Yuda kumsaliti Yesu, Ulikuwa mpango wa Mungu?

Jamani mimi nina swali, ni kuhusu habari ya Yuda aliyemsaliti Yesu, Mungu alimleta YESU duniani kuokoa wanadamu na huo ndio ulikuwa mpango kamili wa Mungu, kifo cha Yesu ulikuwa ni mpango kamili wa Mungu na ndio maana hata Yesu alipoomba kikombe kile kimuepuke bado alikinywea, sasa swali langu linakuja hapa, ni kwa nini Yuda anaonekana ana kosa kwa kumuonyesha Yesu hata akakamatwa na kusulubiwa wakati huo ulikuwa ni mpango wa Mungu, sio kwamba Yuda alitimiza mpango wa Mungu?

Ahanteni kwa majibu yetu yatakayofwata, nitashukuru sana iwapo mtu atanijibu kwa kutumia maandiko

–Star

Advertisements

19 thoughts on “Yuda kumsaliti Yesu, Ulikuwa mpango wa Mungu?

 1. Tuna nafasi sawa mbele za Mungu lakin ni jukumu la kila mmoja kutumia fursa yake vizur.wote tu kazi ya mikono yake hata lusifa alikuwa na nafasi ya kutubu lakini hakuthubutu bali alisimama kinyume chake yeye aliyemuumba.

 2. Nawashukuru wote walio changia mada ya Yuda Iskariote,imenifumbua akili,na kwa hii na ahidi kubadirisha nia yangu nisimsaliti Yesu. endeleeni kutoa mafunishn kwa njia hiyo. mbarikiwe.

 3. Yesu akufa kwa sababu Mungu alimsikiliza na paulo ndo anapinga Mungu, Yesu aliomba, yohana 12,27—waibrania,5,7,,,zaburi,68,20

 4. kwakweli nimefaidika sana na wakristo wote waliochangia mada hii ya yuda..haswa maelezo mazuri ya huyu ndugu wa mwisho hapo juu yangu……kwakweli sisi wanadamu wakatifulani tunaishi kwa akili zetu na utashi wetu na kumkosea mwenyezi mungu pasipo wenyewe kujitambua…lakini mapenzi ya mungu na makusudi yake yanatimia katika neno lake.Mungu aliweka mpango huu ili vizazi vitakavyofuata viamini biblia kuwa ni neno kamili kabisa linalotoka kwake na kujenga imani iliyothabiti kabisa kabisa.Hakuna dini wala kitabu chochote hapa duniani chenye utabiri wa ajabu na kilicho bora kabisa kama BIBLIA.Mungu wetu tangu enzi na enzi kabla ya yuda hata na yesu mwenyewe kuzaliwa alitujulisha hivi:TAZAMA MAMBO YA KWANZA YAMEKUWA NAMI NAYAHUBIRI MAMBO MAPYA KABLA HAYAJATOKEA NAWAPASHENI HABARI ZAKE.Soma( isaya 42:9).Na kuhusu habari hizi za yuda,Mungu wetu YEHOVA alitabiri hivi kupitia nabii zekaria:NIKAWAAMBIA MKIONA VEMA NIPENI UJIRA WANGU,KAMA SIVYO MSINIPE BASI…WAKANIPIMIA VIPANDE 30 VYA FEDHA KUWA NDIYO UJIRA WANGU……Soma(zekaria 11:12-14).Kwakweli ni ajabu na inatia moyo kwelikweli kuona maajabu hayo ya biblia na kutambua kuwa sasa ni HAKIKA KABISA KUWA TUKO KATIKA NJIA SAHIHI YA MUNGU MWENYEWE YANI BIBLIA!!….Hivyo ndugu zangu wakristo lazima tufahamu kuwa mawazo ya mungu na akili zake hazichunguziki ndiyo maana akatuletea njia ya kupata haki mbele zake kwa neema maana kama ingekuwa kweli mpaka leo tujitahidi kupata haki yake kwa sheria na matendo yetu basi ulimwengu wote tungekuwa twasubiri adhabu ya moto wa milele kwa kuwa hakuna aliemkamilifu hata mmoja.soma(mhubiri 7:20)(warumi 3:19-22).Kwa hiyo nimalizie mchango wangu kwa kuunga mkono wachangiaji huko juu kuwa mayuda wako wengi hata leo tena mpaka ndani ya makanisa lakini kwa upumbavu na tamaa zao hizo,neno la mungu linatimia na wokovu wa mungu kwa watu wake unakuwa,usijekushangaa kaenda mbinguni muumini lakini padre wake kanisani na baba yake mzazi wako motoni!!….alichokijua mungu kwa yuda na kukiandika kwamba kitatokea kamwe hakimpi yuda haki yoyote mbele za mungu bali kile kilikuwa ni kipawa cha mungu mwenyewe kujenga misingi imara ya waaminio katika neno lake…hata leo mungu anajua kesho utafanya nini ijapokua wewe mwenyewe hujui ya kesho yatakuwaje kama utamgonga mtu barabarani na gari yako au la!!…ndiyo maana unyenyekevu,utiifu na upendo kwa mungu ni vitu muhimu sana kwetu ili atuweke katika dhamira za pendo lake kwa yale yote yajayo tusiyoyajua kwa hakika yaliyo matakatifu mno mno!!…soma(warumi 11:33-36).Lakini ili tufanikiwe,yesu kristo ndiye jibu la mambo yote na pasipo yeye HAIWEZEKANI HAKIKA!!…Kwa sababu wokovu wetu ni kipawa cha mungu kwetu kwa njia ya yesu kristo kuliko matendo yetu yote ya kufuata sheria za mungu kwa nguvu zetu wenyewe.(galatia 3:10)…mbarikiwe.

