Maisha mengine Baada Ya Haya!

hereafter

Wakristo wengi wanajua kwamba watu wanapokufa wanakwenda aidha mbinguni au kuzimu. Si wote wanaotambua kwamba mbinguni si kituo cha mwisho kwa wenye haki, wala kwamba Kuzimu si kituo cha mwisho kwa wasio haki.

Wafuasi wa Yesu Kristo wanapokufa, roho na nafsi zao huenda mbinguni moja kwa moja, mahali anapokaa Mungu (ona 2Wakor. 5:6-8; Wafilipi 1:21-23; 1Wathes. 4:14). Wakati fulani baadaye, Mungu ataumba mbingu mpya na nchi mpya, na Yerusalemu Mpya utashuka kutoka mbinguni kuja duniani (ona 2Petro 3:13; Ufunuo 21:1, 2). Wenye haki wataishi humo milele.

Wakati wasio haki wanapokufa, wanakwenda moja kwa moja mpaka Kuzimu. Hapo ni mahali pa kusubiria tu mpaka miili yao ifufuliwe. Siku hiyo itakapofika, watasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu na baada ya hukumu watatupwa katika ziwa liwakalo moto na kiberiti – Jehanamu katika Biblia. Hayo yote tutayatazama kwa kinaganaga kabisa, tena na Maandiko husika.

Wasio Haki Wanapokufa

Ili tuweze kuelewa vizuri zaidi kinachotokea kwa wasio haki wanapokufa, inabidi tujifunze neno moja la Kiebrania, na maneno matatu ya Kiyunani. Jap ohayo maneno ya Kiebrania na Kiyunani yanaeleza sehemu tatu tofauti, katika Biblia nyingi yanatafsiriwa kuzimu, kitu ambacho kinaweza kuwapotosha wasomaji.

Tuanze kwa kutazama neno la Kiebrania – Sheol katika Agano la Kale.

Neno Sheol linatajwa zaidi ya mara sitini katika Agano la Kale. Linataja waziwazi makao ya wasio haki baada ya kufa. Kwa mfano: Wakati Kora na wafuasi wake walipomwasi Musa nyikani, Mungu aliwahukumu kwa kufunua ardhi, iliyowameza wote na mali zao. Maandiko yanasema waliangukia Sheol.

Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayho nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni (Hesabu 16:33. Maneno mepesi kukazia).

Baadaye katika historia ya Israeli, Mungu aliwaonya kwamba hasira Yake huwasha moto katika Sheol.

Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, unateketea hata chini ya kuzimu, unakula dunia pamoja na mazao yake, unaunguza misingi ya milima (Kumbu. 32:22. Maneno mepesi kukazia).

Mfalme Daudi alitamka hivi:

Wadhalimu watarejea kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu (Zaburi 9:17. Manenomepesi kukazia).

Kisha aliomba kinyume cha wasio haki, hivi:

Mauti na iwapate kwa ghafula, na washuke kuzimu wangali hai, maana uovu u makaoni mwao na katikati yao (Zaburi 55:15. Maneno mepesi kukazia).

Akiwaonya vijana kuhusu ujanja wa kahaba, Sulemani mwenye hekima aliandika hivi:

Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, hushuka mpaka vyumba vya mauti … Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni (Mithali 7:27; 9:18. Maneno mepesi kukazia).

Sulemani aliandika mithali zingine zenye kutuongoza tuamini kwamba wenye haki hawatakwenda Sheol.

Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu, ili atoke katika kuzimu chini (Mithali 15:24. Maneno mepesi kukazia).

[Mtoto wako] Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa nafsi yake na kuzimu (Mithali 23:14. Manenomepesi kukazia).

Mwishowe, akiwahi kabla ya Yesu kutoa maelezo ya kuzimu, Isaya alizungumza kinabii kuhusu mfalme wa Babeli, aliyekuwa amejitukuza sana, na ambaye angetupwa chini hadi Sheol.

Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, ili kukulaki utakapokuja; huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, naam, walio wakuu wote wa dunia; huwainua wafalme wote wa mataifa, watoke katika viti vyao vya enzi. Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, na sauti ya vinanda vyako; funza wametandazwa chini yako, na vidudu vinakufunika. Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana nay eye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu, mpaka pande za mwisho za shimo. Wao wakuonao watakukazia macho, watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, huyu ndiye aliyetikisa falme, aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? (Isaya 14:9-17. Maneno mepesi kukazia).

Maandiko hayo na mengine yanatufanya tuamini kwamba tangu zamani mpaka sasa, Sheol ni mahali pa mateso ambapo wasio haki hufungiwa baada ya kufa kwao. Bado kuna ushahidi zaidi.

Hades

Ni wazi kwamba neno la Kiyunani – Hades – katika Agano Jipya husema juu ya mahali pale pale panapotajwa na neno la Kiebrania – Sheol – katika Agano la Kale. Ili tuone hili, tunachohitaji kufanya ni kulinganisha Zaburi 16:10 na Matendo 2:27, maana maneno hayo yametumiwa.

Maana hutakuachia kuzimu (Sheol) nafsi yangu, wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu (Zaburi 16:10. Maneno mepesi kukazia).

Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu (Hades); wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu (Matendo 2:27. Maneno mepesi kukazia).

Kama ni hivyo, ni kitu cha kuona kwamba mara zote kumi ambapo kuzimu (Hades) hutajwa katika Agano Jipya, ni mahali pabaya, na mara nyingi husemw akwamba ni mahali pa mateso ambapo waovu hufungiwa baada yakufa (ona Mathayo 11:23; 16:18; Luka 10:15; 16:23; Matendo 2:27; 2:31; Ufunuo 1:18; 6:8; 20:13, 14). Hayo yote huonyesha kwamba Sheol au Hades (kuzimu) ni makao ya wasio haki baada ya kufa – mahali pa mateso.[1]

Je, Yesu Alikwenda Kuzimu (Sheol/Hades)?

Hebu tutafakari zaidi Zaburi 16:10 na jinsi maneno yake yanavyotumiwa na Petro katika Matendo 2:27, mistari miwili yenye kuonyesha kwamba Sheol na Hades ni mahali pale pale. Kulingana na mahubiri ya Petro siku ya Pentekoste, Daudi alikuwa hasemi juu yake mwenyewe katika Zaburi 16:10, bali, kinabii alikuwa anazungumza juu ya Kristo, kwa sababu mwili wa Daudi – kinyume na mwili wa Kristo – uliharibika kabisa (ona Matendo 2:29-31). Kama ndivyo, tunatambua basi kwamba katika Zaburi 16:10, Yesu alikuwa anazungumza na Baba Yake, akitangaza imani Yake kwamba Baba Yake asingeiacha nafsi Yake hukoSheol na kuruhusu mwili Wake upatikane na uharibifu (yaani, uoze).

Kuna wanaotafsiri tamko hilo la Yesu kuwa ni uthibitisho kwamba nafsi Yake ilikwenda Sheol/Hades katika ule muda wa siku tatu kati ya kufa na kufufuka Kwake. Sivyo. Hebu tazama kwa makini maneno ya Yesu kwa Baba Yake.

Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu; wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu (Zaburi 16:10).

Yesu hakumwambia Baba Yake, “Najua nafsi yangu itakaa siku chache huko Sheol/Hades, lakini naamini hutanisahau huko.” Alikuwa anasema hivi, “Ninaamini nitakapokufa, sitatendwa kama wasio haki kwa nafsi yangu kuachwa huko Sheol/Hades. Sitakaa hata dakika moja huko. Ninaamini mpango wako ni kunifufua baada ya siku tatu, nawe hutaruhusu hata mwili wangu kupatikana na uharibifu.”

