Umebarikiwa, Bariki wengine!!

barakaa

Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. – Luka 6:38 SUV

Hii ni ahadi mojawapo ya jinsi ya kupokea baraka za Mungu maishani mwetu. Moyo wa utoaji ni moyo wa upendo, moyo wa utoaji lengo lake ni kuwasaidia na kuwawezesha wengine. Moyo wa utoaji ni njia ambayo Mungu ameiweka ili kutubariki na kuweza kukutana na mahitaji yetu. Yeye mwenyewe ndiye Mtoaji Mkuu, alitupenda hata akamtoa Mwana wake wa pekee ili tuokolewe (Yohana 3:16) na si hivyo tu, ni yeye anayetupa moyo wa upendo na utoaji ili tuweze kupokea baraka zake.
Mungu anapokugusa moyo wako utoe ulichonacho kumbariki mwingine, si kwamba anataka upungukiwe, la hasha, bali anatafuta jinsi ya kukuongezea ili uweze kuendelea kufanyika kuwa baraka kwa wengi zaidi. Tukieelewa na kuamini ya kuwa Yeye aliye chanzo cha baraka zote yuko ndani mwetu hatutakuwa magudulia ya kuhifadhi baraka zake, bali tutakuwa mabomba ya kupitisha baraka za Mungu kwa wanaotuzunguka, maana tumebarikiwa ili tufanyike baraka.
Mzidi kubarikiwa,
Patrick
Advertisements

7 thoughts on “Umebarikiwa, Bariki wengine!!

 1. Shalom wapendwa,
  Somo la utoaji na mibaraka ndilo shetani analotumia kuvuruga kazi ya Mungu kwa sasa na nilichogundua mahubiri haya yameanza kukolea kasi miaka ya mwisho ya 90,mwanzoni 2000 mpaka sasa kwa hapa Tanzania.Sasa hivi waumini wengi wanaamini kadri unvyomtolea Mungu sana ndivyo Mungu atakujibu kwa haraka mahitaji yako,ni kutoa na kudai mibaraka,akili za watu zipo katika kusubiri kupokea.Yesu hakufa msalabani kwa ajili ya watu wapokee mibaraka kwanza,alikufa ili tusamehewe dhambi zetu kwa kumuamini yeye. na kuishi kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu katika maisha yetu.Suala la sadaka,zaka,dhabihu,sadaka ya Nabii isiwe ndio nguzo ya maisha ya wokovu na kuacha lengo la injili.Sadaka itolewe isitolwe injili itasonga.TUNAHITAJI KUFUNGA NA KUOMBA SANA NA TOBA MUNGU ATUSAIDIE KUUVUKA HUU MTEGO SHETANI ALIOLETA KANISANI AMBAPO KIKUBWA KINACHOHUBIRIWA NI MTOLEE MUNGU UBARIKIWE HAIJALISHI UNA DHAMBI LIASI GANI AU UNAENDAJE NA MAISHA YA UTAKATIFU AMBAYO MUNGU ANATUTAKA TUENENDE.Kubweteka na maombi ya mibaraka ndiko kulikofanya ulaya na USA injili kupoa watu walitoa na walibarikiwa kila kitu Sasa hawaoni haja ya kumuomba Mungu kwani wana kila kitu Makazi,pesa,kazi,biashara,teknolojia wanaona wahana jipya la kuomba na kanisani sasa hawaendi,Nilipokuwa Ulaya nilipokuwa nikisali waliniambia nasali kwa sababu nimetoka Afrika nina shida nilihitaji msaada wa Mungu wakaniambia nisihofu kwani ukweli Mungu hayupo NILIWAONA WANAKUFURU KWA SABABU YA MIBARAKA MIKUBWA MUNGU ALIYOWAJILIA.Sasa Ulaya Shetani kafanikiwa sasa kaingia Afrika.Tuvae silaha zote za Mungu tuweze kuzishinda hila za shetani Waefeso 6:11

 2. Wapendwa,

  Nyakati tulizonazo ni nyakati zilizojaa wapendwa wanaotaka sifa sana. Badala ya sifa kwenda kwa Mungu watu sasa wamegeuka kuwa wataka sifa, waabudiwa, waheshimiwa, waishio maisha ya anasa kwa kiwango cha kutisha.