 5. Wapendwa Heri ya mwaka mpya?

  Mbarikiwe sana kwa maelezo yenu mazuri kuhusu mada hii.

  Nimefurahishwa sana na maelezo ya mpendwa CK Lwembe na Patrick Kamera.

  Kwa mtazamo wangu, Yuda alitekeleza unabii wa maandiko bila yeye kujua. Alifanya jambo ambalo kusema kweli hakujua kama lingefika mbali namna ile. Yuda yeye alikuwa na mahitaji ya fedha zaidi. Alikuwa amebanwa na matatizo nyumbani kwake ambayo yalihitaji apate fedha ili kuyatatua kama ilivyo kwa wainjilisti, manabii, wachungaji, maaskofu na mitume baadhi yao wanapokuwa na mahitaji ya kifedha na wakakosa msaada huo hujikuta wakimsaliti Yesu kwa kutenda vitendo viovu.

  Wapo wapendwa wengi tu huwa tunamsaliti Yesu linapofika swala la fedha kuhitajika. Kuna wapendwa wengi hutia saini kwenye nyaraka maofisini kwao au sehemu yoyote ya kazi ambazo siyo halali yao. Wengi humsaliti Yesu sana kwenye fedha. Wale watumikao madhabahuni hutumia vibaya fedha za sadaka na zaka. Wapo waliojilimbikizia fedha na wana majumba ya kifahari na magari ya fahari kuliko hali halisi ya vipato vya waumini wao na uchumi wa taifa hili. Huku nako ni kumsaliti Yesu.

  Je, fedha tunazozipata ni halali au haramu? Ni mara ngapi wewe umepokea fedha ambazo siyo halali na ukazichukua? Au ni kama zile za Yuda alizopata kwa kumkana Yesu aliyeishi naye kwa zaidi ya miaka mitatu? Wapendwa na watumishi kutumia fedha nyingi kwenye mambo ya kifahari badala ya kuwasaidia yatima, wajane, mafukara na masikini; je, huku siyo kumsaliti Yesu sawa na Yuda Iskariote?

  Yuda alipobanwa na mahitaji mengi nyumbani kwake aliona dili mbele yake akaona aliwahi. Inawezekana alikuwa anahitaji fedha za kugharimia matibabu ya watoto wake, au alihitaji fedha za kununua kiwanja, au alihitaji fedha za ujenzi wa jumba lake la kifahari, au alihitaji fedha za kwenda kutalii, au alihitaji fedha za kununua gari lake la kifahari, nk. Alipoona dili la fedha, akasema waoooo, mbona hiyo rahisi tu. Nyie mnamhitaji Yesu? Aaah mbona rahisi tu. Yule mimi namjua sana, ni rafiki yangu, niko karibu yake sana. Kama mnamhitaji mweze kumtia korokoroni huyo jamaa, nyie nipeni dola tu mimi nitawaonesha alipo na nyie mtamkamata.

  Yuda akakamata dola au mshiko akatia mfukoni akawaongoza vijana wa kazi yaani maafande wa kirumi na kuelekea hadi Yesu alipo. Ghafla Yesu anaona kundi la maafande wametinga pale Gethsemane huku wakiwa na mmoja wa wanafunzi wake Yuda Iskariote. Yesu anamwona akija kumbusu kumbe ndo usaliti wenyewe.

  Yuda yeye aliamini kwamba Yesu angetimua mbio na kuwatoka maafande wakabaki kwenye mataa. Siku zote alimjua Yesu kwamba ni mkali sana kwa hilo la kukwepa watu wabaya. Kuna siku Yesu aliwaponyoka watu waliotaka kumuua. Yuda alikuwa anakumbuka sana tukio hilo. Yuda alipoona Yesu hakutimua mbio kuwatoroka maafande wa kirumi alishangaa sana. Daah jamani Yesu ameshindwa kutimua mbio? Yuda alijua kwamba dili lake la kupata fedha limetimia yaani yeye anapata mshiko mfukoni halafu Yesu atimue mbio na mwisho watajiju wale maaskari.

