Familia ya Kikristo

familia

Ni dhahiri kwamba Mungu ndiye aliyeleta wazo la familia. Basi, ni halali kutazamia kwamba atatupa maelekezo jinsi familia zinavyotakiwa kuishi na kutuonya juu ya matatizo yanayoweza kuangamiza au kuharibu familia. Bwana ametupa kanuni nyingi sana katika Neno Lake kuhusu jinsi familia inavyotakiwa kuwa, na wajibu wa kila mshirika katika familia. Maagizo hayo ya KiBiblia yanapofuatwa, familia zitapata baraka zote ambazo Mungu alikusudia wazifurahie. Zinapovunjwa, matokeo yake ni maumivu makali moyoni, na vurugu.

Nafasi Ya Mume Na Mke

Mungu amepanga kwamba familia ya Kikristo iwe katika mfumo fulani. Kwa sababu mfumo huo unaleta uthabiti katika maisha ya familia, Shetani hufanya kazi sana kupotosha mpango aliokusudia Mungu.

Kwanza kabisa ni kwamba, Mungu amepanga mume awe kichwa cha familia. Hii haimpi mume ruhusa ya kutawala mke wake na watoto katika ubinafsi. Mungu amewaita waume kupenda, kulinda, kutimiza mahitaji na kuongoza familia zao kama kichwa. Pia, Mungu alikusudia wake wawe watiifu kwa uongozi wa waume zao. Hili ni wazi, kama Maandiko yanavyosema.

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).

Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila, katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu.

Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama Paulo anavyosema, ni katika kila jambo. Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana dhamiri yake. Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri yake. Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa kuchagua kumtii Yesu.

Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao mara zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12). Maandiko pia yanataja jinsi Abigaili alivyoacha kumtii Nabali mumewe, aliyekuwa mpumbavu, na kwa kufanya hivyo aliepusha tatizo (ona 1Samweli 25:2 – 38).

Neno La Mungu Kwa Waume

Mungu anawaambia hivi waume:

Enyi waume, wapendeni wake zetu kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe, maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. … Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe (Waefeso 5:25, 28-30, 33).

Waume wanaagizwa kuwapenda wake zao kama Kristo anavyolipenda Kanisa. Si wajibu mdogo huo! Mke yeyote atajinyenyekeza kwa furaha kabisa kwa mtu anayempenda kama Yesu – aliyetoa uhai Wake kwa sababu ya upendo wa kujitoa. Sawa na jinsi Kristo anavyoupenda mwili Wake – yaani Kanisa – ndivyo na waume wanavyotakiwa kumpenda mwanamke ambaye ni “mwili mmoja” nao (Waefeso 5:31). Kama mume Mkristo anampenda mkewe kama anavyopaswa, atamtimizia mahitaji yake, atamtunza, atamheshimu, atamsaidia, atamtia moyo, na atatumia muda kuwa naye. Akishindwa katika wajibu wake kumpenda mkewe, mume huyo yuko hatarini kuzuia majibu ya maombi yake mwenyewe.

Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe (1Petro 3:7. Maneno mepesi kukazia).

Kihalisi ni kwamba hapajawahi kuwepo na ndoa isiyokuwa na kutokuelewana na shida mbalimbali. Ila, kwa kujitoa na kukuza tunda la Roho katika maisha yetu, waume na wake wanaweza kujifunza kuishi kwa maelewano na amani, na kufikia mahali pa kutambua baraka zinazozidi kuongezeka za ndoa ya Kikristo. Kila mwenzi anaweza kukua na kufikia ukomavu mkubwa katika kufanana na Kristo kutokana na matatizo yasiyoepukika yanayotokea katika ndoa zote.

Kwa maelezo zaidi juu ya wajibu na majukumu ya waume na wake, tazama Mwanzo 2:15-25; Mithali 19:13; 21:9, 19; 27:15, 16; 31:10-31; 1Wakor. 11:3; 13:1-8; Wakolosai 3:18, 19; 1Timo. 3:4, 5; Tito 2:3-5; 1Petro 3:1-7.

