Najuta kwanini nilikubali kuolewa?

Na: Patrick Sanga

Baada ya mwaka mmoja wa ndoa, Merian asema anajuta kwa nini alikubali kuolewa. Merian na Joseph (haya siyo majina yao halisi) ni mtu na mumewe. Nikiwa katika Mkoa wao kikazi, niliamua kuwatembela wanandoa hawa. Merian alinipokea na kunikaribisha ndani kwa furaha sana. Tukaanza kuongea nami nikamuuliza, Joseph yupo? Akaniambia bado hajarudi kutoka kazini, hata hivyo kaniambia yupo njiani anakuja.

Tukaanza kuzungumuza mambo kadha wa kadha na kisha nikamuuliza mnaendeleaje na ndoa yenu changa? Baada ya kuwa nimemuliza swali hili akacheka na kisha akaanza kwa kusema, nyie maisha haya ya ndoa yaacheni tu, kwa kweli najuta kwa nini nilikubali kuolewa? Kauli hii ilinishtua sana kwa sababu kwanza sikuitegemea na pia ndoa hii ilikuwa ndio imetoka kutimiza mwaka  wa kwanza tu.

Kwa haraka kabla hajaendelea nikamzuia asiseme hayo maneno tena, maana nilijua kadri anavyosema ndivyo anavyozidi kuumba uharibifu kwenye ndoa yake. Akaniambia usinizuie, si umeuliza tunaendeleaje, subiri nimalize kukuelezea. Ndipo akaanza kuniambia kile kilichompelekea kusema anajuta kwa nini alikubali kuolewa (Kwa ufupi ni changamoto ambazo kwa ujumla naweza kusema za kawaida, hata hivyo sitaweza kuziandika hapa kwa sababu maalum).

Katika maelezo yake Merian aliniambia, vijana wengi sana walinifuata ili kunioa, mie nikawakataa, natamani ningeolewa na yoyote kati ya wale wengine, lakini si hapa nilipo na laiti likitokea lolote sasa (kwa maana ya mwenzake kufa) sitakubali kuolewa tena.

Mpenzi msomaji sijui kama unakiona ninachokushirikisha kupitia maisha ya wanandoa wenzetu hawa. Kumbuka ni mwaka mmoja tu wa ndoa, na leo tunashuhudia Merian akijutia maamuzi yake ya kuolewa na Joseph. Licha ya kwamba ni mwaka wa kwanza tu, lakini wawili hawa wameokoka pia.

Maelezo ya dada Merian yaliniletea maswali matano (5) ndani yangu ambayo ndiyo ninayotaka tujifunze kutoka kwake;

Swali la kwanza; Je! Merian, alijua nini maana ya ndoa kabla ya kuolewa?

Swali la pili: Je, Merian alijua aina ya maamuzi anayotaka kufanya kabla ya kuolewa?

Swali la tatu: Je, Merian alimuhusisha Mungu kabla ya kuolewa ili ampate mwenzi sahihi wa kuishi naye?

Swali la nne: Je, Merian alikuwa amejiandaa/andaliwa kifikra kuishi kama mke?

Swali la tano: Je, mpaka sasa, Merian anajua wajibu wake ni nini kwenye ndoa?

Kutokana na maswali haya niliwaza mambo matatu ambayo, nafikiri kama vijana wangefahamu yatawasaidia katika ndoa zao;

 • Moja, ni vema vijana wajifunze kumshirikisha Mungu awaongoze kupata mwenzi sahihi wa maisha, kabla hawajaingia kwenye hizo ndoa.
 • Mbili, ni vema vijana wakajifunza kufikiri kimapana kabla ya kuingia kwenye ndoa. Swali la msingi katika kufungua tafakuri hii, ni kwa nini mtu aoe au kuolewa? Ni swali fupi lakini kama wewe ni mtu ambaye hufikiri kimapana swali hili litakujengea msingi mzuri wa baadaye. Naam kile kitabu cha 1 Wakorinto sura nzima ya saba kikuongoze katika tafakuri hii.
 • Tatu, ni vema vijana wangefunzwa/kuandaliwa vya kutosha kuhusu ndoa na hasa wajibu uliopo mbele yao. Endapo kama Serikali inawasomesha watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea uwezo na maarifa ya kutekeleza majukumu yao, basi ifike mahali kanisa, wazazi, viongozi wa vijana nk makundi haya yaone umuhimu wa kuwaandaa vijana wao kuyakabili maisha ya ndoa.

