Habari njema za Wokovu

habarinjema

Ni mapenzi ya Mungu watu wote waokolewe maana yeye hapendi hata mmoja apotee. Ndio maana tumeagizwa kuihubiri Injili kwa kila kiumbe, kila mtu anayo haki ya kuisikia Injili. Wokovu ni nini na unapatikanaje? 

Hatua ya kwanza ni kukubaliana na Neno la Mungu lisemavyo: kila mmoja ametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu – Warumi 3:23

Pili, Neno linatueleza wazi kuwa mshahara wa dhambi ni mauti bali karama ya Mungu (wokovu) ni uzima wa milele katika Kristo Yesu – Warumi 6:23

Tatu, Mungu ni Upendo na hapendi watu waangamie katika dhambi zao hivyo alimtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo aje na kufa kifo cha mateso na aibu kwa ajili ya dhambi zetu msalabani, ili tuweze kupatanishwa na Mungu. Neno linatuambia kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata kamtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele – Yohana 3:16

Nne, kuna njia moja tu ya kwenda kwa Mungu, nayo ni kupitia kwa Bwana Yesu peke yake. “Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia Kwangu. – Yohana 14: 6
Neno la Mungu linasisitiza ukweli huu kwa maneno haya: Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna Jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. – Matendo 4:12

Sasa basi ukishafahamu ukweli huu unao wajibu wa kuukubali au kuukataa, Mungu ni mwingi wa neema, rehema na upendo ila hamlazimishi mtu yeyote kufanya chochote kile, ila kwa upendo wake anakusihi umgeukie yeye leo upokee wokovu wake, uwe na uhakika wa uzima wa milele tangu sasa na uishi maisha ya amani kuanzia sasa.

Je wokovu unapatikanaje? Mgeukie Mungu leo ukitambua na kukiri kuwa wewe ni mwenye dhambi na huwezi kujiokoa, kisha uamini alichokifanya Bwana Yesu ili kukuokoa, mkaribishe maishani mwako kwa imani, pokea wokovu wake kisha tafuta jamii ya waaminio uanze kushirikiana nao ili uendelee kukua kiroho.

Lakini andiko lasemaje ? ‘‘Lile neno li karibu nawe, li kinywani mwako na moyoni mwako,’’ yaani, ni ile neno la imani tunalolihubiri. Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba ‘‘Yesu ni Bwana.’’ na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu – Warumi 10: 8 – 10

Mungu awabariki. Amen!

Patrick
Advertisements

2 thoughts on “Habari njema za Wokovu

 1. Nimesumbuliwa kidogo na maswali ya Ilpyanda. Halafu nikagundua kwamba hapakuwa na majibu toka kwa Patrick, nafikiri kanuni aliyoisema Patrick hata kwenye huo ujumbe ni uhuru wa mtu kuchagua kuamini Neno la Kristo au kulikataa. Ndiyo maana hakujibu hayo maswali ya Ilpyanda.

  Lakini pia, maswali ya Ilpyanda ni maswali ya mtu asiyekubaliana na barua za Mtume Paulo. Lakini, tunaweza kuthibitisha kirahisi tu kwamba Paulo ni Mtume wa Bwana Yesu na kwamba barua zake zote zimevuviwa. Hata kama tungezitoa baruanza Paulo kwenye biblia (tutakuwa tumeondoa na nyaraka za Petro, na za Yohana, na Kitabu cha Ufunuo, na kitabu cha Matendo ya Mitume) tutabaki na zile Injili nne na nyaraka za Yakobo na Yuda. hata tukifanya hivyo, tutaona tu Habari njema ya ufalme ikihubiriwa, ambayo humwelekea Bwana Yesu kama ndiyo mwanzo na mwisho, kwamba ndiye njia pekee ya kumfikia Mungu, wakati wowote.

  Kama alivyonukuu Patrick, Yohana suta ya tatu yote, Yesu anaongelea jambo moja tu, la Baba kumpa yeye mamlaka ya kuwaokoa wanadamu toka katika dhambi zao.

  Hebu tuondoe injili kwenye biblia, tubakie baai na vitabu vya Agano la kale pekee, Isaya nabii ameandika habari za kuzaliwa mwana, ambaye jina lake ataitwa Immanuel, yaani Mungu pamoja nasi, na utawala wake utakuwa wa kudumu, wa milele, hautaisha, ataitwa mshauri wanajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa ajabu… Na kwamba angezaliwa na bikira.

  Pia Isaya anaandika kwamba, huyu mwana atachubuliwa, atakataliwa, atadharauliwa, atabeba hudhuni zetu, na adhabu ya amani yetu pia, Mungu atafurahia kule kuchubuliwa kwake, na kwamba atakapofanya nafsi yake kuwa toleo la dhambi, Mungu ataikubali, maana hiyo itakuwa ni kwaajili ya kuwahesabia haki wengi, kwakuwa ataubeba uovu wao wote.

  Basi tusipokubaliana na Nabii Isaya, tuondoe pia kitu cha Isaya toka kwenye biblia, turudi kwenye zaburi kadha wa kadha, tuziondoe pia kwenye biblia, turudi kwa Musa, tuondoe vitabu vyake kwenye biblia, maana vyote vinamwongelea Bwana Yesu, na kazi atakayokuja kuifanya kwaajili ya dhambi.

  Nadhani tukiishafanya hivyo tutaishia kulikana Neno la Mungu, na kumfanya Mungu kuwa mwongo. Maana yeye ndiye aliyenena kwa vinywa vya manavii, na ndiye aliyemchagua mwalimu wa namna ya ajabu kabisa Paulo, hata Petro alimkubali kwenye waraka wake.

  Kama tunakubaliana na Neno, kwamba limevuviwa, basi tukubaliane nalo lote; tusichague lile linalokubaliana na mitazamo yetu, tuache Neno la Mungu liseme lisemacho. Na kama tunakataa, tumfanye Mungu kuwa mwongo, na maanaake, Kristo alikufa bure, tungali katika dhambi zetu.

  Kaka Patrick, umenena vema katika waraka wako, mimi nakubaliana nao wote, mtu akitaka kuokoka (ambako ndiko kuzaliwa na Mungu, au kuzaliwa katika Roho) na amkiri Yesu ya kuwa ni Bwana, na ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu.

 2. Mr. Patrick!
  Habari njema ya wokovu unaodhihirisha anza, kwa kusoma ujumbe ufuatao kisha ujibu hoja zangu:
  MITHALI 30:5-6 ” Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.
  6 Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo. ”

  YEREMIA 23:14-16 ”Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.
  15 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.
  16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana. ”

  1-JE, aya hizo unazikubali?

  2-Kila neno la mungu limehakikishwa. Sasa hili isionekane kuwa uongo ni aya gani kwenye biblia au kitabu chochote mungu anamtuma YESU ili aje afe kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu?

  3-WARUMI 10:8-10 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.
  9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
  10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
  a)- Hili neno ni la mungu?
  b)- Kama ni la mungu, kitabu gani Paulo amenukuu ,hili isionekane Paulo kuwa mmoja wa wale manabii wa Yerusalemu, ambao mungu anawatambua kwa kunena maono ya mioyo yao wenyewe?
  c)- MATAYO 7:21 ”Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. ” Kauli hii ya bwana YESU ambae ni mjumbe wa mungu na ile ya Paulo katika warumi 10:8-10 ipi ya kweli?

  Bwana mungu asifiwe!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s