MIMI SIYO KAMA WALE! – Mchungaji Gwajima

gwajima

NA MCHUNGAJI KIONGOZIJOSEPHAT GWAJIMA

Utangulizi

Zaburi 118: 1-29 (sitakufa bali nitaishi ili niyasimulie matendo ya Bwana)

 1. Somo

Maandiko ya msingi  Luka 4:14- 24, Daniel 5:2 -26

Bwana Yesu siku moja alikwenda kwenye sinagogi mahali alipozaliwa na pale alipewa chuo cha nabii Isaya ili asome na aliposema “ Roho wa bwana yu juu yangu kwa maana amenitia mafuta,  aliposema maneno haya yametimia leo wayahudi walikasirika sana wakamtoa Yesu ili wamtupe kwenye ukingo wa mlima na kumwua. Wayahudi walikuwa wamewatupa watu wengi kwenye ukingo lakini Yesu alipofika pale ukingoni alipita kataikati yao kwa maana yeye siyo kama wale ambao walikuwa wakitupwa. Hii inatufundisha kuwa hata wewe mtu uliyeokoka huwezi kupata madhara ya maadui zako kwa maana mtu aliyeokoka ni tofauti na wengine, kwa hiyo uchawi, mitego na majungu ya adui zako  hayana nguvu juu yako kwa jina la Yesu.

Leo tunawatangazia adui zetu wote kwamba yale waliyowafanyia wengine hawawezi kutufanyia kwa maana  sisi siyo kama wale kwa hiyo  mambo yao hayawezi kutupata kwa jina la Yesu. Sisi walokole wa kizazi cha sasa siyo kama wale walokole wa kale walipopigwa shavu moja wakageuza na lingine, waliponyang’anywa kanzu wakatoa na Joho sisi ni watu tofauti tumetumwa kutenda na kutimiza kusudi la Mungu mpaka ulimwengu mzima wajue saa ya Ufufuo na Uzima, kwa hiyo hakuna wa kutuzuia hata kama wamedondosha na kukatisha tamaa wengi lakini sisi siyo kama wale , sisi tunazidi kusonga mbele kwa jina la Yesu.

Vyombo vya hekalu huwa havichezewi kwa maana vimetiwa mafuta, imeandikwa kwenye Daniel 5:2 -26 mfalmwe wa Babeli alipotumia vyombo vya hekalu kwa ajili ya kunywea kwenye sherehe Mungu alikasirika na kumwandikia maneno yafuatayo kwenye ukuta MENE MENE TEKELI NA PERESI, maana yake ufalme wako umepimwa na kuonekana umepungua kwa hiyo amepewa mwenzako.  Kwa hiyo mtu uliyeokoka ni chombo cha hekalu na yeyote anayekuchezea anakatiliwa mbali na wengine wanachukua mahali pao kwa jina la Yesu. Tunawatangazia hata viongozi wa Tanzania wanaowachezea watumishi wa Mungu kuwa ufalme wao umepimwa na kuonekana umepungua kwa hiyo watapewa wenzao.Wayahudi waliposikia Bwana Yesu anasema Roho wa Bwana yu juu yangu walifadhaika sana kwa maana walijua maana ya Roho wa Bwana kuwa juu ya mtu. Roho wa bwana na anapokuwa juu ya mtu , mtu Yule anakuwa na uwezo mkubwa wa kutenda lolote kama ilivyoandikwa Roho wa Bwana akamjia Samson naye akawaua wafilist maelfu, Imeandikwa tena roho wa bwana aliopokuwa juu ya Daud alimwua Goliath kwa hiyo aliposema hivyo walisema huyu naye atapiga mtu . Vile vile aliposema Bwana amenitia mafuta walitafakari kuwa watu wanaotakiwa kutiwa mafuta ni Nabii, Mfalme, Kuhani na Vyombo vya Hekalu. Kwa hiyo waliogopa kwamba mafuta yale labda anataka kuwa mfalme , au nabii kwa hiyo wakaona shaka na kuamua kumtupa ukingoni ili wamwuue na kusudi la mafuta yale lisitimie lakini Yesu alipita katikati yao. Leo nakutangazia mtu uliyeokoka mabaya waliokuandalia adui zako hayatatimia lakini kusudi la Mungu litatimia kwako kwa jina la Yesu.

