Msaada:Wanawake na kufunga vitambaa tena!!

kufuniakakichwa

Hapo zamani tuliwahi kujadili suala la mawigi kwa wanawake kutokana na mtazamo wa Askofu Zakaria Kakobe

https://strictlygospel.wordpress.com/2008/05/11/askofu-kakobe-na-vita-ya-mawigi-ya-wanawake/

Lakini kuna swali linalofanana na hilo kutoka kwa dada Neema, karibuni!

Shalom wapendwa!
Naomba mnisaidie kuhusu hili Neno katika 1 Cor 11: 1-16.
Hivi ni dhambi mwana mke kutembea bila kitambaa kichwani? Ni dhambi kusuka nywele? Mwanamke mkristo anahitaji kuvaaaje naongelea kuhusu kichwa. Anapashwa kukata nywele na kuvaa kitambaa kichwani kila wakati? Mimi sielewi jamani niko confused kwa hili- Naomba mnisadie kuelewa.

Samahini kiswahili siyo lugha yangu ya kwanza ndio maana iwezekana nikaandika makosa. Nashukuru sana. Mungu awabariki.

Neema Gashu

18 thoughts on “Msaada:Wanawake na kufunga vitambaa tena!!

 1. Mungu awabariki wapendwa kwa namna mnavyolipenda neno la Mungu.
  Nami naja ili niliongee pamoja nanyi, nikileta pengine mantiki mupya ya uelefu wa mada inayoendelea.
  1. Tukiweka kiujumla maandiko, nadhani mtu asilaumiwe kwa tafsiri anayoleta kwani ni hiyo ndo anafahamu. Lakini pia tusichange vitu viwili tofautu : kufunika kichwa ni tofauti ya kufunga kichwa. Biblia inaongea juu ya kufunika kichwa. Kwa hiyo anaekifunga asije akalaumu asiyekifunga kwani kwa hiyo mantiki hakuna aliyeyatimiza maandiko.
  2. Wapendwa, Biblia ni NENO la Mungu. Kwa hiyo imeandikwa ndani ya lugha ya Mungu haijalishi ni tafsiri ipi ya lugha unayoitumia. Lugha ya Biblia siyo Kiswahili, wala Kingereza, wala Kinyakisa, …. Ni lugha ya Mungu. Ndo maana inatakiwa ijifunzwe, Mwalimu wa kweli akiwa Roho Mtakatifu. Sasa tukisoma tu hatutafahamu bali tutakariri maneno bila msaada wowote.
  Hebu tuangazie lile neno kama jinsi limeanikwa ndani ya « I Kor 11 : 3 Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.
  4 Kila mwanamume, asalipo, au anapohutubu, naye amefunikwa kichwa, yuaaibisha kichwa chake.
  5 Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa.
  6 Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe.
  7 Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.
  8 Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume.
  9 Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume.
  10 Kwa hiyo imempasa mwanamke awe na dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika.
  11 Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana.
  12 Maana kama mwanamke alitoka katika mwanamume, vile vile mwanamume naye huzaliwa na mwanamke; na vitu vyote asili yake hutoka kwa Mungu. Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu.
  13 Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa?
  14 Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake?
  15 Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi.”

  Kabla sijaeleza chochote, nemependa sana nionyeshe kama maandiko ya Paulo siyo mepesi kusikia. Petro mwenyewe alihakikisha hilo jambo. “2 Petro 3: 15 Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;
  16 vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni VIGUMU KUELEWA nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.”

  Kwa hiyo, wapendwa, katika hiyo shahuku ya kujifunza Biblia, jifunzeni kwa makini kabisa, kwa maana Paulo huyu ni mwalimu wa saikolojia ya juu kama vile alivyofunzwa na Roho Mtakatifu. Petro akiwa mchaguliwa wa Mungu pia mwanzilishi wa kanisa, naye anamshuhudia Paulo kama katika nyaraka zake mna mambo magumu kuelewa. Kwa hiyo kuna hasara kama tukiyashikilia kiujumla pasipo kuyajifunza ipasavyo.

