Kushika Sheria!

sheria

Inaendelea kutoka Mkristo asiyefuata sheria I…

Kushika Sheria Maana yake Nini?

Maneno “kushika sheria” yameeleweka na kutumiwa vibaya sana kuliko kawaida. Kila anayehubiri kujikana, utii au utakatifu siku hizi yuko hatarini kubandikwa jina kwamba yeye ni mhubiri wa kushika sheria. Ni mara nyingi utawasikia wanaojiita Wakristo wakisema hivi: “Nilikuwa mshirika kwenye kanisa linaloshika sheria sana. Mchungaji wetu alikuwa anahubiri kinyume cha kutazama sinema chafu.” Tamko kama hilo linaonyesha kwamba kwa kweli huyo anayesema haelewi maana ya kushika sheria. Maana ya kushika sheria si kushikilia kiwango cha utakatifu kitokanacho na Neno la Mungu. Ni kujaribu kujipatia wokovu – kwa sehemu au wote kabisa – kwa matendo ya mtu. Kama mtu akisema hivi: “Nilikuwa mshirika kwenye kanisa linaloshika sheria sana. Mchungaji wetu alikuwa akihubiri na kutuambia kwamba tungeweza kujitengenezea mahali petu mbinguni kwa kuacha kutazama sinema chafu,” hapo angekuwa amepata kabisa maana ya kushika sheria.

Upotofu wa fundisho hili ni kwamba linatoa njia nyingine ya kupata wokovu kuliko ambayo Mungu amekwisha itoa kwa njia ya Kristo. Ujinga wa mwenye kuamini fundisho hilo ni kwamba yeye anatazamia kisichowezekana – yaani, kwamba anaweza kuwa mzuri kiasi cha kutosha kustahili kuingia mbinguni. Ukweli ni huu: Uwezekano wa sisi kuwa wazuri kiasi cha kutosha kustahili kupata nafasi mbinguni ulimalizika zamani sana: Mara ile ya kwanza Mungu alipotuwajibisha kwa ajili ya dhambi yetu. Kinadharia, kama mtu angeweza kuishi maisha bila dhambi, angeweza kuingia mbinguni bila ya kuhitaji Mwokozi. Lakini kwa sababu sisi sote tumetenda dhambi, kama tunahitaji kuokolewa, basi tunahitaji njia nyingine ya wokovu. Ni dhahiri kwamba njia hiyo inawezekana tu kwa kupitia neema ya Mungu. Habari njema za Injili ni kwamba Mungu amekwisha itoa neema Yake kwetu bila kukiuka viwango Vyake vya utakatifu kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye alichukua mahali petu.

Labda tafsiri bora zaidi ya fundisho la kushika sheria linaelezwa kwa mchoro huu rahisi ufuatao:

MATENDO = WOKOVU

Maana ya mshale ni “hupelekea…”. Mwenye kushika fundisho hilo anafikiri kwamba matendo yake yatapelekea yeye apate wokovu. Kwa sababu moyo wake haujazaliwa mara ya pili, na hauna imani wala pendo kwa Mungu, mtu mwenye kuamini kuhusu kushika sheria hutokeza utii wa nje tu wa Torati huku akijitahidi sana kupata upendeleo wa Mungu kwa matendo yake.

Aina nyingine ya fundisho hili yaweza kuonyeshwa kwa mchoro huu ufuatao:

IMANI + MATENDO = WOKOVU

Huyu anayeamini hivi huongeza imani na matendo pamoja, akifikiri kwamba jumla yake itahakikisha wokovu wake. Kwa sehemu anategemea matendo yake. Hili ndilo fundisho kuhusu kushika sheria ambalo Paulo alilipinga katika waraka wake kwa Wagalatia.

Jinsi Biblia inavyofundisha kuhusu swala hilo inaweza kuonyeshwa kwa mchoro huu rahisi:

IMANI = WOKOVU + MATENDO

Wale wanaoiamini Injili kweli kweli, hawawi wameokolea tu bali wanabadilishwa na ile neema ya Mungu, nao huonyesha kazi ya Mungu katika maisha yao kwa utiifu wao wa furaha. Tofauti na yule anayeshika sheria, utii wa mwamini wa kweli hutoka ndani yake kwa sababu moyo wake umebadilishwa.

Hatimaye tuonyeshe juu ya fundisho linalopinga kushika sheria kwa mchoro ufuatao:

IMANI = WOKOVU – MATENDO

Huyu anayepinga kushika sheria anadhani kwamba imani yake inaleta wokovu wake, hata ingawa matendo ya kuthibitisha kwamba maisha yamebadilishwa hayaonekani. Tena, mara nyingi anakosa kuelewa vizuri vitu vingine vitano, kama ifuatavyo: (1) asili ya imani yenye kuokoa; (2) kusudi la Mungu kuwaokoa watu; (3) kazi kamili ya neema ya Mungu katika maisha ya wale wanaoamini; (4) uhusiano wa Mkristo na sheria ya Mungu; na (5) sababu halisi na umuhimu wa toba. Hebu tutazame hayo yote hatua kwa hatua.

Asili Ya Imani Yenye Kuokoa

Asiyeshika sheria anahesabu imani kuwa si kitu zaidi ya kukubali au kukiri kitu fulani akilini. Yeye hudhani kwamba kukubali kwake kweli fulani za kimafundisho ndiyo imani yenye kuokoa. Kwa kuwa anajua kwamba Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za kila mtu, na kwa kuwa anajua kwamba wokovu si kwa matendo bali ni kwa imani, anafikiri ameokoka.

Hata shetani anajua kwamba Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wote! Shetani pia anajua kwamba watu hawaokolewi kwa matendo bali kwa njia ya imani. Ni kitu gani basi kinachotufanya sisi tufikiri kwamba kujua hayo kunatufanya kuwa wenye haki machoni pa Mungu?