Watu wengi hufikiri chanzo cha matatizo kwenye ndoa zao ni Shetani. Ndio hii ni sababu moja, lakini sababu nyingine kubwa, ni watu wengi kukosa ufahamu wa masuala ya ndoa kabla na baada ya kuingia kwenye hizo ndoa. Naam wakati watu wanasema Shetani anaangamiza ndoa zetu, Mungu anasema, ndoa za watoto wangu zinaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6).

Ni imani yangu kwamba, kama mambo haya yatazingatiwa, sehemu kubwa ya changamoto ambazo wanandoa wanapitia, zingepata ufumbuzi wa haraka. Natoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya ndoa na hasa Wachungaji, Walimu na Viongozi wa makundi ya kiroho, kuanzisha utaratibu wa kuwa na mafunzo maalum kuhusu ndoa, kwa vijana ambao wameweka wazi dhamira zao za kuingia kwenye maisha ya ndoa.

Ni vema pia, hata kwa wale ambao wako ndani ya ndoa, wakawekewa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara, maana kwa mtazamo wangu ndoa ni shule ambayo, wahusika wanapaswa kuongeza (kujifunza) ufahamu wao kila siku, ili kulitumikia vema kusudi la Mungu.

Bwana Yesu na utusaidie watoto wako, Amen!

Advertisements

15 thoughts on “Najuta kwanini nilikubali kuolewa?

 1. Kaka Paulo, Kaka Paulo Kaka Paulo weweee!!

  Hivi umeandika hayo wewe mwenyewe au umeandikiwa? Hebu naomba unijibu Jibu maswali haya ndipo tuendelee:

  1.Umejuaje kuwa mke uliye naye siyo chaguo sahihi?

  2. Ulikuwa unatamani mke wa chaguo la vipi?

  3. Unawezaje kupata mtoto kwa mke ambaye siyo chaguo lako?

  4. Nani alikuambia kuwa ukiishaoa unaweza kumwaacha mke na kuoa upya?

  Hebu jibu maswali hayo kisha tuweze kukusaidia!

 2. jamani nilikuwa na araka na ndoa bila kuchunguza ninae mwowa sasa ivi ninapata shida sana baada ya kugunduwa kwamba mke nilie nae sasa sio chaguo niliyokuwa nina tamani.na istoshe sasaivi nimeshapata nae mto.sasa jamani sjui nifanyeje nimuache au niowe tena?nisaidieni jamani

 3. Bwana Yesu aingilie kati juu ya hili kwani Elimu ya Ndoa ni darasa lisilo isha, maombi hayaondoi kero bali hukupa mwongozo namna ya kuzishinda hizo changamoto.

  Kupewa mchumba au mke/mume na mungu haimaanishi ndo kufuzu changamoto za ndoa. Hakuna ndoa isiyo na maluweluwe japo vimbwanga vyake vinatofautiana.

  Biblia inasema ombeni bila kukoma, tusibweteke as if shetani amelala usingizi. Biblia inasema nikama Simba aungurumaye akitafuta mtu ammeze.

  Kila hatua ya mahusiano inachangamoto zake zinazo tokana na mazingira fulani baina ya watu hao au eneo walilopo.

  OMBENI BILA KUKOMA……………..!!!!!!!!!!!!!!!!!

