Je mbinguni kuna viti vya enzi au kiti cha enzi?

maandiko

Swali tata ambalo bado halijafanyiwa kazi vizuri na pia kuonekana kuwa sio la muhimu sana kulijadili ni juu ya Kiti cha Enzi cha Mungu huko Mbinguni. Lakini pamoja na kuonekana sio la muhimu wapo wengi ambao bado wanatatizwa na swala hili. Maana wanaposoma Biblia wanaona neno hili kisha nikaona Kiti cha enzi – na Yeye aketiye juu yake. Hawaoni neno hili kisha tukaona viti vya enzi mbinguni – vikionyesha Utatu Mtakatifu. Jambo hili nimeshuhudia likiwachanganya wachungaji, wazee wa kanisa na waumini wakubwa kwa wadogo. Misimamo niliyowahi kuishuhudia ni hii: Kiti ni kimoja maana Mungu ni mmoja anatenda kazi katika nafsi tatu. Wengine wakasema Mungu ni mmoja katika nafsi tatu halisi lakini aliyena kiti cha enzi ni Baba pekee yake. Kiti cha enzi ni kimoja tu. Wengine wamechanganyikiwa zaidi na hata kuwa na imani ya kuwa kuna uwili mbinguni (Binitirianism) – hakuna Utatu. Maana wanaposoma Biblia hasa 1 WAKORINTHO 8:6 wanaona Paulo anateta na wapagani juu Nafsi mbili tu.

Somo hili linahitaji kueleza kwa ufupi juu ya kile ambacho Biblia na Roho ya unabii inavyosema na pia wanatheolojia wengine wanachoelewa juu yake.

Zaburi 11:4; 47:8 – inataja Kiti cha enzi huko mbinguni. Wengi wanaposoma fungu hili wanachanganyikiwa kuwa huenda kiti cha enzi ni kimoja tu.

Daniel 7:9, 10 – Lakini Daniel inaeleza juu ya viti vya enzi vilivyoonekana mbinguni wakati wa hukumu. Na pia anamuona Yesu na Baba wote wakiwa wameketi wanaendesha hukumu.

AINA YA VITI VYA ENZI NA KAZI ZAKE.

Katika falme mbalimbali hapa duniani walikuwa wanatumia viti vya enzi kama sehemu ya kutolea haki au hukumu. Zamani mahakama na kiti cha enzi au kifalme vilikuwa vimeungana pamoja katika utendaji wa kazi. Hukumu na Haki za raia zilikuwa zinaamuliwa na mfalme.

Kadhalika hata mbinguni tunaonyeshwa kazi kuu mbili za kiti cha enzi. Zaburi 89: 14. 1. Kutoa Haki. 2. Kutoa Hukumu. Daudi anamuona Mungu akiwa katika kiti chake cha Enzi akifanya maamuzi kwa ajili ya Haki na Hukumu. Huu ndio msingi mkuu wa kiti cha enzi.

Kupitia kazi ya kiti cha enzi hapo ndipo unaona Utatu Mtakatifu ukiwa na majukumu ya kuketi katika Kiti cha enzi. Neno linalotumika hapa ni Kiti cha Enzi linawakilisha hadhi, sifa, utukufu, ukubwa wa aina moja wa Kiti hiki katika ofisi ya Mungu. Kiti cha enzi maana yake kinapotajwa kinaonyesha neno moja kuwa kinakaliwa tu na MUNGU MMOJA! Kiti anachokalia Mwana, au Baba, au Roho vyote ni sawa kwa sifa zote. Hakuna ambacho ni kikuu zaidi ya mwingine.

Kwanini nasema haya? Kwa sababu msingi wa kiti cha enzi ni kutoa Haki na Hukumu. Swali je Mwana ataendesha hukumu? Atatoa Haki? Je Roho ataendesha Hukumu? Atatoa Haki? Baba ataendesha hukumu? Atatoa Haki? JAWABU lisilo na mashaka WOTE WATAENDESHA HUKUMU NA KUTOA HAKI!

Hebu tuangalie mafungu yanayothibitisha maneno haya: 1 YOHANA 5:8, 9. Wote watatoa Ushuhuda siku ya Mwisho.