  Tuyarudiliye maandiko yake Paulo:

  Paulo, anapoanza tufunza pale ku shairi la tatu, anatoa ufafanuzi mupya wa neno KICHWA katika mantiki ya somo lake. Anasema hivi “Lakini NATAKA MJUE YA KUWA KICHWA CHA KILA MWANAMUME NI KRISTO, NA KICHWA CHA MWANAMKE NI MWANAMUME, NA KICHWA CHA KRISTO NI MUNGU.”
  Kwa mantiki hiyo kichwa siyo ile tunayoona lakini Paulo anataka tujue kama mume ndo kichwa ya mwanamke. Akiendela anasema kama imemupasa mke asali akifunika hicho kichwa. Sasa kulingana na mantiki yetu tutadhani ni kichwa chake wakati Paulo anaposema mumewe. Ni somo gumu kusikia lakini, Paulo ndivyo alivyo, hakuficha chochote, alifafanua anachotaka tufahamisha, akaendelea akituletea mwelekezo wake unaolingana na hicho kitu.
  Kwa lugha nyingine, mke hana kichwa ila mume. Na mwanamume hana kichwa ila Kristo. Hivyo mke akiwa msaidizi wa mume imemupasa kuficha(kulinda) kichwa chake ao mumewe. Na mwanamume akiwa chini ya Yesu, Yeye asiye na aibu, amfunue ili aoneshe utukufu wake kwenye mataifa.
  Anaposhuka na somo lake ndipo analifikisha mahala pa kuweka vile vitu vya kiroho katika vielelezo vya kimaisha na vya kimwili akisema “13 Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa?
  14 Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake?”
  Wapendwa, hamfahamu kama kila somo darasani lina vipengele hivyo hivyo ambavyo Paulo amevitia ili tulielewe somo lake angalao kwa kiasi fulani hata kama ni ligumu?
  Basi, Mungu aendelea tuangazia zaidi na nimependa niache kwanza ili kukiwa swali la uelefu mwingine ndipo tuliangazie zaidi.

  Mungu wa mbinguni awabariki

 2. Jumaa, unajua sisi si watu wa enzi za Yesu. Enzi zenyewe unazozisema ni za utamaduni wa wayahudi tu, na sisi nni wangoni, wazaramo, wasukuma, wahehe,……

 3. Jay jay
  Mimi binafsi simpi ruhusa mwanamke kuachilia kichwa chake wazi, na hata ukiangalia watu wa enzi za Bwana Yesu wanawake walikuwa wakifunika vichwa vyao, mbona tusiige mfano huo?

 4. Funika kichwa, funika kichwa, funika kichwa……!

  Ivi kabla ya kuchangia tunayapitia hayo maandiko ili kujua kwa undani kilichoandikwa katikati ya mistari?

  Kwa mfano neno kilemba tumelitoa wapi, je lipo kwenye hayo maandiko?

  Biblia imesema kufunika kichwa, haijasema kufunika kwa kutumia nini, bt nashangaa mtu anaposema imesema mwanamke avae kilemba kichwani. Mnataka kuwafanya wanawake wote wakristo duniani wawe wanaigeria au?

  Kwani nywele hazifuniki kichwa?
  Kwani wigi halifuniki kichwa?

  Na ukichunguza vema hayo maandiko, utagundua kulikuwa na suala la kuwa nywele nyingi vs kunyoa nywele. Ikaonekana kunyoa nywele ilikuwa inamwaibisha mwanamke traditionally(kwa utamaduni wa hao wakorintho).

  Yule mwanamke aliyempangusa Yesu kwa nywele zake kwani alikuwa amezifunika kwa kilemba, au hicho kitendo hakikuwa ibada?

  Ni vema tukajua kuwa suala hili Paul aliliweka hivyo katika kanisa la Korintho kwa sababu katika ile sehemu (nchi) kwa wakati huo kulikuwa na uasi wa wanawake(wake) kinyume na mamlaka ya kutawaliwa na wanaume.

  Ndipo ukawekwa utaratibu wa wanawake ili kuonyesha kuwa wanakubali kuwa chini ya mamlaka za waume zao lazima vichwa vyao viwe vimefunikwa.
  Na wanaume ili kuonesha tofauti kati yao na wanawake, wao wakatakiwa vichwa vyao kutokufunikwa.

  Kwa hiyo ikajengeka utamaduni kuwa ni mwiko kwa mwanamke kuwa hajafunika kichwa akifanya hivyo maana yake huyo amekataa kuwa chini ya mamlka ya mume wake au babaye.