Imani ya kweli yenye kuokoa ni zaidi ya kukiri au kujua kitu kwa akili. Biblia inafafanua imani kwamba ni “kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyo-onekana” (Waebrania 11:1 – Maneno mepesi ni ili kutilia mkazo). Kinachosababisha wokovu ni kuamini kwa moyo (ona Warumi 10:10). Imani ya kweli kila mara inadhihirishwa kwa matendo ya nje.

Lakini, hawa wanaopinga kushika sheria mara nyingi hujaribu kuondoa matendo kwenye imani, na hata wanafikia mahali pa kupambanisha hayo mawili. Wanatamka – kwa utauwa sana – kwamba, kwa sababu wokovu unatokana na neema ya Mungu tu, hawatatazama matendo yao hata moja kwa ajili ya kupata uhakika wa wokovu, wasije “wakatumainia matendo yao.”

Lakini – kama tutakavyoona sasa hivi – hayo hayakuwa mawazo ya Bwana Yesu, au Yohana Mbatizaji, au mtume Yohana, au Paulo, au Petro na hata Yakobo. Kwa mfano: Yohana aliandika kwamba upendo tunaoonyesha kwa waamini wenzetu ni njia mojawapo kati ya nyingi ambazo kwazo tunaweza kutambua ikiwa kweli tumezaliwa mara ya pili. Anasema hivi:

Sisi tunajua [angalia neno hilo: tunajua] ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. … Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake,ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote (1Yohana 3:14, 17-20. Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Yohana aliamini kwamba matendo yetu yanaweza kutuhakikisha juu ya kazi ya neema ya Mungu maishani mwetu. Hii ni tofauti na kutegemea kwamba matendo ya mtu yanampatia wokovu. Matendo yetu mema hayatupi aina fulani ya hisa – yanathibitisha tu kwamba kuna kitu kimetokea. Hutoa uhakikisho wa ziada wa wokovu wetu zaidi ya ule utolewao kwa ahadi za Injili. Tunapoyatazama matendo maishani mwetu, tunaweza kusema, “Mungu asifiwe kwa ajili ya ushahidi huu wa neema ya Mungu itendayo kazi maishani mwangu!” Matendo yetu mema yametendwa “katika Mungu” (Yohana 3:21).

Vile vile Yohana aliandika hivi katika waraka wake wa kwanza:

Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake (1Yohana 3:9-10).

Je, Yohana aliamini kwamba kuzaliwa upya hubadilisha jinsi mtu anavyoishi? Ndiyo! Wale ambao wamezaliwa kweli na Mungu hutenda haki na kuwapenda waamini wenzao. Hii haimaanishi kwamba waamini wa kweli hawatendi dhambi au kwamba kila wakati wanaonyesha pendo kamilifu (ona 1Yohana 1:8-9; 4:17-18). Inachoonyesha ni kwamba haki na upendo ni alama au tabia kuu katika maisha yao, kinyume na wale ambao hawajaokoka, ambao kawaida yao ni tabia isiyo ya haki na ubinafsi. Yohana aliandika mara nyingi sana katika barua yake kuhusu kuishi maisha ya haki na kuwapenda ndugu wengine waaminio ili kuwapa uhakika wa wokovu wale wasomaji wake. Anasema hivi:

Nimewaandikia ninyi mambo hayo [yaani, yaliyomo katika barua hii], ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu (1Yohana 5:13 – Maneno mapesi ni kwa ajili ya mkazo).

Yohana aliamini kwamba wanaokiri Ukristo lazima wachunguze maisha yao ili kupata uhakika kuhusu utendaji kazi wa neema ya Mungu ndani yao, kwa sababu yeye pia aliamini kwamba kuna mlingano kati ya imani na mwenendo.

Asemavyo Paulo Kuhusu Uhusiano Wa Imani Na Matendo

Mtume Paulo hakuamini kwamba matendo na utii vinaweza kuondolewa kwenye imani, au kwamba vitu hivyo vinapingana. Badala yake, katika kitabu cha Warumi aliandika juu ya “utii utokanao na imani” (Warumi 1:5; 16:26). Tafsiri iliyo wazi ya maneno hayo ni kwamba imani huonekana kwa utii. Nikisema hivi: “utii wa Paulo”, maana inayoeleweka ni kwamba Paulo huonyesha utii. Nikisema hivi: “furaha ya wokovu” bila shaka maana yangu ni kwamba wokovu unaonekana kwa furaha. Katika yote hayo mawili ambacho nisingekuwa nasema ni kwamba kimoja ni badala ya kingine, kama wale wanaopinga kushika sheria wanavyotaka tuamini kwamba ndiyo maana ya Paulo anaposema “utii wa imani”. Wao wanadai maana yake ni kwamba hatuna haja ya kuwa na utii, kwa sababu imani ndiyo inasimama badala yake. Hiyo ingekuwa sawa na kusema kwamba ninaposema “utii wa Paulo” maana yake ni kwamba sina haja ya Paulo kwa sababu ninao utii wake, au, kwa mfano ule mwingine, kwamba sihitaji wokovu kwa sababu nina furaha, ambayo ni mbadala unaokubalika.

Paulo hakuona tu kwamba Injili ni kitu cha kuaminiwa, bali pia aliihesabu kuwa ni kitu tunachotakiwa kukitii. Aliwaambia Wakristo Wathesalonike kwamba wale “wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu … wataadhibiwa kwa maangamizi ya milele” (2Wathes. 1:8, 9 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Swali: Kuna nini cha kutii kuhusu Injili? Kwanza: Tunaamriwa na Mungu kuiamini Injili, na tendo la kuamini ni utii (ona Marko 1:15). Basi, inawezekanaje wengine wadai kwamba utii na imani vinapingana, wakati kuamini ni tendo la utii?

