Kukosa maono ni sababu ya kushindwa kwako!! – I

maono

“Pasipo maono watu hushindwa kujizuia”

Maono ni kama kesho ya mtu.

Kesho ni siku ambayo utarajiwa na haijaonekana bayana bado, na hakuna mwanadamu yeyote chini ya jua aijuaye kesho yake ipoje isipokuwa amejuzwa na Mungu ajuaye mambo yote kabla hayajatukia. Kesho ni siku ambayo ni matokeo ya kile kitu ambacho kimefanyika leo; kesho uandaliwa ndani ya leo, Mungu ndiye utoa jawabu kama iwe kama vile ulivyoiandaa.
Kuna msemo wa kiingereza usemao, “Yesterday has passed, today is here, tomorrow never come” hii inaonyesha kuwa katika maisha yote ya mwanadamu kuna siku tatu tu yaani jana, leo na kesho na mwanadamu anapaswa kuzitumia siku zote hizo kwa faida yake mwenyewe na kunufaisha jamii inayomzunguka pia.

Jana ni siku ambayo imepita na ukutengenezea uzoefu (CV) ambao waweza kuwa mzuri au mbaya na kamwe hautoweza kurudi jana kuibadilisha jana yako ila unaweza kuitumia Leo kuifanya kesho isijekuwa kama jana. Jenga tabia njema ya kutojisifia kwa mazuri uliyofanya jana kwa kuwa kujisifia kutakufanya ujisahau kuwa unapaswa kusababisha mambo makubwa kutokea tena na tena kamwe usijaribu kujilaumu kwa vile ulivyoshindwa jana kwa kuwa itakufanya uwe muoga wa kujaribu kufanya mambo makubwa leo. Lakini mazuri ya jana yanaweza kutumika kama marejeo kuwa kama jana nilishinda basi na leo pia naweza kushinda kama ilivyokuwa kwa Daudi aliporejea kuua simba na dubu alipotaka kupambana na Goliathi.

Kesho ni mimba ambayo imetungwa leo na yapaswa kujifungua ni muhimu sana kuzingatia ili kuweza kujifungua mtoto aliye mzuri na hii inatokana na mimba hiyo imetungwaje na katika hali gani. Kujifungua mimba hii kunahitaji nguvu ya mbeba ujauzito na pia Mungu akusaidie kujifungua salama.

Kesho ni ahadi ambayo imetoka kwa Bwana kwa kuwa ahadi ni mambo yatarajiwayo na hayajaonekana bayana bado, hapa ninazungumzia zaidi ndoto au maono ya mtu ambayo ndiyo kesho yenyewe na utarajiwa kutimia na hayajaonekana bayana bado.Kitu chochote unachokifanya leo kinaonyesha kuwa kesho yako itakuwaje.

Ni lazima uione kesho yako ukiwa leo kwa kuwa kesho yako inategemea sana na wewe unaona nini ndani yako mwenyewe ukiwa leo na si kuona tu pia unakiri nini kwa kuwa kuna nguvu katika ukiri wa maneno na si ukiri tu bali ni nini ukifanyacho leo kinaweza kuitimiza kesho yako. Kitu ukionacho ndani yako, ukikiricho na hata kukifanya ugeuka kuwa tabia na kikiwa tabia mwishoni uja katika uhalisia wa utimilifu wake.

Kesho yako haitakuja kama muujiza yaani umeamka na kuiona tu inatimia, hapana ni mchakato mrefu ambao unakuitaji mwamini kutia juhudi za kutosha ili iingie kwenye utimilifu wake. Kama haujaanza kuwaza kuwa kesho yako itakuja kuweje kamwe usijedhania kama kitakuja kutimia kwako kitu ambacho hujawahi kukiwaza hata siku moja, mtu anaweza kuhangaika na kitu ambacho amewahi kukiwaza hapo awali kuliko kile kitu ambacho hajawahi kuwaza kabisa.

Lazima uione ndani yako kwanza. Mwanadamu huwa vile anawaza ndani yake kwa kuwa lile wazo humpa hamasa ya kufanya kazi ili litokee na wazo pia la ndani yake uweza mfanya kukata tamaa ya kufika mbali. Mtu mmoja akasema kuwaza ni kuwaza tu kama umewaza mambo makubwa au madogo ni bora ukawaza vitu vikubwa labda waweza kuwa mtu mkubwa. Lakini kuwaza tu pasipo kuchukua hatua hakufai.

