UKWELI NI UPI BASI? – swali tunalokutana nalo mara kwa mara

changmoto

Katika mazingira tofauti swali hili, tutake tusitake, huwa linajitokeza mawazoni mwetu.

Waweza kurudi nyumbani ukitokea kwenye shughuli zako, umejichokea, wakakujia watoto wako wawili wamegombana na sasa wamekuja kushtaki kwako, huyu anasema hivi na mwenzake anasema vile. Wewe hukuwepo, unabaki kujiuliza, “ukweli ni upi, nani anasema ukweli?”

Linaweza kutokea tukio kubwa linaloathiri maisha ya watu katika jamii, likaripotiwa katika magazeti. Lakini ikatokea kupingana kwa maelezo baina ya magazeti makubwa yenye wafuasi wengi. Hapo ukajikuta ukijiuliza, “ukweli ni upi basi, gazeti lipi linaripoti ukweli?”

Waweza kukuta makundi mawili ya watu wanabishana huku kila upande ukitoa hoja zake nzito nzito kuthibitisha kuwa wao ndio wako sahihi. Katika mazingira hayo, utake usitake, swali hili litakujia tu mawazoni mwako, “hivi ni kundi lipi liko sahihi basi, maana wote wanaonekana kuwa na hoja nzito?”

Mfalme Suleimani naye pia alikutana na changamoto ya jinsi hiyo. Wasomaji wa Biblia wanakifahamu hiki kisa hiki (ambacho kinapatikana katika 1 Wafalme 3:16-28). Wanawake wawili walikuwa wamezaa watoto, mmoja akamlalia mwanaye akamwua (sipati picha mwanamke huyo alivyokuwa mzembe kiasi hicho!) na kufanya ujanja wa kumbadilishia mwenzake. Asubuhi, yule mwanamke ambaye mwanae alikuwa hai akakuta amebadilishiwa mtoto na kuwekewa mfu. Wakati hayo yakitokea hakukuwa na mtu wa tatu ambaye angeweza kutoa ushahidi. Kesi ikamfikia mfalme Sulemani, ambaye hapo nyuma alikuwa amemwomba Mungu hekima (1 Wafalme 3:3-13). Mfalme aliposikiliza maelezo ya wanawake wale wawili, kwa hekima aliyopewa na Mungu akaitisha upanga na kuamuru yule mtoto aliyekuwa hai akatwe vipande viwili halafu wale wanawake wapewe kila mmoja kipande chake. Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi! Mama halisi akasema basi kama ni hivyo mtoto apewe yule mwenzake; ndipo ukweli ukajulikana! Hapo tunaona mfalme Sulemani aliweza kuishinda changamoto ya kung’amua nani alikuwa mkweli baina ya wanawake wale wawili, na kutoa uamuzi sahihi; jambo hili lilizidisha sana heshima kwa aliokuwa akiwaongoza.

Katika 1 Wafalme 22:1-40 tunasoma habari za Ahabu aliyekuwa mfalme wa Israeli, ambaye alitaka kusikia manabii wanasemaje kuhusu yeye kwenda vitani kupambana na Shamu. Manabii 400 wakasema aingie vitani na atashinda. Alipomwita nabii wa Mungu aitwaye Mikaya, huyu akawa na kauli tofauti kuwa akienda vitani atashindwa vibaya. Jambo hilo lilimwuzi mfalme, akamsweka ndani, lakini mwisho wake alipoenda vitani akakutana na mauti yake. Alifanya maamuzi kwa kuzingatia kanuni ya wengi wape, au wengine huisema namna hii: kauli ya wengi ni kauli ya Mungu!

Ujumbe wangu kwako ni huu:

Inapotokea mazingira ambayo ukweli hauko bayana sana, usifanye pupa ya kufanya maamuzi. Usifanye maamuzi kwa kusikiliza upande mmoja tu na kupuuza upande mwingine. Wala usifanya uamuzi kwa staili ya wengi wape, au walio wengi bila shaka wako sahihi. Unahitaji hekima itokayo juu, hivyo mtegemee Mungu akusaidie. Wakati mwingine utahitaji muda hivyo usifanye haraka kuamua. Wakati mwingine itakubidi kufanya utafiti wako mwenyewe kabla ya kujua nani ni mkweli, au taarifa ipi ndiyo sahihi.

Kumbuka kuwa changamoto za jinsi hii tunakutana nazo katika nyanja mbali mbali za maisha, nyumbani, makazini, kwenye nyumba za ibada, katika mahusiano, na kadhalika.

–JWM

Advertisements

5 thoughts on “UKWELI NI UPI BASI? – swali tunalokutana nalo mara kwa mara

 1. NIMEPENDA FUNDISHO HILI! NI HEKIMA YA MUNGU WA KWELI PEKE YAKE NDIYO INAYOTUWEZESHA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI. HEKIMA YA MUNGU MAANA YAKE NI HEKIMA YA NENO, LAKINI NENO LILILOFUNULIWA SIO MAANDIKO KWA KUWA ANDIKO LINAUWA. MBARIKIWE WANA WA ALIYE JUU.

 2. ubarikiwe sana ndg kwa fundisho la aina yake, imo hekma ya Mungu ndani yake. amen.

 3. ukweli umeusema ndg katika Bwana. jambo la kutambua ukweli ni janga kwa wanadamu wote na limekwenda mbali hata kwa watumishi wa mungu hawaujui ukweli wa mambo mengi yanayoendelea katika maisha ya kondoo wanaowaongoza! tatizo mahamuzi mengi tunayochukua yanatawaliwa na hisia zetu , maoni ya wanaotuzunguka ,uelewa wetu finyu juu ya maisha yetu hapa duniani. Biblia inasema hakuna roho ya mtu inayoweza kuyatambua mawazo ya roho ya mtu mwingine ispokua roho ya mungu iwezayo kufumbua mafumbo hata ya Mungu yaliyofichwa maishani mwetu. jambo lifuatalo litatusaidia kama tunataka usalama ktk kutoa mahamuzi yaliyo kweli
  1. lazma tutamani kumpokea Roho Mtakatifu( i.e lazma kuokoka hasa)
  2. lazima kujifunza kumsikiliza Roho Mtakatifu( mungu) hapa pana hitaji maarifa ya kuelewa Mungu hunena vipi na kwa njia gani ktk mazingira gani( walimu njooni mfundishe)
  3. daima jifunze kutokukurupuka wewe mungoje Bwana na wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

 4. Mungu awape hekima na maarifa toka kwa Roho Mtakatifu kuzitambua hila zote za adui hii nimeipenda

 5. JWM,
  Mimi nimefurahishwa sana na mawazo yako. Jambo la msingi hapa ni kwamba, tunatumia nini kuupata ukweli? Mawazo yetu? Hisia zetu? au mitazamo ya watu bila kujali idadi yao? Nini kinatuongoza kupata kupata ukweli!! Nafikiri haya ndiyo yangekuwa ni mojawapo ya maswali wanayopaswa watu kujiuliza badala ya kukokoatana tu.
  Unapoona kuna pande mbili zinakinzana, jua kuwa, upande mmoja lazima utakuwa sahihi na upande mwingine, unadanganya. Jambo la kushangaza sana leo hii, watu wengi hawaelewi namna na wapi pa kuipata KWELI. Wanatumia hisia na mitazamo ya watu. Mungu atusaidie sote.
  Bwana akubariki JWM.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s