  Yuda alipoona Yesu amekubali kutiwa mikononi mwa maafande wa kirumi kwa kweli alishangaa sana. Kwanza hakuamini. Pili alijua kwamba labda pale mbele kidogo atawachomoka maaskari, lakini wapi. Akafuatilia mpaka mwisho bila kuamini kinachotokea mbele yake.

  Mwisho, alipoona Yesu amezidiwa kabisa kwa vichapo na vipigo vya maafande, mateke, virungu, matusi, mate, mapanga, viboko vyote vikawa ni halali kwa Yesu, Yuda akaona sasa hapa aibu ni yake. Atawaambiaje wanafunzi wenzake? Hili lilikuwa swali lake kuu moyoni mwake. Nitamwambiaje kaka Peter, Kaka Yohana, Yakobo, nk? Maswali mengi kichwani yakamjaa. Hizi fedha nitazifanyia kazi gani sasa kama Yesu ameteswa hivyo?

  Yuda akaona majawabu kichwani. Moja, ngoja niwarudishie hawa jamaa fedha zao ili mimi niepuke fedheha hii niliyoisababisha ili wamwache Yesu aende zake. Au waende kuwabembeleza wale maaskari wamwachie basi aende zake. Akaenda akawarushia zile pesa walizompa. Akawabembeleza watafute namna yoyote Yesu aachiwe. Wakamwambia bwana wee utajijua? Shauri yako bwana usituulize sisi. Hilo lako bwana. Sisi tumeshamaliza.

  Yuda alipoona hilo limeshindikana na akatafakari aibu atakazopata mtaani, masimango atakayopata, lawama atakazopewa, akasema potelea mbali, liwalo na liwe bwana. Dawa ni kujiondoa kwa kitanzi tu. Mimi siwezi kuendelea kuishi huku nikishuhudia yanayotokea kwa rafiki yangu Yesu kuteswa hivyo nikiwa ndiye chanzo. Yuda akakamata kamba akajinyonga.

  Swali: JE YUDA ALIFANYA DHAMBI KUMSALITI YESU?

  Wapendwa waliotangulia kusema kweli wamelijibu kwa kina swali hilo wala sina sababu ya kuyarudia yote.

  Lakini ambalo ningeweza kusema hapa ni kwamba Mipango ya Mungu lazima itimie. Mungu atatumia njia yoyote ili kutimiza alichokipanga iwe kwa kumtumia mwanadam au hata mawe yaweza kutumika kutimiza mpango wa Mungu.

  Mwanadam ameumbwa na hulka mbili: KUTAKA AU KUKATAA. Mambo hayo mawili huwa hayaingiliwi na Mungu. Mungu humwacha mwanadam afuate kimojawapo. Hivyo anasema, ‘…nimeweka mbele yako MAUTI + UZIMA, BARAKA + LAANA…..” Mungu anamtaka mwanadam achague kwa hiari yake mojawapo ya hayo.

  Yuda alichagua KUMKATAA YESU kwa hiari yake. Mtu yeyote aliyeokoka au aliyeamini au aliyeongoka (kama anasema CK Lwembe) bado anaweza kuchagua KUMKATAA YESU hata kama alishamwamini Yesu, hata kama alishaokoka au akazaliwa mara ya pili hilo halimfanyi asiwe tena na utashi wa kuweza kumkataa au kumsaliti Yesu kwa hiari yake mwenyewe.

  Tukumbuke kwamba hata kama umeokoka, umeongoka, umezaliwa mara pili, umejazwa Roho Mtakatifu, nk hii haikuondolei utashi wako. Wala Mungu hawezi kukuendesha au kukulazimisha ufanye usiyoyataka. Utashi wako kwa hiari yako kabisa unaweza kumkataa Yesu na ukamsaliti kwa makusudi au kwa kulazimishwa na mazingira unayoishi, umaskini, mamlaka za nchi, mamlaka za ajira, mamlaka za mwili (homoni), tamaa za maisha bora, nk vyote vyaweza kukusababisha ukamsaliti Yesu. Hata Yuda Iskariote kama Biblia ingeandika kila kitu juu yake, unaweza kugundua kwamba huenda alilazimishwa na mojawapo ya sababu kama hizo. Lakini yote kwa yote ni dhambi tu. Yuda alitumia utashi wake kutekeleza usaliti dhidi ya rafikiye Yesu Kristo.

  Je, mpendwa hapo ulipo hujawahi kumsaliti Yesu kwa namna yoyote? Kwa hiyo hata kama umeshazaliwa kwa Roho, kwa maji, kwa kuvuviwa Roho Mt, bado waweza kumsaliti Yesu. Ndiyo maana Yesu anauliza, Je, akija mwana wa Adam ataikuta Imani?

