Tanganyika ni nchi iliyonenwa katika unabii – Mchungaji Mtikila

MTIKILA (1)
HOJA MAALUM
MCHAKATO WA KATIBA MPYA USITISHWE
(ILI UANZE UPYA KWA USAHIHI)

Waheshimiwa Wajumbe, huu ni ushauri wa kizalendo kwa wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kwamba mchakato mzima wa Katiba mpya ubatilishwe pamoja na Rasimu ya Katiba, kwa misingi ifuatayo: KIGEZO CHA KWANZA Mchakato wa Katiba halali ya wananchi lazima uanze na uelimishaji wa wananchi wote, kwa sababu wananchi walio wengi hawajui kabisa suala la Katiba, kiasi cha wengine kudhani katiba ni aina fulani ya mboga, wakati ni jambo la msingi wa Taifa lolote duniani linalomhitaji kila mwananchi ashiriki, kama inavyoagiza Ibara ya 21(2) ya Katiba yetu iliyopo, kwamba ni haki ya kila raia kushiriki kwa ukamilifu. Katiba ya Nchi ni lazima itokane na makubaliano ya raia wote, tena kutokana na uelewa sahihi wa kila mmoja wao. Ndiyo maana hatua ya kwanza na muhimu kuliko zote ya kutengeneza Katiba ya Nchi ni uelimishaji makini wa familia yote, zoezi ambalo linaweza kuchukua miaka, kama wenzetu wa Kenya walivyotumia takriban miaka mitatu kuelimisha umma wao ingawa uliokuwa na ufahamu kuliko umma wetu. Ni dhahiri kwamba hata ukusanyaji wa maoni uliofanyika hauna uhalali, kwa sababu yalichukuliwa maoni ya katabaka ka wananchi wachache sana wenye uelewa. Haijalishi hata kama hao waelewa wachache walitoa maoni mazuri yakatengenezewa Rasimu hii, Katiba inamtaka kila raia aeleweshwe vizuri ili ashiriki kwa ukamilifu. Ni usanii kusema wanakusanya maoni ya watu, wakati watoaji wa maoni wametegewa sheria kandamizi kama za “Uchochezi’’ ili wasizungumzie machafu ya watawala yaliyowatesa kwa miaka 53 ya uhuru, kusudi waweze kuyadhibiti vizuri katika Katiba yao. Ndiyo maana tulisema kwanza yafutwe yale masheria kandamizi, ili raia wakishaelimishwa kuhusu Katiba yao waweze kutoa maoni yao bila woga. Hakuna mjadala hapa, kinachotakiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba, siyo matakwa ya Rais au CCM. Katiba inataka itumike HAKI sawa kuunda chombo cha haki sawa na wajibu sawa kwa nchi yetu kwetu sisi sote na vizazi vyetu vyote vijavyo. Mchakato wa Katiba unaoendeshwa bila uelewa na uhuru kamili wa wananchi, moja kwa moja unakuwa hauna uhalali, haijalishi hata kama mapesa mengi kiasi gani yametumika katika haramu hiyo. Haramu haiwezi kuzaa halali. Bunge maalum la Katiba linapaswa kuukataa. Katiba inayotokana na kugoma kuwapa ufahamu sawa wananchi wote, na kutumia maoni ya kakundi kadogo tu ka wananchi kwa kuwapuuza raia zaidi ya milioni 46 si halali, tena ni ubaguzi wa kikatili na ukiukaji wa Ibara ya 12 na ya 13 ya Katiba ya Jamhuri. Haramu haiwezi kuzaa halali. Ni wajibu wa Bunge maalum la Katiba kuukataa mchakato mzima wa Katiba mpya, kwa uaminifu kwa Mungu, kwa Wana wa Tanganyika na wananchi wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar. KIGEZO CHA PILIKusimamiwa na watawala utengenezaji wa Katiba ya wananchi, tena viongozi wa CCM isiyoficha azma yake ya kutawala juu ya wenzao milele licha ya kuchukiwa vibaya sana na wananchi, kunafuta kabisa uhalali wa mchakato mzima wa Katiba. Serikali ni kiungo kilicho ndani ya Katiba ambayo ni ya Wananchi, kama isemavyo Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri kwamba mamlaka yote ya utawala wa nchi yamo mikononi mwa wananchi wenyewe, yaani hata mamlaka ya utengenezaji wa Katiba yao wanayo wao, si ya Rais au serikali yenye kuajiriwa tu na wananchi! Kitendo cha Rais cha kuteua yeye Tume ya kukusanya Maoni bila kuwaelewesha kwanza wananchi, na kuipa yeye maelekezo, na kuilipa mapesa lukuki kama rushwa, na kuwanyangánya raia haki yao ya kuhoji juu ya uhalali wa muungano, kinapoteza uhalali wa mchakato mzima wa Katiba, Ndugu Wajumbe, kitendo cha Rais cha kuteua yeye wajumbe wa Bunge la Katiba kwa kuzingatia maslahi yake binafsi na ya chama ckake, badala ya kuwaelewesha wananchi wote vyakutosha, ili wachague wao wenyewe wajumbe wao katika Bunge maalum la Katiba yao, kutokana na kuwaamini jinsi walivyo na mzigo juu ya hatima ya nchi yao na hatima yao na watoto wao, kimelikosesha Bunge hili uhalali Bunge maalum la Katiba limekoseshwa uhalali na Rais Kikwete, kwa kupendelea wanasiasa kwa asilimia 90% na hasa wa chama chake, aliowapenyeza kwa wingi kwa kutumia taasisi za kiraia, majority ya wabunge wao katika Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyojitoa katika muungano (kitendo ambacho ni matusi kwa Watanganyika), ilimradi CCM wajipatie theluthi mbili za kujipitishia maslahi yao. Katika Watanganyika milioni 48 wanasiasa wako takriban milioni 5, hivyo kwamba wananchi milioni 43 wamepuuzwa katika mchakato wa Katiba. Kwahiyo Katiba itakayoundwa haitakuwa ya Wananchi au Taifa bali ya katabaka kadogo tu. Miongoni mwa wananchi milioni 43 waliopuuzwa ni Jumuiya ya Wapentecoste (PCT) yenye walokole takriban milioni 10, ambao Rais Kikwete amekataa kuwapa uwakilishi katika Bunge maalum la Katiba! Ndugu wajumbe, kuwanyima wananchi wengi namna hii uwakilishi katika Bunge la Katiba ya wananchi wote, kwa kisingizsio chochote kile, kumefuta kabisa uhalali wa Bunge hili. Katika mchakato halali wa Katiba utakaoanza upya, Wawakilishi wa wananchi watachaguliwa na wananchi wenyewe. Ndugu Wajumbe, hata Libya kulikomwagika mito ya kutisha ya damu, tumeshuhudia juzi wananchi wake wakipiga kura kuwachagua wawakilishi wao katika Bunge lao la Katiba. Bunge letu limekosa uhalali kwa kuteuliwa na mtu mmoja tu badala ya kuchaguliwa na wenye nchi. Rais amekiuka Katiba ya Nchi yetu Ibara ya 8, na Ibara ya 21 (2), na Ibara ya 26 (1). Kwahiyo imetupasa sisi Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kutoa Tamko kwa uaminifu na heshima kwa Taifa letu kwamba: 1. Bunge maalum la Katiba lenyewe halina uhalali. 