Kwanini Arusha, Kwanini Tanzania?

  arusha

Hivi unajua kwa nini mabomu yanalipuliwa Arusha? Unajua kuwa nchi ya Tanzania ina heshima kubwa kwa sababu ya Arusha? Na Je, wajua kuwa amani ya Tanzania inategemea zaidi amani ya Arusha? Sina maana ya kusema kwamba amani ya Tanzania imetoweka ila nashawishika kusema iko hatarini kutoweka endapo watanzania hatutaitazama Tanzania kwa jicho la ndani na kuona kwamba Arusha ni kitovu muhimu au lango la amani yetu na ya nchi jirani kama nionavyo mimi.

 Arusha ni taa ya Tanzania, tukiizima Arusha Tanzania inayojulikana ulimwenguni itapoteza uzuri wake na heshima yake itaota kutu mara moja. Vitu vikubwa vinayoitambulisha Tanzania kimataifa vina mizizi yake Arusha. Hebu kwanza tujikumbushe taarifa chache chungu zinazohusu Arusha ndipo nieleze undani wa kauli zangu za hapo juu.

Hivi karibuni tumeshuhudia matukio mengi ya ajabu nchini Tanzania hasa yahusianayo na milipuko ya mabomu jijini Arusha. Vurugu za hapa na pale zilizotokea mwaka wa uchaguzi mkuu 2010 ziliashiria umuhimu wa jiji hili kwa viongozi wa vyama imara vya kisiasa hapa Tanzania, bomu lililolipuka kanisani likaleta hofu ya ugaidi kwa watanzania wengi hasa wale waishio jijini hapo kwa sababu ninayo hakika kwamba watanzania wengi hawaelewi kwa undani jinsi gani waathirika wa mabomu wanapata maumivu ya muda mrefu au hata ya kudumu hasa pale wanapopata ulemavu, wanapoathirika kisaikolojia, kupoteza ndugu jamaa na marafiki, kuharibiwa kwa mali na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo. Mwaka huu tumeshuhudia mlipuko wa bomu ambao umesababisha vifo kadhaa na majeruhi ya wananchi waliokuwa katika harakati za kusikiliza kampeni za kisiasa kama sehemu ya demokrasia na haki yao ya msingi ya kukutanika. Wengi wanajiuliza swali hili, kwa nini iwe Arusha? Swali hili ndio lilinipa nguvu ya kuandika ili watanzania wajue kilicho nyuma ya pazia.

Najua kuwa si Arusha pekee iliyowahi kukumbwa na mauaji au milipuko ya mabomu lakini kwa kuuelewa uhusiano mkubwa wa Arusha na amani ya Tanzania ninasukumwa kuliangalia jiji hili kwa mtazamo makini na kwa jicho la ndani  kuliko pande yoyote ile ya Tanzania. Hapa najumuisha Arusha, Manyara na Babati kama mkoa mmoja sawa sawa na kipindi cha azimio la Arusha ili kizazi kijacho kitakapo soma makala hii kipate ujumbe ule ule kwa sababu uzito wa makala hii hauwezi kuisha leo wala kesho.

Sifa kubwa ya Tanzania ni amani; nionavyo mimi ni kwa sababu ya uhusiano mkubwa wa watu bila kujali tofauti zao kiimani, kikabila na kisiasa. Nchi nyingi wakiwemo majirani zetu wanahangaika sana kupambana na udini na ukabila. Mwaka 1967 mjini Arusha mwalimu nyerere alizindua Azimio la Arusha lenye msingi katika sera ya Ujamaa na kujitegemea. Azimio hilo lilikuwa ni kwa ajili ya taifa zima na liliwafanya watanzania  wajifunze kuishi kwa ushirika na upendo katika kupambana na maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini, hapo ilitulazimu kuhakikisha amani inakuwa msingi wa umoja na ushirika wetu kwa ajili ya maendeleo. Kwa hiyo si mpango wa Mungu viongozi wa maeneo muhimu kama haya kuwa wasiojali maisha ya watu wala kuthamini amani na utulivu.