  Nikkutakie siku njema, Kheri ya mwaka mpya 2013.

 6. Ndg Kamera,

  Shalom!
  Asante kwa maelezo mazuri.

  Kimsingi, naona tumekidhi haja ya moyo wa muulizaji, basi naona haya mengine ya kunyakuliwa yataivuruga mada.

  Labda tukipata wasaa twaweza kulirejea hilo katika kuuchunguza ukweli ili kuziondoa “wishful thinking” katika hatua zetu, kama ninavyoiona kauli yako hii:
  “Kuhusu ni nani watakaonyakuliwa, ni vizuri tuelewe ya kuwa Kanisa ni Mwili wa Kristo, siyo dhehebu fulani. Madhehebu ni ya wanadamu ila Kanisa la kweli ni lile ambalo Bwana Yesu analijenga na alilisemea maneno haya: “Nitalijenga Kanisa langu na milango ya kuzimu haitalishinda”

  Asante sana, na
  Bwana akubariki katika yote yenye kumpa utukufu Yeye!

 7. Ndugu Ck Lwembe,

  Kama nilivyomjibu mpendwa mwingine hapo juu, Yuda alikuwa na hatia maana kwa utashi wake mwenyewe bila kulazimishwa alimpa Ibilisi nafasi ya kumtumia kumsaliti Bwana Yesu. Kama ulivyosema alikwenda mwenyewe kwa Makuhani kuwapa “dili” la kumsaliti Bwana Yesu

  Marko 14: 14 – 16
  14 Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani,
  15 akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.
  16 Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti..

  Hivyo pamoja na kwamba kwa kufanya hivyo maandiko yalitimizwa na kazi ya ukombozi kukamilika, bado dhambi yake ipo pale pale maana aliishia kujuta tu ila hakutubu na kupokea msamaha ambao Bwana Yesu aliutoa kwa wote waliokuwa wakimbeza na kumtesa na hatimaye kumsulubisha. Hana tofauti na Pilato wala Kayafa wala Makuhani na Wayahudi na askari wa Kirumi ambao walimsulubisha Bwana Yesu maana aliwaombea msamaha wote lakini je ni wangapi kati yao waliotubu na kupokea msamaha huo?

  Luka 23: 34

  34 Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

  Kuhusu ni nani watakaonyakuliwa, ni vizuri tuelewe ya kuwa Kanisa ni Mwili wa Kristo, siyo dhehebu fulani. Madhehebu ni ya wanadamu ila Kanisa la kweli ni lile ambalo Bwana Yesu analijenga na alilisemea maneno haya: “Nitalijenga Kanisa langu na milango ya kuzimu haitalishinda”, ni Kanisa hilo ambalo litanyakuliwa,

  Mungu akubariki!

 8. Ndugu Star Eze,

  Kwa mtazamo wangu ambao umetokana na Neno la Mungu linavyosema kitendo cha Yuda kumsaliti Bwana Yesu kilikuwa ni dhambi. Bwana Yesu mwenyewe alimwambia Pilato,hivi:

  Yohana 19:11

  11 Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.

  Sasa ni Yuda aliyemsaliti Bwana Yesu kwa Kuhani Mkuu na hatimaye ndiye aliyesababisha mpaka afikishwe mbele ya Pilato na kusulubiwa, hivyo Yuda anayo hatia pamoja na ukweli kwamba hatia hiyo ilipelekea maandiko kutimia na wokovu kupatikana kwa kifo na ufufuo wa Bwana Yesu.

 9. Ndiyo, ndg Kamera,

  Nami pia nakushukuru kwa msimamo thabiti wa kubaki katika Maandiko, ubarikiwe kwa hilo. Unajua, sote tunaweza tukakosea, lakini Maandiko hayawezi kukosea kwa sababu hayo ni Mungu!

  Nikiirejea kauli yako kuwa, “Hayo madai yako ya kuwa Yuda hakujuta yanapingana na Maandiko moja kwa moja, soma Mathayo 27: 3 – 5”, labda niseme hivi, kuwa kujuta kunakoambatana na wokovu, mara zote, humuongoza mkristo katika toba; na pia kujuta kwa hao wengine, ni kujuta kwa kawaida kunakoweza kufanywa na mnafiki yeyote yule, kama Yuda! Ndio maana wale wakuu wa makuhani walimshangaa, kwamba yeye ndiye aliyewafuata, wakabargain biashara yake, na walipofikia muafaka wakamlipa ujira wake, sasa anarudi kwao kufanya nini? Wakamwambia hayo yake mwenyewe! Yuda alikuwa ni MNAFIKI, kwa hiyo majuto yake ni majuto ya mwizi yeyote yule, ambaye akipata nafasi huendelea na wizi wake!!! Pia sidhani kwamba kuyaelewa Maandiko katika context hii, inakuwa ni kuyakataa ama kubishana na Maandiko, hapana, nadhani itakuwa kinyume hapo utakapovichukulia vifungu hivyo kuashiria kuwako kwa toba katika nafsi ya Yuda na hivyo siri zote ulizopewa awali ya tukio hilo, kuwa bure kwako, hazikukusaidia kuyaelewa hayo!