 4. Nashukuru kwa maoni mazuri yaliyotolewa na wachangiaji waliotangulia, lakini zaidi kinachohitajika ni hekima kutoka kwa Mungu katika kuishi maisha ya ndoa, unaweza kuwa umeokoka lkn ukakosa hekima, neno la Mungu linatuagiza kuomba hekima, Yakobo 1:5,”Mtu wa kwenu amepungukiwa ………, hivyo ndoa nyingi za wapendwa zinakuwa na shida kwa sababu ya kukosa hekima ya kuishi kwenye ndoa, ndio maana kuna ndoa za wasioamini ni nzuri na zenye ushuhuda mzuri kuliko za waliokoka, kuokoka sio guarantee ya ndoa nzuri, na hata kama ulimshirikisha Mungu mwanzoni kuhusiana na kupata mwenzi na ukapata, kama hautatumia hekima utakuwa hauna tofauti na yule aliyekurupuka.
  mbarikwe tuendelee kujifunza.

 5. asante sana MTUMISHI kwani tunajifunza pia kupitia majaribu kama hayo, mimi mwenye binafsi nawaza sana kuwa je nitafika je katika ndoa ilio mpango wa MUNGU NA kusudi LAKE ELIMU HIYO NA HEKIMA VIJANA WA LEO HATUNA KABISA ENDELEA KUTUSAIDIA PAMOJA NA WATUMISHI WENGINE TAFADHALI NINA KIU NA MAFUNDISHO HAYO KABLA YA NDOA

 6. Mwalimu unaonaje ukaanzisha hili darasa la vijana na semina za ndoa? mwanzo waweza kuwa mgumu lakini mwisho mafanikio yatakwepo na jamii itapona.Hta mwl M
  wakasege na Diana walianza mbali sana .Mimi naona tuliweke ktk maombi jambo hili.

 7. Bwana Yesu asifiwe wapendwa katika Kristo,kiukweli ndoa ni ngumu though ni mpango wa Mungu watu waoane.Maombi ni muhimu sana kabla ya kuingia kwenye ndoa,lakini changamoto inakuja,je utamjuaje kama huyo mtu ni mke/mume sahihi kwako?For sure sina jibu sahihi kuhusu hili sababu tunaona hata ndoa za watumishi wa Mungu zikiyumba,unafikiri hawakuomba kabla ya kuoana?Mungu atusaidie sana.

 8. Ndugu zangu waenda Mbinguni, nawasalimu wote kwa Jina la Yesu. Baada ya salaam hizo nimshukuru Mr. Milanga kwa mchango wake alioutoa kuhusu baadhi ya sababu zinazosababisha ndoa nyingi kuvunjika, au wanandoa kuachana, au kuishi kama maadui katika majumba yao. Luk 16.18 Kila amwachaye mkewe na kumuoa mke mwingine azini naye amwoaye yeye aliyeachwa na Mumewe azini. Kama tunavyohitaji kufundishwa Neno lote la Mungu, yaani Biblia, ni pamoja na Somo la Ndoa. Kuwa na watu wawili wa jinsia mbili tofauti wanakubaliana kuishi pamoja, na hii inakuwa na kwa maisha yao yote mpaka kitu kimoja tu kitakachowatenga KIFO. Na muda wote huo MME anakuwa ana wajibu wake, na MKE anakuwa na wajibu wake. Mmoja anapoacha tu kufanya wajibu wake, tayari hapo AJALI ndipo inapotokea, na ajali inapotokea hapo ndipo Vifo hutokea, majeruhi hupatikana. Ef. 5.33. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe, na mke asikose kumstahi mumewe. ( mtu kupenda mtu kama Nafsi yake mwenyewe) hili linakaaga vinywani tu, halíingii mioyoni likafanyika halisi, Paul akalipeleka zaidi kwa kusema/ KAMA KRISTO ALIVYOLIPENDA KANISA, MPAKA AKALIFIA Ni jambo zito mtu kufa badala ya mtu mwingine, kisa ANAMPENDA. Tumesikia upande mmoja, UPENDE. Ef. 5.22 Enyi wake WATIINI WAUME ZENU, KAMA KUMTII BWANA WETU, KWA MAANA MUME NI KICHWA CHA MKEWE, KAMA KRISTO NAYE NI KICHWA CHA KANISA, NAYE NI MWOKOZI WA MWILI, LAKINI KAMA VILE KANISA LIMTIIVYO KRISTO, VIVYO HIVYO NAO WAWATII WAUME ZAO KATIKA KILA JAMBO.( hapo tumesikia UPENDO NA UTII). Hiyo inaitwa KEEP LEFT. Kiswahili PITA KUSHOTO. Ukitoka Tanzania huku tunapita KUSHOTO, Ukiendesha gari ktk zile Nchi zinazopita KULIA kama America, Rwanda, mpaka akili yako ikae sawa sawa ndio utaendesha gari, vinginevyo, utapita KUSHOTO NA MWENZIO ANAPITA KULIA hapo ndipo ajali itatokea. Na tayari ajali nyingi kwa sasa zimeshatokea, gari nyingi zinahitaji kupelekwa gereji, madereva wengi hawapeleki gereji, wananunua mpya, kwa sababu sheria za barabarani hawazijui, hawakawii kugonga tena, magari mengi yamepata ajali, hata miungurumo ya magari mengi imeharibika. 1Pt 3.7 Kadhalika nanyi waume kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja na neema ya uzima, KUSUDI KUOMBA KWENU KUSIZUILIWE.