Pili ni kwamba, Yesu aliwaagiza watu watubu na kuiamini Injili. Pia alituagiza sisi tuhubiri “toba na msamaha wa dhambi” (Luka 24:47). Paulo alifanya hivyo, akiwatangazia watu kwamba sharti “watubu na kumgeukia Mungu, na kufanya matendo yanayostahili toba” (Matendo 26:20). Kutubu ni tendo la utii, ni itikio kwa agizo la kimungu. Wokovu huanza maishani mwa mtu kwa tendo la utii ambalo nalo ni tendo la imani.

Paulo aliwaandikia Wathesalonike akiwasifu kwa “kazi yao ya imani na upendo” (1Wathes. 1:3 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo). Hakuona imani na matendo kuwa vitu viwili visivyoweza kuchanganywa. Sawa na mtume Yakobo, yeye aliamini kwamba imani ya kweli inatenda kazi. Aliwaandikia Wakristo Wagalatia waliokuwa hatarini kudanganywa na kutekwa wafikiri kwamba tohara ilikuwa lazima kwa ajili ya kuokoka, kama ifuatavyo:

Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo (Wagalatia 5:6 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kama mtume Yohana, Paulo aliamini kwamba imani ya kweli ilifanya kazi kupitia upendo. Upendo ni tunda la msingi sana katika imani. Kwa maneno mengine, Paulo anasema hivi: “Maana, katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana yoyote; ni matendo ya kibinadamu, ila imani huanza kazi ya kimungu katika maisha ya mtu mpaka kumfikisha kwenye mahali ambapo matendo yake ya upendo yanatoka kwa Mungu.”

Maelezo Ya Kitabu Cha Waebrania Kuhusu Imani

Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliamini kwamba kumtii Yesu Kristo ni kitu muhimu kwa ajili ya wokovu. Aliandika hivi:

Naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii(Waebrania 5:9).

Mwandishi angeweza pia kusema kwamba Yesu alifanyika asili ya wokovu wa milele kwa wote wanaomwamini, na angekuwa anasema kitu kile kile. Kwake yeye, imani – kitu ambacho anakitaja zaidi ya mara thelathini katika kitabu chake – ilikuwa inasababisha matendo. Kila mmoja katika wale “mashujaa wa imani” wa sura ya 11 walifanya kitu fulani kwa sababu waliamini.

Katika sura ya tatu na nne ya kitabu cha Waebrania, ona jinsi mwandishi anavyotumia maneno kutokuaminina kutokutii mara kwa mara.

Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao … wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao … (Waebrania 3:19; 4:6 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Kwa sababu wengi katika Waisraeli hawakuziamini habari njema, hawakumtii Mungu. Kwa sababu hawakufanya kile ambacho Mungu aliamuru, walithibitisha kwamba hawakuamini ahadi Yake.

Maneno Ya Yohana Mbatizaji Na Yesu Kuhusu Matendo

Yohana Mbatizaji aliamini kwamba hakuna kutengana kati ya imani na mwenendo. Hebu soma jinsi alivyotumia maneno kuamini na kutii.

Amwaminiye [pisteuo] Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini [apeitheo] Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia (Yohana 3:36 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Kuna kuwa wazi zaidi ya hapo? Na je, inawezekanaje mtu kusema kwamba ni makosa kuchunguza maisha yetu ili kuamua msimamo wetu kiroho tusije “tukategemea matendo yetu kutuokoa”? Narudia tena: Tunapaswa kuchunguza matendo yetu kwa sababu Maandiko yako wazi kabisa kwamba inawezekana kuwa na imani isiyozaa. Kutumaini imani isiyofanya kazi kwamba itatuokoa ni hatari sana, sawa tu na kutumaini kwamba matendo yetu yatatusaidia kupata wokovu. Ulinzi wa pekee unaofaa kinyume cha hatari zote hizo ni kuchunguza matendo yetu ambayo ni uthibitisho wa imani ya kweli, yenye kuokoa.

Yesu vile vile aliamini kwamba imani ilibadilisha mwenendo. Alisema kwamba wale wamwaminio Yeye watatenda matendo yale yale aliyotenda (ona Yohana 14:12). Alitabiri pia kwamba wale ambao “wangetenda matendo mema” wangefurahia “ufufuo wa uzima”, na wale ambao “wangetenda matendo maovu” wangepatikana na “ufufuo wa hukumu” (Yohana 5:29). Pia alionya kwamba wale tu wanaotenda mapenzi ya Mungu ndiyo watakaoingia mbinguni, na kwamba waamini wa kweli na wasio wa kweli wanaweza kujulikana kwa matunda yao (ona Mathayo 7:19-23). Njia ya pekee iliyo sahihi ya kutafsiri maonyo Yake ni kwamba imani yenye kuokoa inathibitishwa kwa utii, isipokuwa kama alikuwa anafundisha kwamba wokovu unapatikana kwa matendo.

Vile vile Yesu alionya kwamba wale tu watendao mapenzi ya Baba Yake ndiyo ndugu na dada Zake (ona Mathayo 12:49-50). Kama tulivyojifunza katika sura iliyopita, mara nyingi Yesu hakusema chochote juu ya imani alipowaita watu waje kuokoka. Aliwaambia wamtafutao kujikana, wajitwike msalaba wao na kumfuata wasije wakapoteza nafsi zao (ona Marko 8:34-38). Aliwaita watu kuingia kwenye uanafunzi wenye gharama, na kujitoa kweli kweli, au imani ya kweli.