Tendo La Ndoa

Mungu ndiye mwanzilishi wa tendo la ndoa, na ni dhahiri kwamba aliliumba ili kustarehesha na kusaidia katika uumbaji. Pamoja na hayo, Biblia inatamka wazi kwamba tendo la ndoa ni la kufurahiwa na wale walioungana pamoja katika agano la ndoa, la kudumu.

Kukutana kimwili nje ya mipaka ya ndoa huitwa zinaa au uasherati. Mtume Paulo alisema kwamba wale watendao mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-11). Ingawa Mkristo anaweza kujaribiwa na pengine kufikia kuanguka katika tendo la uzinzi au uasherati, atajisikia hatia kubwa sana rohoni mwake, itakayompelekea kutubu.

Paulo pia alitoa mafundisho wazi kabisa kuhusu majukumu ya mume na mke kwa mwenzake, kuhusu tendo la ndoa.

Lakini kwa sababu ya zinaa, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe. Vivyo hivyo, mume hana amari juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:2-5).

Mistari hii inaweka wazi kabisa kwamba tendo la ndoa lisitumiwe kama “zawadi” na mume au mke, maana hakuna mwenye mamlaka juu ya mwili wake mwenyewe. Tena, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Si dhambi wala najisi inapokuwa katika ndoa. Paulo aliwatia moyo Wakristo wenye ndoa kushirikiana kimwili. Tena, tunapata ushauri huu kwa waume Wakristo katika kitabu cha Mithali:

Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake ytakutoshe siku zote; na kwa upendo wake ushangilie daima (Mithali 5:18, 19).

Kama wanandoa Wakristo wanataka kufurahia mahusiano kimwili yenye kutosheleza, waume na wake wanahitaji kuelewa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya wanaume na wanawake kwa habari ya kushirikiana kimwili. Kiasili, mwanamume ni mtu wa kimwili sana kwa habari ya kukutana kimwili. Asili ya mwanamke kwa habari ya kukutana kimwili ni kitu cha hisia. (ona Mathayo 5:28 na 1Wakor. 7:1). Wanaume huvutiwa na wanawake wanaowapendeza macho; ila wanawake huvutiwa na wanaume wanaowapendeza kwa sababu zaidi ya kuvutia kimwili. Hivyo, wanawake wenye busara hupendeza ili kuwavutia waume zao wakati wote. Na waume wenye hekima huonyesha upendo wao kwa wake zao kutwa nzima kwa kuwakumbatia na kuwatendea mambo ya ukarimu, badala ya kuwatazamia wake zao “kuwa tayari”

Ni muhimu sana kwa waume Wakristo na wake zao kuzungumza kuhusu mahitaji yao kwa uwazi, na kujifunza juu ya tofauti zao kiasi wanachoweza. Mahusiano kimwili kati ya waume na wake yanaweza kuwa baraka inayozidi kuongezeka kutokana na mawasiliano ya miezi mingi na miaka, na kugunduana na kuzoeana.

Watoto Wa Familia Ya Kikristo

Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kunyenyekea na kutii kabisa wazazi wao Wakristo. Wakifanya hivyo, wameahidiwa maisha marefu na baraka zao.

Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso 6:1-3).

Akina baba Wakristo kama vichwa wa familia zao, wanapewa wajibu wa msingi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivi:

Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana (Waefeso 6:4).

Ona kwamba wajibu wa baba ni wa namna mbili: kuwalea watoto wake katika adabu na maonyo ya Bwana. Hebu tuanze kwa kutazama haja ya kuwafundisha watoto adabu.

Nidhamu Ya Watoto

Mtoto asiyetiwa nidhamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa mbinafsi na muasi kwa mamlaka. Watoto wanapaswa kutiwa nidhamu wakati wowote wanapoacha kwa makusudi kutii sheria halali zilizowekwa na wazazi wao. Watoto wasiadhibiwe kwa makosa au kutowajibika kwa sababu ya utoto. Lakini, watakiwe kukabiliana na matokeo ya makosa yao na kutowajibika kwao, na kwa njia hiyo kuwasaidia kujiandaa kwa ajili ya uhalisi wa maisha ya utu uzima.