  Kama tulivyoona, wana ndoa wengi maombi yao yamezuiliwa, wanakwenda makanisani, wanaomba na hata kufunga, ila hakuna majibu, yamezuiliwa, mpaka waende gereji. Niwakumbushe mambo matatu ambayo shetani ayatumia kusambaratisha ndoa za wengi. 1.siku za mwisho watu watakuwa wenye kuvunja maagano. 2.wasiotaka kufanya suluhu. 3.wasio na shukrani. Ni maombi yangu Mungu ainue WAPATANISHI…. WACHONGANISHI..washushwe. Kol 3.12..Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana, mtu akiwa na SABABU ya kumlaumu mwenzake, kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo nanyi. ( kanisa lina shida kubwa siku tulizonazo, familia nyingi zinakutana na Yesu makanisani, na baada ya ibada wanamwacha humo, wanakwenda nyumbani peke yao, mpaka tena siku ya ibada, Wanandoa nawaombea Mungu alainishe mioyo yenu, upendo, utii, uaminifu vitawale. Mbarikiwe

 9. Mh! Asante mwalimu Milinga kwa muongozo huo.
  JAMANI MNAKUMBUKA MANENO YA WANAFUNZI WA YESU JUU YA NDOA?
  Walisema “kama mambo ya NDOA ni hivi ni afadhali…”

 10. Sio siri huku kuendelea kujilaumu kuwa hatumshirikishi Mungu katika kupata wenzi wetu kunananiudhi sana.

  Matatizo/changamoto za ndoa zipo tu hata kama tumepata wenzi sahihi kabisa toka kwa Mungu.

  Ibrahim na Sara ziliwapata (walichelewa kupata mtoto), Isaka na Rebeka ziliwapata( walichelewa kupata watoto lakini pia kulikuwa na roho y upendeleo kati yao – Isaka alimpenda Esau, na Rebeka alimpenda Yakobo), Yakobo na Rahel na Leah ziliwapata ( Rahel alichelewa kuzaa, lakini pia kulikuwa na mashidano kati yao , nk), Ayubu na mke wake ziliwapata( Ayubu aliugua, mke akamshauri amkufuru Mungu afe, Ayubu kamwona mke wake kama mmoja wa wanawake wapumbavu) Yusuf baba wa kambo wa Yesu na mke wake Mariam wao ziliwaanza kabla hata hawajafunga ndoa ( Mariam alionekana ana mimba), hiyo ishu haikuwa rahisi kama tunavyoisoma leo kwenye biblia, nk

  Hao wote walizishinda hizo changamoto kwa sababu walikuwa wamefunzwa na kufunzika kuhusu ndoa, na kila mmoja akajua nafasi yake.