Akijaribu kueleza maana ya kumwamini, Yesu alifikia mahali pa kuwaambia watu kwamba walihitaji kumlaYeye (ona Yohana 6:47-56), kitu ambacho hata sisi tunakumbushwa kila mara tunaposhiriki Meza ya Bwana. Kumwamini Yesu ni kufanyika mmoja Naye. Tendo la kwanza la imani la mwamini mpya – yaani ubatizo katika maji – ni tangazo hadharani kwamba yeye na Yesu wameunganika katika mauti Yake, kuzikwa na kufufuka Kwake.

Kumwamini Yesu ni kujiunga Naye. Angalia: “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye” (1Wakor. 6:17). Kumwamini Yesu ni kukaa ndani Yake, kama anavyosema Mwenyewe: “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu … Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; nao huyakusanya na kuyatupa motoni, yakateketea” (Yohana 15:4, 6). Itawezekanaje mtu awe na umoja wa namna hiyo na Kristo, na isibadilishe tabia yake?

Asemavyo Yakobo Kuhusu Imani Yenye Kuokoa

Pengine, maelezo maarufu zaidi kuhusu imani yenye kuokoa, na ambayo yanawasumbua sana wale wanaopinga kushika sheria, yanapatikana katika waraka wa Yakobo katika maandiko tuliyotazama kwa kifupi katika sura zilizopita. Anasema hivi:

Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? (Yakobo 2:14).

Jibu dhahiri kwa swali la Yakobo ni Hapana. Imani bia matendo haiokoi.

Pamoja na kwamba kweli hiyo iko wazi hivyo, wanaopinga kushika sheria wa kisasa wangependa tuamini kwamba imani bila matendo inaweza kumwokoa mtu. Wanashikiliaje msimamo kama huo licha ya maneno ya Yakobo? Maelezo yao kuhusu mafundisho ya Yakobo ni magumu kiasi kwamba wasomaji wa Yakobo mwenyewe wasingeweza kuelewa. Cha kwanza: Hawa watu wanataka sisi tuamini kwamba Yakobo hakuwa anazunguma juu ya kuokoka kutokana na kwenda jehanamu, bali kuokoka kutokana na “maisha ya dhambi hapa duniani”. Eti, Yakobo alikuwa anajaribu kuwashawishi wasomaji wake waamini kwamba walipaswa kuwa na matendo pamoja na imani yao kama walitaka kuokolewa kutoka “maisha ya dhambi na mauti” hapa duniani.

Hayo maneno “maisha ya dhambi na mauti” bila shaka maana yake ni maisha ya dhambi. Na, kuokolewakutoka “maisha ya dhambi na mauti hapa duniani” bila shaka maana yake ni kuishi maisha ya utii, yaani, kutenda matendo mema. Basi, baadhi ya hao wanataka tuamini kwamba Yakobo alikuwa anarekebisha kosa kubwa katika mafundisho ya wasomaji wake, kwamba wao walifikiri wanaweza kuishi maisha ya kutii wakiwa na imani isiyokuwa na matendo ya utii! Je, inawezekana kweli kwamba Yakobo aliwaona wasomaji wake kuwa wapumbavu kiasi cha kutojua tayari mambo ambayo wote waliyajua? Na je, hao wanafikiri na sisi ni wapumbavu kiasi hicho, tukubali tafsiri isiyo sahihi ya mafundisho ya Yakobo ambayo yako wazi kabisa?

Katika kuendelea kupinga hoja hiyo, tunasema kwamba maandiko yanayotangulia na yanayofuata maneno ya Yakobo kuhusu uhusiano kati ya imani na matendo ni hukumu ijayo (ona Yakobo 2:12-13; 3:1). Kilichokuwa mawazoni mwa Yakobo ni wokovu wa milele, si wokovu wa muda wa kidunia kutoka “maisha ya dhambi na mauti”.

Imani Ikitenda Kazi Kwa Upendo

Hii tafsiri ya wanaopinga kushika sheria inazidi kuonekana ni ujinga wakati mtu anaposoma maneno ya Yakobo, kama ifuatavyo:

Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, ‘Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba’, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake (Yakobo 2:15-17).

Kuna wafuasi wa fundisho hili wanaotaka tuamini kwamba imani iliyokufa bado ni imani yenye kuokoa, ni kwamba tu ni imani iliyokufa na siyo imani hai yenye kuokoa. Lakini Yakobo tayari amekwisha sema kwamba imani bila matendo haiwezi kumwokoa yeyote, na hiyo ndiyo imani iliyokufa – imani isiyo na matendo.

Inapendeza sana kwamba mfano aliotumia Yakobo kueleza juu ya imani iliyokufa ni picha ya mtu anayekiri Ukristo ambaye hafanyi chochote kumsaidia ndugu au dada ambaye ni maskini. Sawa tu na Yesu, Yohana na Paulo, Yakobo naye aliamini kwamba matunda ya imani ya kweli ni upendo kwa ndugu, wenye kuonyeshwa kwa kukutana na mahitaji yanayowabana.

Yakobo anaendelea kuandika juu ya kutowezekana kwa imani ya kweli kukosa matendo. Anasema hivi:

Lakini mtu atasema, ‘Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?’ (akobo 2:18-20).

Kama anavyosema Yakobo, tena vizuri tu, mtu anaweza kudai kwamba ana imani, lakini hawezi kuthibitisha kwamba ana imani pasipo matendo. Kwa upande mwingine, mtu mwingine anaweza asidai kwamba anayo imani, lakini matendo yake yanasema kitu asicholazimika kudai. Matendo yana sauti kubwa kuliko maneno. Basi, wale wanaosema kwamba wanaamini Mungu ni mmoja (Kumbu. 6:4) lakini hawana matendo yenye kulingana na maneno yao wanajidanganya wenyewe. Pepo pia wanaamini kwamba Mungu ni mmoja, nao wanatenda kama wanavyoamini – wanatetemeka! Ni “wapumbavu” tu ndiyo wasiotambua kwamba imani pasipo matendo “haizai” (au haifai kitu) (Yakobo 2:20). Maana yake ni kwamba haifai kwa lolote.