Hii tafsiri inaweza kuwa sahihi. Wakati Yesu aliposema, “Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu”, hatumaanishi kwamba mwili wa Yesu uliharibika taratibu kwa siku tatu, mpaka uliporejezwa wakati wa kufufuka Kwake. Tunatafsiri kwamba maana yake ni kwamba mwili Wake haukupatikana na aina yoyote ya uharibifu tangu alipokufa hadi alipofufuka.

Vivyo hivyo, tamko Lake kwamba nafsi Yake isingesahauliwa huko Sheol/Hades halihitaji kutafsiriwa kwamba aliachwa Sheol/Hades kwa siku chache, lakini hakusahauliwa huko moja kwa moja.[2] Badala yake, tafsiri sahihi ni kwamba nafsi Yake isingetendewa kama ya mtu asiye haki, kuachwa huko Sheol/Hades. Nafsi Yake isingekaa huko hata dakika moja. Ona pia kwamba Yesu alisema hivi: “Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu.” Hakusema, “Hutaacha nafsi yangu Kuzimu.”

Nafsi Ya Yesu Ilikuwa Wapi Kwa Zile Siku Tatu?

Kumbuka kwamba Yesu aliwaambia wanafunzi Wake angekaa siku tatu – mchana na usiku – katika tumbo la nchi (ona Mathayo 12:40). Hii haiwezi kumaanisha mwili Wake kuwa kaburini kwa siku tatu maana kaburi haliwezi kuhesabiwa kuwa ni “tumbo la nchi”. Yesu alikuwa anazungumza juu ya roho/nafsi Yake kuwa ndani sana katika nchi. Basi, tunaweza kusema kwamba roho/nafsi Yake havikuwa mbinguni kati ya kufa na kufufuka Kwake. Yesu alithibitisha hilo wakati alipofufuka alipomwambia Mariamu kwamba hajapaa bado kwenda kwa Baba Yake (ona Yohana 20:17).

Usisahau kwamba Yesu pia alimwambia yule mwizi aliyetubu pale msalabani kwamba angekuwa pamoja naye huko Paradiso siku hiyo hiyo (ona Luka 23:43). Tukiunganisha hayo yote, twajua kwamba roho/nafsi ya Yesu ilikaa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nchi, na sehemu fulani ya muda huo alikuwa mahali ambapo Yeye mwenyewe alipaita Paradiso. Hilo si jina lingine la mahali pa mateso paitwapo Sheol au Hades!

Yote hayo yanatuongoza kudhani kwamba lazima kuna mahali pengine katika tumbo la nchi licha ya Sheol/Hades, paitwapo Paradiso. Wazo hili linaungwa mkono na kisa ambacho Yesu alisimulia cha watu wawili waliokufa, mmoja mwenye haki na mwingine asiye haki – tajiri na Lazaro.

Palikuwa na mtu mmoja tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimualiyainua macho yake alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia akasema, ‘Ee baba Ibrahimu, nihurumie umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.’ Ibrahimu akasema, ‘Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu’ (Luka 16:19-26. Maneno mepesi kukazia).

Usisahau kwamba Lazaro na yule tajiri hawakuwa katika miili yao baada ya kufa, lakini walikuwa wamesafiri kwenda mahali pao kama roho/nafsi.

Lazaro Alikuwa Wapi?

Ona kwamba yule tajiri alijikuta yuko Kuzimu. Lakini, aliweza kumwona Lazaro mahali pengine, akiwa na Ibrahimu. Lazaro anasemekana alikuwa “kifuani pa Ibrahimu.” Hilo si jina la mahali penyewe bali pengine ni lugha ya kuonyesha faraja ambayo Lazaro alikuwa anapokea kutoka kwa Ibrahimu, baada ya yeye kufika mahali hapo.

Je, kulikuwa na umbali gani kati ya tajiri na Lazaro, baada ya kufa kwao?

