UTOAJI: ANGALIA MADHUMUNI (MOTIVE) YAKO

bukobawadau
Wapendwa wana SG,

Ninamshukuru Mungu kwa kunijalia kuwashirikisha somo hili japo kwa ufupi.

Katika nyakati tunazoishi, swala la utoaji limekuwa ni mada kubwa katika makanisa mengi na kupitia mahubiri yanayorushwa kupitia vyombo vya habari vya Kikristo au vinavyofahamika hivyo. Watu wanahamasishwa kutoa kupitia mafundisho na maneno mengine yenye kutia hamasa. Katika mazingira hayo, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikitafakari kama tunapotoa huwa tunafanya hivyo kwa nia iliyo safi, inayompendeza Mungu tunayesema tunamtolea. Hii ndiyo inayopelekea tafakuri hii. Endelea kusoma!

Ninapozungumzia nia (motive) ya kutoa ninamaanisha lile jambo hasa ambalo linamfanya au KUMSUKUMA mtu kumtolea Mungu (au kutoa kwa imani kuwa anamfanyia Mungu), ambalo kama likiondolewa huyo mtu hatatoa.

Mungu ndiye kielelezo chetu katika swala zima la utoaji. Adamu na mkewe Hawa walipotenda dhambi pale katika bustani ya Edeni, Mungu alimtoa mnyama, akamchinja na kuwapatia ngozi ya kujisitiri (Mwanzo 3:21). Wakati tungali wenye dhambi, Mungu alimtoa Mwana wake wa pekee, Yesu Kristo, ili amwage damu yake kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu (Yohana 3:16). Hii ni mifano michache kati ya mingi ambayo inatuonyesha jinsi Mungu alivyo mtoaji. Yesu pia alipata kusema Mungu anawapatia jua na mvua watu wema na wabaya (Mathayo 5:45). Katika kutoa huko, Mungu anakufanya kwa sababu ya upendo, kwa lugha nyingine, ni upendo ndio unaomsukuma kutoa. Ndiyo maana Maandiko yako wazi kabisa kuwa, Mungu alifanya ule utoaji ulio mkuu kabisa (wa kumtoa Yesu Kristo Mwanae) kwa sababu ya upendo:

Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. (Yohana 3:16, msisitizo wangu)

Je, Mungu Baba alipomtoa Mwanae, tunaweza kusema kulikuwa na faida fulani aliyokuwa akiiwaza hata ikamsukuma kumtoa mwanae? Hapana. Sana sana waliokuwa wakifaidika na utoaji huo ni sisi wanadamu. Faida hiyo ni sisi kufanyika wana wake (Yohana 1:12-13) pamoja na ahadi zote zinazoambatana na hali ya kuwa wana wa Mungu (kwa mfano, soma 2 Petro 1:2-4).

Hebu tumwangalie na Yesu Kristo. Aliutoa uhai wake kwa sababu ya kutupenda tu na sio kutarajia faida fulani (Yohana 10:17-18). Na hata alipowapa watu mikate hakuna faida yoyote aliyoitarajia baadaye.

Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.  Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula.  Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. (Mathayo 14:14-20, msisitizo wangu)

Yesu angeweza kuruhusu umati ule wa watu uondoke kila mtu akajitafutie chakula, lakini kwa sababu ya upendo wake kwao, akaamua kuwapa chakula.

Si tu kwamba Mungu amekuwa akitoa kwa kusukumwa na upendo na si kwa sababu ya matarajio ya faida fulani, bali pia ndivyo ambavyo amekuwa akiagiza wanaomcha Yeye kufanya hivyo kwa kusukumwa na upendo. Upendo ndiyo iwe nia (motive) sahihi ya kutufanya tumtolee.

Tunasoma:

Bwana akanena na Musa, akamwambia,  Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. (Kutoka 25:1-2, msisitizo wangu)

Ni kweli kwamba Mungu ameahidi kuwabariki wale wanaotoa sawa sawa na mapenzi yake, lakini baraka hizo kamwe ZISIWE ndio sababu ya sisi kutoa. Tukumbuke kuwa Mungu anaichunguza mioyo yetu kuona nia zetu katika kila tulifanyalo:

Nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.(Ufunuo 2:23, msisitizo wangu)

Nia ya kufanya huduma na mambo mengine kwa ajili ya Mungu ni moja ya vigezo ambavyo vitatumika katika kupima kazi zetu siku ya kutolewa thawabu, na kazi zetu zikionekana hazifai zitateketea (soma 1 Wakorintho 3:9-15, hata hivyo hilo ni somo lililoko nje ya mada tuliyo nayo sasa).