Watoto wadogo wanapaswa kuadhibiwa kwa kiboko, kama Neno la Mungu linavyofundisha. Lakini watoto wachanga wasipigwe viboko. Hii haina maana kwamba watoto wachanga waruhusiwe kufanya wanachotaka. Inatakiwa tangu wanapozaliwa wajue kwamba mama na baba ndiyo wenye mamlaka. Wanaweza kufundishwa wakiwa wadogo sana maana ya neno “hapana” kuwakuwakataza tu kufanya kitu wanachofanya, au wanachotaka kufanya. Wakianza kuelewa maana ya neno “hapana”, wanaweza kuchapwa kofi dogo tu matakoni ili kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi wanapoendelea kufanya kile ambacho wazazi wanasema kisifanywe. Kama hayo yatafanyika kwa utaratibu na mara kwa mara, watoto watajifunza kuwa watiifu tangu umri mdogo sana.

Pia, wazazi wanaweza kuonyesha mamlaka yao kwa kutounga mkono tabia zisizotakiwa za watoto wao. Mfano ni kuwapa mara moja kitu wanachotaka, wakilia. Kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto walie ili wapate matakwa yao. Au, kama wazazi watakubaliana na madai ya watoto wao kila mara wanaponuna au kukasirika ni kwamba wanawatia moyo kuendelea na tabia hiyo isiyotakiwa. Wazazi wenye hekima huunga mkono tabia nzuri tu katika watoto wao.

Kuchapa kiboko kusilete madhara kimwili, ila kusababishe maumivu ya kutosha kumfanya mtoto yule asiyetii kulia kwa muda kidogo. Kwa njia hiyo, mtoto atajifunza kuunganisha uchungu na kutokutii. Hata Biblia inaunga mkono hilo.

Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema. … Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. … Usimnyime mtoto wako mapigo; maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa nafasi yake na Kuzimu. … Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye (Mithali 13:24; 22:15; 23:13-14; 29:15).

Wazazi wanaposimamia sheria zao, hawana haja ya kuwatisha watoto ili kuwafanya watii Mtoto anapoacha kutii kwa makusudi, achapwe fimbo. Ikiwa mzazi atatishia tu kumchapa mtoto wake ambaye si mtii, anachofanya ni kuunga mkono uasi wa mtoto wake. Matokeo ni kwamba mtoto anajifunza kutokujali utii mpaka vitisho vya wazazi wake vya maneno vinapofikia kiwango fulani cha sauti.

Baada ya kiboko, mtoto anapaswa kukumbatiwa na kuhakikishiwa upendo wa mzazi aliyemchapa.

Mlee Mtoto

Wazazi Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kuwafundisha na kuwalea watoto wao, kama tunavyosoma katika Mithali 22:6, kwamba: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (maneno mepesi kukazia).

Kulea (au kufundisha) si kuadhibu tu mtoto anapoacha kutii, bali ni kumpongeza pia wakati anapofanya vizuri. Watoto kila wakati wanahitaji kusifiwa na wazazi wao ili kuunga mkono tabia zao njema, na mambo mazuri wanayofanya. Watoto wanahitaji kuhakikishiwa mara kwa mara kwamba wanapenda, wanakubalika na kufurahiwa na wazazi wao. Wazazi wanaweza kuonyesha upendo wao kwa kusifu, kuwakumbatia na kuwabusu watoto, na kwa kutumia muda mwingi nao.

“Kulea” maana yake “kufanya atii.” Basi, wazazi Wakristo wasiwape watoto wao uchaguzi kama watakwenda kanisani au kuomba kila siku au hapana. Watoto hawana ufahamu wa kutosha kujua kinachowafaa, au kilicho bora. Ndiyo sababu Mungu aliwapa wazazi. Wazazi watakaofanya bidii na kuweka juhudi na nguvu zao kuhakikisha kwamba watoto wao wanalelewa vizuri, wana ahadi kutoka kwa Mungu kwamba watoto wao hawataacha njia iliyo sawa hata wakiwa wakubwa, kama tulivyosoma katika Mithali 22:6.