  Ni katika dhana kama uliyonayo, wengi wetu hufikia kuamini kuwa Yuda hakuwa na dhambi, kwani alitimiza mpango wa Mungu! Lakini napenda kukuhakikishia kuwa kutimiza mpango wowote ule wa Mungu, hakukufanyi wewe kuwa msafi. Biblia imejaa mifano ya watu wengi sana waliotimiza kusudi la Mungu, kama ni kuwatesa wanae nk, lakini mwishoni waliadhibiwa kwa kulitimiza kusudi hilo hilo!

  Pia Biblia inapokuambia habari za Yuda katika ukamilifu wake, basi inapokuambia, “na mmoja wenu ni shetani (a devil)”, ni vizuri kutumia ufahamu wote uliopewa ili ukufikishe katika uelewa kamili wa jambo. Ndio maana kwa uhakika naweza kukuambia kuwa ndani ya nafsi ya Yuda kulikuwa hakuna TOBA. Na pia ufahamu huo hunionesha zaidi mambo yaliyofichwa, kwani namuona Shetani ndani ya Yuda akijihudhurisha mbele za Bwana kama alivyomuona Ayubu: 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao.” Basi kulingana na Maandiko, kama yanavyotuambia kuwa Mungu alikuwa ndani ya Kristo, je , Kamera haumuoni Yuda anavyojihudhurisha? Hauwaoni hao mapacha, Yuda na Yesu kanisani? Kama walivyokuwa Kaini na Habili! Basi kujinyonga kwa Yuda kulikuwa ni kuondoka kwa Shetani katika mwili, kama alivyoondoka Kristo; Naye Kristo aliporudi katika Roho Mtakatifu, Shetani naye alirudi katika roho ya Mpinga Kristo! Kwahiyo hizo roho mbili zimo kanisani hata leo!!!

  Kuhusu wokovu, Maandiko yako hivyo hivyo unavyoyasoma. Nayo maelezo uliyoyatoa ni sahihi, “Kwa kifupi ukiamini ya kuwa Bwana Yesu alifufuka katika wafu, Mungu anakuhesabia haki.” Basi huku ndiko “KUOKOKA” na hatua hii hukubadilisha, maana unakuwa umetolewa katika ile njia ya kuzimu na kuwekwa katika njia iliyo bora zaidi, ukielekea uzimani. Pia kama ulivyosema, “Sasa ukishamkiri Yesu kama Bwana juu ya maisha yako basi utatii maagizo yake, ubatizo ukiwa agizo lake mojawapo tena la msingi sana”; basi dhihirisho la ukiri wako huambatana na Utii wa maagizo yake yote, ambayo hukuongoza katika ubatizo ili kukukamilisha huko kuokoka kwako, pale unapobatizwa kwa Jina lake Yesu Kristo ili upate ondoleo la dhambi kwa ajili ya kuendelea mbele katika hatua zinazofuata Mdo 2:38). Hatua ya pili ikiwa ni Utakaso, ambayo huziondoa tabia na mazoea yasiyoendana na Mungu. Hatua ya mwisho ni ubatizo wa Roho Mtakatifu, dhihirisho la kukamilishwa kwako, ukiingizwa katika Mwili wa Kristo kwa Ubatizo huo mmoja wanaoupitia wote walio huo Mwili; yaani, “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” Efe 4:5.

  Huo ndio Mwili wa Kristo, uko katika harmony na Neno lake. Lakini hamuwezi kuwa ndani ya mwili mmoja halafu mkatofautiana kwa kiasi unavyozishuhudia tofauti zetu, na bado sote tunakiri kuupitia Ubatizo wa Roho Mtakatifu! Ninaamini sisi ni wale waliookoka tu, kile kiwango walichokuwa mitume pamoja na Yuda akiwa kati yao, ndio maana kuna migongano mingi ya mawazo. Ninaamini kanisa likimpokea Roho Mtakatifu wa Kweli, LITAONGOKA, na Bwana atashuka ili ALINYAKUE kanisa lake utukufuni!! Labda nikuulize Kamera, Yesu akishuka leo hii, ni nani watakao nyakuliwa? Je, watakuwa ni Wasabato, au Wakatoliki, au Wapentekoste- wepi, TAG au EAGT, au Kanisa la Kristo, au Anglikana la mashoga, … nk??? Maana kuhusu jambo hilo Yesu anauliza, Luka 18:8 “…Nevertheless when the Son of man cometh, shall he find faith on earth?” Basi ndg yangu, tujihadhari na ukengeufu, ile APOSTACY, inazidi kujengeka!

