Je Mungu Amekunyamazia?

1

I sam 28:6 Lakini Sauli alipouliza kwa Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Napenda tujifunze kitu hapa, tunaamini kwamba Mungu wetu anasema, na kama tunaamini hivyo ndiyo maana tunamwomba, na tunapomwomba kwa vyovyote huwa tunatarajia, au tunategemea kupokea majibu toka kwake yeye tumwombaye, tumeona Mtumishi wa Mungu Sauli, alikuwa kwenye shida, na akaenda mbele za Mungu kumuomba amsaidie, lakini Biblia inasema Mungu akakaa kimya, nadhani wapo watu wengi wa aina hiyo siku zetu, na wengine hawajui ni kwa nini amekaa kimya, hawasemeshi, wanaomba, majibu hakuna, na wakati mwingine ndiyo mambo yanavyozidi kuharibika, mwisho wengine wanaamua kufanya kama vile Sauli alivyofanya, unajua alifanya nini? Mst 7 Ndipo Sauli akawaambia nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake, watumishi wake wakamwambia, tazama yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Baada ya kuona Mungu hamjibu, akageukia pepo. Ndugu yetu Sauli hakujuwa ni kwa nini alikuwa amekaa kimya, hakujua dawa ambayo angetumia, akaazimu aende akaaguliwe, yawezekana yupo mtu wa hivyo, umeteseka, umeombewa sehemu mbali, watumishi mbali wamekuwekea mikono, lakini tatizo liko pale pale, sasa ufanyeje? Usiende kwa waganga, napenda ufuatane na mimi nitakupatia baadhi ya sababu ambazo zaweza kusababisa Mungu akakaa kimya,

1. Dhambi katika maisha yako. Yoh 9.31 Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi, bali mtu akiwa ni mcha Mugu, na kufanya mapenzi yake, humsikia huyo. Tumeona jambo la kwanza kabisa ambalo laweza kumfanya Mungu akanyamaza ni dhambi, hatasikia, 1saya 59..1..3 Tazama mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia, lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia, kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu, midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu yenu zimenong’ona ubaya. Unaona hapo ametaja viungo kadhaa vinavyohusika na kitu kinachoitwa dhambi, ametaja Mikono, ulimi, mdomo. Kinachotakiwa ni mtu kuepuka dhambi ya aina yoyote, ndiyo Mtume Paul aliwaandikia Wathesalike hivi. IThes 5..23 Mungu wa Amani mwenyewe awatakase kabisa, Nafsi zenu, na roho zenu, na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe mwandamu kama mwanadamu, anazo nafsi tatu, mwili, Nafsi, na roho zote hizo zinatakiwa kushughulikiwa, kutakaswa, mara nyingi watu wameishia mwilini, maana dhambi nyingi zilizoorodheshwa ni za mwili, zile zinazoonekana kwa macho ya damu na nyama, pia aliwawambia Wakorintho vilevile. 2Kor 7..1. Basi wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa Mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu ktk kumcha Mungu. Kwa sababu mtu ana nafsi tatu, zote zinahitajika kuwa safi, kwa sababu hakuna dhambi kubwa wala ndogo Kumb 23..14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuatembea ktk kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako, kwa hiyo na kiwa kitakatifu kituo chako, asije akaona KITU kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha. Unaona kuwa Mungu wetu hakai kimya wakati maadui wanaposogelea, yeye anatembea, aje atuondolee maadui, tuwe tunamwita au hatumwiti, lakini kituo kinatakiwa kiwe safi, kama tulivyoona kuwa ni Mwili, Nafsi, na roho. Japo watu wengi tunasema Mungu hana shughuli na mwili, yeye anaangalia moyo tu, hapana na vyote, Mungu anapenda usafi, na hili limeachwa, ndugu zangu wakati mwingine unapata mgeni, anaingia ndani, viatu anaviacha nje, doh sebule yote inajaa harufu mbaya, na huwa nashangaa mwenye nayo huwa haisikii, mpaka watu mnatazamana, mpaka inafikia mahali mgeni mwingine akifike, inabidi umuwahi tu mlangoni, aa usivue viatu, ingia tu navyo, anadhani ni upendo, umemhurumia asisumbuke kuinama, kuvua, kumbe unaepusha jambo.