Maandiko yanasema yule mtu tajiri alimwona Lazaro kwa mbali,” na tunaambiwa kwamba lilikuwepo “shimo kubwa” kati yao. Basi, umbali kati yao ni wa kukisiwa tu. Ila, inaonekana ni sawa kudhani kwamba umbali wao haukuwa mkubwa sana kama umbali wa tumbo la nchi na mbinguni. Maana ingekuwa hivyo, isingewezekana kwa tajiri kumwona Lazaro (bila ya msaada wa Mungu), na isingekuwepo haja ya kusema kwamba kuna “shimo kubwa” kati ya maeneo hayo mawili, lililoko makusudi ili kumzuia mtu asivuke kutoka upande mmoja hadi mwingine. Tena, yule mtu tajiri “alipaza sauti yake” kumwita Ibrahimu, na Ibrahimu akamjibu. Basi hii inatufanya tudhani kwamba walikuwa karibu tu kiasi cha kuzungumza.

Yote hayo yanatufanya tuamini kwamba Lazaro hakuwa mahali tunapoita mbinguni bali katika eneo tofauti ndani ya nchi.[3] Bila shaka hapo ndipo Yesu alipaita Paradiso wakati aliposema na yule mwizi aliyetubu. Hiyo paradiso katika tumbo la nchi ndipo wenye haki wa Agano la Kale walikwenda baada ya kuf akwao. Hapo ndipo Lazaro alipokwenda, na ndipo Yesu na yule mwizi aliyetubu walipokwenda.

Bila shaka nabii Samweli alikwenda huko pia baada ya kufa kwake. Tunasoma katika 1Samweli 28 kwamba, wakati Mungu aliporuhusu roho ya Samweli kutokea na kuzungumza na Sauli kinabii, yule mchawi wa Endori alimtaja Samweli kuwa “kama mungu anayepanda kutoka nchi” (1Sam. 28:13. Maneno mepesi kukazia). Samweli mwenyewe alimwambia Sauli hivi: “Mbona umenitaabisha kwa kunipandisha?” (1Sam. 28:15. Maneno mepesi kukazia). Inaonekana roho/nafsi ya Samweli ilikuwa Paradiso katika nchi.

Maandiko ni kama yanaunga mkono wazo kwamba, wakati wa kufufuka kwa Kristo, Paradiso ilifunguliwa na waliokuwemo kutoka, na wenye haki wote waliokufa katika kipindi cha Agano la Kale walipelekwa mbinguni na Yesu. Biblia inasema kwamba wakati Yesu alipopaa mbinguni kutoka pande za mwisho za nchi, “aliteka mateka” (Waefeso 4:8, 9; Zaburi 68:18). Hao mateka bila shaka ni wote waliokuwa wanakaa Paradiso. Yesu hakuwafungua watu kutoka Sheol/Hades![4]

Yesu Alihubiria Roho Zilizokuwa Gerezani

Maandiko pia yanatuambia kwamba Yesu alitangaza kitu fulani kwa kundi la watu – roho za watu – wakati fulani kati ya kufa na kufufuka Kwake. Tunasoma hivyo katika 1Petro 3.

Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani watu wanane, waliokoka kwa maji (1Petro 3:18-20).

Fungu hili la Maandiko linazua maswali ambayo hayana majibu. Kw anini Yesu aende kutoa tangazo kwa watu wasiotii, waliokufa wakati wa gharika ya Nuhu? Aliwaambia nini?

Pamoja na hayo, andiko hilo linaunga mkono ukweli kwamba Yesu hakukaa siku zote tatu mchana na usiku kati ya kufa na kufufuka Kwake, huko Paradiso.

Jehanamu

Siku hizi, miili ya wenye haki inapokufa, roho/nafsi zao huenda mbinguni moja kwa moja (ona 2Wakor. 5:6-8; Wafilipi 1:21-23; 1Wathes. 4:14).

Wasio haki bado wanakwenda Sheol/Hades, ambapo wanateswa na kusubiri ufufuo wa miili yao, na hukumu yao ya mwisho, na wao kutupwa katika “ziwa la moto”, mahali ambapo ni tofauti na Sheol/Hades.