  Ubarikiwe!

 10. Kamera……umenifungua macho kaka ila kwa mtazamo wako unaona alichokifanya Yuda ni dhambi au sio dhambi?wewe umeelewaje biblia biblia kuhusu hilo swala?

  shukrani

 11. Ndugu Ck Lwembe,

  Kwanza kabisa nashukuru ya kwamba umesisitiza tusimame katika Maandiko, ila nimesikitika kidogo ya kwamba baada ya kusema hivyo umebainisha kuwa huyaamini Maandiko yasemavyo, ngoja nikupe mfano mmoja, wewe umesema hivi:

  Hata wazo la kwamba Yuda alijuta, kwa kule kujaribu kurudisha vile vipande 30 vya fedha, latokana na kutokuiamini Biblia katika inachokuambia. Iwapo unawaza kuwa Yuda alikuwa na majuto, basi Kaini itakuwa ni zaidi, maana wote hao hawana ile Mbegu ya Mungu, ule Uzao, ndani yao (1Yoh 3:9). Kwa hiyo hawajui hata kutubu maana yake nini. Kama Yuda alikuwa na majuto, basi itakuwa ni juu ya ule mfuko aliokuwa akiubeba na kujichotea fedha kiwizi, kufikia mwisho kutokana Yesu kukamatwa! Na hilo linadhihirisha Maandiko, maana huyo alikuwa ni wa KUPOTEA, “son of perdition”, basi wewe kuwaza kuwa angetubu, inaonesha hujatulia!

  Mimi nasema hivi: Hayo madai yako ya kuwa Yuda hakujuta yanapingana na Maandiko moja kwa moja, soma Mathayo 27: 3 – 5:

  3 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.
  4 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.
  5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

  Je utayaamini Maandiko yasemavyo au utaendelea kubishana nayo?

  Pili, kwenye suala la kuokoka, hapo naona mwenzangu umechanganya kunde na maharage, Maandiko yako wazi kabisa kuwa Bwana Yesu alkamilisha kazi ya kutukomboa kwa kifo chake msalabani na ufufuo wake. Kabla ya hatua hiyo hakuna watu waliokuwa wameokoka, Ni kweli wengi walimwamini ili hiyo haikuwa imani iletayo wokovu, kumbuka wale Wayahudi waliomwamini (Yohana 8:30) ambao aliishia kuwaambia “ninyi ni wa baba yenu ibilisi? (Yohana 8:44) , Pia kumbuka hata wanafunzi wake alisema ya kuwa ana mengi ya kuwaambia ila hawataweza kuyastahimili ila akija Roho Mtakatifu ambaye atakaa ndani yao atawaongoza na kuwatia katika kweli yote (Yohana 16:12 – 15) kumbuka wakati huo Roho Mt. hakuwa ndani yao bado maana kazi ya wokovu wa mwanadamu haikuwa imekamilika. Kuwapa uwezo wa kutoa pepo na kuponya wagonjwa siyo ushahidi wa wokovu maana hizo ni karama, kumbuka hata punda alipewa alitumiwa kumhubiria nabii ila yule punda hakuwa ameokoka, na ndio maana Bwana Yesu alisema wengi watakuja siku ile wakisema tulifanya hili na lile kwa jina lako ila yeye atawaambia siwajui, somo hapo ni kwamba Mungu anaweza kumtumia yeyote (aliyeokoka au asiyeokoka) na chochote ili kukamilisha malengo yake na ndio maana aliwaambia wafurahi majina yao kuandikwa mbinguni (wokovu wa kweli ambao angewaletea baada ya muda si mrefu) na siyo pepo kuwatii..

  Tuendelee kuangalia maandiko yasemavyo kuhusu wokovu na kuhesabiwa haki.

  Warumi 10: 8 – 10:

  8 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.
  9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
  10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

  Hapo tunaona wazi kuwa tunahesabiwa haki kwa kuamini mioyoni ya kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu. Kwa kifupi ukiamini ya kuwa Bwana Yesu alifufuka katika wafu, Mungu anakuhesabia haki.

  Kingine ni wokovu, imebainishwa wazi kuwa wokovu unapatikana kwa kumkiri Bwana Yesu ya kuwa ni Bwana kwa kinywa chako, ukifanya hivyo unapata wokovu, Sasa ukishamkiri Yesu kama Bwana juu ya maisha yako basi utatii maagizo yake, ubatizo uikiwa agizo lake mojawapo tena la msingi sana.

  Nihitimishe kwa kusema hata leo hii, kama ilivyokuwa nyakati za Kanisa la mwanzo wapo watumishi wa kweli, walioitikia wito wa Mungu na wanamtumikia kwa uaminifu na wanaendelea kukua katika Neema ya Mungu na pia wapo wale watumishi wa mshahara wanaoangalia matumbo yao na kutanguliza maslahi yao binafsi, hilo halifichiki wala halipingiki ili maandiko yanasema Mungu anawajua walio wake na kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.