Mithali 23:7 “7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.” Yaani ukitangulia tu kuona kuwa wewe ni maskini mkubwa ni lizima uwe, ni lazima ujifunze kuona vyema. Watu wakubwa duniani kabla ya kuwa vile walivyo, walitangulia kuona ukubwa ndani yao kwanza na kisha wakaanza kufanya kazi kwa kuwa ile picha waliyoiona ndani yao uwatesa kuifikia.

Katika biblia neno ‘unaona nini?’ limeonekana mara saba na siku za wiki zipo saba, ina maana ya kusema kila asubuhi BWANA uweza kukuuliza ‘unaona nini?’ mpaka zikaisha siku saba za wiki na itakapoanza jumatatu ataanza na unona nini? tena mpaka Ijumaa huku akiunganisha na neno usiogope kwa kila siku uionayo katika uwepo wako duniani.

Kofi Anan ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa baada ya kuingia UN katika nafasi ya kawaida tu akamwandikia mama yake ujumbe na kumtaarifu kuwa siku moja ni lazima aje kuwa katibu wa umoja wa mataifa. Alivyoona ndivyo ilikuja kutokea na kule kuona kwake kulimlazimu kutotulia na kuwa na juhudi kubwa sana ili badae aje kuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa.

Kama kuna picha tayari unaiona ndani yako ya jinsi vile unavyopaswa kuwa ni muhimu sana kuzingatia kuwa picha ile ni nguvu ya kukufanya upigane hata kuitimiza; ila mbaya zaidi ni kwa mtu asiye na maono kwa kuwa hana picha ndani yake ni vigumu kwa yeye kufanya kitu cha msingi.

Maandiko yanasema katika Mithali 28:19 kuwa “18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia”, tafsiri ya asili ya kiebrania kutoka katika neno ‘hazon’ utafsiri maandiko haya kwa kumaanisha mafunuo ya neno la Mungu, na uendelea kwa kumaanisha kuwa pasipo neno la Mungu kufunuliwa kwa watu ni lazima watu waende katika njia ya upotevuni. Mahali popote ambapo neno la Mungu halijafunuliwa ni lazima watu waangamie na kuendelea katika njia zao wenyewe kwa kuwa bado uwa kwenye mabano ya wafanye kipi na kuacha kipi.

Kwa kuangalia maono pia mtu yeyote ambaye hajafunuliwa ni maono gani alionayo ni kazi sana kuwa katika njia sahihi. Jamii inayotuzunguka watu wengi hukosa maono na ndiyo maana huishia kufanya vitu vya ajabu sana. Maono ni ile picha ya ndani aionayo mtu kwa habari ya kesho yake na kama mtu haoni picha yoyote ndani yake ni vigumu kufanya vitu vya msingi vya kimaendeleo.

Mtu mwenye maono hata kama anaonekana maskini kwa wakati huo ni mtu wa tofauti kwa kuwa maono ni muongozo wa utendaji kazi wa mtu huyo na ni lazima afanye mambo ambayo yanapelekea utimilifu wa maono hayo na uishi maisha ya kujizuia katika mambo yoyote ambayo hayamsaidii kufikia mwisho wake. Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata maono yake yawe yametimia. Maono utoa muongozo wa jinsi mtu apasavyo kuwa na hata jamii ya kushirikiana nayo.

Nikiwa sehemu Fulani nahudumu baada ya huduma nikamuuliza kijana mmoja unatakakuja kuwa nani? yule kijana akanambia nataka kuja kuwa dereva na alikuwa anasoma na nilipomuuliza kwa nini anataka kuja kuwa dereva akanambia ni kwa sababu wazazi wake hawana uwezo wa kumuendeleza kimasomo, nilitafakari kuwa mtu huyu anataka kuja kuwa dereva kwa ajili ya hali ngumu ya kiuchumi ni vizuri ila katika mazungumzo nikagundua kuwa amekata tamaa ya kufanikiwa zaidi kwa sababu ya hali yake ila mwenye maono hata kama ana hali ngumu kamwe hatoacha kuukiri ushindi wake kuwa pamoja na ugumu uliopo ninaweza nikafika pale napokusudia na hata kama nitachelewa kulingana na vikwazo vya hali niliyonayo sasa ila nitahakikisha nimefika.