Hili ziwa la moto linaelezwakwa neno la tatu ambalo wakati mwingine hutafsiriwa kuzimu. Neno hilo ni la Kiyunani – Gehenna. Ni jina linalotokana na mahali pa kutupa takataka nje ya Yerusalemu katika bonde la Hinomu, maali penye uozo mkubwa, penye funza na mabuu, na mahali ambapo daima palitoka moshi na kuwaka moto.

Yesu alipozungumza kuhusu Gehenna, alipataja kama mahali ambapo watu wangetupwa kimwili. Kwa mfano: Alisema hivi katika Injili ya Mathayo:

Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum [Gehenna]. … Msiwaogope wauuao mwili wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum [Gehenna] (Mathayo 5:30; 10:28. Maneno mepesikukazia).

Gehenna na Hades si mahali pale pale kwa sababu Maandiko yanasema kwamba wasio haki hupelekwa Hades kama roho/nafsi bila miili. Baada ya miaka elfu moja ya utawala wa Kristo ndipo miili ya wasio haki itakapofufuliwa na kusimama mbele za hukumu ya Mungu, kisha watatupwa katika ziwa la moto, au Gehenna (ona Ufunuo 20:5, 11-15). Tena, siku moja Hades penyewe patatupwa katika hilo ziwa la moto (ona Ufunuo 20:14). Basi, ni mahali tofauti na ziwa la moto.

Tartarus

Neno la nne ambalo mara nyingi hutafsiriwa kuzimu katika Maandiko ni la Kiyunani – tartaros. Linapatikana mara moja tu katika Agano Jipya.

Kwa maana ikiwa Mungu hakuwachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni [tartaros] akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu (2Petro 2:4).

Kikawaida, tartaros hudhaniwa kuwa ni gereza maalum kwa ajili ya malaika fulani waliotenda dhambi. Basi, si Sheol/Hades wala si Gehenna. Hata Yuda anaandika juu ya malaika walio kifungoni, hivi:

Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu (Yuda ms. 6).

Ubaya Wa Kuzimu

Mwenye dhambi anapokufa pasipo kutubu, hapati nafasi nyingine ya toba. Mambo yake yanakuwa yamekwisha. Biblia inasema hivi: “Watu wamewekewa kufa mara moja, na baada ya kufa, hukumu” (Waebrania 9:27).

Kuzimu ni kwa milele, na wale waliofungiwa huko hawana matumaini ya kutoka. Yesu alisema hivi kuhusu hukumu ya baadaye ya wasio haki, “Na hao watakwenda katika adhabu ya milele, bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Mathayo 25:46. Maneno mepesi kukazia). Adhabu ya wasio haki huko kuzimu ni ya haki, sawa ambayo uzima wa milele kwa wenye haki ulivyo haki.

Paulo naye aliandika hivi:

Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi … wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wamoto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasiotii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake (2Wathes. 1:6-9. Maneno mepesi kukazia).

Kuzimu ni mahali penye mateso yasiyoelezeka kwa sababu itakuwa adhabu isiyo na mwisho. Wasio haki watabeba hatia yao milele na kuteseka kwa hasira ya Mungu wakiwa wamefungiwa huko milele, katika moto usiozimika.

Yesu alipaelezea huko kama mahali penye “giza la nje,” ambapo kutakuwa na “kilio na kusaga meno,” mahali ambapo “funza wake hawafi, wala moto wake hauzimiki” (Mathayo 22:13; Marko 9:44). Tunahitaji kuwaonya watu kuhusu mahali hapo na kuwaambia juu ya wokovu upatikano katika Kristo tu!

Kuna dhehebu moja linalofundisha dhana ya purgatory – mahali pa utakaso, ambapo waamini watateseka kwa muda ili kusafishwa dhambi zao na kuweza kustahilishwa kuingia mbinguni. Wazo hilo halipatikani popote katika Biblia.