Pia, watoto wanapaswa kuongezewa majukumu wanavyozidi kukua. Lengo la mzazi mwenye kufanikiwa ni kumwandaa mtoto hatua kwa hatua ili kuwajibika kabisa akiwa mtu mzima. Mtoto anapozidi kukua, apewe uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Tena, yule kijana mkubwa anapaswa kuelewa kwamba daima akubali wajibu utokanao na maamuzi yake, na kwamba wazazi wake hawatakuwepo siku zote “kumwokoa” katika matatizo.

Wajibu Wa Wazazi Kufundisha

Kama tusomavyo katika Waefeso 6:4, akina baba si tu kwamba wanawajibika kuwafundisha adabu watoto wao, bali pia wanatazamiwa kuwafundisha katika Bwana. Si wajibu wa kanisa kumpa mtoto mafundisho kuhusu maadili ya KiBiblia, tabia za Kikristo au theolojia – ni kazi ya baba. Wazazi wanaoachia wajibu wote kwa mwalimu wa Shule ya Jumapili awafundishe watoto wao kuhusu Mungu wanakosea sana. Mungu aliwaamuru Waisraeli hivi, kwa njia ya Musa:

Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo (Kumbu. 6:6, 7. Maneno mepesi kukazia).

Wazazi Wakristo wawafundishe watoto wao kuhusu Mungu tangu wakiwa wadogo, wakiwaambia Yeye ni nani na anawapenda kiasi gani. Watoto wadogo wafundishe habari za kuzaliwa kwa Yesu, maisha Yake, kifo na kufufuka Kwake. Watoto wengi wanaweza kuelewa ujumbe wa Injili wanapokuwa na umri wa miaka mitano au sita, na wanaweza kufanya uamuzi wa kumfuata Kristo. Baada ya hivyo (wakiwa na miaka sita au saba, na wakati mwingine hata wakiwa wadogo zaidi), wanaweza kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha kama ishara kwamba wamejazwa. Pamoja na hayo, hatuwezi kuweka sheria kuhusu jambo hili kwa sababu kila mtoto yuko tofauti. Ila hoja ni kwamba, wazazi Wakristo wanapaswa kutoa nafasi ya kwanza kwenye kuwafundisha watoto wao mambo ya kiroho.

Amri Kumi Za Kuwapenda Watoto Wako

1). Usiwatie watoto wako mahali pagumu (ona Waefeso 6:4). Watoto wasitazamiwe kutenda kama watu wazima. Ukitazamia mengi kupita kiasi kutoka kwa watoto wako, wataacha kujitahidi kukupendeza maana wanajua haiwezekani.

2). Usilinganishe watoto wako na watoto wengine. Wajulishe jinsi unavyofurahia sifa zao za kipekee na karama au vipaji vyao kutoka kwa Mungu. Wakubali wao kama wao.

3). Wape majukumu nyumbani, ili wajue kwamba wao ni sehemu muhimu sana ya familia hiyo. Kufanikiwa ni matofali yanayojenga kujiamini katika maisha ya mtu.

4). Tumia muda kuwa na watoto wako. Hiyo inawajulisha kwamba wao ni wa maana kwako. Kuwapa vitu haichukui nafasi ya wewe kujitoa kwao. Tena, watoto hushawishiwa zaidi na wale wanaokaa nao muda mwingi.

5). Ikibidi useme kitu kibaya, jaribu kukisema kwa uzuri. Mimi sikuwahi kuwaambia watoto wangu kwamba ni “wabaya” walipoacha kunitii. Badala yake, nilikuwa namwambia hivi kijana wangu, “Wewe ni mtoto mzuri, na watoto wazuri hawafanyi ulichofanya!” (Kisha nilikuwa namchapa kiboko.)

6). Tambua kwamba, neno “hapana” linamaanisha “ninakujali”. Watoto wanaporuhusiwa mambo yao kila wakati wanatambua kwama hujali kiasi cha kutosha kuwakataza chochote wakati wowote.