  Na mwanaume kufika kichwa ikawa ni sawa na kujifananisha na mwanamke.

  Ndipo utaratibu huo ukatumika katika kanisa pia kumaanisha jambo hilohilo la mwanamke kuonesha kuwa yuko chini ya mwanaume, na chini ya baba yake (kwa wasioolewa).

  Lakini Paul akaliweka kiimani zaidi kuwa mwanaume pia afuate utamaduni wa kutofunika kichwa(kutokuwa na nywele nyingi) kwa ajil yai kumtii Kristo.

  Hata hivyo, kumbukeni katika utamaduni wa kiyahudi, wanaume walikuwa wanafunika vichwa wanaposoma gombo au wanaposoma vyuo vya manabii, kinyume na hiki ambacho kinafanyika kwa wakorintho.

 5. Ndugu zangu ktk kristo nimesoma mjadala na nimebarikiwa,wapendwa kwa kuongezea ni kuwa ni kweli lazima tufunike kichwa tuwapo ktk ibada na mapambo ya aina yoyote yale ambayo hukuzaliwa nayo kwamba umeyakuta ukubwani huruhusiwi unatakiwa ukae jinsi ulivo hata kupaka lipstics na chochote kile cha kuongeza umaridadi au muonekano havimpendezi Mungu.Alivo tuumba ndio yeye anapenda tuwe ivo neno linasema tusiifatishe namna ya dunia hii na pia tusiipende dunia .Hili neno litahukumu wanawake wengi sana wa kikristo wanaosema Mungu anaangalia moyo.Jamani mbinguni si lelemama wapendwa kunahitaji kujikana nafsi hasa na ni neema.Nayasema haya kwa kuwa kuna ushuhuda mmoja nilisoma wa mpendwa mmoja aliyepelekwa jehanam na kukuta wanawake wa kikristo wengi waliokua wanajipamba kama wafanyavo mataifa.Hivyo ni uamuzi wako.Mungu atusaidie.

 6. Mungu aturehemu wakati wote.Roho Mtakatifu atusaidie kanisa.Yule anayeongozwa na Roho wa Yesu anajua tafsiri ya maandiko na jinsi ya kuvaa na kuenenda wala hafundishwi au kushawishiwa na dhehebu au viongozi wa dini. Wapo wana wa Mungu ambao hupewa tafsiri na uthibitisho wa Maandiko katika ulimwengu wa roho.Watu wa namna hii huwa wanajadili mambo kwa hekima ya Kristo na hujizuia ktk mijadala mingi. Kiwango cha upotoshaji wa neno la Mungu kiko juu mno na hii ni zaidi ya hasara kwa kanisa.

 7. Bado ninahitaji kueleweshwa zaidi maana nyakati zinabadilika na teknolojia nayo inabadilika, zamani mtu akiokoka hata kupaka losheni ilikuwa dhambi, hata kumiliki gari tu ilikuwa anasa mana makanisa yalikuwa hayajajengwa ilikuwa ni bora utoe pesa hiyo ikajenge Kanisa… Mwanamke hajazuiwa kujipamba ila ajipambe kwa kiasi na kiasi hicho ndo shida kila mmoja anatafsiri yake kuhusu kiasi…. Naona kuvaa hereni si dhambi ni pambo tu…

 8. Ndugu kwa nini tunailazimisha Biblia iwe sawa na matakwa yetu? Wanawake wanapaswa kufunika vichwa vyao wakati wa ibada kama Neno la MUNGU lisemavyo na si tofauti ya hapo. biblia inasema akifanyacho mtu ndicho kilichoujaza moyo wake. kwa hio mtu anapovaa wigi, kusuka na mavazi mengine huanzia ndani yake!

 9. Bwana Yesu asifiwe.
  Tafadhali nina swali ambayo inayonisumbua hadi sasa na naomba ufafanuzi toka kwenu.
  1.kwanini katika ibada maskofu usali wakiwa wamevaa kofia(kufunika kichwa).je hiyo uwendana na maandiko ya biblia?
  2.kwanini mazehebu zingine,mwanamke hapewi nafasi ya huduma kanisani.
  3.kati ya ubatizo wa maji na maji madogo,upi uliyobora zaidi kibiblia.
  ni mimi TONY MALANYIBWA toka kambi ya nyarugusu,mkoa wa kigoma,wilaya ya kasulu.