Mambo yote tuyafanyayo, ikiwemo utoaji, hatuna budi kuyafanya kwa kusukumwa na upendo, vinginevyo ni kazi bure.

Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo. (1 Wakorintho 16:14, msisitizo wangu)

Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. (1 Wakorintho 13:1-3, msisitizo wangu)

Utajuaje kwamba unatoa kwa sababu ya kutaka baraka? Jibu ni rahisi! Jiulize, je kama ukiambiwa hakuna baraka za kimwili utakazozipata kwa sababu umetoa, je uko tayari kutoa fedha na mali zako kwa ajili ya kazi ya injili au kusaidia wapendwa wengine? Jibu unalo!

Hebu tuangalie Wakristo wa kanisa la kwanza walifanyaje katika swala la utoaji.

Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho mojawala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.   Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.  Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa,  wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.  Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,  alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume. (Matendo ya Mitume 4:32-37, msisitizo wangu)

Bila shaka Wakristo hawa walishirikiana kile walichokuwa nacho kuwasaidia wengine miongoni mwao waliokuwa na uhitaji kwa sababu walisukumwa na upendo, wakikumbuka maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo aliposema:

Amri mpya nawapa, MpendaneKama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.  Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu,mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi(Yohana 13:34-35, msisitizo wangu)

Upendo huu miongoni mwa jamii ya waaminio hauonekani kwa kauli tupu za “Nawapenda wote”, “Mungu awabariki”, na nyingine za jinsi hiyo. Unaonekana kwa vitendo. Tunasoma:

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.  Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitajiakamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?  Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. (1 Yohana 3:16-18, msisitizo wangu)

Wakristo wa kule Filipi walitoa vitu vyao kumsaidia mtume Paulo alipokuwa na uhitaji katika safari zake za uinjilisti:

Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi.  Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.  Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.  Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.  Lakini mlifanya vema,mliposhiriki nami katika dhiki yangu.  Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu.  Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja.  Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.  Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.  Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. (Wafilipi 4:10-19, msisitizo wangu)

Kuna mambo ya msingi ya kujifunza hapa:

1. Wakristo wa kule Filipi walimpenda na kumjali mtume Paulo na hivyo kufikiri jinsi ya kumsaidia. Katika Biblia ya Kiingereza, tafsiri ya King James, inasema:
But I rejoiced in the Lord greatly, that now at the last your care of me hath flourished again; wherein ye were also careful, but ye lacked opportunity. (Phillipians 4:10).

2. Upendo ule waliokuwa nao wapendwa wa kule Filipi uliwasukuma kushiriki na mtume Paulo katika dhiki aliyokuwa akiipitia ya uhitaji. Walishiriki dhiki hiyo kwa kutoa vitu na kumtumia, na sio maneno matupu ya ‘Mungu akubariki mpakwa mafuta wa Bwana’! Walifanya hivyo mara kadhaa na si mara moja tu na kumsahau.

3. Utoaji huu wa Wakristo wa kule Filipi ulimpendeza Mungu, na hilo ndilo ambalo lilimfanya Mungu awe tayari kuwabariki na kuwapa thawabu kwa matendo yao mema. Neno la Mungu linatuagiza tusichoke kutenda mema, hasa kwa jamii ya waaminio (Wagalatia 6:10). Baraka na thawabu hizi hazikuwa vitu vilivyowasukuma kutoa, bali matokeo ya utoaji wao uliosukumwa na upendo, jambo ambalo lilimpendeza Mungu.

Mtume Paulo alipokuwa akiwaandikia Wakristo wa kule Korintho (2 Wakorintho 8 – 9), alisimulia jinsi makanisa ya Makedonia walivyotoa kwa ukarimu mkubwa licha ya umaskini waliokuwa nao (2 Wakorintho 8:1-5), na kuwahimiza Wakristo wa Korintho wafanye vivyo hivyo (2 Wakorintho 8:7; 9:5).