  Kama kumshirikisha Mungu kungekuwa ndo suluhisho la ndoa, nisingetegemea kuona ndoa za waliookoka nazo ziko kwenye misukoksuko hata na wengine kuachana kabisa- si wao wameokoka! Lakini matatizo ya ndoa kwa sehemu kubwa hayako katika mambo ambayo ni ya kiroho sana, la hasha. Ni katika mambo ya kawaida kabisa ya kibinadamu.

  Kwa mfano kama alivyosema ndg Milinga hapo juu kuhusu matumizi ya fedha,ni suala la kujifunza tu na kuamua kubadilika.
  Mambo ya kusiklizana na kuheshumiana na kushirikishana katika mambo yote, hayo yote ni mambo tu ya kijamii ya kujifunza.

  Lakini mfumo dume bwana ukijumlisha na ujuaji wa wanawake wengi siku hizi ni shida tupu, ndoa hata hazimalizi miaka miwili.

 11. Mr. Milinga Mungu akubariki sana nimejifunza kitu cha thamani sana ndani ya maelezo yako. God bless you.

 12. Napenda kuwaasa wapendwa kwamba kuishi katika ndoa kwa miaka 40 au zaidi tangu kufunga ndoa yahitaji tunda lisilooza la uvumilivu. Ni vigumu sana ndoa yako kustahimili kuishi duniani zaidi ya miaka hata miwili au hata mmoja sembuse miaka 40 ijayo kama hakuna tunda “lisilooza” la uvumilivu. Yafuatayo kwenye ndo huwa wengi yanawashinda kuvumilia:

  1. Kunyimwa unyumba (tendo la ndoa).

  Hii inaongoza sana duniani. Matatizo mengi huanzia hapa. Mwanamke anaweza kumunyima mume au mume kumnyima mke. Kama umeoana na mtu asiye na uvumilivu ndoa itaanguka haraka sana. Ukiona ndoa imekaa mwaka mmoja tu na kuanza kusambaratika chanzo kikuu (kwa mujibu wa utafiti) ni ukosefu wa tendo la ndoa ndani ya ndoa. Au ni uwepo wa tendo hilo siyo kwa ukamilifu unaotakiwa. Na kama umeoana na mtu asiyeweza kuvumilia yaani hakulelewa katika mazingira ya uvumilivu na anaweza kutulia hata kama atanyimwa kwa mwezi mzima, basi ndoa inaenda kusambaa ndani ya mwaka mmoja.

  2. Matumizi mabovu ya fedha:

  Sababu nyingine zinazosababisha ndoa kusambaa ni mmoja wa wanandoa kutokuwa makini katika matumizi ya fedha zinazopatikana. Mwanamke kama analipwa mshahara hataki pesa yake itumiwe na mwenzie au mume hali kadhalika pesa zote azipatazo mke hajui zinaishia wapi. Yaani haoni maendeleo yoyote yafanyikayo kwa faida ya familia. Hii huleta ghadhabu kwa mwanandoa na husababisha ndoa kusambaa.

  3. Kuchelewa kupata uzao:

  Utafiti pia unaonesha kwamba wanandoa wengi wakichelewa kupata uzao hali hiyo huhatarisha ndoa hiyo. Muda wa chini sana wa kuvumilia kusubiria kupata mtoto huwa ni mwaka mmoja. Kamwa wanandoa watakaa zaidi ya mwaka mmoja bila kupata uzao majaribu ya ndoa kusambaratika yanaanza. Tena yanaanzia kanisani. Wapendwa ndio wanaokuwa wa kwanza kuanza kutoa masimango kwa wanandoa. Mdogo wangu aishie Dar alichelewa kupata uzao kwa miaka 2. Wapendwa wengi wa kanisani ndio waliokuwa mstari wa mbele kutoa masimango ambayo kwa kweli yalianza kuihatarisha ndoa hiyo. Mdogo wangu yule asingevumilia na kumtia moyo mwenzake ndoa ilikuwa imeanza kupata mpasuko.