Yesu ameketi katika kiti cha Rehema (HAKI). WAEBRANIA 4:16 (WARUMI 8:33,34).  Pia kumbuka kuwa Baba ni mwingi wa Rehema (KUTOKA 34:6, 7); na pia Roho Mtakatifu anatuonea rehema. (WARUMI 8:26). Kiti cha rehema maana yake ni sawa na upatanisho, maombezi. Biblia inataja kazi za Roho Mtakatifu ni pamoja na kutoa Haki, Hukumu, kutuonya juu ya dhambi. YOHANA 16: 7 – 11.

Soma pia kitabu cha Early Writings, Mama White anasema wakati wa hukumu Baba atamuuliza Yesu juu ya Jina langu akisema Damu! Damu! Basi jina langu linapita akinyamaza ni hukumu ya moto. UFUNUO 20:11- 12 – Yohana anamuona Yesu ameketi katika kiti cheupe kikubwa cha enzi kwa Hukumu. Pia Daniel 7 Baba naye aliketi katika kiti hicho. Hata na Roho Mtakatifu anashuhudia tena ushuhuda wake ni kamili. YOHANA 5: 19 – 24; WAEFESO 4: 30; WAEBRANIA 10: 29 -31.

Yohana anaona katika njozi matukio ya hukumu yakianzia katika UFUNUO 12 na 20. Anaona katika UFUNUO 20:1-3 yakianzia duniani, hatimaye fungu 4 – 6 yanahamia mbinguni; mwishowe yanarudi tena duniani katika fungu la 7 – 11 ambapo viti vya enzi vya Shetani na yule Mnyama vinateketezwa kwa moto kisha Kiti cha enzi cha Mungu kinabaki kutawala Milele. Hili linaamaanisha kuwa maana ya Kiti cha enzi kwa tafsiri rahisi kupita yote ni UTAWALA WA MUNGU. Kwamba ni viti vya namna gani hilo sio muhimu kwa sasa bali la muhimu ni kuwa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu watatawala Milele. Soma DANIELI 7:22, 27; ZEKARIA 14:9; RUMI 14:10; UFUNUO 5:13; WAEFESO 1: 13 – 14.

MANDHARI YA MBINGUNI KAMA ILIVYOONEKANA.

Matendo ya Mitume 7: 49; Isaya 66:1 – Biblia inasema kuwa mbingu yote ni Kiti cha enzi cha Mungu. Kwa tangazo hili ni kuwa mbingu ni makazi ya Mungu. Hivyo jibu rahisi kwa walio na mashaka kuwa je mbinguni kuna viti vya enzi vitatu, jawabu ni NDIO! Maana mbingu yote ni makao ya Utatu Mtakatifu. Viti hivi vitazidi utukufu wa viti vingine vya enzi vya viumbe wengine wa mbinguni. Soma hili katika UFUNUO 11:16. Biblia inataja neno viti vya enzi mara 47 bila kutaja kiti cha Shetani na cha yule mnyama.

MATHAYO 19:28 – Yesu anasema kuwa viti vya enzi vitazidiana utukufu. Kuna ambavyo vitakaliwa na Utatu Mtakatifu; na pia vitakavyokaliwa na viumbe wakiwamo wanadamu wakati wa hukumu. WAEBRANIA 1:8; 9:14 – Kiti chake ni cha Milele!

UFUNUO 3:21 – Yohana anaona viti vya enzi vya Baba na Mwana. Kiingereza kinatenganisha katika nafsi kama ilivyo katika mamlaka ya ubatizo kwa kila nafsi! {Baptizing them in the name of the Father and of the Son and of the Holy Spirit. This is not: Baptizing them in the name of the Father and the son and the Holy Spirit or the Father, the Son, and the Holy Spirit.}

WAEBRANIA 1:3 – Paulo anaomuona Yesu alipopaa juu aliketi kando ya Mungu Baba.

UFUNUO 22:1, 3 – Yohana anaona Mbinguni na pia ndani ya Jiji jipya la Yerusalem mpya viti vya enzi vya Baba na Mwana.