Ebu tuwe safi kama Biblia inavyotutaka kama tulivyoona kwamba Mungu anatembelea vituo vyetu, vinatakiwa kuwa safi, asije akaona kitu, mpaka chumbani, wengine nguo chafu zinawekwa uvunguni, na kisha unafunga madirisha, hakuna hewa, inalazimika hewa kuwa nzito, lazima utakoroma tu, mpaka unakosa raha. Ebr 12..1 Basi na sisi pia kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na DHAMBI ILE ituzingayo upesi, na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumeona kuwa Mungu akiona KITU anageuka na kutuacha, napo tumeona ipo le Dhambi inayotuzinga kwa upesi. Nimeeleza kuwa dhambi siyo lazima ziwe nyingi ndipo Mungu asitusikie, pia sio lazima vitu visivyofaa viwe vingi ndiyo Mungu ageuke na kutuacha, hata kama ni kimoja. Dawa ya dhambi ni kuitubia tu, wala siyo kuificha, au kujifanya haipo, kweli wanadamu hawaioni, lakini yeye Mungu anaiona, hakuna kitu tunachoweza kumficha, wanadamu tuta-over look, lakini siyo Mungu, dhambi zipo za aina mbalimbali. Siwezi kuziorodhesha dhambi zote, leo niiseme hii moja inayotesa wengi. Kumb 23..21..22 Utakapoweka Nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa, kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako,nayo hivi itakuwa DHAMBI kwako. Lakini ukizuia usiweke Nadhiri, haitakuwa dhambi kwako, yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya, kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, NI SADAKA YA HIARI ULIYOAHIDI KWA KINYWA CHAKO. Hii ni dhambi ambayo imetesa wengi, kumbuka, kinywa chako kimewahi kumwambia Mungu nini? Na hivi wengine ni watembeaji sana, wanafika kanisa hili wanaahidi, wanatamka, wanaondoka, wanasema, wanashangiliwa, wanajisikia vizuri, wanaishia hapo, wengi wamefanya hivyo, na bado kesho wataendelea kuahidi, mkoa hata mkoa, wilaya hata wilaya. Halafu kabla mtu huyu hajatimiza anaingia kufunga na kuomba, anamgoja Mungu aseme naye, ngoja nikukumbushe, Biblia inasema unapoenda kutoa sadaka, ukakumbuka kuwa na jambo na mtu usitoe, iache hapo mkapatane.

Sasa wewe unaingia na huku una neno na Mungu, ulimwambia utafanya kile na kile, kheri uache kwanza hayo maombi, upatanane naye, na kupatana naye ni kutimiza vile ulivyo muahidi. 2. Unaomba na huku jibu unalo tayari. Math 26..44 Akawaacha tena akaenda, akaomba mara tatu, akisema maneno yale yale.(yapi) ms 39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifuli fuli, akaomba akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Watu wengi wanaomba kulingana na vile wanataka, wanapangilia, wanasema Mungu nataka iwe hivi, nataka nioe huyu, nataka niolewe na huyu, anamalizia kusema Amen. Yaani iwe hivyo, Mungu anashangaa, hakupewa nafasi yoyote, ameshirikishwa jambo ambalo huyu ndugu analitaka, anamalizia najua wewe ni baba, ulisema baba hawezi kumpa mtoto nyoka, wala jiwe, mtu anabeba begi, anaondoka kwenye maombi, akisemda nimeomba Mungu, kumbe angesema nimemwamuru Mungu.