Pamoja na kuwa mfanya kazi wa ndani kwa Potifa na kisha kupelekwa gerezani na kuwa mfungwa, bado Yusufu aliendelea kuitazama na kuikili ndoto yake ya kuja kuwa mtu mkubwa, mazingira mabaya na ya kukatisha tamaa hayakumfanya Yusufu akate tamaa na kubadilisha aina ya ndoto. Ni ukweli sana kuwa ugumu wa maisha ni sababu kuu sana ya kusababisha watu kuyaacha maono yao ya uhalisia na kuingia katika mengine ambayo si maono yao.

Mtu asiye na maono ni lazima mambo yake yawe ovyo ovyo kwa kuwa hakuna mwongozo sahihi unaoweza kumzuia asifanye yale ambayo anataka kufanya. Maono ni muongozo kwa mtu mwenye nayo katika mambo yote na umuongoza kuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi na kuwa na watu sahihi. Na ni nadra sana kumkuta mtu mwenye maono anafanya mambo ambayo hayawezi kumsaidia kufikia utimilifu wa maono yake.

Ni muhimu sana kwa mtu kuiona kesho yake ndani yake na aione katika uzuri ndipo anaweza tumia muda wake vizuri kutimiza yale ayaonayo. Kuona ni jambo jema sana ila mtu aweza ogopa kuwaza mambo makubwa na hii utokana na mtu kujidharau na kuona kuwa ana uwezo mdogo sana ndani yake, hili ni tatizo la kiimani, kutojitambua na kujidharau; ni lazima utoke kwenye eneo hili la kukosa kutokujiamini na uanze kuona kuwa unaweza.

Maono makubwa, uleta taabu kubwa, (The greater the revelation, the greater tribulation)

Wakati Fulani nikiwa na rafiki yangu akanena na kunambia “the greater revelation, the greater tribulation,” akimaanisha kuwa ‘maono makubwa uambatana na taabu kubwa). Ukifuatilia kwenye biblia utaona kuwa watu wote waliobeba maono makubwa ndio watu waliopata taabu kubwa hata utimilifu wa maono yao. Usikate tamaa unapoona majaribu yamekuwa ni makubwa sana kwa upande wako, kaa utulie huku ukitafakari kuwa ni uzito wa maono uliyonayo ndiyo sababu kuu ya kuteseka kwako.

Mfano ni Mtume Yohana aliyepata maono ya kitabu cha ufunuo akiwa katikati ya mateso makubwa na kuwekwa katika kisiwa cha Patmo na Mtume Paulo ambaye alipata mateso makubwa kulingana na ukubwa wa maono aliyokuwa amebeba. Kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?

Katika jamii ya waswahili huu ni msemo ambao umekuwa ukitumika sana na ni miongoni mwa misemo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa sana. Ni kweli kuwa wapo watu wafanyao mambo makubwa na yakatokea lakini wengine ushindwa kufanya mambo hayo. Wafanikiwao nao ni watu kama walivyo watu wengine ila utofauti mkubwa ujengwa katika namna ya kufikiria na pia katika namna ya kufanya mambo, watu wote walio juu ukifuatilia historia zao utakuta walikuwa ni watu wa kawaida sana, ila ndani yao waliweka nia na kuamua kupambana kufikia hatua kubwa na za juu, na watu wa namna hii hata walipopata mafanikio madogo hawakubweteka na kujisahau bali uzidi kusonga mbele kupata mafanikio makubwa zaidi. Kama wao wamejaribu wakaweza kwa kutia nia na wewe ukitia nia kwa lolote ufanyalo ni lazima utaweza tu.