 10. Watu mlioumbwa kwa mfano na Sura ya Mungu: KUNA MAMBO KADHAA YANAYOTUFANYA KUITII KWELI YA JAMBO HILI
  A) KUTHAMINI UUMBAJI
  Akiumbacho Mungu ni chema , mungu ametuumba na kuona vile alivyotuumba ni vyema. Hivyo kujitengeneza kwa namna ya usukaji si vema kwa maana ni kutijiamini kwamba tumeumbwa Vema Soma Mwanzo 1:31 hiyo tumwakilishe katika matendo na mwonekano wetu
  Tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanzo 1:26

  B) KUITII INJILI
  “Kujipamba kwenu, KUSIWE KUJIPAMBA KWA NJE, YAANI, KUSUKA NYWELE; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu,iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.” (1 Petro 3:3-4)
  “Vivyo hivyo Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi;si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na na lulu, wala kwa nguo za thamani.” 1 Timotheo 2:9

  C) KUTOENDANA NA MATAIFA
  Soma kisa cha Esta.2:12-16
  Esta hakuhitaji kitu chochote juu ya mwili wake lakini alionekana mzuri kupita wana wake wote na kupata kibali mbele ya mfalme.
  Rastafarians Hutumia vifungu vya Biblia katika kutetea hoja zao mfano;
  Huvuta bangi na Mbegu wakitumia fungu Kwa nini wanatumia mimea ya bangi? Hutumia fungu la Mwanzo 1:29. “ Mungu akasema tazama nimewapa kila mche utoao mbegu,juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;”hivyo kwa wao huvuta bangi na kuhalalisha kwa kutumia biblia na fungu hili. PILI, asili yao kusuka rasta ni katika Waamuzi 13:15 ,Waamuzi 16:13. Hivyo kufunga vishungi saba wakisema wanamfuata Samson na vishungi saba lakini pia. Biblia ina sema Simba wa Yuda ni Yesu lakini wao Hutumia biblia wakisema simba wa Yuda ni Haille Sellasie na kwao ni Masihi hivyo misuko ya nywele ya Rasta ni ya imani ya wasioamini Kristu ni masihi bali Selassie nao huweka vipini katika misuko hiyo kama ilivyo misuko ya Wanawake wa kisasa.
  Mtu aliye iliyeitwa mteule Muisraeli kiroho haigi tabia zisizo za asili ya Uumbaji na za wale walioitwa kuwa waisraeli wa Kiroho. Kumbuka neno lisemalo aliye chini ya kristo ameziacha tamaa zote za mwili.
  Wamisri Walivaa mawigi kwa kuwa walinyoa vipara kwa kuwa Misri kulikuwa na chawa wengi na joto kali hivyo pale walipotaka kuonekana na nywele walificha vipara vyao kwa wigi za Manyoya ya Kondoo na nywele za Binadamu.
  Waroma walikata nywele za watumwa na kufanya mawigi.
  Mfalme Louis wa Ufaransa mpagani aliyewaua wakristo wengi katika Matengenezo na baadae mawazo yake kuchangia uchomaji wa biblia kwa miaka mitatu ufaransa alizaliwa kabla ya wakati wake na hivyo alivaa wigi ambapo fashion ikaingia katika mahakama na na mitaani kuenea sana watu wakipinga muumbaji na kazi zake. Mpaka sasa baadhi ya mabunge kama Kenya huvaa wigi kwa spika kwani Louis aliendeleza mambo ya mahakama na baadae wigi likatumika kama sehemu ya kuenzi mpango huo.
  Mkristu haigi yasiyo yasiyo na msingi wa Biblia na maana kwa maana kila neno tendo litaletwa hukumuni.
  D) KUWA NA KIASI NA KUWA WAKILI MWEMA WA UTUME
  Moja ya sifa za mkristo ni utunzaji wa muda na fedha kwa ajili ya injili. Kutumia shilingi elfu fedha kwa ususi badal ya kununulia watu wanaotaka kumjua Kristu Kristu Biblia au mtu mwenye njaa, au asiyevikwa au kumpelekea mgonjwa chakula hospitali ni kutokuwa wajumbe wa injili na watu wanaompenda Kristo.
  C) KUTENGENEZA MVUTO WA DHATI KWA MWONEKANO WA NDANI TABIA
  Moja ya ndoa kuharika sana siku hizi ni wanaume kuwapenda Wanawake kwa mvuto wa mwonekano usio wa asili. Mfano halufu halisi ya mtu inapovutwa na mwanamke au mwanamme huweza kuchochea mvuto asilia kwani halufu inamchango katika ubongo kuchochea mvuto halisi lakini parfume zimechangia kuwavuta watu kwa manukato yasiyo halisi. Na kupoza halufu halisi ya mwili.
  Mwonekano halisi kwa sura na mfano wa Mungu kwa Yesu alivyojidhihirisha kwetu kama alivyo si kwa kunyoa kiduku au mariam kuvaa wigi au Esta kukataa vifaa vya Urembo na Wanawake kama Sara
  (1 Petro 3:3-4)
  1 Timotheo 2:9
  Bwana atusaidie tunapoamua kuitii injili na sio watu. Maana si kusoma injili bali kuitii ndiko kunakotutakasa wakristu wengi na wachungaji watashindwa kusimama si kwa kuwa hawakusoma bali hawakuitii Injili maana kutii injili ndio kunatutakasa. “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndio kweli” YOHANA 17:17
  “KUJIPAMBA KWENU, KUSIWE KUJIPAMBA KWA NJE, YAANI, KUSUKA NYWELE; NA KUJITIA DHAHABU, NA KUVALIA MAVAZI; BALI KUWE UTU WA MOYONI USIOONEKANA, KATIKA MAPAMBO YASIYOHARIBIKA; YAANI, ROHO YA UPOLE NA UTULIVU,ILIYO YA THAMANI KUU MBELE ZA MUNGU.” (1 Petro 3:3-4)