Lakini unaweza ukahoji mbona Biblia inataja viti viwili tu; Roho Mtakatifu hatajwi. Lipo fungu moja ambalo linaweza kukubali Nafsi ya Tatu ya Mungu kuwa na Kiti cha Enzi. Soma ISAYA 6:3 – Mtakatifu! Mtakatifu! Mtakatifu! Inawakilisha Utatu Mtakatifu ambao Isaya anaona kuwa imekuwa kosa kwake kushuhudia utakufu wao. Kumbuka Biblia inasema Wako Watatu washuhudiao Mbinguni. ( 1 YOHANA 5:7-8.) Mwandishi mmoja aliyeandika nyongeza ya Biblia Zondervan NIV Study Bible [NIV: New International Version] anasema hivi:

“Mtakatifu! Mtakatifu! Mtakatifu! Angalia Walawi 11:44 na zingatia Ufun. 4:8. Kurudiwa mara tatu inasisitiza Utakatifu wa Mungu usiona ukomo (the triple repetition underscores  God’s infinite). Zingatia kurudiwa mara tatu kulikotumika kwa hekalu la BWANA katika Yer. 7:4 inasisitiza uhakika wa watu juu ya ulinzi [Usalama] wa Yerusalemu kwa sababu ya uwepo wa lile hekalu. BWANA MWENYEZI.” [1]

Jambo hili linaporudiwa mara tatu  pia ni utambulisho wa Nafsi tatu za Uungu.

“Mtakatifu! Mtakatifu! Mtakatifu! Kwanini itamkwe mara tatu? Ni utambuaji wa “Bwana wa Majeshi” hili lijumuisha kwamba ni Yesu kabla ya kufanyika Mwili. Yeye atakayekuja na Amekuja. Hata hivyo neno Mtakatifu kurudiwa mara tatu vile vile linafafanua tabia za Mungu Mmoja aliyedhihirishwa (funuliwa) kama Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.”[2]

Paulo katika WAEFESO 1: 13 -14 anathibitisha kuwa Roho Mtakatifu atamiliki katika miliki Yake. Huwezi ukawa mtawala asiye na miliki, na ukiwa na miliki maana yake lazima uwe na Ikulu yenye kiti cha enzi. Hivyo Roho Mtakatifu atamiliki kwa sababu anacho kiti chake cha enzi – kama mtawala wa malimwengu yote. Ikiwa ana kitu sharti akikalie maana ni Mtawala.

Naamini kwa maelezo haya machache yanahitimisha kuwa Utatu Mtakatifu utaketi katika Kiti cha Enzi maana ni kiti cha Mungu. Jina la Mungu ni jina la Ofisi yao wote. Nakumbuka Mchungaji John Kisaka aliwahi kutoa Gazeti la Maranatha lilofafanua maana ya Mungu mmoja maana yake nini. Na kwanini hatuna miungu watatu bali Mmoja katika Nafsi Tatu. Pr. Kisaka alitoa mfano juu ya ofisi ya Rais. Rais ni jina la Mtawala. Ni ofisi ambayo inachukuliwa na mtu mmoja yeyote mwenye sifa za kuwa Rais. Lakini Rais siyo jina la mtu fulani tu bali ni la mtu yeyote aliye na sifa za kuwa rais wan chi. Mfano Rais Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa, na sasa Rais Kikwete. Wote hawa wanamamlaka sawa wanapokuwa katika ofisi hiyo. Ila siyo jina la Mkapa au Kikwete. Mungu ni Mmoja ambaye katika ofisi hiyo kuna nafsi Tatu ambazo zinamamlaka sawa. Mwana, Baba, na Roho ni ofisi ya Mungu. Wana hadhi ya Mungu. Hatuna Miungu wengi – la. Au hatuna Marais wengi bali Rais ni mmoja katika wanne waliongoza nchi hii. Siyo mwenye haki ya kuitwa rais ni mmoja tu la bali wote wamepitia hadhi hiyo. Huo ni mfano katika lugha ya kibinadamu ili kufafanua kidogo.

 By Pr. F. Mwanga

4 thoughts on “Je mbinguni kuna viti vya enzi au kiti cha enzi?

