Neema ya Mungu inavyo okoa

ushuhuda

Bwana Yesu asifiwe wapendwa,

Napenda kuwashirikisha ushuhuda huu ambao dada mmoja aliutoa Kanisani leo Jumapili tarehe 9/9/2012 wakati akimshukuru Mungu kwa mtoto wake wa kiume kutimiza miaka mitano ya kuzaliwa.

Mama huyu alipata ujauzito wa mtoto huyu wakati akiwa katika maisha ya ukahaba na ulevi wa kutisha sana. Mama mkwe, yaani mama wa bwana aliyempa ujauzito alipofahamu ya kuwa dada huyu alikuwa na mimba ya kijana wake alimkabili na kumwambia alikuwa hataki kabisa kijana wake azae na yeye. Hakutaka kabisa awe na mjukuu ambaye mama yake anaishi maisha machafu na ya ulevi wa hali ya juu. Hivyo akamtaka aitoe ile mimba.

Dada huyu baada ya kuambiwa hivyo na mkwewe hakuona sababu ya kuendelea kutunza mimba isiyotakiwa na wenyewe, akakubaliana nafsini mwake kwenda kuitoa mimba ile. Lakini kabla hajaenda kuitoa, nafsini mwake ikazuka hoja ya pili. Akatafakari umri wake ulikuwa ni miaka 28, akawaza iwapo ataitoa ile mimba ni lini atakuja kuzaa? Au aishi bila mtoto maisha yake yote? Akaona hapana, hata kama mtoto huyo kwao hatakiwi, lakini yeye anamhitaji.

Hivyo akaitunza ile mimba na hatimaye akajifungua mtoto wa kiume.

Yule mtoto alipozaliwa akaanza kusumbuliwa na magonjwa yasiyoisha, ya mfululizo. Hata alipofika miezi tisa hali yake ilishakuwa mbaya sana, akiwa ni mdhaifu na aliyenyongea, hafanani hata kidogo na umri aliokuwa nao. Mama huyu akasimulia jinsi ambavyo alipokuwa akimnyonyesha mtoto wake anapaliwa, maziwa yanaingia njia ya hewa, hali mabayo inatengeneza nimonia na kumfanya awe katika hali kama ya kuelekea kupoteza uhai. Alipokuwa akifikishwa wodini mama huyu analia kwa kuomboleza katika hali ya kukata tamaa. Nimonia, malaria na magonjwa mengi mengine yakawa yameufanya mwili wa mtoto yule kuwa ndio nyumbani kwao.

Hali hii ilikuwa ikijirudia kwa namna nyingi mbalimbali, huku mama huyu akizunguka huku na huku kutafuta tiba, ikiwemo kwa waganga na kila hospitali ambayo aliimudu, hatimaye akagundua hakuna sehemu iliyobakia ya  kuweza kumsaidia. Ndipo alipoamua kumpeleka mtoto wake kwenye Kanisa linaloamini wokovu ili aombewe pengine angepata nafuu.

Siku ya kwanza alipompeleka mtoto huyu Kanisani alikwenda hali akiwa amekunywa pombe nyingi na kulewa. Mchungaji wa Kanisa lile alipomwona na kumsikiliza mara moja alitambua kuwa yule dada alikuwa katika ulevi mwingi. Hakufanya maombi kwa mtoto yule, bali alimshauri huyu dada siku akiamua kumleta tena mwanae ilio aombewe basi ahakikishe hanywi pombe kabisa siku hiyo. Aende kanisani pale bila kuwa amelewa. Yule dada akaondoka na mtoto wake.

Baada ye siku chache huku hali ya yule mtoto ikiendelea kuzorota, dada yule akampeleka tena pale Kanisani huku safari hii akiwa hajanywa pombe. Alipofika yule Mchungaji akampokea vizuri na kuanza kumwombea mtoto wake ili afunguliwe na kifungo kile cha magonjwa. Wakati maombi yakiendelea, mtoto yule wa miezi tisa alipiga ukelele mkali sana, huku akirusha haja ndogo kwa kasi. Baada ya muda alinyamaza, Mchungaji akamaliza maombi yake na kumruhusu yule mama kuondoka na mtoto wake.

Tangu siku hiyo hali ya mtoto ile ikaanza kuimarika. Yale magonjwa ambayo hayakuwahi kukoma tangu alipozaliwa yakakoma na kumwacha yule mtoto. Akaanza kupata afya na kukua kama watoto wengine wazima wanavyokuwa.

Dada huyu baada ya kuona mambo ambayo Bwana Yesu amemtendea mtoto wake akaamua kubadilika. Akaamua kuendelea kusali katika Kanisa lile ili awe karibu na Mchungaji aliyemwombea mtoto wake ili azidi kumwombea. Taratibu hali ya ulevi ikamtoka dada huyu kutokana na mafundisho aliyokuwa akipata pale Kanisani, na hatimaye akaamua kuokoka na kumpokea Yesu Kristo ili awe Bwana na Mwokozi wa maisha yake.