  4. Kupata watoto wa jinsia moja.

  Zipo ndo nyingi zimesambaratika kutokana na kwamba uzao uliopatikana umekuwa wa jinsia moja. Kama watazaa watoto wa kike peke yake au wa kiume tu, ndoa hiyo iko mashakani. Wapo wanandoa wanaotengana kwa sababu tu mimba ya tatu amezaliwa mtoto wa jinsia ile ile ya watoto wawili waliokwishatangulia.

  5. Mmoja kuwa na upungufu wa Nguvu za Kiume/Kike

  Wanandoa wengi wamesambaratisha ndoa zao kutokana na kwamba mmoja wa wanandoa alikumbwa na tatizo la kupungukiwa nguvu za kufanya tendo la ndoa. Mwanamke akipungukiwa nguvu za kike anakuwa hawezi kumfurahisha mume. Anakaa kama gogo wakati wa tendo la ndoa. Hashughuliki kabisa. Yupoyupo tu. Sehemu zake za siri ziko kavu mno. Hali kama hii huhatarisha ndoa. Mume naye akiwa hana nguvu za kiume anashindwa kumpa haki mkewe. Hawezi kwa sababu hana uwezo kabisa wa kufanya tendo la ndoa. Mke atavumilia mwezi wa kwanza, wa pili, tatu, nne, tano, sita, nk mwisho uvumilivu utamshinda.

  6. Familia kubwa au Familiamtandao

  Familia kubwa au Mtandao (extended family).Hili nalo huleta migogoro sana kwenye ndoa. Kumshirikisha Mungu kabla ya ndoa hakuondoi uwezekano wa kuwa na familia pana iliyotandaa pande zote. Wajomba, mashangazi, mawifi, wadogo zako, wazazi, binamu, mashemeji, nk. yote haya huwa mzigo kwa familia nyingi kiasi kwamba mwanandoa mmoja (hasa wanawake) hulemewa sana na hatimaye kuona kama hali ikiendelea hivyo bora arudi kwao kwani hapo alipo ni kama ameolewa na ukoo mzima. Hana raha wala uhuru na mumewe.

  Bado ninazo hoja nyingi, lakini naomba kwa leo nimalize kwa kusema kwamba ndoa nyingi hazisambaratki kwa sababu vijana hawakupewa mafundisho ya jinsi ya kumshirikisha Mungu ili awasaidie kupata wenzi wao walio sahihi. Ukweli ni kwamba mwenzi sahihi HATOKI KANISANI. Wala hapatikani kwa kuomba sana Mungu. Huwezi kupata mke au mume mwema kwa sababu wewe ni mwombaji sana au umehudhuria mafunzo mengi ya ndoa, NO.

  Sababu zote hizo nilizozitoa huweza kumkuta mtu yeyote yule. Swala la familia pana linawasumbua sana wake wengi wa wachungaji na watumishi wa Mungu. Swala la matumizi mabaya ya fedha au mmoja kutoridhika jinsi mwenzie atumiavyo fedha linawakumba wote. Kupungukiwa nguvu za kike/kiume linawakumba watu wote hata waliookoka, hata kama uliomba sana na kupata semina nyingi laweza kukupata na kuhatarisha ndoa yako kutoweza kusimama hata kwa mwaka mmoja.

  Kwa hiyo, swala la kuwezesha ndoa kudumu kwa muda mrefu halitokani na mtu kuomba sana Mungu bali linatokana na sababu nyingi sana zikiwemo zinazotenezwa na jamii inayotuzunguka, wapendwa, ndugu, uchumi, afya zetu, nk. Kinachoweza kusaidia ndoa zetu zidumu sana ni malezi mazuri na makuzi mema ya uvumilivu na usawa tunayowapa watotot wetu wa kike na kiume. Kama malezi ni mabovu toka utotoni hata kama umeokoka malezi hayo yatakuathiri hadi ukubwani. Nguvu za kiume/kike zikiisha mwilini mwako kama siyo roho ya uvumilivu huenda ndoa ikashindwa hata kumaliza miaka miwili tu. Kwa heri kwa sasa.