2. Mchakato wa Katiba mpya uanze upya kwa usahihi, kwa kuanza na kufuta sharia kandamizi na kuuelewesha umma kwa makini. Kuitishwa Kongamano la Kitaifa la Katiba hakuwezi kukwepeka katika utengenezaji wa Katiba halali ya wananchi, ambao lazima ufuatie ueleweshaji makini wa wananchi wote, kusudi wote watoe maoni yao kwa uelewa na uzalendo. Ni hilo Kongamano ambalo litateua serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa, ambayo itasimamia mchakato mzima wa Katiba kizalendo na bila upendeleo. Baada ya kukamilisha utengenezaji wa Katiba, Serikali ya mpito ya umoja wa Kitaifa itaitumia Katiba hiyo kwa uchaguzi, na kukabidhi uongozi kwa Serikali mpya itakayochaguliwa kwa Katiba hiyo mpya. Utaratibu huu wa kupata Katiba halali ya wananchi unawezekana tu ikiwa CCM itakuwa imepona ubinafsi na uchoyo wa madaraka, na ikiwa kweli CCM wanayo dhamiri safi na ustarabu wa kuheshimu usawa wa wananchi wote. CCM walikataa utaratibu huu wa haki na usawa, kwa sababu ya uovu wao wa kutaka wawe watawala tu wengine wote tuwe watawaliwa wasio na haki kama wao, unaowafanya wazidi kuchukiwa nchini kote na kubaki kutawala kwa nguvu za dola badala ya ridhaa ya wananchi. KIGEZO CHA TATU Tamko la kiimla la Rais Kikwete kwamba muungano usijadiliwe katika mchakato wa Katiba mpya ya wananchi, linafuta uhalali wa mchakato wenyewe pia. Kwani muungano ni uhusiano wa nchi mbili unaopaswa kuwa wa hiari ya raia wenyewe na siyo ya watawala! Rais amekiuka Ibara ya nane ya Katiba ya Nchi. Upungufu huu wa Rais unachangiwa na udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na Bunge la Jamhuri, alipolihutubia kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, alipotamka kuwa hataitii Katiba kama vile msahafu, bali katika mambo mengine atatumia busara yake! Badala ya kumwondoa katika ajira ya wananchi aliyoiapia kwamba ataitii na kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi, akainua msahafu juu na kumwambia Mwenyezi Mungu amsaidie, Wabunge wetu walimshangilia! Si ajabu leo Rais kujisahau akatumia imla katika suala la muungano, wakati ndio msingi wa mengine yote katika mchakato wa Katiba mpya! Rais anapaswa kufahamu kuwa suala la muungano linahusu Uhuru wa Wazanzibari na Uhuru wa Wana wa Tanganyika! Msingi wa Taifa la Watanganyika ni Uhuru wa Tanganyika, kama na Taifa la Wazanzibari lilivyoanza na Uhuru wa Zanzibar.Muungano wao ni uhusiano tu wa nchi na nchi, ambao malengo pekee huwa ni maslahi, hivyo kwamba muungano ukithibitika kuwa unaathiri Uhuru wetu na uchumi wetu sisi Watanganyikatunapaswa kujitoa mara moja, kama ilivyojitoa rasmi Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Ndiyo maana Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha lile Azimio la kuundwa Serikali ya Tanganyika, mwaka 1994, hivyo kwamba wajibu wa Bunge maalum la Katiba ni kuwawajibisha wale waliokiuka Uamuzi huo wa Bunge, ambao kikatiba una uzito wa Sheria, na kuhakikisha kwamba Azimio hili linatekelezwa. Katika Nchi yenye Utawala wa Sheria hakuna kujadili jambo lililopitishwa na Bunge, bali utekelezaji tu wa hilo lililopitishwa. Usahihi (Constitutionality) wa agizo la Rais Kikwete kwamba muungano usijadiliwe katika mchakato wa Katiba mpya ya wananchi, ungesimama katika uadilifu wake wa kuzingatia kiapo chake cha kuitii na kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi, akitetea Azimio lililopitishwa na Bunge la Jamhuri la kuundwa Serikali ya Tanganyika kwamba ni la kutekelezwa tu na siyo kujadiliwa(Suala hili la “muungano” limeelezwa kwa kina zaidi katika Sehemu ya Pili ya Waraka huu) Mchakato pekee ulio na uhalali ni wa Katiba ya Watanganyika, ambao wanapaswa kuunda Serikali yao. Uhuru wao hauhamishiki wala haubadilishiki kwani ni haki yao ya Msingi ya kujitunza uhai wao na watoto wao ndani ya mipaka ya ardhi yao. Haki ya Watanganyika ya Uhuru wao walipewa na Mungu, kama wanadamu wengine wote katika mipaka ya ardhi yao. Ni matusi makubwa kwa Watanganyikia hata kama hawasemi, kwa Zanzibar iliyojitoa katika muungano kuleta wawakilishi wengi kuzidi Tanganyika yenyewe katika Bunge maalum la Katiba, ambalo kimsingi ni la Watanganyika, tena wakaleta mpaka na baraza lao la Wawakilishi lililouvunja muungano kwa kuitoa Zanzibar, bila hata haya kwa kuwachukulia Watanganyika kuwa ‘mataahira’ tu! Saa ya ukombozi ni sasa! Matusi kwa Watanganyika ni machungu zaidi wakoloni wao waliojitoa katika muungano, ambao wako milioni 1 tu, wanapokuwa na wajumbe wengi kuwazidi Watanganyika milioni 48, kiasi cha Wazanzibari kutulazimisha kwa huo uwingi wao kuwa chini ya Uwenyekiti wa muda wa Kificho wao katika Bunge maalum la Katiba! Kutokana na ule unyani, tende na halua zimewafanya wauzaji wa Uhuru na heshima ya Watanganyika wafanye makusudi kwamba chaguzi zote zikifanyika Watanganyika wawe katika minyororo ya Wazanzibari. Ndugu Wajumbe, kila mwadamu aliumbwa na nationalistic spiritau uhanga kwa ajili ya nchi yake pamoja na ndugu zake wa Taifa lake. Ndiyo maana wazee wetu walipouzana utumwani kwa tamaa ya tende na halua tu, wazungu waliotutangulia kustarabika walitudhania kuwa aina fulani ya nyani. Siyo ajabu kuonekana hata leo Mtanganyika anauza au kutoujali utaifa wake na ardhi yake na utambulisho wake (national identity), kwani bado tunao watumwa wenye “unyani” wa kuuza utaifa wetu