Tamko la Maaskofu kuhusu uchinjaji na hali ya mwelekeo wa kisiasa nchini

askofu

JUKWAA LA WA WAKRISTO TANZANIA (TCF)

“ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA” (Lk.2:14)

TAMKO LA PAMOJA LA MKUTANO MKUU WA DHARURA WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

1.
Utangulizi

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha Taasisi Kuu za Makanisa nchini kama ifuatavyo:-

Jumuiya ya Kikristo Tanzania – CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania – TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania – PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (Watazamaji)

Katika Mkutano wake Mkuu wa Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini, Jijini Dar es Salaam, tarehe 8 Machi, 2013; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na mauaji na mashambulizi ya viongozi wa dini; na hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya uhalifu huo unaotekelezwa na Waislamu wachache. Katika taswira hiyo, Kanisa lilitathmini juu ya wajibu, utume, na sauti yake ya kinabii kwa taifa letu kuhusiana na mambo hayo.

2. Hali halisi ilivyo hivi sasa hapa nchini kwa mtazamo wa Kanisa 

Ushahidi wa kihistoria na kimazingira unaonyesha wazi kuwa kwa sasa Kanisa nchini Tanzania limo katika kipindi cha mateso ya kimfumo (systematic persecution), kama vipindi vingine 10 vya mateso katika Historia ya Kanisa hapa duniani. Pamoja na mateso haya ya kimfumo, tunatambua wazi kuwa wanaotekeleza haya ni kikundi kidogo tu cha Waislamu wa Tanzania, kama wale wengine wa Barani Afrika (k.m. Boko Haram kule Nigeria). Waislamu walio wengi hawafurahii mambo yanayotokea. Wao pia wanaitazamia Serikali kuthibiti hawa wachache wanaochafua dini ya Kiislamu na kuwafanya Waislamu wote waonekane kuwa maadui wa Ukristo, jambo ambalo siyo kweli.

Kutokana na hali hiyo, mkutano mkuu wa dharura wa Jukwaa la Wakristo umeyaangalia maeneo makuu yenye migogoro ikiwa ni pamoja na:
2.1. Mgororo wa nani anastahili kuchinja kitoweo Hivi karibuni hapa nchini tumeshuhuduia mgogoro juu ya uchinjaji wa mifugo ambayo nyama yake inapaswa kuuzwa kwa watu wa imani mbalimbali wakiwemo Wakristo na Waislamu. Tunafahamu kwamba sheria ya nchi yetu inaweka bayana juu ya usalama wa nyama hizo kiafya, lakini sheria haielekezi kuwa dini fulani ndiyo waumini wake wanapaswa kuchinja mifugo hiyo. Kwa misingi hiyo Kanisa linatamka kuwa:-
a) Hoja ya dini moja kudai kuhodhi (exclusive right) uchinjaji wa mifugo kwa misingi ya imani yake ni kinyume cha haki ya uhuru wa kuabudu ambayo amepewa kila mtu ndani ya nchi hii kikatiba katika Ibara 19.

b) Kwa kuwa kuchinja wanyama na ndege ni Ibada kwa Waislamu, Kanisa litambue na kuheshimu jambo hilo. Lakini pamoja na kutambua haki ya Waislamu kujichinjia wanyama na ndege kama Ibada kwao, Wakristo wasilazimishwe kula nyama zilizochinjwa kwa misingi ya Ibada za Kiislamu. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania ni wa dini mbalimbali na mila za makabila mbalimbali, tunaitaka Serikali itamke wazi kuwa kila raia ana uhuru wa kufuata imani yake katika suala la uchinjaji. 
c) Kuhusiana na jambo hili tunashindwa kabisa kuelewa msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali. Wakati wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia ni Muislamu, ulipotokea ugomvi wa mabucha ya nyama ya nguruwe Dar es Salaam, Rais huyu Mstaafu kwa kulinda Katiba ya nchi ambayo aliapa kuilinda, alisema mwenyewe kwa nguvu zote kuwa kila mtu ana uhuru wa kula anachotaka na mtu wa dini moja asimhukumu mtu wa dini nyingine kwa kile anachokula. Baada ya Rais Mstaafu kukemea jambo hili, hali ikawa ya amani na utulivu. Kwa nini Serikali yetu ya sasa inapata kigugumizi kuhusiana na suala zima la nani achinje?
d) Kwa mantiki hiyo hapo juu katika kipengele cha a-c, Wakristo wanaitaka Serikali iweke utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu ili kila Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka. Sambamba na kuitaka Serikali kufanya hivyo, tunawakumbusha Wakristo wote Tanzania kuelewa kuwa watakuwa hawajavunja sheria yoyote ya nchi wakiamua kujichinjia kitoweo chao wenyewe. Kuhusiana na tangazo hili kwa Wakristo wote, tunaitaka mihimili ya dola (Serikali na Mahakama) kuheshimu Katiba ya Nchi yetu, na kipekee kuhusiana na jambo hili Ibara ile ya 19.
e) Kwa upande mwingine, kwa kuwa tayari zipo bidhaa za vyakula katika nchi hii ambazo zina nembo ya ‘halal’ na nyingine hazina nembo hiyo, huu ni uthibitisho kuwa vyakula hivyo vimegawanywa kwa kufuata misingi ya imani za kidini. Kwa hiyo, madai ya kugawanya machinjio na mabucha kwa kufuata misingi ya dini sio jambo jipya kwa sasa katika nchi hii.
2.2 Uchomaji wa Makanisa ulioambatana na vitisho na mauaji ya viongozi wa KanisaKanisa linalaani vikali mauaji ya kidini yanayoendelea kufanywa pamoja na vitisho (systematic persecution) kwa viongozi wa Kanisa na Wakristo wote kwa ujumla.