 11. Lghtness, kama kila mtu atafuata akili zake zinavyomtuma, kitafsiri na kimapenzi yake, basi Biblia ina kazi gani? Ungetupa na kifungu ambacho Mungu amesema hayatazami mavazi tunayovaa, ila anatazama mioyo yetu tu, hilo lingetufaa sana!!!

  Jitahidi kusema kile Biblia isemacho, kama isemavyo utakuwa salama!

 12. kwa upande wangu sioni kuwa ni dhambi hizo ni sheria za agano la kale kutokana na makabila ya wayahudi wanawake walikuwa wanafunika nywele kwa mimi haina shida kuvaa au kutokuvaa Mungu anatazama moyo na sio mavazi

 13. Dada Neema na woote,
  Suala hili la wanawake kufunika vichwa vyao ni suala la kiBiblia, kwahiyo, iwapo kuna utata wowote wa kitafsiri katika jambo hili, kulingana na mapokeo au kanuni za kidhehebu au chochote kile, kimsingi twapaswa turudi katika Biblia ili kuipata tafsiri halisi ya jambo hili, nayo Maandiko yanatusisitizia jambo hilo la kuyaacha Maandiko yajitafsiri yenyewe, 2Petro 1:20-21 “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”

  Basi jambo hilo laweza kuwa dhahiri kwako hapo utakapofika katika kuliamini Neno hilo, ili Maandiko yenyewe yakuongoze katika tafsiri yake yenyewe, kwani Mungu hajawahi kupungukiwa na chochote kile hata amuhitaji binadamu kumtafsiria jambo lake!

  Hivyo, hilo Neno katika 1Kor 11:1-16, kwa hayo yanayomhusu mwanamke, iwapo utayasoma kama yalivyo, ukiachilia mbali shawishi za dini, ni dhahiri kuwa hautatatizika. Lakini kwa vile shawishi zilitangulia, basi twende pamoja tuyaangalie hayo yanayohusu, ili tuwe na uhakika wa kiMaandiko wa hilo litupasalo.