 12. Ndg Kamera,
  Kwamba una mtazamo tofauti na wengine, nadhani hilo ni kweli, lakini nadhani mtazamo wenye faida ni ule unaoelekezwa na Maandiko.

  Mambo ya Yuda, haitulazimu kuanza kuyakisia wakati Maandiko yameyafunua. Agano Jipya ni mambo ya kiroho zaidi kuliko kimwili. Kwahiyo Biblia inaposema Shetani, iwapo tutakaa katika mawazo ya kutegemea kumuona Shetani akikatiza mitaani, basi itatuchukua muda mrefu kuyaelewa Maandiko! Pia kudhania kwamba Yuda ndiye aliyemsababishia Yesu kuuawa, utakuwa umeikosa dhana nzima, maana Yuda yeye alifanya biashara tu juu ya jambo lililoamuliwa tayari, yeye aliwarahisishia shida waliyokuwa nayo, lakini maamuzi ya kumuua Yesu yalikwisha pitishwa huko kwenye vikao vya “Sinodi”.

  Hata wazo la kwamba Yuda alijuta, kwa kule kujaribu kurudisha vile vipande 30 vya fedha, latokana na kutokuiamini Biblia katika inachokuambia. Iwapo unawaza kuwa Yuda alikuwa na majuto, basi Kaini itakuwa ni zaidi, maana wote hao hawana ile Mbegu ya Mungu, ule Uzao, ndani yao (1Yoh 3:9). Kwa hiyo hawajui hata kutubu maana yake nini. Kama Yuda alikuwa na majuto, basi itakuwa ni juu ya ule mfuko aliokuwa akiubeba na kujichotea fedha kiwizi, kufikia mwisho kutokana Yesu kukamatwa! Na hilo linadhihirisha Maandiko, maana huyo alikuwa ni wa KUPOTEA, “son of perdition”, basi wewe kuwaza kuwa angetubu, inaonesha hujatulia!

  Katika suala la “KUOKOKA”, bado ni vizuri tuyafuate Maandiko kuliko kujitungia mambo yetu tunavyodhani sisi! Kuzaliwa mara ya pili na kuokoka ni vitu viwili tofauti. Unaweza kuwa umeokoka na ukawa hujazaliwa mara ya pili. Mafundisho yetu katika ujumla wake yameua kuzaliwa mara ya pili kwa kukubadilisha na kuokoka. Kulingana na Maandiko Kuokoka ni Kuhesabiwa Haki. Yaani pale unapoliamini Neno la Mungu. Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka”; basi huyo anayepita katika hatua hiyo ndiye aliyeokoka, hatua ambayo Yuda aliipitia ndio maana unamuona akiombea wagonjwa na kutoa mapepo na kuhubiri Injili! Sidhani kama mpagani anaweza kuyafanya hayo katika kiwango hicho. Yuda Iskariote, jina lake lilikuwa limeandikwa katika Kitabu cha Uzima, kwani Kristo aliwaambia, pale alipowatuma, wale 70, kwenda kuhubiri Habari Njema, waliporudi wakiyafurahia hayo, maana pepo wamewatii, ndipo akawaambia, Luka 10:20
  ”Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Huku ndiko KUOKOKA!!

  Basi unaweza ukayafanya hayo yote na zaidi na ukawa bado hujazaliwa mara ya pili, yaani ukawa HAUJAONGOKA! Wakati mwingine ni vigumu kuyakubali mambo hayo, kutokana na mapokeo yanayotushikilia. Lakini hebu turudi katika Maandiko ili tuitazame hali hiyo tupate uhakika zaidi. Luka 22:32 “Lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” Basi utasema kuwa Petro na mitume wote pamoja na Yuda, walikuwa hawajamwamini Yesu, huyo ambaye kwaye wameacha mambo yote na kumfuata? Injili itavurugika!!!

  Basi ndg Kamera mambo ndivyo yalivyo, unayaona? Wako akina Yuda kibao wanahudumu na vipawa kemkem, lakini watazame kwenye lile “fuko”, macho yao yote yako hapo, makanisa ni matajiri kuliko waumini wao, wanazifurahia baraka, wananunua magari ya kifahari, majumba ya kifahari at the expense of their kondoo, wanawanyonya mpaka damu, yaani wachungaji na mitume na manabii, wengi wao ni vampires!!

  Mbarikiwe!