Mtiririko wa matukio mbali mbali ya nyuma yanatudhihirishia kuwa kumekuwepo na mpango wa muda mrefu wa haya yanayotokea sasa hivi. Tarehe 15 Januari 2011, kundi la Waumini wa Kiislamu walipokutana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, miongoni mwao walikuwamo mashehe, walijadili hali ya nchi ya Tanzania kuongozwa kwa mfumo wa kidini. Mkutano huo ulihitimishwa kwa kutoa tamko dhidi ya kile kilichoitwa mfumo Kristo katika nchi yetu!

Japo Serikali na vyombo vyake vya usalama wa Taifa vimekuwa vikipata taarifa za vitisho dhidi ya viongozi wa Kanisa, mauaji, kuchomwa kwa nyumba za ibada, pamoja na maneno ya uchochezi kupitia mihadhara, vipeperushi, CD na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na taasisi zinazofahamika, hata hivyo Serikali kwa kiasi kikubwa imeshindwa kuchukua hatua kwa wakati muafaka na wanasubiri hadi maovu yatendeke ndipo ati waanze kufanya uchunguzi. Kwa Serikali yetu inaonekana wazi kuwa katika hili ile methali kwamba “Kinga ni bora kuliko tiba” haina maana yoyote. Hii ni kuonyesha udhaifu mkubwa wa vyombo vya usalama wa Taifa au pia kwamba vyombo hivi vinafurahia kutoweka kwa amani nchini mwetu, jambo ambalo linalifanya Kanisa nchini Tanzania liamini kwamba matukio haya yanayoendelea kutokea ni dalili kuwa Serikali ina agenda ya siri dhidi ya Ukristo.

Kutokana na hayo Jukwaa la Wakristo Tanzania linatamka kama ifuatavyo:
a) Tunatambua kwamba ni jukumu la Serikali kuwatendea raia wake kwa usawa na bila ya ubaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi wa Kanisa wanatamka kwamba Serikali imeshindwa kuheshimu Katiba juu ya hizi haki za raia wake na kupelekea waamini wa dini ya Kikristo kukosa imani na Serikali iliyoko madarakani, hasa kuhusu ulinzi na usalama wao na mali zao kama inavyoagizwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Kama Serikali inaona haiwezi kuwahakikishia wananchi usalama wa uhai wao na mali zao, na hivyo kuwafanya waishi maisha ya hofu inayotokana na vitisho, basi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, hakuna sababu ya Serikali iliyoko madarakani kung’ang’ania kuongoza nchi.

b) Kwa kuwa ulinzi wa raia ni haki ya kikatiba na kisheria, Serikali inatakiwa iwalinde raia wake. Kama Serikali imeshindwa kuwalinda raia wake, Kanisa linataka Serikali ikiri hivyo ili Kanisa liwaambie wananchi waiwajibishe Serikali na Viongozi wanaoifanya Serikali ishindwe kutimiza wajibu wake.

Jukwaa la Wakristo linasema:
Kama Serikali haitachukua hatua za makusudi dhidi ya mambo haya yaliyoainishwa hapo juu, Kanisa litachukua hatua ya kuwaambia waamini wake kwamba Serikali iliyoko madarakani inaibeba dini moja, na hivyo Kanisa litatafakari upya uhusiano wake na Serikali.