 13. Ni vema vijana tujifunze kumshirikisha Mungu atuongoze kupata wenzi sahihi wa maisha, kabla yakuingia kwenye hizo ndoa. mana yakikukuta hakika majuto ni mjukuu.

 14. Nina rafiki zangu wengi wa kike na wa kiume ambao tumekuwa marafiki kwa miaka mingi sasa. Wengine (wa kiume) tumewa kuishi wote geto na kwenye hostel wakati niko chuo. Ilikuwa na bado inatokea kutofautiani wakati mwingine, lakini hiyo haijawa sababu ya kuvunja urafiki wetu au kushindwa kuishi kwa furaha na ushirikiano kama marafiki.

  Kitu kinachonishangaza kuhusu matatizo ya ndoa ni hiki; Kwa nini kwenye urafiki wetu na watu mbalimbali tunaweza kuvumiliana tukakaa kama marafiki kwa miaka nenda rudi, lakini kwenye ndoa ambayo na yenyewe ni urafiki lakini wa kiwango cha juu kabisa kuliko urafiki wowote mtu anashindwa kuifurahia hata kwa mwaka mmoja tu?

  Kuna fumbo gani la matatizo kwenye urafiki wa ndoa ambalo watu hawawezi kuliona kabla ya kuoana lakini wakishaona tu na lenyewe ndio linaanza kuonekana?

  Mara nyingi sana tunapenda kusema ‘tumshirikishe Mungu kwenye kuoa/kuolewa kwetu’, lakini tangu nimeanza kuona watu hasa vijana wanapewa huo msisitizo sioni kama taarifa za matatizo ya ndoa zimepungua, naona zinazidi kuongezeka. Je ni kwamba watu hawamwombi Mungu?

  Lakini pia huku kumshirikisha Mungu huwa kuna maana gani au ni kupi hasa jamani?
  Ni nani kwenye biblia basi ambaye alimshirikisha Mungu kwa maana ambayo huwa inamaanishwa leo ya kumshirikisha Mungu, yaani kulipeleka suala la kutafuta mwenzi kwenue maombi kabla hujafanya maamuzi?

  Je ni Isaka kumpata Rebeca? mimi nasema hapana, hakuomba
  Je ni Yakobo kumpata Recho au Leah? Mimi nakataa kabisa’ hakuomba
  Je Ni Yusufu kumpata Mariam? Hapana, hata yeye sioni kama alimshirikisha Mungu kwa kuomba.

  Maana ya kumshirikisha Mungu kwa upande wangu sio kuomba, maana kama ingekuwa ni hivyo kusingekuwa na mitume na manabii pamoja na watumishi wakubwa wa Mungu wanapitia matatizo kwenye ndoa zao. Think of Ben Hinn, hata mzee Ayubu wa kwenye biblia waligombana na mke wake. Je hawakuomba Mungu kabla ya kuoa?

  Pia lazima wtujichunguze tabia zetu kwenye ndoa kama ziko sawa kabla ya kuanza kuwalaumu wenzi wetu kwa kwa matatizo yanayojitokeza, maana tunaweza kuwa tumeyasababisha wenyewe halafu tunabaki kulaumu. Lazima tujiulize je tunawajibika sawasawa kwa wenzi wetu, tuna majibu mazuri kwa wenzi wetu, tunawatimizia yaliyo haki yao, na je sis si wabinafsi na wenye misimamo dhidi ya mawazo ya wenzi wetu, n.k?

  Msimamo wangu kwa kifupi nauweka hivi; Tunatakiwa kuoana na watu tunaowafahamu kitabia pamoja na historia zao. Au kwa maneno mengine, unatakiwa kuoa au kuolewa na mtu ambaye ni rafiki yako kwanza. Siamini katika kupata mwenza kwa njia ya ufunuo kama ndio msingi wa kupata wenza sahihi, ispokuwa inaweza kufanyika hivyo kwa kusudi mahsusi la Mungu.Na tuhakikishe kuwa tumejua kuwa tunaweza kuishi nao kabla hatujafnya maamuzi ya kuoana.