Imani Hai Ya Ibrahimu

Yakobo anaendeleza hoja yake akimtaja Ibrahimu, ambaye alihesabiwa haki kwa imani kuwa kama mfano wa mtu mwenye imani hai. Anasema hivi:

Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu’. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake (Yakobo 2:21-14).

Sasa, Yakobo aseme kwa uwazi upi kuliko huo? Imani ya Ibrahimu ilikuwa imani hai iliyomtii Mungu. Si imani bila matendo iliyomfanya kuhesabiwa haki bali ni imani iliyothibitishwa kwa matendo. Yakobo anaendelea mpaka anafikia mahali pa kusema kitu ambacho, kikiondolewa kwenye mantiki yake, kinaweza kuhesabiwa kuwa uzushi. Anasema hivi: “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:24).

Sasa: Baadhi ya hao wenye kuamini kutokushika sheria wanajiondoaje katika tatizo ambalo Yakobo anawaingiza? Wanafikiri kwamba Yakobo hakumaanisha Ibrahimu alihesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo yake, bali alihesabiwa haki mbele za wanadamu. Lakini hilo nalo ni upuzi. Je, tuamini kwamba wasomaji wa Yakobo waliamini mtu angeweza kuhesabiwa haki mbele za wanadamu bila matendo, na kwamba Yakobo aliona kosa hilo kuwa ni kubwa sana kiasi cha kuwaandikia ili kuwakemea? Je, kweli hicho ndicho kitu alichoandika Yakobo ili kirekebishwe?

Ona pia kwamba Yakobo hakusema chochote kuhusu Ibrahimu kuhesabiwa haki mbele za watu. Zaidi: Wakati Ibrahimu alipokuwa karibu kumtoa Isaka kama dhabihu, hapakwepo watu wengine ili kuona tendo lake hilo la utii ambalo inasemekana lilimfanya ahesabiwe haki mbele za watu. Ila, Mungu alikuwa anatazama, Naye alisema kitu mara moja baada ya kuona tendo la utii la Ibrahimu. Alisema hivi:

“Sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee… Kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu” (Mwanzo 22:12; 16-18).

Tukio zima lilikuwa kipimo kutoka kwa Mungu (ona Mwanzo 22:1), ili kuona kitu ambacho Ibrahimu angefanya. Zaidi ni kwamba, Yakobo anasema wakati Ibrahimu alipomtii Mungu, andiko lilitimizwa linalosema, “Na Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki” (Yakobo 2:23). Sasa, Ibrahimu alihesabiwa kuwa mwenye haki mbele za nani – Mungu au wanadamu? Ni dhahiri kwamba alihesabiwa haki mbele za Mungu.

Hii haimaanishi kwamba Ibrahimu hakuhesabiwa haki na Mungu miaka kabla ya kukaribia kumtoa Isaka sadaka. Maandiko yanatuambia hivyo (ona Mwanzo 15:6; Warumi 4:3). Lakini, tendo la kushangaza la Ibrahimu la kutii, alipokuwa karibu kumtoa mwana wake sadaka, lilionyesha imani hai aliyokuwa nayo tangu alipoanza kuamini. Wakati huu imani yake ilikuwa inakamilishwa kwa matendo yake. Imani iliyosababisha Ibrahimu kutangazwa mwenye haki na Mungu ilikuwa imani ya kweli, iliyothibitishwa kwa utii wake.

Je, Yakobo Hapingani Na Paulo?

Lakini, mbona Paulo aliandika kwamba “mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria” (Warumi 3:28 – Maneno mepesi ili kutilia mkazo)? Je, hayo hayapingani na kile ambacho Yakobo anasema juu ya sisi kuhesabiwa haki kwa matendo yetu, kama yeye naye anasema anachosema Paulo – kuhusu kuhesabiwa haki mbele za Mungu?

Jibu ni hapana – Paulo na Yakobo walikuwa wanazungumza juu ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu, na maneno yao yanayoonekana kama yanapingana ni rahisi tu kuyaunganisha. Paulo alikuwa anasema na washika sheria waliohesabu kwamba Torati ndiyo njia ya kuokoka. Alitaka wao wajue kwamba wokovu hauwezi kupatikana kwa juhudi zozote dhaifu za mwanadamu za kushika Torati. Wokovu ni zawadi itolewayo bure, ambayo imepatikana kwa neema ya Mungu, yenye kupokelewa kwa imani.

Ila – Yakobo alikuwa anasema na wale ambao walikuwa wamepotosha kweli ya wokovu kwa neema kwa njia ya imani, na kuifanya kibali cha kutenda dhambi. Wito wao ulikuwa “kuhesabiwa haki kwa imani tu,” lakini, kama wapingao kushika sheria wa kisasa, walikuwa wameifasiri imani kuwa si kitu zaidi ya ukiri tu wa kinywa – imani inayoweza kukosa matendo yoyote yanayoambatana nayo. Yakobo aliandika kupinga uongo huo, akifafanua vizuri sana ili aeleweke, kama ifuatavyo: “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:24). Sababu iliyomwezesha Yakobo kutoa tamko kama hilo ni kwamba matendo yetu huonyesha imani yetu, ambayo kwa hiyo tunahesabiwa kuwa wenye haki mbele za Mungu.