kwa tende na halua. Ni matusi kuiita Tanganyika “Tanzania Bara” “Unyani” ule ndio unaowafanya baadhi ya Watanganyika wafurahie kongwa la utumwa wetu kwa Wazanzibari, ambao hata baada ya kujitoa rasmi katika muungano feki, bado wanaendelea kutawala Watanganyika na kuishi kwa damu yao, Manzibari mmoja akiwa amepewa thamani ya Watanganyika 48 katika kuitawala Tanganyika, lakini gharama za nchi zote mbili zinabebwa na Watanganyika! KIGEZO CHA NNE Mchakato wa Katiba ukiwa nje ya misingi ya Katiba na Sheria unakuwa BATILI. Rais, Wajumbe wa Tume ya kuratibu maoni na Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, wanalazimishwa na Ibara ya 26(1) kutii Katiba na Sheria za nchi. Kwa sababu wakipuuza au kukiuka Katiba au Sheria wanakuwa wamepoteza uhalali wa hiyo Tume au hilo Bunge pamoja na maamuzi yake Mfano wa kwanza ni kitendo cha Rais cha kupokonya haki ya wananchi ya kujichagulia wao wenyewe wawakilishi wao katika Bunge maalum la Katiba, akatuteua yeye sisi wajumbe wa Bunge hilo! Ni kosa kubwa pia Rais kuteua yeye Tume ya kuratibu maoni, ambayo kimsingi ilipasa kuchaguliwa na wananchi wenyewe! Rasimu ya Katiba inayotokana na makosa haya haiwi na uhalali, kwa sababu ni ya watawala na siyo ya wananchi, tena ni ukiukaji wa Ibara ya 8 ya Katiba. Isitoshe, Rais aliipa Tume yake ya kuratibu maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Katiba posho ya shilingi 500,000 kwa siku mbali ya mamilioni ya mshahara mwisho wa mwezi, nyumba yenye kodi ya shilingi milioni kadhaa kwa mwezi, shangingi la zaidi ya shilingi milioni 60 kila mmoja, na madereva akawalipia posho ya shilingi 220,000 kila mmoja kwa siku, lakini akawadhalilisha Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba lenye kuikataa au kuipitisha hiyo Rasimu, yaani liko juu kabisa ya hiyo Tume, kwa kuwapa posho ya dereva wa mjumbe wa Tume ya shilingi 220,000 tu! Kwa busara hata ya mtoto mdogo, Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba anapaswa kupewa mafao ya juu kuliko mjumbe wa Tume ya Warioba. Kama Rais alifanya kosa kuwapendelea wajumbe wa Tume yake ya Maoni, basi hapaswi kusahihisha kosa kwa kosa kubwa zaidi! Kama Rais hawezi kusahihisha kosa lake kwa kuwabana wajumbe wa Tume ya Warioba warudishe mabilioni ya fedha aliyowapa, ili wawe wamelipwa kwa usahihi yaani chini ya kiwango cha Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, basi usahihi na busara pekee ni kuwalipa Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba juu zaidi kuliko wajumbe wa Tume. Tena ni marufuku kukiuka Ibara ya 13 ya Katiba ya Nchi kwa kuwalipa Wabunge wa Bunge la Muungano mishahara na posho zao juu ya mafao ya Bunge maalum la Katiba. Ikiwa kosa hili limefanyika ni lazima na Wajumbe 201 walioteuliwa wepewe hiyo tofauti, ili kufuta kosa kubwa ladiscrimination lililofanyika. Hili ni suala lisilohitaji mjadala wala kubembeleza mtu, bali ni suala la usahihi na busara. Mfano wa pili nikitendo cha Tume ya Warioba ya kuratibu maoni na mchakato mzima kwa jumla, cha kupuuza kesi muhimu sana iliyo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, ambayo wananchi wanataka uvunjwe muungano unaounganisha Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika! Katiba inayotokana na kutojali Katiba na Sheria na kudharau Mahakama kiasi hiki haiwezi kuwa na uhalali. Mfano wa tatu ni kitendo cha Tume ya kuratibu maoni ya Katiba, inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani Joseph Warioba, cha kuendelea na kukusanya maoni juu ya Haki ya kila raia ya kugombea Urais, Ubunge, udiwani na serikali za mitaa bila kujiunga na chama cha siasa, na kuiingiza haki hii katika Rasimu ya Katiba ili eti itolewe uamuzi na Bunge maalum la Katiba, wakati uamuzi ulikwishatolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania! Hata baada ya kuhujumiwa na Mahakama ya Rufaa, wananchi walirudishiwa Haki hii na Mahakama ya Afrika, ambako Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Wanasheria sita! Mchakato wenye kudharau Mahakama mpaka za kimataifa kiasi hiki hauna uhalali wala hauwezi kuzalisha Katiba yenye uhalali! Ni dhahiri kwamba huu ni mchakato feki, uliokosa kabisa hata maadili mema ya taaluma ya Sheria! Mfano wa nne ni kitendo cha Tume ya maoni cha kupuuza hata Sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Tanzania ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika. Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba tunao wajibu wa kubatilisha mchakato huu kwa kuwadhalilisha wananchi na kukiuka Katiba ya Nchi yetu na Utawala wa Sheria, kwa kupuuza Hukumu ya Mahakama ya Afrika iliyotoa Haki ya kila raia wa Nchi yetu ya kugombea Urais, Ubunge na Udiwani bila kulazimika kujiunga na chama cha siasa. Kwa uovu wao bado waliendelea na ukusanyaji wa maoni kuhusu Mgombea binafsi hata baada ya Mahakama ya Afrika kumpa kila raia wa Nchi yetu haki hii. Isitoshe wameiingiza HAKI hii hata katika Rasimu ya Katiba, kwamba eti Bunge maalum la Katiba liijadili bila kujali Hukumu ya Mahakama ya Afrika, badala ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba inaingizwa ipasavyo katika Katiba hata hiyo mpya ikiwa tayari, na katika Sheria husika za Nchi! Wajibu wa Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba mpya ni kuibatilisha Rasimu hii ya Katiba, na kuagiza kwamba Mchakato wa uundaji wa Katiba uanze upya kwa usahihi, uzalendo, na kwa uzingatiaji wa Katiba na Sheria kwa makini. Hoja hii imewasilishwa na Mjumbe wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila. Mungu ibariki Tanganyika