  Mfano wangu mzuri wa kupata mke/mme huu hapa: Naomba tusome hadithi ya Boaz alivyomuoa Ruthu. Na ili kukuhakikishia kuwa mtindo(style) waliotumia ambao unaonekana kuwa wa kimwili sana kumbe ndo yalikuwa mapenzi ya Mungu, kutoka kwao Masihi au Yesu kristo alizaliwa.

  Na kufanya kama wao walivyofanya kwa upande wangu huko ndiko kumshirikisha Mungu. Ni kujua kanuni za kumpata mke mwema ambapo ni pamoja na kufuatilia historia yake. Ruthu hakuwa mwanamke wa kawaida kwa pande zote mbili: kiroho alikuwa ni mwanamke mwenye imani isiyo ya kawaida, na kwa upande wa kimwili alikuwa mwanamke mwelevu na mchapakazi na Boaz alikuwa analijua hilo
  ( Soma hasa Ruthu 3-4, lakini kwa kumjua Ruthu alikuwa mwanamke wa namna gani soma Kuanzia sura ya kwanza)

  Tubarikiwe!

 15. Bwana Yesu asifiwe,natumai hamjambo wana wa Mungu.mimi naamini hivi hata kama watu wameomba wakapata wenzi sahihi bado shetani yupo kuwachakachua na kuwatoa katika devine union.

  Jambo moja kubwa nililojifunza kwa wanandoa wengi na watu wengine ambao si wanandoa ni KUTOKUA TAYARI KUFANYA SULUHU pindi wanapokabiliwa na changamoto au kutofautiana. Kitendo hiki hukuza sana migogoro,huenda ukakuta tatizo anzilishi ni dogo sana tena ni aibu kusema eti linamfanya mtu kutamani kukimbia ndoa,lakini kwakuwa liliachwa unsolved litazaa mengine.

  Pia shida nyingine kubwa ni watu wanafunga ndoa za kikristo lakini si NDOA TAKATIFU. Hizi ndoa za kikristo ni ndoa zinazofungwa kwa itikadi ya dini yaani mtu anafarijika kuona kaoa/kaolewa kanisani LAKINI uliza je mtaishi kama NENO LA MUNGU linavyoelekeza???? Wengi wetu hatuishi hivyo so ndoa zetu nyingi ni za kidini lakini hazina mizizi ktk neno la MUNGU.

  Hebu tafakari mke amtii mume wake kwa kila jambo, ndo Biblia iansema hivyo na Mume ampende mke wake kama Kristo alivyopenda kanisa lake.Hapo kutii si kwa kurespond tendo fulani jema alilotendewa na mumewe NO!! Atii tu na mwanaume kumpenda mkewe si hadi afanyiwe mambo mazuri ajabu NO!! Ampende tu pamoja na udhaifu wake maana Kristo alilipenda kanisa lingali chafu tena dhambini akalifia.

  Mwishowe niseme hivi,biblia inasema tusimpe shetani NAFASI ila sisi tunampa linafasi sana kupitia tofauti zenu kwenye mahusiano yetu.Kwa nini tusimshirikishe MUNGU mbona yeye amesema tumtwike yeye fadhaa zetu maana hujishughulisha sana na mambo yetu??TUNa shida ya UZEMBE au KUPUUZIA na kusimamia na kuamini kile alichosema MUNGU kuhusu sisi.Hata kama uliomba ukapewa mwenzi wako na MUNGU si mwisho wa kumshirikisha MUNGU maana mna personality na makuzi tofauti sasa mtakosaje kuwa na kutofautiana???

  Nimejaribu tuuuu!!!
  Download the latest BlackBerry® applications from Zantel on http://www.zantel.com/zantelapps

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s