Nia Zetu zifanywe upya

neno

Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu – Warumi 12: 2

Na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; – Waefeso 4: 23

Neno la Mungu linatukumbusha sisi tunaomwamini Bwana Yesu kama Bwana na Mwokozi wetu ya kwamba, ili tuweze kuishi maisha ya ushindi ni lazima tuendelee kufanywa upya katika roho za nia zetu kila siku, au kwa maneno mengine, mawazo na mitizamo yetu inabidi ibadilike kuendana na Neno la Mungu linavyosema. Tusikubali kuishi tena kama watu wasio na tumaini, Neno linatuambia ya kwamba Mungu anatutakia mema siku zote za maisha yetu ( Yeremia 29: 11, 3 Yohana 1: 2).

Labda nitoe mfano mmoja halisi; tuseme umekabiliwa na tatizo la ugonjwa, badala ya kuwaza na kusema kama wengine wasiomjua Mungu maneno kama vile “ugonjwa huu utaniua”, au “huu ni ugonjwa wangu”, au “kila mwaka lazima niugue hivi”, badili kauli yako ukatae huo ugonjwa na dalili zake zote ukikiri Neno linavyosema “kwa kupigwa kwake mimi nimepona”, “Jehovah Rapha, Bwana ndiye mponyaji wangu”. Kumbuka pia Bwana Yesu alitupa mamlaka akisema “waniaminio…wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya”.

Tunazo ahadi nyingi tu katika Neno la Mungu kuhusu uponyaji, mahitaji na mambo mbalimbali, yaamini na kuyakiri uushuhudie mkono wa Mungu maishani mwako! Kwa kifupi, kufanywa upya katika roho ya nia zetu, ni kitendo cha kudhamiria KULIAMINI Neno la Mungu KULIKO mazingira yetu. Tutambue ya kuwa Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, hivyo basi Neno lake siku zote ni kweli (Warumi 3:4) na sisi tuna haki na kila ahadi kwa sababu ya kazi kamilifu ya ukombozi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani.

Tuelewe ya kwamba sisi hatuko peke yetu tena, tunaye Roho Mtakatifu ndani yetu naye atatuwezesha kuliamini Neno linavyosema na kukubaliana nalo kuanzia kwenye mitazamo yetu, mioyo yetu na hatimaye kwenye kauli zetu na matendo yetu, ili tuishi maisha ya ushindi kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Amen!

Mbarikiwe watakatifu wa Bwana Yesu,

–Patrick
Advertisements

8 thoughts on “Nia Zetu zifanywe upya

 1. Ubarikiwe kwa somo zuri Mungu akubariki na akupe mafunuo zaidi na zaidi sio kama wanadamu watakavyo bali kama Mungu atakavyo.by mwakalonge

 2. Mpendwa Mkandya,

  Nashukuru kwa ufafanuzi wako mzuri kuhusu nia zetu kufanywa upya. Kufanywa upya nia zetu ni somo pana na linahusisha nyanja zote za maisha yetu kwani nia zetu ambazo ziko kwenye nafsi zetu ndipo uamuzi au niseme utashi wetu ulipo, ulivyoelezea ni sawa kabisa maana ni sehemu ya nia zetu kufanywa upya. Hivyo basi kichwa cha habari nilichokiweka sidhani kama kinakinzana au kinatofautiana na nilichokiandika.

  Labda niseme nilicholenga mimi zaidi ni kubadilishwa kwa namna tunavyofikiri tunapokabiliana na changamoto mbalimbali. Nia zetu zikifanywa upya, bila shaka tutania mema na pia hatutaifuatisha namna ya dunia hii katika kuenenda kwetu. Tutaweza kutenda tofauti na wasiomjua Mungu ikiwa tutawaza tofauti, na hilo litawezekana ikiwa tu nia zetu zitafanywa upya kwa Neno la Mungu.

  Kama ulivyoainisha, kufanywa upya nia zetu kunatubadilisha mitazamo yetu na mienendo yetu lna kauli zetu pia. Hatuwezi kudai tumefanywa upya nia zetu na hapohapo kuendelea kuongea kama wasiomjua Mungu na Neno lake, na Neno lakie tusisahau linajumuisha ahadi zake pia.