Wayahudi walifadhaika pia Yesu aliposema kuwa nimetiwa mafuta kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao. wayahudi walikasirika sana kwa maana ndani ya hekalu kulikuwa na watu ambao wamewafunga watu kwenye magereza ya kiroho yaani kwemye magonjwa, balaa, mikosi umasikini nakadhalika. Kwa sababu  tabia za shetani ni kuwafunga watu  bila kuwaachia kwenye magereza yake kama ilivyoandikwa  Isaya 14:17-18, Matendo 27:42 .  kwa hiyo shetani na wakala wake walikasirika sana waliposikia Yesu anataka kuwafungua watu kutoka kwenye magereza ya mateso. Mungu naye mpango wake ni kuwaweka huru wafungwa kama ilivyoandikwa kwenye Yeremia 33 : 7, Zaburi 68:6, Ezekiel 16:53 Hosea 6:11,Nami kama mtumishi wa Mungu leo nawatangazia wafungwa wote kufunguliwa kwao, wafungwa wa magonjwa, wafungwa wa balaa, wafungwa wa madeni, wafungwa wa umasikini, wote nawatangazia uhuru leo kwa jina la Yesu.

Wayahudi walifadhaika pia Yesu aliposema kuwafanya vipovu wapate kuona tena, wayahudi walikuwa wamewatia upofu watu wengi ili wafuate desturi za mafarisayo bila kuona hatima yao.kwa hiyo  Yesu alipotangaza kuwafungua vipofu walikasirika sana kwa maana walijua udhalimu wao utadhihirika mbele za watu . Nami mtumishi wa Mungu nawatangazia vipofu wa kiroho waone tena , naondoa kila utando ulioweka kwenye macho ya watu ili wasione kwa jina la Yesu. Nawatangazia Watanzania wote waliokuwa wametiwa upofu hata wasijue kinachoendelea kwenye nchi yao naamuru waone tena na wajua hatima ya nchi yao kwa jina la Yesu.

Wayahudi walifadhaika pia Yesu aliposema nimekuja kuwaweka huru watu waliosetwa, maana desturi ya mafarisayo ilikuwa kuwaseta (kuwagandamiza) watu na kuwaweka chini ili wao wawe juu.

Nami mtumishi wa Mungu nawatangazia kuinuliwa watu wote waliogandamizwa na magonjwa, umasikini, madeni kwa jina la Yesu.

Wayahudi walikasirika aliposema kuwa amekuja kuutangaza mwaka wa Bwana, kwa maana wayahudi walikuwa na mwaka wa maachilio lakini walikuwa hawaachilie kama ilivyo .kwa hiyo Yesu aliposema kutangaza maachilio ya wale wakosaji walikasirika sana. Nami mtumishi wa Mungu nawatangazia msamaha  watu wote waliofungwa kwa sababu ya shida zao kwa jina la Yesu.

Kwa jina la Yesu , Roho wa Bwana yu juu yangu kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri masikini habari njema,kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kuutangaza mwaka wa bwana uliokubaliwa.Ukiri

 1. Maombi

Kwa damu ya Yesu najitakasa, Bwana naomba upako wa kufanya vita dhidi ya wale waliotaka nitumbukie kwenye mashimo ya uharibifu kwa jina la Yesu. Kwa damu ya Yesu nawateka na kuwatumbukiza wao kwenye mashimo waliyoyaandaa kwa ajili yangu kwa jina la YesuKwa jina la Yesu naamuru mtu yeyote aliyeandaa shimo la mauti, magonjwa ajali na mikosi  atumbikie mwenyewe kwa jina la Yesu.