3. Wakristo walioko Zanzibar
Wakristo walioko Zanzibar wanatishiwa maisha yao na mali zao zinaharibiwa mara kwa mara, kiasi cha wengine kuamua kuhamia Tanzania Bara. Kigezo cha unyanyasaji huo ni suala la udini na muungano. Inaonekana ni kama vile Watanzania waliozaliwa Bara hawana haki ya kuishi Visiwani. Na kumbe wale waliozaliwa Visiwani wafikapo Barani wana haki zote. Kanisa linaitaka Serikali iwahakikishie Wakristo walioko Zanzibar usalama wao na wa mali zao maana hiyo ni haki yao ya Kikatiba.

4. Vitisho na mauaji ya Wanakanisa
Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ichukue hatua za makusudi za kuzuia vitisho na mauaji kwa Viongozi wa Kanisa na Wakristo kwa ujumla. Vinginevyo Kanisa litautangazia ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi mojawapo inayovunja haki za binadamu kwa ubaguzi wa kidini na kulitesa Kanisa kimfumo.

5. Matumizi ya Vyombo vya Habari:
Kwa kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimeruhusu vitumiwe kuwatukana Viongozi wa Kanisa, tunatoa nafasi kwa vyombo hivyo kuomba radhi; vinginevyo tutaitaka dunia ivielewe kuwa navyo ni sehemu ya chanzo cha migogoro. Pia tunachukua nafasi hii kuvitahadharisha vyombo mbalimbali vya habari kupima kwa kina ni nini kinachosemwa na viongozi wa kidini ili kuviepusha vyombo hivyo kutumika kwa nia ya uchochezi; yasije yakatukuta kama yale yaliyotokea kule Rwanda 1994.

6. Hitimisho:
Kanisa linaendelea kusisitiza kuwa silaha kuu ya Mkristo katika nyakati hizi ni maombi na kufunga. Kwa mantiki hiyo, Kanisa linawataka Wakristo wote nchini Tanzania kuungana kwa pamoja katika maombi na kufunga kwa muda wa siku saba kwa ajili ya hali hii iliyojitokeza hapa nchini. Maombi hayo na mfungo vifanyike kabla ya Pasaka, yaani kuanzia, tarehe 24/3/2013 hadi 30/3/2013.

Kwa niaba ya Maaskofu 177 walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa Dharura wa Jukwaa la Wakristo na kutoa maazimio hayo.

1. Askofu Peter Kitula – Mwenyekiti CCT

2. Askofu Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa Rais TEC
3. Askofu David Batenzi Mwenyekiti PCT

DAR ES SALAAM, 19.03.2013

Advertisements

15 thoughts on “Tamko la Maaskofu kuhusu uchinjaji na hali ya mwelekeo wa kisiasa nchini

 1. Donald SL
  Hebu fafanua kidogo huo uongo wa fundisho la 666. Umetuacha kidogo

 2. Ni hivi noel PAUL alisema tusile nyama zilizotolewa sadaka kwa miungu na pia zilizosongolewa tusile unasoma BIBLE kwel?

 3. Wakristo tuna neema moja kwamba tunapokipokea chakula kwa shukrani na kwa kuomba,Mungu hukitakasa kutokana na kuomba kwetu,kwahiyo hata kama kina dua baya zile nuksi zinaondoka kwa jina la Yesu

 4. Tamko limejitosheleza kabisa, tatizo ni pale niliporudi toka Easter Conference huko Kidugala kwa Mkoa wa Njombe, mchana ule ule wa j3 nikasikia hotuba ya JK redioni.

  Sehemu ya hotuba alidondoa tamko hili. Sijabahatika kusikia tamko la waislam anaodai nao wanalalamika. Hii ni ajabu kweli; eti wauaji wanalalamika kuwa…ina maana hawakupewa nafasi ya kutosha kuua idadi waliyotaka; ndio maana wanalalamika serikali kuwaonea.

  Mungu wetu ni Mkuu, nayakumbuka maneno ya Rev. Yohana Marko mwaka 1990 kwwenye Easter Conference yangu ya Kwanza Tosamaganga, alisema…’Wao wanazungumzia magari ya vita, bali sisi tutalitaja jina la Bwana…” ule ulikuwa unabii na sasa unatimia

  Mungu ibariki Tz

 5. Mmary: kwanini waisilam hamtaki kula zilizochinjwa na wakristo? hiyo ni dharau kubwa sana kubalini na sisi tuchinje mle

 6. Blastus; nimesema haya kwa kuzingatia umoja ni nguvu(people’s power) hata jeshi likikosa umoja hupoteza ushindi……..

 7. Donald, hili si suala tu la kuwa nyuma ya viongozi wetu,bt ni wakati wa mkristu mmoja mmoja kuhakikisha aman inapatkana lakini serikali iliangalie hili kwa upana sna na siyo kupuuza kama wanavyofanya kwenye mambo mengine yaliyopita.