7). Tazamia watoto wako kukuiga wewe. Watoto hujifunza kwa mifano ya wazazi wao. Mzazi mwenye busara hawezi kumwambia mtoto wake, “Fanya ninavyokwambia. Usifanye kama ninavyofanya mimi.”

8). Usiwaokoe watoto wako na matatizo yao yote. Ondoa mawe yanayoweza kuwakwaza tu; acha mawe ya kukanyagia yabakie mbele yao.

9). Mtumikie (na kumfuata) Mungu kwa moyo wako wote. Nimeona kwamba watoto wa wazazi waliopoa kiroho huwa hawamfuati Mungu wakiwa watu wazima. Watoto Wakristo wa wazazi ambao hawajaokoka, na watoto wa wazazi Wakristo waliojitoa kabisa kwa Mungu huendelea na wokovu hata “wakiondoka kwenye kiota” – nyumbani.

10). Wafundishe watoto wako Neno la Mungu. Mara nyingi wazazi hutoa nafasi ya kwanza kwa elimu ya watoto wao, na kushindwa kuwapa elimu ya muhimu zaidi wanayoweza kupata – elimu ya Biblia.

Nafasi Ya Huduma, Ndoa Na Familia

Pengine kosa kubwa la kawaida kabisa lifanywalo na viongozi wa Kikristo ni kutokujali ndoa zao na familia zao kwa sababu ya kujitoa kwenye huduma. Wanajihesabia haki kwa kusema kwamba kujitoa kwao “ni kwa ajili ya kazi ya Bwana.”

Kosa hili hurekebika wakati mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anapotambua kwamba utii wake halisi na kujitoa kwake kwa Mungu huonekana kwa mahusiano yake na mke wake na watoto. Mtumishi hawezi kudai kwamba amejitoa kwa Mungu ikiwa hampendi mke wake kama Kristo anavyolipenda kanisa, au kama atapuuzia kutumia muda unaotakiwa na watoto wake, ili kuwalea na kuwakuza katika kicho na kumcha Bwana.

Tena, kumpuuza mwenzi na watoto kwa sababu ya “huduma” ni ishara ya huduma ya kimwili kabisa, inayofanywa kwa nguvu za mtu binafsi. Wachungaji wengi wenye makanisa wanaobeba mizigo mizito ni mfano wa hili, maana wanajichosha ili kuhakikisha kwamba kila utaratibu wa kanisa unakwenda vizuri.

Yesu aliahidi kwamba mzigo Wake ni mwepesi na nira Yake ni laini (ona Mathayo 11:30). Hamwiti mtumishi yeyote kuonyesha anavyopenda dunia au anavyolipenda kanisa kwa kutowapenda watu wa familia yake. Sifa mojawapo ya mzee ni kwamba, “awe mwenye kuisimamia nyumba yake vema” (1Timo. 3:4). Mahusiano yake na familia yake ni kipimo cha uwezo wake kufanya huduma.

Wale walioitwa kufanya huduma za kusafiri na ambao inawabidi kuwa nje ya nyumbani mara kwa mara lazima watumie muda wa ziada kufikiri kuhusu familia zao wanapokuwa nyumbani. Washirika wengine katika mwili wa Kristo wafanye kinachowezekana ili kufanikisha hilo. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anatambua kwamba watoto wake mwenyewe ndiyo wanafunzi wake wa kwanza. Akishindwa hapo, hana haki ya kujaribu kuwafundisha wengine walio nje ya nyumbani mwake kuwa wanafunzi.