 Imeandikwa kila achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe , naamuru mashimo yote waliochimba adui zangu watumbukie wenyewe kwa jina la Yesu. Ninakataa kutumbikia kwenye shimo waliloliandaa kwa ajili yangu au watoto wangu kwa jina la Yesu, nawatangazia adui zangu kuwa mimi siyo kama wale waliofanikiwa kuwatumbukiza, nakataa kutumbukia kwenye shimo la magonjwa, balaa, mikosi  umasikini na mauti, nakataa kuangamia nakataa kuteketea kwa mitego na mashimo yao kwa jina la Yesu.

Imeandikwa kila silaha itakayofanyika juu yangu haitofanikiwa, Katika jina la Yesu nawasukumia nyie kwenye Mashimo ya mauti mliyoyachimba, naamuru silaha zote za maangamizi mlizonitengeneza kwenye ulimwengu wa roho ziwanase wenyewe kwa jina la Yesu. Imeandikwa sitakufa bali nitaishi nami niyasimulie matendo ya Mungu,  nakataa kufa kwa ajali, magonjwa kuvamiwa au kunyweshwa sumu kwa jina la Yesu. Naamuru mashimo yote ya mauti yaliyotengezwa kwa ajili yangu yawameze adui zangu kwa jina la Yesu.

  ‘’AMEN’’

IBADA YA JUMAPILI TAREHE 15-06-2014

Advertisements

7 thoughts on “MIMI SIYO KAMA WALE! – Mchungaji Gwajima

 1. Kwa kiwango chochote utakachoipimia hotuba hii, utaiona moja kwa moja kwamba ni ‘mahubiri pori’; yaani lile jambo la “kukatiliwa mbali” alilolisema mtume Paulo, RUM. 11:22, “Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.”

  Nalo jambo hili ndilo hili linatutimilia pasi ufahamu! Wengi wetu huyachukulia matamshi ya kinabii tunayoyasoma ktk Biblia zetu kana kwamba yatatukia huko mbele ktk siku fulani, yaani yatawafika watu wengine na si sisi, lakini ndiyo haya yanayo endelea katikati yetu!

  Jaribu kuwaza, injili kama hii, Mungu ataipokea kwa kigezo gani? Ni matango mwitu, yataishia kuwaua wote wanaoyala. Unapoliacha Neno la Mungu, ile Injili waliyoihubiri mitume, basi unakuwa umeuacha Uzima na hivyo ni lazima uanze kunyauka; nayo dalili ya kunyauka ndio Injili pori kama hizi ambazo mwishoni huwa vijiti vikavu tayari kwa kuni!!! Mungu hashughuliki na watu waliokatiliwa mbali na kurudishwa huko porini walikotolewa, amewaacha waendelee na Vipawa vya dini hivyo visivyo na majuto wala mwelekeo!

  Mungu alisema ktk siku za mwisho kutakuwa na Njaa ya Neno la Mungu. Ninaamini hiki ndicho tunacho kishuhudia leo hii, makundi yetu, hayo yaliyokatiliwa mbali, yakihangaika huku na kule kutafuta chakula, lile Neno. Sasa unafahamu kwamba mtu akizidiwa kwa njaa, hata kama ni mtanashati na amelelewa ktk wingi wa vyakula, bali vikikosekana kabisa, unaweza kumkuta akihangaika huko jalalani! Ndio maana ni muhimu na ni wajibu usiokwepeka kwa wahubiri, na wahudumu wote wa Neno la Mungu, kuwalisha watu chakula kinachofaa kwa wakati na si kuwalisha mavyakula yaliyochacha kama haya yanayolipindua Neno la Mungu na hivyo kuishia kuwadumaza wote wanaolipokea!