 8. Pongezi kwenu Maaskofu wetu kwa kutafakari mustakabari wa nchi yetu kwa hekima kubwa..ni wakati wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuyafanyia kazi hayo ili kulinda tunda la amani ya nchi yetu na UPENDO IWE NGUZO MUHIMU.

 9. Magreth ngoja nikwambie kitu kimoja ambacho mimi nimekigundua. Viongozi wetu wengi hata na viongozi wengi wa kiislam hawakuweza kuyafanya haya wanayofanya leo wakati Mwalimu akiwepo si kwa sababu walikuwa wanakubaliana nae, na si kwa sababu walikuwa wanamtii. Bali ni kwa sababu walikuwa wanamuogopa kama ilivyo panya kwa paka.

  Kwa hiyo alipoondoka tu wakaamua kuwa halisi sasa. Ndio maana yote aliyokuwa anayakemea ndio haswa leo yanafanyika.

  Halaf kwa wale wanajaribu kuhoji kuhusu Jk kuwa inawezekanaje akawa ni chaguo la Mungu kutokana na anayoyanfnya, naomba niwakumbushe jambo moja.( hasa ndugu yangu Mtangoo).

  Mimi ni miongoni mwa watu wanaoamini kuwa kweli Jk ni chaguo la Mungu ni si kwa sababu kuwa kila mamlaka hutoka kwa Mungu, bali ni kutokana kabisa na huo unabii uliotolewa kuwa yeye ni chaguo la Mungu.

  Sikia, ili ujue kwa nini naamini hivyo; Karibu kila uovu uliokuwa umejificha kwa watawala katika hii nchi umekuja kufichuka wakati wa utawala wa Jk.

  -Tusingejua EPA, Meremeta, mikataba ya madini nk kama si Jk)

  -Tusingejua kuwa viongozi huingia madarakani kwa rushwa kama si Jk

  -Chama tawala kisingekoma kuwadanganya wanachi kama si Jk. Ni yeye aliyesaidia chama tawala kubomoka kama unavyokiona leo na pengine kitakufa kabisa ili tuanze enzi nyingine

  -Je asingekuwa yeye ungeuona wapi huo upendeleo wa watu wa dini moja kushika nyadhifa nyeti nyingi za kitaifa kama ulivyotuchanganulia hapo juu bwana Mtangoo? jambo ambalo limetuamsha wakristo wa Tanzania kumtafuta Mungu kwa kufunga kwa pamoja kama walivyotangaza maaskofu wetu

  -Amini usiamini kama si Jk tusingeweza kuona huu uhuru wa habari na mawasiliano tulionao leo ambao kimsingi ndo umekuwa chachu ya ukombozi wa wanyonge wa nchi hii, e.g blog kama hii SG, magazeti n.k

  -Kama si Jk tusingejua kuwa kuna wachungaji wanauza unga (dawa za kulevya)

  -Kama si Jk tusingejua siri mbalimbali za ikulu

  Mungu alimchagua SAULI kuwa mfalme wa Israel japokuwa alikuwa mwovu lakini alikuwa chaguo la Mungu kwa kusudi maalum la Mungu kwa taifa lile.

  Kama Jk katusaidia kuyatambua yote hayo yaliyokuwa yamefichika miaka na miaka, na kutuonesha njia kwa ajili ya ukombozi wa nchi yetu kwa nini tunakuwa wagumu kuamini kuwa yeye ni chaguo la Mungu?

  Tuinueni macho yetu juu maana saa ya ukombozi wa nchi hii imekaribia mno. Najua kuna wengine wetu watalala mauti kwa ajili ya harakati za ukombozi huu kama mch. Mathayo wa Buseresere na Padri wa Zanzibar. Lakini hii ndio njia ambayo Mungu ameamua kuitumia kwa ajili ya kuitoa Tanzania katika laana za matambiko ambayo yamekuwepo miaka nenda rudi,pamoja na mauaji wa ndugu zetu albino.