Sehemu ya Pili
ULAZIMA WA KUVUNJA KINACHOITWA ‘MUUNGANO’
(Kwa ajili ya Uhuru wa Wana wa Tanganyika)

Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, Moja ya maajabu ya dunia ni sisi Watanganyika kulikubali kongwa la utumwa kwa Wazanzibari kama mataahira, tukakubali hata kudhalilika kama koloni lao, wakati ni Watanganyika wale wale waliomwaga damu yao kwa ajili ya uhuru wa watu wengine! Hii si ile laana tuliyotabiriwa katika Torati tu, bali tu waathirika pia wa ushirikina kama wa “mwenge” na political anesthesia iliyotupofusha kifikra, ikatupandikiza roho ya woga, na kutuhasi maumbile ya binadamu wote ya uhanga kwa ajili ya uhuru wao na utu wao. Ndivyo wahusika walivyofanikiwa kutufanya sisi Watanganyika tusione vibaya kudhalilika kama watumwa au mifugo ya watu wengine!Wajumbe tukumbuke kwamba Uhuru wa kila nchi hautokani na itikadi ya mtu wala ya chama, bali ni mpango wa Mungu kama ilivyoandikwa Kwa maana Mwenyezi Mungu ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote, na ndiye aliyefanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao, ili wamtafute Yeye Mungu ingawa ni kwa kumpapasa papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wao. Ndiyo maana kila taifa lina ibada na wimbo wake wa kumtafuta Mungu aibariki nchi yake, na kuidumishia uhuru na umoja wake kama familia moja kubwa. Kuhusu mipaka ya Utaifa wa kila Nchi, Mungu alipiga marufuku watawala wasithubutu kubadili alama za mipaka watakayoona aliiweka kwa kuwatumia waliokuwa kabla yao, na amesisitiza kwamba yule atakayethubutu kufanya hivyo na alaaniwe, na wote waseme Amina. Tena tumewekewa masharti katika Torati kwamba kila nchi itawaze mtu mwenye sifa zipi ili aweze kuongoza taifa lake kama inavyompendeza Yeye Mwenyezi Mungu, atawalaye juu ya falme zote za wanadamu. Laana ya Tanganyika ilianzia hapo, ilipomtawaza mtawala aliyegeuza sifa na utukufu wa Mungu apewe yeye, kama alivyofanya Lucifer hata akatupwa chini.