Tumemsikia Yesu Mwana wa Mungu akiomba, Biblia inasema akaenda akisema maneno yale yale, kwamba kikombe hiki kiniepuke, lakini si kama nitakavyo bali MAPENZI YAKO YATIMIZWE. Bila kuweka hilo, angemaliza tu kwamba kikombe hiki kiniepuke, Amen, abebe begi aelekee Kapernaum, na huku nyuma unajua kile ambacho kingetokea? Luka 22..43 Malaika kutoka Mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Wacha nikwambie, wapo watu waliomba wakiwa gethseman, na kwa kuwa hawakuruhusu mapenzi ya Mungu walibeba begi wakaenda kapernaum, Malaika alikuja Gethseman hakumkuta, ilibidi arudi na majibu, akaenda akasema nimekuta hayupo, ebu nikuonye ninachosema utanielewa vizuri kabisa. 1say 50..2 Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je mimi sina nguvu za kuponya? Unaona mpaka anashangaa watu wengine, alituma majibu yao Gethseman, akakuta hawapo, kwa kusema hivyo majibu ya wengi yanarudi. Naendelea kuzielezea baadhi ya sababu zinazo weza kumfanya Mungu akamnyamazia mtu.

3. KURUDIWA. Ebr 12..5…8. Tena mmesahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye, Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye HUMPIGA kila mwana amkubaliye.ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili, Mungu awatendea kama wana, maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Neno linaeleza vizuri, tunaelewa wote kuwa mzazi hafurahi mtoto wake anapofanya vitu ambavyo si vizuri, wakati mwingine atamwonya kwa maneno, wakati mwingine atamfinya, wakati mwingine atamtandika, wakristo wengi hawalijui, kila kinachowatokea kisicho kizuri, ni kukemea tu, leo nikusaidia, wakati mwingine ni kiboko cha Mungu, na wewe unakemea, atakaa kimya, dawa ni toba tu, wewe sikiliza shuhuda za watu wengi wanaposhuhudia, unasikia wanamlaumu sana shetani, ni sawa kwamba shetani ndiye analeta mabaya kwetu, lakini imekuwaje akuguse? Kwa nini ameruhusiwa akuguse?

Soma hapa 1Yoh 5.18. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatenda dhambi, bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA wala yule mwovu hamgusi. Unaona aliyezaliwa na Mungu akijilinda, mwovu wala hawezi kumgusa, na ukiona amemgusa mtu, basi ujue ameruhusiwa, Bwana akasema katika Yoh 15.5 Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu, nami ndani yake huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lolote. Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka, watu huyakusanya na kuyatupa motoni na kuteketea. Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Tunatakiwa kukaa ndani yake, naye ndani yetu, hii ni kusema kila unalofanya, cheki kwanza Neno linasemaje kuhusu hili ninalotaka kufanya? Vinginevyo, tutaamua uamuzi usio sawa na Neno, yeye atakaa kimya.

Kama tukiomba kitu kilicho nje ya Mapenzi ya Mungu (Neno) atakaa kimya, 1Yoh5..14 Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Tukimwendea Mungu kwa Neno lake, bila kuliongeza wala kulipunguza, hawezi kukaa kimya, lazima atatimiza, maana yeye hawezi kabisa kusema uongo, sasa kinachotakiwa ni kufanya bidii kulijua Neno, na utajua lipi? Kol 3..16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu ktk hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa Zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Tutaliwekaje Neno la Mungu mioyoni, ni kwa kulisoma, kulitafakari, kulipa nafasi, siku tulizo nazo Neno halipewi nafasi, nilialikwa mahali, tukakaa masaa 7 watu wakiimba, mwisho nikakaribishwa, mkaribishaji alisema, tunamkaribisha Mhubiri atuletee Neno la Mungu kifupi. Nimekamwambia, hilo silijui, hilo la kifupi. Alishtuka, alinishangaa kusema ati kifupi silijui, unajua wakati mwingi tumempatia Mungu mpaka, tukumbuke kuwa masaa ni yake, akitaka kuyatumia kukushughulikia ni yeye ndiye anajua, wakati tumekuwa na haraka mpaka tukaondoka hata kabla hajaja, na huwa tumetoka majumbani, na tunataka haraka haraka kurudi tena majumbani, zab 78..41 Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu, wakampa mpaka Mtakatifu wa Israel.