Katika nyakati zetu kuna wahubiri wengi wanaowahimiza watu kumtolea Mungu kama watu wanaowekeza (invest) kwenye biashara. Mafundisho ya jinsi hiyo, ambayo sijaweza kuyapata katika Maandiko Matakatifu (kama nilivyojaribu kufafanua hapo juu), yanawafanya wale wanaoyapokea kumtolea Mungu kwa lengo la kutajirika. Kauli kama “Mtolee Mungu atazidisha mara mia moja (wakinukuu Mathayo 19:29), ukitoa shilingi elfu moja utapata laki moja, ukitoa shilingi laki moja utapata sh 100,000 x 100 = shilingi 10,000,000, ukitoa shilingi milioni moja utapata shilingi milioni 100″ kamwe haziwaelekezi watu kumtolea Mungu kwa sababu ya upendo wao kwake, kazi yake na watu wake bali zinawahimiza kutoa kwa ajili ya kupata faida. Na mara nyingi wahubiri wanaotoa kauli za jinsi hiyo huwaelekeza wanaowasikiliza kutoa kwenye huduma zao! Na kama utachukua hatua za ziada za kufuatilia maisha yao, aghalabu utakuta wengi wa wahubiri hao wanaishi maisha ya anasa mno kwa kiwango ambacho hata wasioamini wanabaki midomo wazi kwa mshangao!

Ni kwa nini tumefikia hapo?

Maandiko yanasema wazi wazi kuwa, katika siku za mwisho watu wengi watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha na kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu (2 Timotheo 3:1-5). Hali hii imewavaa hata wahubiri wengi wa kizazi hiki, ambao wamegeuza injili kuwa mradi wa kujinufaisha. Wanachokifanya wahubiri wa jinsi hii – Mungu awabariki wale wachache ambao bado wanamcha Yeye – ni kuhubiri mafundisho potofu yanayowapendeza watu walio wengi (2 Timotheo 4:1-4) na kuwaghilibu ili watoe pesa kwenye huduma zao, ili wahubiri hawa waweze kutajirika.

Kwamba watu tofauti huweza kuhubiri injili kwa nia na malengo tofauti ni jambo ambalo mtume Paulo aliliandika:

Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema.  Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili;  bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu.  Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. (Wafilipi 1:15-18, msisitizo wangu)

Kama watoto wa Mungu tunaotafuta kuishi sawa sawa na mapenzi ya Mungu, hatuna budi kumtolea kwa nia iliyo sahihi, nayo ni upendo wetu kwake, kazi yake na kwa jamii ya waaminio wenye uhitaji. Upendo ndio utusukume kufanya hivyo na si jambo jingine liwalo lote.

Mungu awabariki; asante kwa kusoma hadi mwisho!

–Joel

Advertisements

5 thoughts on “UTOAJI: ANGALIA MADHUMUNI (MOTIVE) YAKO

  1. Taswira na matendo yetu kwa mambo tuyafahamuyo uvyaweza kutazamwa kama chokaa iliyoporomoka na kutupwa nje ya mji. Mungu huyaondoa mawe mabovu nna kutia mengine yanayofaa; yenye ukweli; kupitia kwa kujitolea kwake Kristo, tumetakaswa, tukatiwa upyachokaa na kuongozwa naye Roho mtakatify jinsi ya kuishi kwa kuziegengea sheria za Mungu. Lakini tunaweza kuathirika na kuzuka kwa gonjwa liitwalo ukutabasi wa uongo na mawazo maovu.

  2. Bwana Yesu asifiwe, Mtumishi Mungu akubariki kwa somo lako zuri. Watu wengi sio wasomaji wa Neno la Mungu hivyo hutegemea sana wahubiri na wahubiri wanatumia nafasi hiyo kujinufaisha wenyewe. Ingekuwa vizuri kama somo hili lingewafikia wakristo wengi zaidi ili waelewe kuwa kutoa kunatoka rohoni kutokana na upendo alionao mtu kwa Mungu.