UHURU WA TANGANYIKA

Ndugu Wajumbe, Tanganyika ni nchi iliyonenwa katika unabii, ikiambiwa “Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa”, yaani isiyotulia kujijenga kimaendeleo ili watoto wake wamwishie Mungu katika furaha aliyowakusudia, bali inayojitoa kafara kwa ajili ya maslahi ya nchi zingine kama Zanzibar, kama mshumaa unavyowaangaza wengine kwa kujiyeyusha wenyewe, jambo ambalo limeonywa katika Torati kwamba ni laana. Tanganyika inavyodhalilika na kunajisika na kuliwa na Zanzibar ndiyo hali inayoitwa “muungano”! Mwenyezi Mungu aliubariki Uhuru wa Tanganyika (Kanani ya Afrika) tarehe 9 Desemba 1961, kwa kushusha nchini kote viumbe vilivyokuwa na bendera ya Tangantika, vikiwa ni pamoja na nzige, aina ya viwavi juu ya miti, senene, maua na upinde kama wa mvua. Wanaothubutu kuchezea Uhuru wa Tanganyika wana ujasiri gani kuliko Ibilisi, kama imeandikwa katika mambo yanayogusa utukufu wa Mungu hata mashewtani waamini na kutetemeka? Historia ya kweli ya Tanganyika na uhuru wetu ilichakachuliwa, ili kumvika yule dikteta uungu wa taifa letu, lakini ukweli unatayarishwa kwa ajili ya watoto wetu na vizazi vyetu vijavyo. Kwa ufupi Uhuru wetu tulipewa na UNO mwaka 1961 kupitia kwa Mwingereza, aliyekuwa na dhamana ya kutuandaa ili tupate kujitawala wenyewe. UHURU ni haki ya msingi ya Binadamu wote ulimwenguni ya Self determination. ikiwa sehemu muhimu ya utu wao (essential and basic ingredient of their humanity). Ndiyo maana kama kiitwacho ‘muungano’ kinaathiri uhuru na heshima ya Tanganyika ni lazima kitokomezwe! Swali: UHURU ni nini? Kwanini damu nyingi imemwagika duniani kwa ajili ya Uhuru, mpaka na ya Watanganyika ikapotea kwa ajili ya Uhuru wa watu wengine? Kwanini kongwa la ‘muungano’ linalazimishwa kwa Watanganyika wakati linaathiri Uhuru na utu wa Watanganyika, hata tukawa mithili ya koloni la Wazanzibari? Jibu: Uhuru ni HAKI ya msingi ya watu wa kila nchi ya kujitunza wao wenyewe na watoto wao ndani ya mipaka ya ardhi yao, kwa utaratibu waliojiwekea wenyewe (Katiba) na kuutumia kujiundia chombo chao wenyewe (Serikali) cha kutunzia vizuri iwezekanavyo uhai wao ndani ya mipaka ya ardhi yao, ili wapate kuishi kwa furaha kwa siku zote alizowapa Mwenyezi Mungu kuwepo duniani, wakiwa na utambulisho wao (national identity) kama familia kubwa inayojiamulia mambo yake yenyewe kwa ajili ya hatima yake. Hii ni Haki ya Watanganyika pia, na UNO ilitupatia rasmi Uhuru wetu kwa sababu ni Haki ya Msingi ya Binadamu wote(The right to self determination), haki ambayo ni kiungo cha mwanadamu sawa na mguu au kichwa chake, niHaki isiyoweza kuhamishika wala kubadilishika (a Basic Right which is an ingredient of humanity, which is non transferable and non exchangeable. It is the basic right to our territorial integrity, self governance, sovereignty and national identity as sons and daughters of the soil, our Mother Tanganyika). Kuiita Tanganyika ‘Tanzania Bara’ ni matusi kwa Mungu na Watanganyika

KUVUNJA KONGWA LA UTUMWA KWA WATANGANYIKA LIITWALO “MUUNGANO”