Mfumo wa kuzaa kwa viumbe
Nikiwa na rafiki yangu tunazungumza na kutiana moyo kwa habari ya safari tuliyonayo akazungumza neno jema sana kuhusu maono kwa kufananisha na wanyama kuwa wanyama wadogo ubeba mimba na kujifungua kwa muda mfupi; wengine uwa miezi mitatu(3), wengine ni sita(6) na wengine ni tisa(9), tofauti uwa kwa wanyama wakubwa kama tembo wao ubeba mimba yao kwa muda mrefu sana ukilinganisha na wanyama wengine, hii ni kwa sababu ya ile asili yao ya ukubwa ambayo Mungu amewawekea.

Kwa kuutazama mfano huu ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa maono makubwa uweza chukua muda mrefu sana kabla ya kutoka na mtu mwenye maono makubwa uchukua muda mrefu pia kufikia utimilifu wa maono yale. Usiumie kwa nini wengine wanatoka upesi na wewe unapambana ila bado; fahamu aina ya maono uliyobeba pengine ni mazito kama mimba ya tembo na kama ndivyo yaweza kaa muda mrefu hata utimilifu wake ila yatatokea tu kwa kuwa maono ni kama mimba.

Mbali na wanyama pia kwa mimea kuna neno jema la kujifunza kwa kuwa kuna miti ambayo upandwa na kukua kwa muda mfupi na uvunwa ndani ya muda mfupi huo ila kuna mimea ambayo ukaa sana na uchukua miaka mingi sana hata kufikia utimilifu wake, kwa kuchukulia mifano kama mnazi, hata mbuyu ukaa kwa kitambo kirefu sana hata kuja kutoa matunda yake.

Hii inaonyesha kuna utofauti mkubwa sana wa utimilifu wa maono ya mtu mmoja mpaka mwingine, kuna wengine ambao ushuhudia utimilifu wa maono yao kwa haraka sana ukilinganisha na wengine. Muda wa kuchelewa kwa maono ya mtu Ibilisi uhutumia sana kuwa shawishi watu kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nao, na uweza sema, mbona hujabarikiwa kama Fulani na Fulani na wewe unamtumikia Mungu kama wao, au ulimaliza nao chuoni au shuleni au ni marafiki wa karibu ukishiriki nao mengi sana ila wao wamekupita kufanikiwa kwa kuwa Mungu hajali mambo yako na uwapenda wenzako kuliko wewe; wewe usikatishwe tamaa na sauti ya kinyonge namna hiyo songa mbele maana utimilifu wako unakuja na ufanikiwaji wa mtu mmoja na mwingine uwa tofauti na kwa nyakati tofauti tofauti.

Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata atimize maono aliyonayo na hata akishindwa mara moja uinuka na kujitia nguvu na kutokata tamaa na ni maono ambayo umsaidia mtu kuishi kwa kuukomboa wakati, kuweka vipaumbele vya maisha ambavyo vitampelekea kufikia utimilifu wa maono nhayo, kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ambao watamsaidia kufikia hatima ya maisha yake.

Itaendelea sehemu ya pili

–Kelvin Kitaso

Advertisements

10 thoughts on “Kukosa maono ni sababu ya kushindwa kwako!! – I

 1. Amen Mtumishi wa Mungu, Mungu akuzidishie roho ya ufahamu na maarifa nimesoma asubuhi ya leo nami nimepata kitu, asante maana umenitia nguvu mpya ndani yangu. Endelea kutufundisha mengi zaidi.

 2. Nashukuru mtumishi Christina kwa kuongezea vitu vya msingi sana sana… Nakuomba usikose kupata nakala yako ya kitabu cha huyu ndiye adui wa mafanikio yako ambacho kimebeba mambo mengi zaidi ya hayo.

 3. HAYA NDIYO MAFUNDISHO YANAYOLETA UKOMBOZI
  NDANI YA KANISA(KUJITAMBUA KIROHO).
  Mtumishi kelvin ubarikiwe katika maarifa.Tunasubiri sehemu ya
  pili ya mafundisho haya kuhusu MAONO.
  Naomba nieleze kidogo kile ambacho ROHO WA KRISTO ananiongoza
  kuongezea hapa.Ningependa niunganishe MITHALI 29:18 ambayo
  inasema “Pasipo MAONO watu huacha kujizuia….” na YOELI 2:28 ambayo inasema “……..nitamimina roho yangu juu ya wote wenye
  mwili, na wana wenu, waume kwa wake,watatabiri,wazee wenu
  wataota ndoto na vijana wenu wataona MAONO”