  Jambo la kwanza, yatupasa tutambue nafasi ya mwanamke. Hapa tunaona kuwa katika chain ya uongozi, au uwajibikaji, mwanamke amewekwa katika nafsi ya mwisho, juu yake yuko mwanamume ambaye ndiye kichwa chake. Kifungu cha 5 kinasema, “Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa.” Unaona dada Neema? Yaani mwanamke anaposali bila kufunika kichwa chake, anamuaibisha mumewe au baba yake, kwa huyo asiyeolewa, maana ndiye anayemmiliki. Pia hiyo aibu anayoileta huyo mwanamke, inafanana na ile ya mwanamke aliyenyolewa nywele zake! Hakuna fumbo hapo, inahitaji unyofu wa moyo tu kuyapokea hayo! Unaona, sioni mahali panaposema mwanamke asisuke nywele zake, bali naona akizinyoa ni jambo la aibu!!

  Pia kwa kadiri ninavyoyasoma Maandiko hayo, naona msisitizo mkubwa uko katika kufunikwa kichwa na kutokukata nywele zake. Afunikwe kwa kitu gani? Kitambaa, au sufuria au gunia? Kwa kadiri utakavyoendelea kuyasikiliza hayo mafundisho, yasingeweza kuishia njiani bila kutuonesha hicho cha kufunikia au kifuniko. Ndipo katika kifungu cha 15 Roho Mtakatifu analifunga somo hilo kwa kutuonesha hicho kimpasacho mwanamke mkristo kufunikia kichwa chake, “Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi.”!!! Umeelewa dada Neema? Nywele zako, Mungu amekupa ili ziwe hicho kifuniko (KJV But if a woman have long hair, it is a glory to her: for her hair is given her for a covering). Kwa hiyo unapozinyoa nywele zako, unamuaibisha mumeo, ambaye pia kwa aibu hiyo anamuaibisha Kristo kwa kushindwa kwake katika jukumu la kukumiliki, ndiyo kusema familia hiyo, Mungu ataitenga maana imejaa aibu!

  Kwahiyo kwa kifupi, suala la mwanamke mwenye nywele zake ndefu alizopewa na Mungu, kutembea bila kuvaa kitambaa kichwani si dhambi, wala kuvaa kitambaa hicho hakumuongezei thawabu yoyote. Pia kusuka nywele si dhambi kulingana na Maandiko hayo kama yalivyo, nyongeza yoyote juu ya hapo ni uongo wa kidini usio na tija yoyote, kama ambavyo wanawake hufungishwa vitambaa kinyume na maelekezo hayo kutokana na viongozi wao kuondoka na nusu ya jambo au kukosa ufunuo wa jambo hilo! Kwa jambo la kukata nywele, kama tulivyoona katika Maandiko ni AIBU, basi sidhani kwamba maisha ya aibu yanamfaa mkristo! Basi USIKATE nywele zako, maana nafahamu mkristo anakuwa uweponi mwa Bwana kwa masaa 24, sasa ukimjia Mungu na hiyo panky yako au kipara, jua ya kwamba atakupa kisogo! Na iwapo umezikata basi UNAPASWA kufunga hicho kitambaa au vazi lolote wakati wote ili kuepusha hiyo aibu!

  Ubarikiwe!

 14. ilizuiwa kuacha vichwa wazi kwa kuwa nywele zao zilikuwa ndefu kiasi kwamba ilikuwa inaleta mshangao kwa watu,lakini kwa wenye nywele za ki afrika vipilipili sioni kama ni lazima

 15. Kufunika kichwa ni pale tu unapokuwa ibadani (Yaani ile ibada ya kikristo ya siku ya kwanza ya Juma aka Jumapili) ya kumega mkate na kunywa kutoka katika kikombe kimoja cha divai kuadhimisha tendo la ukombozi kwa njia ya Kristo pale msalabani.

  Kwa nini?

  Jibu: Kichwa cha mwanamke kinapokuwa wazi huashiria utukufu kwake na kwa mwanaume, na kichwa cha mwanaume kinapokuwa wazi huashiria utukufu kwa Kristo. Kwa hiyo ili kumpa Yesu utukufu wote hakuna budi kwa wanawake wote wakiwa Kanisani kufunika vichwa vyao na wanaume kuacha vichwa vyao wazi. Swala ni kufunika kichwa haijalishi kama umesuka au haujasuka.

  Kwingine kote nje ya ibada, hakuna kanuni inayomwagiza mwanamke kufunika kichwa chake. Ni ruksa kuacha wazi ukiwa umesuka au haujasuka.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s