MUUNGANO NI NINI? ULIUNDWA NA NANI? KWA LENGO GANI? Ndugu Wajumbe, Bilashaka inaeleweka kwamba muungano ni uhusiano tu wa nchi moja na nyingine, kwa ajili ya maslahi, na hasa ya kiuchumi. Kwani kinachoitwa “Muungano wa Tanzania” kisingeweza kuumba upya nchi zetu, au kuondoa bahari inayotutenganisha, bali ni muungano wa huduma kuu za kiutawala zinazoendesha maisha ya kila siku ya hizi nchi mbili. Yaani muungano halali ni uchangiaji nusu kwa nusu wa gharama ya uendeshaji wa maisha ya nchi washirika, kwa ajili ya faida sawa zilizokusudiwa kwa pande zote za huo uhusiano. Ukweli ni kwamba walichohitaji Watanganyika baada ya uhuru wao ni kuijenga nchi yao na kuboresha maisha yao, kwa kutowesha umasikini, ujinga na maradhi, kwa kutumia kizalendo raslimali zao lukuki. Wala Tanganyika haikuhitaji chochote kutoka Zanzibar. Kiitwacho muungano kilitokana na vita baridi kati ya mataifa mababe ya Magharibi na ya Mashariki yaani Wakomunisti, baada ya mapinduzi ya Zanzibar, ambapo Wakomunisti waliwawahi Wamarekani kukamatana na utawala mpya wa Zanzibar, kama walivyokuwa wamewawahi Cuba hata wakaweka huko makombora yao yaliyohatarisha usalama wa Marekani. Marekani ilipozisitukia siri za mahasimu wao za kutaka kuweka makombora yao Zanzibar, walimkimbilia Mzee Kenyatta kumbembeleza afanye muungano hata wa bandia na Zanzibar, ili uwasaidie kuwadhibiti kabisa Wakomunisti wasijichimbie Zanzibar na kuweka makombora yao kama walivyokuwa wamefanya Cuba, kwa sera ya kutofungamana na upande wowote wa hiyo vita baridi. Ujumbe wa CIA ulipotimuliwa na Kenyatta kwamba marufuku kuchezea Uhuru wa Kenya walioupata kwa damu, ndipo ulipotumika usaliti na ukibaraka wa Julius Nyerere! Karume akadanywa kwamba setalaiti zao eti zimeona manowari za kivita zikielekea kupokonya nchi aliyoikomboa, sharti la kumsaidia likawa aungane na Nyerere ili msaada upitie kwake.Katika kutekeleza matakwa ya CIA ni kweli kwamba baada ya «muungano» Nyerere aligeuka kipaza sauti kikuu cha kaulimbiu yaKutofungamana na upande wowote, na ni kweli kwamba kwa mbinu hizi Wamarekani walifanikiwa kuwahujumu Wakomunisti wasitegemissiles zao Zanzibar. Kwa jinsi Nyerere alivyoutoa kafara Uhuru wa Tanganyika kwa ajili ya maslahi ya Marekani, na bado akaweza kuwapofusha Watanganyika kifikra wasitetee uhuru wao hata kwa damu, na kuwadhibiti wasifahamu siri yake badala yake wamwone yeye kama mungu wao wakati ndiye adui mkuu wa uhuru wao, Kenyatta alighadhabika sana na kusema, Hakika Nyerere anatawala maiti! Katika kuficha doa la ukibaraka wa Nyerere kwa Marekani na usaliti wake kwa Watanganyika, ili kumwezesha asifiwe na kuadhimishwa milele, zilitungwa sababu FEKI za kijinga mno za huu muungano : 1. Eti ‘usalama’, kwamba adui wa Zanzibar angeweza kujificha kwetu na adui zetu wakajificha Zanzibar. Huu ni upuzi mtupu kwavile visiwa vingi ni majirani wa nchi za mabara, lakini hawana miungano wala kuhujumiana, wala hatari ya vita hailetwi na visiwa, kama ambavyo vita yetu na Uganda haikutokana na visiwa. 2. Eti kwa sababu Zanzibar kuna makabila yanayotoka Tanganyika! Basi tungeungana na Kenya waliko Wajaluo, Wamasai, Wakurya, Wapare na Wachaga wengi zaidi ya mara tatu ya Wanzibari wote, au Msumbiji waliko Wayao, Wanyasa na Wamakonde wengi kuliko Wazanzibari, au Zambia waliko Wanyamwanga wengi pia. Hiki ni kigezo cha kufilisika kifikra, kilicholenga kumfichia Nyerere uuzaji wake wa uhuru wa Tanganyika kwa maslahi ya Marekani. Muungano wenyewe ulikuwa uangaliwe upya baada ya miaka 10, kama bado ungehitajika tuendelee nao au la. Na Karume akiwa shujaa wa kuweka hatima ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mikononi mwa Wazanzibari wenyewe, alitarajiwa kurudisha heshima ya Utaifa wa Wazanzibari, kwani alikwishaanza hata kupinga sera nyingine za Nyerere zisivuke kisiwa cha Chumbe, ziishie huko huko Tanganyika. Karume aliuawa baada ya miaka nane ya muungano, katika mazingira ya kutatanisha. Baada ya kugundua juhudi na mikakati ya Nyerere ya kuficha kabisa kiini cha muungano, yaani siri ya kutumiwa na Marekani akauza uhuru wa Tanganyika, Zanzibar ilikataa kabisa kuchangia gharama za huo muungano, ikijua kuwa Nyerere lazima angebeba mzigo wote kwa ajili ya kutoruhusu muungano wake uvunjike, kwavile ukivunjika lazima siri ya uhujumu wake wa Uhuru wa Watanganyika itafunuka, na kumfanya achukiwe na kulaaniwa milele. Nyerere alifaulu kujiweka mahali pa mungu katika mioyo ya watu, na genge la kimafia la CCM linalodumisha ibada yake kama vile ndiyo hirizi yao ya kutawala nchi milele, ndilo linalolazimisha kongwa la utumwa la muungano pamoja na makafara yake ya kutawalia akili za watu, kama vile mbio za mwenge, bila kujali jinsi kongwa hili linavyoimaliza Tanganyika kiuchumi na kuifanya koloni la Wazanzibari. Ndugu wajumbe, kwavile muungano unaathiri uhuru wa wana wa Tanganyika na hatima yao, Bunge maalum la Katiba linalazimika kujiridhisha kwanza kabisa na uhalali wake, kwa kuzingatia majeraha ya kiuchumi na Uhuru wa Tanganyika. Ukweli ni kwamba Tanganyika ni kafara inayoliwa bure na Zanzibar ambayo tangu mwaka 1964 hadi leo imeishi kwa zaidi ya shilingi trilioni 120 za damu ya Watanganyika, ambazo ni lazima ieleweke zitalipwaje. Saa ya ukombozi ni sasa! Ukupe na ukoloni wa Zanzibar kwa Tanganyika unaoitwa muungano ndio uliopelekea kufutwa matibabu ya bure ya wana wa Tanganyika, bila kujali wanavyokufa ovyo leo kwa magonjwa ambayo yanatibila! Ukupe huu ndio uliolazimisha kufutwa elimu nzuri ya bure ya wana wa Tanganyika, ukapelekea wengi wa watoto wa Tanganyika sasa kuishia uzururaji, umachinga, na kubwia unga na kuelekea kuwa taifa la uhalifu na upunguani! Kulazimisha maisha ya raha na utajirisho kwa Wazanzibari kwa jasho la Watanganyika na raslimali za Watanganyika ni maandalizi ya mmwagiko wa damu, ambao unaepukika leo kwa kuvunja muungano!