  Ni kweli Maandiko yanatutaka tuwape watu vitu ili tuweze kubarikiwa. Na hii ndiyo injili mimi ninayoipenda sana katika Agano jipya zidi ya ile ya kusema TOA ZAKA ILI UBARIKIWE. Ukweli ni kwamba utoaji wa zaka ulimezwa na andiko hilo la Mark 6:38.

  Kama andiko hilo lingefundishwa vizuri hapengekuwa na haja ya watu kulazimishwa kutoa ZAKA kama sheria. Kuwapa watu (wenye uhitaji kama vile yatima, wajane, wakimbizi,mafukara na masikini kabisa) ndiyo ujumbe mkuu unaopaswa kuhubiriwa makanisa yote.

  Kumbuka Wachungaji hawakatazwi kufanya kazi zenye kuwaletea kipato na wala hawatajwi kama watu maskini katika jamii, hivyo kuwapa vitu ili ubarikiwe siyo lazima kama ilivyo kwa wale makundi yenye uhitaji sana kanisani au mtaani.

  Nakuhakikishia yafuatayo kama utatii andiko hilo la Mark 6:38 utaona yafuatayo:

  1. Kama utawapa yatima na wajane mavazi, Mungu atakupa mibaraka sana ya nguo. Hautapunhukiwa mavazi.

  2. Kama utawapa chakula wajane na yatima na maskini kabisa Mungu atajaza maghala yako ya chakula hata nafasi itakuwa ndogo kwako. Lile andiko lisemalo leteni zaka kamili hapa ndipo limemezwa kabisa.

  3. Kama utawapa wenye uhitaji fedha au misaada ya pesa wenye uhitaji hasa yatima, wajane maskini na wakimbizi Mungu naye atakubariki sana kifedha mpaka utashangaa sana.

  WAPENI WATU VITU NANYI MTAPEWA KIPIMO CHA KUJAA NA KUSHINDILIWA.

  Hata hivyo, epuka kuwapa watu vitu au pesa kisha ukaanza kutafuta kuonekana kwenye Televisheni, Redio au magazeti.

  Usiwape watu vitu na kuanza kujisifu mbele za watu au madhabahuni oooooh unajua yule jamaa ile nguo anayovaa munajua mimi ndo nimempa……, oooh unajua yule jamaa alikuwa maskini sana, mimi ndo nimemsaidiaa, ooh …… Ukifanya hivyo wewe ni sawa na Mpagani tu. wala hutapata thawabu yoyote hapa duniani walaa mbinguni.

  Unapaswa kutoa kwa watu tena hata mkono wako wa kushoto usijue kitu gani umetoa. Achana na utamaduni wa kutoa mbele za watu ili upate kupigiwa vigeregere na makofi. Utakuwa sawa na farisayo tu.

  Nenda nyumba ya mjane, yatima, vipofu, walemavu, peleka vitu au pesa kimya kimya wala usitake watu wakuone au waseme asante. Ikiwezekana tafuta mtu umtume akupelekee. Tafuta kiroba cha unga, nguo, maharage, pesa, sabuni, viatu, ndala, mashuka, mabati, simenti, sukari, matunda, nk mpe dereva wa taxi au bodaboda mwambie akupelekee mzigo huo kwa mtu unayetaka kumpatia vitu hivyo. Yaani ikiwezekana yule anayepelekewa msaada asijue hata aliyetoa ni nani.

  HAPO NDIPO UTABARIKIWA SANA KWA KIPIMO CHA KUJAA NA KUSHINDILIWA HATA GHALA ZAKO ZITAKUWA HAZITOSHI. AKAUNTI YAKO YA BENKI HAITAISHIWA PESA KAMWE.

  Hii ndiyo Injili ya Ufalme achana na Torati ya Musa iliyotaka watu walete Zaka ili wabarikiwe.