Maandiko yanafundisha kwamba katika hukumu za siku za baadaye, karima (au mwelekeo) ya milele kwa watu fulani itaamuliwa na matendo yao (ona Mathayo 12:36-37; 25:31-46; Yohana 5:28-29; Ufunuo 20:12-13). Hii ni kwa sababu matendo ndiyo huthibitisha imani. Basi kwa hali hiyo, kama Yakobo alivyotamka, matendo ya watu huwahesabia haki mbele za Mungu.

Yakobo anamalizia mafundisho yake kuhusu asili ya imani yenye kuokoa kwa kutumia mfano mwingine wa Biblia wa mtu aliyeokolewa kwa imani iliyotenda kazi.

Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:25-26).

Je, nini kingempata Rahabu kama angekuwa na imani isiyokuwa na matendo (kama basi inawezekana)? Angeangamia na kila mtu aliyeangamia Yeriko. Lakini imani yake hai inasimama siku hizi kama mfano kwa wote ambao wanataka kuokolewa kutokana na ghadhabu ya Mungu. Rahabu hakuwa mkataa kushika sheria.

Wenye kufuata imani hiyo wanapenda kutumia yule mwizi pale msalabani kwamba ni mfano wa mtu aliyeokolewa kwa imani ambayo haikuwa na matendo. Lakini, wasome Maandiko vizuri zaidi. Huyo mwizi aliyetubu alionyesha imani yake hai kwa matendo katika masaa yake ya mwisho maishani. Kwanza alitubu waziwazi kwamba alikuwa mwenye dhambi. Pili: Alitamka kwamba Yesu hakuwa na hatia, na hakustahili kifo, akifikia mahali pa kumtetea kwa yule mwizi mwingine, hata kumkemea. Tatu: Yeye alimtazama Yesu kuwa asili ya wokovu, na mbele ya kundi lenye kudhihaki, alimwomba waziwazi ampe wokovu (ona Luka 23:40-43). Yule mwizi aliyetubu alikuwa hana nafasi ya kuonyesha imani yake kwa njia nyingine zaidi ya hiyo. Hata hivyo, katika dakika chache alizokuwa nazo, alionyesha imani yake kuliko inayoonyeshwa na wanaojiita Wakristo kwa miaka mingi ya maisha yao.

Kweli ya pili ambayo wapingao kushika sheria wanashindwa kuipata ni hii:

Kusudi La Mungu Kuwaokoa Watu

Muda mrefu tu kabla ya kuandikwa kwa Agano Jipya na Yesu kutembea hapa duniani, Mungu alidhihirisha wazi wazi kusudi Lake kuwaokoa watu – alitaka kuwafanya watakatifu. Kwa mfano, Bwana anasema hivi kupitia nabii Yeremia:

“ ‘Angalia, siku zinakuja’ asema BWANA, ‘nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililofanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao’, asema BWANA. ‘Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile,’ asema BWANA; ‘Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake na kila mtu ndugu yake wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao,’ asema Bwana; ‘maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena’.” (Yeremia 31:31-34)

Unabii huu mzima unarudiwa tena katika Waebrania 8:8-12, na mwandishi wa Waebrania anahesabu kwamba unawahusu waamini wote wa Agano Jipya.

Kwanza: Ona kwamba Mungu anaahidi kufanya agano jipya ambalo halitakuwa kama lile la kale (31:31-32). Lingekuwaje tofauti? Agano la kale lilivunjwa na wengi katika Israeli, lakini isingekuwa hivyo kwa wale walio chini ya agano jipya. Kwa nini? Kwa sababu Mungu angefanya kazi isiyo ya kawaida maishani mwao.

Angeiweka sheria Yake ndani yao, akiiandika kwenye mioyo yao. Matokeo ni kwamba angekuwa Mungu wao na wao wangekuwa watu Wake (31:33). Chini ya agano la kale, Bwana alikusudia kuwa Mungu wa Waisraeli nao wawe watu Wake, lakini haikufanyika hivyo kwa sababu waliasi agano lile. Hawakumtii, na kwa kufanya hivyo walithibitisha kwamba hakuwa Mungu wao, nao hawakuwa watu Wake. Lakini kupitia kwa Yeremia, Bwana aliwaahidi wale wote chini ya agano jipya kwamba Yeye angekuwa Mungu wao na wao wangekuwawatu Wake. Ingekuwa hivyo kwa sababu wangemtii. Asili ya utii wao ingekuwa ile kazi Yake ndani yao.

Kila mmoja katika agano jipya ange”mjua Bwana” kweli kweli, kwa sababu wamesamehewa dhambi zao. Hii ni picha nyingine kuhusu uhusiano wao thabiti. Yohana aliandika hivi: “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, ‘Nimemjua,’ wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake” (1Yohana 2:3-4). Kusudi la Mungu kwa ajili yetu tangu zamani ni kwamba tumjue kweli kweli.

Unabii mwingine unaofanana na huo, wenye kuwahusu waamini wote wa agano jipya unapatikana katika Ezekieli 36:27. Hapo Mungu aliahidi hivi: “Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.” Matokeo ya kumweka Roho Mtakatifu ndani yetu yangekuwa utii wetu. Kama Mungu alitaka kutusamehe tu, asingemweka Roho Mtakatifu ndani yetu. Lakini, hakutaka kutusamehe tu, bali pia alitaka kutubadilisha. Hakutaka kutufanya wenye haki kisheria tu, bali alitaka kutufanya wenye haki kimatendo. Hakutaka Yesu awe kama sisi tu, alitaka na sisi tuwe kama Yesu. Kama jinsi mtume Paulo alivyoandika: “Maana wale aliowajua tangu asili [yaani sisi] aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake … (Warumi 8:29). Hilo ndilo lililokuwa kusudi Lake tangu mwanzo.