  Jamani, jichungeni na hizo Cult nyingi zinazoinuka kila kukicha, zimejiviringisha ktk kundi la manabii wa Uongo! Nimewahi kuwakuta watu watanashati, tena maarufu, smart people, mhubiri kawapandisha munkari kwa injili ya uongo, akawaingiza ktk kudai matamanio yao, akiwaambia kuwa vitu hivyo ni halali yao na walikwisha pewa isipokuwa shetani aliwaibia; basi nikamuona mmoja, amevaa suti kali, anadai: “Nadai vogue langu, achilia vogue langu……; Ntakupiga vibao, achiliaaaaa!!!!! Kwa Imani nimelipata, na sasa naliendesha, vruuuuum!” Jamani anaendesha vogue bila hata bima! Ibada ilipokwisha nilimuona anagombea basi la bure la Kanisa lao!!!!

  Mbarikiwe!!!

 2. Asante Mtumishi kwa neno lafaraja.
  Tumuombe mungu sana atusaidie kujua kusudi la mungu juu ya maisha yetu, kuwahubiria watu habari njema za ufalme wa mungu. Mungu ni Roho nao wamuambuduo yeye imewapasa kumuabudu katika Roho na Kweli. Mimi naomba siku zote hii kweli iniongoze katika kweli yote, iniweke huru kama neno la mungu linavyosema.

  Mahubiri mengi na mafundisho mengi ya nyakati za sasa yanazama sana katika kuufurahisha mwili (yaani mambo ya mwilini), mimi ninadhani watumishi mtusaidie kutuongoza sana na mambo ya Rohoni ili tuweze kuurithi ufalme wa Mungu. Tulijue neno, tuliishi neno maana vitu na mali vitapita lakini NENO LA MUNGU HALITAPITA KAMWE. Yesu alitumia kauli mbiu ya “NJOONI KWANGU NINYI NYOTE MSUMBUKAO NA KULEMEWA NA MIZIGO YA DHAMBI, NAMI NITAWAPUMZISHA” Mkazo wake mkubwa ulikua ni kwenye Roho za watu, na ndio maana yule mtoza ushuru (Lazaro) alipobahatika kuonana na Yesu aliamua kutoa ahadi ya kulipa pesa zake kwa yeyote aliyemtoza sivyo, maana alitambua na aliona kuwa na Yesu ndio ilikua jambo la maana zaidi kuliko zile pesa alizokua akiwatoza watu zaidi. Mfano wa Tajiri na Lazaro pia unatufundisha ni jinsi gani matajiri walivyo na nafasi ndogo sana ya kuurithi ufalme wa Mungu kuliko yule masikini.

  Niko pamoja nawe katika kuujenga Mwili wa Kristo. Ubarikiwe Mtumishi

 3. ISAIAH 8:16
  “BIND UP THE TESTIMONY, SEAL THE LAW AMONG MY DISCIPLES.”

  WATU WANAOONGEA KWA AJILI YA KAZI YA MUNGU WAMEFUNGIWA USHUHUDA
  WALA HAWAPINGI NENO LA MUNGU.

 4. “NA WAENDE KWA SHERIA NA USHUHUDA; IKIWA HAWASEMI SAWASAWA NA NENO HILI, BILA SHAKA KWA HAO HAPANA ASUBUHI.”

  ISAYA 8:20

 5. Mchungaji ameeleza maneno mengi, amenukuu maandiko pia, nice vema. Lakini kabisa sijaelewa, Mimi najua kuwa mtu akiokoka anafanyika kuwa mtoto wa Mungu, sasa kuna utafauti upi katika wale waliookolewa? Biblia inasema, kabla ya kuwepo misingi ya Dunia Mungu aliwajua Watoto wake, kwa maana hiyo WOKOVU ulikwisha kufanyika hata kabla ya kuzaliwa huyo aliyeokoka!

  Vilevile, Biblia inafundisha kuwa wote tumeokolewa kwa namna moja tu yaani KWA NEEMA, sass no KWA vipi, waliokoka huko nyuma wawe na “AMRI” nyingine na wale wanaookolewa sasasa? Watoto wa Baba mmoja iweje walelewe kwa Sheria mbili tofauti?