 3. Ndugu yangu Lazarus,

  Hao wanaojinufaisha kwa kuwakamua kondoo ndio waleee “wachungaji wa mshahara” ambao Bwana Yesu alisema ndio wezi wenyewe hao (Yohana 10), uchungaji kwao siyo huduma bali ni kazi, wanachunga kwa ajili ya ujira, ndio maana wanadiriki hata kupindisha na kupotosha maandiko ili mradi tu wajinufaishe wenyewe.

  Inabidi watu wafundishwe Injili ya kweli, Injili ya Yesu Kristo na siyo hiyo injili potofu inayowafanya watu wafikirie na kuamini kuwa Mungu hatawabariki wasipotoa hizo elfu elfu wanazoambiwa na mhubiri. Neno la Mungu limejaa ahadi za Mungu kukutana na mahitaji yetu na kujibu maombi yetu sisi watoto wake tukimwomba kwa jina la Yesu kama ambavyo Bwana Yesu alituambia na kutuhakikishia mara kadhaa. ( Mathayo 7:7, Marko 11:24, Yohana 14:13 – 14, Waefeso 1:3, Wafilipi 4:19, 1 Petro 5:7)

  Hatupokei baraka kwa kuwa eti tumetoa au tumetozwa kiasi fulani cha pesa, hapana, tunapokea kwa sababu ya kile Bwana Yesu alichokifanya pale msalabani kwa ajili yetu, kutupatanisha na Mungu na sisi kufanyika kuwa wenye Haki mbele zake na kuwa watoto wa Mungu; kama wenye haki wa Mungu tunaishi kwa imani, tumeingia katika pumziko lake. .

  Tunapokea kwa misingi ya uhusiano wetu na Mungu na huo uhusiano wetu na yeye ni wa Baba na mwana, na hilo limewezekana kwa sababu ya Bwana Yesu tu na si vinginevyo. Sisi ni wana wa Mungu, tusikubali kuyumbishwa na mafundisho yanayojaribu kuitweza kazi kamilifu ya Bwana Yesu ya kutupatanisha na Mungu.

  Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? – Warumi 8:32.

  Uzidi kubarikiwa na Bwana Yesu,

  Patrick

 4. PATRICK,
  kwa upande wa “Kondoo” nimeelewa. Vipi Wachungaji ambao, hujinufaisha kupitia matoleo huwakamua bila huruma Kondoo waliopewa kuwachunga, wanawafyonza hadi Damu! Wakati wao wanazidi kula kuku na kubadili gari kama mashati,hawana mipango kwa Wajane,Yatima,Masikini wala Wazee”Utasikia toa ndg sadaka nzuri, usitoe miatano tano, toeni kuanzia alfu ubarikiwe, ukitoa laki nitakuombea maombi ya Milioni!” Hawa, siyo wezi? Maana ukiacha Wanasiasa wanaofuata kwa kuishi kwa anasa ni Wachungaji!
  Lazarus

 5. Tukiliangalia Neno kwa ujumla wake tunaona kwamba uvivu na/au uzururaji vinapingwa, hivyo yeyote atakayejaribu kukwepa kufanya kazi na kutaka kupewa huyo hastahili kupewa chochote maana huyo si mhitaji wa kweli bali anachojaribu kufanya ni kuiba na hiyo ni mojawapo ya kazi za yule mwovu.

  Tukumbuke ya kuwa Neno la Mungu pia linasema, “asiyefanya kazi na asile” – 2 Wathesalonike 3:10 – 13 inasema hivi:

  10 Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. 11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.
  12 Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. 13 Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.

  Neno pia linatuagiza kuacha kuiba na kufanya kazi kwa mikono yetu ili tuweze kupata cha kumgawia mhitaji, Waefeso 4:28 inasema hivi:

  28 Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.

  Mbarikiwe na Bwana Yesu,

  Patrick

 6. TUWAPEJE WATU VITU? FAFANUA MTUMISHI. WATU WENGINE WANAITUMIA HIYO ILI WAPATE BILA KUFANYA KAZI, HILI LA UTOAJI SHETANI AMEWEKA KITI CHAKE, WOTE MTOAJI NA MPEWAJI WAMEKUWA WATEJA WA SHETANI KWA KIWANGO KIKUBWA, je tatizo ni nini? FUNZO LA UTOAJI LINAFUNDISHWA IPASAVYO HUKO MAKANISANI?

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s