  3. Asante sana mtumishi wa Mungu Joel, nimesoma hadi mwisho , ukweli wako kwa habari ya kumtolea Mungu kwa upendo, tukitoa kwa upendo , na tukitoa kwa kufahamu kuwa Mungu ametubariki hili tuwe baraka , na pia tukitoa kwa kutii neno lake linachosema , Hapo baraka zake zitazidi kuja kwetu hata pasipo kumshikia Mungu bango kuwa nimempa fulani na mimi nipe mara mia , Mungu anapoangalia ndani ya moyo wako , na akiona umetoa kwa upendo na uhaminifu na utii hakika atalitendea kazi , Uzuri wa Mungu wetu anaangalia ndani ya moyo ,1 Sawmeli 16:6. Bwana aangalii kama binadamu aangaliavyo ,maana wanadamu uitazama sura ya nje bali Bwana uitazama mioyo. Na kwa Kain na Abel Mungu aliona ni nani aliyetoa sadaka ya kweli, Juzi tu niliongea na mama fulani rafiki yangu akasema nimejiandikisha kumtolea kutoa kiasi fulani cha pesa kanisani, mchungaji ametangaza kuwa walio na kiasi fulani wasimame watoe au waaidi, na walio na kiasi fulani nao wasimame watoe au waahidi, akataja makundi kama matatu ya kiasi cha pesa kubwa, nikamuuliza hivi unapotoa unamtolea mchungaji au Mungu? , akasema Mungu nikasema sasa kwa nini kujiandikisha maana mimi ninalojua utoaji ni kati ya mtu na Mungu wake , kama unamtolea Mungu , nikasema hakuna mchungaji wa kuniambia nitoe kiasi fulani , nikasema unapokuwa umetoa kwa namna hiyo unakuwa umempa mchungaji siyo Mungu maana Mungu anasema kuwa kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake , si kwa uzuni wala kwa kulazimishwa , maana Mungu umpenda yule atoaye kwa moyo wa ukunjufu, na pia anasema apandaye haba atavuna haba , apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu2 kolintho 9:6-7, kwa hiyo hapo ni kuangalia una nini mfukoni , na ninamuomba Roh mtakatifu anisaidie kujua ni kiasi gani nimtolee Mungu wangu, hii ni muhimu maana wapo watu wengine wana pesa ya kutosha mfukoni lakini unakuta ikifika kumtolea Mungu wanampa hile change iliyobaki jana usiku watoto walipoenda kununua mafuta ya taa, hapo sasa ndipo inabidi tujifunze kumtolea Mungu kwa upendo, nimejifunza kwa dada yangu mmoja amenipa darasa na ni mfano wa kuigwa , alisema kuwa yeye alipokuwa shule wazazi wake wanamtumia pesa ya matumizi alikuwa haitumii yote , anachukua kiasi fulani anabana matumizi na kiasi kikubwa alikuwa anawasaidia watumishi wa Mungu wanaofanya kazi ktk mazingira magumu sana kule vijijini. Hapo unaona dada huyu alikuwa akitoa kwa moyo wa upendo , alikuwa anawatanguliza wengiene kabla yake, na huu ndiyo upendo kamili na Mungu anapenda tunapomtolea kwa style hii. Mungu amemuona yule dada sasa hivi yuko USA. anaendelea kumtafuta Mungu kwa nguvu zake zote, na anaendelea kufaidi matunda ya wokovu pia Mungu anaendelea kumtumia kwa jinsi ya ajabu kabisa kusaidia wengine anaishi maisha matakatifu sifa na utukufu ni kwa Bwana ,. Sisemi kuwa kila mtu Mungu atamfanya aende Marekani kama alivyomfanyia huyu dada yangu, lakini nasema Mungu anaona tunapomtolea kwa uhaminifu na upendo , na ukalimu , tunapokuwa na mzigo wa kusaidia wengine anaona kabisa. hii tabia ya wachungaji kusema toa kiasi fulani inasikitisha maana wapo watu ambao wana nia na hamu ya kumtolea Mungu lakini mfukoni wana shilingi 1000 tu, au mia tano, je hawa hawawezi kubarikiwa? au je wasimtolee Mungu kwa vile wana kiasi kidogo? lakini mtumishi anaposimama akatangaza kabisa kuwa wanaotaka kutoa kiasi fulani wasiamame anakuwa anawadhalilisha wasio na pesa nyingi, na pia anaweza kuzuia baraka zao, na pia hii inaonyesha kabisa kuwa ukitoa pesa kubwa wewe ndiye utakuwa na jina kanisani, wanasaau kuwa Bwana alisema ktk Matayo 6:1 tusifanye mema machoni pa watu kusudi mtazamwe na wao, kwa maana mkifanya hivyo hampati thawabu kwa baba yenu aliye mbinguni. Tuombeane wapendwa ktk kipengere cha kumtolea Bwana , maana wengi wetu bado hatujapata uhuru na kujifunza kuhusu kumtolea Mungu. Nawapenda nyote.

  4. Namshukuru Mungu kwa kukufunulia neno lake, hakika nimejifunza na nimebarikiwa sana na neno hili. Roho wa Mungu aendelee kukuongoza daima. Ubarikiwe

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s