–David Servant

Advertisements

4 thoughts on “Familia ya Kikristo

 1. Bwana Yesu asifiwe sana!

  Hekima ya Mungu aliye hai ni ya ajabu na inatisha mno!Ni Moto ulao yaani Moto
  unaoteketeza ujinga na upumbavu wote wa wanadamu.Hekima ya Mungu ni Yesu(1WAKORINTHO 1:30).Lakini pia Yesu ni HAKI,UTAKATIFU na UKOMBOZI.Yesu
  ni NENO la Mungu(YOHANA 1:1,14).Kwahiyo kulingana na mchanganuo huu,Neno
  la Mungu ni HEKIMA,HAKI,UTAKATIFU na UKOMBOZI unaoteketeza ujinga na upumbavu ulio ndani ya nafsi zetu.Kwakuwa Neno la Mungu ni Roho na tena ni uzima(YOHANA 6:63).Basi,HEKIMA,HAKI,UTAKATIFU na UKOMBOZI ni Roho ya uzima.Kazi ya Roho ya uzima ndani ya mioyo yetu ni kutuwezesha kufundishana
  na kuonyana tukiwa tumesimama katika UKOMBOZI,HAKI,UTAKATIFU na HEKIMA
  YA YESU (WAKOLOSAI 3:16).Tunapopishana katika kufundishana na kuonyana ni
  dhahiri kwamba kuna changamoto katika utendaji wa Roho ya uzima inayotamani
  sana KUZIWEKA HURU NAFSI ZETU(2 WAKORINTHO 3:17).

  Tusipokubali kuishi ndani ya UNYENYEKEVU WA YESU(WAFILIPI 2:3-4),nafsi zetu
  zitaendelea kubaki katika utumwa wa kutolielewa NENO LA KRISTO.Siku zote kinachotafutwa na shetani na wajumbe wake ni KUHARIBU UNYENYEKEVU WA NAFSI ZA WATEULE WA MUNGU.Ndiyo maana nafsi zetu zinatawaliwa na MASHINDANO,UBINAFSI,MAJIVUNO,KIBURI,DHARAU,JEURI NA UKAIDI.ROHO YA KUJIFANYA TUNALIJUA SANA NENO LA MUNGU NDIYO INAYOTAWALA NAFSI
  ZETU KULIKO ROHO WA KRISTO!!! Matokeo yake tunajichanganya wenyewe na
  kuwavuruga kabisa wale wanaojifunza kutoka kwetu ambao bado hawajaweza
  kupambanua ya mkono wa kushoto na wa kulia,naomba tuwe na huruma!(YONA 4:11).Mungu aturehemu na pia atusaidie kuwa na roho ya unyenyekevu ili tuijue
  KWELI YOTE.

  Somo hili la FAMILIA YA KIKRISTO ni nyeti mno kwasababu LINATUFUNULIA
  SIRI YA NDOA ZA WATEULE NA NDOA KATI YA KRISTO NA KANISA.Ni siri nzito
  na ya kutisha sana inayoitwa ROHO YA UTII.Ni siri ambayo shetani na wajumbe
  wake wanaangaika usiku na mchana kuifunika na wanachokifanya ni kuifundisha katika madhehebu zao kwa namna isiyo sahihi ili KIMILIKI IMANI ZA WATEULE
  WALIOWACHUKUA MATEKA.ROHO YA UTII ndiyo iliyoficha siri ya IMANI ILIYO HAI.
  Aliyeleta somo hili na kuliweka mezani na mchangia mada wa pili WANAZUNGUMZA
  LUGHA MOJA isipokuwa njia wanazopita ni tofauti lakini maana ni ile ile!!

  Mungu wangu awabariki wateule wote wanaoendelea kulitafakari somo hili.
  Ni lazima tukubali kwamba sisi ni wanafunzi na mwalimu wetu ni mmoja tu
  anaitwa ROHO MTAKATIFU(1 YOHANA 2:20,27).

 2. Mtumishi David,

  Mimi binafsi nimeona kuwa katika somo hili “Familia ya Kikristo” umetumia akili zaidi, lakini kiukweli vipo vituvitu kadhaa ambavyo vinabidi uvitazame upya kwa kuzingatia zaidi Neno na uviweka sawasawa, kwakuwa somo hili ni ‘Biblia nzima’, nikimaanisha kuwa somo hili linagusa Roho na Mwili. Umesema sawa kuwa mwanzilishi wa ndoa ni Mungu mwenyewe, ambapo kufahamu mwanzo wa hilo inabidi kurudi katika ile Bustani ya Edeni.