 13. nashukuru wachangiaji wote mana hili swali najiuliza kila siku sipati jibu, nazidi kufwatilia kwa wachangiaji watakaofwata

 14. Mimi nina mtazamo tofauti kidogo na wengine kwenye masuala haya:

  1. Ilibidi Bwana Yesu asalitiwe na mmoja wa watu wa karibu sana naye ili mpango wa Mungu wa wokovu na maandiko yatimie (Zaburi 41:9), lakini Yuda kama mwanadamu mwenye utashi alikuwa na dhambi katika kufanya hivyo, ndio maana dhamira yake ikamshitaki akajuta, akajaribu kurudisha vile vipande 30 vya fedha na hata akaishia kujiua. Ninaamini kama angelitubu angesamehewa.

  2. Yuda alikuwa ni binadamu aliyetumiwa na shetani ili kumsaliti Bwana Yesu ila Yuda hakuwa shetani. Tukisema kuwa Yuda alikuwa shetani kwa sababu tu Bwana Yesu alisema “nimewachagua ninyi thenashara na mmoja wenu ni shetani” kama ushahidi wa ushetani wa Yuda, tutasemaje basi kuhusu Petro, maana Bwana Yesu alimwambia Petro “rudi nyuma yangu Shetani” (Mathayo 16:23), je Petro naye ni shetani? Hapo ndipo umuhimu wa kuligawanya Neno kwa usahihi unapojitokeza.

  3. Wokovu ulikamilishwa kwa kufa na kufufuka kwa Bwana Yesu. Hivyo basi hakuna mtu aliyekuwa ameokoka kabla ya Bwana Yesu kusulubiwa, kufa na kufufuka. Hivyo Yuda na mitume wote na wote waliomwamini hawakuwa wamezaliwa upya kwa Roho Mtakatifu. Waliokoka baada ya kufufuka kwake Bwana Yesu alipowavuvia na kuwaambia pokeeni Roho Mtakatifu. (Yohana 20: 22) na baadaye wakajazwa Roho Mtakatifu (Matendo 2) kama alivyowaambia katika Matendo 1:8.

  Mbarikiwe wapendwa.

 15. Katika Isaya 45:7 Mungu anatuambia, “Mimi naiumba nuru, na kuihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote” (I form the light, and create darkness; I make peace, and create evil); kwa hiyo twafahamu ya kwambaMungu ameviumba vyote kwa ajili ya utukufu wake.

  Sasa, Yuda, kwa kadiri tunavyozijua habari zake, alikuwa ni mkristo kama tulivyo sisi. Twafahamu kwamba alikuwa ni yule aliyeokoka, na alitumika katika kanisa kama ambavyo nasi twatumika leo hii. Aliihubiri Injili na kuombea wagonjwa na kukemea pepo kama manabii na mitume na wachungaji wetu wanavyoyatimiza hayo leo. Lakini pia twafahamu kuwa alikuwa ni shetani, “Je, mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani?” Yoh 6:70. Basi swali la kujiuliza ni je, shetani anaweza kutenda dhambi??

  Kwa hiyo kujua kuwa shetani anakuwamo kanisani, ni jambo la maarifa, kwa kazi gani? Luka 22:31 “…tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano”, hiyo ndiyo kazi aliyonayo Shetani kanisani!

  Pia, licha ya kwamba Yuda alikuwa ameokoka, lakini bado alikuwa ni mwizi, Yoh12:6 “ Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akivichukua vilivyotiwa humo.” Ni mara ngapi tunasikia wizi au udokozi wa sadaka makanisani mwetu? Katika kutokutosheka kwake na hivyo alivyokuwa akiviiba, tamaa ikamsogeza mbele zaidi na kumuingiza katika biashara ya usaliti, Mt 26:15 “… Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelethini vya fedha.”

  Basi, kama tunavyoyaona mambo ya Yuda, hatua za maisha yake ya wokovu ndio hizo, na mwisho tunaambiwa kuwa alipotea, Yoh 17:12 “…ila yule mwana wa upotevu..”!!!
  Kwahiyo, kwamba Yuda alitimiza mpango wa Mungu, hilo ni kweli kabisa, tena alizaliwa kwa kazi hiyo, ndio maana aliyatimiza Maandiko.

  Kuhusu Yuda kuwa na dhambi, kwa ufahamu nilionao kulingana na Maandiko, Yuda HANA dhambi kwa vile yeye mwenyewe ni DHAMBI!!!

  Mbarikiwe, nyoote!

 16. Bwana Yesu asifiwe…nitapeleka hili swali bible study kwetu nione wapendwa watasemaje…ila mimi ninavyofahamu ni kwamba kila kilichofanikisha Yesu kusulubiwa Mungu alijua kitatokea na angeweza kukizuia kama angetaka lakini hakuzuia sababu Yesu alijitolea kuja duniani kwa kazi hiyo…Mbarikiwe sana.

 17. Mungu alinena nitamtoa mwana kondoo(YESU) nae atateswa na kufa msalabani kwa ajiri ya watu wangu….Hivyo basi yuda alitumika kwa ajili ya kutimiza andiko na mpango wa Mungu….YUDA hana dhambi.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s