Kweli ya tatu ambayo huwa wanaipuuza ni hii:

Kazi Kamilifu Ya Neema Ya Mungu Maishani Mwa Waaminio

Mada iliyopita inapelekea tuingie kwenye hii vizuri sana. Wale wanaopinga kushika sheria wanaamini neema ya Mungu itatusamehe, lakini wanashindwa kutambua kwamba Mungu hutoa vingi zaidi katika neema Yake. Neema ile ile yenye kusamehe pia hutubadilisha.

Neema imeelezwa kuwa ni upendeleo ambao mtu hastahili kuupata. Ndivyo ilivyo. Licha ya uasi wetu, Mungu amemtuma Mwana Wake ili kufa kama dhabihu badala yetu, na kutupa sisi utajiri usiopimika. Hatustahili neema kama hiyo. Lakini wengine, kama anavyosema Yuda, wana “badili neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi” (uda ms. 4). Yaani, wanahesabu upendeleo wa Mungu kuwa kibali cha kutenda dhambi, wakirahisisha kile ambacho kimemgharimu Yeye sana, wakiendelea kwenye njia yao ya kutaka kujitosheleza.

Hilo si itikio ambalo Mungu analitazamia kutoka kwa wale waliopokea neema Yake. Yeye anatazamia kwamba mioyo yetu itayeyuka tunapoanguka mbele Zake kifudifudi, tukiona aibu, tukitubu na tukijaa shukrani. Kama Paulo alivyoandika, neema ya Mungu “yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:12).

Ni dhahiri kwamba tangu siku za kwanza za kanisa, walikuwepo watu wenye imani hii japo hawakuitwa hivyo. Paulo alipinga hoja zao pamoja na maoni yao ya makosa kuhusu neema ya Mungu katika barua zake nyingi. Kwa mfano: Aliwaandikia hivi Warumi:

Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? (Warumi 6:1-2).

Hiyo ndiyo hoja ya hao watu, mbaya kabisa: Hebu tumpe Mungu nafasi zaidi ya kuongeza neema Yake kwa kuendelea kutenda dhambi! Kwa Paulo, wazo la kuishi hivyo ni baya na lenye kuchukiza, kama ambavyo haliwezekani pia. “Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (6:2) Paulo anaelekeza hoja yake kwenye nguvu ya kubadilisha maisha ya neema ya Mungu katika kuzaliwa upya. Wale ambao wamemwamini Yesu kweli kweli wamekufa kwa dhambi.

Paulo anaeleza katika mistari michache inayofuata jinsi hayo yanavyotokea: Ni kwa sisi kuwa ndani ya Kristo aliyekufa na kufufuka. Hivyo na sisi tumekufa na kurudi kuishi tena ili “kuenenda katika upya wa uzima” (Warmi 6:4). Tulipokufa ndani ya Kristo, nguvu ya dhambi ilivunjwa juu yetu. Dhambi ilikuwa nguvu ya kiroho iliyotushika mateka, lakini sasa sisi si watumwa wa dhambi tena kwa sababu “yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi” (Warumi 6:7). Ingawa bado tuna uwezo wa kujaribiwa na dhambi na hata kujitolea kwake, hali yetu ya sasa si kama ilivyokuwa kabla hatujazaliwa mara ya pili. Wakati huo, dhambi ilikuwa sehemu ya asili yetu kiroho na ilikuwa na nguvu juu yetu. Basi, ilikuwa kama haiwezekani kwetu sisi kumtii Mungu. Lakini kwa sasa, inawezekana sana kwetu kumtii Mungu, na bila shaka wale ambao wamejitolea wenyewe kwa Kristo katika imani tiifu watatenda kitakatifu sasa kwa sababu wanaweza kufanya hivyo.

Neema Ili Kuwa Watakatifu

Ahadi ya habari njema za neema ya Mungu si tu kwamba tunaweza kusamehewa, bali kwamba tunaweza kufanywa watakatifu. Maandiko yanaonyesha kwamba kuna mabadiliko ya msingi wakati wa kuzaliwa upya, kazi ya Mungu ambayo inatusafisha kabisa kihalisi. Baada ya hapo kuna kazi ya Mungu inayoendelea maishani mwetu, ambayo Maandiko mara nyingi yanaitaja kuwa ni utakaso. Hebu fikiri juu ya ujumbe wa ajabu unaopatikana katika mistari hii ifuatayo:

Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu (1Wakor. 6:9-11).

Katika kanisa la Korintho walikuwepo wenye dhambi wa zamani ambao walikuwa wamefungwa na baadhi ya dhambi hizo za kutisha sana kwa wanadamu. Lakini wakawa wamewekwa huru na kubadilishwa kwa Roho Mtakatifu. Je, si huzuni sana kwamba neema ya Mungu inavyongojea kwa upendo ili kusamehe na kuwaweka huru walawiti, wezi, wazinzi na walevi, kanisa linaandaa mipango ya kuunda makundi ya kuwasaidia “Wakristo” waelewe na waweze kuishi na shida zao hizo? Wakati Neno la Mungu la milele linaposhuhudia juu ya nguvu za kushinda dhambi zilizomo katika Injili, kanisa linaingia katika nadharia za kidunia na kufuata ushauri wa saikolojia. Paulo hakuionea haya Injili – tofauti na wengi walio kanisani leo – kwa sababu alijua kwamba ni “uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16). Neno la Kiyunani alilotumia kwa “wokovu” katika mistari hii – sozo – linaweza kufasiriwa ukombozi. Nguvu za Mungu katika Injili zinaweza kumkomboa yeyote kutoka kwa chochote.