  Katika Mithali 29:18 suala la MAONO linahusanishwa na watu,hatujambiwa kama ni vijana au wazee.Katika Yoeli 2:28 suala
  la MAONO linahusanishwa na vijana.Ukweli ni kwamba MAONO
  huanzia utotoni na kimsingi ni kwamba mtu anazaliwa nayo.Katika ujana ndicho kipindi ambacho anatakiwa kuyaelewa vizuri maono
  yake na kuanza kuyatekeleza kwa kutumia ile nguvu ya ujana
  ambayo Mungu ameiweka ndani yake.Ndiyo maana mzee Yohana
  anasema kwa msisitizo kwamba “……..nimewaandikia nyinyi vijana
  kwa sababu MNA NGUVU, na NENO LA MUNGU linakaa ndani yenu,
  nanyi MMEMSHINDA YULE MWOVU”-1 YOHANA 2:14,Kwahiyo kijana anapaswa
  kusimamia mafunuo ya neno la Mungu ambayo Mungu ameyaweka
  ndani ya moyo wake kwa mfumo wa picha(MAONO) kwa kutumia
  nguvu anazopewa na Roho Mtakatifu ili KUHARIBU MAKUSUDI YA
  SHETANI katika eneo la maono aliloitiwa.Katika uzee ni kipindi cha
  kukamilisha maono na kutafuta mtu wa kumuachia kijiti.Mfame Daudi
  alipoondoka mwanae Suleimani akakalia kiti chake.

  Mzee Yohana anasema katika ule mstari wa 15 kwamba ili vijana
  watimize maono ambayo Mungu ameweka ndani yao WANATAKIWA
  WASIIPENDE DUNIA WALA MAMBO YALIYOMO KATIKA DUNIA.Katika
  mstari wa 16 Mzee Yohana anataja baadhi ya mambo ambayo
  yanawafanya vijana washindwe kuyajua,kuyasimamia na kuyatimiza
  MAONO YAO(yale ambayo Mungu ameweka ndani yao).
  Anasema hivi “Maana kila kilichomo duniani yaani, TAMAA YA MWILI,
  na TAMAA YA MACHO, na KIBURI CHA UZIMA,havitokani na Baba
  bali vyatokana na dunia.Katika Mstari wa 17 Mzee Yohana anatoa siri
  kwamba ili mteule aweze kushinda katika maisha ya wokovu NI LAZIMA AJUE NA KUSIMAMIA MAONO ambayo Mungu amemuitia.
  Anasema hivi “Na dunia inapita,pamoja na tamaa zake, BALI YEYE
  AFANYAYE MAPENZI YA MUNGU ADUMU HATA MILELE”.Dhambi
  ndiyo sumu kali inayoua MAONO YA VIJANA.

  Mfano mzuri na ulio hai tunauona katika maisha ya Yusufu.Mungu
  alianza kumjulisha MAONO YAKE akiwa chini ya miaka 17.Yusufu
  alichukiwa na ndugu zake kwa sababu ya tabia yake ya UAMINIFU
  na utakatifu.Yusufu alikuwa ni kijana mdogo aliyechukia DHAMBI na
  ndiyo jambo lililomfanya Baba yake ampende kuliko watoto wengine.
  Chuki ya ndugu zake ilizidi zaidi baada ya Yusufu kufanya kosa la
  kuyaanika wazi MAONO YAKE(Soma MWANZO 37:1-20).

  Ngoja tuone Roho Mtakatifu anatupeleka wapi…………………

 4. Ameen! ubarikiwe sana mtu wa Mungu nyanchiwa
  … Ahsante strictly gospel kwa kuwa dhana njema ya kupeleka ujumbe wa Mungu.

 5. haleluya Mtumishi wa Bwana Kelvin Nashukuru Sana na Mungu akuzidishie Hekima katika hayo, Nimesoma ujumbe huu asubuhi ya leo na kufurahi sana, Maamuzi yako leo ndio matokeo ya kesho na inategemea ni jinsi gani umebeba maono yako, Ndio maana Neno la Mungu linauliza “UNAONA NINI?” nasi yapasa kuitii sauti ya Mungu.UBarikiwe sana

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s