  Niseme, “kuingia na kutoka kwako ndiko kunaninyima usingizi”. Ndugu yangu, ukiingia ingia tu, lakini mara unafungua mlango unaingia mara tena unafungua mlango unatoka, mimi nashindwa kupata ‘Utulivu’! Labda niseme hivi; Kwanza ieleweke wazi kuwa Biblia haiongelei watu walio nje ya “Kanisa” Kwa hiyo unapozungumzia Familia ya Kikristo ni lazima iwe ni Familia inayotakiwa na Biblia (Neno la Mungu) na si vinginevyo. Vitu ninavyoviona umeviacha bila kuwa sawa, kwa ujumla ni kama ifuatavyo:-

  Umesema, “Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila, katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu”
  kabla ya kusema hivyo umenukuu Biblia pale panaposema hivi, “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).”
  Hapo ndipo ninapoona unaingia na kutoka! Mwanamke ni mwili wa mmewe, lakini mwili hauwi hai usipokuwa na roho. Kristo anatiiwa kwa vyote kwa mwili na roho, roho hutii na mwili hutumika ili kuthibitisha ule utii wa rohoni (Imani na matendo), vivyo hivyo mme naye anapaswa kutiiwa na mkewe kwa vyote yaani mwili na roho (Imani na matendo), kwasababu kama Kristo ni roho ya kanisa, basi na mme ni roho kwa mkewe! Maana kukiwa na kukinzana kati ya mwili na roho kitendo hicho hutokeza matokeo hasi. Kwa hiyo, kutii kunaanzia rohoni na ndipo mwili hutokeza nje kutii huko, utaona kuwa, bila utii hakupo kupendwa, ingawa Kupenda hutangulia bila kuuona utii!
  Biblia inasema “bila roho mwili hauwezi kuwa hai” Kristo ni Roho katika kanisa, kanisa ni mwili wa Kristo, kwa hiyo, bila Kristo kanisa haliwezi kuwa hai! Lakini kichwa cha mwanamme ni Kristo, hivyo bila Kristo mme hawi ‘hai’; Kumbe kama ndivyo hivyo, Mme ni kichwa cha mkewe na mke ni mwili wa mme, basi utaona kuwa mwanamke roho yake ni mmewe! Biblia inasema, “Natamaa yako itakuwa juu ya mmeo, naye atakutawala” Tamaa hutokana na mwili, lakini roho ndiyo inapaswa itawale, maana inauwezo wa kama tamaa hiyo itokeze kile ilichotamani ama tamaa hiyo ifutwe! Kwa kifupi mke si roho bali mmewe. Biblia inasema, Kristo ni mwokozi wa Kanisa (Mwili); Lakini Biblia hiyohiyo inasema Mme naye ni mwokozi wa Mwili. Sasa David unapo sema, “Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo” unaipata wapi hiyo?

  Umezidi kuchanganya zaidi unaposema hivi, “Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama Paulo anavyosema, ni katika kila jambo. Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana dhamiri yake….” Imeamliwa mke amtii mme kwa kila jambo, basi ni kwa kila jambo. Kuweka neno ‘lakini’ ni nyongeza, na Biblia inasema “Nyongeza” yoyote ikiogezwa dhidi ya ukweli, nyongeza hiyo inatoka kwa Yule mwovu! Kama mme atakuwa hayupo pamoja na Kristo, na kumtaka mke wake avunje Neno la Mungu, huyo si mme anayezungumziwa na Biblia kuwa ni kichwa, huyo ni mme asiye amini, Biblia inasema, mke au mme akiamua kukaa kindoa na mwenza asiyeamini ni hiari ya mhusika mwenyewe, maana asiyeamini hutakasika kwa mwenza wake wa kindoa aliyeamini. Kama mke ama mme anaona kuwa anaondolewa katika Neno na mwenza wake asiyeamini, ana hiari ya kumuacha!. Kwa hiyo, fundisho kama hilo kuwa mke atii mme kwa sehemu, na kujifanya kuwa ati anatii zaidi Kristo halifai, hata wewe. Katika hilo ‘uliingia’ (ulikubaliana na Neno) uliposema, ”Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri yake” !