Lakini, sehemu kubwa ya kanisa siku hizi aidha wanaona aibu au hawajui kuhusu nguvu za kukomboa zilizo katika Injili. Wakijficha chini ya upendo, watenda dhambi waliozoea wanaambiwa “kwa huruma” kwamba Mungu katika neema Yake anawapokea kama walivyo. Ni kweli kwamba Mungu anampenda kila mtu kama alivyo, lakini atawakubali tu kama watamwamini Mwana Wake na kugeuka na kuacha dhambi. Wakifanya hivyo, hatawaacha kama walivyo, bali atawaweka huru. Mimi binafsi nimeona mashoga, walevi, walevi wa dawa za kulevya, wazinzi na waasherati wengi tu wakiwekwa huru kutokana na dhambi zao dakika ile walipotubu na kumwita Yesu. Je, Mungu hana nguvu kiasi hicho? Kulingana na 1Wakorintho 6:9-11, anazo nguvu kiasi hicho na zaidi!

Kusema Ukweli Katika Upendo

Kama kweli tulikuwa tunawapenda watu waliofungwa na dhambi, tungewaambia ukweli. Je, tunafikiri kwamba sisi tuna upendo kuliko Mungu, tunapowashauri watu kwa bidii sana kwamba wajitahidi tu kuchukuliana na hali huku wanaendelea kutenda dhambi ambazo Mungu anataka kuwakomboa nazo? Je, Yesu alikuwa mkali sana alipomwambia yule mwanamke aliyeshikwa katika uzinzi, “Enenda zako, na usitende dhambi tena” (Yohana 8:11)? Je, ilitakiwa awe na huruma kidogo na kusema, “Ninakukubali kama ulivyo. Inaonekana wewe umeshikwa sana na ngono, na bila shaka inatokana na jinsi ulivyolelewa. Matendo yako yanaonyesha kwamba unatamani upendo ambao baba yako hakukupa. Kwa hiyo, usijisikie hatia. Hatia inaweza kuharibu haiba zetu sana. Ninakushauri kwamba uende na ujiunge na kundi la watu wanaotoka katika tabia kama hiyo yako. Baada ya muda, ninatumaini kwamba utaweza kushinda tamaa yako kwa msaada wa nguvu kuu zaidi”?

Ujumbe wa Yesu kwetu sisi sote baada ya kukutana Naye ni huu: “Enenda zako, na usitende dhambi tena.” Kwa nguvu za Roho Mtakatifu katika kuzaliwa upya halisi, nguvu za dhambi huvunjwa na kufanya iwezekane kwetu kutii. Wale ambao wamezaliwa upya kweli ni viumbe vipya ndani ya Kristo (ona 2Wakor. 5:17) ambao wanaweza kusema kwa uhakika kabisa, “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu” (Wagalatia 2:20). Mungu anatenda kazi ndani yao, “kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:13), Naye anaahidi kwamba ataikamilisha ile kazi njema aliyoianza ndani yao (ona Wafilipi 1:6).

Kama nilivyokwisha sema kabla, kama Mungu alichotaka ni kutusamehe dhambi tu, asingemweka Roho Wake Mtakatifu ndani yetu. Ni dhahiri kwamba kwa sehemu, kusudi Lake la kutupa sisi Roho Mtakatifu ilikuwa kutufanya watakatifu. Neema ya Mungu inafanya zaidi ya kutusamehe – inatukomboa na kutubadilisha.

Wazo la nne ambalo wanaopinga kushika sheria hawalielewi ni:

Uhusiano Wa Mkristo Na Sheria Ya Mungu….

Itaendelea sehemu ya Mwisho.

–David

Advertisements

One thought on “Kushika Sheria!

 1. “BALI ISRAELI WAKIIFUATA SHERIA YA HAKI, HAWAKUIFUATILIA ILE SHERIA. kWA SABABU GANI? KWA SABABU HAWAKUIFUATA KWA NJIA YA IMANI, BALI KANA KWAMBA KWANJIA MATENDO. WAKAJIKWAA JUU YA JIWE LILE LIKWAZALO.” WARUMI 9:30-32

  YESU ALISHIKA AMRI, SHERIA NA MAAGIZO, MWEKE MOYONI MATENDO YA SHERIA YATATIMIZWA NDANI YAKO. TUSIJITWIKE MZIGO.

  “KWA MAANA HUKU NDIKO KUMPENDA MUNGU, KWAMBA TUZISHIKE AMRI ZAKE” 1 YOHANA 5:3

  MWEKE YESU KATIKA KIBAO CHA MOYO WAKO. ATAKUWEZESHA KWA NGUVU ZAKO UTAJIKWAA. MAANA YEYE ALIZISHIKA.

  “MAANA HILI NDILO AGANO NITAKALOAGANA NA NYUMBA YA ISRAELI, BAADA YA SIKU ILE, ASEMA BWANA; NITAWAPA SHERIA ZANGU KATIKA NIA ZAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAZIANDIKA; NAMI NITAKUWA MUNGU WAO, NAO WATAKUWA WATU WANGU.” WAEBRANIA 8:10

  WARUMI 8:3,4
  “MAANA YALE YASIYOWEZEKANA NA SHERIA, KWAVILE ILIVYOKUWA DHAIFU KWA SABABU YA MWILI, MUNGU, KWA KUMTUMA MWANAWE MWENYEWE KATIKA MFANO WA MWILI ULIO WA DHAMBI, NA KWA SABABU YA DHAMBI, ALIIHUKUMU DHAMBI KATIKA MWILI ILI MAAGIZO YA TORATI YATIMIZWE NDANI YETU SISI, TUSIOENENDA KWA KUFUATA MAMBO YA MWILI, BALI MAMBO YA ROHO.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s