  Isitoshe kubadilika kwa mitazamo kunaongozwa na Neno lisemavyo na Neno ni pamoja na ahadi zote zilizomo ndani yake, hivyo basi ushahidi wa kuwa umefanywa upya nia yako katika eneo fulani, utajidhihirisha pale utakapolikiri Neno unapokabiliana na changamoto katika eneo husika, tofauti na asiyelijua Neno lisemavyo katika eneo hilohilo ataifuatisha namna ya dunia katika kauli zake. Kwa maneno mengine kauli zetu ni njia mojawapo inayodhihirisha kama tumefanywa upya nia zetu au la, maana kimtokacho mtu ndicho kilichoujaza moyo wake.

  Ndugu Mkandya, Mungu azidi kukubariki kwa kulipanua somo hili la kufanywa upya nia zetu kwenda mbele na ndani zaidi ya kukiri tu ahadi za Mungu.

  Blessings,

  Patrick

 3. Patrick ufafanuzi na mifano uliyoitoa ni tofauti na mada yenyewe.
  Suala la kufanywa upya nia zetu halihusiani na kukiri ahadi za Mungu, bali ni suala linalohusu usafi wa moyo na kutenda haki.

  Kwa mfano kama mtu alikuwa mwizi, akiokoka anatakiwa kupata kipato kwa kufanya kazi halali.

  Yaani nia zetu ktk kuwaza na kutenda kwetu ziwe njema.
  Asante.

 4. Bwana Patrick,asante kwa somo zuri. Hata hivyo kichwa cha somo na ufafanuzi wako havihusiani kabisa.

  Unapoongelea suala la kufanywa upya kwa nia ya mkristo au mtu aliyezaliwa mara ya pili hakuhusiani sana na mtu huyo kumwamini Mungu kwa ajili ya ahadi zake. Bali kunahusiana zaidi na suala la mwenendo wa kitabia wa huyo mtu, ambako huzaa utakatifu.

  Kwamba badala ya mtu huyo kuwaza au kunia maovu ndani ya moyo au nia yake, anatakiwa anie mema.

  Kwa mfano badala ya kuwaza kwenda kuiba kama alikuwa mwibaji, anatakiwa awaze kufanya kazi halali ili kujipatia kipato chake, badala ya kuwa na choyo dhidi ya ndugu yake, anatakiwa kuwa na moyo wa ukarimu, badala ya kumwona mwanamke kama chombo cha starehe, amwone sasa kuwa ni mtu aliyeumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu, badala ya kuhubiri injili kwa nia ya kupata pesa, mtu ahubiri kwa ajili ya kuwafanya watu wamrudie Mungu, badala ya kuimba ili kupata sifa toka kwa watu, aimbe kwa ajili ya Mugu kupewa utukufu, badala ya kuongea matusi, mtu aongee maneno yenye kubariki asikiaye, nk.

  Kwa kifupi tunaambiwa tuwe na nia njema sawasawa na neno la Mungu kwa kila tulifanyalo.

  Hiyo ndiyo maana ya kufanywa upya kwa nia zetu. Ni suala ambalo kwa sehemu kubwa linahusiana na mambo ya utauwa au utakatifu.
  Ndio maana akasema kama ambavyo tulivitoa viungo vyetu kwa ajili ya kumtumikia shetani sasa tuvitoe viungo hivyohivyo kwa nia tofauti- yaani kwa nia ya kumtumikia Mungu.

  Kuwa mtu aliyekuwa anatumia ulimi wake kufanya umbea sasa autumie ulimi huohuo kwa ajili ya kumnena kristo, aaliyekuwa anatumiasauti yake kumwimbia shetani sasa aitumie sauti hiyihiyo kwa ajili ya kumwimbia Mungu, aliyetumia mwili wake kwa ajili ya kumchezea shetani sasa atumie mwili huohuo kwa ajili ya kumchezea Mungu, n.k

  Hayo ya kukiri ahadi sawasawa na neno la Mungu ni mambo tu ya kimaarifa,kwamba mtu akipata marifa ya neno la Mungu limesema nini juu ya suala linalomkabili atajua jinsi ya kuidai ahadi hiyo.

  Barikiwa.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s