  Lakini ‘ulitoka’ nje (Ulikinzana na Neno) tena uliposema, “Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa kuchagua kumtii Yesu”. Ndugu yangu utake utake usitake Mme ni Bwana wa mkewe, maandiko yanasema, hebu sikia 1petro 3:6 inavyosema, “6kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, akamwita ‘bwana.’ Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema na bila kuogopa jambo lo lote. Na pahala pengine panasema, “….na mmeo atakutawala” mtawala ndiye ‘Bwana’ Mke anapata kumfahamu Kristo ki ukweli kupitia mmewe, Neno linasema “….naye kama hajaelewa jambo lolote akamuulize mmewe…” wala mke mwenye mme wa ukweli, hawezi kusema kuwa yeye anamtii Kristo kulikoni mmewe, kwani mwili wawezaje kujitenga na roho, kisha mwili huo ukaendelea kuwa hai? Biblia inasema, “Wawili usipopatana watumbukia wote shimoni”

  Hoja nyingine ambayo “umetoka nje” na ambayo hukuthubutu kurudi ndani ni pale uliposema, “Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao mara zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12)…….”

  David, Biblia inasema, Ibrahimu na Mungu walikuwa marafiki. Haupo urafiki ukaitwa urafiki wa kweli kama wahusika hawapo pamoja kwa upendo, ni kweli wanaweza kupata wakati wakatofautiana, lakini hawadumu katika tofauti zao! Naweza kusema hivi, Mungu alipomwambia Ibrahimu amsikilize Sara, Mungu ‘alimrudishia upuuzi wake’ Ibrahimu; Kwa kuwa Ibrahimu ndiye aliyetangulia ‘kumpuuza’ Mungu. Ibrahimu anajua kuwa ‘Mke’ anatawaliwa na Mmewe na anapaswa aelekezwe na mmewe, hebu ona mfano kwa Yakobo na mkewe Raheli, kwa shauri kama lilelile, hebu ona,
  Mwanzo 30:1 “Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, ‘‘Nipe watoto, la sivyo nitakufa!’’ Ona jibu la Yakobo,
  Mwanzo 30:2 inasema, “2Yakobo akamkasirikia akamwambia, ‘‘Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?’’
  Hebu ona mazungumzo ya Ibrahimu na mkewe Sara, katika Mwanzo 16:1-2
  “iBasi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mtumishi wa kike Mmisri jina lake Hagari, 2hivyo Sarai akamwambia Abramu, ‘‘BWANA amenizuilia kupata watoto. Nenda, ukakutane kimwili na mtumishi wangu wa kike, huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.’’
  Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema”. Tutaiona wazi tofauti ya wanaume hawa wawili, ni kwamba, tukio linafanana, lakini mmoja (Ibrahimu) Kwanza, Ibrahimu alishapewa tayari ahadi na Mungu juu ya uzao wake kwa sarai mkewe, lakini la pili, alikuwa aliambiwa wazi wazi na Sarai mkewe kuwa Mungu ndiye amezuia uzazi! Tukija kwa upande wa yule wa pili (Yakobo) Kwanza, Yakobo yeye hakuwa na ahadi ya kupata uzao kwa Raheli mkewe, lakini la pili, yeye Yakobo ndiye aliyemjurisha Raheli mkewe kuwa Mungu ndiye aliyezuia uzazi kwa Raheli!.
  . Kumbuka Mwanamme kama kichwa ndiye mwenyejukumu la kuiongoza familia yake kuishikilia ahadi na kuisikia Sauti ya Mungu wakati wote. Ikiwa Mungu (Kristo) ndiye kichwa cha mwanamme, unaonaje kichwa kikiutii mwili, si dharau kwa Kichwa chake chenyewe? Hicho ndicho kilichofanyika kaika hiyo Mwanzo 21:10-12). Uliyonukuu, kwa hiyo si kweli kwamba Ibrahimu alikuwa ameachwa na Mungu, ati Mungu akawa na Sarai pekee wakati huo.
  Labda niishie hapo kwanza kwa leo kwani,
  “Ufahamu ni chembe ya uhai”
  Mabinza LS.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s