Tangu hapo hali ya maisha ya wokovu ya dada huyu imeimarika sana sana, na leo hii yapata mwaka wa nne katika wokovu, anamtumikia Mungu kwa namna ya pekee na ya kujitoa kwa hali ya juu sana kwa ajili ya kumtumikia Mungu, huku akiwa ni mwombaji mkubwa. Hamu yake kubwa ni kufika mbinguni baada ya maisha ya ushindi hapa duniani.

Hakika ushuhuda huu umenigusa sana. Inaonyesha ni jinsi gani kanisa la Mungu linapaswa kujiandaa kutoa majibu ambayo wanadamu hawawezi kuyapata mahali pengine popote, ili Bwana Yesu atukuzwe na ajulikane ndiye Mungu wa pekee wa kweli. Iwapo mama huyu asingepata majibu ya shida za mtoto wake asingebaki Kanisani pale na hatimaye kuokolewa. Ni dhahiri angerudi kuendelea kuhangaika wa waganga, na pengine maisha yangezidi kuharibika na kumpelekea kuangamia.

Hii ni mojawapo kati ya njia nyingi sana ambazo Bwana Yesu huzitumia ili kuwaokoa watu wengi, hasa wale walioshindikana kwa njia za mahubiri ya kawaida.

Ombi langu na ujumbe wangu kwa Kanisa la Mungu ni kuwa tuendelee kufanya juhudi kubwa kuutafuta uso wa Mungu.Kanisa liwe ni mahali pa makimbilio. Watu wote wafahamu ya kuwa hakuna uzima, usalama wala amani nje ya Kanisa la Mungu.

Wanapokimbilia kwetu watukute tupo tayari kuwapatia majibu, kuwahubiria, kuwafundisha na kuwaelekeza. Kanisa la Bwana litaongezeka, roho nyingi sana zitaokolewa, na wokovu wa watu hawa utajengwa katika misingi imara sana ya shuhuda za jinsi Mungu alivyowatoa katika hali mbaya, yaani wao wenyewe wanakuwa ni mashahidi wa nafsi zao ya kwamba Bwana Yesu anaishi milele, na anahusika moja kwa moja na maisha yao.

Bwana Yesu anatufundisha kupitia neno lake ya kuwa, mtu anayesamehewa sana hupenda sana, anayesamehewa kidogo, hupenda kidogo.

Tutafakari Adiko hili:

Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.

-Luka 7:41-47.

Mungu awabariki.

Rev. Deo Mbona

Advertisements

6 thoughts on “Neema ya Mungu inavyo okoa

 1. Kweli Mungu wetu ni mkuu sana na matendo yake ni ya ajabu mno anafanya mambo ya
  kushangaza mno.Njia zake hazichunguziki na mawazo yake ni mafumbo makubwa,anastahihili sifa na utukufu milele HALELUYA

 2. Huu ushuhuda nimeupenda sana ndugu yangu ubarikiwe kwa kazi yako nnzuri.GALATIA 6:9,Daniel 12:3-4

 3. Nimefurahi saana, kusikia kuwa huyo mwanamke alikuja na pombe zake kwa Yesu!
  Isaya 1:18 “ Haya njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Huyo mwanamke, ninaamini alipokea uponyaji katika siku ile ya kwanza aliyokuja kusemezana na Kristo. Kwamba Kristo alikuwa ndani ya mhudumu ni dhahiri. Basi yale maelekezo aliyoyatii huyo mwanamke, hapo waliposemezana, kurudi kwake kesho yake, ni udhihirisho wa Upendo wa Mungu uliojaa msamaha kwa wote wamwendeao, katika hali zao halisi, ilimradi wawe tayari kusikiliza kwa utii wanayoambiwa na kuyatekeleza hayo kwani ndio Uzima wenyewe, kama tunavyomuona huyo mwanamke na mwanaye; WAMEPONA WOTE!!!

  Bwana asema, “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.”
  Basi tusisite kumwitikia Bwana, maana yeye ametuita, twendeni na uchafu wetu yeye atatusafisha. Tusifanye mioyo migumu, si mmeuona huo Upanga unaoambatana na kiburi!!

  Mbarikiwe nyoote!

 4. Bwana Yesu asifiwe wapendwa hakika ushuhuda huu umenigusa nakuunga mkono kwamba ni kweli kabisa watu wanahitaji majibu, maana wasipopata majibu wataishia kwa waganga , watumishi tunahitaji kuutafuta uso wa Mungu ili atupe majibu maana ni yeye aliyesema Mungu akiwa upande wetu hakuna lililo juu yetu, akimaanisha magonjwa,umaskini, uchawi na uganga

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s