Unaona tatizo walilokuwa nalo Wana wa Israel, walimpa mpaka, walimpangia muda, miezi, miaka, yeye ni Mungu, sisi tunachotakiwa ni kumpatia nafasi, kuwa tayari, tusimlazimishe vile tunataka, akikutaka leo kubali, akikutaka mwezi ujao kubali, vinginevyo akikutaka leo, nawe upange siku unayotaka ngoja nikuonyeshe. Mith 1..24…28 Kwa kuwa nimeita nanyi mkakataa, nimeunyosha mkono wangu asiangalie mtu, bali mmebatilisha shauri langu, wala hamkutaka maonyo yangu,Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu nitadhihaki hofu yenu ifikapo, hofu yenu ifikapo kama tufani, na msiba wenu ufikapo kama kisuli suli, dhiki na taabu zitakapowafikia, ndipo watakaponiita. Lakini sitaitika, watanitafuta kwa bidii, wasinione. Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Bwana. Mungu amejieleza vizuri kwa mwanadamu, tatizo liko kwa mwanadamu, anadhani yeye aliyeumba muda eti haujali, ni yeye aliuumba, anaujali kabisa, utumie vizuri, ameeleza vizuri kabisa hapo juu kuwa kwa muda niliokutaka wewe hukupatikana, ulikuwa busy, na mimi sasa utakapo nitafuta kwa wakati unaotaka wewe, nami nitakuwa busy, wakati huo na shughuli zingine, nilikwambia uache shughuli zako uje, hukuwa tayari, na wakati wewe unanitafuta nitakuwa na shughuli zangu zingine, ndiyo maana wengine amenyamaza, wengine anacheka, wakati wewe unaita, una shida, umemaanisha yeye anacheka, tunatakiwa tufundishwe namna ya kutumia mida yetu, masaa, miezi, miaka, ni vizuri ufike mahali unajiuliza sasa mwaka imeisha nimefanya nini, naplan kufanya nini kwa ajili ya Bwana?. Muda ni tatizo kubwa kwa wanadamu.

Wakati umekuwa ni tatizo, kanisani unakuta mtu anaelewa vizuri saa ya Ibada kuanza, lakini hajali, anaingia imeanza, anatoka haijaisha, unaona jambo la kawaida, Ebr 12..16,17 Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadae kuurithi baraka, alikataliwa, (maana hakuona nafasi ya kutubu) ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi. Kumbe machozi nayo yapo yasiyo na maana, hata yangetoka bado tatizo liko pale pale, ebu tuwe tayari wakati Mungu anatuhitaji, tusimwambie kesho, Kut 8.8..10. Musa aliimuliza Farao kuwa alikuwa anataka amuombee lini ili vyura wakatoke katika nchi, wakae mtoni. Inasikitisha Faraoh akamwambia Musa KESHO. Ni kwa Faraoh aseme kesho, muombaji ni Musa (yupo) muombwaji ni Mungu(yupo). Watolewaji ni vyura (wapo) sasa kesho inatoka wapi? Leo kuna tatizo gani? Wapendwa wengi ni wa kesho, nawatakia kila la kheri mbarikiwe na Bwana. Amen.

Advertisements

3 thoughts on “Je Mungu Amekunyamazia?

  1. Ni nini maana ya kupungukiwa na uukufu wa Mungu? Ina maanisha kuwa hakuna kati yetu aliyemwamini na kumthamini Mungu jinsi tupasavyo. Hatujaridhishwa na ukuu wake wala kutembea kwa njia zake. Tumetafuta kutoshelezwa kwa vitu vingine na kuzithamanisha zaidi ya Mungu, ambayo ni kiini cha kuabudu sanamu (Warumi 1:21-23). Tangu dhambi ilipoingia ulimwenguni sote tumefanya upinzani mkuu dhidi ya Mungu kuwa hazina ambaye huturidhisha kwa yote (Waefeso 2:3). Hili ni kosa la kutisha kwa ukuu wa mungu (Yeremia 2:12-13).

  2. Wagalatia 4:4-7; 3:26 …Mungu alimtuma Mwanawe…ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu ali mtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Yohana 1:12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 1 Yohana 2:1 Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s