Sifa hii iko wazi ndio maana ndugu zetu wa Rwanda na Burundi walipokumbwa na machafuko mwaka 1994 watuhumiwa wa vita vile walifikishwa katika jiji hili ambalo ni kitovu cha amani. Arusha wakati huo haikuwa na International Criminal Court (ICC) yaani mahakama ya uhalifu wa kivita lakini juhudi za kimataifa zilifanyika hatimaye zikajengwa, ICC ya kule The Heague ilikuwepo lakini kwa kuwa amani ya majirani haiwaitaji majaji wa ulaya basi Arusha lilikuwa ndio suluhisho pekee japo kuna uwezekeno mkubwa hata waliojenga mahakama hizo kushindwa kuelewa siri hii. Kwani Bukoba, Kigoma, Dodoma au Mwanza hakuna maeneo ya kujenga mahakama za kimataifa? Au nchi kama Msumbiji na Zambia hazina maeneo kwa ajili ya mahakama hizo? Suala si miundo mbinu bali ni miundombinu ya amani ndani ya Arusha na Tanzania. Huu ni uwezo wangu wa kufikiri si kwa kusoma vitabu vya historia! Nasisitiza “Amani ya majirani na Afrika yote inategemea amani ya Tanzania.”

Upekee wa rasilimali ya madini ya Tanzanite yanayochimbwa Arusha unaitofautisha Tanzania na nchi zote duniani hata zile nchi zinazosemekana kuwa na rasilimali nyingi kuliko Tanzania, kama Brazil na Jamhuru ya Kidemokrasia Ya Kongo. Katika kuangalia upekee unaweza kujiuliza ni utamaduni upi wa watanzania unaodumu hata sasa na kutambulika na wageni kama si ule wa wamasai? Katika muktadha kama huu unaweza kukubaliana na mimi kwamba Tanzania inang’aa ndani na kimataifa si tu kwa sababu ya milima Kilimanjaro na maziwa makubwa au kwa Tanzanite bali kwa sababu ya amani na hayo mengine ndio yanafuata.

Yaliyotokea Arusha ni muhimu kuyadhibiti mapema sana kabla maovu haya hayajaanza kutokea mahala kwengineko, hapa imetupasa watanzania kuweka mbele utaifa wetu kabla ya kuangalia mahitaji yetu binafsi, ndio maana ili kuondoa tope la damu nasisitiza kufunga koki ya bomba na si kukausha maji kwa vumbi. Namaanisha kutunza amani kama msingi wa maendelea ya Taifa letu badala ya kujipanga kukabiliana na machafuko ambayo kimsingi sioni sababu ya nchi yetu kumwaga damu. Ipo mifano mingi ya nchi za Afrika zilizochafuka na kuyumba kwa sababu ya kuchezea amani waliyokuwa nayo, nafikiri kusema Tanzania haina amani ni ufinyu wa fikra, je unayafahamu maisha ya watu wa Somalia? Unajua kinachoendelea sasa kule Misri? Muda mwingine nadhani badala ya kulaumu na kulewa amani hii, tunatakiwa kutumia vizuri kwa kutoa michango chanya ya mawazo itakayoimarisha taifa letu badala ya kulalamika tu kila kuitwapo leo. Ni ombi langu kwa watanzania kuithamini amani yetu, kuthamini taifa letu, kujali maisha ya watu na kujenga mustakabali wa taifa imara kila sekta, Inawezekana!

Na  Mussa Kisoma

Advertisements

2 thoughts on “Kwanini Arusha, Kwanini Tanzania?

  1. Naona kuwa mtazamo wako hauko sahihi. Umejenga hoja kutokana na matukio. Angalia usiwe miongoni mwa wanaojadili matukio badala ya hoja. Wapo wahubiri wengi huandaa Neno la kuhubiri siku ya Jumapili mimbarani kutokana na matukio waliyoyaona barabarani au mtaani na kuyafanya kama vile eti ni Mungu amewapa Neno. Et “Hilo ndilo neno nililopewa na Mungu kwa siku ya leo”.

    Kulipuka kwa mabomu mawili Arusha, kuwepo kwa mahakama ya ICTR, Azimio la Arusha, nk haviwezi kuufanya mji wa Arusha kuwa na upekee katika ulimwengu huu na nchi hii. Hayo ni matukio tu siyo hoja. Kama ni mabomu hata Mbeya, Iringa, Dar, Mwanza, Dom, Kigoma, Kongo, Afrika kusini, nk yanatokea. Kama ni mahakama kila za kimataifa Arusha iliwekwa kama ambavyo ingweza kuweka popote.

    Nadhani hoja yako ilikuwa ni KUOMBA AMANI TANZANIA IDUMU na wala siyo kwa sababu Arusha pamevurugika. Kama ingekuwa ni mimi nadhani kitovu cha Amani ya nchi hii ningesema ni jiji la Dar es salaam na wala siyo Arusha.

  2. hakuna kitu ulichoandika kikaeleweka, uenda ni kwasababu ambayo umeisema” unaandika kutokana na uelewa wako” ni tatizo

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s