 1. Mungu ni Roho (Yoh 4:24), sasa Kristo huyo Bwana, yeye hakuwa Roho bali mwili wa nyama, isipokuwa huyo Mungu, ambaye ni Roho, ndiye aliyekuwa ndani ya ule mwili uitwao Yesu; 2Kor 5:19 “…yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake” umeelewa ndg Elvis? Nafsi mbili zinafanya miungu wawili, au lugha imepoteza maana! Uungu wa Yesu Kristo unatokana na Mungu kuwa ndani ya ule mwili. kwa hiyo unapomsikia Yesu akimzungumzia Baba yake, jua hivyo kwamba yu ndani yake!!!

 2. Swali tata ambalo bado halijafanyiwa kazi vizuri na pia kuonekana kuwa sio la muhimu sana kulijadili ni juu ya Kiti cha Enzi cha Mungu huko Mbinguni. Lakini pamoja na kuonekana sio la muhimu wapo wengi ambao bado wanatatizwa na swala hili. Maana wanaposoma Biblia wanaona neno hili kisha nikaona Kiti cha enzi – na Yeye aketiye juu yake. Hawaoni neno hili kisha tukaona viti vya enzi mbinguni – vikionyesha Utatu Mtakatifu. Jambo hili nimeshuhudia likiwachanganya wachungaji, wazee wa kanisa na waumini wakubwa kwa wadogo. Misimamo niliyowahi kuishuhudia ni hii: Kiti ni kimoja maana Mungu ni mmoja anatenda kazi katika nafsi tatu. Wengine wakasema Mungu ni mmoja katika nafsi tatu halisi lakini aliyena kiti cha enzi ni Baba pekee yake. Kiti cha enzi ni kimoja tu. Wengine wamechanganyikiwa zaidi na hata kuwa na imani ya kuwa kuna uwili mbinguni (Binitirianism) – hakuna Utatu. Maana wanaposoma Biblia hasa 1 WAKORINTHO 8:6 wanaona Paulo anateta na wapagani juu Nafsi mbili tu.

 3. Mwisho wa mambo ukifika tutajua yote!
  Kulihangaikia sana hili ni sawa na kuhamgaikia swali la Mungu alitokea wapi.

  Kujua viko vitatu, viwili,kimoja haitabadilisha chochote.

  Nafikiri katika mijadala fulani iliyopita tulisema sana kuwa suala la utatu halionekani kwenye maandiko matakatifu, bali ni mawazo tu ya watu kama yalivyokuwa mawazo ya Petro ya kutaka kujenga vibanda vitatu kana kwamba alikuwa ameambiwa Musa na Eliya wanarudi kuishi duiani tena.

 4. Pr. Mwanga,
  Mfano ulioutoa wa hao marais watatu ambao wawili walikwisha maliza term zao, sioni ni kwa jinsi gani mamlaka zao zitakuwa sawa na rais aliye madarakani! Huo mfano haujitoshelezi wala hauendani na suala hilo la Utatu.

  Mfano halisi wa UTATU MTAKATIFU ni huu:
  Jakaya M. Kikwete ni :
  1. Rais wa Tanzania
  2. Amirijeshi wa jeshi la Wananchi wa Tanzania
  3. Mwenyekiti wa CCM Taifa
  Sasa hawa si watu watatu tofauti bali ni mtu mmoja tu anayehudumu nafasi tatu!

  Suala la UTATU si la Kibiblia, kama unalo Andiko linalosema Mungu ni UTATU, tuletee hilo kuliko hii michezo ya kuigiza ya kina “Mama White” eti: “Mama White anasema wakati wa hukumu Baba atamuuliza Yesu juu ya Jina langu akisema Damu! Damu! Basi jina langu linapita akinyamaza ni hukumu ya moto. “; huu ni UPAGANI kama wa “Maria mama wa Mungu utuombee”!!!

  Kiti cha Enzi kiko kimoja tu, na ukiona pameandikwa viti basi jua hao wanaovikalia ni Kanisa kwa ajili ya kuhukumu!

  Asante, jitahidi kuja na Kweli ya Maandiko na si hadithi za “Damu! Damu!” na kuwafanya watu wapatwe na majinamizi!!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s