ARDHI YA TANGANYIKA KAMWE SI YA MUUNGANO

Ndugu wajumbe, muungano umewapa bure Wazanzibari ardhi ya Watanganyika, na siyo siri kwamba Wazanzibari wanajimilikisha kwa kasi kuliko Watanganyika wenyewe, wanaogeuzwa na muungano kuwa wakimbizi katika nchi yao wenyewe. Watanganyika wamepofushwa akili wasiione hatari kwamba walikuwa milioni 8.5 tu walipokabidhiwa nchi yao tarehe 9 Desemba 1961, lakini leo wako milioni 48 wakati ardhi yao haijaongezeka hata inchi moja! Wazanzibari wanashauriwa waanze kuwauzia Watanganyika ardhi yao waliyokuwa wamewatapeli kwa kigezo cha «muungano» sasa watapata pesa nzuri, kuliko watakapoamka Wana wa Tanganyika kuitwaa ardhi yao. Ndugu wajumbe, mbali ya Tanganyika kuangamizwa na muungano kiuchumi, tangu mwaka 1964 ilipoteza Uhuru wake kwa kupokonywa haki yake ya kuwa na Katiba yake na serikali yake yenyewe ndani ya mipaka ya ardhi yake! Tusingoje Watanganyika wamwage damu kwa ajili ya Uhuru wao, bali Bunge hili litumike kuwapa haki yao kwa kuvunja kongwa hili la ‘muungano’ kwa amani. Saa ya ukombozi ni sasa!