Wenye Haki Baada Ya Kufa

Wakati aaminiye anapokufa, roho yake inakwenda mbinguni mara moja, kwenda kuwa na Bwana. Paulo aliweka wazi jambo hili alipoandika kuhusu kifo chake mwenyewe.

Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana (Wafilipi 1:21-23. Maneno mepesi kukazia).

Ona kwamba Paulo alisema anatamani kwenda, na kama akienda, angekuwa na Kristo. Roho yake isingeingia katika hali fulani ya kupoteza fahamu huku akisubiria ufufuo (kama ambavyo wengine hudhani – kwa bahati mbaya sana).

Vile vile ona kwamba Paulo alisema kwake kufa kungekuwa faida. Huo ni ukweli ikiwa angekufa na kwenda mbinguni.

Katika barua yake ya pili kwa Wakorintho, Paulo alitangaza kwamba wakati roho ya aaminiye inapotoka katika mwili, huyo mwamini alikuwa “pamoja na Bwana”.

Basi siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana. … Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana (2Wakor. 5:6-8).

Hoja nyingine yenye kuunga mkono imo katika maneno haya aliyoandika Paulo:

Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye (1Wathes. 4:13, 14).

Kama Yesu atakuja na wale “waliolala” kutoka mbinguni, maana yake ni kwamba wako mbinguni pamoja Naye wakati huu.

Fununu Ya Mbinguni

Je, mbinguni pakoje? Kwa akili zetu finyu hatuwezi kupokea kikamilifu utukufu wote unaotungojea huko, na Biblia inatupa fununu kidogo tu. Ukweli wa kusisimua sana kuhusu mbinguni kwa waaminio ni kwamba tutamwona Bwana na Mwokozi wetu Yesu, na Mungu Baba yetu uso kwa uso. Tutakaa “nyumbani mwa Baba”.

Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi nanyi mwepo (Yohana 14:2, 3).

Tutakapofika mbinguni, siri nyingi ambazo akili zetu haziwezi kelewa kwa sasa, zitaeleweka. Paulo aliandika hivi:

Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi ninavyojuliwa sana (1Wakor. 13:12).

Kitabu cha Ufunuo kinatupa picha bora zaidi ya jinsi mbinguni palivyo. Mbinguni hapatakuwa mahali pa watu kuketi tu kwenye mawingu na kupiga vinubi kutwa kucha! Panaelezwa kuwa penye shughuli nyingi, uzuri wa ajabu, tofauti nyingi, na furaha isiyoelezeka.

Yohana ambaye alipata maono ya mbinguni, aliona kwanza kiti cha enzi cha Mungu, ambacho ni kiini cha ulimwengu wote.

Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi. Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu. Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu na heshima na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa (Ufunuo 4:2-11).

Yohana alijitahidi sana kueleza kwa lugha ya mbinguni mambo ambayo hayawezi kulinganishwa na chochote hapa duniani. Ukweli ni kwamba hatuna jinsi ya kuelewa kila kitu alichokiona mpaka tutakapojionea sisi wenyewe. Lakini, inapendeza sana kusoma.

Maelezo ya mbinguni yenye kusisimua sana yanapatikana katika Ufunuo sura ya 21 na 22, mahali ambapo Yohana alieleza kuhusu Yerusalemu Mpya, ambayo kwa sasa iko mbinguni, ila itashuka duniani baada ya kile kipindi cha utawala wa Yesu wa miaka elfu moja.

Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu, wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri. Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili. … Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake. Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa. … Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi. Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. … Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu. Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo. … Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele (Ufunuo 21:10 – 22:5).

Kila mfuasi wa Yesu atazamie maajabu hayo yote, mradi atadumu katika imani. Bila shaka tutatumia zile siku za kwanza tukiwa mbinguni kuambiana hivi: “Loo! Kumbe hiki ndicho Yohana alikuwa anajaribu kueleza katika Kitabu cha Ufunuo?”

–Imetafsiriwa na huduma ya David Servant

Advertisements

One thought on “Maisha mengine Baada Ya Haya!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s