  Namshukuru Mungu kwa kulihusisha kanisa moja kwa moja katika ukombozi huu, ili misingi ya nchi hii irudi kwa Mungu

  Mwisho, JK hajatumwa na Mungu kuja kuyakomesha maovu yaliyopo, bali kuja kuyafunua tu. Yuko mmoja ajaye huyo ndiye atakayekwenda kuyakomesha. Kwa hiyo tusimlaumu watumishi wa Mungu,yeye katimiza wajibu wake wa kuyaweka wazi.

  Nawapongeza sana maaskofu wetu!

 10. Katika Jina lililokuu kupita majina yote Yesu Christo wa Nazaret, nazivunja Roho zote, na mamlaka yote, ya Roho ya ubaguzi na U dini , yenye mizizi na machafuko, naipeleka kuishitaki kwenye mahakama kuu ya mbinguni, roho yenye vurugu isitawale Tanzania kamwe ,navuruga mitambo yote na mitego yote ya Ibilisi, naiwashia moto kuiunguza na kuiteketeza leo 2013 isikae ifurukute tena hapa nyumbani Tanzania katika Jina la Yesu Christo mwenye funguo za mamlaka yote , mbinguni Duniani na Ahera. Amen

  Baba wa taifa hayati Mwalimu Nyerere alituonya sana juu ya Tabaka za Udini. tumelelewa , katika kuheshimiana na bila kujali tofauti zetu za udini, mradi usivunje sheria. Ambayo ni misingi mizuri ambayo nchi nyingi zinafuata. kupendana na kuishi kwa Amani inashinda fedha na mali za utajiri tulionao. nchi nyingi Tajiri zimekalia mali, lakini zinakosa Amani. mali bila Amani ni bure.

  nchi jirani Kenya zinatushangaa jinsi tulivyolelewa kupendana na kuoana bila kujali ukabila tofauti tulionao. Namuomba Mungu pia tuendelee kuheshimiana katika u-tofauti wa Imani zetu.

 11. Maaskofu hawa ambao ni watumishi wa Mungu na viongozi wetu wametoa tamko sahihi na lenye kujenga nchi yetu. Na kama alivyochangia Ndugu John ya kwamba wapo waliosema kuwa Rais wetu Mheshimiwa KIkwete ni chaguo la Mungu, hata mimi naungana nao kwa kuamini ya kwamba walizingatia maneno ya Mtume Paulo yasemayo “…………; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu” (Warumi 13: 1ff) Kuhusu hali ya vurugu na uhasama kati ya waumini wa dini hizi kubwa mbili, si jambo jema hata kidogo na ndilo ambalo Mababa hawa wameliongelea na kutoa tamko zito nami nawaunga mkono. Tamko hili ni kuikumbusha na kuitahadharisha serikali yetu kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani na kuheshimu imani na dini ya mtu mwingine. Tuweke maanani pia ya kwamba Watanzania wote si Wakristo na Waislamu tu; wapo wengine hawana dini yoyote ila wana imani yao na miungu yao. Wote sisi tunahitaji kuheshimiana. Mimi sioni ubaya wowote kuongozwa na Mwislamu au Mkristo iwapo atafuata taratibu na sheria za nchi kwa manufaa ya wote bila ubaguzi. Nitampinga kiongozi Mkristo akiutumia Ukristo wake kumdhalilisha na kumwona mwingine hafai; vivyo hivyo nitapingana na Mwislamu akifanya hivyo.
  Shalom

 12. Kati ya waliokuwamo kwenye tamko hilo wapo waliosema Kikwete ni chaguo la Mungu. ila na sisi hatukuuliza chaguo la Mungu yupi? Baada ya chaguo la Mungu huyo kuingia madarakani sasa tunaona
  1. Rais – Muislam
  2. Makamu wa Rais – Muislam
  3. waziri mkuu – Mkristo
  4. Jaji mkuu – Muislam
  5. IGP – Muislam
  6. Mkurugenzi wa usalama wa Taifa – Muislam
  7. Spika wa Bunge – Mkristo
  8. mwenyekiti wa ccm – Muislam
  9. katibu mkuu wa ccm – uislam
  Maeneo yote muhimu chaguo la Mungu limeweka waislam. nina wasiwasi kama maaskofu wetu wengine sio waislam na hasa yule aliyekuwa Dar akahamishwa kagera (kilaini)

 13. inapendependeza sana watumishi wa Mungu siyo sahihi kabisa wa watu wa imani fulani kuwadhalilisha wenzao eti kwa kisingizio kwamba dini yao ni bora zaidi

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s