KUUNDWA SERIKALI YA TANGANYIKA

Ndiyo maana mwaka 1994 Bunge la huo ‘muungano’ lenyewe lilipitisha Azimio la Kuundwa Serikali ya Tanganyika, ambalo bado liko hai.Kama kweli utawala wetu ni wa Kikatiba na Kisheria, basi ni wajibu wa Bunge hili la Katiba kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanganyika inaundwa, bila mjadala wowote kwa sababu ni Sheria, yaani uamuzi uliopitishwa na Bunge la Jamhuri. Ni muhimu kwa kila Mjumbe wa Bunge la Katiba kupitia Hansard ya Azimio hili Takatifu. DP ilimwandikia Rais Kikwete na waziri wake wa Fedha hayati William Mgimwa, waziri wa masuala ya muungano katika ofisi ya Makamu wa Rais na Waziri wa Sheria, kwamba watuambie ni kiasi gani cha fedha ya Watanganyika iliyotunza maisha ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar tangu mwaka 1964 (ambayo inakisiwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni 120), lakini hatukujibiwa!Lakini Mahakamani watatueleza tena kwa adabu. Ndugu Wajumbe, mmeelewa kwamba Muungano ni unyang’anyi wa Haki ya Msingi ya Uhuru wa Tanganyika, ambao nchi nyingi zimeupata kwa kumwagika damu, hata yetu sisi Watanganyika. Ukoloni ni nchi yoyote kuwa na viongozi wa ngazi za urais, uwaziri, ukatibu mkuu, ukurugenzi wa taasisi za kiserikali, ukuu wa mikoa na wilaya n.k kutoka nchi nyingine, kama Tanganyika inavyokaliwa na watawala kutoka Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Saa ya ukombozi ni sasa! Huu ni ukoloni halisi, hakuna mjadala, siyo muungano kwa sababu ni Tanganyika tu kuliwa na kutawaliwa na Wazanzibari, lakini ni marufuku kabisa Mtanganyika kuthubutu kwenda kuitawala Zanzubar. Ni sawa kabisa na Waingereza walivyokuja kuitawala Tanganyika, lakini ni marufuku kabisa Mtanganyika kwenda Ulaya akaitawale Uingereza! Saa ya ukombozi ni sasa! Ndugu Wajumbe, utumwa na udhalili wa Watanganyikakwa watu wa Zanzibari ni pamoja na Wazanzibari milioni moja kuja kukamata nusu ya Bunge la Watanganyika milioni 48, tena kwa mabilioni ya mapesa ya Watanganyika wenyewe. Ni tusi la thamani ya Mzanzibari mmoja kuwa sawa na Watanganyika 48! Isitoshe Wazanzibari wanakuja kutunga sheria ziwabane Watanganyika, wao wakiwa na Bunge lao wenyewe kule kwao, ambalo ni marufuku watumwa wao wa Tanganyika kuingiza pua zao humo! Hili ni kongwa la ukoloni linaloitesa Tanganyika. Muungano unavunja Ibara ya 12 na ya 13 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano, zinazotaka Watanganyika nao wawe na Katiba na Serikali yao wenyewe kama Wazanzibari walivyo nazo, na kuishi kwa damu yao pia kama wao wanavyoishi kwa damu yetu ingawa wenzetu hawanayo, wanategemea ukupe kwa Tanganyika. Muungano hata umefika kulaaniwa na Watanganyika hadharani kwa uchungu, kwamba Mzanzibari anakuja na msuli katika Bunge lao asilolichangia hata senti moja, na kuondoka na Prado la mataahira wa Tanganyika! Muungano huu ni ubeberu dhidi ya Wana wa Tanganyika, ambao ni lazima utokomezwe kwa amani. Ndugu Wajumbe, utwana huu wa wana wa Tanganyika unaonekana hata katika ‘mabwana’ wa Zanzibar kuwa wengi zaidi katika Bunge hili la Katiba, lakini gharama zote wanaumia Watanganyika! Tusi la ‘utaahira’ wa Watanganyika limezidishwa kwa kulileta katika Bunge maalum la KatibaBaraza la Wawakilishi, lililoitoa Zanzibar katika muungano kwa mabadiliko lililofanya katika Katiba yao! Wazanzibari wamejitoa kabisa katika muungano. Wamebaki kutumia neno muungano kwa ajili ya kuendeleza ukupe wao kwa Watanganyika (parasitic advantages). Katika mabadiliko hayo Wazanzibari wamefuta kipengele kilichowaingiza katika huo Muungano kwa Tamko kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, kwa Tamko kwamba sasa Zanzibar ni Nchi iliyo huru, au Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Ni dhahiri kwamba watu wa Jamhuri ya Zanzibar wameletwa katika Bunge hili la Katiba ambalo haliwahusu baada ya kujitoa rasmi katika muungano, ili watumiwe kwa maslahi ya kikundi cha ki-Mafia cha CCM kinachotaka kutawala milele, hata kwa kuhonga Uhuru wa Tanganyika! Waheshimiwa Wajumbe, haya ni mambo yanayobatilisha kabisa uhalali wa Rasimu ya Katiba, pamoja na mchakato wenyewe ulioitengeneza! Bunge hili la Katiba linapaswa kuvunja kongwa la utumwa kwa Watanganyika. Ni kongwa la kutokomezwa hata kwa kumwaga damu nyingi kuliko tulivyoimwaga kwa ajili ya Uhuru wa watu wengine! Bunge maalum la Katiba linafahamu kwamba kiitwacho “Muungano” kiliwarudisha Watanganyika katika utumwa na ukoloni, kama lilivyothibitisha Bunge la huo Muungano mwaka 1994 (Ni muhimu kila mjumbe wa Bunge maalum la Katiba apewe nakala ya Hansard hiyo ili aweze kuwajibika impasavyo), Bunge likapitisha Azimio la kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika, ambalo kisheria bado liko HAI likisubiri kutekelezwa tu. Azimio la Bunge la kuundwa Serikali ya Tanganyika liko hai kwa sababu Bunge halijawahi kupitisha Azimio mbadala la kubatilisha Azimio lake hilo, na sababu za kuundwa Serikali ya Tanganyika ni nzito zaidi leo kuliko hata wakati ule. Kilichotokea ni kwamba Nyerere aliwafokea Wabunge kwamba wao eti ni kamati ya siasa ya chama chake CCM, ambacho sera yake ni muungano wa serikali mbili tu, hivyo akawashambulia wale wanaotaka Serikali ya Tanganyika kwamba watoke CCM waende DP. Wabunge walinywea kwa sababu wangejitoa CCM wangekuwa wamejivua Ubunge, kwani Wabunge walikuwa bado ni kutoka CCM peke yake. Lakini Azimio hili liko hai, na ni Sheria ambayo Bunge maalum la Katiba ni lazima liitii. Wala Nyerere hakuwa mkweli kwa sababu Bunge lile halikuwa la CCM bali la Taifa, na lilichaguliwa na wananchi wote. Rasimu hii imepoteza kabisa uhalali mbele ya Bunge maalum la Katiba, kwa kutozingatia Azimio hili! Kwahiyo Rasimu ya Katiba ni batili. Ni wajibu wa Bunge maalum la Katiba kuhoji kwanini Serikali ya Tanganyika haijaundwa hadi leo, na kusitisha zoezi la Katiba ya muunganompaka Watanganyika waunde kwanza Katiba yao na kuwa na Serikali yao.

Imewasilishwa na Mchungaji C. Mtikila wa Democratic Party (DP)
Advertisements

3 thoughts on “Tanganyika ni nchi iliyonenwa katika unabii – Mchungaji Mtikila

  1. Mchungaji Christopher Mtikila ni mtanganyika makini hata mimi namuunga mkono 100% ila mataahira aliyoyataja ni mengi katika ngazi muhimu za maamuzi kuliko wazalendo wanaotetea Tanganyika Huru. Viva Rev. Christopher Mtikila may God bless and protect you always.

  2. Jones,

    Unamkubali sana Kamanda Mtikila kwa lipi? kwamba Tanganyika ilinenwa ktk unabii?

    Press on

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s