Mashamba ni meupe, Mavuno yapo tayari!

mhubiri

Wapendwa, badala ya kuishia kulalamika tukisema “watu wamezidi kuwa na mioyo migumu”, au “watu wamejaa dhambi tu” au “hawataki kumwamini Yesu” au “uasi umeongezeka” na hivyo kuishia kuwakatia tamaa kwamba wamepitiliza hata kuja kumgeukia Bwana Yesu na kuokoka ni vigumu, tuwe na mtazamo wa Bwana Yesu mwenyewe:

37 Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.  – Mathayo 9:37 SUV

Bwana Yesu hakuishia hapo bali alituachia na maelekezo ya jinsi ya kuomba kwa suala la mavuno, badala ya kumwomba Mungu atuletee mavuno, yaani watu wapate kumjua na kumwamini Bwana Yesu, tunapaswa kumwomba Mungu apeleke au atume watendakazi kwenye mavuno yake kwa ajili ya kuvuna kwani mavuno yapo tayari tena yameshaiva.

35Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. – Yohana 4:35b SUV

38 Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. – Mathayo 9:38 SUV

Isitoshe, tumepewa Agizo Kuu la kuihubiri Injli kwa kila kiumbe (Marko 16:15) na mamlaka ya kulitekeleza hilo tumekabidhiwa. Bwana Yesu ameahidi kuwa nasi hata ukamilifu wa dahari hivyo tusibakie kujifungia kuomba tuuuuu watu waokoke au waje kanisani kwetu, hapana tukishaomba tutoke tuwafuate huko waliko. Inasikitisha kuona kuna huduma zilizojikita katika kufunga na kuomba tu ili watu waokoke na kufunguliwa toka vifungo vya ibilisi badala ya kutii Agizo Kuu la Bwana Yesu la kuihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Naomba nieleweke, kufunga na kuomba ni vizuri sana hakupingani na Maandiko, ila hatuwezi kutumia kufunga na kuomba kama mbadala wa kutii Agizo la Mungu kwetu la kuwa mashahidi wake na kuihubiri Injili, hilo siyo sahihi. Katika hizi zama za Agano Jipya sisi ni ukuhani wa kifalme, hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kuwa mwombaji na pia shahidi wa Kristo, hatuko katika zama zile za kujifungia hekaluni kuomba kama ilivyokuwa kabla ya Kristo kuja na kutupatanisha naye kwa njia ya kifo chake pale msalabani na ufufuo wake.

Bwana Yesu alituagiza tuihubiri Injili kwani Injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye. Tusiishie tu kuomba Mungu adhihirishe uweza wake kupitia kwetu, badala yake tumruhusu audhihirishe uweza wake kwa kuihubiri Injili, kumbuka “Injili ni uweza wa Mungu…” Warumi 1:16

Bwana Yesu alikwenda katika miji yote na vijiji hakusubiri watu wamjie kwenye Sinagogi au kule Hekaluni Yerusalemu, Mitume na Kanisa la mwanzo nao walianzia pale walipokuwa na kisha wakatoka wakawaendea watu kila mahali na wakiwaletea Habari Njema za wokovu.

Mavuno ni mengi na tena yapo tayari kabisa, tatizo siyo uhaba wa mavuno bali ni uhaba wa watendakazi.

mhubiri

Wapo wengi wanaomwamini Bwana Yesu,  wapo wengi wanaomshabikia, wapo wengi wanaomwita “Bwana,Bwana”, wapo wengi wanaopenda kuzipokea baraka zake maishani mwao, na pia wapo wengine wenye “huduma zao” ila siyo watendakazi ambao Bwana anawahitaji kwa ajili ya mavuno yake.

Wapendwa, nashauri tuache kumshabikia tu Bwana Yesu, tumwamini kikwelikweli, tukubali kuongozwa na Roho wake Mtakatifu tusiendekeze matendo ya mwili ambayo ni pamoja na ubinafsi – ile hali ya “mradi nishaokoka na kubarikiwa mimi basi wengine watajijua”! Tukiongozwa na Roho Mtakatifu basi hata ule upendo wa Mungu uliomiminwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu (Warumi 5:5) utatufanya tuwapende wengine na kutaka na wao waupate wokovu.

Mavuno yametuzunguka kila kona hatuna haja ya kwenda mbali kuyaona, ni kiasi tu cha “kuinua macho na kutazama…” hapo ulipo, kuwa mtenda kazi, anza kuvuna. Pengine unajiuliza, sasa nifanyeje basi? Ni rahisi tu: Washirikishe kile ambacho Bwana Yesu amekifanya maishani mwako – wewe ni shahidi wake (Matendo 1:8) na shahidi husema alichoshuhudia yeye mwenyewe. Ikiwa Bwana Yesu amekuokoa, amekuponya, amekutendea muujiza au wema wowote, uaminifu wake umeuona, ni vizuri kuwashirikisha wale wasiomjua na Roho Mtakatifu atautumia ushuhuda wako kuwavuta kwake.

Wapendwa, tungalipo ulimwenguni sisi ni nuru ya ulimwengu hivyo tuifanye kazi ya Mungu maadam ni mchana maana usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. (Yohana 9:4)

Mbarikiwe,

Patrick.

Advertisements

One thought on “Mashamba ni meupe, Mavuno yapo tayari!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s