  Nakumbuka katika kitabu cha LUKA ndiyo kuna patikana yale maelekezo Kuwait, ” ukipigwa shavu la kulia mgeuzie na la kushoto. Na ukiombwa kanzu toa na koto” ikiwa na maana kwa kifupi tusilipe VISASI, kama ndivyo mchungaji anataka kusemaje? Tulipe visasi? Biblia inasema wanaopotosha maandiko ni MANABII WA UONGO! Mimi sijaelewa, mchungaji anafundisha nini?

  “Ufahamu no chembe ya uhai!”

 6. Ni hotuba au mahubiri yanayosisimua sana; ninavyoyaona, yanaweza hata kuiamsha misukule!

  Ngoja ninukuu kisehemu cha hotuba hiyo nzuri na ya kupendeza:
  “”Leo tunawatangazia adui zetu wote kwamba yale waliyowafanyia wengine hawawezi kutufanyia kwa maana sisi siyo kama wale kwa hiyo mambo yao hayawezi kutupata kwa jina la Yesu. Sisi walokole wa kizazi cha sasa siyo kama wale walokole wa kale walipopigwa shavu moja wakageuza na lingine, waliponyang’anywa kanzu wakatoa na Joho sisi ni watu tofauti tumetumwa kutenda na kutimiza kusudi la Mungu mpaka ulimwengu mzima wajue saa ya Ufufuo na Uzima, kwa hiyo hakuna wa kutuzuia hata kama wamedondosha na kukatisha tamaa wengi lakini sisi siyo kama wale, sisi tunazidi kusonga mbele kwa jina la Yesu.””

  Lakini, jambo la kwamba sisi si kama wale walioyageuza mashavu yao, linapaswa liongozwe na Maandiko, ili tujue ni kwa jinsi gani, na ni kwanini au kwa kusudi gani wale waliyageuza hayo mashavu yao wachapwe vibao zaidi; kwamba Injili hiyo ilikomea wapi hata sisi tuwe tusio husika na ujumbe huo wenye Nguvu ya kukufanya uwageuzie na shavu la pili?

  Hebu itazame hii Injili ya kale, waliyohubiriwa walokole wa kale na jinsi ilivyowafanyia:
  Mt 5:38 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; 39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. 40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia …”

  43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; 44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, 45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni… ”

  Yhn 18:22
  22 Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu? 23Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?”

  Mdo 23: 2 Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. 3 Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria? 4Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? 5 Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako…”

  Paulo alikuwa akilirejea lile neno la Kristo linalowahusu hao watu wa dini waliokalia viti vya Hukumu: Mt 23:27 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.”

  Ndipo wale misukule wa dini wasio na uwezo wa kulihifadhi Neno la Mungu ndani yao, licha ya kuuona ukiukwaji wa Haki ulioamriwa na Kuhani Mkuu huyo aliye msimamizi wa Sheria, ambaye kwa ukiukwaji alioufanya amekuwa ni huyo aliyepakwa chokaa, kutoa mng’aro wenye kulaghai; wakamwambia Paulo kuwa anamtukana Kuhani Mkuu!!!!

  Hiyo ndiyo Injili ya kale, nguvu yake ilijidhihirisha ndani ya wote walioipokea, hata kifoni! Ni Injili inayoyakamata maisha yote ya Mkristo, ikiuondoa woga na utegemezi unaozalisha hofu za kufikirika nk ikiujaza moyo imani na Amani ya Kristo iliyowawezesha hao kuwa wakipekee.

  Basi tunapoisikia injili hii mpya inayoitamatisha hiyo Injili ya kale, ikiwaelekeza wakristo kupigana na wachawi nk, linakuwa ni jambo la kuvutia, ndio maana tunapenda kujifunza zaidi kuhusu mambo haya, ni kivipi, ni ufunuo mpya wa kinabii unayoivuka Injili ????

  Gbu all!

 7. Bwana Yesu asifiwe, mungu akubariki kwa neno lako linalosema MIMI SIYO KAMA WALE.nilivyosoma moyo wngu umepata nguvu na faraja.maadui zangu hawataniweza kwa jina la yesu watapigwa na kuangamia.

  naomba maombi kwani nina mchumba ila amebadilika anawanawake wengine

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s