 14: 17 yasema ufalme wa Mungu ni haki, imani na furaha katika Roho Mtakatifu. Kwa hivyo ikiwa umetekeleza na kufanya yale yote ambayo Mungu amekuagiza ufanye kwa kazi ya mikono yako ili kumtukuza, kumsifu na kumuinua mahali pa juu zaidi, ni kwa nini basi moyo wako uiname kwa mateso unapohitimisha uumbaji wa kazi za mikono yako mwisho wa siku za kuumba, uhisi kupungukiwa, kutofarijika na kama vile jasho lote umetoa kujenga haikuwa na maana yoyote, ukimbie kwa Mungu siku ya saba ukilia, kulalamika huku moyo umekunjamana zaidi ya moyo wa Hana mkewe Elkana?! Kwa viwango hivyo vya kutoridhika, unafunga baraka zako!

Ni kwamba unastahili kupumzika, ukafurahi kama vile Mungu alivyopumzika, akafurahi. Lakini adui alikuibia na alichokuibia ni kustareheshwa pande zote, wewe ukawa unachoona ni dhiki tu. Zab 11: 3 inazungumzia msingi kuharibika kuwa kama ule msingi wa tangu mwanzoni ukiwa umeshaharibika na kuibiwa na adui, hata uwe na haki ya kustahili, utafanya nini?
MATUNDA (Gal 5: 22,23; Mt 12: 23) inakupa HESHIMA (Uf 5: 12; Kut 7)

–Amani Sarepta

Advertisements

3 thoughts on “Uumbaji Umerejea “Hapo Mwanzo…”

 1. Ndugu yangu Amani,

  Haya unayo zungumza si wewe pekee uliye aminishwa na cha ajabu wote mna copy na kupest kwakuwa mmeambiwa ndio sahihi na wala hamkuruhusiwa kupembua wala kupata ushahidi wa kimaandiko. Naona ulicho kitoa hakina maana wala mantiki, jifunze zaidi neno la Mungu na kuacha mapokeo ya mafunuo kutoka kwa waalimu wa uongo.

  Ahsante
  Tujifunze zaidi

 2. ASANTE CK LWEMBE. INAFAA Bw.AMANI APITIE ZILE MAADA ZA UUMBAJI ZILIZOTANGULIA AZIONE ILI APATE PA KUANZIA!

 3. Ndg Amani Sarepta,

  Shalom!

  Nimefurahi kuliona somo ulilolileta kuhusu Uumbaji kurejea “Hapo Mwanzo.”

  Katika mtiririko uliolileta somo hili, naona ni mchanganyiko mzuri wa simulizi ya mafundisho ya kimakundi kuliko Neno la Mungu! Ninawiwa kusema hivyo kutokana na majumuisho uliyoyafanya ambayo nimeshindwa kupata rejea zake za kiMaandiko. Kwa mfano, kumfanya Shetani ni “marehemu”; hili naliona si la kimaandiko maana hatujafika katika ile hatua ya yeye kutupwa katika ziwa la moto (Ufu 20:14), basi wewe kutuambia kuwa Shetani ni “marehemu”, hilo ladhihirisha kuwa yu hai na anaendelea na mikakati yake ya kudanganya watu mpaka amefikia kujifanya marehemu ili watu walale milango wazi!

  Pia maelezo unayoendelea nayo, naona yamejengwa juu ya msingi dhaifu. Nanukuu:
  “”Tunaona Mwa 1: 1-2 “1Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya vilindi vya uso wa maji…” (…ibilisi alikuwepo tayari wakati Mungu anaumba); “Roho wa Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” (Roho Mtakatifu naye alikuwepo hata kabla ya Pentekoste na ikawa anaweza kutambua kwamba haambatani na giza wala ukiwa bali tu anapaswa kutulia juu ya uso wa maji ambaye ni Neno/Yesu).””
  Unasema Ibilisi alikuwepo wakati Mungu anaumba, mimi nadhani umedanganyika saana kiasi Injili yote imekukimbia! Hakuna Biblia inayofundisha hayo mambo yako!!! pia kama vyote vimeumbwa kwa Neno, ambaye ndiye Yesu, sasa aweje tena yeye huyo aliyeyaumba hayo maji awe maji hayo hayo?

  Sehemu nyingine unasema,
  “Jaribu kuvuta picha, Yesu akiwa sambamba na Mungu Baba wakitamka “Hiki kiwepo, kile kiwepo…” na inakuwa!”
  Haya mambo ya Yesu kuwa sambamba na Mungu Baba katika uumbaji unayatoa wapi? Je, hayo si mafundisho potofu?

  Nashindwa kuendelea kutokana na Msingi uliojengea hoja zako kuwa si wa KWELI, basi kuzungumzia mambo ya kufikirika hayatatufaidia chochote, labda kama unaweza kuyadhihirisha hayo machache kimaandiko.

  Ubarikiwe

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s